Taarifa ya Utekelezaji wa Kazi za Chama 2004 – 2009

Katika mwezi wa Aprili 2008, Mwenyekiti alikutana na wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam katika ukumbi wa Diamond Jubilee ili kufafanua hatua ya CCM kukiuka makubaliano ya mazungumzo kati yake na CUF, ikiwa ni kujibu hotuba ya Rais Kikwete kwa taifa, ambayo ilikuwa inajaribu kuhalalisha uamuzi wa chama chake wa kuja na ajenda mpya ya kura ya maoni kwenye mazungumzo hayo. Mwenyekiti alibainisha kuwa ajenda hiyo ilikuwa ni usanii na kiini macho cha kisiasa chenye dhamira ya kuikwamisha CUF na kwamba CUF haikuwa tayari kushirikiana na CCM kuwaghilibu Watanzania na walimwengu kwa ujumla kwa mazungumzo yasiyokwisha. Huo umekuwa ndio msingi wa ufafanuzi wa Chama hadi sasa juu ya kukwama kufikiwa kwa suluhisho la kudumu la mpasuko wa kisiasa wa Zanzibar.

Mwenyekiti wa CUF, Prof. Ibrahim Lipumba, akitoa hotuba ya ufunguzi kwenye Mkutano Mkuu wa Nne wa Taifa tarehe 23 Februari, 2009

Mwenyekiti wa CUF, Prof. Ibrahim Lipumba, akitoa hotuba ya ufunguzi kwenye Mkutano Mkuu wa Nne wa Taifa tarehe 23 Februari, 2009

YALIYOMO

Sura ya Kwanza: Utangulizi

Sura ya Pili: Ofisi ya Mwenyekiti Taifa

Sura ya Tatu: Ofisi ya Makamu Mwenyekiti

Sura ya Nne: Ofisi ya Katibu Mkuu

Sura ya Tano: Ofisi za Naibu Katibu Mkuu: Tanzania Bara na Zanzibar

Sura ya Sita: Kurugenzi za Chama
i. Kurugenzi ya Oganaizesheni
ii. Kurugenzi ya Siasa
iii. Kurugenzi ya Haki za Binaadamu na Mahusiano ya Umma
iv. Kurugenzi ya Blue Guards
v. Kurugenzi ya Fedha na Uchumi

Sura ya Saba: CUF Katika Jumuiya ya Kimataifa:
Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa

Sura ya Nane: Tathmini
i. Nguvu za Chama kwa Miaka Mitano
ii. Mapungufu ya Chama kwa Miaka Mitano
iii. Fursa za Chama kwa Miaka Mitano
iv. Matarajio ya Chama kwa Miaka Mitano

Sura ya Tisa: Hitimisho na Mapendekezo

SURA YA KWANZA

UTANGULIZI

Tarehe 20 hadi 21 Novemba, 1992, katika Jengo la Hoteli ya Starlight, jijini Dar es Salaam, kundi la Watanzania kutoka Tanzania Bara na Zanzibar lilikutana na kutoa tamko lifuatalo:

“Baada ya kuruhusika kuanzishwa kwa vyama vingi vya siasa humu nchini Tanzania, mapema mwezi wa Julai, 1992.

“SISI WATANZANIA WA PANDE ZOTE MBILI ZA JAMHURI YETU, TANZANIA BARA na ZANZIBAR, tuliamua kukutana mjini Dar es Salaam katika Ukumbi wa Starlight Hotel kama waasisi na kutafakari kwa kina na kuzingatia kwa uzalendo kuhusu maendeleo ya nchi yetu. Tuliangalia na kuchambua kwa undani namna maisha ya watu wetu yalivyokwishafikishwa katika kipindi cha miaka 28 ya Muungano wetu chini ya mfumo wa ukiritimba wa Siasa ya Chama kimoja.

“TUMETAMBUA kuwa nchi yetu na watu wake mahala walipofikishwa hivi sasa, wataweza kunufaika zaidi kimaendeleo, kisiasa, na kijamii endapo wataikumbatia kwa ukamilifu fursa pekee ya kihistoria iliyoanzishwa ya mfumo wa demokrasia ya kweli, yenye amani na utulivu katika maisha ya watu walio huru. Tumegundua pia kuwa nchi yetu ni tajiri katika maliasili zilizomo ardhini, majini na hewani. Maliasili hizi zinaweza kutumiwa kwa manufaa na maslahi ya wananchi wote, juhudi ya kila mmoja wetu aliyeko mjini na kijijini, aliyeko shambani na kazini maadamu tu taifa na vyombo vyake vinaheshimu, kulinda demokrasia na haki za binaadamu na haki za watu kama zilivyotangazwa na Umoja wa Mataifa na Umoja wa Nchi Huru za Afrika.

“KWA KUWA sisi Watanzania tuliokutana Dar es Salaam kwa muda wa siku mbili, tarehe 20 – 21 Novemba 1992, tunaamini kuwa Haki za Binaadamu na Haki za Watu, kama zilivyotangazwa katika Tangazo la Haki za Binaadamu la Umoja wa Mataifa, na Hati ya Umoja wa Nchi Huru za Afrika juu ya Haki za Binaadamu na Haki za Watu, ndio msingi wa sheria na kanuni zinazotakiwa kuongoza nchi;

“KWA KUWA tunaamini kwamba kufuatana na imani yetu ya Haki za Binaadamu na Haki za Watu, wanawake wana haki ya kushiriki katika maamuzi yanayohusu maisha yao ya kisiasa, kiuchumi na kijamii bila ubaguzi kwa misingi ya jinsia au mila;

“HIVYO BASI TUNATAMKA KWAMBA, sisi tuliokutana Dar es Salaam tarehe 20 mpaka tarehe 21 Novemba 1992 tumeamua kuunda Chama cha Siasa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kitakachoitwa THE CIVIC UNITED FRONT (CUF – Chama Cha Wananchi).

“Tumeamua kuunda chama hiki THE CIVIC UNITED FRONT (CUF – Chama Cha Wananchi) kwa nia ya kuwaunganisha watu wa Tanzania wenye imani na demokrasia ya kweli ambapo wananchi wenyewe ndio wenye mamlaka, madaraka na uamuzi wa mwisho kuhusu mambo ya nchi yao.

“Tumechukuwa uamuzi huo wa kihistoria ili kutekeleza imani yetu ya Haki za Binaadamu na Haki za Watu kwa kutumia Itikadi au falsafa yetu mpya itakayojulikana kwa jina la UTAJIRISHO, yaani “Neema kwa Wote.”

“NA KWA HIVYO:

i) Tunasisitiza kuwa ni jukumu la Chama chetu kujenga nchi yetu upya kwa kuthamini ubinaadamu, utu wa mtu binafsi, na nafasi ya kila mtu, kazi, uzoefu wake, ujuzi wake, ubunifu wake, elimu yake na juhudi yake kama mwananchi wa Jamhuri kwa kutumia Utajiri wa maliasili ya nchi yetu iliyopo angani, nchi kavu na baharini, ili kuitekeleza Sera ya Chama ya Ustawi wa Maendeleo ya kila Mtanzania wa Bara na wa Zanzibar, katika ukamilifu wa nafsi yake kiroho, kiakili, kimwili, kitabia na kijamii. Utekelezaji huo utazingatia kwa namna gani Watanzania wote watajenga na kuimarisha ushirikiano mwema wa wote wale wanaopigania haki katika nchi yetu na katika nchi za Kiafrika na za ulimwengu ambao bado haki za binaadamu na haki za watu zinapuuzwa na kuvunjwa.

ii) Tunasisitiza kwa Watanzania wenzetu kuwa, kazi kubwa ya Chama hichi itakuwa kushirikisha upya jamii ya Watanzania iliyozindukana, jamii ambayo iko vijijini na mijini, ili itende wajibu wake wa kuiletea Tanzania maendeleo zaidi ya kweli na yenye ustawi, kwa kuviongoza vyombo vya dola vitende haki sawa kwa wote na kwa wananchi kukwepa uonevu na ukiritimba wa mawazo.

iii) Lengo hili litafikiwa tu kwa kuupa fursa na uhuru kamili umma kwa jumla, na watu binafsi waliozindukana waweze kubuni njia za kiuchumi zenye urari wenye tija na ambazo zitaleta maendeleo yenye maslahi yao ili kuimarisha amani ya kweli itokanayo na uchumi wenye haki kwa nay a kuifikisha nchi katika enzi ya utajiri wa wastani kwa wote.

iv) Hali kadhalika, Katiba hii ya Chama pamoja na kanuni zake zimetungwa kuzingatia Katiba zote za nchi zetu. Pia Katiba hii imezingatia kwa makini masharti muhimu ya vifungu vya Sheria Na. 5 ya 1992 inayohusu USAJILI WA VYAMA VYA SIASA TANZANIA. Hivyo, Katiba hii ina madhumuni ya kulinda amani, umoja wa taifa na utulivu kwa kuing’anga’ania demokrasia ya kweli katika shughuli zote za Dola ili kufikia matumaini yetu ya kuunda Chama cha Kitaifa kwa misingi tuliyoieleza hapo juu.

“SISI WAASISI WA CHAMA HIKI tutatilia mkazo kufanya maamuzi yetu kwa njia za kidemokrasia na za amani. Daima tutatumia utaratibu mzuri wenye heshima katika kuwashirikisha wananchi wenzetu kuunga mkono Chama chetu na Sera zake.

“Kwa hivyo tunasisitiza kwa kila mwananchi atakayejiunga na Chama hiki akumbuke kuwa amani ni kichocheo cha maendeleo na utamaduni wa Chama chetu.”

Tamko hili ndilo lililokizaa ramsi chama cha THE CIVIC UNITED FRONT (CUF – Chama Cha Wananchi), ambacho sasa kinatimiza miaka 17 tangu kuasisiwa kwake. Tangu hapo hadi sasa, dira na mwelekeo wa CUF umekuwa kama ulivyoasisiwa na waasisi wake. Chama hiki kimejengwa, kwa mfano, katika imani ya haki za binaadamu na haki za watu na hivyo dira yake ni haki sawa kwa wote.

Miaka hii mitano imekuwa ya kupanda na kushuka, kupata na kukosa, lakini zaidi ya yote, kama uchambuzi wa ripoti hii unavyoonesha, imekuwa ni miaka ya kujifunza na kujijenga upya. Kwa mfano, ni ndani ya kipindi hiki, ndipo kwa mara ya kwanza CUF ilipojiwekea Mpango Mkakati wa Chama (Strategic Plan – SP), ambao ni wa kisayansi na wenye kutekelezeka. Kwa muda sasa, Mpango huo umekuwa ndio dira, tegemeo, muongozo, na kwa hakika, ndiyo maisha ya CUF.

Taarifa hii ya Kazi za Chama kwa Kipindi cha Miaka Mitano inayowasilishwa kama tathmini ya CUF kuanzia 2004 hadi 2009 inaonesha namna ambavyo Chama kimefanikiwa au kutofanikiwa katika kulinda misingi na dhamira ya uanzishwaji wake.

Kwa sababu ya kurahisisha ufahamu, Taarifa hii inagawiwa katika sehemu kuu tisa (9) ambazo ni Utangulizi, Ofisi ya Mwenyekiti wa Taifa, Ofisi ya Makamu Mwenyekiti, Ofisi ya Katibu Mkuu, Ofisi za Manaibu Katibu Mkuu, Kurugenzi za Chama, CUF Katika Jumuiya ya Kimataifa, Tathmini ya Jumla na Hitimisho.

Sehemu hizi tisa (9) zinakusudiwa kuchora picha ya jumla ya utendaji wa Chama, nguvu na mafanikio yake, udhaifu na mapungufu yake, matatizo na vikwazo kiliokabiliana navyo na pia fursa ambazo Chama kimezipata na kuzitumia ndani ya kipindi hiki cha miaka mitano. Bila ya shaka, baada ya kuangazia mambo hayo, Taarifa hii itaweza kutoa, angalau kwa mukhtasari na kwa makisio, mwelekeo na matarajio ya Chama kwa miaka mingine mitano ijayo.

SURA YA PILI

OFISI YA MWENYEKITI

2.1 Utangulizi

Mwenyekiti wa Chama wa Taifa ndiye kiongozi mkuu wa shughuli za chama katika ngazi ya taifa na pia ndiye pia msemaji mkuu wa chama.

Kifungu cha 68 (1) (a) – (i), ambacho kinazungumzia nafasi ya Mwenyekiti wa Chama wa Taifa na kazi zake, kinayataja majukumu ya ofisi ya Mwenyekiti kuwa ni haya yafuatayo:

i) Kuongoza shughuli za Chama kitaifa;
ii) Kukisemea Chama kwa mujibu wa katiba na maelekezo ya Mkutano Mkuu wa Taifa na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa;
iii) Kujenga uhusiano mzuri na viongozi wa kitaifa wa vyama vyengine vya siasa ndani na nje ya nchi;
iv) Kuteua Wakurugenzi na Mainaibu Wakurugenzi wa Chama kitaifa kwa kusahuriana na Makamu Mwenyekiti;
v) Kuteua wanachama kumi (10) kuwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa;
vi) Kuteua Katibu wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Chama;
vii) Kupendekeza majina ya watu wanaofaa kuwa Manaibu Katibu Mkuu.

Katika kutekeleza majukumu haya ya kikatiba, baina ya mwaka 2004 na 2009, kazi za Ofisi ya Mwenyekiti wa Chama Taifa zinaweza kugawiwa katika maeneo yafuatayo:

i) Kazi za Ofisini
ii) Uimarishaji wa Chama
iii) Vikao vya Chama
iv) Mashirikiano na Vyama vya Siasa na Taasisi za Nchini
v) Mikutano na Waandishi wa Habari
vi) Mazungumzo na Wageni, Mabalozi na Uhusiano na Jumuiya ya Kimataifa
vii) Kuhudhuria Shughuli Rasmi za Kiserikali na za Kijamii

Mkutano Mkuu wa Taifa wa Tatu (23 – 28 Februari, 2004) ulimchagua Mheshimiwa Profesa Ibrahim Haruna Lipumba kuwa Mwenyekiti wa Taifa wa Chama. Katika kipindi hiki kinachomalizika sasa, Profesa Lipumba amekiongoza Chama kwa umakini na umahiri mkubwa.

2.2 Kazi za Ofisini

Kazi za ofisini za Mwenyekiti wa Chama Taifa, ni pamoja na ufanyaji na utoaji wa maamuzi, miongozo na usimamizi wa shughuli mbali mbali za chama na vile vile kukutana na wageni mbali mbali ambao huitembelea ofisi yake.

Ndani ya kipindi hiki cha miaka mitano, Mwenyekiti amekutana na viongozi mbali mbali wa chama, amezungumza na viongozi wa vyama tofauti vya kisiasa nchini, taasisi za kitaifa na kimataifa na pia amezungumza na waandishi wa habari.

Mnamo katikati na kuelekea mwishoni mwa mwaka 2007, Mwenyekiti hakuweza kufanya kazi nyingi za chama kutokana na kuhitajika kwenye majukumu mengine ya kimataifa yanayohusiana na taaluma yake ya uchumi. Taasisi ya Utafiti ijulikanayo kama African Economic Research Consortium (EARC) ilimpa jukumu la kutathmini shughuli zifanywazo na vyuo vikuu Yaoundé (Cameroon), Cape Town (Afrika Kusini), Swaziland, na Eduardo Moundlane (Msumbiji). Kazi hii aliifanya kuanzia Agosti, 2007.

Pia shughuli za Mwenyekiti katika taasisi za kimataifa ziliendelea tena hadi mwanzoni mwa mwaka 2008, ambapo alikuwa ameajiriwa kwa muda mfupi na Umoja wa Mataifa katika ofisi za Umoja huo, Geneva kushughulikia Mpango wa Upunguzaji Umasikini kwa Mataifa Masikini Duniani. Kwa kuwa, kwa mujibu wa katiba, shughuli za Mwenyekiti zinaweza kufanywa na Makamu Mwenyekiti inapotokezea Mwenyekiti hayupo, basi shughuli za ofisi ya Mwenyekiti zilihamishiwa kwenye ofisi ya Makamo Mwenyekiti kwa kipindi hiki chote.

2.3 Uimarishaji wa Chama

Kuimarisha Chama ni pamoja na kuitisha mikutano ya hadhara, kutembelea wilaya, majimbo ya uchaguzi na kutangaza misimamo na maazimio ya chama kwa umma.

Kuanzia mwishoni mwa mwaka 2006 hadi mwanzoni mwa mwaka 2007, Mwenyekiti alishiriki katika ufunguzi wa ofisi kadhaa za kata za Chama katika Wilaya za Dar es Salaam; alihutubia mikutano mingi ya hadhara, na aliwasilisha mada katika warsha na makongamano mbali mbali.

Miongoni mwa mikutano ya hadhara aliyohutubia Mwenyekiti katika kipindi hiki ni ule wa Novemba 2006 huko Wete, Pemba, ambapo Chama kiliitisha maandamano ya kumlaani Amani Karume kwa kauli zake zilizokuwa zinahatarisha kuuongeza mpasuko wa kisiasa wa Zanzibar.

Pia katika mwezi Disemba 2006, Mwenyekiti alikutana na Wabunge, Wawakilishi na Madiwani wa CUF kisiwani Pemba kuzungumza nao kuhusu nafasi na jukumu lao katika maendeleo ya kisiwa hicho.

Miongoni mwa ofisi za kata alizofungua ni ile ya Mzimuni, katika wilaya ya Kinondoni, tarehe 2 Januari, 2007; ambako pia alizungumza na wanachama na Jopo la Wazee wa wilaya ya Kinondoni.

Vile vile alifungua semina ya waratibu wa chama katika ukumbi wa Ofisi Kuu, Buguruni tarehe 13 Januari, 2007 na katika mwezi Novemba Mwenyekiti alifungua kikao cha Baraza Kuu la Wanawake kilichofanyika katika Mkoa wa Pwani.

Katika kipindi cha kati ya 2007 na 2008, suala la mazungumzo ya kutafuta suluhisho la kudumu la mpasuko wa kisiasa Zanzibar lilichukua nafasi kubwa ya shughuli za Ofisi ya Mwenyekiti katika dhana nzima ya uimarishaji wa Chama. Mara kadhaa, alipokuwa hayupo nchini Mwenyekiti alipaswa aidha kurudi mara moja au kutoa maagizo, matamko au misimamo ya kufuatwa na timu ya Chama kwenye mazungumzo hayo.

Kwa mfano, katika mwezi wa Agosti 2007, alipaswa kusitisha kwa muda shughuli zake za utafiti wa vyuo vikuu vya Afrika (AERC) kwa ajili ya kuja kuongoza kikao cha dharura cha Baraza Kuu la Uongozi la Taifa kilichoitishwa ili kujadili kusuasua kwa mazungumzo hayo na baada ya hapo akatoa tamko la kumtaka Rais Jakaya Kikwete kuingilia kati mazungumzo hayo au vyenginevyo CUF ingelijitoa ifikapo tarehe 14 ya mwezi huo.

Na baada ya upande wa pili wa mazungumzo hayo, yaani CCM, kuyavunja hapo mwezi Machi 2008, Mwenyekiti alifanya ziara kadhaa kwa taasisi mbali mbali za ndani ya nchi, ofisi za kibalozi, vyombo vya usalama, maandamano na mikutano ya hadhara ili kuwasilisha msimamo wa Chama, ambao ni kuwataka CCM kuheshimu na kusaini makubaliano yaliyofikiwa katika vikao vya timu za mazungumzo za vyama hivyo.

Kwa mfano, baina ya mwezi Aprili na Mei 2008, Mwenyekiti alikuwa amekutana na viongozi wakuu wa dini za Kikristo na Kiislamu kuwataka waingilie kati mazungumzo hayo, Mkuu wa Majeshi na Mkuu wa Jeshi la Polisi, viongozi wa Jumuiya ya Waandishi Habari Wanawake (TAMWA) na Jukwaa la Wahariri, jijini Dar es Salaam.

Maandamano na mikutano ya hadhara yalifanyika Unguja, Pemba, Dar es Salaam, Tanga na Tabora kati ya Mei 12 na Juni 6, 2008, ambamo mote ujumbe wa CUF ulikuwa ni mmoja tu: kusaini makubaliano na kuanza utekelezaji wake. Huo umekuwa ndio msimamo wa Chama hadi sasa.

Katika mwezi wa Aprili 2008, Mwenyekiti alikutana na wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam katika ukumbi wa Diamond Jubilee ili kufafanua hatua ya CCM kukiuka makubaliano ya mazungumzo kati yake na CUF, ikiwa ni kujibu hotuba ya Rais Kikwete kwa taifa, ambayo ilikuwa inajaribu kuhalalisha uamuzi wa chama chake wa kuja na ajenda mpya ya kura ya maoni kwenye mazungumzo hayo. Mwenyekiti alibainisha kuwa ajenda hiyo ilikuwa ni usanii na kiini macho cha kisiasa chenye dhamira ya kuikwamisha CUF na kwamba CUF haikuwa tayari kushirikiana na CCM kuwaghilibu Watanzania na walimwengu kwa ujumla kwa mazungumzo yasiyokwisha. Huo umekuwa ndio msingi wa ufafanuzi wa Chama hadi sasa juu ya kukwama kufikiwa kwa suluhisho la kudumu la mpasuko wa kisiasa wa Zanzibar.

Suala jengine ambalo limeshughulikiwa kikamilifu na Ofisi ya Mwenyekiti katika dhana hii ya uimarishaji wa chama ni kutoa matamko, muongozo na msimamo wa Chama kuhusiana na suala zima la ufisadi wa serikali za CCM. Tangu mwanzoni mwa mwaka 2005, Mwenyekiti, Profesa Ibrahim Lipumba amekuwa msemaji wa mara kwa mara juu ya namna ambavyo serikali ya CCM imekuwa ikishiriki katika ufisadi mkubwa unaoiangamiza nchi.

Kwa mfano, katika mwaka 2004 Mwenyekiti alikuwa ameonya juu ya ununuzi wa rada kutoka kwa kampuni ya BAE Systems ya Uingereza kwamba, kwanza rada yenyewe ilikuwa haihitajiki na pili ununuzi wenyewe ulikuwa una harufu kali ya rushwa.

Mwenyekiti alikuwa pia ameonya kuhusu ujenzi wa minara pacha ya Benki Kuu (BoT) kwamba ulikuwa umefanywa kwa gharama kubwa sana kuliko hali halisi na hivyo kuonesha kuwa palikuwa na rushwa. Mwenyekiti pia alionya kuhusu uanzishwaji, umiliki na uendeshwaji wa kampuni ya Meremeta Gold. Na juu ya yote, Mwenyekiti aliliweka bayana suala la kashfa ya Akaunti ya Madeni ya Nje ya BoT (EPA) na kuonesha kuwa kuna uchotaji mkubwa wa fedha za umma.

Katika siku za karibuni, baada ya suala hili kukua na kuchukua sura mpya ya kesi ya umma dhidi ya dola, mwezi Agosti 2008 Mwenyekiti aliitisha Kongamano Maalum, likiwa na mada ya “Ukosefu wa Uongozi na Hatima ya Tanzania”, katika ukumbi wa Diamond Jubilee kuzungumzia, ufisadi huo wa EPA pamoja na masuala ya kuporomoka kwa uchumi, hali ngumu za maisha ya wananchi, migomo ya wafanyakazi, migomo ya wanafunzi, nyufa katika Muungano, mpasuko wa kisiasa Zanzibar na migogoro ya kidini.

Katika mwezi Septemba 2008, Ofisi ya Mwenyekiti ilimuandikia Mkurugenzi wa Shirika la Fedha Duniani (IMF), Dominique Strauss-Kahn, kulilaumu shirika hilo kwa taarifa zilizokuwa zimeripotiwa kwamba limeridhika na hatua za Serikali ya Tanzania katika kushughulikia ufisadi wa EPA na hiyo kutoa tafsiri kwamba IMF iko tayari kuivumilia kutokuchua hatua za kisheria dhidi ya watuhumiwa. Baadaye Shirikika hilo lilijibu kwa njia ya kusambaza taarifa kwa waandishi wa habari kutokea New York, Marekani, kutoa msimamo wake ambao uliendana na matakwa ya Chama. Na ili kushinikiza watuhumiwa hao wa EPA wachukuliwe hatua, Mwenyekiti aliongoza maandamano makubwa ya Watanzania katika miji ya Dar es Salaam na Mwanza katika mwezi wa Oktoba 2008.

Dhana ya uimarishaji wa chama inahusu pia utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Chama, ambapo katika mwezi Septemba 2008, Mwenyekiti alifanya ziara maalum za Operation Strategic Planning Implementation (OSPI), kwa wilaya zote tatu za Mkoa wa Dar es Salaam. Alifanya ziara katika Wilaya ya Tanga Mjini kwa lengo la kushiriki kwenye sherehe za kuwapongenza wanachama na wananchi wa kata ya Ngamiani Kati na kata ya Chongoleani kwa ushindi walioupata katika chaguzi ndogo za Udiwani kwenye kata hizo. Pia alizindua Tume za Uchaguzi za CUF katika mwezi Oktoba 2008. Aidha katika mwezi wa Desemba, 2008 Mwenyekiti alifanya ziara katika Mikoa ya Lindi na Mtwara ambako alifungua matawi mapya na kuwapa wanachama wapya kadi za uanachama na kufanya mikutano ya hadhara. Tarehe 31 Januari, 2009 Mwenyekiti alishiriki katika mkutano wa hadhara wa Kumbukumbu ya Mauaji ya Wapigania Haki na Demokrasia waliouawa na Vikosi vya Ulinzi vya Serikali tarehe 26 -27 Januari, 2001 katika maandamano ya kudai kurudiwa kwa Uchaguzi Mkuu wa Zanziabr wa mwaka 2000. Katika Mkutano huo ambao ulifanyika Viwanja vya Kibandamaiti Zanzibar, Mwenyekiti wa Chama Taifa akiwa Mgeni Rasmi, alitoa hotuba kali ya kulaani mauaji hayo pamoja na vitendo vya ukandamizaji wa demokrasia nchini, kutahadharisha juu ya haja ya kuchukuliwa hatua za kuepusha matukio kama hayo kujirudia na kutaka iwekwe misingi ya kufanyika uchaguzi huru na wa haki ili kuheshimu matakwa ya wananchi.

2.4 Vikao vya Chama

Kwa mujibu wa Katiba, Mwenyekiti ana jukumu la kuongoza na kusimamia vikao vya juu vya Chama vikiwemo vikao vya Baraza Kuu la Uongozi la Taifa (BKUT) na Kamati ya Ulinzi na Usalama (KUU). Pia akiwa mwalikwa, huwa anahudhuria baadhi ya vikao vya Kamati ya Utendaji ya Taifa (KUT).

Ndani ya kipindi hiki cha miaka mitano, Mwenyekiti amekuwa akihudhuria vikao vyote hivyo, anapokuwa ndani ya nchi. Kwa mfano, mwishoni mwa mwaka 2006 aliongoza vikao vitatu vya KUU, alihudhuria kikao cha Disemba 2006 cha KUT na Februari 2007 aliongoza kikao cha kawaida cha BKUT, jijini Dar es Salaam; aliongoza kikao cha dharura cha BKUT cha Machi 17, 2008 mjini Zanzibar kuhusiana na Makubaliano yaliyofikiwa baina ya timu mbili za mazungumzo za vyama vya CUF na CCM juu ya kuupatia ufumbuzi wa kudumu mgogoro wa kisiasa wa Zanzibar na mwanzoni mwa mwezi Oktoba 2008, aliongoza kikao maalum cha kutathmini ziara za OSPI kwa wilaya tatu za Mkoa wa Dar es Salaam.

2.5 Mashirikiano na Vyama vya Siasa na Taasisi za Nchini

Kujenga mahusiano na mashirikiano kati ya Chama, kama taasisi ya kisiasa, na taasisi nyengine za kisiasa na ama zisizo za kisiasa ni katika majukumu ya Ofisi ya Mwenyekiti wa Chama Taifa. Nafasi ya mahusiano haya kwa Chama ni kubwa na muhimu sana katika kufikia malengo ya Chama.

Mawasiliano baina ya Chama na taasisi hizo yana faida kubwa tatu:

i) Kukiongezea Chama wigo wa kutambuliwa na kutambulika kama taasisi makini ya kisiasa;
ii) Kukichorea taswira nzuri mbele ya jumuiya na jamii husika;
iii) Kuvuna uzoefu wa kuongoza na kufanya kazi za siasa ya Chama.

Baina ya mwaka 2004 na 2009, Ofisi ya Mwenyekiti imeshiriki katika kuanzisha, kuendeleza na pia kustawisha mahusiano baina ya Chama na taasisi nyengine ndani ya nchi kwa kutumia njia mbili kubwa: moja ni kupitia ushirikiano wa vyama vinne vya CUF, CHADEMA, NCCR-Mageuzi na TLP na ya pili ni kupitia Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) kinachoundwa na vyama vya siasa vyenye uwakilishi Bungeni.

Suala la ushirikiano wa vyama vya upinzani lilishika kasi baada ya matokeo ya uchaguzi mkuu wa 2005. Ushirikiano katika shughuli za kisiasa ulianzishwa na Ofisi ya Mwenyekiti ilisimamia uhusiano baina ya CUF, CHADEMA, TLP na NCCR-Mageuzi. Chini ya kivuli cha ushirikiano huu, vyama hivyo vimeweza kuitisha maandamano, midahalo na mikutano mbali mbali ya hadhara katika kipindi cha kati ya mwaka 2006 na 2008.

Kwa mfano, Januari 2007 viongozi wa vyama hivyo waliongoza maandamano ya kuishinikiza serikali kuwachukulia hatua washiriki wa ununuzi wa rada uliofanyika mwishoni mwa miaka ya ’90 na kuendesha uchunguzi wa kina wa kashfa ya ununuzi wa rada hiyo.

Katika mwezi huo huo pia, Mwenyekiti alifungua mjadala wa kitaifa kuhusu hoja na haja ya Katiba Mpya katika kongamano lililoandaliwa na CUF na kuhudhuriwa na taasisi mbali mbali za kisiasa, kidini, kijamii na wasomi jijini Dar es Salaam.

Kwenye mwezi wa Juni na Julai 2007, ushirikiano huo wa vyama ulifanya ziara katika mikoa ya Kigoma na Kagera na Ofisi ya Mwenyekiti ilishiriki kikamilifu katika ziara hizo zilizosaidia kukieneza Chama kwa wapiga kura chini ya mwamvuli wa ushirikiano.

Katika mwezi Juni 2008, Mwenyekiti na mwenzake wa Chadema walihudhuria chakula maalum kilichotayarishwa na Wabunge wa Upinzani na Mwenyekiti aliwahutubia wabunge hao katika ofisi za Bunge mjini Dodoma kuhusiana na dhima yao katika uchambuzi wa Bajeti ya Serikali.

Pia, kwa kuwa CUF ni mwanachama mwanzilishi wa Kituo cha Demokrasia cha Tanzania (TCD), Mwenyekiti amekuwa akihudhuria katika vikao vya Kituo hiki tangu kuanzishwa kwake. Disemba 2006, kwa mfano, alishiriki katika mkutano wa vyama 42 vya Afrika ulioandaliwa na TCD jijini Dar es Salaam.

Katika viongozi wa taasisi za ndani, Mwenyekiti alionana na kufanya mazungumzo na Askofu Selvester Gamanywa ambaye ni Kiongozi wa Kanisa la Pentecoste nchini, Askofu mstaafu Eliezer Sandoro wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Kiongozi wa Shura ya Maimamu Tanzania Sheikh Mussa Kundecha na Sheikh Issa Ponda, Askofu Mokiwa wa Kanisa la Anglikana, Muadhama Kadinali Policarp Pengo wa Kanisa Katoliki Tanzania, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama nchini CDF Mwamunyange, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) Bw. Saidi Mwema, Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA), Ananilea Nkya, na Mheshimiwa Edward Lowassa (akiwa Waziri Mkuu) na Mheshimiwa John Malecela (Waziri Mkuu mstaafu).

2.6 Mikutano na Vyombo vya Habari

Nafasi ya vyombo vya habari katika kujenga ama kubomoa taswira ya Chama ni kubwa na ina umuhimu wa pekee. Chama imara ni lazima kiwe na mkakati wa kujijenga mbele ya vyombo vya habari ili vyombo hivyo visaidie katika kuisambaza taswira njema ya Chama kwa umma. Kwa kuelewa umuhimu wa hilo, ndiyo maana Chama kimempa wajibu Mwenyekiti wake wa kuwa msemaji wake mkuu. Hili limesaidia sana kujenga taswira ya Chama chenye uongozi ulio makini.

Kwa kipindi cha miaka mitano hii, Mwenyekiti, kwa niaba ya Chama, amekuwa akitumia nafasi yake kuwasiliana na umma kupitia vyombo hivyo vya habari, ambapo amekuwa akiibua hoja, kujibu hoja, kushauri, kukosoa na hata kuipongeza serikali pale anapoona kuwa inastahiki kupongezwa.

Amekuwa akifanya hivyo ama kwa kutumia njia ya Taarifa kwa Vyombo vya Habari, Mikutano na Waandishi wa Habari au kwa njia ya kufanya mahojiano ya moja kwa moja na vyombo hivyo au wawakilishi wao. Mahojiano hayo yamefanywa kwa kupitia vyombo vya ndani na nje ya Tanzania.

Kwa mfano, kuelekea Kumbukumbu za Mauaji ya Januari 2001 za mwaka 2007, Mwenyekiti alizungumza na waandishi wa habari kuhusu maafa hayo, akikumbushia ahadi za Rais mstaafu Benjamin Mkapa na pia mapendekezo ya Tume ya Hashim Mbita juu ya mauaji hayo.

Hadi kufikia Agosti 2007, tayari kulikuwa na kila dalili za kukwama kwa mazungumzo ya kutafuta suluhu ya kisiasa ya Zanzibar na Mwenyekiti alitumia vyema vyombo vya habari kuwasilisha msimamo wa Chama kwa jambo hilo. Tangu hapo, hadi sasa imani ya vyombo vingi vya habari kuhusiana na mazungumzo hayo imekuwa ni ukweli kwamba CUF ilitimiza wajibu wake kama taasisi ya kisiasa, lakini CCM ikashindwa kuheshimu kauli yake.

Taarifa hii inatambua kuwa Mwenyekiti amekuwa akionekana na kusikikana mara kwa mara kwenye vyombo vya habari vya ndani na nje, jambo ambalo limekijengea jina Chama miongoni mwa hadhira za vyombo hivyo. Mfano wa vyombo ambavyo ujumbe wa Mwenyekiti umekuwa ukipatikana kwa kipindi hiki ni Televisheni ya Taifa (TBC1), Channel 10, Star TV, ITV, Times FM Radio, Wapo Radio, Radio Mlimani, Voice of America, Deutsche Welle, Australian TV (kupitia kipindi cha Foreign Correspondents) BBC, Radio France International, Idhaa ya Kiswahili ya Radio Iran, magazeti takriban yote yanayochapishwa kwa lugha za Kiswahili na Kiingereza nchini na mitandao mbalimbali.

2.7 Mazungumzo na Wageni, Mabalozi na Uhusiano na Jumuiya ya Kimataifa

Kujijenga kwenye jukwaa la kimataifa ni jambo la lazima kwa vyama vya siasa si kwa sababu tu ya kupata mashirikiano na misaada ya kugharamia harakati za kisiasa, ambazo ni ghali sana bila ya misaada ya kifedha na au vitendea kazi, bali pia kwa kwa sababu jumuiya ya kimataifa ikitaka inaweza kuzibana serikali za kidhalimu kama ya kwetu kuheshimu haki za binaadamu na maamuzi ya kidemokrasia.

Ofisi ya Mwenyekiti imekuwa ikijitahidi kujenga mahusiano na jumuiya ya kimataifa kwa kuwasilisha na kufafanua hoja mbali mbali za CUF na haja ya kuheshimiwa kwa maamuzi ya umma kupitia kura. Pia Ofisi hii imekuwa ikitumia fursa yake ya kukutana na wawakilishi wa jumuiya ya kimataifa kujenga taswira yake na kuonesha nini Chama inachokisimamia.

Ofisi hii imekuwa ikitumia njia mbili katika kufanikisha lengo hili la kuwa karibu na jumuiya ya kimataifa: moja ni kupitia ziara za wageni au mabalozi wa nchi za nje waliopo nchini, na pili ni kupitia mtandao wa Liberal International (LI) na au African Liberal Network (ALN), ambayo CUF ni mwanachama wake.

Njia ya pili ni kupitia ziara zinazofanywa na mabalozi katika ofisi za CUF. Kwa mfano, katika mwezi Oktoba 2006 Mwenyekiti alikutana kwa mazungumzo na aliyekuwa Balozi wa Marekani nchini wakati huo, Michael Ritzer, na Mkurugenzi Mdogo anayehusika na masuala ya Afrika katika Serikali ya Marekani, Bi Deborah R. Malac. Mazungumzo hayo yalihusu hali ya kisiasa ya Zanzibar, haja ya kuundwa kwa Tume mpya ya Uchaguzi, hali ya kilimo nchini na sera ya CUF kuhusiana na sekta hiyo.

Disemba 2006, Mwenyekiti alizungumza na Balozi Mdogo wa Ujerumani, Ingo Herbert, kuhusiana na suala hilo hilo la Zanzibar na Januari 2007 alikutana na Balozi Mdogo wa Cuba kuzungumzia, pamoja na mengine, sera ya Marekani kuelekea Cuba.

Juni 2008, Ofisi ya Mwenyekiti ilifanya mazungumzo na ujumbe wa Centre Party (Hoyre) of Norway ukiwa na Bi Inger Bigum, Bi Anna Marie na Bi Appie Mkoba, kuhusiana na masuala kadhaa ya kimaendeleo. Chama hicho kinasaidia miradi ya maendeleo ya elimu wilayani Magu, ambapo CUF ni miongoni mwa vyama vinavyoshiriki katika usimamizi wake.

Julai 2008, Mwenyekiti aliupokea ofisini kwake na kufanya mazungumzo na ujumbe wa wabunge saba kutoka Bunge la Uingereza. Alizungumza nao kuhusu hali ya kisiasa ya Zanzibar, muundo wa Chama, uwakilishi Bungeni, Ufisadi na Sera ya Nje ya CUF.

Mwezi Oktoba 2008, Mwenyekiti alifanya mazungumzo na ugeni kutoka Taasisi ya Friedrich Naumann Foundation (FNSt) ya Ujerumani. Maofisa, viongozi na watendaji mbali mbali wa CUF wamekuwa wakipokea mafunzo kwa msaada wa taasisi hii tangu mwaka 2004.

Kupitia mitandano ya Kiliberali ya LI na ALN, Mwenyekiti alihudhuria Mkutano Mkuu wa LI Novemba 2006 uliofanyika Marrakesh, Morocco, ambako alitoa mada ‘Democracy and Economic Development in Africa.’ Sambamba na mkutano huo kulifanyika mkutano wa kujadili rasimu ya katiba ya ya ALN ambayo ilikuja kupitishwa na mkutano wa ALN wa Dakar, Senegal, Februari 2007. Mwenyekiti pia alifanya mazungumzo na wajumbe wa vyama rafiki vya VENSTRE cha Norway, Democratic Progressive Party (DPP) cha Taiwan na Liberal Party cha Sweden.

Baina ya mwezi Januari na Februari 2007, Mwenyekiti alihudhuria kongamano linalohusu Lobbying and Advocacy sambamba na mkutano mkuu wa ALN jijini Dakar, Senegal.

Mwenyekiti pia katika kipindi hiki alionana na Rais Abdilaye Wade wa Senegeal, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Bwana Don MacKinon, Kiongozi wa Chama Cha Democratic Alliance (DA) na Mkuu wa Upinzani katika Bunge la Afrika Kusini, Bw. Tony Leon.

Matokeo ya ushiriki huu wa ofisi ya Mwenyekiti kwa shughuli hizi zinazoiunganisha CUF na jukwaa la kimataifa ni kukijengea heshima Chama na kukipa nafasi yake katika siasa za kilimwengu. Miongoni mwa mafanikio yake ni kuchaguliwa kwa Mjumbe wa BKUT, Mhe. Ismail Jussa, kuwa Makamo wa Rais wa ALN kwa Kanda ya Afrika Mashariki.

2.8 Kuhudhuria Shughuli Rasmi za Kiserikali na za Kijamii

CUF ni chama cha kitaifa kinachosimamia utaifa wa Taifa hili. Linapokuja suala la kitaifa, Chama hiki hufuata utaratibu ule ule wa kizalendo na kuchukua nafasi yake kwa suala kama hilo. Kwa msingi huo, Mwenyekiti amekuwa akihudhuria shughuli zote za kitaifa za nchi zikiwemo maadhimisho ya Uhuru wa Tanganyika, Muungano, Siku za Ukimwi, Maalbino, Watu Wenye Ulemavu na hata misiba ya kitaifa.

CUF pia ni Chama Cha Wananchi kwa maana yake halisi; kimeundwa na kinaongozwa na wananchi na kinashughulika na mambo ya wananchi. Linapokuja suala linalohusu mambo ya jamii, chama hiki huchukua msimamo na mtazamo wa kijamii. Wakati wowote, kwa hivyo, linapotokea tukio la kitaifa na au kijamii, Mwenyekiti anapokuwa nchini, hushiriki.

Katika kipindi cha miaka mitano, 2004 hadi 2009, Mwenyekiti alipewa mwaliko na alihudhuria kwenye kikao cha bajeti cha 2008/2009, na pia alihudhuria msiba wa Marehemu Juma Jamaldin Akukweti mwanzoni mwa mwaka 2007.

Mwenyekiti pia alishiriki katika mechi ya kirafiki baina ya Timu ya Taifa ya Tanzania na ya Congo Disemba, 2006. Alihudhuria mazishi ya Mwenyekiti wa CUF kata ya Mburahati, Mhe. Said Duwiya, Disemba 2007; mazishi ya Mhe. Jokha Kassim aliyekuwa Kiongozi wa Wanawake Temeke, na ya Mhe. Ghania Solanji, aliyekuwa Katibu wa Serikali ya Mtaa wa Mtogole kupitia CUF, Februari 2007.

SURA YA TATU

OFISI YA MAKAMO MWENYEKITI

3.1 Utangulizi

Kifungu cha 69 cha Katiba ya Chama ya 1992 (Toleo la 2003) ndicho kinachoanzisha nafasi ya Makamo Mwenyekiti na, hivyo Ofisi yake, na pia kuorodhesha majukumu yake.

Kimsingi, Makamo Mwenyekiti ndiye msaidizi na mshauri mkuu wa Mwenyekiti wa Chama katika ngazi ya kitaifa na pia amepewa jukumu mahsusi la kusimamia utekelezaji wa Itikadi ya Utajirisho na Tume ya Uchumi na Ustawi wa Taifa.

Majukumu mengine ya Makamo Mwenyekiti ni yale yale ya Mwenyekiti hasa katika mazingira ambapo Mwenyekiti anakuwa hayupo.

Maeneo yafuatayo yanaangaliwa na Taarifa hii kama kipimo cha utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Makamo Mwenyekiti kwa kipindi cha 2004 – 2009:

i) Kazi za Ofisi
ii) Vikao vya Chama
iii) Uimarishaji wa Chama na Shughuli za Kijamii

Mkutano Mkuu wa Taifa wa Tatu (23 – 28 Februari, 2004) ulimchagua Mheshimiwa Machano Khamis Ali, kutoka Zanzibar, kuwa Makamo Mwenyekiti wa Chama ambapo ameshikilia wadhifa huo hadi sasa. Mheshimiwa Machano ametumia busara na hekima katika kukabiliana na changamoto kadhaa alipokuwa anatekeleza majukumu yake.

3.2 Kazi za Ofisi

Makamo Mwenyekiti ana makao yake makuu Zanzibar na hivyo kazi zake za kiofisi zinafanyika zaidi akiwa Zanzibar na pia kwa kile kipindi anachokuwa Tanzania Bara. Kazi za ofisi zinahusisha, pamoja na mengine, kufanya maamuzi, kutoa muongozo, kufuatilia maamuzi yaliyokwishafanywa na vikao vya juu vya uongozi, na kukutana na wageni wa Chama.

Kwa kipindi hiki cha miaka mitano, Makamo Mwenyekiti amekuwa akionana na wageni mbali mbali wa Chama, wazee na wanachama wa kawaida ofisini kwake kujadili na kubadilishana mawazo kuhusu mwenendo na maendeleo ya Chama na maombi binafsi ya wanachama.

Vile vile amekuwa akionana na baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani kushauriana kuhusu mustakbali wa kisiasa nchini.

Mwishoni mwa mwaka 2006 Makamo Mwenyekiti alionana na mmiliki wa nyumba inayotumiwa na Chama kama ofisi ya Jimbo la Konde, kisiwani Pemba kujadiliana kuhusu matengenezo ya nyumba hiyo ambayo mmiliki huyo aliitoa kwa Chama ikiwa nzima, lakini haijafanyiwa matengenezo yoyote hadi sasa licha ya kuwa mbovu.

Katika kujenga mahusiano mema baina ya Chama na vyama vingine vya kisiasa, mwezi Juni 2007 Makamo Mwenyekiti alialikwa na kuhudhuria kufungua Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa Chama cha NRA uliofanyika Zanzibar. Vile vile aliteuliwa kuwa mjumbe wa TCD kutoka Chama Cha Wananchi (CUF).

Kwa kipindi cha kuanzia 2006 hadi sasa, hali ya kisiasa Zanzibar imekuwa ikichukua nafasi kubwa ya mwenendo na utamaduni wa siasa za visiwa hivyo na limekuwa ni jukumu la Makamo Mwenyekiti kutoa mwelekeo na msimamo wa Chama panapohusika masuala kama vile kukwama kwa mazungumzo ya CUF na CCM, mjadala wa hadhi ya Zanzibar kwenye Muungano, n.k.

Katika mwezi Juni 2007, Makamo Mwenyekiti alionana na wazee wa Jimbo la Makunduchi, alikuwa mgeni rasmi katika Kongamano la Wanawake na pia katika Mkutano Mkuu wa Wilaya ya Mjini Unguja.

3.3 Vikao vya Chama

Makamo Mwenyekiti amehudhuria takriban vikao vyote vya kawaida vya Chama ambavyo vimefanyika na yeye akiwapo ndani ya nchi.

Makamo Mwenyekiti alihudhuria na kushiriki kwa ukamilifu katika vikao vyote vya Baraza Kuu la Uongozi la Taifa na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Taifa. Pale ambapo Mwenyekiti hakuweza kuhudhuria, Makamu Mwenyekiti aliviongoza vikao hivyo kwa umakini mkubwa.
.
Mbali ya vikao hivyo, amehudhuria kwa mwaliko baadhi ya vikao vya Kamati ya Uendaji ya Taifa kwa mfano Disemba 2007, KUT iliitisha mkutano wa dharura kuhusiana na Hali ya Kisiasa Nchini na Hatua za Tanzania kujiunga na Shirikisho la Afrika Mashariki.

Makamo Mwenyekiti amekuwa akishiriki vikao vya BKUT vya tathmini ya OSPI katika Makao Makuu na pia vikao vya Kamati ya Utendaji ya Wilaya ya Mjini ambavyo yeye ni mjumbe wake.

3.4 Uimarishaji wa Chama

Uimarishaji wa Chama huanza katika ngazi za chini kama ulivyo Muongozo wa Mpango Mkakati wa Chama. Kukiimarisha Chama kunamaanisha kuwa na viongozi na wanachama wanaofanya kazi ya kitaasisi ya Chama kuanzia chini hadi juu. Hili huweza kufanyika kwa njia za ziara, tathmini na uhakiki wa Chama na kusimamia uimarikaji wa taasisi za Chama. Njia hii huitwa harakati za kuimarisha Chama ndani ya Chama. Limekuwa ni jukumu la Makamo Mwenyekiti kuona hilo linafanyika.

Kuimarisha Chama pia kunamaanisha kukikaribisha Chama kwa wananchi hata wasiokuwa wanachama ili wakijue na wakiamini. Kuwavuta wananchi wengine kuja kwenye Chama kunahitaji kukutana nao, kufanya mikutano, maandamano, makongamano na njia nyengine za kujenga madaraja ya mawasiliano. Hizi ni harakati za kuimarisha Chama nje ya Chama. Limekuwa pia ni jukumu la Makamo Mwenyekiti kushiriki katika njia hizo za mawasiliano.

Kwa upande wa harakati za kuimarisha Chama ndani ya Chama, Makamo Mwenyekiti amekuwa akishiriki katika kazi za kuimarisha taasisi zilizopo tayari na pia kuanzisha mpya kwa mujibu wa Katiba. Kwa mfano, Makamo Mwenyekiti alizindua mafunzo ya Blue Guards wa Wilaya sita za Unguja na alikuwa mgeni rasmi katika ufungaji wa mafunzo kama hayo kwa Kanda ya Dar es Salaam kati ya mwezi Novemba 2006 na Februari 2007. Katika kipindi hicho hicho alizindua kikao cha mwanzo cha Kamati ya Viongozi wa Wilaya za Unguja.

Ndani ya mwezi wa Juni 2007, Makamo alifanya ziara kwa Mkoa mzima wa Dar es Salaam kuhamasisha ushiriki wa wanachama katika uchaguzi wa ndani ambao ulifanyika mwaka huo na katika mwezi uliofuatia wa Julai alishiriki kwenye mafunzo ya Mpango Mkakati wa Chama yaliyofanyika White Sands Hotel, Dar es Salaam. Mwezi wa Agosti na Septemba 2007, Makamo alikuwa katika ziara refu ya kuimarisha Chama katika mikoa ya Mtwara, Lindi, Ruvuma (Kanda ya Kusini) na mikoa ya Mwanza na Kagera (Kanda ya Ziwa) ambako alifungua matawi mapya, alipokea wanachama wapya na alihakiki uhai na utendaji wa Chama katika maeneo hayo.

Shughuli za Makamo Mwenyekiti kuimarisha Chama ndani ya Chama katika mwaka 2008 zilijumuisha jitihada kubwa ya kutatua migogoro katika wilaya za Kinondoni na Kisarawe na ziara katika mikoa ya Kigoma na Rukwa katika mwezi wa Februari kutathmini uhai na utendaji kazi wa Chama. Katika mwezi Mei alifanya ziara kama hiyo kwenye wilaya sita za Unguja na kuzindua rasmi wajasiri wa Chama wa wilaya ya Kusini Unguja katika mwezi wa Juni, 2008.

Kuanzia mwezi Julai 2008 hadi sasa, Makamo amekuwa mshiriki wa moja kwa moja wa Operesheni Chukua Nchi iliyopangwa katika Kisiwa cha Unguja, ambapo amekuwa akizungumza na Wenyeviti wa Wilaya angalau kila mwezi mara moja ofisini kwake, Zanzibar. Makamo pia amefanya ziara ya majimbo 19 ya Unguja katika mwezi Septemba, 2008 ikiwa ni sehemu ya Operesheni hii. Hizo zote ni miongoni mwa harakati za uimarishaji Chama ndani ya Chama.

Katika shughuli za uimarishaji Chama nje ya Chama, ambapo muelekeo ni kuvuna uungwaji mkono kutoka kwa makundi mengine ambayo bado hayajawa wanachama wetu kwa kujenga taswira ya kuaminika na kukubalika, Makamo ameshiriki katika matukio kadhaa yakiwemo maandamano, mikutano ya hadhara, makongamano, na shughuli za kijamii.

Kwa mfano, Makamo alishiriki katika maandamano ya kupinga kauli ya Amani Karume kuhusu kutokuwepo kwa mpasuko wa kisiasa Zanzibar, yaliyofanyika Wete, Pemba katika mwezi Novemba 2006. Alifanya mazungumzo maalum na uongozi wa chama cha NRA Zanzibar katika mwezi Julai, 2008 na pia kwenye shughuli mbali mbali za kijamii, ziwe za furaha au za misiba, zilizowapata aidha wanachama au wananchi wa kawaida katika kipindi hiki. Makamo amehudhuria kwenye mazishi, matukio yanayohitaji misaada na katika sherehe za harusi, mialiko ya futari na kadhalika, yakiwemo mazishi ya mwanzilishi wa CUF, Mhe. Masoud Omar Said wa Wete, Pemba Mei 2008 na ya Mzee Ali Hamad (Mzee Khator) huko Kambini Pemba, Disemba, 2008.

Kumbukumbu za Mauaji ya Januari 2001 katika mwaka 2007 zilifanyika kwa maeneo, ambapo Makamo alishiriki katika kumbukumbu hizo kisiwani Pemba kwa kuwaombea marehemu katika Wilaya ya Micheweni. Vile vile alishiriki katika maadhimisho hayo katika mkutano wa hadhara uliofanyika tarehe 31 Januari, 2009 katika Viwanja vya Kibandamaiti, Zanzibar. Aidha Makamo Mwenyekiti alifanya ziara za kuzitambulisha Sekretarieti za Vijana na Wazee katika wilaya zote sita za Unguja katika mwezi wa Disemba, 2008 na Februari, 2009.

SURA YA NNE

OFISI YA KATIBU MKUU

4.1 Utangulizi

Kifungu cha 70 (1) – (3) ndicho kinachoanzisha nafasi ya Katibu Mkuu wa Chama, majukumu na wajibu wake. Kifungu hicho kinamueleza kuwa yeye ndiye muwajibikaji mkuu wa shughuli zote za utendaji za chama kitaifa, kwamba ndiye dhamana wa ofisi za Makao Makuu na Ofisi Kuu ya Chama na kwamba ndiye muwajibikaji mkuu wa mali na fedha zote za Chama katika ngazi ya Taifa.

Kazi nyengine za ofisi ya Katibu Mkuu ni kujenga mahusiano mema na ofisi nyengine kama hiyo kutoka vyama vyengine ndani na nje ya nchi na kuhifadhi kumbukumbu zote za kimaandishi za Chama.

Katika kuangalia utekelezaji wa majukumu hayo, Taarifa hii inayagawa katika mafungu yafuatayo:

i) Kazi za Ofisini na Vikao vya Chama
ii) Uimarishaji wa Chama
iii) Shughuli za Kijamii na za Kitaifa
iv) Mahusiano na Vyombo vya Habari
v) Mgogoro wa Kisiasa Zanzibar
vi) Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa
vii) Uangalizi wa Mahesabu ya Ndani
viii) Udhibiti wa Utekelezaji Mkakati wa Chama (Strategic Plan)

Mkutano Mkuu wa Taifa wa Tatu (23 – 28 Februari, 2004) ulimchagua Maalim Seif Sharif Hamad kuwa Katibu Mkuu wa Chama na ameendelea na wadhifa huo hadi sasa.

4.2 Kazi za Ofisini na Vikao vya Chama

Kazi za ofisini zinajumuisha kusimamia na kufanya vikao vya kawaida na vya dharura vya chama pamoja na kusimamia utekelezaji wa maamuzi yaliyoamuliwa na vikao vya juu ya Chama na ambayo, kama mwajibikaji mkuu wa shughuli za utendaji, anapaswa kuyasimamia. Pia kazi hizi hujumuisha kupokea na kuzungumza na wageni mbali mbali wanaotembelea Ofisi ya Katibu Mkuu.

Vikao vya kawaida kwa mujibu wa Katiba ni pamoja na vya Kamati ya Utendaji ya Taifa, Baraza Kuu la Uongozi la Taifa na Kamati ya Ulinzi na Usalama; na vikao vya dharura vinaweza kufanyika wakati wowote kutokana na haja maalum inayojitokeza. Kwa kipindi chote hiki, Ofisi ya Katibu Mkuu imesimamia kuona kwamba vikao vyote hivyo vimefanyika kama inavyohitajika kwa mujibu wa Katiba ya Chama na kwa kiasi kikubwa ndiyo msingi wa kujengeka CUF kitaasisi na kuepuka migogoro ya ndani.

Miongoni mwa wageni waliotembelea na kupokewa na Ofisi ya Katibu Mkuu kwa mazungumzo katika kipindi cha miezi ya Julai – Septemba 2004, ni Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa, na Naibu wake, Mwakilishi Mkaazi wa NDI wa Nairobi. (Kwa wageni wa kimataifa, Sura ya Saba ya Taarifa hii inazungumzia kwa urefu masuala hayo)

Katika mwezi wa Januari 2007, Katibu Mkuu alifanya vikao vya ndani na wajumbe wa BKUT, viongozi wa wilaya, majimbo, kata, mabaraza ya wanawake na vijana na makamanda wa Blue Guards (BG) katika maeneo ya Unguja, Dar es Salaam na Pemba kwa madhumuni ya kuwapa taarifa kuhusiana na hatua za utatuzi wa mgogoro wa Zanzibar na mtazamo wa CUF kuhusu uharakishwaji wa uundwaji wa Shirikisho la Afrika Mashariki.

Baina ya Juni na Septemba 2007, Katibu Mkuu alihudhuria vikao vyote vya Chama ambapo miongoni mwao ni vile vya KUT, BKUT, na KUU.

4.3 Uimarishaji wa Chama

Baina ya Julai na Septemba 2004, Katibu Mkuu alifanya mikutano ya hadhara Tanzania Bara na Zanzibar na kushiriki katika maandamano ya uhamasishaji katika mikoa ya Kagera, Mwanza na Dar es Salaam. Pia alifanya ziara fupi fupi katika wilaya za Kondoa (Dodoma), Muheza (Tanga) na Mkuranga (Pwani). Ziara kama hiyo ambayo ilipangwa kufanyika katika jimbo la Donge (Kaskazini Unguja) ilizuiliwa mara mbili na Jeshi la Polisi kwa maelezo kwamba wakaazi wa huko hawataki.

Katika mwezi wa Julai mwaka 2004, Katibu Mkuu alifanya ziara za kuhakiki Chama katika wilaya zote nne za kisiwa cha Pemba. Katika tathmini ya ziara hizo Katibu Mkuu aligundua na kurekebisha mapungufu mbali mbali ya Chama kama vile ukosefu wa vikao vya kikatiba na wanachama kutolipa ada zao za uanachama. Ziara kama hiyo pia ilifanyika katika kisiwa cha Unguja mnamo mwezi Septemba 2004 na hivyo tathmini na uhakiki ukafanyika katika wilaya zote za Unguja.

Katibu Mkuu pia alitumia ziara hizo za Unguja na Pemba kuhamasisha wanachama na wapenzi wa Chama kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, ambalo lilikuwa lianze tarehe 1 Novemba, 2004. Mwaka 2005 ulikuwa ni mwaka wa Uchaguzi Mkuu Tanzania. Katibu Mkuu alitumia muda wote kwa maandalizi ya uchaguzi, uhamasishaji wa wapiga kura, kufanya kampeni nchi nzima na kujiandaa kwa uchaguzi kama mgombea kiti cha Urais wa Zanzibar. Katibu Mkuu alipata mafanikio makubwa kwa vile wananchi walivyojitokeza kupiga kura na kukiunga mkono Chama licha ya wizi wa kura na kuporwa kwa ushindi uliofanywa na CCM ikisaidiwa na Serikali zake na vyombo vya dola kwa mara ya tatu mfululizo.

Katika mwezi wa Novemba 2006, Ofisi ya Katibu Mkuu ilifanikisha kuandaa, kuendesha na kusimamia mafunzo maalum kwa Wakurugenzi na Watendaji wote wa Makao Makuu na Ofisi Kuu kuhusiana na Mkakati wa Chama na Majukumu ya Kila Kurugenzi, Maadili ya Uongozi, Dhana ya Ulinzi katika Chama na Uongozi Mpya katika Chama kwa Viongozi na Watendaji wa Kitaifa yaliyofanyika katika Hoteli ya Belinda Ocean Resort, Dar es Salaam.

Baina ya Juni na Oktoba 2007, Chama kilikuwa na chaguzi zake za ndani na Katibu Mkuu alishiriki kikamilifu katika chaguzi hizo, ikiwa ni pamoja na kutatua migogoro na matatizo yanayohusiana na chaguzi. Kwa mfano, ndani ya kipindi hicho, Katibu Mkuu alifanya ziara katika mikoa ya Tanga, Morogoro na Pwani, ambako baadhi ya wilaya zilikumbwa na matatizo ya kiutendaji na kisiasa na akatoa muongozo wa kufuatwa kutatua matatizo na migogoro hiyo.

Pemba imekuwa ikihesabiwa kuwa ngome kuu ya Chama na Mkakati wa Chama unaelekeza kuendelea kuidhibiti kwa muda wote. Katika kuhakikisha lengo hilo, Katibu Mkuu alifanya ziara ya kisiwa cha Pemba Novemba 2007, ambapo alizungumza na viongozi wa ngazi zote za Chama, na kupitia wilaya zote, majimbo yote na mkusanyiko wa matawi karibu yote. Kwa kiwango cha ndani ya Chama, ziara hiyo ilihitimishwa kwa mkutano wa mjumuiko wa viongozi wote wa Chama kisiwani Pemba, kwenye ukumbi wa mikutano wa Madungu, Chake Chake, Pemba, ambapo kwa kiwango cha nje ya Chama, Katibu Mkuu alikuwa akihutubia katika mikutano ya hadhara iliyokuwa ikifanyika katika kila wilaya baada ya kumalizika kwa ziara kwenye wilaya husika. Wilaya hizo ni Micheweni, Wete, Mkoani na Chake Chake.

Kwa kuwa Mwenyekiti wa Chama Taifa, Prof. Ibrahim Lipumba, alikuwa nje ya nchi kwa kipindi chote cha mwisho wa mwaka 2007, Chama kiliamua kufanya kurejea kwake kuwa ni tukio kubwa na hivyo ikaamuliwa kufanya mapokezi makubwa ya Januari 27, 2008 ambayo yalikuwa yanaambatana na maadhimisho ya Kumbukumbu ya Mauaji ya Januari 26 na 27, 2001. Katibu Mkuu, kwa hivyo, akafanya ziara ya wilaya zote za mkoa wa Dar es Salaam kuhamasisha mapokezi hayo.

Sambamba na hilo, Katibu Mkuu alitekeleza agizo la BKUT lililotaka Wabunge na wajumbe wa BLW kuelezwa juu ya utendaji wao wa kazi, kukosolewa na kutakiwa kujirekebisha katika mkutano wake na viongozi hao uliofanyika mwishoni mwa mwezi Novemba, 2008 huko Mtambile kisiwani Pemba.

Mwezi Januari 2008, ikiwa ni miezi 7 baada ya kuanzishwa kwa ushirikiano usiokuwa rasmi wa vyama vinne vya siasa (CUF, CHADEMA, TLP, na NCCR-Mageuzi), CUF iliandaa Kongamano la Katiba Mpya kwenye Hoteli ya Peacock, Dar es Salaam, na Katibu Mkuu akapewa jukumu na Kongamano hilo la kuteua Kamati ya watu watano ya kumalizia rasimu ya Katiba Mpya na kuiwasilisha kwa wananchi.

Baina ya Februari hadi Juni 2008, Katibu Mkuu alifanya ziara katika visiwa vya Unguja na Pemba na mikoa ya Dar es Salaam na Tanga, ambapo ziara yake ya kisiwa cha Unguja ya mwezi wa Machi ilirikodiwa kama ya aina ya kipekee kwa kufufua kwake ari na msisimko mpya wa wanachama, hasa baada ya kulegalega na hatimaye kuvunjika kwa mazungumzo baina ya CUF na CCM. Ziara hii ilikipatia Chama wanachama wapya zaidi ya 3,947.

Katika ziara za mikoa ya Dar es Salaam na Tanga, Katibu Mkuu alifanya mikutano ya ndani na ya hadhara iliyolenga kuhakiki, kuhamasisha na kuimarisha nguvu za Chama katika maeneo haya ya Mpango Mkakati.

Baina ya Julai na Oktoba 2008, kazi ya uimarishaji chama katika wilaya za Pemba na Unguja iliendelea na kufanya mikutano miwili ya hadhara mahsusi kuzungumzia msimamo wa CUF juu ya hadhi ya Zanzibar kwenye Muungano na nishati ya Mafuta. Ndani ya kipindi hiki pia, Katibu Mkuu aliendeleza Operesheni Chukua Nchi kwa kufanya mkutano wa hadhara katika jimbo la Chaani, Kaskazini Unguja, kujibu hotuba ya Rais Jakaya Kikwete ya Agosti 2008, Bungeni, juu ya hadhi ya Zanzibar.

Mikutano hii ya Zanzibar imewekwa kwenye rikodi kama nyenzo zilizosaidia sana kujenga umoja wa Wazanzibari, kama ilivyo sera na mtazamo wa CUF, na kupunguza tofauti baina ya wafuasi wa CUF na CCM visiwani Zanzibar. Vile vile mikutano imeongeza heshima ya Chama miongoni mwa Wazanzibari wanaoamini kuwa ni CUF tu ndiyo inayosimamia maslahi ya Zanzibar huku ikileta hasara kubwa kwa CCM ambayo imepoteza imani ya hata wanachama wake shupavu wanaokiona kuwa hakisimamii maslahi ya Zanzibar na Wazanzibari ndani ya Muungano.

Ndani ya kipindi hicho pia Katibu Mkuu alihudhuria semina za Operation Strategic Plan Implementation (OSPI) na mafunzo kwa Wajasiri wa Chama, Zanzibar na Tanzania Bara pamoja na kushiriki mafunzo ya viongozi wa Wilaya za mikoa ya Morogoro, Mjini/Magharibi na semina ya wajumbe wa BKUT ilyofanyika Ofisi Kuu ya Chama Buguruni, Dar es Salaam.

Pia Katibu Mkuu alifanya ziara katika wilaya ya Kwimba, mkoani Mwanza, ambako pia alipata fursa ya kuhudhuria sherehe za ushindi wa Chama katika kata ya Nyambiti na uzinduzi wa SACCOS ya wilaya hiyo ya Kwimba.

Katika mwezi wa Novemba, 2008, Katibu Mkuu pia alifanya ziara katika Wilaya za Bukoba Mjini, Bukoba Vijijini, na Muleba kwa madhumuni ya kutekeleza OSPI. Halikadhalika, katika mwezi wa Disemba, 2008, Katibu Mkuu alitembelea majimbo yote ya Wilaya ya Micheweni huko Pemba kwa madhumuni ya kukagua uhai wa Chama, kuhami ngome yetu, na kuhamasisha wananchi wajitokeze katika mchakato wa kuboresha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura. Katibu Mkuu aidha alitembelea Wilaya za Mvomero, Kata ya Ngerengere, Morogoro Vijijini, na Mkinga katika mwezi wa Januari, 2009 kwa madhumuni ya kukagua shughuli za Chama.

Kwa kuwa msimamo wa CUF umekuwa ni kupinga na kupiga vita ufisadi, Chama kiliandaa maandamano makubwa ya kushinikiza watuhumiwa wa kashfa ya EPA kupelekwa kwenye vyombo vya sheria na Katibu Mkuu akiwa na viongozi wa juu wa Chama waliongoza waandamanaji katika mkoa wa Dar es Salaam katika mwezi Oktoba kwa ajili hiyo.

4.4 Mahusiano na Vyombo vya Habari

Baada ya kumalizika kwa uchaguzi wa 2005 na matokeo kuwa kama yalivyokuwa, umuhimu wa vyombo vya habari umeongezeka. Vile vile mazungumzo yaliyovurugwa na CCM ya kutafuta suluhu ya kudumu ya mpasuko wa kisiasa Zanzibar pia yameongeza umuhimu huo. Kuvitumia vyema vyombo hivyo halikubakia tena kuwa suala la kuchagua ikiwa lifanyike ama la, bali limekuwa suala la wajibu lililohitaji kuandaliwa mkakati maalum.

Ofisi ya Katibu Mkuu ikiwa inahusika moja kwa moja na shughuli za siku kwa siku za Chama, imekuwa ikitumia vyema fursa ya kukutana na waandishi, wahariri na wahusika wengine wa vyombo vya habari kwa lengo la kujenga taswira ya Chama na kuifanya misimamo ya Chama ifahamike kwa umma.

Katika kipindi cha mwaka 2004 na 2005 ulikuwa ni wakati wa zoezi la uandikishaji kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na pia matayarisho ya Uchaguzi Mkuu wa Tanzania wa mwaka 2005, ambapo katika matukio yote mawili Ofisi ya Katibu Mkuu ilikuwa katika harakati za michakato ya maandalizi na utekelezaji wa shughuli hizo muhimu nchini. Katibu Mkuu alikuwa karibu sana na waandishi wa habari wakati huo kuelimisha wananchi kuhusu shughuli hizo, kuzungumza na vyombo vya ndani na nje kuhusu maendeleo na dosari zilizojitokeza katika zoezi la uandikishaji wapiga kura pamoja na shughuli za uchaguzi zikiwemo kampeni, Tume za Uchaguzi, Upigaji kura, vikwazo vilivyowekwa dhidi ya CUF, utumiaji wa nguvu za ziada wa vyombo vya dola hadi kufikia kutolewa kwa matokeo ya uchaguzi huo. Hata baada ya uchaguzi Katibu Mkuu aliendelea kueleza ulimwengu kupitia vyombo vya ndani na nje ya nchi kuhusu uporwaji wa haki ya wananchi na ushindi wao uliofanywa na CCM na Serikali zake.

Baina ya Novemba 2006 na Februari 2007, kwa mfano, Katibu Mkuu alizungumza na waandishi na wahariri mbali mbali akiwemo mwandishi mashuhuri wa kimataifa, Jonathan Power, Mhariri wa gazeti la Rai, Muhingo Rweyemamu, Mhariri wa Tanzania Daima, Absalom Kibanda, Mhariri wa Sunday Citizen, Sakina Datoo na waandishi wa Mwanachi, Mkinga Mkinga na Boniface Makene. Katika kipindi hicho pia, alifanya mahojiano na Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Ujerumani, na Idhaa ya Kiswahili ya Radio Tehran ya Iran.

Kati ya Juni na Oktoba 2007, kazi za Katibu Mkuu kwenye vyombo vya habari zilijumuisha mahojiano yake kuhusu maendeleo ya mazungumzo ya CCM na CUF, kumbukumbu za miaka minane ya kifo cha Mwalimu Julius Nyerere na hali ya utendaji wa SMZ. Ufafanuzi wa nukta hii upo katika sehemu ya Kurugenzi ya Haki za Binaadamu na Mahusiano ya Umma.

Mwezi Novemba 2007, ambapo zilishaonekana kila dalili za CCM kwenda kinyume na kauli yake kwenye mazungumzo yake na CUF, Katibu Mkuu alifanya mahojiano maalum na gazeti la Rai kuhusu umuhimu wa amani na utulivu nchini, kuheshimu demokrasia, ulazima wa kuwepo kwa suluhisho la kudumu kwa mpasuko wa kisiasa wa Zanzibar na haja ya umoja wa Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla.

Kuvurugwa kwa mazungumzo hayo na CCM hapo Machi 2008, kulifanya uhusiano baina ya Ofisi ya Katibu Mkuu na vyombo vya habari kuchukua sura mpya, kwani kwa namna kesi nzima ilivyowasilishwa kwa umahiri na CUF kwa umma, ilibainika wazi kwamba CUF ilikuwa imetimiza wajibu wake huku CCM ikiwa imekwenda kinyume na kauli ya Mwenyekiti wake, Rais Kikwete, ya Disemba 2005 Bungeni, kwamba alikuwa na dhamira ya kweli ya kutatua matatizo ya Zanzibar. Vyombo vingi vya habari viliripoti, kuchapisha na kuchambua kadhia hiyo katika muelekeo ulioendana na uhalisia huo na huku Katibu Mkuu akiwa ndiye kinara wa marejeo ya habari, taarifa na uchambuzi huo.

Sambamba na hilo, mgogoro wa kisiasa wa Zanzibar unakwenda bega kwa bega na hali ngumu ya maisha, iliyochochewa pia na kukosekana kwa umeme katika kisiwa cha Unguja kwa karibuni mwezi mzima katika mwezi Mei/Juni 2008. Yote hayo yalizungumziwa na Katibu Mkuu katika vyombo vya habari.

Kati ya Julai na Oktoba 2008 mada kuu za Katibu Mkuu katika mazungumzo yake na vyombo vya habari zilikuwa ni masuala ya Muungano, Ufisadi, na kufeli kwa CCM kutekeleza makubaliano yaliyofikiwa baina yake na CUF.

4.5 Juhudi za Kuupatia Ufumbuzi Mgogoro wa Kisiasa wa Zanzibar

Tangu kufanyika kwa uchaguzi wa kwanza chini ya mfumo wa vyama vingi hapo mwaka 1995, Zanzibar imeingia katika mgogoro wa kisiasa kutokana na uendeshaji na usimamizi mbovu wa chaguzi zote zinazofanyika. Chama cha CUF kinaamini kuwa aidha kimekuwa kikishinda katika nafasi ya Urais wa Zanzibar au uchaguzi huwa unachafuliwa kabla ya kufikia kiwango cha kutangazwa kwa matokeo, na hivyo hakikubaliani na ushindi wa CCM unaotangazwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar.

Mgogoro unaondelea sasa, ambao unatokana na uchaguzi wa mwisho wa Oktoba 2005, uliahidiwa kutatuliwa na Rais Jakaya Kikwete mara tu alipoingia madarakani mwaka 2005. Kwa nia ya kulinda amani ya nchi na mshikamano wa kitaifa, CUF ilitafuta, kushawishi na mwisho kukubaliana na mwito wa Rais Kikwete wa vyama vya CUF na CCM kukutana kwa mazungumzo yenye dhamira hiyo. Halmashauri Kuu ya CCM iliamua rasmi chama hicho kizungumze na CUF katika mkutano wake wa mwishoni mwa mwezi Disemba 2006 na CUF ikakubaliana na uamuzi huo. Ofisi ya Katibu Mkuu, ikiwa ndiyo muwajibikaji mkuu wa shughuli za Chama, ilikuwa na jukumu la kuona kuwa dhamira hiyo inafikiwa haraka iwezekanavyo ili kuondokana na mkwamo huo wa kisiasa unaopelekea pia mkwamo wa kiuchumi na kijamii.

Lakini hata kabla ya uamuzi huo rasmi wa CCM, katika kipindi chote cha baina ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa 2005 na Novemba 2006 Katibu Mkuu na wasaidizi wake waliendeleza jitihada za kutafuta ufumbuzi huo kwa mazungumzo yasiyo rasmi kati yao na baadhi ya viongozi wa CCM na pia baina yao na baadhi ya maofisa wa kibalozi wa nchi za nje waliopo Dar es Salaam na ambao nchi zao zinafuatilia kwa karibu suala hili. Ndani ya kipindi hicho, rikodi zinaonesha kuwa Katibu Mkuu alifanya vikao visivyopungua 10, ambavyo hata hivyo havikutangazwa kutokana na suala lenyewe kuwa katika hatua za awali na kulihitajika tahadhari ya hali ya juu.

Kilichokuwa kimehofiwa na Ofisi ya Katibu Mkuu ni kwamba kundi la wahafidhina wa Zanzibar ndani ya CCM halikuwa tayari kwa suluhu ya kudumu, kwani ni mtazamo wa CUF kuwa kundi hilo la watu wachache linafaidika na mgogoro uliopo, hivyo suala la kuweka usiri na tahadhari lilikuwa lazima. Ushahidi ni kuwa, taarifa zilipopenya za kuwapo kwa nia ya mazungumzo, Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Amani Karume, akitanguliwa na wasaidizi wake wa karibu alijitokeza hadharani kupinga jitihada zozote za kuupatia ufumbuzi mgogoro wa Zanzibar. CUF ilimpinga Karume kwa hilo na Novemba 2006 Katibu Mkuu akishirikiana na viongozi wanzake wa juu wa Chama waliongoza maandamano na kuhutubia mikutano ya hadhara Dar es Salaam na Unguja kulaani kauli za Makamo Mwenyekiti huyo wa CCM na kumuunga mkono Rais Jakaya Kikwete katika jitihada za kuupatia ufumbuzi wa kudumu mgogoro wa Zanzibar kwa njia ya mazungumzo.

Baada ya tamko la wazi la CUF kuridhia kuingia kwenye mazungumzo na CCM, Ofisi ya Katibu Mkuu iliwasiliana moja kwa moja na Ofisi ya Katibu Mkuu wa CCM kwa nia ya kuanzisha mazungumzo, ambapo kikao cha mwanzo baina ya timu mbili za vyama hivyo kilifanyika tarehe 17 Januari 2007, Zanzibar, na cha pili tarehe 26 Januari 2007, Dar es Salaam. Hivyo ndivyo vikao vilivyoweka msingi wa mazungumzo hayo.

Lakini jitihada za Ofisi ya Katibu Mkuu kulimaliza tatizo la Zanzibar kwa njia ya mazungumzo zilikuwa zikitiwa dosari mara kwa mara na upande wa CCM ambao tangu mwanzo walikuwa hawaonekani kuwa na dhamira njema. Matokeo yake ni kuwa mazungumzo yalikwama baina ya Juni na Agosti 2007, CCM ikifanya hila za kuyavuruga kwa kuyachelewesha na au kuyapotosha yale yaliyokuwa yamekwisha kuzungumzwa. Katibu Mkuu akiwa Mwenyekiti wa CUF katika mazungumzo hayo alishiriki kikamilifu katika mpango wa kuyakwamua na hatimaye aliongoza kongamano lililofanyika Hoteli ya Peacock, Dar es Salaam, tarehe 18 Agosti 2007 lilitoa tamko rasmi la Chama kukubali ombi la Rais Kikwete kuendelea na mazungumzo.

Matokeo ya tamko hilo la Katibu Mkuu ilikuwa ni kikao cha Kamati ya Mazungumzo iliyojumuisha Makatibu Wakuu kilichofanyika tarehe 7 Septemba 2007 katika Hoteli ya Courtyard Protea, Dar es Salaam kilichoweka utaratibu wa kukamilisha mazungumzo hayo kama ilivyokuwa imeagizwa na BKUT.

Baada ya kikao hicho cha Septemba 2007, Katibu Mkuu aliendelea kukutana na timu ya mazungumzo kabla, wakati na baada ya mazungumzo ili kupokea taarifa za maendeleo ya mazungumzo pamoja na kutoa muongozo. Katika kikao chengine cha Makatibu Wakuu cha Januari 2008, kilichofanyika pia Hoteli ya Courtyard, Dar es Salaam, Katibu Mkuu alielezea wazi msimamo wa CUF katika kufikia suluhisho la kudumu.

Bahati mbaya ni kwamba hatimaye mazungumzo haya yalivurugwa kwa makusudi na CCM iliyokuja na pendekezo jipya, ambalo halikuwemo katika makubaliano ya awali ya timu za mazungumzo, la kura ya maoni kwa uanzishwaji wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar hapo mwezi Machi 2008. Kuanzia hapo hadi sasa, Katibu Mkuu amekuwa mshiriki wa moja kwa moja wa kutekeleza mkakati ulioandaliwa na kuamuliwa na Chama wa kukabiliana na matokeo na matukio yoyote yanayojitokeza kutokana na kukwamishwa kwa mazungumzo hayo. Miongoni mwa shughuli zilizomo kwenye mkakati huo ni kuzungumza na wananchi moja kwa moja au kupitia mikutano na vyombo vya habari kuhusiana na msimamo wa CUF.

4.6 Shughuli za Kijamii na za Kitaifa

“Siasa ni watu na watu ndio njia na ndio lengo katika utaratibu wa siasa za kistaarabu.” Maana ya usemi huu ni kwamba siasa hutumikia watu, hutokana na watu na zinamilikiwa na watu na, hivyo basi, bila ya kuwa mtu wa watu, hakuna fursa ya kuwa mwanasiasa. Ukweli huo ndio unaokipa Chama hichi jina la Chama Cha Wananchi, chama cha watu, kwa maana hiyo.

Shughuli za Ofisi ya Katibu Mkuu, kwa hivyo, ni pamoja na kuhakikisha kuwa Chama hiki kinabakia kuwa cha watu wenyewe, huku kila kundi la kijamii likijihisi kuwa na sehemu yake kwenye Chama na Uongozi wake. Mjengeko wa kijamii na kitamaduni wa jamii zetu unatanua uwajibikaji wa kisiasa kutoka ofisini na kwenye vikao vya chama hadi kwenye mabaraza kwenye vikao vya harusi, misiba, na shughuli nyingine za kijamii.

Imekuwa ni sehemu ya programu ya Ofisi ya Katibu Mkuu kikazi kushiriki katika mikusanyiko ya watu, kutembelea wagonjwa, kuwafariji wafiwa na wanaopatwa na maafa mingine ya kimaumbile, kuhudhuria harusi, mazishi na matukio mengine ya kijamii na kitamaduni. Ushiriki umekuwa na nafasi muhimu katika kujenga taswira ya Chama mbele ya jamii.

Katika utekelezaji wa jukumu hilo, kwenye mwezi Disemba 2006, Katibu Mkuu akiongozana na Mwenyekiti walikwenda kumjulia hali aliyekuwa Waziri wa Nchi Afisi ya Waziri Mkuu (Uratibu na Bunge), Marehemu Juma Jamaldin Akukweti, aliyekuwa amepata ajali ya ndege. Na katika mwezi huo huo, Katibu Mkuu alishiriki katika Baraza la Idi lililotayarishwa na SMZ katika ukumbi wa Makumbusho ya Kasri la Mfalme yaliyo Forodhani, Mji Mkongwe, Zanzibar.

Kwa kuwa ilikuwa ni miezi miwili tangu kuibuka upya kwa mgogoro wa Zanzibar kufuatia kuvurugwa kwa uchaguzi mkuu wa 2005 na CUF kutangaza kutokumtambua Amani Karume kama Rais wa Zanzibar, kuwepo kwa Katibu Mkuu kwenye hafla hiyo kulipelekea vyombo vingi vya habari kuliripoti tukio hilo kama ni ishara njema za kumalizika kwa mgogoro wa Zanzibar.

Mwishoni mwa mwezi Januari 2007, nyumba ya mjumbe wa BKUT na mwasisi wa CUF, Mhe. Ali Haji Pandu, iliungua moto na Katibu Mkuu aliongoza mkutano maalum wa viongozi wa Chama wa wilaya sita za Unguja uliofanyika Kilimahewa, Wilaya ya Magharibi, kuzungumzia maafa hayo na njia za kusaidia. Hatimaye, wanachama walitoa mchango wao mkubwa katika kuijenga upya nyumba hiyo.

Kumbukumbu za saba za Mauaji ya Januari 2001 zilifanyika kwa maeneo na Katibu Mkuu alishiriki katika kisomo maalum cha khitma ya kuwaombea wahanga wa maafa hayo huko Msikiti wa Mbuyuni, mjini Zanzibar.

Agosti 2007, Katibu Mkuu alikuwa mgeni rasmi katika shughuli za kukabidhi trekta lenye thamani ya shilingi milioni 38 kwa wananchi wa Wilaya ya Chake Chake lililotolewa na Mbunge wa Jimbo la Wawi, Mhe. Hamad Rashid Mohammed. Mwezi uliofuata, yaani Septemba 2007, alishiriki katika kisomo maalum cha khitma kumuombea aliyekuwa Mwenyekiti wa Wilaya ya Wete, Marehemu Suleiman Seif Hamad.

Pia wiki nzima ya mwisho wa mwezi huo alikuwa akitembelea wagonjwa katika wilaya za kisiwa cha Pemba, ambapo aliwajulia hali karibuni wagonjwa wote katika hospitali za Abdullah Mzee ya Mkoani na Micheweni. Akiwa katika ziara hiyo, pia alikabidhi mashuka 30 kwa wagonjwa wa Hospitali ya Micheweni yaliyotolewa na Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Mgeni Jadi Kadika.

Vile vile aliwatembelea wachezaji wa timu ya mpira wa miguu ya Chipukizi ya Pemba, ambayo ilikuwa imefuzu kuingia kwenye michezo ya Kombe la Afrika, CAF, na kuzungumza nao. Katibu Mkuu alipokea ombi la kupata wafadhili kwa ajili ya kushiriki mashindano hayo kwani SMZ ilikuwa imewaeleza kuwa haikuwa na uwezo wa kuwagharamia. Katibu Mkuu alifanikisha kuwapatia msaada japokuwa haukuwa mkubwa.

Ziara kama hizo ziliendelea katika mwezi Oktoba 2007 kwenye wilaya zote sita za kisiwa cha Unguja, ingawa alizuiwa na SMZ kutembelea wagonjwa katika Hospitali za Kivunge (Kaskazini) na Makunduchi (Kusini). Hata hivyo, kwa kuwa tukio hilo lilitangazwa na vyombo vya habari, lilisaidia kujenga heshima ya Katibu Mkuu na Chama na kuifedhehesha CCM na SMZ. Vile vile alimtembelea Mwenyekiti Mstaafu wa Chama, Mzee Musobi Mageni Musobi, nyumbani kwake huko Kwimba na alienda kumpa mkono wa pole Mhe. Severina Mwijage, Mbunge Viti Maalum vya Wanawake, alipopatwa na msiba wa kufiwa na mototo wake huko Kagera.

Kwenye mwezi huo huo wa Oktoba, Katibu Mkuu alikuwa mgeni rasmi katika Baraza la Idi lililoandaliwa na CUF na kuhudhuriwa na takribani watu 400 kutoka pembe zote za kisiwa cha Unguja.

Suala jengine muhimu katika shughuli za kijamii ni kuwapa moyo wanachama ambao ama wamekifanyia jambo kubwa Chama na au wamepatwa na matatizo makubwa kutokana na msimamo wao kwa Chama. Rikodi zinaonesha kuwa baina ya mwezi Novemba 2007 na Februari 2008, Katibu Mkuu aliwatambua na kuwapokea mashujaa 29 wa Chama waliokuwa wamehukumiwa kifungo au kulipa fidia kutokana na kumjeruhi Sheha wa Kiwani, kisiwani Pemba.

Pamoja na kushiriki matukio ya kijamii, Katibu Mkuu pia huwa anashiriki matukio yenye sura ya kitaifa kama vile Sherehe za Mapinduzi, Mabaraza ya Idi, Maulidi na nyenginezo anazoalikwa na Serikali. Kwa mfano, Januari 12, 2007 na 2008 alishiriki sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar kwenye viwanja vya Amani kufuatia mualiko wa SMZ. Faida za kushiriki mialiko kama hii ni mbili: kwanza, kuwajengea wana-CUF uwezo wa kujiamini mbele ya taasisi za kiserikali ambazo zimekuwa zikilaumiwa kwa vitendo vya kuwakandamiza wanachama visiwani Zanzibar na, pili, ni kupunguza ukuta wa mtengano baina ya CCM na CUF, kwani kila pande hizi mbili zinapokaribiana ndipo fursa ya kuzungumza na kupunguza tofauti inavyoongezeka.

4.7 Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa

Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa kama Idara ilihamishiwa katika Ofisi ya Katibu Mkuu kufuatia mabadiliko madogo ya Muundo wa Sekretarieti ya Chama yaliyofanyika Aprili 2006. Kabla ya hapo kulikuwa na Kurugenzi kamili ya Haki za Binaadamu na Mambo ya Nje, ambayo iliunganisha shughuli za Kimataifa na suala la haki za binaadamu. Kwa minajili ya ufafanuzi, ripoti hii inaziweka taarifa na uchambuzi wa Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa katika Sura ya Saba.

4.8 Uangalizi wa Mahesabu ya Ndani

Kwa mujibu wa Katiba, Katibu Mkuu ndiye dhamana wa mali na fedha zote za Chama na, kwa hivyo, ana jukumu la kusimamia matumizi ya mali na fedha hizo. Huu ndio msingi wa kuwa na muangalizi wa mahesabu ya ndani moja kwa moja kwenye Ofisi ya Katibu Mkuu kufuatilia taratibu za mapato na matumizi ya Chama na kuandika ripoti juu ya ukaguzi wa fedha anaoufanya ndani ya Chama. Jukumu la mwangalizi pia ni kutoa ushauri kwa wahasibu na washika fedha wa Chama.

Pamoja na kutekeleza majukumu hayo, tangu kuanzishwa kwa kitengo hiki, mwangalizi ametoa ushauri wa namna ya kuanzisha utumiaji wa kompyuta katika kuweka rikodi ya matumizi ya fedha za Chama. Hivi sasa Chama kinahifadhi na kuratibu shughuli zake za kifedha kwa kutumia njia hiyo ya kisasa.

Kazi ya uchunguzi na uchambuzi wa mapato ya Chama imekuwa ikiendelea na pale inapohitajika taarifa zake zimekuwa zikiwasilishwa kwa vikao vya juu vya Chama, Mkaguzi wa Nje na kwa ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini. Rikodi za kimaandishi zilizopo zinaashiria kwamba hadi sasa Ofisi hii ya Mkaguzi wa Ndani ni kwamba kazi ya udhibiti wa mapato na matumizi inakwenda vizuri.

Maoni ya Mkaguzi wa Ndani anayoyawasilisha kupitia tarifa zake kwa Katibu Mkuu yamekuwa yakizingatiwa na kufanyiwa kazi ipasavyo.

4.9 Usimamizi wa Utekelezaji wa Mpango Mkakati (Strategic Plan)

Mpango Mkakati (Strategic Plan, SP) ni mpango maalum ulioanzishwa na Chama kwa madhumuni ya kukijenga kitaasisi na kisayansi. Kwa madhumuni ya kufuatilia vyema utekelezaji wake, na kwa matakwa ya Katiba yanayotaka kwamba Katibu Mkuu awe ndiye msimamizi mkuu wa shughuli za kila siku za utendaji wa Chama, usimamizi wa SP umewekwa chini ya Ofisi ya Katibu Mkuu na kutengewa msimamizi wake maalum anayeitwa Mdhibiti wa SP na ambaye anaripoti moja kwa moja kwa Katibu Mkuu.

Jukumu la mdhibiti ni kuwasiliana na watekelezaji wote wa SP mara kwa mara ili kuhakikisha kuwa utekelezaji unakwenda kama ulivyopangwa. Vile vile ana jukumu la kushauri na kutoa maelekezo ya jinsi ya kutekeleza majukumu hayo pale ushauri na maelekezo yanapohitajika. Pia anatakiwa kuandika taarifa juu ya mwenendo wa utekelezaji wa SP, hali halisi, vikwazo na pia kutoa ushauri wa namna ya kukabiliana na kuvishinda vikwazo hivyo.

Kumbukumbu za kimaandishi zinaashiria utekelezwaji mzuri wa majukumu haya huku kukiwa na ufuatiliaji wa karibu wa Katibu Mkuu mwenyewe. Kwa mfano, katika mwezi Julai 2007, Katibu Mkuu aliongoza na kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kuhakiki na kupitia SP akiwa ni miongoni mwa viongozi wakuu kwa upande wa Chama. Kazi hiyo iliyoratibiwa na mtaalamu wa kimataifa ilifanyika kwa siku nne katika hoteli ya White Sands, Dar es Salaam na kugharamiwa na Taasisi ya Friedrich Naumann.

Vile vile rikodi zinaonesha kuwa Mdhibiti wa SP amekuwa akiwasiliana na Wakurugenzi mara kwa mara juu ya utekelezaji wa SP.

Katika siku za hivi karibuni, uhakiki wa SP umeonesha kuwa utekelezaji wa majukumu umebadilika kidogo na hivyo hivi sasa kila Mkurugenzi amepatiwa marekebisho ya sehemu yake ya utekelezaji huku kukiwa na msisitizo wa kipekee kwenye uwasilishaji wa muda maalum wa utekelezaji wa majukumu hayo (Time Action Plan).

Kumewekwa utaratibu mpya wa kutoa taarifa za utekelezaji wa SP kila wiki kama kipimo kinachosimamiwa moja kwa moja na Katibu Mkuu mwenyewe na rikodi zinaonesha mafanikio yameanza kupatikana katika yale maeneo yaliyotolewa taarifa.

Katika wakati huu ambapo ushindani wa kisiasa haupo baina ya CUF na CCM tu, bali pia baina ya CUF na vyama vyengine vinavyopigania utawala, OSPI imebainika kuwa ndio njia sahihi ya kutumia kuelekea Chama imara na madhubuti chenye uwezo wa kuiondosha CCM madarakani.

SURA YA TANO

OFISI ZA MANAIBU KATIBU MKUU

5.1 Utangulizi

Ofisi ya Naibu Katibu Mkuu inaanzishwa na Ibara ya 72 ya Katiba ya Chama ya mwaka 1992 toleo la 2003, na majukumu yake yanaelezwa katika Ibara ya 73 ya Katiba hiyo. Kwa mujibu wa Ibara hizo, Naibu Katibu Mkuu ndiye Mshauri Mkuu na Msaidizi Mkuu wa Katibu Mkuu. Ibara hizo zinaweka Manaibu wawili wa Katibu Mkuu: mmoja kwa upande wa Tanzania Bara, na mwengine kwa upande wa Zanzibar. Kwa kuwa Katibu Mkuu wa sasa anatoka Zanzibar, kulingana na matakwa ya Katiba, Naibu Katibu Mkuu anayemfuata kimadaraka ni yule anayetoka Tanzania Bara.

Kwa mujibu wa Katiba, majukumu ya Manaibu Katibu Mkuu ni pamoja na yafuatayo:

(i) Katibu wa Kamati ya Utendaji ya Taifa na Mdhamini wa Masjala ya Chama.
(ii) Kusimamia shughuli, taratibu na kanuni za utawala za Chama za kila siku katika eneo lake la kazi.
(iii) Kuwa Msimamizi wa Uandishi na utunzaji wa mihutasari ya vikao vya taifa.
(iv) Kusimamia na kuratibu utekelezaji wa sera za Chama unaofanywa na serikali inayotokana na Chama.
(v) Kushughulikia elimu na mafunzo ya siasa kwa wanachama na viongozi wa Chama, pamoja na mafunzo ya uongozi na utendaji bora wa shughuli za Chama.
(vi) Kusimamia heshima na nidhamu ya watumishi wa Chama katika Makao Makuu na Ofisi Kuu.

Kutokana na mabadiliko ya miundo ya Kurugenzi yaliyofanywa na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa kufuatilia kupitishwa kwa Mpango Mkakati wa Chama (SP) hapo mwaka 2006, majukumu yaliyotajwa hapo juu yalihamishiwa kutoka Ofisi ya Naibu Katibu Mkuu na kupelekwa katika Kurugenzi ya Oganaizesheni [majukumu (i), (ii), (iii), na (vi)]; na katika Kurugenzi ya Siasa [jukumu (v)]. Hivyo Naibu Katibu Mkuu amebakishwa na jukumu moja tu la (iv) la kusimamia na kuratibu utekelezaji wa sera za Chama unaofanywa na Serikali itokanayo na Chama. Na kwa kuwa kwa sasa hakuna serikali kuu inayoongozwa na Chama, ukweli ni kwamba hata jukumu hilo halipo. Kwa hivyo kila Naibu Katibu Mkuu amebaki na jukumu la kuwa Mshauri na Msaidizi Mkuu wa Katibu Mkuu katika eneo lake la kazi.

Kutokana na Manaibu Katibu Mkuu kupungukiwa sana na majukumu, Mwenyekiti wa Taifa, kwa ridhaa ya Baraza Kuu la Uongozi la Taifa, aliwateua Manaibu Katibu Mkuu kuongoza Kurugenzi, huku wakiendelea kuwa Manaibu Katibu Mkuu.

5.2 NAIBU KATIBU MKUU (BARA)

Tangu baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2004 hadi sasa, Naibu Katibu Mkuu (Bara) ni Mheshimiwa Wilfred Muganyizi Lwakatare.

Ripoti hii kwa ofisi hii itagawika katika sehemu mbili:
(a) Kipindi kabla ya Marekebisho ya miundo ya Kurugenzi (2004 – 2006)
(b) Kipindi baada ya Marekebisho ya miundo ya Kurugenzi (2006 – 2009)

(a) Kipindi cha 2004 – 2006

Katika kipindi hicho, mbali na kuwa Naibu Katibu Mkuu, Mheshimiwa Lwakatare pia alikuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Jimbo la Bukoba Mjini na Kiongozi wa Upinzani katika Bunge.

Katika kipindi hicho Ofisi ya Naibu Katibu Mkuu (Bara) ilisimamia kwa ufanisi wa kutosheleza majukumu yote yaliyoelezwa na Katiba ya Chama kama yalivyonukuliwa hapo juu. Miongoni mwa kazi zilizofanywa na Naibu Katibu Mkuu (Bara) ni pamoja na :

(i) Usimamizi wa zoezi la uandikishaji wa Wapiga Kura katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kuanzia Machi – Oktoba, 2004.

(ii) Kusimamia maandalizi ya Uchaguzi wa Serikali za Vitongoji, Vijiji na Mitaa ikiwemo Operation Chukua Jiji la Dar es Salaam (OCJ – DSM) katika mwaka 2004.

(iii) Utayarishaji na usambazaji wa nyaraka muhimu kadhaa kwa Wilaya zote za Bara, kwa mfano waraka wa kuwapa nafasi wanachama kuomba nafasi za utendaji Ofisi Kuu.

(iv) Uhamasishaji wa wananchi kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa 2005, na kugombea Ubunge Jimbo la Bukoba Mjini ambapo alifaulu kuchaguliwa kuwa Mbunge.

(v) Usimamizi wa vikao vya Kamati ya Utendaji ya Taifa, Baraza Kuu la Uongozi la Taifa (vilipofanyika Ofisi Kuu), Vikao vya Wakurugenzi na Watendaji wa Ofisi Kuu na kusimamia uandishi wa mihutasari ya vikao hivyo na utunzaji wa mihutasari hiyo.

(vi) Usimamizi wa nidhamu ya viongozi na watumishi walioko chini yake, kuratibu na kuyatafutia ufumbuzi malalamiko kadhaa kutoka ngazi za chini za uongozi na ya wanachama.

(vii) Kuongea na vyombo vya habari kwa madhumuni ya kufafanua sera na maamuzi ya kitaifa ya Chama.
(viii) Kusimamia mafunzo kwa viongozi na watendaji wa Chama, yakiwemo mafunzo ya Wakufunzi (TOT) yaliyofadhiliwa na Friedrich Naumann Foundation (FNF), mafunzo ya uundwaji wa Jumuiya ya Wanawake yaliyofadhiliwa na Tazanzania Centre for Democracy (TCD).
(ix) Kutembelea ofisi za mabalozi kadhaa wanaowakilisha nchi zao Tanzania kwa madhumuni ya kutafuta nafasi za mafunzo kwa viongozi na watendaji wa Chama. Miongoni mwa Ofisi za Mabalozi alizotembelea ni pamoja na zile za Ufini (Finland), Uswidi (Sweden), na pia British Council na nyenginezo.
(x) Kufanya ziara katika wilaya kadhaa zikiwemo wilaya za Kanda ya Pwani, Kaskazini, Kati, Nyanda za Juu Kusini, Kusini na Unguja kwa ajili ya maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa 2005.
(xi) Kuratibu ziara za Viongozi Wakuu wa Chama katika Wilaya mbali mbali za Tanzania Bara.
(xii) Usimamizi wa utengenezaji wa muongozo na mgawanyo wa kazi kwa Kurugenzi kwa mujibu wa matakwa ya Mpango Mkakati wa Chama.
(xiii) Uratibu wa semina elekezi ya Wabunge na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi watokanao na Chama juu ya kuyafahamu vyema majukumu yao.
(xiv) Kukiwakilisha Chama katika Kamati ya Maofisa wa Vyama ya Tanzania Centre for Democracy. Pia kukiwakilisha Chama katika Kamati ya Maofisa wa vyama vinavyounda Ushirikiano wa vyama vya CUF, CHADEMA, NCCR-Mageuzi na TLP.
(xv) Uratibu wa mchakato wa madai ya Katiba mpya za Nchi na Tume Huru za za Uchaguzi.
(xvi) Akiwa Kiongozi wa Upinzani katika Bunge, Naibu Katibu Mkuu (Bara) aliwasilisha Bungeni, maoni ya Chama kuhusu Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa ya 1992 na Maadili ya Vyama vya Siasa pamoja na malalamiko juu ya nafasi ya Mtendaji wa Mtaa.

(b) Kipindi cha 2006 – 2009) :
Katika kipindi hiki Mheshimiwa Lwakatare alisita kuwa Mbunge na Kiongozi wa Upinzani katika Bunge. Hata hivyo aliteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Siasa. Hivyo aliiongoza Kurugenzi hiyo huku akiendelea kuwa Naibu Katibu Mkuu (Bara). Shughuli alizozifanya akiwa Mkurugenzi wa Siasa zitaelezwa katika Sura ya sita ya Ripoti hii.
Majukumu yake kama Naibu Katibu Mkuu (Bara) aliyaendeleza katika kipindi hiki.
Kazi nyengine alizozifanya katika kipindi hiki ni pamoja na zifuatazo:
(i) Usimamizi wa uundwaji wa Mabaraza ya Wanawake, Vijana na Wazee mwezi Julai, 2007.
(ii) Kuendelea na usimamizi wa mchakato wa wa madai ya Katiba mpya za Nchi na Tume huru za Uchaguzi ikiwa ni pamoja na kuandaa mikutano ya wadau ya kuandaa mpango mkakati, uteuzi wa Kamati ya Kuandika Mapendekezo ya Katiba Mpya za Nchi, kuitisha vikao vya Sekretarieti na Kamati ya Kudumu ya Madai ya Katiba.
(iii) Kufanya ziara za uhamasishaji wa Uchaguzi wa ndani ya Chama katika wilaya zote sita za Unguja, na katika wilaya za Mikoa ya Dodoma na Singida katika mwaka 2007.
(iv) Kufanya ziara ya uhamasishaji wananchi ili washiriki katika zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika Kanda za Kusini, Kati, Ziwa, Nyanda za Juu Kusini na Kaskazini katika mwaka 2007.
(v) Kusimamia mchakato wa uteuzi wa majasiri wa Chama wa kusimamia na kuratibu utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Chama (OSPI).
(vi) Usimamizi wa maandalizi ya na kushiriki katika maandamano kadhaa na mikutano ya hadhara ya kitaifa.
(vii) Kuhudhuria makongomano na semina za kimataifa katika nchi za Msumbiji,, Malawi, Afrika Kusini, na Uingereza.
(viii) Kushiriki katika mikutano ya Tanzania Centre for Democracy (TCD), ESAURP, FNF, African Liberal Network (ALN), Netherlands Institute for Multi-Party Democracy (NIMD), Chama cha VENSTRE cha Norway, DEMOFINLAND, KIC na taasisi nyengine kwa lengo la kukuza ushirikiano, kuendeleza mchakato wa demokrasia na pia kujipatia mafunzo.
(ix) Usimamizi wa vikao vya mashirikiano wa vyama vya siasa vinne yaliyopelekea Viongozi Wakuu vyama hivyo kutia saini Makubaliano ya Ushirikiano hapo tarehe 9 Mei, 2007.
(x) Kushiriki katika ziara ya pamoja ya viongozi wakuu wa vyama vya siasa viliyomo katika Ushirikiano wa vyama katika mikoa ya Mwanza, Tabora, Rukwa na Ruvuma katika mwaka wa 2007.
(xi) Mara zote ambapo Katibu Mkuu anapokuwa hayupo nchini, Naibu Katibu Mkuu (Bara) ndio hukaimu nafasi hiyo na kutekeleza majukumu yanayopaswa kutekelezwa na Katibu Mkuu.

Miongoni mwa kazi zilizotekelezwa na Naibu Katibu Mkuu (Bara) kuna mambo mawili yanayohitaji maelezo ya ziada. Mambo hayo ni :
(a) Mchakato wa Madai ya Katiba, na
(b) Ushirikiano wa Vyama vinne vya Siasa.

(a) Mchakato wa Madai ya Katiba:
Kwa sababu ya umuhimu wa kupatikana kwa Katiba mpya za nchi ambazo ni muhimu kwa kuendeleza na kupanua misingi ya demokrasia nchini, Chama cha Wananchi (CUF) kiliandaa na kusimamia Kongamano la kwanza la wadau wote nchini. Kongomano hilo lilifanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Peackock jijini Dar es Salaam na kuongozwa na Mwenyekiti wa Taifa wa CUF, Mheshimiwa Profesa Ibrahim Haruna Lipumba. Kongomano hilo lilikubaliana kwa kauli moja kuanzishwa kwa mchakato wa kudai Katiba Mpya za Nchi ambazo zitaanzisha Tume Huru za Uchaguzi. Pia Kongomano hilo liliunda Kamati ya Kudumu ya Madai ya Katiba na kumteua Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad kuwa Mwenyekiti wa Kamati hiyo. Kongomano pia liliteua Sekretarieti ya Madai ya Katiba mpya na kumteua Mheshimiwa Wilfred Muganyizi Lwakatare kuwa Mwenyekiti wa Sekretarieti.
Kongomano lilitoa jukumu la kuundwa kwa Kamati ya Kuandika Rasimu ya Katiba Mpya kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu. Mwenyekiti aliteua Kamati hiyo chini ya uongozi wa Dk. Sengondo Mvungi, mwanasheria, mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Mkuu wa Idara ya Sheria ya chama cha NCCR-Mageuzi.
Kamati ya Kuandika Rasimu ya Katiba ilitimiza jukumu lake vyema. Mapema mwaka huu, Rasimu hiyo imewasilishwa mbele ya Kamati ya Kudumu na baada ya kufanyiwa marekebisho madogo madogo, imewasilishwa katika Kongomano la wadau wote. Kongomano limeidhinisha Rasimu hiyo. Kazi iliyobaki sasa ni kuichapisha rasimu hiyo na kuisambaza kwa wananchi ili nao watoe mapendekezo yao. Kisha Kamati ya Kuandika Rasimu ya Katiba iyazingatie mapendekezo ya wananchi na kuandika rasimu ya mwisho, ambayo baada ya kuidhinishwa na Kamati ya Kudumu itawasilishwa kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Zanzibar kwa mazingatio yao. Kisha zitafuata hatua za kudai Katiba kulingana na vipi Serikali mbili hizo zimeyapokea mapendekezo hayo.
Shughuli hii imechelewa kutokana na ukweli kuwa gharama karibu zote za mchakato wa madai ya Katiba mpya za Nchi zimebebwa na CUF, na baada ya kupitishwa kwa Mpango Mkakati wa Chama, kipaumbele kimewekwa katika utekelezaji wa Mpango Mkakati huo. Kwa ufupi tumekuwa na ukosefu wa fedha za kuendeleza mchakato huo.

(b) Ushirikiano wa Vyama vinne vya Siasa:
Ushirikiano miongoni mwa Vyama vya Siasa vinne vya CUF, CHADEMA, NCCR-Mageuzi na TLP ulianzishwa kwa ajili ya kuchanganya nguvu ili kupambana na Chama Cha Mapinduzi (CCM). Viongozi wakuu wa vyama hivyo walijikita kwenye falsafa ya Umoja ni Nguvu na Utengano ni Udhaifu. Ilikubaliwa kutoka awali kuwa gharama za kuendesha Ushirikiano huo zibebwe na vyama vinne vyenyewe kwa mpangilio wa:
CUF 40%
CHADEMA 30%
NCCR- Mageuzi 15%
TLP 15%
Pamoja na kukubaliana kwa utaratibu huo, uzoefu umeonesha kuwa mzigo mkubwa sana wa gharama za uendeshaji wa ushirikiano huo zinabebwa na CUF. CUF kwa sababu siku zote inaamini katika umoja, ilikubali kuubeba mzigo huo kwa moyo mkunjufu.
Mwanzoni ilionekana vyama vyote vinne viliingia katika ushirikiano huo kwa nia safi, na kwa kweli dalili zilionesha kuwa mambo yangekuwa mazuri. Ziara za pamoja ziliandaliwa na kufanywa. Wananchi walipokea vyema ushirikiano huo na ziara katika mikoa yote zilikuwa za mafanikio makubwa.
Bahati mbaya, baadae ilidhihirika kuwa baadhi ya wenza wetu waliitumia vibaya fursa iliyotolewa na Ushirikiano kwa kuibomoa CUF na kujijenga wao kupitia mgongo wa CUF. Baadhi ya viongozi wa baadhi ya vyama vya Ushirikiano walijenga tabia ya kuwahadaa viongozi wa CUF na kuwarubuni ili waache kuunga mkono CUF na badala yake wajiunge na vyama hivyo. Lililotushangaza ni kuwa baadhi ya vyama hivyo badala ya kutafuta wanachama kutoka CCM, wakitafuta wanachama wa CUF. Viongozi wengi wa CUF wa ngazi za chini walililamikia jambo hili. Uongozi wa kitaifa ukawa unawapoza viongozi hao wa ngazi za chini na kuwaomba kuwa na subira.
Mambo yalichafuka hasa ulipowadia uchaguzi mdogo wa Jimbo la Tarime. CHADEMA ilisimamisha Mgombea na kuviomba vyama vyengine kukiunga mkono. CUF, pamoja na kuwa na mgombea mzuri kuliko wengine, ilikubali ombi hilo. Viongozi wa CUF wa Wilaya ya Tarime na wilaya jirani, kwa idhini ya uongozi wa kitaifa wa CUF ulishiriki kwa ukamilifu katika kumpigia kampeni mgombea wa CHADEMA licha ya kwamba hapo awali CUF ilitangaza kutounga mkono mgombea yeyote.

NCCR-Mageuzi haikulikubali ombi la CHADEMA na hivyo ikasimamisha mgombea wake. TLP ilimuunga mkono mgombea wa NCCR-Mageuzi na viongozi wake wakuu walishiriki katika kumfanyia kampeni mgombea huyo wa NCCR-Mageuzi.
Pakatokea kutoelewana kukubwa baina ya CHADEMA kwa upande mmoja na NCCR-Mageuzi na TLP kwa upande mwengine. CHADEMA wakafikia kusema Ushirikiano haupo tena, na kwamba wao wako tayari kushirikiana na CUF tu, lakini hawako tayari kushirikiana na NCCR-Mageuzi na TLP. NCCR-Mageuzi na TLP nao kwa upande wao wakasema hawako tayari kushirikiana na CHADEMA bali wako tayari kushirikiana na CUF. Hivyo CUF iliwekwa katikati.
Baraza Kuu la Uongozi la Taifa likaamua kuwa ni vyema kupata misimamo ya vyama hivyo vitatu juu ya kuendelea kwa Ushirikiano au kinyume chake. Katibu Mkuu akaviandikia vyama vyote vitatu, na majibu yao hayakututia moyo, ingawa hakuna chama kilichopinga moja kwa moja kuendelezwa kwa Ushirikiano.
Ulipojitokeza Uchaguzi mdogo wa Jimbo la Mbeya Vijijini, CUF ilikiomba CHADEMA kimuunge mkono mgombea wa CUF kwa vile katika Uchaguzi Mkuu wa 2005 CUF ilishika nafasi ya pili katika jimbo hilo. CHADEMA walilikataa ombi hilo, pamoja na kwamba CUF ilwaunga mkono wagombea wa CHADEMA katika chaguzi ndogo za Kiteto na Tarime. Ikumbukwe kwamba katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Tunduru ambako CUF ina nguvu kubwa, CHADEMA pia iliweka mgombea wake na kulikataa ombi la kumuunga mkono mgombea wa CUF.
Katika mazingira hayo, Baraza Kuu la Uongozi la Taifa limeamua kwa sasa kuweka nguvu kubwa zaidi katika kukiimarisha chama chetu. CUF haijakataa kuendeleza Ushirikiano. Mazingira yakibadilika na ikionekana vyama vyote vya Ushirikiano vina nia ya dhati ya kushirikiana, CUF itakuwa tayari kufanya hivyo.

5.3 NAIBU KATIBU MKUU (ZANZIBAR)

Tangu baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2004 hadi sasa, Naibu Katibu Mkuu (Zanzibar) ni Mheshimiwa Juma Duni Haji.

Taarifa hii kwa ofisi hii itagawika katika sehemu mbili:
(c) Kipindi kabla ya Marekebisho ya miundo ya Kurugenzi (2004 – 2006)
(d) Kipindi baada ya Marekebisho ya miundo ya Kurugenzi (2006 – 2009)

(c) Kipindi cha 2004 – 2006

Katika kipindi hicho, mbali na kuwa Naibu Katibu Mkuu, Mheshimiwa Juma Duni Haji pia alikuwa Mgombea Mwenza wa Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano kwa tiketi ya CUF.

Katika kipindi hicho Ofisi ya Naibu Katibu Mkuu (Zanzibar) ilisimamia kwa ufanisi wa kutosheleza majukumu yote yaliyoelezwa na Katiba ya Chama kama yalivyonukuliwa hapo juu. Miongoni mwa kazi zilizofanywa na Naibu Katibu Mkuu (Zanzibar) ni pamoja na :

(i) Utayarishaji na usambazaji wa nyaraka muhimu kadhaa kwa Wilaya zote za Zanzibar, kwa mfano waraka wa kuwapa nafasi wanachama kuomba nafasi za utendaji Mkao Makuu, na Uhamasishaji wa wananchi kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa 2005, na kuwa Mgombea Mwenza wa Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano kupitia CUF.

(ii) Usimamizi wa vikao vya Kamati ya Utendaji ya Taifa, Baraza Kuu la Uongozi la Taifa (vilipofanyika Zanzibar), Vikao vya Wakurugenzi na Watendaji wa Makao Makuu na kusimamia uandishi wa mihutasari ya vikao hivyo na utunzaji wa mihutasari hiyo.
(iii) Usimamizi wa nidhamu ya viongozi na watumishi walioko chini yake, kuratibu na kuyatafutia ufumbuzi malalamiko kadhaa kutoka ngazi za chini za uongozi na na wanachama kwa upande wa Zanzibar.
(iv) Kuzungumza na vyombo vya habari kwa madhumuni ya kufafanua sera na maamuzi ya kitaifa ya Chama.
(v) Kwa kushirikiana na Naibu Katibu Mkuu (Bara), Naibu Katibu Mkuu (Zanzibar) alisimamia mafunzo kwa viongozi na watendaji wa Chama, yakiwemo mafunzo ya Wakufunzi (TOT) yaliyofadhiliwa na Friedrich Naumann Foundation (FNF), mafunzo ya uundwaji wa Jumuiya ya Wanawake yaliyofadhiliwa na Tazania Centre for Democracy (TCD).
(vi) Kufanya ziara katika wilaya kadhaa zikiwemo wilaya za Unguja na Pemba na wilaya karibu zote za Bara kwa ajili ya maandalizi na kampeni kwa Uchaguzi Mkuu wa 2005.
(vii) Kushiriki katika uzinduzi wa Timu ya Kampeni ya Mgombea Urais wa Zanzibar na kushiriki katika kutayarisha Ilani ya Uchaguzi ya CUF kwa Zanzibar na kwa Jamhuri ya Muungano.
(viii) Kuongoza Maofisa wa CUF katika mikutano na Tume ya Uchahguzi ya Zanzibar kuzungumzia masuala ya Daftari la Kudumu la Wapiga Kura baada ya kugundulika kuweko kwa njama za kutaka kuyachanganya madaftari ya Jamhuri ya Muungano na Zanzibar.
(ix) Kushiriki katika maandamano, mikutano ya hadhara na kukutana na waandishi wa habari kwa ajili ya kuzitangaza sera za Chama.
(x) Kushiriki na kuwasilisha mada mbali mbali katika makongomano na semina za kitaifa na kimataifa hapa nchini na nje ya nchi kwa niaba ya Chama.
(xi) Kuwapokea na kufanya nao mazungumzo wageni mbali mbali waliotembelea Makao Makuu, akiwemo Msajili wa Vyama vya Siasa, Balozi wa Uingereza, Balozi wa Norway na Balozi mdogo wa Marekani hapa nchini.
(xii) Kuwa mlezi wa Wilaya ya Kinondoni na kufanya shughuli kadhaa za uhamasishaji na kutatua migogoro iliyozuka katika wilaya hiyo.

(d) Kipindi cha 2006 – 2009:
Katika kipindi hiki Mheshimiwa Juma Duni Haji aliteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Fedha na Uchumi. Hivyo, aliiongoza Kurugenzi hiyo huku akiendelea kuwa Naibu Katibu Mkuu (Zanzibar). Shughuli alizozifanya akiwa Mkurugenzi wa Fedha na Uchumi zitaelezwa katika Sura ya Sita ya Taarifa hii.
Majukumu yake kama Naibu Katibu Mkuu (Zanzibar) aliyaendeleza katika kipindi hiki.
Kazi nyengine alizozifanya katika kipindi hiki ni pamoja na zifuatazo:

(i) Kukaimu nafasi ya Katibu Mkuu pale ambo Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu (Bara) wanapokuwa hawapo nchini.

(ii) Kuwa Mjumbe katika Timu ya CUF ya Mazungumzo ya Kuutafutia Ufumbuzi wa Kudumu Mgogoro wa Kisiasa wa Zanzibar baina ya CCM na CUF.

(iii) Kuwapokea na kufanya nao mazungumzo wageni wanaotembelea Makao Makuu, wakiwemo wageni wa kimataifa, wa kitaifa, viongozi wa Chama na wanachama.

(iv) Kumuwakilisha Mwenyekiti, Makamo Mwenyekiti na Katibu Mkuu katika mikutano ya kitaifa, na katika semina, warsha na makongomano yanayofanywa ndani na nje ya nchi na wakati mwengine kuwasilisha mada.

(v) Kuongoza ujumbe wa Wakurugenzi na Maafisa Dawati wa Chama katika ziara ya Afrika Kusini walikokwenda kujifunza mbinu mbali mbali za kuendesha Chama wakiwa wageni wa Chama cha Democratic Alliance cha nchi hiyo chini ya ufadhili wa FNF.

SURA YA SITA

KURUGENZI ZA CHAMA

6.1 Utangulizi

Ibara ya 82 ya Katiba ya Chama ya 1992, Toleo la 2003 inatoa mamlaka kwa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa kuanzisha Kurugenzi katika ngazi ya taifa kwa ajili ya kurahisisha na kufanikisha utendaji bora wa kazi za Chama.

Kabla ya marekebisho ya miundo ya Kurugenzi ya mwaka 2006, Chama ngazi ya Taifa kilikuwa na Kurugenzi zifuatazo:-

(i) Kurugenzi ya Mipango na Chaguzi
(ii) Kurugenzi ya Habari naUenezi wa Sera
(iii) Kurugenzi ya Rasilimali, Uchumi na Fedha
(iv) Kurugenzi ya Haki za Binadamu na Mambo ya Nje
(v) Kurugenzi ya Wanawake
(vi) Kurugenzi ya Vijana.

Katika ngazi ya Wilaya kulikuwa na Vitengo vinavyolingana na Kurugenzi za Kitaifa.

Kufuatia marekebisho ya miundo ya Kurugenzi ya 2006, Kurugenzi zimekuwa kama ifuatavyo:-

(i) Kurugenzi ya Oganaizesheni
(ii) Kurugenzi ya Siasa
(iii) Kurugenzi Haki za Binadamu na Mahusiano na Umma
(iv) Kurugenzi ya Blue Guards.
(v) Kurugenzi ya Fedha na Uchumi

Kwa ngazi ya Wilaya kumeanzishwa Vitengo vinavyolingana na Kurugenzi hizo za Kitaifa.

Katika muundo mpya, Kurugenzi za Vijana na Wanawake zimefutwa kufuatilia matakwa ya Mpango Mkakati wa Chama (SP) ya kuanzishwa kwa Jumuiya za Wanawake, Vijana na Wazee. Taarifa kuhusu Jumuiya hizo inapatikana katika Sura ya Sita ya Taarifa hii. Hata hivyo, usimamizi wa Jumuiya zote tatu umewekwa chini ya Kurugenzi ya Siasa, ambayo pia ina jukumu la kuratibu na kusimamia shughuli za Wabunge na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, Madiwani na Viongozi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji watokanao na Chama.

Kitengo cha Mambo ya Nje kilichokuwa sehemu ya Kurugenzi ya Haki za binadamu na Mambo ya Nje sasa kimehamishiwa Ofisi ya Katibu Mkuu. Katibu Mkuu amewekewa Msaidizi Maalum, Mheshimiwa Ismail Jussa, wa kumsaidia katika kutekeleza majukumu ya Kitengo hicho ambacho pia kinahusika na Uhusiano wa Kimataifa.

Kitengo cha Haki za Binadamu kimeunganishwa na Kitengo cha Mahusiano na Umma na kufanya Kurugenzi mpya ya Haki za Binadamu na Mahusiano na Umma. Mbali ya kushughulikia masuala ya Haki za Binadamu, Kurugenzi hii pia inafanya shughuli za ukusanyaji na utoaji habari na uenezi wa sera, maamuzi na kujenga taswira nzuri ya Chama chetu.

6.1 KURUGENZI YA OGANAIZESHENI

Taarifa ya Kurugenzi ya Oganaizesheni itakuwa na sehemu sita zifuatazo:-

1. Utangulizi
2. Utawala na Uendeshaji
3. Usimamizi waVikao vya Kitaifa na Uandishi na Utunzaji wa Kumbukumbu
4. Mipango ya Kukijenga na Kukiimarisha Chama
5. Kuandaa na Kusimamia Chaguzi
6. Huduma kwa Wilaya

6.1.1 Utangulizi:

Kurugenzi ya Oganaizesheni ilianzishwa mara baada ya Uchaguzi Mkuu wa Ndani ya Chama wa 2004 wakati huo ikijulikana kama Kurugenzi ya Mipango na Chaguzi, na imeendelea kuwepo baada ya marekebisho ya miundo ya Kurugenzi ya 2006. Hata hivyo, Kurugenzi hii baada ya marakebisho ya 2006 imeongezewa majukumu ambayo awali yalikuwa chini Ofisi za Manaibu Katibu Mkuu. Majukumu yaliyoongezwa ni pamoja na :-

(i) Kuwa Katibu wa Kamati ya Utendaji ya Taifa na Mdhamini wa Masjala ya Chama.

(ii) Kusimamia shughuli, taratibu na kanuni za utawala na uendeshaji za Chama za kila siku.

(iii) Kuwa Msimamizi wa Uandishi na utunzaji wa mihutasari ya vikao vya taifa.

(iv) Kusimamia nidhamu ya watumishi wa Chama katika Makao Makuu na Ofisi Kuu.

Shughuli ambazo Kurugenzi inaendelea nazo tangu 2004 ni pamoja na zifuatazo:

(v) Kusimamia mipango ya kukijenga na kukiimarisha Chama.

(vi) Kusimamia mawasiliano na ngazi za chini, hususan, ngazi ya wilaya.

(vii) Kuandaa na kusimamia chaguzi za ndani ya Chama na chaguzi za kiserikali zinazoshirikisha vyama vyengine vya siasa.

(viii) Kutoa huduma kwa wilaya.

(ix) Kutayarisha na kuendeleza database ya chama.

Katika kipindi cha 2004 – 2006 Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Oganaizesheni alikuwa Mheshimiwa Hamad Masoud Hamad kutoka Zanzibar, na Naibu Mkurugenzi alikuwa Mheshimiwa Khamis Iddi Katuga kutoka Tanzania Bara. Baada ya marekebisho ya miundo ya Kurugenzi ya 2006, Mheshimiwa Hamad Masoud Hamad aliendelea kuwa Mkurugenzi wa Kurugenzi hii, na Naibu Mkurugenzi akateuliwa Mheshimiwa Joran Bashange kutoka Tanzania Bara.

Mheshimiwa Katuga alitoka katika Chama na hatimaye akajiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM)

Kurugenzi hii ina madawati yafuatayo:-
(i) Utawala na Uendeshaji
(ii) Mawasiliano ndani ya Chama
(iii) Usalama wa Vifaa
(iv) Takwimu

6.1.2 Utawala na Uendeshaji:

Ili Kurugenzi iweze kusimamia vizuri majukumu yake katika utawala na uendeshaji, umuhimu wa kuwa na bajeti inayokidhi mahitaji ni muhimu. Hivyo Kurugenzi kila mwaka ilijitahidi kuandaa mapendekezo ya bajeti yake, au pale ilipotakiwa kufanya hivyo na kuziwasilisha kwa Kurugenzi ya Fedha na Uchumi kwa muda uliotakiwa.

Bajeti ya kuendesha na kusimamia chaguzi ndani ya Chama ilipanda kuanzia mwishoni mwa 2006 hadi mwishoni mwa 2008 kutokana na uamuzi wa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa kuendesha chaguzi hizo kwa kanda. Kila mwezi Kurugenzi ilitumia sio chini ya shilingi milioni tano na nusu (5,500,000/=) kwa ajili ya kuhudumia chaguzi hizo.

Kutokana na kupitishwa kwa Mpango Mkakati wa Chama (SP), iliamuliwa katika semina elekezi iliyofanyika katika Hoteli ya Belinda, Dar es Salaam, kwamba kila Kurugenzi ya Chama ipatiwe vifaa muhimu vya kuiwezesha kutimiza majukumu yake. Kazi ya kutafuta na kununua vifaa hivyo ilikuwa chini ya usimamizi wa Kurugenzi ya Oganaizesheni. Kurugenzi iliratibu ununuzi wa vifaa hivyo. Utaratibu mzuri wa ununuzi wa vifaa umewekwa na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa limeunda Kamati Maalum ya Manunuzi ya Chama. Kurugenzi inaweka kumbukumbu za manunuzi yote, pamoja na stakbadhi za manunuzi hayo.

Kurugenzi inasimamia vizuri mahudhurio ya watendaji katika Makao Makuu na Ofisi Kuu na wale wasiohudhuria au kuchelewa kufika kazini kumbukumbu zao huwekwa na kila mwisho wa mwezi hatua za nidhamu huchukuliwa dhidi yao kulingana na agizo la Katibu Mkuu. Kurugenzi pia inasimamia nidhamu ya watendaji Makao Makuu na Ofisi Kuu. Hata hivyo, utendaji wa ufanisi kwa kila mtendaji uko chini ya Kurugenzi ambayo mtendaji husika anatenda kazi zake.

Kurugenzi pia ni dhamana wa masjala ya Chama. Barua zote zinazoingia Makao Makuu au Ofisi Kuu hupokelewa na maafisa masjala na kisha kuwasilishwa kwa Katibu Mkuu ambaye baada ya kuziona huelekeza Kurugenzi ya kupelekewa kila barua. Kurugenzi kwa maagizo ya Katibu Mkuu, huzijibu barua zinazohusiana na Kurugenzi hii. Pia Kurugenzi imesambaza matoleo (circulars) kadhaa, hasa yale yanayohusiana na utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Chama kwa wilaya zote nchini.

Suala ambalo limekuwa ni la matatizo makubwa ni magari ya kuwawezesha viongozi na watendaji kusafiri katika utendaji wa shughuli zao. Magari yaliyopo ni machache na karibu yote yana uchakavu mkubwa unaosababisha magari hayo kupelekwa gereji kwa matengenezo mara kwa mara. Hili husababisha gharama kubwa kwa Chama. Aidha bei ya mafuta nayo iko juu na hivyo wakati mwengine magari kutoweza kusafiri kutokana na gharama kubwa za mafuta.

Kwa sababu Chama kama taasisi kinahitaji kuwa na usafiri wa kuaminika, uamuzi wa kuyauza baadhi ya magari yaliyochakaa sana na fedha zitakazopatikana ziongezewe nyengine ili kukunua magari mapya ya kuaminika umeshatolewa na Bodi ya Wadhamini. Tunategemea magari yaliyopo kuuzwa kwa awamu (phasing out) na magari mapya kununuliwa kulingana na uwezo wa kifedha wa Chama.

Kurugenzi ya Oganaizesheni, kwa maagizo ya Baraza Kuu la Uongozi la Taifa, imekuwa ikitoa huduma ya maji bure kwa wakaazi wanaoishi karibu na Ofisi Kuu, Buguruni.

6.1.3 Usimamizi wa Vikao vya Kitaifa na Uandishi na Utunzaji wa kumbukumbu za vikao:

Kurugenzi imejitahidi kuandaa na kusimamia vikao vya Baraza Kuu la Uongozi la Taifa na vya Kamati ya Utendaji ya Taifa kwa mujibu wa matakwa ya Katiba. Kwa kweli katika suala la vikao, Chama kimepata mafanikio makubwa, kwani hakuna kikao cha kawaida ambacho hakikuitishwa. Hili limetoa fursa kwa wajumbe wa vikao hivyo kujadili mambo mazito ya Chama na ya nchi na kutoa maamuzi, maazimio na maelekezo mazito, katika baadhi ya nyakati. Kufanyika kwa vikao vya kawaida na vya dharura kumeleta faida zifuatazo: kwanza kuondoa migogoro katika ngazi ya kitaifa kwa vile mambo yote yanawekwa bayana, kujengwa kwa utaratibu wa kujikosoa na kukosoana, na pia wakati mwengine kuchukuliwa hatua za nidhamu mapema na pia kuelimishana. Pili, kuwepo kwa vikao vya kawaida kumukijengea Chama heshima kutokana na maamuzi sahihi yanayotolewa na vikao hivyo. Tatu kuwepo kwa vikao vya kawaida kunatoa fursa kwa wajumbe kuhakikisha kuwa yale yaliyoamuliwa katika vikao vya nyuma yametekelezwa na kwa kiwango gani cha ufanisi.

Mbali na vikao vya Baraza Kuu la Uongozi la Taifa na Kamati ya Utendaji ya Taifa ambavyo vipo kwa mujibu wa Katiba ya Chama, Katibu Mkuu ameanzisha utaratibu wa kukutana na Wakurugenzi na Manaibu Wakurugenzi wa kila upande wa Jamhuri ya Muungano kila wiki. Utaratibu huu umesaidia sana katika kujenga mshikamano na maelewano baina ya Wakurugenzi wa kila upande na kuondoa, kwa kiasi kikubwa, mivutano na hali ya kutiliana shaka miongoni mwa Wakurugenzi. Utaratibu huu umesaidia sana kujenga kuaminiana, na kuwafanya Wakurugenzi wa kila upande kufanya kazi kama timu moja. Aidha, utaratibu huu unamuwezesha kila Mkurugenzi kujua Kurugenzi nyengine zinafanya shughuli gani katika kipindi husika, na pia kushauriana juu ya njia bora za kukabiliana na matatizo yanayojitokeza katika vipindi baina ya kikao kimoja cha Kamati ya Utendaji ya Taifa na chengine. Taarifa ya vikao hivyo vya mashauriano kwa kila upande huwasilishwa katika kikao cha Kamati ya Utendaji ya Taifa kinachofuata kwa madhumuni ya kutaarifiana mambo yaliyoshughulikiwa na kila upande, na kwamba kama kuna maamuzi yanayohitajika yachukuliwe na Kamati ya Utendaji ya Taifa basi uamuzi uchukuliwe.

Kurugenzi ya Oganaizesheni, licha ya kuandaa vikao hivyo, pia husimamia Sekretarieti ya Kamati ya Utendaji ya Taifa ambayo ndio yenye jukumu la kuchapisha nyaraka za agenda za vikao zinazotayarishwa na Kurugenzi husika, kisha kuzisambaza kwa wajumbe wa kikao husika kwa wakati. Sekretarieti pia ina jukumu la kuchukua kumbukumbu za vikao hivyo na kisha kutayarisha mihutasari ya vikao hivyo kwa ajili ya kuwasilishwa katika vikao vinavyofuata. Usimamizi wa Sekretarieti hii pamoja na kuipatia zana na vifaa vya kufanya shughuli zake kwa ufanisi uko chini ya Kurugenzi hii. Kwa hakika shughuli hii imesimamiwa vizuri na Kurugenzi na kuwa na mafanikio ya kujivunia.

6.1.4 Mipango ya Kukijenga na Kukiimarisha Chama:

Madhumuni ya chama cha siasa chochote kilicho makini ni kushika hatamu za dola. Katika nchi ambazo ni za kidemokrasia au zenye kudai kuwa ni za kidemokrasia chama huweza kushika hatamu za dola kupitia uchaguzi huru na wa haki. Ili chama kiweze kushinda uchaguzi hakina budi kikubalike na wananchi walio wengi. Hivyo jukumu kubwa la chama cha siasa makini ni kujijenga na kujiimarisha ili wananchi wakitambue na wajenge nacho imani. Kwa msingi huo, kazi kubwa ya Chama Cha Wananchi (CUF), kupitia Kurugenzi yake ya Oganaisesheni ni kujijenga hadi kufika kwa wananchi wenyewe mijini na vijijini.

Katika ujenzi na uimarishaji wa Chama, Kurugenzi iliandaa ziara mbali mbali za viongozi wakuu wa Chama. Katika kipindi cha Julai 2007 – Desemba 2008, Makamo Mwenyekiti wa Chama ametembelea takriban wilaya zote za Tanzania Bara kuhamasisha uchaguzi wa Chama ndani ya Chama. Mwenyekiti wa Taifa mara baada ya kurejea nchini mwezi Januari 2008, amefanya ziara mikoa ya Lindi, Mtwara, Mara, Tabora, Mbeya, Tanga, Mwanza, Dar es Salaam, na pia kutembelea visiwa vya Unguja na Pemba ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Chama na kuhutubia mikutano ya hadhara. Katibu Mkuu kadhalika amefanya ziara kadhaa katika mikoa ya Kagera, Tanga, Morogoro, Lindi, Mwanza na visiwa vya Unguja na Pemba. Ziara hizo zimekuwa na mafanikio makubwa; hususan zile za Unguja na Pemba ambazo ziliingiza wanachama wapya 12,698. Manaibu Katibu Wakuu nao kwa nyakati tofauti wamefanya ziara katika wilaya mbali mbali pande zote za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katika kuendelea kutekeleza jukumu hilo muhimu, Kurugenzi hii ya Oganaizesheni katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, hususan tangu kupitishwa kwa Mpango Mkakati wa Chama (SP) hapo 2006, imefanya au kusimamia shughuli zifuatazo:

(a) Kuzitaka Wilaya zote, kupitia matoleo (circulars) kuhakikisha kuwa:
(i) Kila kijiji walau kina tawi moja la Chama.
(ii) Matawi yote yanakuwa na Mratibu mmoja kwa kila nyumba ishirini.
(iii) Kuwatumia viongozi wa Chama wenye nyadhifa za kiserikali na wasiokuwa na nyadhifa hizo pamoja na waliokuwa wagombea wa Chama katika chaguzi za Ubunge, Uwakilishi na Udiwani katika kukijenga Chama.
(iv) Kuwataka viongozi wa ngazi za chini kuwatambua watu mashuhuri na wenye kauli katika jamii na kujenga nao mahusiano mazuri, na kuwafanya wakikubali Chama.

Matoleo hayo yalitolewa na kusambazwa katika wilaya zote. Kwa bahati mbaya Kurugenzi haikufaulu kupata marejesho (feedback) kutoka Wilaya. Ndio maana ikaanzishwa OSPI (Operation Strategic Plan Implementation) ili viongozi na wajasiri wa Chama washuke hadi chini kufuatilia utekelezaji wa Mpango Mkakati.

(b) Kurugenzi imefuatilia kwa karibu uwekaji wa Waratibu wa Chama. Kwa upande wa Zanzibar, kazi hii imefanikiwa kwa kiwango cha asilimia 85%. Kwa upande wa Tanzania Bara kuna mafanikio ya kiasi katika maeneo ya SP, na hususan katika Wilaya za Mkoa wa Dar es Salaam, Bukoba (M), Bukoba (V), Muleba, Tanga (M), Tunduru, na Kilwa.

(c) Baada ya kuasisiwa OSPI, Kurugenzi imefanikiwa kuwatumia vyema Wajasiri wa Chama ambao hutafutwa na kuandaliwa na Kurugenzi ya Siasa. Wajasiri hao hupelekwa katika maeneo ya SP kabla viongozi wakuu na timu zao kuwasili, na hubaki huko baada ya viongozi hao kuondoka. Wajasiri hushirikiana na viongozi wa Wilaya, Majimbo na Kata katika kazi za ujenzi na uimarishaji wa Chama. Kwa kweli maeneo ambayo Wajasiri wamepelekwa kuna mafanikio makubwa, hasa katika kuingiza wanachama wapya, kufungua matawi mapya ya Chama, na kuwekwa kwa Waratibu wa Chama.

6.1.5 Kuandaa na Kusimamia Chaguzi:

Chama Cha Wananchi (CUF) kinashughulikia chaguzi kuu za aina mbili:

(a) Chaguzi za Chama Ndani ya Chama; na
(b) Chaguzi za Nchi zinazoshirikisha vyama vya siasa vyengine.

(a) Chaguzi za Chama Ndani ya Chama:

Chama chetu kimejiwekea utaratibu wa kupata viongozi wa kukiendesha Chama mara moja katika kila muhula wa miaka mitano. Uchaguzi wa muhula uliopita ulifikia kilele kwa uchaguzi wa uongozi wa kitaifa uliofanywa na Mkutano Mkuu wa Taifa wa Tatu wa Chama uliofanyika tarehe 23 – 28 Februari, 2004. Hivyo uongozi ulioko madarakani unafikia mwisho wake mara kabla ya kuchaguliwa uongozi mpya wa kitaifa katika Mkutano Mkuu wa Taifa huu wa tarehe 23 – 27 Februari, 2009.

Katika kuhakikisha kuwa uchaguzi wa uongozi mpya unafanywa kwa njia za kidemokrasia zilizo wazi na kuwa na uchaguzi wa haki, Baraza Kuu liliamua kwa makusudi kuwa uchaguzi wetu katika ngazi za chini ufanyike kikanda na kwa awamu. Njia hiyo ilionekana ni sahihi katika kuhakikisha kuwa ngazi ya Taifa inasimamia kwa makini chaguzi kuanzia ngazi ya kata kwa upande wa Tanzania Bara, ambako katika sehemu nyingi Chama bado hakijaota mizizi. Kwa upande wa Zanzibar Ngazi ya Taifa ilisimamia ngazi ya Wilaya tu. Halikadhalika uamuzi wa kuendesha chaguzi za ndani ya Chama kikanda ulitokana na kuwa ni njia bora ya kumudu gharama za kuendesha uchaguzi huo kwa nchi nzima ambayo ni kubwa sana.

Katika kufanikisha chaguzi kuanzia ngazi ya matawi hadi wilaya kwa kila kanda, utaratibu ufuatao ulifuatwa:

(i) Kuandaa ziara ya uhamasishaji kwa kila wilaya iliyomo katika husika.
(ii) Katika kuhakikisha uchaguzi unaendeshwa vyema na kuondoa malalamiko ya msingi yatokanayo na usambazaji na ugawaji wa fomu za kugombea, Timu tangulizi ziliasisiwa katika baadhi ya maeneo, hususan ya SP, ambazo zilihakikisha kupatikana kwa fomu na hata wagombea bora katika maeneo hayo ya uchaguzi.
(iii) Kuwapeleka wasimamizi wa chaguzi kila wilaya ambao walisimamia chaguzi katika kata, na kisha kusimamia uchaguzi wa wilaya ili kupata viongozi wa wilaya.

Kwa wilaya chache, ilibidi wasimamizi wapelekwe kusimamia chaguzi kuanzia ngazi za matawi. Morogoro Mjini ni miongoni mwa wilaya hizo. Katika baadhi ya wilaya chaguzi zilibidi ziahirishwe zaidi ya mara moja kutokana na matatizo yaliyojitokeza. Miongoni mwa wilaya hizo ni Kibaha, Urambo, Biharamulo, Kigoma (V), Misungwi, Kilindi, Morogoro(M), Morogoro(V), Kinondoni na Uyui.

Pia utaratibu uliwekwa wa wagombea waliokuwa hawakururidhika kukata rufaa. Baraza Kuu la Uongozi la Taifa liliunda Kamati ya Rufaa ambayo iliweza kusikiliza jumla ya rufaa 50 kwa Tanzania Bara na Zanzibar. Kuna maeneo machache (Morogoro Mjini, Biharamulo na Kata ya Mwananyamala, Dar es Salaam) ambako wahusika hawakuridhika na maamuzi ya Kamati ya Rufaa na hao rufaa zao itabidi zisikilizwe na Kamati ya Rufaa ya Mkutano Mkuu.

Pamoja na matatizo yaliyojitokeza hapa na pale jumla ya wilaya 99 (73.88%) zimefanikiwa kukamilisha uchaguzi na zimewakilishwa katika Mkutano Mkuu huu.

(b) Chaguzi za Nchi:

Chama cha Wananchi (CUF) kilishiriki kikamilifu katika chaguzi za Serikali za Vitongoji, Vijiji na Mitaa za 2004, na katika Uchaguzi Mkuu wa nchi wa 2005. Kurugenzi ya Oganaizesheni ilihusika kikamilifu katika chaguzi zote.

Kurugenzi ilikuwa na jukumu la kuhakikisha kuwa Chama kinapata wagombea katika nafasi nyingi iwezekanavyo katika chaguzi hizo. Chama kiliweka wagombea ubunge 215 (92.67%), uwakilishi 50 (100%), madiwani 2022 (77.71%) na sehemu kubwa ya wagombea katika vijiji, vitongoji na mitaa. Katika hili mafanikio ya ushindi yaliyopatikana ni kama ifuatavyo; Wenyeviti wa Vitongoji 2,101 (3.7%), Wenyeviti wa Vijiji 294 (2.9%), Wajumbe wa Halmashauri ya Vijiji 6,894 (4.01), Wenyeviti wa Mitaa 157 (5.97%), Wajumbe wa Halmashauri ya Mitaa 786 (7.18%) na Wajumbe wa Halmashauri ya Mitaa Viti Maalum Wanawake 350 (6.63%).

Kwa maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa 2005, Kurugenzi ilijitahidi kutafuta wagombea wa udiwani , ubunge na uwakilishi, na Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mgombea Urais wa Zanzibar. Kwa upande wa Urais wa Jamhuri ya Muungano, Mgombea wa Chama alipata, kwa mujibu wa takwimu za Tume ya Taifa ya Uchaguzi, jumla ya kura 1,158,851 (10.27%) na kuwa mshindi wa pili kwa wingi wa kura.

Kwa upande wa Mgombea Urais wa Zanzibar, kama kawaida uchaguzi ulichafuliwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar pamoja na vyombo vya dola vya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Hivyo Chama hakikuyakubali matokeo hayo. Uchaguzi wa Zanzibar ulikithiri kwa mizengwe, vitisho na ukiukaji wa hali ya juu wa haki za binadamu.

Kwa uchaguzi wa Uwakilishi, Tume ya Uchaguzi ilitangaza ushindi kwa wagombea wa CUF kumi na tisa (19) mmoja kutoka kisiwa cha Unguja chenye majimbo thelathini na mbili (32) na waliobaki kutoka kisiwa cha Pemba chenye majimbo kumi na nane (18).

Matokeo ya uchaguzi wa ubunge yalikuwa kama ya Uchaguzi wa Wawakilishi kwa upande wa Zanzibar, yaani ushindi waliotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi ni kumi na tisa (19). Kwa upande wa Bara, hali ilikuwa ni ya kusikitisha. Hakuna hata Mbunge mmoja wa kuchaguliwa aliyetangawzwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

Kutokana na hali hiyo, kwa upande wa Baraza la Wawakilishi Chama kiliunda Kambi ya Upinzani katika Baraza na kutoa Kiongozi wa Upinzani katika Baraza (Mhe. Abubakar Khamis Bakary). Kwa upande wa Bunge Chama chetu ndicho kilichofanikiwa kuwa na Wabunge wengi zaidi kuliko chama kingine chochote cha upinzani kwa kuwa na Wabunge wengi wa kuchaguliwa (19) na Wabunge Viti Maalum Wanawake (11) ambapo saba (7) walitoka Tanzania Bara na wanne (4) walitoka Zanzibar. Hawa waliungana na Wabunge kutoka Baraza la Wawakilishi (2) na hivyo kuwa na jumla ya wabunge thelathini na mbili (32) katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa kushirikiana na vyama vingine vya upinzani, Wabunge wa Chama chetu wameunda Kambi ya Upinzani Bungeni na kutoa Kiongozi wa Kambi ya Upinzani katika Bunge (Mhe. Hamad Rashid Mohamed).

Kwa upande wa Madiwani tulishinda viti 123 na tukapata Madiwani Viti Maalum Wanawake 49. Jedwali lifuatalo linaonyesha ushindi wa Ubunge na Uwakilishi.

USHINDI WA CUF KATIKA UCHAGUZI WA UBUNGE NA UWAKILISHI

Wilaya Idadi ya Majimbo Idadi ya Wabunge wa CUF waliochaguliwa Idadi ya Wawakilishi wa CUF waliochaguliwa
Micheweni 4 4 4
Wete 5 5 5
Chake Chake 4 4 4
Mkoani 5 5 5
Mjini 10 1 1
Magharibi 9 – –
Kati 3 – –
Kaskazini “A” 5 – –
Kaskazini “B” 3 – –
Kusini 2 – –
Tanzania Bara 182 – –
Jumla 232 19 19

Kabla ya Chama kuingia katika chaguzi hizo, ilibidi Kurugenzi iandae mipango ya kukabiliana na chaguzi hizo, ikiwemo mipango ya kuhamasisha wananchi kujitokeza kuomba nafasi za kugombea. Pia Kurugenzi ilibeba jukumu la kutafuta na kuwafundisha mawakala kwa wagombea Ubunge na Uwakilishi, Udiwani na Urais wa Zanzibar na Urais wa Jamhuri ya Muungano. Baadhi ya mawakala, kwa bahati mbaya hawakulipwa, kutokana na fedha kukabidhiwa wagombea na mameneja wa kampeni wa uchaguzi wa majimbo na wengine hawakuwa waaminifu na hivyo kutowalipa mawakala. Hili limekuwa likilalamikiwa hadi hii leo. Lakini pia tatizo lilijitokeza pale ambapo mawakala walishindwa kuwasilisha fomu za matokeo kama ushahidi kuwa kweli walitumika kama mawakala wa Chama. Bado malalamiko yapo. Baraza Kuu la Uongozi la Taifa liliamua kuwa mawakala ambao bado hawajalipwa waombwe radhi kupitia viongozi wa wilaya zao. Kurugenzi imezifahamisha Wilaya juu ya uamuzi huo na kunakili taarifa hiyo kwa kata zote. Pengine wilaya zimeshindwa kuwafahamisha mawakala tatizo hili ndio maana bado malalamiko yanaendelea.

6.1.6 Huduma kwa Wilaya:

Huduma kwa Wilaya zimeendelea kutolewa katika kipindi chote cha miaka mitano. Mambo muhimu ambayo Makao Makuu na Ofisi Kuu yanatoa kama huduma kwa wilaya ni pamoja na :

(a) Kupeleka ruzuku kila mwezi
(b) Kupeleka nyenzo za kazi kama kadi, bendera, Katiba, na Kanuni
(c) Kuwa na mawasiliano ya karibu na Wilaya.

(a) Ruzuku kwa Wilaya:

Mkutano Mkuu wa Taifa wa Tatu wa Kawaida uliofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia tarehe 23 – 28 Februari, 2004 uliagiza, miongoni mwa mambo mengine, kila Wilaya ya Chama ipatiwe ruzuku ya kuwezesha Wilaya alau kulipia kodi ya ofisi zao. Kwanza iliamuliwa kuwa kila mwezi kila wilaya ipate ruzuku ya shilingi elfu kumi tu (10,000/-). Baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2005 ambapo ruzuku ya Chama ilipanda marudufu, Baraza Kuu la Uongozi la Taifa liliiagiza Kamati ya Utendaji ya Taifa iwe inapeleka katika kila wilaya ruzuku ya shilingi laki moja kwa mwezi (100,000/). Baraza Kuu likaweka masharti ya fedha hizo kupelekwa Wilayani. Miongoni mwa masharti hayo ni pamoja na:

(i) Wilaya ifungue Akaunti Benki
(ii) Kabla ya kupelekewa ruzuku ya mwezi, basi Katibu wa Wilaya awasilishe maamuzi ya Kamati ya Utendaji ya Wilaya kuonyesha jinsi gani fedha hizo zitumike, na pia Taarifa ya Mapato na Matumizi.

Kurugenzi imejitahidi kutekeleza maagizo ya vikao hivyo vikuu vya Chama kwa kiwango kikubwa. Wakati mwengine kutokana na kuzuka kwa mambo ya dharura, Kamati ya Utendaji ya Taifa huamua kusitisha kupeleka fedha hizo kwa kipindi cha fulani ili zipatikane fedha za kukidhi dharura iliyojitokeza. Wakati mwengine Wilaya hushindwa kukidhi masharti yaliyowekwa na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa na hivyo kukosa kupelekewa fedha zao kwa wakati. Mara nyengine Wilaya hudai kuwa haipati ruzuku yake, kumbe viongozi wa wilaya hiyo huwa hawajenda benki kwa kipindi kirefu, na wanapoelezwa waende hukuta fedha za miezi kadhaa zimerundikana.

Pamoja na yote hayo, Wilaya 121 zimemudu kutekeleza maamuzi ya Baraza Kuu la Uongozi la Taifa kwa kutuma taarifa zao za Mapato na Matumizi, au alau kutuma taarifa ya kibenki na hivyo kutimiza sifa ya kutumiwa ruzuku. Jumla ya TShs. 53,300,000/= (2006), TShs. 86,190,000/= (2007) na TShs. 73,500,000/= (2008) zimetumwa katika Wilaya.

Pamoja na kasoro za hapa na pale, kwa kiwango kikubwa huduma hii hufikishwa wilayani.

(b) Kupeleka Nyenzo za Kazi wilayani:

(i) Katika shughuli ya kujenga na kuimarisha Chama, suala la vitendea kazi kama bendera, Katiba, Kanuni na bidhaa zenye nembo ya Chama kama T-Shirts, vitenge, kanga, kofia, beji, n.k. ni muhimu sana. Kurugenzi kulingana na uwezo wa kifedha wa Chama katika kipindi cha Julai 2006 na Januari 2009, imeweza kuchapisha bendera za matawi 11,000, bendera za waratibu 17,800, Katiba (2003) za Chama nakala 6,963 na kadi 200,000 zenye thamani ya jumla ya TShs. 43,754,100/= na kuzisambaza katika Wilaya mbali mbali, Tanzania Bara na Zanzibar. Ama kuhusu bidhaa zenye nembo za Chama, sera iliyoamuliwa na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa ni kuiacha kazi hiyo ifanywe na watu binafsi wenye mapenzi na Chama ili watengeneze bidhaa hizo na kuziuza wao wenyewe. Chama katika hili kinatakiwa kuhakikisha kuwa nembo na alama zake hazipotoshwi, na kuwaomba watengenezaji wauze kwa bei nafuu ili wanachama na wananchi wengi zaidi waweze kumudu kuzinunua.

Kumekuwa na malalamiko mengi kutoka wilayani na ngazi nyengine za Chama kwamba bendera na katiba hazitoshi. Hili ni kweli. Sababu ni kwamba Chama kinakuwa kwa haraka, mahitaji ya vifaa hivyo yanaongezeka kila uchao, lakini uwezo wa kifedha wa Chama haulingani na mahitaji halisi. Hata hivyo juhudi zitaendelea kuchukuliwa ili kuhakikisha kuwa upungufu uliopo tunaupunguza.

(ii) Katika kuziwezesha Wilaya kukabiliana na tatizo la usafiri, Chama kilinunua na kusambaza pikipiki 160 katika wilaya. Ziko wilaya ambazo zimezitunza vizuri pikipiki hizo. Lakini pia kuna wilaya ambazo hawakuzitunza ipasavyo pikipiki hizo. Katika baadhi ya wilaya, pikipiki zimeuzwa, au kukongolewa, na kuna madai ya piki piki kuibiwa au kuwekwa rehani. Tatizo linalolalamikiwa sana ni gharama za matengenezo na mafuta ya kuendeshea pikipiki hizo. Uamuzi wa Baraza Kuu ni kuwa gharama hizo zitokane na ruzuku ambayo kila Wilaya hupata.

(iii) Katika baadhi ya Wilaya, Kata na Majimbo, Chama, kupitia Kurugenzi ya Oganaizesheni kimetoa baiskeli kwa malengo ya kusaidia usafiri katika maeneo hayo.

(iv) Aidha, Chama, kupitia Kurugenzi ya Oganaizesheni kimetoa mabomba (Megaphones na Public Address System) chache sana na kuzigawa katika baadhi ya Wilaya, Tanzania Bara na Zanzibar.

(c) Mawasiliano na Wilaya:

Jukumu la kuwa na mawasiliano ya mara kwa mara baina ya Makao Makuu au Ofisi Kuu na Wilaya ni la Kurugenzi ya Oganaizesheni. Lazima tukiri kuwa pamekuwa na kasoro kubwa ya mawasiliano baina ya Makao Makuu na Ofisi Kuu kwa upande mmoja na wilaya kwa upande wa pili. Ni kweli, ukiacha matoleo machache yanayopelekwa wilayani, mara nyingi huwa hakuna miongozo wala maelekezo yanayotoka Taifa kwenda ngazi za chini. Au mara nyengine barua kutoka wilayani hazijibiwi kabisa, au huchukua muda mrefu kujibiwa tena kwa lugha ya mkato. Wakati mwengine viongozi wa wilaya wanapopiga simu kuulizia mambo kadhaa au kutaka maelekezo, hujibiwa kwa lugha isiyoridhisha. Hii ni kasoro ambayo hata Baraza Kuu la Uongozi la Taifa imeibaini na kujaribu kuirekebisha. Pamoja na marekebisho hayo, pengine hali haijawa ya kuridhisha. Hivyo juhudi zitazidi kuchukuliwa katika kipindi kijacho kurekebisha kasoro hii. Kwa upande mwingine pamekuwa na uzito wa kuwasilisha taarifa mbali mbali toka wilayani; hususan mihutasari ya vikao, taarifa za mapato na matumizi, takwimu za wanachama, waratibu na matukio muhimu, hali ambayo inakwaza utendaji Makao Makuu na Ofisi Kuu za Chama.

Mwisho:

Pamoja na ufinyu wa bajeti, na kasoro za kibinaadamu, Kurugenzi ya Oganaizesheni imejitahidi sana kutekeleza wajibu wake. Tunakiri kuwepo kwa upungufu wa kibinaadamu hapa na pale, lakini juhudi zimechukuliwa na zitaendelea kuchukuliwa kurekebisha mapungufu kila yanapojitokeza.

6.2 KURUGENZI YA SIASA:

Taarifa ya Kurugenzi ya Siasa ina sehemu tano zifuatazo:

1. Utangulizi
2. Idara ya Mafunzo
3. Idara ya Utafiti
4. Idara ya Sera, na
5. Idara ya Makundi

6.2.1 Utangulizi:

Kurugenzi ya Siasa ilianzishwa na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa baada ya kupitishwa kwa Mpango Mkakati wa Chama (SP) hapo 2006. Kurugenzi hii ilianzishwa kwa madhumuni ya kuimarisha uwezo wa kiutendaji wa Chama. Ilionekana kuna umuhimu wa kuongeza uwezo wa kiutendaji wa viongozi na watendaji wa chama katika ngazi zote. Hivyo suala la mafunzo lilipewa kipaumbele katika ujenzi na uimarishaji wa Chama.

Halikadhalika, ili Chama kijipe uwezo wa kuyachambua mambo muhimu ya nchini na hata ya nje ya nchi na kufanya maamuzi sahihi, suala la utafiti haliwezi kupuuzwa. Utafiti wa kina utakiwezesha Chama kupitia sera zake na hata kubuni sera mpya za Chama.

Aidha, makundi maalum katika jamii, kama vijana, wanawake na wazee, yana umuhimu mkubwa katika kukifanya Chama kikubalike nchini. Kwa kulitambua hilo, Baraza Kuu la Uongozi la Taifa liliamua kuyaondoa mabaraza ya vijana, wanawake na wazee, na badala yake makundi hayo kuundiwa jumuiya za Chama.

Viongozi wenye nyadhifa za kiserikali wanaotokana na Chama, kama Viongozi wa Serikali za Vitongoji, Vijiji na Mitaa, Madiwani, Wabunge na Wawakilishi wana mchango mkubwa katika kukifanya Chama kikubalike na jamii. Viongozi hao wakitekeleza vizuri sera za Chama, au pale wanapoikosoa serikali na kueleza sera mbadala za Chama, wananchi watajenga imani na matumaini na Chama, na hivyo kujiongezea uungwaji mkono katika jamii.

Kwa hivyo itaonekana wazi kuwa Kurugenzi hii inabeba jukumu zito la kukifanya Chama chetu kiwe na uwezo wa kutenda shughuli zake kitaalamu na kwa ufanisi, na hivyo kukifanya Chama kitawale nyoyo za Watanzania.

Mwenyekiti wa Taifa, Mheshimiwa Profesa Ibrahim Haruna Lipumba alimteua Mheshimiwa Wilfred Munganyizi Lwakatare, Naibu Katibu Mkuu (Bara) kuwa Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Siasa, na Mheshimiwa Dk. Juma Ameir Muchi kutoka Zanzibar, kuwa Naibu Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Siasa.

6.2.2. Idara ya Mafunzo:

Mara baada ya kuundwa kwake, Kurugenzi ya Siasa ilitayarisha Mpango Kazi wa Kurugenzi wenye nia ya kutekeleza majukumu ya Mpango Mkakati wa Chama (SP) kwa yale majukumu yaliyoko chini ya Kurugenzi hii. Kazi hiyo iliwasilishwa katika kikao cha Kamati ya Utendaji ya Taifa ambayo baada ya kufanya marekebisho madogo madogo, iliupitisha. Hivyo kazi ya utekelezaji ilianza mara moja.

Miongoni mwa shughuli muhimu zilizofanywa na Idara ya Mafunzo ni pamoja na zifuatazo:

(i) Kutoa mafunzo kwa Madiwani wa Tanzania Bara na wa Zanzibar katika awamu mbili na katika kanda nne. Kazi hii ilianza 2006 na kuendelea hadi 2008. Kanda hizo ni Morogoro, Pemba, Lindi, Bukoba na Mwanza na idadi ya Madiwani 88 Tanzania Bara na 81 Zanzibar wamepatiwa mafunzo hayo.

(ii) Kuratibu mafunzo yaliyotolewa kwa Wabunge na Wawakilishi wa CUF kwa madhumuni ya kuwajengea uwezo mkubwa zaidi wa kuandika hotuba na kuchangia mijadala katika Bunge na Baraza la Wawakilishi, na pia kutambua wajibu wao wakiwa wawakilishi wa wananchi. Mafunzo hayo yalifadhiliwa na Friedrich Naumann Foundation na yalifanyika katika Hoteli ya White Sands, Dar es Salaam katika 2007 na Zanzibar Beach Resort 2008.

(iii) Kuratibu mafunzo ya Wakufunzi (TOT) yaliyotolewa kwa awamu mbili, moja 2006 mafunzo ya wawezeshaji kwa ajili ya Madiwani awamu ya kwanza, 2007 mafunzo ya Wawezeshaji kwa ajili ya Madiwani awamu ya pili na 2008 Mafunzo ya wawezeshaji kwa ajili ya Viongozi wa Wilaya katika 2007 na ya pili katika 2008, mafunzo yaliyofadhiliwa na Friedrich Naumann Foundation na Chama cha Venstre cha Norway.

(iv) Kuratibu safari ya Mheshimiwa Thuwaiba Idris ya Ujerumani alikokwenda kuchukua mafunzo ya Advanced Facilitation Training na ambayo yalifadhiliwa na Friedrich Naumann Foundation katika 2007.

(v) Kuratibu mafunzo kwa viongozi wa Wilaya za Tanzania Bara na Zanzibar kwa lengo la kuwapa viongozi hao mbinu za kujipanga katika kulikabili zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura. Mafunzo hayo kwa 2008 mpaka 2009 yalitolewa kwa Wilaya zifuatazo:

S/NO WILAYA IDADI YA VIONGOZI
1. Micheweni 10
2. Chake Chake 10
3. Kati 10
4. Kaskazini B 10
5. Wete 10
6. Mkoani 10
7. Kusini 10
8. Kaskazini A 10
9. Mjini 10
10. Magharibi 10
11. Ilala 8
12. Kinondoni 8
13. Mkuranga 8
14. Bukoba (M) 8
15. Bukoba (V) 8
16. Muleba 8
17. Temeke 8
18. Morogoro (M) 8
19. Morogoro (V) 8
20. Kilwa 8
21. Liwale 8
22. Mafia 8
23. Lindi 8
24. Nachingwea 8
25. Rungwa 8
26. Mtwara (V) 8
27. Tandahimba 8
28. Newala 8
29. Geita 8
30. Kwimba 8
31. Sengerema 8

Mafunzo haya yanafadhiliwa na Chama cha Venstre cha Norway.

(vi) Kuratibu mafunzo kwa Wenyeviti, Makatibu, na Wakuu wa Vitengo vya Wilaya yaliyotolewa kwa ajili ya kuwapa au kuwaongezea uwezo viongozi hao kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi. Mafunzo hayo yalitolewa kwa viongozi wa Wilaya za Pemba, Unguja, Dar es Salaam, Bukoba (M) na Bukoba (V). Pia yalitolwa kwa viongozi wa Wilaya za Mkuranga, Kilwa na Lindi. Mafunzo kwa viongozi wa wilaya nyengine yatatolewa katika 2009. Mafunzo hayo yote yanafadhiliwa na Chama cha Venstre cha Norway.

(vii) Kuratibu programu ya mafunzo yanayotolewa na International Academy for Leadership (IAF) kwa ajili ya viongozi na wanachama wa CUF. Mafunzo hayo hutolewa Ujerumani, na hata nchi nyengine.

(viii) Yalifanyika mafunzo ya utafiti tarehe 8 – 14 Septemba, 2008 Dar es Salaam. Jumla ya Watafiti 25 wametayarishwa kukisaidia Chama katika kufanya tafiti mbali mbali na kuwasaidia Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Wabunge.

(ix) Ilifanyika Semina juu ya Katiba, Sheria na Maendeleo ya Zanzibar iliyofanyika Unguja na Pemba 2007 na iliendeshwa na Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar. Jumla ya Viongozi 20 wa CUF walipata mafunzo hayo.

(x) Chuo Kikuu cha Dar es Salaam chini ya mpango wa Utafiti na Mafunzo kuhusu Demokrasia (REDET) kinaendelea kutoa mafuzo kwa vijana wa vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu Zanzibar. Jumla ya vijana 50 huchaguliwa kwa kila muhula wa mafunzo na kila baada ya miezi mitatu. CUF imeshapeleka vijana 240 katika mihula 12. CUF inapewa nafasi 20, CCM nafasi 20 na vyama vyengine nafasi 10 kwa kila muhula kwa uwiano sawa kati ya wanawake na wanaume.

6.2.3 Idara ya Utafiti:

Idara ya Utafiti imekabiliwa na matatizo mawili makubwa: Ukosefu au upungufu mkubwa wa fedha, na ukosefu wa watafiti wenye utaalamu wa kutosha wa kufanikisha shughuli za utafiti. Baada ya kuundwa kwake, Idara ilikuwa na afisa mmoja tu kwa upande wa Ofisi Kuu, na mmoja tu kwa upande wa Makao Makuu, ambaye ndiye aliyetarajiwa kufanya tafiti zote muhimu, jukumu ambalo lilikuwa gumu kwake. Hali hii imeanza kubadilika baada ya Chama kuchukua juhudi za makusudi za kuwashawishi wasomi, hasa wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu kujiunga na Chama na kukitumikia Chama kwa njia ya kujitolea.

Vijana wa vyuo vya elimu ya juu waliotafutwa na Wabunge wa CUF kwa ajili ya kuwasaidia shughuli zao Bungeni katika tafiti wamekubali pia kukisaidia Chama kwa upande wa Tanzania Bara. Tayari vijana hao wamepatiwa ofisi yao katika Ofisi Kuu na sasa kazi ya kuweka samani na vifaa vya kuwawezesha kufanya kazi zao kwa utulivu inaendelea.

Kwa upande wa Zanzibar, wamepatikana vijana kutoka vyuo vya elimu ya juu ambao nao wamekubali kukifanyia utafiti Chama katika nyanja mbali mbali. Kurugenzi inawatafutia ofisi na vifaa vya kuwawezesha kufanikisha kazi hii.

Katika kipindi hiki tangu ianzishwe, Idara imefanikiwa kufanya shughuli zifuatazo:-

(a) Kukusanya maoni ya Wazee katika Mkoa wa Dar es Salaam juu
ya Mazungumzo baina ya CUF na CCM ya kuupatia ufumbuzi
wa kudumu mgogoro wa kisiasa wa Zanzibar; juu ya Ushirikiano
wa vyama vya siasa vinne, CUF, CHADEMA, NCCR-Mageuzi,
na TLP; na baada ya mazungumzo ya CCM na CUF kutofanikiwa. Kazi ilifanyika 2007 na 2008. Taarifa za maoni hayo zilifanyiwa uchambuzi na kutolewa mapendekezo ambayo yalifikishwa kwa viongozi wakuu wa Chama.

(b) Kufanya utafiti juu ya utendaji wa Serikali ya Awamu ya Nne inayoongozwa na Rais Jakaya Mrisho Kikwete. Mambo yaliyofanyiwa utafiti baina ya Mei – Agosti, 2006 ni:
i. Adha ya usafiri kwa wanafunzi katika Jiji la Dar es Salaam.
ii. Kupanda kwa gharama za maisha.
iii. Mikataba mibovu ambayo iliingiwa na Serikali.
iv. Ukosefu wa Utawala bora nchini.
v. Utoaji wa huduma ya elimu kwa wanyonge.
vi. Ununuzi wa rada.

Kwa kipindi cha Oktoba, 2006 – Juni 2007, mambo yaliyoshughulikiwa katika Utafiti ni:

(i) Madai ya Serikali kuhusu kupata faida ndogo katika sekta ya madini.
(ii) Taarifa ya Kuharakishwa kwa Uundwaji wa Shirikisho la Afrika
Mashariki.
(iii) Matatizo ya wafanya biashara ndogo ndogo (Wamachinga).
(iv) Taarifa ya kunyimwa mikopo wanafunzi wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu (DUCE).
(v) Sera za uchumi, fedha, biashara na uwekezaji.
(vi) Operesheni Bomoa bomoa (Tabata).

(c) Idara pia ilijishughulisha na kufanya utafiti kuhusu uimara, udhaifu, fursa na
hatari zinazozikabili Chama baina ya Mei 2006 na Novemba 2007. Mambo ya Chama yaliyofanyiwa utafiti ni pamoja na :-

(i) Matatizo yaliyojitokeza kabla na baada ya kikao cha Barza la Taifa la Wanawake lililofanyika Mei 2006.
(ii) Mikakati ya Chama na utekelezaji wake.
(iii) Jinsi ya kuwaenzi waasisi wa Chama.
(iv) Udhaifu wa Chama kutumia usanii na wasanii katika kujitangaza.
(v) Wimbi la viongozi wa kitaifa wa CUF kuhamia CCM.
(vi) Uchaguzi Mdogo wa Jimbo la Tunduru wa 2007.

(d) Idara ilishughulikia kulifanyia uhakiki Daftari la Kudumu la Wapiga Kura la Zanzibar la 2005.

(e) Idara ilifanya utafiti kuhusu vyama vya siasa vyengine. Miongoni mwa yaliyoshughulikiwa katika kipindi kilichopita ni:

(i) Ahadi za CCM ya “Maisha Bora kwa kila Mtanzania”.
(ii) Taarifa ya wana-CCM wa Kanda ya Ziwa kulalamikia kutelekezwa na Serikali ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete.
(iii) Taarifa ya CCM ya kukiri kuwa chama hicho kimejaa rushwa.
(iv) Jinsi CCM ilivyopoteza dira na mwelekeo baada ya miaka thelathini tangu kuzaliwa kwake.

Taarifa za utafiti huwa zinafikishwa kwa Idara ya Sera kwa kufanyiwa kazi na pia kwa viongozi wakuu wa Chama ambao huyatumia katika hotuba zao katika mikutano ya hadhara, katika makongomano na semina na katika kupanga mikakati ya kuipiku CCM.

Idara hii ni muhimu sana, na katika kipindi kijacho itaimarishwa zaidi kwa kuipatia fedha zaidi na watafiti wenye uwezo, wakiwemo wasomi. Watendaji waliopo sasa watapatiwa mafunzo zaidi.

6.2.4 Idara ya Sera:

Idara ya Sera imeanzishwa kwa malengo yafuatayo:

(a) Kuhakikisha kuwa wakati wote Chama kinakuwa na sera, mipango na mikakati inayokwenda na wakati, kwa kuzingatia mabadiliko ya kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni yanayotokea katika jamii, na pia kwa kuzingatia muelekeo wa Serikali, CCM na vyama vyengine.
(b) Kupokea na kutumia matokeo ya tafiti zinazofanywa na Idara ya Utafiti na taasisi nyengine na kuyachambua na kuyatumia katika kukishauri Chama kuangalia upya sera, mipango na mikakati yake.
(c) Kupokea maoni ya wanachama na wapenzi wa Chama juu ya marekebisho ya Katiba, Utayarishaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama, na Sera za Chama, kuyafanyia uchambuzi maoni hayo na kisha kukishauri chama ipasavyo.
(d) Idara ilisimamia kwa ukamilifu mchakato wa kukusanya maoni juu ya uharakishwaji wa uundwaji wa Shirikisho la Afrika Mashariki.

Tangi kuanzishwa kwake, Idara hii imekuwa ikiratibu mchakato wa kuandaliwa kwa rasimu ya Katiba mpya za nchi kwa kushirikiana na wadau wengine na wasomi waliobobea katika fani ya sheria zinazohusiana na katiba (constitutional lawyers). Pia Idara imekuwa ikishirikiana na taasisi na mashirika ya ndani na nje ya nchi kwa madhumuni ya kukusanya taarifa ambazo zitaisaidia Idara katika kutekeleza wajibu wake.

Kwa wakati huu, Idara imeanza matayarisho ya rasimu za Ilani za Uchaguzi za Chama kwa ajili ya Uchaguzi wa Serikali za Vitongoji, Vijiji na Mitaa unaotazamiwa kufanyika mwezo Oktoba 2009.

Matarajio ya Idara ni kujiongezea uwezo wa kitaaluma na kuongeza watendaji ili iweze kuyakabili majukumu ya kukishauri Chama juu ya mambo ya sera kwa ufanisi wa kuridhisha.

6.2.5 Idara ya Makundi:

Kama ilivyoelezwa katika utangulizi wa Kurugenzi hii, Idara ya Makundi inashughulikia makundi matatu muhimu katika jamii: Wanawake, Vijana na Wazee. Pia inashughulikia utendaji wa kazi wa viongozi wa kiserikali watokanao na Chama kama Wabunge, Wawakilishi, Madiwani na Viongozi wa Serikali za Vitongoji, Vijiji na Mitaa. Idara huwa inaratibu na kuunganisha shughuli za makundi, na pia kufuatilia utendaji wa viongozi waliomo serikalini wa ngazi mbali mbali watokanao na Chama.

Taarifa kwa kila kundi ni kama ifuatavyo:

6.2.5.1 Jumuiya ya Wanawake wa CUF:

Hadi Machi 2006 kulikuwa na mfumo wa Mabaraza ya Wanawake ambayo yalifanikisha kufanya Mkutano Mkuu wao Februari 2005. Mkutano Mkuu huo uliwapatia wanawake uongozi wa kitaifa. Mabaraza wakati huo yalikuwa yakifanya kazi chini ya Kurugenzi ya Wanawake.

Baada ya kupitishwa kwa Mpango Mkakati wa Chama (SP) uliopelekea kufanyika marekebisho makubwa ya miundo ya kurugenzi, Kurugenzi ya Wanawake ilivunjwa na badala yake kuidhinishwa kuundwa kwa Jumuiya ya Wanawake. Uongozi wa kitaifa wa Baraza la Wanawake walitwishwa mzigo wa kuyabadilisha mabaraza kwa kuunda Jumuiya ya Wanawake. Viongozi wakuu wa Baraza la Taifa la Wanawake walikuwa Mheshimiwa Aziza Nabahan kutoka Zanzibar (Mwenyekiti) na Mheshimiwa Ashura Amanzi kutoka Tanzania Bara (Kaimu Katibu). Viongozi hao wakawa Viongozi Wakuu wa Jumuiya ya Wanawake na wanaendelea na nyadhifa hizo hadi sasa.

Shughuli zilizofanywa na Jumuiya hiyo tangu kuanzishwa kwake ni pamoja na zifuatazo:

(i) Kufanya ziara katika wilaya takriban 30 za SP za Tanzania Bara na wilaya zote za Zanzibar kwa ajili ya kuelezea wanawake uundwaji wa jumuiya yao na kuwahamasisha wajiunge nayo.
(ii) Kutembelea baadhi ya taasisi zenye watu wanaohitaji kusaidiwa na kutoa misaada ya kibinadamu kwa wananchi walioko katika taasisi hizo. Mfano ni Hospitali ya Ocean Road ambako wagonjwa wa saratani ya matiti walifarijiwa.
(iii) Kushiriki katika kuhamasisha wanawake wajitokeze kwa wingi wakati wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura; na pia kuwahamasisha wanawake wanachama kujitokeza kugombea nafasi za uongozi katika uchaguzi wa ndani ya Chama wa ngazi zote.
(iv) Kuandaa rasimu ya Kanuni zitakazoiongoza Jumuiya. Rasimu tayari imeshaidhinishwa na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa.
(v) Kaimu Katibu wa Jumuiya alipata ziara ya mafunzo huko Finland. Mafunzo yalikuwa juu ya ushiriki wa wanawake katika siasa.
(vi) Kuratibu mafunzo kwa wanawake 24 wa CUF yaliyohusu mikakati ya uchaguzi na mawasiliamno katika jamii. Mafunzo hayo yalifadhiliwa na Chama cha Liberal Democrats cha Uingereza.
(vii) Ilifanyika semina kuhusu UKIMWI kwa Wajumbe wa Baraza la Wanawake Taifa la CUF Bagamoyo chini ya ufadhili wa AMREF 2007.

Pamoja na shughuli hiyo, Viongozi Wakuu wa Chama hawajaridhika na jinsi Jumuiya hii inavyofanya shughuli zake. Bado kazi ya kuwashawishi wanawake wajiunge na Chama haijafanyika ipasavyo. Jumuiya imekuwa hekaheka na hamasa za siasa. Kutokana na hali hiyo, Viongozi Wakuu wa Chama walikutana na Mwenyekiti na Kaimu Katibu wa Jumuiya kuwaeleza kutoridhishwa kwao na jumuiya inavyoendeshwa na kuwapa miongozo ya jinsi ya kuimarisha Jumuiya.

Kipindi kijacho Chama kitaweka msisitizo katika Jumuiya hii na kuisaidia ili iwafikie wanawake huko vijijini na mijini. Haina budi kuwa jumuiya ya umma wa wanawake badala ya kuwa jumuiya ya wanawake wachache wateule.

6.2.5.2 Jumuiya ya Vijana wa CUF:

Kabla ya kuundwa kwa Jumuiya kulikuwa na Mabaraza ya Vijana ambayo yalikuwa chini ya Kurugenzi ya Vijana. Kufuatia kupitishwa Mpango Mkakati wa Chama ambao ulipelekea mabadiliko ya miundo ya Kurugenzi, Kurugenzi ya Vijana, kama Kurugenzi ya Wanawake, ilivunjwa. Badala yake kukaidhinishwa na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa kuundwa kwa Jumuiya ya Vijana. Mabaraza ya vijana yakatakiwa yajibadili kuwa sehemu ya Jumuiya ya Vijana.

Iliamuliwa kuwa uundwaji wa Jumuiya uende kwa awamu kutokana na ufinyu wa bajeti ya Chama. Baada ya Jumuiya ya Wanawake kuwa imepiga hatua, Baraza Kuu liliidhinisha mchakato wa kuunda Jumuiya ya Vijana uanze kwa kuteuliwa Sekretarieti ya Kitaifa ya Vijana ambayo ndio yenye dhamana ya kuunda Jumuiya hiyo. Sekretarieti hiyo ya kitaifa ya Vijana inaongozwa na Mheshimiwa Mohamed Babu kutoka Tanzania Bara (Mwenyekiti) na Mheshimiwa Khalifa Abdalla Khalifa kutoka Zanzibar kuwa Katibu. Jumiya imekabidhiwa jumla ya shilingi milioni kumi (10,000,000/=) kama mtaji wa kuanzia. Jumuiya, kupitia Sekretarieti yake imetakiwa ijitegemee kifedha kwa kutafuta vyanzo vyake vya kupata fedha.

Tangu ianze kazi, Sekretarieti ya Vijana imefanya shughuli zifuatazo:

(i) Kujitambulisha kwa viongozi wa wilaya zote za Unguja, na Wilaya za Mkoa wa Dar es Salaam na Tanga kwa upande wa Tanzania Bara.
(ii) Kuandaa Kongomano kwa wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu Dar es Salaam, na mada ikiwa “Uchangiaji wa Gharama za Elimu kwa Wanafunzi Maskini” iliyowasilishwa na Mheshimiwa Juma Duni Haji, Naibu Katibu mkuu (Zanzibar) na Mkurugenzi wa Fedha na Uchumi wa CUF.
(iii) Kuandaa Kongomano kwa wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu huko Zanzibar, mada ikiwa “Mustakbali wa Muungano na Hatima ya Zanzibar” iliyowasilishwa na Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad.
(iv) Kuendelea na kutembelea wilaya kadhaa kwa madhumuni ya kujitambulisha na kutoa maelekezo juu ya hatua za uundwaji wa Jumuiya.

Sekretarieti ya Taifa ya Vijana imeazimia ifikapo mwisho wa mwaka huu wa 2009 Jumuiya iwe imeshasimama.

6.2.5.3 Jumuiya ya Wazee wa CUF:

Kundi la wazee katika chama chetu lilikuwa bado halijakusanywa na kuandaliwa kwa kukijenga, kukiimarisha na kukieneza Chama. Hata hivyo ni ukweli ulio wazi kuwa miongoni mwa waasisi wa chama chetu ni wazee. Wazee katika sehemu mbali mbali za nchi yetu wamejitokeza kukiunga mkono Chama na wamekuwa wakidai kuwa na kitengo au idara yao.

Kwa muda mrefu madai hayo ya wazee yalikuwa bado hayajachukuliwa hatua, licha ya Kurugenzi ya Siasa kutoa maagizo kuwa mabaraza ya wazee yaundwe katika kila ngazi. Katika baadhi ya wilaya, agizo hilo limetekelezwa, na wazee kujiwekea uongozi wao. Katika jiji la Dar es Salaam kikundi cha wazee walijipanga na wakawa wanafanya shughuli kadhaa, zikiwemo kukutana na mabalozi wa nchi za nje kupeleka madai/maombi kadhaa kwa niaba ya wazee wa CUF wa nchi nzima.

Kufuatia kupitishwa kwa Mpango Mkakati wa Chama (SP) iliamiliwa kuwa pamoja na kuundwa kwa Jumuiya za Wanawake na Vijana, pia iundwe Jumuiya ya Wazee. Kutokana na ufinyu wa bajeti ya Chama shughuli hiyo iliahirishwa hadi hivi mwishoni mwa mwaka jana.

Baraza Kuu la Uongozi la Taifa lilipitisha uamuzi kuwa sasa wakati umefika wa kuanzishwa Jumuiya ya Wazee kwa kuanzia kuwa na Sekretarieti ya Kitaifa ya Wazee. Baraza Kuu likaelekeza juu ya mambo ya kuzingatiwa katika uundaji wa Sekretarieti hiyo. Baada ya kupokea maelekezo ya Baraza Kuu, Kurugenzi ya Siasa ikapendekeza majina ya wazee wanaofaa kuingizwa katika Sekretarieti hiyo. Kamati ya Utendaji ya Taifa ya Chama ikafanya uteuzi wa wazee 20 (12 kutoka Tanzania Bara, na 8 kutoka Zanzibar) kuunda Sekretarieti hiyo katika mwezi wa Disemba 2008. Pia Kamati ya Utendaji ya Taifa iliidhinisha kutengwa kwa shilingi milioni kumi (10,000,000/-) kwa ajili ya kuiwezesha Sekretarieti ya Kitaifa ya Wazee kuanza mchakato wa kuunda Jumuiya ya Wazee. Hatua ya mwanzo inayotazamiwa kuchukuliwa na Sekretarieti ya Wazee ni kuandaa Mpango Kazi utakaotumika kuunda Jumuiya hiyo.

Inatazamiwa kuwa ifikapo mwezi Disemba 2009, Jumuiya ya Wazee itakuwa imeshasimama.

6.2.5.4 Wabunge, Wawakilishi, Madiwani na Viongozi wa Serikali za Vitongoji, Vijiji na Mitaa

Kama ilivyoelezwa huko kabla, Kurugenzi ya Siasa ndio yenye jukumu la kufuatilia utendaji wa viongozi wa kiserikali watokanao na Chama. Idara inayohusika na kusimamia jukumu hili ni Idara ya Makundi.

Idara imekuwa ikipokea taarifa za utendaji wa kazi wa Kambi ya Upinzani katika Bunge na ile ya Baraza la wawakilishi kutoka kwa Viongozi wa Upinzani katika Bunge na katika Baraza la Wawakilishi. Pia Idara hupokea taarifa za kazi za Wabunge na Wawakilishi wanazozifanya katika majimbo yao walikochaguliwa, na pia katika Wilaya za SP ambazo kila Mbunge na Mwakilishi amepangiwa kuilea. Taarifa hizo hufanyiwa uchambuzi na kisha kuwasilishwa katika vikao vya Kamati ya Utendaji ya Taifa na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa.

Kwa njia hii Chama kinaweza kufuatilia shughuli za Wabunge na Wawakilishi. Ukiacha wachache miongoni mwao, Wabunge na Wawakilishi wanafanya kazi nzuri hasa katika Wilaya walizopangiwa kuzilea. Hata hivyo kumekuwa na malalamiko kadhaa dhidi ya Wabunge na Wawakilishi katika majimbo walikochaguliwa. Viongozi Wakuu wa Chama wamejitahidi sana kuyashughulikia malalamiko hayo kupitia mikutano yao na Wabunge na Wawakilishi, na pia katika ziara ambazo Viongozi Wakuu hao huzifanya katika majimbo ya Wabunge na Wawakilishi hao.

Kuhusu Madiwani watokanao na Chama, Kurugenzi ya Siasa imeweza kusimamia kuundwa kwa Umoja wa Madiwani wa CUF nchini. Umoja huo unawaunganisha madiwani wa CUF ili wapate fursa ya kubadilishana uzoefu na kupeana maarifa ya kuwasaidia katika kutimiza wajibu wao.

Idara pia imeanzisha utaratibu wa kudai na kupokea taarifa za utekelezaji wa majukumu kwa upande wa madiwani wa CUF na kuzifanyia uchambuzi taarifa hizo na kisha kuziwasilisha katika vikao vya Kamati ya Utendaji ya Taifa na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa, vikao ambavyo hutoa miongozo na maelekezo kadhaa kwa madiwani hao.

Kwa utaratibu huu, Chama kinaweza kufuatilia utendaji wa viongozi hawa muhimu, pale panapohitajika, msaada hutolewa kwa madiwani ili kuwafanya wapate ufanisi bora wa kazi.

Viongozi wa Serikali za Vitongoji, Vijiji na Mitaa ni muhimu kwani hawa wako karibu sana na wananchi. Pale viongozi hao wanapofanya vizuri, hukijengea Chama sifa, na hivyo kuwa chachu kwa wananchi kuona kuwa CUF ipo kwa ajili ya wananchi. Pale wanapofanya vibaya, basi hukitia dosari Chama na hivyo kuathiri taswira yake katika jamii.

Yapo malalamiko kuwa baadhi ya viongozi hawa wamejiweka mbali na Chama katika maeneo yao, na pia wachache miongoni mwao wameiga utamaduni wa CCM wa kujali zaidi maslahi yao binafsi. Taarifa hizo zikipatikana hushughulikiwa kwa kuwarekebisha viongozi husika.

Mpaka sasa Makao Makuu haijawa na utaratibu wa kuaminika wa kuwa karibu na viongozi hawa. Katika kipindi kijacho jitihada za makusudi zitachukuliwa kubuni utaratibu utakaoiwezesha Idara kufuatilia kwa karibu utendaji kazi wa viongozi hawa muhimu, na pale itapohitajika hatua za haraka za kuwarekebisha ziweze kuchukuliwa mapema iwezekanavyo.

Mwisho:

Kurugenzi ya Siasa, ikilinganishwa na Kurugenzi nyengine, ni changa. Katika uchanga wake huo Kurugenzi imeweza kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi wa kuridhisha. Bila shaka yapo mapungufu. Jitihada za kuyaondoa mapungufu hayo zitaendelea kuchukuliwa. Kurugenzi hii ikifanikiwa kutekeleza majukumu yake, itakiwezesha Chama kuwa imara zaidi na kuwa na taswira nzuri machoni mwa umma, na hivyo kujiongezea umaarufu nchini na nje ya nchi. Hilo ndilo lengo letu. Tutajitahidi tulifikie.

6.3. KURUGENZI YA HAKI ZA BINADAMU NA MAHUSIANO YA UMMA

Taarifa ya Kurugenzi hii imegawika katika sehemu tano zifuatazo:

1. Utangulizi
2. Idara ya Haki za Binadamu
3. Idara ya Harakati na Matukio (Action and Events)
4. Idara ya Habari Uchambuzi (Media Analysis)
5. Idara ya Habari – Mahusiano na Vyombo vya Habari (Media Work)

6.3.1 Utangulizi:

Kurugenzi hii imekuwepo tangu kuanzishwa kwa chama chetu mwaka 1992, katika muundo na mfumo tofauti na uliopo sasa. Msingi mmoja mkubwa wa Chama chetu cha CUF ni kutetea kulindwa na kuheshimiwa kwa Haki za Binadamu. Hivyo Chama kimekuwa kikiweka kipaumbele kwenye suala hili mara zote ndani ya uhai wake wa kisiasa. Hali kadhalika suala la kukitangaza Chama nalo limekuwepo tangu awali na liliundiwa Kurugenzi yake.

Baada ya kupitishwa kwa Mpango Mkakati wa Chama, 2006 na kufanya mabadiliko katika muundo wa Kurugenzi, Baraza Kuu la Uongozi la Taifa liliunda Kurugenzi hii kwa kuiunganisha na iliyokuwa Kurugenzi ya Habari na Uenezi wa Sera na Idara ya Haki za Binadamu iliyokuwa katika Kurugenzi ya Haki za Binadamu na Mambo ya Nje, na kuwa KURUGENZI YA HAKI ZA BINAADAMU NA MAHUSIANO YAUMMA.

Malengo na majukumu ya Kurugenzi hii ni haya yafuatayo:

a) Kuhakikisha kuwa katika jamii haki za binaadamu zinalindwa na kuheshimiwa na kupinga kila aina ya ukiukwaji wa haki za binadamu.
b) Kuhamasisha wanachama na umma kwa jumla na kutoa elimu ya uraia kwa lengo la kuwafanya wananchi kujua haki zao kupitia njia za semina, makongomano, warsha, mikutano ya hadhara, vipindi vya redio na televisheni, magazeti, vipeperushi, kanda za video/audio, sanaa na kadhalika.
c) Kufuatilia matukio yote yanayohusu uvunjwaji na ukiukwaji wa haki za binadamu na kushughulikia mambo yote ya kimahakama yanayowagusa wanachama wetu na Chama.
d) Kusimamia na kuhakikisha kuwa kesi za kisiasa wanazobambikiziwa viongozi na wanachama wa CUF zinafuatiliwa hadi kumalizika kwake kwa kutoa ushauri wa kisheria na pale uwezo unaporuhusu hata kutoa msaada wa utetezi Mahakamani.
e) Kuwahudumia waathirika wa matukio ya ukiukwaji na uvunjwaji wa haki za binadamu kwa kadiri ya uwezo wa Chama, kulingana na taratibu zilizowekwa na Chama.
f) Kufuatilia matukio ya kimaafa yanayotokea nchini kwa kufuata misingi na taratibu zilizowekwa na Chama.
g) Kukitangaza Chama kwa kutoa taarifa mbali mbali za utendaji na ukosoaji wa sera na utendaji usioridhisha wa serikali zilizoko madarakani.
h) Kujenga mahusiano mazuri na vyombo vya habari na waandishi wa habari kwa madhumuni ya kupata fursa ya kuhakikisha habari sahihi za Chama zinaripotiwa.
i) Kuanzisha vyombo vya habari vya Chama ikiwa ni pamoja na gazeti, kituo cha redio na kituo cha televisheni, na kuvisimamia ipasavyo.
j) Kufuatilia masuala ya habari na vyombo vya habari na kufanya uchambuzi wa habari zinazotoka kila siku ili kukiwezesha Chama kuchukua hatua za haraka kutegemeana na aina ya habari na athari zake kwa Chama.
k) Kuwaandalia viongozi wakuu wa Chama mikutano na waandishi wa habari (Press Conferences), kutoa taarifa kwa vyombo vya habari (Press Releases), na kuandaa mikutano ya hadhara, maandamano na maadhimisho ya kumbukumbu mbali mbali za chama.

Mkurugenzi aliyekuwa akiiongoza Kurugenzi ya Habari na Uenezi wa Sera kuanzia 2004-2006 ni Richard Hiza Tambwe. Baada ya kutoteuliwa tena kuwa Mkurugenzi, Richard Hiza Tambwe alikihama Chama na kuhamia CCM. Baada ya kubadilika kwa muundo wa Kurugenzi za Chama Taifa mwaka 2006, Mwenyekiti wa Taifa Mheshimiwa Profesa Ibrahim H. Lipumba, kwa mamlaka aliyopewa na Katiba ya Chama alimteua Mheshimiwa Mbarala Maharagande kutoka Tanzania Bara kuwa Mjumbe wa Baraza Kuu la Uongozi Taifa na kumfanya kuwa Kaimu Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Haki za Binaadamu na Mahusiano ya Umma na Mheshimiwa Salim Bimani kutoka Zanzibar kuwa Naibu Mkurugenzi wake.

6.3.2 Idara ya Haki za Binadamu:

Katika kipindi cha mwaka 2004 – 2009, Kurugenzi imepokea na kufuatilia taarifa mbali mbali za ukiukwaji na uvunjwaji wa haki za binadamu kutoka maeneo mengi nchini na kuzifanyia uchambuzi wa kina taarifa hizo pamoja na zile zilizoripotiwa katika vyombo vya habari. Uchambuzi umebainisha kuwa hali bado haijawa ya kuridhisha, hasa katika suala la utoaji haki katika Mahakama, Mabaraza ya Vijiji na ya Kata. Kumekuwepo kwa uporaji mkubwa wa ardhi, unyanyasaji wa raia wa hali ya juu kutokana na wananchi kushindwa kulipa michango mbali mbali inayopangwa na serikali za mitaa na vijiji katika maeneo yao, malipo duni ya mazao yao, na migogoro ya wakulima na wafugaji inayoendelea kujitokeza kila uchao, na pia kubambikizwa kesi. Kumekuwapo pia na hali ya kusikitisha katika Mkoa wa Mara wa mapigano ya kikabila na kiukoo, wakulima na wafugaji na serikali kushindwa kuishughulikia ipasavyo katika baadhi ya mikoa ikiwemo mkoa wa Mara, Dodoma, Morogoro, na kwengineko.

Aidha, katika maeneo ambayo Chama kina nguvu, viongozi wa serikali wa ngazi mbali mbali wamekuwa wakishirikiana na CCM kutoa vitisho kwa viongozi na wanachama wa CUF, na hata kwa wananchi kwa jumla kwa lengo la kuwafanya waogope kukiunga mkono Chama chetu. Tabia ya kuwabambikizia kesi viongozi na wanachama mashuhuri wa CUF imeendelezwa katika maeneo mengi ya Tanzania.

Zaidi ya hayo, katika maeneo ambayo CUF imeshinda kuongoza serikali za vitongoji, vijiji au mitaa viongozi wa serikali hizo kutoka CUF hunyimwa ushirikiano kutoka kwa watendaji wa serikali wa ngazi husika. Viongozi wa serikali, hasa baadhi ya Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa hutumia madaraka yao vibaya kwa kuwanyanyasa viongozi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji kutoka CUF, na wakati mwengine kuzivunja serikali hizo bila kufuata utaratibu kama ulivyowekwa na sheria.

Hata hivyo, katika kipindi baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2005 matumizi ya nguvu ya ziada za polisi yamepungua sana ikilinganishwa na hali iliyokuwepo katika kipindi kilichopita wakati wa utawala wa IGP Omar Mahita na hasa wakati wa uchaguzi. Kesi zinazohusiana na kushitakiwa viongozi na wanachama zimepungua kwa kiasi kikubwa kipindi hiki. Ziko kesi ambazo bado zinaendelea katika Mahakama mbali mbali nchini, baadhi yao zinatetewa na kampuni ya uwakili ya Taslima Law Chambers.

Mpaka mwaka 2006 kwa upande wa Tanzania Bara tulikuwa na kesi zilizotajwa kuwepo Mahakamani 286. Baada ya kuzitambua, kuliwekwa mkakati madhubuti wa kukabiliana nazo na kujiwekea lengo la kuzipunguza asilimia 75 ya kesi hizo kwa namna tofauti hadi kufikia Juni 2008. Kwa sasa zipo kesi zinazojulikana Ofisi Kuu zipatazo 46 zinazoendelea katika Mahakama mbali mbali nchini jambo ambalo limeleta faraja na kufikia lengo la awali tulilolikusudia. Miongoni mwa kesi zilizokuwa zikisimamiwa na Chama ni kesi za kudai matokeo ya Ubunge na ya Udiwani yabatilishwe kutokana na kukiukwa kwa taratibu. Kwa bahati mbaya kesi zetu zote za ubunge tumeshindwa, lakini kwa bahati njema za udiwani tulizoshitakiwa na ambazo zimeshamalizika tumeshinda. Kesi nyingine ni za madai na jinai na nyingi kati ya hizo tumeshinda.

Ndani ya kipindi hiki cha mwaka 2006-2008 Kurugenzi imepitia upya mkataba kati ya Chama na Wakili wetu, ili kufikia makubaliano juu ya utaratibu mpya wa wakili kuzihudumia kesi za Chama. Pamoja na mapungufu yaliyojitokeza, kwa jumla pia wakili wetu amejitahidi kujituma na kujitolea kwa mapenzi ya chama chake kufanya kazi ya ziada kuwatetea viongozi na wanachama katika sehemu mbali mbali nchini. Hata hivyo kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa mwishoni mwa mwaka huu 2009 na kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, Kurugenzi inajipanga upya na kutafuta njia mbali mbali za kuweza kuleta ufanisi zaidi katika suala hili la msaada na huduma za kisheria kwa viongozi, wanachama na wagombea wetu watakaokabiliwa na matukio yatakayohitaji msaada wa kisheria ili kufikia malengo ya Chama.

Kurugenzi pia imekuwa ikifuatilia masuala yote yanayohusu ukiukwaji na uvunjwaji wa haki za binadamu na kushughulikia mambo yote ya kimahakama yanayohusu Chama na matukio ya kimaafa yaliyotokea kulingana na misingi na taratibu ambazo Chama imejiwekea.

Kwa kushirikiana na Makatibu wa Wilaya na Wakuu wa Vitengo vya Haki za Binadamu na Mawasiliano na Umma katika Wilaya, Kurugenzi imeweza kuratibu na kusimamia matukio ya uvunjwaji wa haki za binadamu katika wilaya mbali mbali nchini. Kurugenzi ilisimama kidete kuhakikisha kuwa kesi ambazo viongozi na wanachama wetu wamebambikiziwa zinamalizika kwa ushindi. Katika hili hatuna budi kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wetu wote kwa ujumla wao, akiwemo Mhe. Hamad Rashid Mohamed (Kiongozi wa Upinzani Bungeni) na Mhe. Masoud Salim wa Jimbo la Mtambile, Pemba, kwa jitihada zao kwa nafasi zao kuhakikisha kuwa masuala yote ya kesi yanayofikishwa kwao wanayasimamia na kesi hizo zinafutwa.

Jedwali la Orodha ya Uhakiki wa Kesi mpaka Disemba 2008
katika Mikoa/Wilaya

Na.
Mkoa
Wilaya Idadi ya kesi
Hatua iliyofikia.
1. Dar es salaam Kinondoni 2, Ilala 0, Temeke 3 5
2. Tanga Korogwe 1, Tanga (M) 1 2
3. Mwanza Sengerema 2, Geita 1 3
4. Kigoma Kigoma Vijijini 1 1
5. Tabora Urambo 2 2
6. Mbeya Mbeya (V) 1
7. Arusha – –
8. Kilimanjaro – –
9. Pwani Rufiji 1, Mkuranga 1 2
10. Morogoro Morogoro (V) 1, (M) 2 3
11. Iringa – –
12. Rukwa – –
13. Ruvuma Tunduru 2 2
14. Mtwara Tandahimba 1 1
15 Lindi Lindi (M) 1, (V) 2, Ruangwa 1 kilwa 2 6
16 Dodoma Kondoa 3 3
17 Shinyanga Maswa 2, shinyanga (M) (V) 2 4
18 Mara Serengeti 1, Musoma 2 3
19 Kagera Bukoba (M) (V) 3 3
20 Manyara – –
21 Singida – –
Jumla Ndogo 41
Mahakama Kuu 5 – Kesi ya Uchaguzi 2005 Morogoro(M) 1 Hatua ya kufaili Rufaa.

– Kesi ya kijiji cha Magole –kilosa Morogoro. 1 Imepangwa kusikilizwa Feb, 2009
– Kesi ya Uchaguzi Rufaa Bukoba(M) 1 Imepangwa kusikilizwa Jan, 2009 baada ya Jaji1 kujitoa.
– Kesi ya Madai/kisiasa Morogoro (M) 1 Hatua ya kufaili Rufaa.
– Kesi ya Chama dhidi ya Omari Mahita. 1 Baada ya ufuatiliaji wa muda mrefu Oktoba 2008, imejibiwa na msajili wa mahakama kuwa maamuzi yatatolewa hivi karibuni, baada ya Jaji aliyepangiwa awali kuteuliwa kuwa Jaji wa mahakama ya Rufaa. Hatua iliyokuwepo ni kwa Majaji kutoa uamuzi wa pingamizi la Mahita kutaka asishitakiwe kwa kuwa alitenda hivyo kwa nafasi yake ya IGP na hivyo Mahakama kutoa uamuzi kama ana mashtaka ya kujibu au la.
Jumla Kuu 46

TANBIHI:
– Maelekezo kwa wanachama wetu kufungua kesi za madai kwa usumbufu walioupata kutokana na ubambikizwaji wa kesi yametolewa kwa utekelezaji.
– Hata hivyo huenda zikawepo kesi zaidi ya hizi katika Mahakama mbali mbali nchini lakini Kurugenzi haijapata taarifa rasmi, na au hazina uzito mkubwa wa kuweza kusimamiwa na ngazi ya Taifa na badala yake kutoa ushauri wa kisheria au kuwatayarishia hati ya mashtaka na pia kushauri kimkakati katika kufikia mwisho.

Kurugenzi imeendeleza utaratibu wake wa kuwahudumia waathirika wa matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu kwa kadiri ya uwezo uliokuwepo na kuratibu ziara mbali mbali za Mwenyekiti Taifa kwa madhumuni ya kuwajulia hali wagonjwa, wafiwa, na kadhalika.

Kwa upande wa Zanzibar, Kurugenzi ilifuatilia jumla ya kesi 465 katika Mahakama mbali mbali za Unguja na Pemba, na ambazo zilikuwa zikiwakabili wanachama na wapenzi wa Chama takriban 1,450. Nyingi ya kesi hizo zilikuwa za kubambikiziwa na hasa katika kipindi cha uandikishaji wa Daftari la Wwapiga Kura, wakati wa kampeni, wakati wa uchaguzi mkuu wa 2005 na baada ya kutolewa matokeo ya uchaguzi.

Kwa juhudi kubwa iliyochukuliwa na Kurugenzi ikishirikiana kikamilifu na Mawakili wajasiri na wazalendo, Mhe. Ussi Khamis Haji, Mhe. Is-hak Ismail Sharif, Mhe. Nassor Khamis, Mhe. Hamad Kibanda na Mhe. Ali Omar Ali, waliwezesha kufanikisha kuzitetea kesi zote na hatimaye kesi hizo zimemalizika, na wanachama wetu wakawa huru.

Katika kipindi chote cha uandikishaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, kipindi cha kampeni na kipindi cha uchaguzi, Kurugenzi ilikuwa ikichapisha na kusambaza kijarida cha kila wiki kutoa muhtasari wa matukio ya uvunjwaji wa haki za binadamu, matamko ya Chama juu ya uvunjwaji huo, na miongozo ya kufuatwa na wanachama.

Yafuatayo ni matukio ya kinyama na ya kikatili yaliyofanywa na vijana wa CCM (Janjaweed) walioandaliwa makusudi wakishirikiana na vikosi vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na majeshi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwahujumu wanachama wetu:

(i) Kuuliwa kwa kupigwa risasi mwanafunzi wa umri wa miaka 16, Juma Omar katika Wilaya ya Mkoani, Pemba kulikofanywa na askari wa JKU na KMKM.
(ii) Kujeruhiwa vibaya wanachama 53 kwa kupigwa mapanga na kuteswa katika eneo la Kinuni, Wilaya ya Magharibi, Unguja kulikofanywa na Janjaweed.
(iii) Kuharibiwa mali kwa kuchomwa moto kulikofanywa na vikosi vya SMZ kwa kushirikiana na Janjaweed ikiwa ni pamoja na Kiwanda cha Mbao cha SANA na nyumba za watu, Wilaya ya Magharibi, Unguja.
(iv) Kuteswa, kuvunjiwa majumba, kunajisiwa kwa wanawake, kupigwa kwa wananchi na viongozi wa CUF, wakiwemo Wabunge na Wawakilishi, wa Shehia ya Piki, Wilaya ya Wete, Pemba kulikofanywa na vikosi vya SMZ.
(v) Kupigwa risasi wanachama wakati Polisi wakiwazuia wananchi wasiende katika mkutano wa kampeni wa CUF katika Jimbo la Donge, Wilaya ya Kaskazini B, Unguja.
(vi) Kuuawa kwa kugongwa kwa makusudi na gari ambalo walikuwa wamepanda wanachama wa CUF waliokuwa wakienda katika mkutano wa kampeni Chaani kulikofanywa na askari wa KMKM. Tukio hili lilitokea maeneo ya Mtoni, Wilaya ya Magharibi, Unguja.

Kurugenzi ilifuatilia matukio hayo kwa karibu na kutoa msaada wa kila aina kwa wahusika.

Kurugenzi ikishirikiana na Makatibu wa Wilaya imefanikisha kuratibu ziara za Katibu Mkuu kuwakagua wagonjwa na kuhani wafiwa wa Wilaya zote za Zanzibar zaidi ya mara 6, ziara ambazo zilileta mafanikio makubwa sana kwa Chama chetu ya kujenga taswira njema ya viongozi wakuu kuwa karibu na watu wao.

Aidha Kurugenzi iliwahamasisha wanachama kutoa msaada wa hali na mali kwa muasisi wa Chama na mjumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa, Mhe. Ali Haji Pandu ambaye alifikwa na janga la kuunguliwa na nyumba yake na vitu vyote vilivyokuwemo ndani. Pia Kurugenzi iliratibu na kuhamasisha shughuli ya kutoa msaada kwa Katibu wa CUF wa Jimbo la Jang’ombe baada kufikwa na janga la nyumba yake kuzama ardhini.

Kurugenzi iliendelea kuwafariji na kuwapa misaada mayatima na waathirika wengine wa ukatili uliofanywa na majeshi ya Serikali yaMuungano tarehe 26 – 27 Januari, 2001 wakati wa maandamano ya kudai haki. Pamoja na hayo Kurugenzi inaendelea kuwashughulikia kimatibabu wale walioathirika waliokuwa bado hali zao hazijawa nzuri.

Kurugenzi imeshirikiana kikamilifu na Viongozi wa Kambi za Upinzani Bungeni na Baraza la Wawakilishi pamoja na Wabunge na Wawakilishi wote kwa kuwasilisha na kuzisimamia kero mbali mbali za wananchi hasa wale walionyang’anywa maeneo ya ardhi ambayo SMZ ilitaka kuyahodhi kwa visingizio tofauti na kuzisemea na baadhi yake zimezipatiwa ufumbuzi.

6.3.3 Harakati na Matukio:

Kwa upande wa Tanzania Bara, katika kipindi cha 2004 – 2009 Kurugenzi imefanikiwa kuandaa, kusimamia na kufanya mikutano ya hadhara iliyohudhuriwa na viongozi wa kitaifa 170 nchini kote, maandamano makubwa 11, mapokezi makubwa mawili (2) ya Mwenyekiti wa Taifa aliporejea nchini kutoka nje, na maadhimisho ya tarehe 26 – 27 Januari karibu kila mwaka na maadhimisho mengine ya kichama.

Kurugenzi pia iliandaa na kufanya makongomano, warsha na semina mbali mbali kwa lengo la kuwaelimisha wananchi kujua haki zao, na kutoa elimu ya uraia kwa umma kupitia vyombo vya habari kufuatana na haja na wakati husika.

Mkurugenzi alishiriki katika uhamasishaji wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura mwaka 2008 katika mikoa na wilaya za Dar es Salaam, Mbeya, Lindi, Mtwara, Morogoro, Dodoma, na Tabora, ambapo makongomano na mikutano ya hadhara ya uhamasishaji ilifanyika.

Mkurugenzi alifanya ziara ya ukaguzi wa uhai wa chama na uhamasishaji mwaka 2006 katika wilaya za mikoa ya Tabora, Mwanza, Mara, Arusha, Tanga, na mwaka 2008 Lindi na Mtwara (ziara iliyoongozwa na Mwenyekiti Taifa) na kushiriki katika uchaguzi wa marudio katika wilaya ya Tunduru na Uchaguzi wa Udiwani kata ya Kasharu- Bukoba Vijijini.

Katika ziara hizo, Kurugenzi imefanikiwa pia kusambaza nyaraka mbali mbali muhimu ikiwa ni pamoja na nakala za Katiba ya Jamhuri ya Muungano, Muongozo wa namna ya kuandaa Mpango Mkakati wa Ushindi, na nakala ya kitabu cha hotuba ya Mwenyekiti Taifa aliyoitoa Diamond Jubilee- 2008 kuhusu ‘Ukosefu wa Uongozi na Hatima ya Tanzania’.

Kwa upande wa Zanzibar, Kurugenzi ilifanya kazi ya ziada kabla ya uchaguzi mkuu wa 2005 kuwahamasisha wananchi wakiunge mkono Chama kwa kuwachagua wagombea waliotokana na Chama. Pamoja na wizi wa kura, vitisho, na kila aina ya uchafuzi, CUF ilipata ushindi wa kujivunia kwa kushinda majimbo yote 18 ya Pemba na jimbo la Mji Mkongwe, Unguja. Pia Mgombea Urais wa CUF alipata kura zaidi ya asilimia 55%, ingawa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ilimpa kura asilimia 47% tu.

Katika kipindi cha kampeni za uchaguzi wa mwaka 2005, Kurugenzi ilishirikiana na Timu ya Kampeni ya Mgombea Urais, kuratibu na kusimamia mikutano ya kampeni 50, mmoja kwa kila jimbo la Zanzibar. Kuanzia 2006 hadi sasa Kurugenzi imeratibu, kusimamia na kufanya jumla ya mikutano 152, jumla ya maandamano makubwa 6 na maadhimisho 3.

Kurugenzi pia iliwahamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kutoa maoni yao juu ya uharakishwaji wa uundwaji wa Shirikisho la Afrika Mashariki. Wito wa Chama uliitikiwa na wananchi wengi walifika mbele ya Tume iliyoundwa ya kukusanya maoni na kutoa maoni yao kwa kujenga hoja nzito za kupinga uharakishwaji huo.

Naibu Mkurugenzi alifanya ziara za uhamasishaji na kampeni za uchaguzi mkuu katika Wilaya za Lushoto, Handeni, Kasulu, Biharamulo, Muleba Kaskazini, Bukoba Mjini na Vijijini, Rufiji, Kibiti, Bagamoyo, Temeke, Kinondoni, Nzega, Bukene, Kondoa, na Morogoro Mjini

6.3.4 Idara ya Habari:

Idara ya Habari ina majukumu mawili makubwa:-

(a) Mahusiano na Vyombo vya Habari (Media Work)
(b) Uchambuzi wa Habari (Media Analysis)

6.3.4.1 Mahusiano na Vyombo vya Habari (Media Work):

Katika eneo la Mahusiano na Vyombo vya Habari (Media Work), Kurugenzi kwa Tanzania Bara na Zanzibar, imefanya au kuwezesha kufanyika mambo yafuatayo tangu mwaka 2004 hadi 2008:

(i) Kuhuisha mahusiano mazuri na vyombo na waandishi wa habari kiasi kwamba sasa habari za Chama zimekuwa zikiripotiwa vyema kwa kiasi cha kuridhisha.
(ii) Kufanyika kwa mikutano ya mara kwa mara na waandishi wa habari kuzungumzia masuala mbali mbali ya kitaifa yanayohusiana na uchumi, siasa na jamii kila inapotokea haja ya kufanya hivyo.
(iii) Kuwashirikisha Wabunge na Wawakilishi wanaotokana na Chama katika kuhakikisha kuwa habari kuhusu kazi na maeneo yao yanaripotiwa vyema.
(iv) Kupata vipindi katika vituo vya redio na televisheni, na kupata nafasi katika magazeti mbali mbali na hivyo kuuwezesha umma kusikia habari za CUF.
(v) Kufanikisha kutolewa habari za njaa iliyowaathiri wananchi wa Wilaya ya Micheweni, Pemba, ambapo Idara ilishirikiana kwa karibu na waandishi wa habari hususan magazeti na televisheni kulikoikera SMZ na hivyo kuamuru baadhi ya waandishi kuwekwa ndani kwa kuripoti ukweli. Chama kilifarijika kuona kuwa waandishi waliowekwa ndani hawakutetereka katika kutimiza wajibu wao wa kuuarifu ukweli umma wa Watanzania.
(vi) Kuweka wa kuhifadhi kumbukumbu za habari mbali mbali.
(vii) Kusimamia mradi wa uanzishwaji wa redio ya Chama, ambapo taratibu zote za kisheria zimefuatwa na sasa panasubiriwa maamuzi ya Mamlaka ya Mawasiliano (TRCA) kwa kibali cha kuruhusu kuanzishwa na kuendeshwa kwa kituo hicho.
(viii) Kuwezesha jumla ya taarifa zinazohusu CUF au zilizotolewa na CUF kufikia jumla ya 233 kwa mwaka 2006 pekee. Jumla ya taarifa 125 ziandikwa katika kurasa za mbele za magazeti kadhaa ya Kiswahili na ya Kiingereza.
(ix) Kufanikisha jumla ya taarifa kwa vyombo vya habari (Press Releases) 385 Kwa Tanzania Bara na 166 Kwa Zanzibar kuripotiwa vizuri katika vyombo vingi vya habari vya ndani na nje ya nchi, na kuwezesha kufanyika kwa mikutano na waandishi wa habari (Press Conferences) 64 zilizofanywa na viongozi wakuu wa chama.

6.3.4.2 Uchambuzi wa Habari (Media Analysis):

Katika eneo la uchambuzi wa habari, Idara imekusanya, kuchambua na kutoa maoni juu ya taarifa kadhaa zilizoripotiwa na kupewa umuhimu mkubwa katika vyombo vya habari. Miongoni mwa taarifa zilizofanyiwa uchambuzi ni pamoja na:

(i) Mwaka 2004/05 ulikuwa mwaka wa uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu na masuala mengi ya habari yalihusiana na kampeni za uchaguzi mkuu.
(ii) Mwaka 2006 Kashfa ya uzalishaji wa umeme ya Richmond/Dowans.
(iii) Kesi ya mauaji dhidi ya Abdalla Zombe na ile ya Omar Mahita kuhusiana na kampeni chafu za kuihusisha CUF na ujambazi.
(iv) Kashfa ya wizi wa fedha katika Akaunti ya Madeni ya Nje ya Benki Kuu – EPA.
(v) Mgomo wa wafanyakazi wa Shirika la Reli – TRL.
(vi) Kujiuzulu kwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa na kuvunjwa kwa Baraza la Mawaziri.
(vii) Kukwama kwa Mazungumzo ya Muafaka baina ya CCM na CUF.
(viii) Kashfa nyengine ya umeme iliyohusu mkataba wa shilingi bilioni 155, ambapo mitambo haikuwahi kuzalisha hata unit moja ya umeme huko Mwanza.
(ix) Kauli za watu mashuhuri kama Mheshimiwa Joseph Sinde Warioba na Profesa Issa Shivji juu ya hatima ya Tanzania kisiasa na kiuchumi.
(x) Ubomoaji wa nyumba za wananchi Tabata Dampo.
(xi) Kashfa ya Mgodi wa Kiwira ambapo Rais Mstaafu Benjamin Mkapa na Waziri wake Daniel Yona walijiuzia mgodi huo kwa bei poa.
(xii) Uchaguzi wa Kenya na Muafaka wa PNU na ODM na kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Kenya.
(xiii) Mauaji ya Wageni huko Afrika Kusini.
(xiv) Kujiuzulu kwa Ditopile Mzuzuri baada ya kumuua kwa kumpiga risasi dereva wa daladala.
(xv) Kifo cha Ditopile Mzuzuri.
(xvi) Kifo cha aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu, Daudi Balali.
(xvii) Mkutano wa Sullivan, Arusha.
(xviii) Bajeti ya Serikali ya mwaka 2006/07, 2007/08 na 2008/9.
(xix) Kifo cha Chacha Zakayo Wangwe.
(xx) Mjala wa hadhi ya Zanzibar katika Muungano.
(xxi) Vurugu katika chaguzi za Jumuiya za CCM, hususan Umoja wa Vijana na Umoja wa Wanawake.
(xxii) Uchaguzi mdogo wa Tarime.
(xxiii) Mgomo wa walimu.
(xxiv) Mgogoro na migomo ya wanafunzi wa wa vyuo vya elimu ya juu.
(xxv) Kuyumba kwa ushirikiano wa vyama vinne vya siasa.
(xxvi) Mauaji ya Maalbino.
(xxvii) Kongomano la CUF juu ya Ukosefu wa Uongozi na Hatima ya Tanzania.
(xxviii) Hali ya Kisiasa Zimbabwe, na
(xxix) Uchaguzi wa Marekani ambapo hatimaye Barack Obama aliibuka na ushindi mkubwa.

Taarifa hizo na nyengine zilifanyiwa uchambuzi wa kina ili kujua taathira zake kwa nchi yetu, chama na wananchi kwa ujumla. Matokeo ya uchambuzi hutumiwa katika kukisaidia Chama kujenga mikakati sahihi na ya kuisaidia nchi na wananchi wake, na kukiendeleza mbele Chama zaidi chama chetu.

Uzalishaji wa Gazeti la Fahamu:

Kurugenzi ilikuwa inalisimamia gazeti la Fahamu ambalo lilikuwa linatoka kila wiki mara moja. Gazeti lilikuwa likienda vizuri mbali na mapungufu yaliyokuwa yanajitokeza hapa na pale kutokana na kutokuwapo rekodi nzuri za malipo ya fedha za matangazo kutoka Hazina kupitia matangazo ya wastaafu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki – EAC. Uhai wa chombo cha habari ikiwa ni gazeti au kingine ni uwezekano wa kupata matangazo yanayolipiwa vizuri. Kati ya Julai 2007 – Mei 2008, gazeti lilikuwa likiendeshwa kwa hasara kubwa kwa kutopata matangazo ya kuliwezesha kujiendesha. Ili kuepusha kukiingiza chama katika hasara ikaonekana ni vyema kutafuta njia mbadala ya kuliendesha gazeti hilo ambapo sasa kwa kushirikiana na wabunge na wadau wengine tunatafuta njia bora ya kuingia makubaliano ya namna gani ya kuboresha usimamizi kwa madhumuni ya kuliwezesha kurejea tena mtaani.

Mwisho:

Kwa ujumla Kurugenzi ya Haki za Binadamu na Mahusiano ya Umma imefanya kazi nzuri, hasa katika kipindi kufuatia kupitishwa kwa Mpango Mkakati wa Chama (SP). Pamoja na matatizo yaliyotokea baada ya watu waliopandikizwa Ofisi Kuu na kutokea vurugu na baadhi ya waandishi wa habari, kuvunjwa kamera ya video, umakini wa Mkurugenzi na Naibu Mkurugenzi wa Kurugenzi hii, ulikiwezesha Chama kurudisha imani ya waandishi wa habari kwake na kuendeleza mahusiano mema baina ya CUF na waandishi wa habari na vyombo vya habari wanavyovitumikia. Ndio maana sasa CUF inasikika vizuri na kutajwa katika vyombo vya habari kila mara mbali na mfumo wa kifisadi ulioingia katika sekta hii muhimu katika uwanja wa siasa za ushindani.

Ni matarajio ya Kurugenzi yetu kuweza kujipanga vizuri zaidi na kuendeleza mahusiano hayo yaliyokwishawekewa msingi mzuri kuelekea chaguzi za serikali za mitaa mwaka huu 2009 na uchaguzi mkuu mwaka 2010, ili chama chetu kiweze kufanya vizuri na kushinda chaguzi hizo na kuunda Serikali ya CUF.

6.4 KURUGENZI YA BLUE GUARDS

Taarifa ya Kurugenzi hii ina sehemu zifuatazo:

(a) Utangulizi
(b) Kamati ya Ulinzi na Usalama (KUU)
(c) Utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Chama (SP)
(d) Uimarishaji wa Chama, na
(e) Kazi za Kawaida na za Kiofisi

6.4.1 Utangulizi:

Kurugenzi ya Blue Guards iliundwa 2006 kufuatia marekebisho ya miundo ya Kurugenzi baada ya kupitishwa kwa Mpango Mkakati wa Chama (SP). Kazi zote za Kurugenzi hii huko kabla zikifanywa kupitia Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Chama (KUU). Kurugenzi hii imeundwa ili kuendeleza na kuimarisha dhana ya Chama ya kuwa na ulizi wa kuaminika ili kuhakikisha mambo yafuatayo:-

(a) Kuhakikisha usalama wa Chama nchini kote
(b) Kukikinga Chama dhidi ya njama za ndani na nje ya Chama za kukisambaratisha
(c) Kuhakikisha kuwa viongozi wakuu, majengo na shughuli za Chama zinalindwa na wakati wote kuwa katika hali ya usalama.

Katika mada ya Ulinzi na Usalama wa Chama aliyoitoa kwa washiriki wa Mafunzo ya Viongozi na Watendaji Wakuu wa Chama, Novemba 2006, Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad, aliyataja malengo ya ulinzi katika Chama kuwa ni:

(i) Kuhakikisha kuwa Chama kinafanya shughuli zake na kufikia malengo yake pasi na kizuizi kutoka ndani au nje ya Chama.
(ii) Kuhakikisha kuwa maslahi muhimu ya Chama yanapatikana ili kiweze kunawiri kwa kukubalika na umma, kiwe na uhuru wa kubuni na kusimamia sera zake kwa ufanisi, kiweze kuwaunganisha wanachama wake, kiweze kujenga mshikamano miongoni mwa viongozi, na baina ya viongozi na wafuasi wake, na baina ya wanachama wenyewe.
(iii) Kuhakikisha kwamba Chama kinakamata hatamu za dola na kinaongoza katika eneo kubwa la nchi kuliko chama chengine chochote nchini Tanzania.

Ni dhahiri kuwa Kurugenzi ya Blue Guards pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama zimekabidhiwa, kimsingi, jukumu la uhai mzima wa Chama, uimarikaji wake na pia dhamana ya kukipeleka kwenye madaraka ya nchi.

Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Blue Guards ndiye pia Katibu wa Kamati ya Ulinzi na Usalama. Naibu Mkurugenzi wa Kurugenzi hiyo ndiye pia Naibu Katibu wa Kamati ya Ulinzi na Usalama.

Katika uteuzi wa Wakurugenzi na Manaibu Wakurugenzi uliofanywa na Mwenyekiti wa Taifa wa CUF, Mheshimiwa Profesa Ibrahim Haruna Lipumba mwaka 2006, Mheshimiwa Said Miraaj Abdullah kutoka Zanzibar aliteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Kurugenzi hii na pia kuwa Katibu wa Kamati ya Ulinzi na Usalama. Mheshimiwa Mazee Rajabu Mazee kutoka Tanzania Bara, aliteuliwa kuwa Naibu Mkurugenzi wa Kurugenzi hii na Naibu Katibu wa Kamati ya Ulinzi na Usalama.

Kuanzia mwaka 2004 hadi 2006, kabla ya kupitishwa kwa Mpango Mkakati wa Chama (SP), Mheshimiwa Juma Othman Juma, kutoka Zanzibar, alikuwa ndiye Katibu wa Ulinzi na Usalama, na hakukuwa na Naibu.

Katika mwezi wa Oktoba, 2008 Mheshimiwa Said Miraaj Abdullah alijiuzulu nyadhifa zake zote za uongozi zikiwemo Mjumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Taifa, Katibu wa Kamati ya Ulinzi na Usalama na Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Blue Guards. Baada ya kukubali ombi la kujiuzulu kwa Mheshimiwa Said Miraaj Abdullah, Mwenyekiti wa Taifa alimteua Mheshimiwa Mazee Rajabu Mazee, kutoka Tanzania Bara, kuwa Katibu wa Kamati ya Ulinzi na Usalama na pia kuwa Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Blue Guards. Mwenyekiti huyo pia alimteua Mheshimiwa Salim Bimani, kutoka Zanzibar, kuwa Kaimu Naibu Katibu wa Kamati ya Ulinzi na Usalama, na pia kuwa Kaimu Naibu Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Blue Guards, pamoja na kuendelea na wadhifa wake wa Naibu Mkurugenzi wa Haki za Binadamu na Mahusiano na Umma. Baraza Kuu la Uongozi la Taifa lilithibitisha uteuzi huo.

6.4.2 Kamati ya Ulinzi na Usalama:

Kwa mujibu wa Ibara ya 76 ya Katiba ya Chama, Kamati ya Ulinzi na Usalama inaongozwa na Mwenyekiti wa Taifa wa Chama. Miongoni mwa Wajumbe wake ni pamoja na Makamo Mwenyekiti na Katibu Mkuu. Pia wamo viongozi wakubwa wenye nyadhifa za kiserikali, hususan Viongozi wa Upinzani katika Bunge na Baraza la Wawakilishi.

Hivyo, uzito wa Kamati ya Ulinzi na Usalama uko wazi. Ni Kamati hii yenye jukumu la kuhakikisha kuwa Chama sio tu kuwa kiko salama, bali pia kinaimarika na kuota mizizi, na kuweza kukabiliana na changamoto zote zinazojitokeza na kuchukua hatua za kawaida na za dharura kukihami Chama.

Kamati ya Ulinzi na Usalama katika kipindi cha kuanzia mwaka 2004 – 2006 kabla ya kufanyika kwa mabadiliko ya miundo ya Kurugenzi ilifanya jumla ya vikao 6 vya kawaida na vikao 5 vya dharura. Na kuanzia 2006 – 2008 KUU imefanya jumla ya vikao 7 vya kawaida na vikao 7 vya dharura.

Katika vikao vyake, KUU hujadili hali ya kisiasa nchini na jinsi hali hiyo inavyoiathiri nchi kiusalama, kiuchumi, kijamii na kimaendeleo. KUU hujadili kwa kina sababu za hali hiyo na pale inapohitajika hutoa tahadhari kwa Serikali. Lakini pia KUU hujadili hali ya maendeleo ndani ya Chama, hatari zinazokikabili, fursa, udhaifu na kulishauri Baraza Kuu la Uongozi la Taifa kuchukua hatua zipasazo.

Katika mambo ambayo yalikuwa yanapewa umuhimu mkubwa katika vikao vya KUU ni Mazungumzo baina ya CCM na CUF ya kuupatia ufumbuzi wa kudumu Mgogoro wa Kisiasa Zanzibar na kuishauri Timu ya Mazungumzo ya CUF hatua za kuchukuliwa, na pia kulishauri Baraza Kuu miongozo za kuipa Timu ya CUF katika mazungumzo hayo.

Kamati ya Ulinzi na Usalama pia iliishughulikia migogoro ya ndani ya Chama pale ilipoanza kuchipuka na hivyo kuiwahi kabla ya kuleta athari kubwa katika umoja na mshikamano wa Chama.

Kwa kweli Chama chetu kiko salama na hali ni shwari. Kwa kiasi kikubwa hali hiyo imechangiwa na umakini wa Kamati ya Ulinzi na Usalama, chini ya Uenyekiti mahiri wa Mwenyekiti wa Taifa, Mheshimiwa Profesa Ibrahim Lipumba, na utendaji uliotukuka wa watendaji wakuu wa KUU, Katibu na Naibu Katibu wa KUU.

6.4.3 Utekelezaji wa SP:

Baina ya Juni na Oktoba 2007, Kurugenzi ilifanya mambo yafuatayo ikiwa ni utekelezaji wa SP kwa upande wa Kurugenzi ya Blue Guards:

(i) Kuendeleza mafunzo ya ulinzi kwa vijana wa Blue Guards, mafunzo ambayo yalijumuisha maadili, siasa, utawala, historia, sheria za nchi, zikiwemo sheria za polisi na vyama vingi vya siasa, na itikadi ya Chama.
(ii) Kuwapatia baadhi ya vijana wa Blue Guards mafunzo ya udereva, IT, uandishi wa habari kwa viwango vya cheti na wengine kufikia diploma.
(iii) Kuwapatia baadhi ya vijana wa Blue Guards mafunzo ya kujihami kwa kutumia mikono (karate).
(iv) Kutoa mafunzo juu ya wajibu wa Blue Guards na Kamati za Ulinzi na Usalama za wilaya na ngazi za chini kwa wilaya 28 Tanzania Bara na Zanzibar.
(v) Kufanya uhakiki wa vijana wa Blue Guards katika ngazi za matawi, majimbo/kata kwa Tanzania Bara na Zanzibar kwa lengo la kujua idadi yao na kuweka rekodi zao.
(vi) Kukabidhi vitambulisho kwa baadhi ya vijana wa Blue Guards.

Kwa kipindi cha Novemba 2007 – Novemba 2008, utekelezaji wa SP uliofanywa na Kurugenzi hii ni kama ifuatavyo:-

(i) Kukamilisha muundo wa Blue Guards katika wilaya 68 kwa Tanzania Bara na Zanzibar.
(ii) Kuwapatia mafunzo ya upishi vijana wanane (8).
(iii) Kuendeleza mafunzo ya maadili, siasa, utawala, historia sheria na itikadi ya Chama katika wilaya 13 nyengine za Bara.
(iv) Kukabidhi vitambulisho kwa vijana wengine wa Blue Guards.
(v) Kuendelea kufanya uhakiki wa vijana wa Blue Guards katika baadhi ya wilaya.
(vi) Kutoa mafunzo ya uandishi wa taarifa mbali mbali kwa vijana wa Blue Guards katika baadhi ya wilaya, Zanzibar na Tanzania Bara.
(vii) Kutoa mafunzo ya ukakamavu (martial arts) kwa vijana wa Blue Guards katika baadhi ya wilaya za Tanzania Bara na za Zanzibar.

6.4.4 Uimarishaji wa Chama:

Kurugenzi ya Blue Guards imekuwa ikifanya shughuli za kukijenga na kukiimarisha Chama kwa kushirikiana na Kurugenzi nyengine, pia kwa njia zake peke yake. Katika hili Kurugenzi imefanya kazi zifuatazo:

(i) Kwa kushirikiana na Ofisi ya Katibu Mkuu, Kurugenzi baina ya Novemba 2007 – Januari 2008 ilifanya ziara katika majimbo yote 18 ya Pemba kukagua uhai wa Chama, kuimarisha matawi na kuhamasisha wananchi, hasa vijana wajiunge na CUF. Ziara kama hiyo ilifanyika kwa majimbo yote 32 ya Unguja baina ya Februari – Aprili 2008.
(ii) Kwa kushirikiana na Kurugenzi nyengine, Kurugenzi ilifanya ziara katika wilaya za ya Kanda ya Kusini kwa lengo la kuwahamasisha wananchi kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura. Ziara kama hiyo ilifanyika katika mikoa ya Kusini Nyanda za Juu, Kanda ya Ziwa na Kanda ya Kati.
(iii) Kushiriki katika ziara ya Makamo Mwenyekiti ya kuhamasisha ujenzi wa Chama na kuhimiza wanachama kujitokeza katika chaguzi za Chama za ngazi zote.
(iv) Kusaidia kutatua migogoro katika Wilaya za Newala, Sikonge, Tandahimba, Bagamoyo, Kilwa, Kinondoni, Ilala, Kondoa, Urambo na Tanga kwa Tanzania Bara; na Majimbo ya Micheweni, Wete, Kojani, Mtambwe, Ziwani, Chake Chake, Mtambile na Mkanyageni na Wilaya ya Magharibi, kwa upande wa Zanzibar.
(v) Kushiriki katika kuzindua Waratibu wa Chama katika Wilaya za Ilala, Temeke na Kinondoni katika Mkoa wa Dar es Salaam.
(vi) Kushiriki katika mikutano ya ndani na ya hadhara katika Wilaya za Ilala, Kinondoni, Temeke, Tandahimba, Newala, Nanyumbu, Tunduru, Tanga, Muheza, Mbinga, Liwale, Tabora (M), Nachingwea, Ruangwa, Lindi (M), Lindi (V), Mtwara (M), Mtwara (V), Masasi, Songea (M), Songea (V), Rufiji, Mkuranga na kuingiza wanachama wapya zaidi ya 5,000.
(vii) Kutoa ulinzi wa kuaminika katika shughuli zote za Chama zikiwemo maandamano, mikutano ya hadhara, makongomano na semina.
(viii) Kuhakikisha Viongozi Wakuu wa Chama wanapata ulinzi mahiri na wa kuaminika kwa kuwapa ulinzi wa vijana wa Blue Guards muda wote.
(ix) Kuhakikisha majengo ya Chama yako salama kwa kuyapa ulinzi wa vijana wa Blue Guards muda wote.
(x) Kushiriki katika ziara ya Makamo Mwenyekiti ya Utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Chama (OSPI) katika majimbo 17 ya Unguja.
(xi) Kushiriki katika kampeni za Uchaguzi mdogo wa Jimbo la Tunduru, na kata za Chongoleani na Ngamiani Kati ambako CUF ilipata ushindi.

6.4.5 Kazi za Kawaida na za Kiofisi:

Kazi hizi zinajumuisha kuwepo kwa mawasiliano baina ya Kurugenzi na vitengo vya Blue Guards vya wilaya, na baina ya Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Taifa na Kamati za Ulinzi na Usalama za wilaya.

Hadi mwishoni mwaka 2008, Kurugenzi ilishakamilisha kuweka mtandao wa mawasiliano na wilaya 68 za Tanzania Bara na Zanzibar. Mtandao huu umesaidia sana kutuma taarifa kwenda na kutoka wilayani kwa wakati na hivyo kuongeza ufanisi katika kutekeleza majukumu ya Kurugenzi.

Shughuli nyengine za utendaji wa siku kwa siku zinaendelea, zikiwemo za utawala katika Kurugenzi, kuchukua hatua za kinidhamu kwa watendaji wa Kurugenzi na vijana wa Blue Guards pale inapobidi, na kukutana na wageni kutoka wilaya na nje ya Chama.

Mwisho

Kurugenzi imepata mafanikio makubwa katika kujenga mtandao wa vijana wa Blue Guards nchini, kutoa mafunzo kwa vijana hao, kukilinda Chama, Viongozi wake Wakuu na majengo yake. Malengo yetu katika kipindi kijacho ni kuendeleza mafanikio yaliyopatikana na kuondoa mapungufu yaliyojitokeza katika kipindi kinachomalizika.

6.5 KURUGENZI YA FEDHA NA UCHUMI:

Taarifa ya Kurugenzi ya Fedha na Uchumi ina sehemu zifuatazo:

(a) Utangulizi
(b) Bodi ya Wadhamini
(c) Utayarishaji wa Bajeti ya Chama
(d) Utafutaji wa Vyanzo vya Fedha, na
(e) Ukaguzi wa Hesabu za Chama

6.5.1 Utangulizi:

Kurugenzi hii, kwa majina tofauti imekuwepo tangu Chama kilipoanzishwa, mwaka 1992. Katika vipindi vyote vilivyopita tatizo kubwa la Kurugenzi limekuwa ni kuwa na vyanzo vya mapato ukiacha ruzuku kutoka serikalini iliyoanza kutolewa baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995. Pia kumekuwa na tatizo la kudhibiti vizuri hicho kidogo kinachopatikana.

Kuanzia mwaka 2006, baada ya kupitishwa kwa mabadiliko ya miundo ya Kurugenzi, Kurugenzi hii imekuwa ikongozwa na Mheshimiwa Juma Duni Haji, ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu (Zanzibar) akiwa ni Mkurugenzi, na Mheshimiwa Salim Omar Mandari kutoka Tanzania Bara akiwa ni Naibu Mkurugenzi.

6.5.2 Bodi ya Wadhamini:

Katiba ya Chama, katika Ibara ya 75 inaanzisha Bodi ya Wadhamini yenye jukumu la kuwa dhamana wa mali zote za Chama. Mkurugenzi na Naibu Mkurugenzi wa Fedha na Uchumi ndio Katibu na Naibu Katibu wa Bodi hiyo, na ndio wenye jukumu la kuitisha vikao vya Bodi.

Baina ya mwaka 2004 – 2006 kabla ya kupitishwa kwa Mpango Mkakati wa Chama (SP) Bodi iliweza kufanya jumla ya vikao 6 na baina ya 2006 baada ya kufanyika mabadiliko ya miundo ya Kurugenzi, Bodi ya Wadhamini imefanya jumla ya vikao 4.

Katika vikao hivyo Bodi hupokea taarifa za mapato na matumizi ya Chama, kuyapitia, kuyachambua na kuona mapungufu na kutoa miongozo ya kurekebisha mapungufu hayo. Aidha Bodi hupokea Ripoti za Ukaguzi wa Mkaguzi wa Nje na kuchambua maoni na mapendekezo ya Mkaguzi huyo na kisha kutoa maelekezo kwa Kurugenzi. Halikadhalika, Bodi hupokea taarifa ya mali na vifaa vinavyomilikiwa na Chama, uchakavu wa mali hizo, utunzaji wake, kuidhinisha kuuzwa kwa vifaa vilivyochakaa, na mipango ya kununua mali na vifaa vipya vya kazi.

Kwa jumla Bodi imetimiza jukumu lake la kuona mali na vifaa vya Chama vinatunzwa vizuri, na kuhakikisha udhibiti wa fedha za Chama na kwamba taratibu na kanuni za matumizi na ununuzi kama zilivyowekwa na Baraza Kuu zinatekelezwa ipasavyo.

6.5.3 Utayarishaji wa Bajeti ya Chama:

Kurugenzi ina kazi nzito ya kutayarisha makadirio na mapato ya Chama kitaifa, hasa ikizingatiwa kuwa vyanzo vya mapato ni vichache na mahitaji ya matumizi ni makubwa na yanaendelea kukua mwaka hadi mwaka.

Kila mwaka Kurugenzi huzitaka Kurugenzi nyengine kutayarisha makadirio ya matumizi yao na kuyawasilisha kwa Kurugenzi ya Fedha na Uchumi, ambayo kwa kuzingatia mapato yanayotarajiwa kuingia, hupendekeza kima cha matumizi kwa kasma ya kila Kurugenzi. Mapendekezo hayo huwasilishwa katika vikao vya Kamati ya Utendaji ya Taifa na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa kwa maamuzi.

Kurugenzi imekuwa ikitegemea mapato kutoka ruzuku ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano na michango ya asilimia kumi (10%) ya mshahara wa kila Mbunge na Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi. Kwa bahati mbaya, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar haijawahi kutoa ruzuku kwa CUF, ingawa kuna tetesi kuwa SMZ hutoa ruzuku kwa CCM. Kurugenzi imejitahidi kila njia kudai ruzuku hiyo kutoka SMZ, ambayo kwa mujibu wa Sheria Na. 5 ya Vyama vya Siasa ya 1992 ya Jamhuri ya Muungano na Sheria ya Ruzuku Na. 6 ya Zanzibar ni haki ya Chama, lakini jitihada hizo zimegonga mwamba.

Ni dhahiri kuwa chanzo kikubwa cha fedha za Chama ni ruzuku kutoka Serikali ya Muungano. Hiki sio chanzo cha kutegemewa sana. Kwani kwanza kima halisi cha ruzuku hiyo kinategemea idadi ya kura za Urais na idadi ya Wabunge chama kilivyopata katika uchaguzi uliopita. Serikali ilioko madarakani ikiamua kuhujumu uchaguzi na kukipatia Chama kura na Wabunge wachache, fedha za ruzuku zitapungua. Lakini pia chama tawala baada ya kujiimarisha kimapato kinaweza kutumia wingi wa Wabunge wake katika Bunge kuondoa ruzuku ya serikali kwa vyama vya siasa. Ingawa hatuyatarajii hayo, lakini ukweli ni kwamba hali hii tegemezi ni hatari kwa uhai wa Chama chetu. Hivyo umuhimu wa kutafuta vyanzo vyengine vya mapato hauwezi kupuuzwa.

6.5.4 Utafutaji wa Vyanzo vya Fedha:

Kwa mujibu wa Mpango Mkakati wa Chama (SP), miongoni mwa majukumu ya Kurugenzi ya Fedha na Uchumi ni kutafuta vyanzo mbadala vya mapato ili kukiondolea Chama utegemezi wa chanzo kimoja tu kikuu cha mapato: Ruzuku ya Serikali ya Muungano. Katika kutekeleza lengo hilo, Kurugenzi imefikiria njia kadhaa za kulifanikisha. Miongoni mwa njia hizo ni kuweka utaratibu wa kuomba michango ya hiari kutoka kwa wanachama, wapenzi wa Chama, na watu, ndani na nje ya nchi, wenye kuunga mkono harakati za kuleta demokrasia ya kweli nchini. Kurugenzi imewaandaa wanachama kadhaa, kuwapa mafunzo ya kutafuta michango hiyo kwa kutumia barua maalum za maombi zenye saini ya Mwenyekiti wa Taifa wa Chama na Katibu Mkuu. Kila mwanachama anayefanya kazi hiyo atalipwa asilimia iliyokubaliwa katika mkataba baina ya mkusanyaji na Kurugenzi kulingana na makusanyo aliyoweza kupata. Kazi hii imeanza katika robo ya mwisho ya mwaka 2008, na hivyo bado ni mapema kujua kiwango cha mafanikio yake.

Halikadhalika Kurugenzi imewekeza katika ununzi wa viwanja, ambavyo thamani yake inapanda kila kukicha. Kurugenzi pia imeingia mkataba na wafanyabiashara kadhaa wenye mapenzi na Chama kuwekeza katika miradi kadhaa. Dalili zinaonesha kuwa kuna uwezekano wa kupata mafanikio makubwa. Kurugenzi imo katika kutafuta mbinu nyengine za kupata mapato.

6.5.5 Ukaguzi wa hesabu za Chama:

Kurugenzi imejitahidi kuweka utaratibu mzuri wa mahesabu, na kutunza kumbukumbu zote za mapato na matumizi. Ukaguzi unaofanywa na Mkaguzi wa Ndani aliyeko katika Ofisi ya Katibu Mkuu kubaini kasoro na kutaka zirekebishwe kabla ya hesabu hizo kupelekwa kwa Mkaguzi wa Nje. Kurugenzi imefanikiwa kupeleka hesabu zake kwa ukaguzi wa Mkaguzi wa Nje kwa wakati kila mwaka. Kwa miaka yote tangu 2004 Chama kinapata cheti nadhifu (Clean Certificate) kutoka kwa Mkaguzi wa Nje. Kasoro ndogo ndogo zinazogunduliwa hurekebishwa katika mwaka unaofuata.

CUF ni miongoni mwa vyama vichache vinavyowasilisha hesabu zilizokaguliwa kwa wakati kila mwaka kwa Msajili wa Vyama vya Siasa kama sheria inavyoagiza. Msajili mwenyewe ni shahidi wa hili.

Taarifa za hesabu zilizokaguliwa kwa miaka kuanzia 2004 hadi 2008 zimeambatanishwa na taarifa hii katika Viambatisho.

Mwisho:

Kwa jumla, Kurugenzi imeweza kujitahidi kulipa madeni kwa sehemu kubwa, na tangu mwaka 2007 Kurugenzi imeweza kujibana kwa kujiepusha na kujiingiza katika madeni mapya. Ni mategemeo yetu katika kipindi kijacho madeni yote yatalipwa na kujizuia kukopa.

Halikadhalika utunzaji wa hesabu umekuwa wa kuridhisha pamoja na uchache wa fedha ikilinganishwa na mahitaji ya matumizi. Shughuli muhimu za Chama zinafanyika na Chama hakijakwama. Ni kweli muda mwengine hujitokeza matumizi ya dharura ambayo hupelekea kukorogeka kwa bajeti, lakini hili litapungua sana kutokana na maamuzi ya kutenga kiasi fulani cha fedha kwa kila mwezi kwa kukabiliana na dharura zinazozuka.

SURA YA SABA

MAMBO YA NJE NA UHUSIANO WA KIMATAIFA

8.1 Utangulizi

Kipindi cha miaka mitano iliyopita kimeshuhudia mafanikio makubwa ya CUF katika eneo la mashauri ya nchi za nje na mahusiano ya kimataifa ambayo hayakuwahi kufikiwa katika historia ya Chama chetu. Shughuli hizi kwanza zilifanyika chini ya Kurugenzi ya Mambo ya Nje na Haki za Binadamu (2004 – 2006) na baadaye, kufuatia marekebisho makubwa ya muundo wa Chama, kuhamishiwa katika Ofisi ya Katibu Mkuu chini ya Idara Maalum ya Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa (2006 – 2008). Idara hii inaongozwa na Mhe. Ismail Jussa.

Maeneo ambayo yameonyesha mafanikio makubwa katika kipindi hiki ni pamoja na Chama kujitangaza na kutambulika vyema katika duniani, Chama kushiriki kikamilifu na kwa nguvu kubwa zaidi katika jumuiya za kimataifa ambazo kimejiunga kikiwa ni mwanachama, Chama kuanzisha mahusiano ya moja kwa moja na baadhi ya vyama vya siasa vyenye kufuata mrengo wa siasa wa kiliberali, Chama kutumia na kupata fursa mbali mbali za misaada kutoka katika jumuiya na vyama rafiki na Chama kuweza kkujitangaza kupitia vyombo vya habari vya kimataifa.

CUF kimeweza kujitangaza na kutambulika vyema duniani kupitia ziara za viongozi wa Chama katika nchi mbali mbali zenye ushawishi mkubwa katika maendeleo ya demokrasia, kwa kuanzisha mfumo imara wa mawasiliano kati ya Makao Makuu na Ofisi za Kibalozi za nchi za nje na mashirika ya kimataifa zilizopo hapa nchini na pia kwa kutumia mawasiliano kupitia mtandao wa internet.

8.2 Ziara za Nje

Mara baada ya kumalizika kwa Mkutano Mkuu wa Taifa wa tarehe 24 – 28 Februari, 2004 na uchaguzi wa uongozi wa Chama kukamilika, Katibu Mkuu wa Chama, Maalim Seif Sharif Hamad, akiambatana na Naibu Mkurugenzi wa Mambo ya Nje na Haki za Binadamu, Mhe. Ismail Jussa, walifanya ziara ya nchi 14 kwa lengo la kukitangaza Chama na kwenda kusafisha propaganda chafu zilizokuwa zikienezwa na CCM dhidi ya CUF. Ziara hiyo iliyofanyika kati ya Machi, Aprili na Mei, 2004 iliufikisha ujumbe huo wa Chama katika nchi za Marekani, Canada, Uingereza, Uholanzi, Ujerumani, Ufaransa, Sweden, Denmark, Norway, Finland, Belgium, Italy, Spain na Oman.

Mwaka 2005, Mwenyekiti wa Chama, Mhe. Prof. Ibrahim Lipumba, naye alifanya ziara nchini Oman. Ziara nyengine zilifanyika mwaka 2006 ambapo Mwenyekiti wa Chama na Katibu Mkuu walitembelea nchi za Uingereza, Sweden, Denmark, Norway na Taiwan.

Katika ziara hizi, viongozi wa Chama waliweza kuonana na viongozi wa ngazi za juu wa Serikali za nchi hizo, vyama vya siasa, wabunge wa Serikali na wa Upinzani na Kamati za Mabunge, mashirika yanayotetea haki za binadamu na ukuzaji wa demokrasia, vyombo vya habari vya kimataifa, vyuo vikuu, taasisi za elimu ya juu na taasisi za utafiti. Viongozi hao pia waliweza kutembelea makao makuu ya Umoja wa Mataifa huko New York, Jumuiya ya Madola (The Commonwealth) huko London, na Umoja wa Ulaya huko Brussels.

Katika ziara hizo zote, ujumbe wa Chama umekuwa ukiwapa taarifa za kina pamoja na kujibu masuala na hoja mbali mbali zinazohusu itikadi na sera za Chama, misimamo ya Chama kuhusiana na mambo yanayojitokeza ndani na nje ya nchi, shughuli za CUF katika kuongoza Upinzani Rasmi Bungeni na katika Baraza la Wawakilishi na pia vitendo vya kuhujumu demokrasia na haki za binadamu na ufisadi unaofanywa na CCM na Serikali zake.

Matokeo ya ziara hizo yamekiwezesha CUF kuwa chama kinachojulikana na kufahamika zaidi katika jumuiya ya kimataifa kuliko chama kingine chochote cha siasa cha hapa Tanzania.

8.3 Mahusiano na Ofisi za Kibalozi

Mbali na ziara hizo, mahusiano ya kimataifa kati ya CUF na nchi na mashirika mbali mbali ya kigeni yameweza kuimarishwa kupitia mfumo imara wa mawasiliano kati ya Makao Makuu na Ofisi za Kibalozi zilizopo Dar es Salaam na Ofisi ndogo (Konseli) zilizopo Zanzibar. CUF kimekuwa na utaratibu wa kipekee na wa uhakika wa kubadilishana taarifa kuhusiana na mambo mbali mbali yanayotendeka hapa nchini na nje ya nchi na Ofisi hizo. Hali hiyo imepelekea kufikisha taarifa za matukio, mtazamo na maoni ya CUF kwa haraka kwenda katika Wizara za Mambo ya Nje ya nchi husika kupitia Ofisi zao za Kibalozi. Miongoni mwa Ofisi za Kibalozi ambazo Chama Makao Makuu kimekuwa na mawasiliano ya kudumu na ya mara kwa mara ni pamoja na zile za Marekani, Canada, Uingereza, Uholanzi, Ujerumani, Ufaransa, Denmark, Sweden, Norway, Finland, Belgium, India, Afrika Kusini na Zambia.

Chama pia kimekuwa na mahusiano mazuri na mawasiliano ya karibu na Ofisi za mashirika na jumuiya kama Umoja wa Mataifa (UN), Umoja wa Ulaya (EU), Benki ya Dunia (World Bank), Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Shirika la Kiliberali la Friedrich Naumann Stiftung (FNSt).

Matokeo ya kazi nzuri iliyofanyika ya kukuza mahusiano kwa kupitia ziara za nje au ofisi za kibalozi hapa nchini yamewezesha viongozi kadhaa wa ngazi za juu wa nchi za kigeni wanaotembelea Tanzania kutaka kuonana na kufanya mazungumzo na uongozi wa CUF. Hawa ni pamoja na Waziri Mkuu Anders Fogh Rasmussen wa Denmark, Waziri Mdogo wa Mambo ya Nje wa Marekani anayeshugulikia masuala ya Afrika, Dr. Jendaye Frazer, Waziri wa Masuala ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Uingereza, Lord Triesman, Rais wa zamani wa Finland, Marti Ahtisari, Waziri Mkuu Raila Odinga wa Kenya, Waziri Mkuu Jens Stoltenberg wa Norway, na Waziri wa Ushirikiano wa Kimataifa wa Norway, Bibi Hilda Johnson.

8.4 Ushiriki katika Jumuiya za Kimataifa

Ijapokuwa CUF kilikuwa chama cha siasa cha kwanza nchini Tanzania kujitambulisha na kujiunga na Umoja wa Vyama vya Kiliberali Duniani (Liberal International – LI) na jumuiya zinazohusiana nayo hapo mwaka 1994 kama mwanachama mwangalizi (Observer) na baadaye kama mwanachama kamili mwaka 1997 lakini kwa muda mrefu, kilikuwa hakijashiriki kisawa sawa na kujenga jina katika jumuiya hizo.

Kipindi cha miaka mitano iliyopita kimeshuhudia ushiriki mkubwa na unaotambuliwa na kuheshimiwa wa CUF katika jumuiya hizi. Kwanza CUF imefanikiwa kubaki na msimamo wa kujua mwelekeo wake wa kiitikadi katika mrengo wa siasa (Uliberali), tofauti na vyema vyengine vya siasa hapa nchini ambavyo vimebadilisha mrengo wa kisiasa kwa kufuata maslahi binafsi zaidi. Lakini mafanikio makubwa zaidi yamekuwa ni yale ya CUF kushiriki kikamilifu katika kutimiza wajibu wake kimataifa.

CUF kimeweza kulipa madeni yote ya nyuma na kufanikiwa kulipa ada ya uanachama wa Liberal International kwa miaka yote hii mitano. Kimeshiriki vikao kadhaa vya Kamati ya Utendaji (Executive Committee) na kutoa michango yake kikamilifu katika kuandaa agenda za Mikutano Mikuu ya Umoja huo.

Mwaka 2004, Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, alikuwa mmojawapo wa wahutubiaji wakuu (guest speakers) katika ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa 52 wa Liberal International huko Budapest, Hungary na hotuba yake iliyohusu haja ya kutafsiri upya maana ya misingi ya demokrasia ya kiliberali katika zama hizi hasa kwa kuzingatia mahitaji ya Bara la Afrika badala ya ile ya nchi wahisani ambayo mara nyingi hujali maslahi yake ilipokelewa vyema na kwa hisia kubwa kutoka kwa washiriki.

Mwaka 2006, Mwenyekiti wa CUF, Mhe. Prof. Ibrahim Lipumba, alipewa heshima ya kuwa msemaji mkuu wa Bara la Afrika katika Mkutano Mkuu wa 54 wa Liberal International uliofanyika huko Marrakech, Morocco. Hotuba ya Mhe. Prof. Lipumba iliyohusu Demokrasia na Maendeleo barani Afrika ilifurahiwa na iliweza kuchapishwa katika jarida maalum la Umoja huo.

Mwaka 2006, Mwenyekiti wa CUF pia alipata fursa ya kuwa mwakilishi wa Afrika na kutoa hotuba kwa niaba ya vyama vya siasa vya kiliberali vya Afrika katika mkutano uliohusu maendeleo ya kidemokrasia duniani na changamoto zake uliofanyika huko Taipei, Taiwan.

Mwezi Desemba 2007, Msaidizi Maalum wa Katibu Mkuu wa CUF katika Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa, Mhe. Ismail Jussa, alialikwa kutoa mada inayohusu Usafirishaji haramu wa binadamu na Athari zake kwa Wanawake (Gender Aspects of Human Trafficking) katika Mkutano wa Pamoja wa Liberal International na Umoja wa Vyama vya Kiliberali wa Asia (Council of Asian Liberal and Democrats – CALD).

Mwenyekiti wa CUF pia alikiwakilisha Chama katika Mkutano wa 55 wa Liberal International uliofanyika mwezi Mei, 2008 huko Belfast, Ireland ya Kaskazini.

Ukiacha shughuli hizo za LI, CUF katika kipindi cha miaka mitano iliyopita kimeshiriki kikamilifu katika shughuli za Umoja wa Vyama vya Kiliberali vya Afrika (Africa Liberal Network – ALN). Kimeshiriki katika mikutano na semina za mafunzo za ALN zilizofanyika Johannesburg (Afrika Kusini), Maputo (Mozambique), Lusaka (Zambia) na Dakar (Senegal).

Tarehe 2 – 4 Agosti, 2008, CUF kilipata heshima ya pekee ya kuwa mwenyeji wa Mkutano Mkuu wa ALN pamoja na semina ya kuandaa Mkakati wa kuimarisha ALN, shughuli ambazo zilifanyika katika hoteli ya Golden Tulip, mjini Dar es Salaam. Vyama 12 vya siasa vya Afrika vilishiriki mkutano huo ambavyo ni CUF (Tanzania), PDD (Mozambique), RDR (Cote d’Ivoire), DA (South Africa), UPND (Zambia), SNP (Seychelles), PSD (Tunisia), ANADER (DRC), ADF-RDA (Burkina Faso), UDF (Malawi), UC (Morocco), na PDS (Senegal).

8.5 Mahusiano na Vyama vya Siasa

Mbali ya mahusiano kupitia jumuiya za kimataifa, CUF kimeweza kuimarisha mahusiano ya moja kwa moja na vyama vya siasa vyenye kufuata mrengo wa kiliberali au ule unaofanana na huo na pia kuanzisha mahusiano mapya na vyama vyengine. Mahusiano yetu na Chama cha Liberal Democrats cha Uingereza yameendelea kuimarika kupitia ziara za viongozi wa vyama vyetu viwili nchini Uingereza na Tanzania. Mwezi Septemba 2005, Katibu Mkuu wa CUF akiwa pia ni Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CUF alialikwa kuwa mgeni maalum na kupewa heshima ya kuuhutubia Mkutano Mkuu wa Chama cha Liberal Democrats uliofanyika Blackpool, Uingereza. Chama hicho kimeendelea kutoa misaada mbali mbali kwa CUF kupitia shirika la Westminster Foundation for Democracy.

Ndani ya kipindi hiki, CUF kimeanzisha mahusiano pia na vyama vya Democratic Alliance – DA (Afrika Kusini), UPND (Zambia), Seychelles Nationalist Party – SNP (The Seychelles), Venstre (Norway), Democratic Progressive Party – DPP (Taiwan), Folkpartiet – Liberal Party (Sweden) na VVD na D66 (The Netherlands).

Mahusiano haya ya moja kwa moja ya Chama na Chama yamewezesha kufanya ziara za kubadilishana uzoefu, kualikana na kuhudhuria katika Mikutano Mikuu ya vyama rafiki na pia kupata misaada mbali mbali inayotolewa kupitia Taasisi zilizoanzishwa na nchi husika kwa kuvisaidia vyama vyenye mahusiano na vyama vya siasa katika nchi hizo. Mwenyekiti wa Chama, Mhe. Prof. Lipumba, alipata heshima ya kuwa mgeni rasmi katika Mkutano Mkuu wa DA uliofanyika mwaka 2007 huko Afrika Kusini. Viongozi wa CUF wamealikwa kufanya ziara za mafunzo na DPP huko Taiwan. Viongozi wa Venstre kutoka Norway wametembelea Tanzania mara mbili (2005 na 2007).

Hivi karibuni, mawasiliano yameanza yenye lengo la kuanzisha mahusiano na chama cha Forum for Democratic Change – FDC cha Uganda na chama cha Orange Democratic Movement – ODM cha Kenya. Lengo ni kukuza mahusiano na vyama vya siasa vilivyo makini katika nchi za Afrika Mashariki.

8.6 Misaada kupitia Vyama na Taasisi Rafiki

Kutokana na mahusiano mazuri yanayoimarika kati ya CUF na vyama vya siasa na mashirika ya kimataifa yenye malengo kama ya Chama chetu, na kutokana na ushiriki mkubwa katika jumuiya ambazo CUF ni mwanachama, tumeweza kufanikisha kuongeza misaada inayotolewa kwetu na hivyo kujiongezea uwezo zaidi wa kufanikisha shughuli zetu.

Shirika la Friedrich Naumann Stiftung (FNSt) la Ujerumani limeendelea kuwa mshirika mkuu wa CUF katika kukijengea Chama uwezo kupitia programu mbali mbali za mafunzo zilizotengenezwa na kuendeshwa kwa pamoja kati ya Shirika hilo na CUF. Semina za mafunzo hapa nchini na ziara za mafunzo nje ya nchi zimeendelea kufanyika na kukifaidisha mno Chama, viongozi na watendaji wake. Mafunzo yanayohusu itikadi ya Uliberali, sera za CUF, mfumo na muundo wa utawala, uendeshaji wa kampeni, na utekelezaji bora wa shughuli za Bunge na Baraza la Wawakilishi na Madiwani yametolewa katika kipindi hiki kuanzia ngazi ya Taifa hadi Wilaya. FNSt pia wamekipatia chama msaada wa mashine ya power point, laptop na vifaa vyengine vya kutolea mafunzo.

Chama rafiki cha Liberal Democrats kupitia Shirika la Westminster Foundation for Democracy kimefanikisha kufanyika kwa mafunzo yaliyowashirikisha viongozi wa kitaifa yanayohusu ujenzi wa taswira bora ya Chama na jinsi ya kuimarisha mfumo wa mawasiliano na utangazaji wa Chama na pia mafunzo kwa viongozi na watendaji wa Umoja wa Wanawake wa CUF. Chama hicho pia kimewezesha CUF kupata msaada wa pikipiki 60 ambazo zilikuwa ni sehemu ya pikipiki zilizotolewa kwa wilaya kadhaa za Chama, seti 5 kwa mwaka 2004 na seti 6 kwa mwaka 2008 za mabomba ya mikutano ya hadhara (PA Systems), mabomba 20 ya mkono (megaphones), pamoja na mashine za photocopy 2 na risograph printers 2, computers 5 na printers 5 kwa ajili ya Makao Makuu na Ofisi Kuu za Chama.

Mahusiano na Chama cha Venstre cha Norway yamepelekea kupatikana kwa msaada kupitia Norwegian Centre for Democracy Support kuanzia mwaka 2008 na kuendelea mwaka 2009 ambapo Venstre inashirikiana na CUF kuendesha mafunzo ya viongozi wakuu wa wilaya waliochaguliwa katika uchaguzi uliomalizika mwaka jana. Mpango wa mafunzo hayo umepangwa uwe wa kuendelea ili kuwajengea uwezo zaidi viongozi na watendaji wakuu wa ngazi ya wilaya wa CUF.

Pia ushiriki wa CUF wa programu za Taasisi ya The Netherlands Institute for Multi-Party Democracy (NIMD) ya Uholanzi umekiwezesha Chama kuendelea kupata msaada wa kuendesha mafunzo mbali mbali yaliyotolewa kwa watendaji wa Makao Makuu na Ofisi Kuu na pia viongozi na watendaji wa Wilaya za Chama kwa kipindi chote cha 2004 – 2009.

8.7 Mahusiano na Vyombo vya Habari vya Kimataifa

Kupitia ziara zinazofanywa na viongozi wa CUF na mawasiliano kwa njia ya mtandao wa internet, Chama chetu kimeweza kuanzisha mahusiano na vyombo kadhaa vya habari vya kimataifa. Habari zinazohusu CUF zimechapishwa na kutangazwa kupitia magazeti kama Washington Post na New York Times (Marekani), Politiken (Denmark), Aftenposten (Norway), Le Figaro na Indian Ocean Newsletter (Ufaransa), Finacial Times, NewAfrican, African Business, Africa Analysis, na Focus on Africa (Uingereza), idhaa za redio za BBC (Uingereza), Duetsche Welle (Ujerumani), VOA (Marekani), Radio France International (Ufaransa) naRadio Iran, na pia vituo vya televisheni kama Australian TV (Foreign Correspondents), BBC, CNN, VoA (Journal Africa), Al Jazeera na nyenginezo.

Kutokana na shughuli hizi, CUF kimebakia kuwa chama cha siasa kinachoongoza kwa kutambulika kwake kimataifa miongoni mwa vyama vyote vya siasa hapa Tanzania. Ni changamoto inayoukabili uongozi wa Chama utakaoshika madaraka kwa kipindi cha miaka mitano ijayo kuendeleza mafanikio hayo na kufikia mengine zaidi ili jina la CUF liendelee kung’ara kimataifa kama linavyong’ara hapa Tanzania.

SURA YA NANE

TATHMINI YA JUMLA

9.1 Utangulizi

Kipindi cha kuanzia 2004 hadi 2008 kimekuwa muhimu kwa ukuwaji wa Chama kutokana na ukweli kwamba kwa mara ya mwanzo Chama kilianzisha Mpango Mkakati wake ambao umekuwa ndiyo dira ya utekelezaji inayoweza kufanyiwa tathmini, kupimika na kurekebishika.

Uchaguzi Mkuu wa mwisho kufanyika nchini, yaani wa 2005, unachukuliwa na Taarifa hii kama kigezo cha tathmini ya hali halisi ya Chama kwa kipindi hiki na muakisiko wake ndio unaotumiwa kutathmini nguvu na mafanikio, mapungufu na udhaifu, matatizo na vikwazo na fursa za Chama kwa kipindi hicho na pia kuweka msingi wa matarajio ya Chama kwa miaka mingine mitano ijayo. Kwa madhumuni ya kurahisisha na kubainisha lengo la pamoja la Chama, sehemu hii itazingatia hali ya Chama kwa ujumla wake na sio kwa kutumia kitengo kimoja kimoja.

9.1 Nguvu na Mafanikio

Matayarisho ya Chama kwa Uchaguzi Mkuu wa 2005 yanaingia katika kumbukumbu za historia ya CUF kama ishara na ya nguvu na mafanikio ya Chama hiki kwa miaka mitano iliyopita. Kwa mara ya kwanza Chama kiliweza kuweka wagombea 164 wa ubunge, ambao ni wengi kuliko mara nyengine mbili zilizopita, yaani 1995 na 2000. Mara hii pia Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano na wasaidizi wake walipita karibu kila eneo la Tanzania ambako muitiko wa wananchi ulikuwa ni mkubwa kuliko wakati mwengine wowote huko nyuma. Vile vile Bajeti ya Chama kwa uchaguzi huu ilikuwa ina fungu kubwa zaidi ya mara nyengine zote. Mwisho, Chama kilitoa msaada wa kifedha kwa wagombea wote wa Ubunge.

Na licha ya kuwa Uchaguzi Mkuu huo nao ulivurugwa na Serikali za CCM, bado nafasi ya Chama imeendelea kuwa nzuri machoni kwa wapiga kura hadi sasa. Kwa Zanzibar, ambako ni wazi kiwango cha kuvunjika moyo kwa wapiga kura kilikuwa kikubwa mara baada ya matokeo ya 2005 kutangazwa, sasa hali imerudi katika mstari wake na Chama kinakwenda mbele. Kwa upande wa Tanzania Bara, ambako nako hali ilikaribiana na hiyo, ari na nguvu ya wanachama na wafuasi imeanza kurudi upya na kazi inaendelea vyema.

Ni wazi kuwa katika hali ya kawaida matokeo na matukio yaliyoambatana na Uchaguzi Mkuu wa 2005 kwa Tanzania Bara na kwa Zanzibar yalitarajiwa kukisambaratisha Chama, lakini kimeweza kusimama tena baada ya dhoruba zile kwa sababu sita zifuatazo:

a) CUF ni Chama pekee ambacho Watanzania wanakiona mbadala wa CCM.
b) CUF ni Chama cha kitaifa: mtandao wake ni mkubwa kuliko vyama vyengine vya upinzani.
c) CUF ni Chama chenye oganaizesheni na kinachoedeshwa kitaasisi na sio kama kampuni ya mtu binafsi.
d) CUF kinaUongozi madhubuti na jasiri.
e) CUF kina wanachama wazalendo na wanaojitolea.
f) CUF kina sera nzuri zinazotekelezeka na ambazo baadhi yake sasa zimekuwa zikichukuliwa na kutumiwa hata na serikali za CCM kutokana na ubora wake.

Mambo haya sita ndiyo nguvu na hivyo sababu ya mafanikio ya Chama pale ambapo kimefanikiwa. Hivi sasa, kwa mfano, CUF kimesambaa katika mikoa mingi ya Tanzania Bara kuliko ilivyokuwa hapo kabla. Muongozo wa SP ya Chama umeigawa nchi katika Kanda na kuagiza msisitizo kuwekwa katika kanda maalum ambazo zinaashiria kuwepo, kukubalika na hivyo kuhakikisha ushindi wa Chama katika chaguzi kinazoshiriki. Baada ya uchaguzi wa 2005, tathmini iliyofanywa ilionyesha mapungufu katika eneo hili na mikakati ikawekwa kukabiliana nayo. Mwenyekiti alichukua jitihada maalum za kukisambaza Chama na sasa mtandao wa Chama umekuwa mkubwa zaidi ya ulivyokuwa kabla ya kipindi hiki na hiyo imekuwa ni nguvu za Chama.

Nguvu nyengine ya Chama kwa sasa ni uhusiano wake na vyombo vya habari. Kazi ambayo imefanywa na uongozi wa Chama, hasa kupitia Kurugenzi ya HBMU na Idara ya Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa katika Ofisi ya Katibu Mkuu, imesaidia sana kuvileta vyombo vya habari katika nafasi ya kukiangalia Chama vizuri. Taarifa zilizokusanywa baada ya 2006, zinaonesha kuwa vyombo vya ndani vya habari vimeanza kuchupa mstari wa utiifu vilivyokuwa nao kwa CCM pekee na sasa vinakichukulia CUF kama chama mbadala (Rejea taarifa za HBMU na Idara ya Mambo ya Nje).

Kwa siku za karibuni, Chama pia kimeongezewa nguvu kwa kupata kundi la vijana wasomi kujiunga nacho kwa ajili ya kazi za ndani kama vile Kitengo vya Utafiti, Jumuiya ya Vijana, na Kiteno cha Ukuzaji wa Sera ambao wanafanya kazi za awali za kukuza mfumo wa utekelezaji. Taarifa za Kurugenzi ya Siasa zinaonesha kuwa jitihada ambayo imekuwa ikifanyika ya kuwafikia vijana wa kundi hili imeanza kuzaa matunda mema. Huko nyuma, ilikuwa si rahisi kwa vijana wasomi kujiunga na CUF kwa kuwa taswira iliyokuwa imejengeka ni kwamba kujiunga na Chama kungeliweza kuzuia fursa za kujiendeleza kielimu na kiuchumi kwa vijana hao, mambo ambayo huhitajika na kila kijana.

Mifano ya karibuni zaidi ni pale Chama kilipoandaa Kongamano maalum la kujadili Ukosefu wa Uongozi na Hatima ya Tanzania la Agosti 28, 2008 (Dar es Salaam), Kongamano kwa Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu Kuhusu Mikopo la Oktoba 25, 2008 na Kongamano Maalum kwa Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu kuhusu Hatima ya Zanzibar na Mustakbali wa Muungano la Disemba 4, 2008 (Zanzibar), ambapo idadi ya wanafunzi wa taasisi za elimu ya juu waliohudhuria na kuchangia ilikuwa kubwa.

Kwa hivyo, ndani ya kipindi hiki, Chama kimesimama kama taasisi imara ya kisiasa kwa kujijengea kuaminika miongoni mwa Watanzania. Kuna muitikio mkubwa kwa sera na misimamo ya CUF miongoni mwa wananchi. Kwa mfano, mtazamo wa uongozi wa CUF juu ya uwezo mdogo wa Rais Jakaya Kikwete ndio pia mtazamo wa wananchi wakiwemo waandishi na wachambuzi wa siasa, wasomi, viongozi wa taasisi za kijamii na kidini na hivyo hata wananchi wa kawaida. Neno ‘usanii’ ambalo CUF ililitumia kwa mara ya mwanzo kuelezea staili ya uongozi wa Rais Kikwete, chama na serikali yake, limekuwa ni neno lililokubalika sasa kuzungumzia muktadha huo. Mapambano yaliyoasisiwa na CUF kuanzia 2004 hadi 2006 dhidi ya ufisadi sasa ndiyo alama ya mapambano dhidi ya CCM na Serikali zake kandamizi. Msimamo wa CUF kuhusu hadhi ya Zanzibar ndani ya Muungano, umekuwa sasa ndio msimamo wa Wazanzibari wengine wote. Tamko la Mwenyekiti wa Taifa wa CUF Mhe. Prof. Ibrahim Lipumba kutahadharisha juu ya kuwepo kwa ombwe la kiuongozi (leadership vacuum) katika utendaji wa Rais Kikwete sasa ndiyo maoni ya wachambuzi wote makini na wa vyama vyengine vya siasa vya upinzani.

Kwa hivyo, CUF imekuwa na nguvu ya kukubalika kuonesha njia na wengine wakafuata na ni maoni ya Taarifa hii kuwa hilo limewezeshwa kwa kiasi kikubwa kutokana na aina ya uongozi uliopo na vile vile kufuatwa kwa Muongozo wa SP.

9.2 Udhaifu na Mapungufu

Ukichukuliwa tena Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005 kama kigezo cha tathmini hii, basi matokeo ya kabla wakati wa uchaguzi na baada ya uchaguzi huo imejengeka picha ya aina ya udhaifu na mapungufu ya Chama. Mapungufu hayo yaligunduliwa na Kamati ya Katibu Mkuu ya kukifanyia tathmini ya kina Chama mara baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005 na matokeo yake yasiyoridhisha. Kamati hiyo iliorodhesha kasoro na mapungufu yafuatayo:-

(a) Kuwepo kwa mipango tofauti na inayopingana katika ujenzi wa Chama na katika kukabiliana na chaguzi, na hivyo kukosa mwelekeo mmoja wenye shabaha na dhamira zinazofanana.
(b) Ukosefu wa uwajibikaji na nidhamu miongoni mwa viongozi na watendaji wa Chama.
(c) Muundo dhaifu wa Chama katika Makao Makuu na Ofisi Kuu na watendaji kutojua dhamana na wajibu wao na hivyo kusababisha migongano ya majukumu.
(d) Ufinyu wa mfumo wa inteligensia (Intelligence) ya Chama.
(e) Viongozi wasiowajibika katika ngazi mbali mbali za Chama.

Huo ndio udhaifu uliogundulika mapema mwaka 2006 ambao ulipelekea kubuniwa kwa Mpango Mkakati wa Chama (SP). Kwa maneno mengine SP ilibuniwa kukabiliana na mapungufu hayo na mengine. Hatuwezi kudai kuwa utekelezaji wa SP hadi sasa umefanikiwa kuyaondosha mapungufu hayo yote. Hata hivyo kumekuwa na hali bora kuliko ilivyokuwa hapo 2006. Bado baadhi ya mapungufu hayo yanakikabili Chama pamoja na juhudi zinazoendelea kuchukuliwa kuyaondosha kabisa.

Katika ngazi ya taifa migogoro imepungua kwa asilimia kubwa. Viongozi wanafanya kazi kama timu moja. Lakini ni ukweli usiopingika kuwa matatizo ya migogoro isiyokuwa ya lazima bado inaziandama baadhi ya wilaya, majimbo/kata na hata matawi. Migogoro hiyo huathiri uwezo wa Chama kupambana na wapinzani wake katika Chaguzi, hasa za vitongoji, vijiji na mitaa.

Mapungufu mengine ni pamoja na kupungukiwa na tafiti zilizofanywa kitaalamu na kwa kina. Kuundwa kwa Special Task Force (STF) chini ya Katibu Mkuu kumesaidia kupunguza viongozi wasiowajibika katika ngazi za chini. Hata hivyo wakati mwengine tatizo liliojitokeza ni kuwa wanachama wazuri wenye uwezo hufanyiwa mizengwe ili wasiombe nafasi za uongozi, na hivyo Baraza Kuu kujikuta linalazimika kuwateua viongozi wale wale ambao wana kasoro nyingi kugombea nafasi hizo. Kwa maana nyengine, bado hatujafanikiwa kuwaondoa viongozi wasiowajibika kwa asilimia mia moja. Wakati huo huo, pamoja na juhudi za Kamati ya Ulinzi na Usalama na Kurugenzi ya Blue Guards kuimarisha Intelligence katika Chama bado kunahitajika kazi ya ya ziada kujiimarisha katika eneo hilo.

Bila ya utafiti wa kina unaotoa matokeo sahihi, nadharia ya uongozi wa kisasa wa kisiasa inabaki kuwa njozi. Mifano ni mingi ya kushindwa kwa mipango ya Chama kwa sababu ya ukosefu wa utafiti. Kamati ya Katibu Mkuu ilithibitisha kuwa Operesheni Nguvu ya Umma ya mwaka 2005 haikufanikiwa kwa kuwa hakukuwa na utafiti wa kina kabla. Pengine hata kushindwa kwa Mazungumzo baina ya CCM na CUF ya kuupatia ufumbuzi wa kudumu Mgogoro wa Kisiasa wa Zanzibar, kushindwa kwa Ushirikiano wa Vyama vinne vya Siasa vya Upinzani, kumetokana na sababu hiyo hiyo.

9.3 Vikwazo Dhidi ya Chama

Miongoni mwa vikwazo ambavyo vimekikabili Chama ndani ya kipindi hiki ni ukosefu wa fedha za kutosha. Chanzo kikubwa cha mapato ya Chama kimeendelea kuwa ruzuku kutoka serikalini (98%) na michango ya Wawakilishi na Wabunge. SMZ, hata hivyo, haijawahi kukipatia Chama ruzuku yake inayopaswa kulipwa kwa muda wote. Hadi Novemba 2006, Chama kilikuwa kinaidai SMZ zaidi ya shilingi bilioni 1.5 na kiasi hicho kimekuwa kikiongezeka kila mwezi. Juhudi za kuishinikiza SMZ ilipe deni hilo hazijafanikiwa hadi sasa.

Lakini hata kama kila senti ya ruzuku inalipwa na serikali zote mbili kwa Chama, bado hiki kinaendelea kuwa si chanzo cha kuaminika kwa Chama, kwani siku kinapokauka, ndio Chama nacho kinadhoofika. Kutokuwa na mikakati mingine ya uhakika ya kupatia fedha nyingi na za hakika kunakikwamisha Chama.

Mkakati wa Kurugenzi ya Fedha na Uchumi kukifanya Chama kujitegemea kwa mapato kupitia miradi na michango ya hiari bado haujafanikiwa hadi sasa na matarajio ya mafanikio hayapo kwa siku za karibuni. Ingawa Chama kilipitisha maamuzi kwamba wabunge na wawakilishi wachangie 10% ya mishahara yao kwa Chama, hichi nacho pia si chanzo cha uhakika kuweza kuiendesha taasisi kubwa kama chama cha CUF.

Kikwazo chengine ni ukubwa wa taswira ya CCM inayojengwa kwenye vyombo vya habari, taasisi za kijamii, kidini na vyombo vya dola. Kwa kutumia njia halali au haramu, CCM imeweza kujizatiti kwenye taasisi hizo ambazo ni nyenzo muhimu ya mabadiliko ya kidemokrasia. Kupenya ngome hizo imekuwa changamoto kubwa kwa CUF na ingawa kazi inaendelea, bado ni mapema kuamini kuwa mafanikio ni makubwa ya kujisifia.

Kwa namna moja ama nyengine, taasisi hizo zimekuwa zikishirikiana na CCM kuizorotesha CUF. Kwa mfano, katika mkesha wa upigaji kura katika Uchaguzi Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 2005, aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi Omar Mahita, alijitokeza kwenye vyombo vya habari na visu akidai kuwa ni silaha za CUF ambazo ingelizitumia ikishindwa uchaguzi na pia ilionekana kulikuwa na mkakati wa makusudi wa kuzuia kampeni za mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano kupitia CUF zisitangazwe katika vyombo vya habari. Kuelekea uchaguzi mkuu wa Zanzibar, aliyekuwa Amiri Jeshi Mkuu, Benjamin Mkapa, alipeleka vikosi vya kijeshi na silaha za kivita visiwani humo ili kuizuia CUF isiingie madarakani, makanisa na taasisi nyengine za kidini zilijitokea wazi wazi kumuunga mkono mgombea wa CCM wa Muungano kwa madai kuwa ni chaguo la Mungu, na matukio mengine kadha wa kadha. Yote haya yamebakia kuwa ni vikwazo dhidi ya CUF.

9.4 Fursa za Chama

Kipindi hiki cha miaka mitano, hakikuwa cha vikwazo na matatizo tu kwa Chama, bali kilikuwa pia ni kipindi kilichozalisha fursa kadhaa na ambazo baadhi yake zilitumiwa vyema na CUF katika kujiimarisha.

Fursa ya kwanza na muhimu kuliko zote ni kuanzishwa kwa SP ya Chama. Ni mpango huu, kuliko jambo jengine lolote, ambalo limeweza kutumika na CUF kama nyenzo ya kujijenga kama taasisi imara ya kisiasa. SP imesaidia sana kuipandisha CUF daraja ya kuwa chama cha kisayansi, kwa maana ya kuwa chama kinachofanya mambo yanayopimika, kujaribika na kuthibitika. Muundo wa sasa wa Chama, kama ulivyo, ni matokeo ya SP. Utendaji kazi mzuri wa Chama ulivyo sasa ni matokeo ya SP. Nidhamu ya watendaji Makao Makuu na Ofisi Kuu ni matokeo ya SP. Kwa hivyo ni sawa kuitaja hapa, SP! SP! SP!, kama fursa kubwa ya CUF.

Fursa nyingine ambayo CUF imeitumia ni kasoro kubwa ya uongozi wa CCM. Ombwe la kiuongozi (Leadership Vacuum) ambalo utawala wa Rais Kikwete umekuwa ukilionesha limekuwa na manufaa kwa CUF kwa sababu mbili: kwanza, ni CUF ndiyo iliyomkosoa Kikwete binafsi tangu mwanzoni kwamba si kiongozi anayewafaa Watanzania. Kadiri siku zinavyokwenda hilo limekuwa likidhihirika kutokana na kushindwa kwake na Watanzania wamekuwa wakijirudi kwa kauli ya CUF. Pili, ni CUF ndiyo iliyosimama ya pili kwenye uchaguzi mkuu wa 2005 (kama ilivyokuwa kwa mwa mwaka 2000), kwa hivyo kimekuwa chama mbadala kinachoangaliwa na wapiga kura hata kwa 2010. Ndani ya kipindi hiki, CUF imetumia kila jukwaa ililolipata kusisitiza kushindwa uongozi na kuchoka kwa CCM na Rais Kikwete na kuhakikisha kuwa ni CUF pekee kilichobaki kwa matumaini ya Watanzania. Na hilo limekuwa likiitikiwa vyema, angalau kwa kutathmini muakisiko unaoonekana kupitia vyombo vya habari, mikusanyiko inayoandaliwa na Chama na mazungumzo ya kawaida.

Fursa nyengine ni kufeli kwa mazungumzo kati ya CUF na CCM. Ingawa katika hali ya kawaida hiki kilitakiwa kiwe ni kikwazo kwa CUF, lakini umahiri wa uongozi wa CUF katika siasa za diplomasia zimekigeuza kikwazo kuwa fursa. Kutokana na ukweli kwamba ni CCM ndiyo ‘iliyochafua mazingira’ katika suala hili, CUF ilipata fursa ya kujitangaza na kujizolea kiwango kikubwa cha imani na kukubalika miongoni mwa jamii kuwa ndicho kilichosimama kwenye ukweli na kwenye msimamo wa Umoja wa Wazanzibari na CCM ikafahamika kwamba ilisimama kwenye mgawanyiko wa Wazanzibari. Kauli zilizotolewa na Rais Kikwete alipokuwa ziarani Zanzibar hivi karibuni zimezidi kuwadhihirishia Watanzania dhamira mbaya na ovu za CCM za kuendelea kuwagawa Wazanzibari.

CCM pia imefeli katika kashfa za ufisadi zinazowakabili viongozi wake, imefeli katika kulieleza kwa ufasha suala la hadhi ya Zanzibar na imefeli katika kuleta Maisha bora kwa kila Mtanzania kama ilivyokuwa imeahidi. Katika kufeli huko, CUF imenyakua fursa za kujitangaza, kujieneza na kujizolea ufuasi mkubwa miongoni mwa Watanzania.

9.5 Matarajio ya Chama kwa Miaka Mitano Ijayo:
Katika mada yake “Ukosefu wa Uongozi na Hatima ya Tanzania”, Mwenyekiti wa CUF, Prof. Ibrahim Lipumba, anaainisha kwamba Chama Cha Mapindui (CCM) kilichopo madarakani sasa kimeshazeeka na kuchoka sana kiasi ya kwamba kimeishiwa na mawazo ya kuongoza nchi vizuri:
“Baada ya miaka 47 ya utawala wa CCM na watangulizi wake, ni wazi kuwa CCM imechoka na haina tena mawazo mapya ya kukabiliana na changamoto mpya zinazohitajika kututoa katika umaskini huu wa kutupwa na kutupeleka katika maendeleo na ustawi. CCM imechoka ndiyo maana imeshindwa kuwaongoza Watanzania kutumia neema ya utajiri wa rasilimali tulizo nazo na kuwatoa katika dimbwi la umaskini linalowazonga. CCM imechoka ndiyo maana inaendelea kuwalisha Watanzania takwimu za kukua kwa uchumi huku wananchi walio wengi wakiendelea kuishi bila hata ya kumiliki mlo mmoja ulotimia kwa siku. CCM imechoka ndiyo maana imekuja na sera zinazopalilia tofauti kubwa ya kipato kati ya tabaka la matajiri wachache na tabaka la walalahoi wengi. CCM imechoka ndiyo maana inaimba wimbo wa kupambana na ufisadi huku ikiendelea kuwakumbatia mafisadi. CCM imechoka ndiyo maana imefikia mahala imesababisha kugawanyika kwa Taifa katika misingi ya kidini. CCM imechoka ndiyo maana imeshindwa hata kukabiliana na changamoto za kuuimarisha Muungano wetu kwa misingi ya haki na usawa kati ya Tanganyika na Zanzibar. CCM imechoka ndiyo maana imepoteza dira na mwelekeo ikilipeleka Taifa kusikojulikana. CCM imechoka ndiyo maana hata yenyewe imegawanyika. CCM imechoka ndiyo maana hadi sasa imewachosha Watanzania na Watanzania wameichoka CCM na CCM imechoka ndiyo maana sasa Watanzania tunapaswa kuipumzisha.” (Lipumba, 2008)
Ndani ya sura hii ya kuchoka kwa CCM ndimo mlimo matarajio ya Chama kwa miaka mitano ijao – yaani kuipiku CCM. Nchi inataka mabadiliko na CUF ina matarajio, malengo na dhamira ya kuwa kinara wa kusimamia na kuyaongoza mabadiliko hayo. Prof. Lipumba (2008) anasema:
“Watanzania tunawajibika kujipanga kuleta mabadiliko. Tusipojipanga vizuri na kuwang’oa mafisadi wa CCM, umaskini utaongezeka na nchi inaweza kusambaratika. Lakini agenda ya mabadiliko katika nchi kama Tanzania ambayo watawala wake wamejipenyeza katika kila sekta ya maisha ya wananchi haiwezi kuwa ni jukumu la wanasiasa pekee. Viongozi wa kisiasa wa vyama vinavyoamini katika mageuzi ya kweli tumejitolea kuongoza harakati za kuleta mabadiliko haya. Wengine harakati hizi zimetugharimu sana lakini hatulijutii hilo. Tunaona fahari kwamba tumeweza kujitolea kwa ajili ya kuwaletea mabadiliko Watanzania. Imetuchukua muda mrefu kwa wananchi kuweza kuamini mabadiliko yanawezekana hapa nchini. Lakini sasa Watanzania wameanza kuamka na kuunga mkono kwa nguvu haja ya kuleta mabadiliko.
“Watanzania wanataka mabadiliko yatakayowapa uongozi wa namna bora ya kutumia neema ya utajiri wa rasilimali tulizo nazo ili kuwatoa katika dimbwi la umaskini linalowazonga na kuwalekeza katika maendeleo na ustawi kwa wote. Watanzania wanataka mabadiliko yatakayomhakikishia kila Mtanzania anamiliki alau milo mitatu ilotimia kwa siku. Watanzania wanataka mabadiliko yatakayomhakikishia kila Mtanzania anaongeza kipato chake kupitia kazi halali na jasho lake na kumhakikishia kwamba gharama za maisha hazipandi kiholela. Watanzania wanataka mabadiliko yatakayowapa huduma za msingi za afya zilizo bora, na kuwahakikishia watoto wao wanapata elimu bora ya msingi na sekondari. Watanzania wanataka mabadiliko yatakayowapa maji safi na salama, na miundombinu ya umeme na barabara iliyo imara itakayowezesha sekta binafsi kuongeza ajira kwa vijana wetu. Watanzania wanataka mabadiliko yatakayosafisha uoza wa ufisadi na rushwa na yatakayoleta uwajibikaji na utawala wa sheria. Watanzania wanataka mabadiliko yatakayojenga misingi imara ya umoja, udugu na mapenzi kati ya wananchi wenye imani tofauti za kidini, wa makabila, rangi, na jinsia tofauti. Watanzania wanataka mabadiliko ambayo yataupa uhai mpya Muungano wetu na kuuimarisha uweze kukabiliana na changamoto mpya kwa kuhakikisha haki na usawa kati ya Tanganyika na Zanzibar, na hivyo kuvutia nchi nyengine kujiunga nasi. Watanzania wanataka mabadiliko yatakayowapa dira na mwelekeo mpya utakaolipeleka Taifa katika jamii inayozingatia haki sawa kwa wote na yenye uchumi imara unaotoa ajira na tija kwa wananchi wote. Watanzania wanataka mabadiliko yatakayowapa uongozi makini, thabiti na wenye uzalendo wa kweli kwa Taifa letu. Watanzania wanataka mabadiliko kwa sababu sasa wako tayari kwa mabadiliko.”
Ni CUF tu, na sio chama chengine chochote, kilichoko tayari kuwaongoza Watanzania kuleta mabadiliko hayo, kwa hivyo basi ndani ya picha ya taasisi ya kuleta mabadiliko ndimo ilimo ndoto ya CUF kwa miaka mitano ijayo.
Lakini, bila ya shaka, iliishi miaka zaidi ya mitano kabla ya hiyo mitano ijayo ikiwa na ndoto hiyo hiyo ambayo haikuweza kuitimiza. Kwa nini iweze kuitimiza ndani ya miaka mitano ya sasa? Jibu lipo katika Mkakati wa Chama (SP).

Miaka mitano ijayo, kwa mujibu wa SP kama ilivyohakikiwa Julai 2008, Chama kimejipangia malengo yanayopimika, yanayotekelezeka na yanayofuatilika katika kukipatia ushindi katika uchaguzi wa Serikali za Vitongoji, Vijiji na Mitaa wa 2009, na katika Uchaguzi Mkuu wa 2010. Malengo hayo yatakapotimia, CUF haitakuwa tu Chama imara, bali kitakuwa Chama kitakachoongoza Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Zanzibar.

SURA YA TISA

HITIMISHO

10.1 Hitimisho

Miaka mitano ya kufanya kazi ya siasa katika mazingira kama ya Tanzania si muda mdogo sana. Ni kipindi kirefu na chenye mengi. Ndani ya kipindi hiki, CUF imeendelea kuishi kama taasisi imara ya kisiasa licha ya misukosuko ya hapa na pale ambayo imekuwa ikiikabili. Uvunjwaji wa haki za binaadamu uliopindukia mipaka katika visiwa vya Unguja na Pemba katika zoezi la Uchaguzi Mkuu wa 2005, kwa mfano, ulikuwa na athari kubwa kwa Chama. Viongozi na wananchi waliojeruhiwa na kupatwa na madhara mengine walipaswa kusaidiwa kwa kila hali na Chama kama rikodi za Kurugenzi ya Haki za Binaadamu na Mahusiano ya Umma zinavyoonesha. Matukio mengine yaliwagusa wananchi moja kwa moja na kutishia kuiingiza nchi katika mapambano baina ya dola na raia. CUF ilisimama imara kuona hilo halitokei. Kwa hili CUF imepiga hatua nyingi mbele za kupevuka.

Uvunjwaji huo wa haki za binaadamu ulifanyika pia Tanzania Bara, na bado Chama kikaweza kuwadhibiti wanachama na wafuasi wake dhidi ya hatua yoyote ya kuchukua sheria mkononi mwao. Hiki kimekuwa ni kiwango cha hali ya juu ya kuwajibika kisiasa kwa Chama. Kimekuwa daima kikienda mbele, na kimeapa kutorudi nyuma.

Matukio na matokeo ya kabla, wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2005 kwa pande zote mbili, yaani ule wa Zanzibar na ule wa Muungano, hayakuwa mazuri kwa CUF, lakini iliweza kusimama kama taasisi imara muda wote. Imeendelea kufanya kila linalowezekana kuhakikisha umoja, mshikamano na siasa za ustaarabu zinadumishwa ndani ya Chama na ndani ya nchi. Hata yalipofeli Mazungumzo ya CUF na CCM, CUF iliweza kudhibiti hali ndani ya Chama na miongoni mwa wafuasi. Daima imekuwa ikienda mbele!

Kubuniwa na kuzinduliwa Mpango Mkakati wa Chama (SP) ni katika hatua kubwa mbele ambayo imeweka alama katika uendeshaji wa siasa katika nchi yetu. Hivi sasa, kila kitu kinapaswa kuakisika na matakwa ya SP na hilo linapofanyika, CUF inazidi kusonga mbele.

Maeneo mengine yanayoonesha kuwa CUF inasonga mbele ni:

• Kuanzishwa kwa Jumuiya za Vijana, Wanawake na Wazee
• Kuanzishwa kwa Kitengo cha Utafiti
• Kubadilisha Muundo wa Sekreterieti ya Chama
• Kupunguza ukubwa wa Chama kimuundo
• Kusafisha jina la CUF na kujenga taswira njema ya Chama kwenye jumuiya ya kimataifa na vyombo vya habari
• Kubadilisha uongozi wa ngazi tofauti ndani ya Chama kwa njia ya chaguzi huru na za haki
• Kutanua mtandao wa Chama hadi chini (grass roots)
• Kuwa mbadala wa CCM katika masuala ya kisera na kisiasa
• Kuwavuta vijana wasomi kuunga mkono Chama

10.2 Mapendekezo

Wakati CUF ikisonga mbele hivyo, njia ya kuelekea huko mbele si tambarare kila wakati. Kumekuwepo na mambo kadhaa yanayojitokeza kukwaza na hivyo kuifanya kasi ya mwendo kuwa ndogo na baadhi ya wakati safari kukatikia njiani.

Kama ilivyooneshwa katika Sura ya Nane ya Taarifa hii, matatizo makubwa yanayokikabili Chama yaliyotajwa yanapaswa kuchukuliwa hatua za haraka kurekebishwa. Hayo ni pamoja na:

10.2.1 Ufinyu wa Bajeti ya Chama

Kuendelea kutegemea ruzuku kutoka serikalini kama chanzo kikuu cha mapato ya Chama ni tatizo. Inapendekezwa kwamba Kurugenzi ya Fedha na Uchumi itekeleze ahadi zake za kubuni mipango ya ukusanyaji mapato nje ya ruzuku za serikali. Suala la kuandaa na kusimamia kampeni za uchangishaji fedha na kuwekeza kwa ubia na wafanyabiashara wenye mapenzi na Chama lipewe kipaumbele na Chama.

10.2.2 Ukubwa wa Taswira ya CCM

Udhibiti wa CCM kwa taasisi za kijamii, kidini, habari na vyombo vya dola umewezekana kwa kuwa chama hicho kimeweza kujipenyeza ndani ya taasisi hizo kwa sura tafauti na hasa kupitia nguvu za dola. Bila ya dola, CCM itaporomoka kama chama cha siasa. CCM pia inatunia fedha nyingi katika kudumisha taswira yake huko. Bila ya shaka CUF haiwezi kutumia pesa nyingi, ambazo haina, katika kujenga taswira yake lakini inaweza kutumia mbinu za ushawishi na ushiriki katika taasisi na vyombo hivyo.

Vile vile inapendekezwa kuwa Chama kitumie nguvu yake ndogo ya kifedha na rasilimali watu kiliyo nayo katika kuhakikisha kuwapo kwa vyombo vya habari vinavyomilikiwa na Chama au vinavyokiunga mkono. Inapendekezwa kuwa gazeti la Chama lifufuliwe, mpango wa radio na televisheni uingizwe matendoni haraka iwezekanavyo na huduma ya CUF kwenye mtandao iendelezwe.

10.2.3 Uongozi Usiowajibika

Uongozi usiojali dhamana yake na wala usiowajibika ni mzigo na si msaada kwa Chama. Hatua kali za kinidhamu zinapaswa kuchukuliwa haraka kwa kiongozi wa aina hiyo anapobainika. Viongozi wanaokisaliti Chama na au kuonesha kiwango cha chini ya uwajibikaji, ubadhirifu wa rasilimali za Chama na au utumiaji mbaya wa nafasi zao za uongozi, wawe wanawajibishwa inavyostahili.

Hilo linawezekana ikiwa uwazi utakuwa ndio msingi wa utendaji kazi.

10.2.4 Ufinyu wa Intelligence na Ukosefu wa Utafiti

Kitengo cha Utafiti kiongezewe nguvu za kifedha na watendaji wenye sifa na uwezo. Halikadhalika Kitengo cha Intelligence kijengwe upya, na kiimarishwe kwa kuongezewa uwezo wa kifedha na watendaji wenye uwezo, waaminifu kwa kwa Chama, wenye tabia njema, na wenye uadilifu. Kwa vitengo vyote viwili mafunzo ya mara kwa mara ya kuongeza ujuzi wa watendaji wake na kuelimishwa mbinu mpya za utendaji liwe ni jambo linalopewa umuhimu mkubwa.

Izingatiwe kuwa katika dunia ya leo siasa haziendeshwi kwa kubahatisha au kurukia mambo bila ya utafiti wa kina na uchambuzi wa kisayansi.

MWISHO:

Ni matumaini ya Baraza Kuu la Uongozi la Taifa linalomaliza muda wake kuwa Mkutano Mkuu wa Taifa huu wa Nne utaipokea taarifa hii, kuijadili, na kuipitisha, na kisha kutoa miongozo yake ambayo yatakuwa ni dira ya ujenzi na uimarishaji wa chama chetu kwa miaka mitano ijayo.

HAKI SAWA KWA WOTE

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s