Na Asha Bani
KIONGOZI wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Hamad Rashid Mohamed, amesema watafanya kila liwezekanalo kulinda kura kwa lengo la kulinda nafasi zao katika chaguzi mbalimbali.
Hayo aliyasema jana katika Mkutano Mkuu wa Nne wa Chama cha Wananchi (CUF) ambao unaendelea katika Viwanja vya Diamond Jubilee wakati akiwasilisha taarifa za shughuli za kambi anayoiongoza bungeni na kuongeza kwa sasa wanajipanga vyema ili kuhakikisha kuwa wapinzani wanashinda uchaguzi mkuu ujao.
Alisema kuwa chama chao hakina uwezo wa kifedha wa kuweza kuwapatia ushindi lakini Chama cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi uliopita kimetumia sh bilioni 25 huku wabunge wake kwa wakipata ruzuku ya bilioni 1.3.
Alisema kuwa mbali na kutumia fedha nyingi katika chaguzi mbalimbali lakini pia wanatumia vyombo vya dola katika kuwaangamiza na kuwafanya kushindwa katika nafasi mbalimbali za ngazi ya taifa.
Hamad aliongeza wabunge wa Kambi ya Upinzani Bungeni mara nyingi wamekuwa katika mikakati mbalimbali ya kuhakikisha kuwa serikali inaweza kubadilisha katiba ya nchi ili kuweza kulinda maslahi ya nchi.
Katika mkutano huo, mwenyekiti wa chama hiki anayemaliza muda wake, Profesa Ibrahim Lipumba, alilaumu gazeti moja la kila siku (si Tanzania Daima) kwa kuandika habari iliyopotosha ukweli kuwa CUF ilikialika Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na kukataa kuhudhuria.
Alifafanua kuwa mwaliko ulipelekwa kwa Katibu Mkuu wa CHADEMA, Wilbrod Slaa, na kujibu kuwa hangeweza kufika kwa kuwa alikuwa na udhuru.
Chanzo: freemedia.co.tz