Tanzania inahitaji mabadiliko – Lipumba

Mkutano Mkuu unatazamiwa kupokea agenda mbali mbali zinazowasilishwa kwake na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa, kuzijadili na kisha kuzitolea maamuzi na maelekezo ambayo yanakuwa ndiyo mwongozo wa utendaji wa Chama kwa miaka mitano inayofuata. Mkutano Mkuu huu una agenda kuu nne (4) ambazo zitawasilishwa kwenu. Wajumbe mtapokea Taarifa ya Kazi za Chama kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia 2004 hadi 2009. Taarifa hii inaeleza kwa kina utekelezaji wa majukumu ya Ofisi za Viongozi Wakuu wa Chama pamoja na Kurugenzi za Chama, inafanya tathmini ya utekelezaji huo na kutoa mapendekezo ya hatua za kuchukuliwa katika kuimarisha utendaji wa Chama.

Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Nne wa Taifa

Baadhi ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Nne wa Taifa wakiimba wimbo ya chama.

HOTUBA YA MWENYEKITI WA TAIFA WA THE CIVIC UNITED FRONT (CUF – CHAMA CHA WANANCHI), MHE. PROF. IBRAHIM HARUNA LIPUMBA KWENYE UFUNGUZI WA MKUTANO MKUU WA NNE WA TAIFA WA CHAMA ULIOFANYIKA KATIKA UKUMBI WA DIAMOND JUBILEE, MJINI DAR ES SALAAM, 23 FEBRUARI, 2009

Mheshimiwa Mgeni Rasmi, Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Mheshimiwa John Tendwa,
Mheshimiwa Makamo Mwenyekiti wa CUF,
Mheshimiwa Katibu Mkuu wa CUF,
Mheshimiwa Makamo Mwenyekiti Mstaafu wa CUF, Mzee Shaaban Khamis Mloo,
Waheshimiwa Manaibu Katibu Mkuu wa CUF wa Tanzania Bara na Zanzibar,
Waheshimiwa Wenyeviti, Makatibu Wakuu na Wawakilishi wa Vyama vya Siasa nchini,
Waheshimiwa Mabalozi wanaowakilisha nchi zao hapa Tanzania,
Waheshimiwa Wakuu wa Taasisi na Madhehebu ya Dini mbali mbali wa hapa nchini,
Waheshimiwa Wakuu wa Taasisi mbali mbali za Kijamii na Asasi za Kiraia hapa nchini,
Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la CUF,
Waheshimiwa Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Nne wa Taifa wa CUF,
Waheshimiwa Wageni Waalikwa,
Mabibi na Mabwana,

Awali ya yote napenda kuchukua fursa hii, kwa niaba ya Baraza Kuu la Uongozi la Taifa, kuwakaribisha nyote katika Mkutano Mkuu wa Nne wa Taifa wa Chama Cha Wananchi (CUF) unaofanyika hapa mjini Dar es Salaam. Hatuna budi kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kutujaalia kuweza kukutana hapa leo katika hali ya afya njema na furaha tele. Nawashukuru wajumbe nyote wa Mkutano Mkuu mnaotoka pembe zote za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kufanikisha mahudhurio yenu katika Mkutano Mkuu huu. Kuwepo kwenu hapa ndipo kunakowezesha kufanyika kwa Mkutano Mkuu.

Nawapa pole wajumbe nyote ambao mmesafiri masafa marefu kuweza kuja hapa Dar es Salaam kwa machovu na usumbufu mlioupata wakati wa safari. Kuja kwenu ni kutimiza wajibu na matakwa muhimu ya Katiba yetu na ya kidemokrasia. Nachukua nafasi hii pia, kwa niaba yenu wajumbe wa Mkutano Mkuu, kuwakaribisha wageni wetu waalikwa waliokuja kuungana nasi hapa leo na kushuhudia jinsi wana-CUF tunavyotekeleza demokrasia ndani ya Chama chetu.

Nawakaribisha na kuwashukuru kwa dhati kabisa viongozi wa vyama vya siasa, mabalozi wanaowakilisha nchi zao hapa nchini, wawakilishi wa mashirika ya kimataifa yenye ofisi zao Tanzania, wakuu wa taasisi na madhehebu ya dini mbali mbali, na wakuu wa taasisi mbali mbali za kijamii na vyama visivyo vya kiserikali kwa kuupokea mwaliko wetu na kukubali kwao kuja kushirikiana nasi hapa katika ufunguzi wa Mkutano Mkuu huu.

Nawahakikishia kuwa tunathamini sana imani na ushirikiano wenu kwetu. Naomba pia kuchukua fursa hii kuwashukuru wale wote walioshiriki kwa namna moja au nyingine katika maandalizi ya Mkutano Mkuu huu. Sina haja ya kusema mengi, hali halisi ya huduma tokea wajumbe walipoanza kufika na mandhari ya ukumbi huu yanaonyesha kazi kubwa iliyofanyika. Nafasi ya Mkutano Mkuu wa Taifa Waheshimiwa Wajumbe wa Mkutano Mkuu na Watanzania wenzangu, kama mnavyojua, Mkutano Mkuu wa Taifa ndiyo kikao cha juu kabisa cha Chama Cha Wananchi (CUF).

Mkutano Mkuu unatazamiwa kupokea agenda mbali mbali zinazowasilishwa kwake na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa, kuzijadili na kisha kuzitolea maamuzi na maelekezo ambayo yanakuwa ndiyo mwongozo wa utendaji wa Chama kwa miaka mitano inayofuata. Mkutano Mkuu huu una agenda kuu nne (4) ambazo zitawasilishwa kwenu. Wajumbe mtapokea Taarifa ya Kazi za Chama kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia 2004 hadi 2009. Taarifa hii inaeleza kwa kina utekelezaji wa majukumu ya Ofisi za Viongozi Wakuu wa Chama pamoja na Kurugenzi za Chama, inafanya tathmini ya utekelezaji huo na kutoa mapendekezo ya hatua za kuchukuliwa katika kuimarisha utendaji wa Chama.

Ni matumaini yangu kwamba wajumbe mtaichambua Taarifa hiyo kwa nia ya kujenga na kutoa maelekezo yanayofaa kwa ajili ya kuzingatiwa na uongozi wa Chama kwa siku zinazokuja. Kwa kuwa CUF ndiyo Chama kikuu cha Upinzani hapa nchini kinachounda na kuongoza Serikali vivuli katika Bunge na Baraza la Wawakilishi, Mkutano Mkuu pia utapokea Taarifa ya Kazi za Kambi za Upinzani katika vyombo hivyo viwili. Hizi ni taarifa muhimu zinazoonesha utekelezaji wa majukumu ya CUF katika kuwatumikia Watanzania nje ya Chama. Sina haja ya kueleza kwa undani kazi iliyofanywa na CUF katika vyombo hivyo kwani hayo yana nafasi yake katika Mkutano huu lakini nina haki ya kueleza kwamba Wabunge na Wawakilishi wa CUF chini ya uongozi wa Mheshimiwa Hamad RashidMohamed na Mheshimiwa Abubakar Khamis Bakary wamefanya kazi kubwa ya kuwatetea Watanzania, kazi ambayo inazifanya Serikali za CCM zikose usingizi. Watanzania wanazidi kujenga imani na CUF kutokana na utendaji wa Wabunge na Wawakilishi katika vyombo hivyo vya kutunga sheria. Chama Cha Wananchi (CUF) pia ni Chama kinachokwenda na wakati katika kuangalia mahitaji ya kisiasa, kiuchumi na kijamii ya Watanzania katika wakati husika. Kwa msingi huo, agenda ya tatu ya Mkutano Mkuu huu itakuwa ni kufanya marekebisho ya Katiba ya Chama ya 1992 ili ikidhi mahitaji ya wakati huu ya Watanzania. Mapendekezo yanayoletwa kwenu yanakusudia kuongeza ushiriki wa wanawake katika vyombo vyote vya maamuzi vya Chama kwa angalau asilimia 30, kupanua demokrasia ndani ya Chama kwa kuanzisha utaratibu wa wagombea wa CUF wa nafasi za Ubunge, Uwakilishi, Udiwani na viongozi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji kupigiwa kura za maoni na wanachama katika maeneo yao badala ya wajumbe wa vikao tu, kuanzisha rasmi Jumuiya za Chama za Wanawake, Vijana na Wazee na taratibu zitakazoongoza Jumuiya hizo, na kuimarisha ufanisi na uwajibikaji wa viongozi wa Chama kwa kupanua wigo wa wanachama wanaoweza kushikilia nafasi za utendaji katika Chama. Ni imani yangu kwamba wajumbe mtayazingatia yote haya katika kufanya maamuzi muhimu yatakayoipelekea CUF kujipanga vizuri zaidi katika kuwatumikia Watanzania na kuwaletea mabadiliko ya uongozi wanayoyadai kwa nguvu hivi sasa. Agenda ya mwisho ya Mkutano Mkuu huu itakuwa ni kukamilisha Uchaguzi wa Chama ndani ya Chama kwa kufanya uchaguzi wa ngazi ya taifa unaojumuisha uchaguzi wa Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Katibu Mkuu, wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa wa viti maalum vya wanawake. Hili ni jukumu muhimu sana katika kutekeleza demokrasia ndani ya Chama. Hatuwezi kudai demokrasia katika nchi lakini tukawa hatuitekelezi ndani ya Chama. Kila aliyeomba nafasi ya uongozi katika Chama atapata haki ya kujieleza na kufanya kampeni mbele ya Mkutano Mkuu huu na wajumbe watapata nafasi ya kumhoji. Nachukua nafasi hii kuwaomba wajumbe kwamba tuendeleze utamaduni mwema uliokwisha jengeka ndani ya CUF wa kufanya uchaguzi wa kistaarabu na ulio safi. Tukatae kampeni chafu za aina yoyote ile na tuchague viongozi bora watakaoendeleza kazi ya kukijenga na kukiimarisha Chama hadi kufikia malengo yake ya kushika madaraka ya dola hapa nchini. Kukwama kwa Maendeleo ya Demokrasia Waheshimiwa Wajumbe wa Mkutano Mkuu na Watanzania wenzangu, tumekutana hapa baada ya miaka mitano tokea uongozi wa Chama uliopo ulipochaguliwa katika Mkutano Mkuu wa Tatu uliofanyika Februari 2004. Hiki kimekuwa ni kipindi muhimu sana katika maendeleo ya Chama chetu. Ni muhimu kujitathmini hali imekuwaje katika kipindi hicho. Sote tunaelewa kuwa chama chochote makini cha siasa huwa na lengo la kutaka kupewa ridhaa na wananchi ili kishike madaraka ya kuongoza serikali na kutekeleza sera zake ambazo zitawaletea unafuu au kuondoa kabisa matatizo yanayowakabili na kuwaletea maisha mema na yenye tija na manufaa kwao. Kwa msingi huo, ujenzi wa misingi ya demokrasia katika nchi ni jambo muhimu sana. Kipindi cha miaka mitano iliyopita kimeshuhudia, pamoja na mambo mengine kufanyika kwa uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji mwaka 2004 na pia uchaguzi mkuu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Rais wa Zanzibar, Wabunge, Wawakilishi na Madiwani mwaka 2005. Chaguzi hizi kwa mara nyingine tena zimekuwa kielelezo cha kukwama kwa maendeleo ya demokrasia katika nchi yetu. Uchaguzi wa Serikali za mitaa, vijiji na vitongoji ulivurugwa kutokana na Serikali kuendelea kukataa uchaguzi huo kusimamiwa katika taratibu zinazoeleweka chini ya Tume huru ya uchaguzi. Badala yake watendaji wa Serikali wameendelea kuendesha na kuusimamia uchaguzi huo katika hali inayowanyima wananchi haki yao ya msingi ya kuwa na uchaguzi huru na wa haki na badala yake kuhakikisha CCM inaendelea kutawala hata kama wananchi hawana imani nayo. Inasikitisha katika uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2004, katika mtaa wa Mbagala Kiburugwa, wilaya ya Temeke, mwanafunzi wa shule, Khalid Omar Mfaume aliuawa kwa kupigwa risasi na vyombo vya dola. Risasi iliyomuua Khalid Omar Mfaume haikupigwa na polisi bali ilipigwa na Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke. Hata hivyo polisi hawakumkamata na hawajamkamata aliyeua na mpaka leo hajafikishwa Mahakamani. Ninaisihi serikali kuwa uchaguzi wa mwaka huu wa 2009, uzingatie makubaliano ya wadau vikiwemo vyama vya siasa, serikali na asasi za kiraia yaliyofikiwa katika mkutano uliofanyika Morogoro tarehe 19 Februari 2009 ulioongozwa na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Mheshimiwa John Tendwa. Wadau wote walikubaliana pamoja na mambo mengine kutowahusisha watendaji wa vijiji na kata (VEO na WEO) katika zoezi la kuandaa orodha ya wapiga kura wa uchaguzi wa serikali za mitaa. Vyama vya siasa vilionesha ukomavu wa kisiasa wa hali ya juu katika mkutano wa Morogoro mpaka wadau wote wakafikia muafaka. Ni muhimu sana kwa Serikali kuheshimu makubaliano hayo kama alivyoahidi Mhe. Celina Ompeshi Kombani, Waziri wa Nchi, TAMISEMI wakati akifunga Mkutano wa Wadau Morogoro. Waheshimiwa Wajumbe wa Mkutano Mkuu na Watanzania wenzangu, ukiacha uchaguzi huo wa serikali za mitaa, Uchaguzi Mkuu wa 2005 nao uliendelea kutawaliwa na vituko vile vile. Umeendelea kufanyika katika mazingira ya Katiba ya mfumo wa chama kimoja iliyotungwa mwaka 1977, umeendelea kufanyika chini ya Sheria ya Uchaguzi iliyotungwa kukidhi matakwa ya mfumo wa chama kimoja, umeendelea kusimamiwa na kuendeshwa na Tume ya Uchaguzi ya Taifa ambayo imepoteza imani ya Watanzania na hasa imani yetu vyama vya siasa vya upinzani. Matokeo yake yamekuwa yale yale ya CCM kufanya wizi mtupu wa kishindo wa kura. Mkakati maalum ulipangwa kuhakikisha kuwa CUF haipati hata kiti kimoja cha ubunge cha kuchaguliwa upande wa Tanzania Bara licha ya kupata asilimia 14 ya kura zote za wagombea ubunge hapa nchini. Mpango uliobuniwa ulikuwa ni kulazimisha Watanzania wa Bara waione CUF kuwa ni chama cha Kizanzibari na hivyo waache kukiunga mkono. Hata hivyo, hali halisi imeendelea kuonesha kuwa CUF ndiyo tegemeo pekee la ukombozi wa kweli wa Watanzania wote, Bara na Zanzibar. Kwa upande wa Zanzibar, hali ya kuvuruga chaguzi iliendelea mwaka 2005 kama ilivyokuwa kwa 1995 na 2000. CUF ilishinda uchaguzi wa Rais wa Zanzibar na Wawakilishi lakini hila, mbinu na nguvu zilitumika kuizuia isitangaziwe ushindi ambao Wazanzibari wamekuwa wakiipa CUF kwa mara tatu mfululizo. Ni bahati mbaya kwamba Rais Jakaya Kikwete ameshindwa hata kutimiza ahadi yake ya kuyasimamia na kuyaongoza mazungumzo ya Muafaka baada ya kuvurugwa kwa uchaguzi huo ili kupata ufumbuzi wa kudumu wa mpasuko wa kisiasa Zanzibar. Kikao alichokiongoza yeye cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM ndicho kilichoupiga teke Muafaka na yeye kushindwa kuchukua hatua zozote za kuunusuru tokea wakati huo, mwezi Maachi 2008 hadi sasa, ikiwa ni karibu mwaka mzima. Lakini uchafuzi huo wote wa CCM haujairejesha nyuma azma ya CUF katika kufikia malengo yake ya kuwakomboa Watanzania. Kuhusu Muafaka, CUF tumeweka wazi msimamo wetu ambao pia tuliurejea mbele ya Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Mheshimiwa Kamalesh Sharma, nilipokutana naye alipotembelea Ofisi Kuu ya CUF tarehe 20 Februari, 2009 kwamba hatutakubali kubariki usanii wa CCM na Rais Kikwete wa eti kuitisha uchaguzi mwingine kwa njia ya kura ya maoni kwa lengo la kutibu matatizo yaliyotokana na uchaguzi kutokuwa huru na wa haki. Na kupitia mkutano huu, nataka nirejee tena kwamba CUF haitokubali kuanzisha mazungumzo mapya yenye lengo la kupoteza muda na kuwahadaa Watanzania. Ikiwa Rais Kikwete ana lengo la kweli la kuona Muafaka unafikiwa na kusainiwa, basi awakutanishe viongozi wakuu wa pande mbili zinazovutana Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad wa CUF na Mheshimiwa Amani Karume wa CCM, ili wafunge makubaliano hayo na kuweka utaratibu wa kuyatekeleza. Waheshimiwa Wajumbe wa Mkutano Mkuu, ni imani ya Watanzania walio wengi kwamba ukuaji wa demokrasia hauwezi kufikiwa katika mfumo wa katiba uliopo sasa ambao umerithiwa kutoka enzi za chama kimoja chini ya dhana ya Chama kushika hatamu. Watanzania wanaona umefika wakati tupate Katiba mpya ya kidemokrasia itakayokidhi mahitaji ya mfumo wa vyama vingi vya siasa na pia ujenzi wa demokrasia pana na shirikishi. Kwa kutambua haja hiyo, CUF imeendelea kuchukua nafasi yake kama Chama Mbadala na Chama kiongozi katika kuleta mageuzi ya kisiasa, kiuchumi, na kijamii hapa nchini kwa kuanzisha, kuendeleza na kuongoza harakati za Watanzania kuandika Katiba mpya ya kidemokrasia kwa Tanzania. Wiki iliyopita tu, nimeongoza kongamano lililopitia rasimu ya awali ya Katiba mpya ambayo baada ya mchakato wa kuiweka vyema kukamilika, tutaipeleka Serikalini na pia kuisambaza kwa wadau wengine wote ili kujenga mtandao imara wa kuongoza mapambano ya kuhakikisha kuwa malengo hayo ya kupata Katiba mpya yanafikiwa. Tunawapa ujumbe watawala wa CCM ambao siku zote wameyakataa madai ya Katiba mpya kujiandaa maana sasa Watanzania wameamka na hawatakubali tena kuburuzwa. Katiba mpya inayopendekezwa inaweka misingi imara ya kidemokrasia kwa kuimarisha misingi ya utenganishaji wa madaraka baina ya mihimili mikuu mitatu ya Dola yaani Utawala, Bunge na Mahakama, kupunguza madaraka makubwa aliyopewa Rais, kuimarisha madaraka ya Bunge katika kutekeleza wajibu wake wa kuisimamia Serikali, kuongeza uhuru wa Mahakama ili zisiweze kuingiliwa katika utoaji haki, kuifanya Tume ya Uchaguzi iwe Tume huru yenye muundo wake unaojitegemea, kuimarisha misingi ya haki za binadamu na uhuru wa mtu, kuimarisha uhuru wa habari, kuingiza vifungu vinavyoanzisha, kufafanua na kutafsiri Maadili ya Taifa na kujenga Muungano imara chini ya mfumo wa Shirikisho la Serikali tatu. Haya ni baadhi tu ya mambo muhimu yanayozingatiwa katika rasimu hiyo ya awali ambayo itaendelea kujadiliwa na wadau na kuzidi kupatiwa michango itakayoifanya iwe Katiba bora kwa mahitaji ya Tanzania ya sasa na ya siku zijazo. Kushindwa Uongozi kwa CCM Waheshimiwa Wajumbe wa Mkutano Mkuu na Watanzania wenzangu, tunakutana hapa ikiwa tumeingia mwaka wa nne tokea kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa nchi ambao uliirudisha madarakani CCM kupitia Serikali ya Awamu ya Nne inayoongozwa na Rais Jakaya Kikwete. Wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa 2005, Chama Cha Mapinduzi (CCM) na mgombea wake wa Urais waliahidi kuwa ikiwa watachaguliwa na kuunda Serikali ya Awamu ya Nne watahakikisha kutakuwa na Maisha bora kwa kila Mtanzania. Mimi niliwatahadharisha Watanzania kwamba CCM ni chama kilichochoka, na hata kama kingetoa Rais mwenye uwezo mkubwa, Rais huyo angeshindwa kuwaletea Watanzania mabadiliko ya maana. Nilieleza kuwa nchi yetu inahitaji kuongozwa na chama makini kitakachowahamasisha na kuwawezesha Watanzania wawe wabunifu na kujenga uchumi wenye manufaa kwa wananchi wote. Wengi walidhani kuwa labda niliyasema hayo kwa sababu nilikuwa mgombea ninayetoka upinzani na hivyo nisingetegemewa kukisifia chama hicho. Nilieleza pia kuwa taifa letu linakabiliwa na ongezeko la rushwa na ufisadi kwa ari mpya, nguvu mpya na kasi mpya. Sikuwa natania. Hali halisi ya mwananchi wa kawaida inaonesha wazi kuwa badala ya maisha bora kwa kila Mtanzania kuna maisha magumu zaidi kwa kila Mtanzania wa kawaida. Kwa hakika, mwaka wa nne sasa tokea Rais Kikwete aingie madarakani, ni wazi kwamba Taifa limekabiliwa na ukosefu wa uongozi kutokana na CCM kushindwa kuongoza. Maeneo tisa yanadhihirisha jinsi CCM ilivyoshindwa kuongoza na kuwafanya Watanzania wasijue wanakopelekwa. Maeneo hayo ni pamoja na kupanda kwa kasi ya kutisha kwa gharama za maisha, kuongezeka kwa ufisadi, kuyumba kwa uchumi, migomo ya wafanyakazi, migomo ya wanafunzi, kuongezeka kwa nyufa katika Muungano, kuibuka kwa mpasuko wa kidini, kuporomoka kwa maadili ya Taifa, na kushindwa kuumaliza mpasuko wa kisiasa Zanzibar. Lakini ni bahati mbaya kwamba achilia mbali kuyatafutia ufumbuzi matatizo haya ambayo yakiachiwa yanaweza hata kuhatarisha usalama wa Taifa, Rais Kikwete anaonekana kufanya usanii wa kutoyaona. Katika hotuba aliyoitoa Bungeni tarehe 21 Agosti 2008, Rais Kikwete alieleza kuwa mambo ni mazuri katika nchi, kwamba uchumi unakua, ajira zinaongezeka na ahadi alizozitoa kwa Watanzania amezitekeleza na anaendelea kuzitekekeza. Suala la kujiuliza mwaka huu wa nne tangu Rais Kikwete kuingia madarakani ni kama kweli kuna maisha bora kwa kila Mtanzania au angalau matumaini ya kuelekea huko? Watanzania wenzangu, mnaelewa fika hali ngumu ya maisha na kutopatikana kwa ajira. Desemba 2005, wakati Rais Kikwete anaingia madarakani, kwa wakazi wa Dar es Salaam, bei ya kilo ya unga wa sembe ilikuwa shilingi 250/- hivi sasa ni shilingi 800/-; bei ya kilo ya mchele ilikuwa shilingi 500/- hivi sasa ni shilingi 1300/-; bei ya kilo ya maharage ilikuwa shilingi 400/- hivi sasa ni shilingi 1200/; bei ya kilo ya sukari ilikuwa shilingi 600/- hivi sasa ni shilingi 1300/. Mafuta ya kula, ndoo ya lita 20 ilikuwa shilingi 10,500/- hivi sasa ni shilingi 43,000/-. Nazi moja ilikuwa shilingi 100/- hivi sasa ni shilingi 350/-. Gunia moja la mkaa lilikuwa shilingi 3,500/- hivi sasa ni shilingi 24,000/-. Nyama, kuku na samaki havishikiki. Hata dagaa wamekuwa kitoweo cha anasa ambapo kilo moja ya dagaa wa Kigoma sasa inauzwa shilingi 8,000/- ukilinganisha na shilingi 3,000/- wakati Rais Kikwete anaingia madarakani mwezi Desemba, 2005. Wananchi wa Kanda ya Ziwa wanaambulia kula mapanki – mifupa ya samaki iliyobakia baada ya minofu ya samaki kukatwa na kusafirishwa Ulaya. Hata mapanki yamepanda bei! Haya ndiyo matokeo ya uongozi wa Rais Kikwete wa kuleta Maisha bora kwa kila Mtanzania. Alau angetupa pole Watanzania kwa maisha magumu; badala yake anatukejeli na kutueleza mambo ni mazuri, uchumi unakua, na ajira zinaongezeka. Athari ya kupanda sana bei ya vyakula ni mbaya zaidi kwa kina mama wajawazito na watoto wachanga. Mama mjamzito akikosa lishe bora atajifungua mtoto mwenye utapiamlo na asiye na afya njema. Watoto wachanga wasipokuwa na lishe bora wanaathirika sana katika maisha yao yote ya baadaye kwa sababu hawajengi vizuri miili yao, kinga ya mwili na ubongo. Mtoto mchanga asiyepata lishe bora na virutubisho vya mwili hukua akiwa na uwezo mdogo wa kujifunza na kufundishika. Ni ukatili mkubwa kwa watoto kwa jamii kushindwa kuweka utaratibu wa kuhakikisha kuwa kina mama wajawazito na watoto wachanga wanapata lishe bora. Upatikanaji wa huduma za afya unaendelea kuwa kitendawili kwa Watanzania wengi. Wananchi walihuzunishwa sana na kifo cha mama mjamzito aliyenyimwa huduma za kujifungua katika hospitali ya Mwananyamala kwa kutokuwa na vifaa vya kujifungulia wala fedha za kuvinunulia. Kina mama wajawazito wanaojifungua katika hali ngumu na bila msaada wa mkunga aliyehitimu ni wengi mno. Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa vifo vya kina mama wajawazito. Ukosefu wa uongozi umesababisha kushindwa kutumia elimu na utaalamu unaoeleweka kuhakisha kina mama wa Tanzania wanapata huduma bora za kujifungua. Kina mama wengi wanaojifungua katika hospitali na zahanati za serikali, huduma ni mbovu, kejeli na matusi ni mengi. Watanzania wenzangu, serikali isiyomjali na kumheshimu mama mjamzito, haiwezi kumheshimu na kumjali raia wa kawaida kwani sisi sote tumezaliwa na kina mama. Maradhi kama vile malaria, safura na maradhi mengine ya minyoo, kipindupindu na kichocho yanaweza kuzuiwa na wanaougua kutibiwa. Tunahitaji kuwa na mtandao mzuri wa zahanati na vituo vya afya na upatikanaji wa madawa ya uhakika ya kutibu maradhi haya. Waheshimiwa Wajumbe wa Mkutano Mkuu na Watanzania wenzangu, kushindwa uongozi kwa CCM na Rais Kikwete pia kunadhihirika katika mapambano dhidi ya ufisadi. Ufisadi ni matumizi ya dhamana na wadhifa uliopewa na umma kwa manufaa yako binafsi. Inajumuisha kudai na kupokea rushwa, matumizi mabaya ya fedha na rasilimali za umma na kuiba fedha za umma. Rushwa ni adui wa haki, na pia ni adui mkubwa wa maendeleo. Rushwa ni saratani (cancer) inayoua uchumi na kuwanyima wananchi haki ya maisha mazuri na maendeleo. Chanzo kikubwa cha rushwa ni ukiritimba wa madaraka, mishahara midogo ya watendaji serikalini, maamuzi yasiyofuata taratibu zinazoeleweka na kutowajibishwa kwa wanaoshiriki katika vitendo vya rushwa. Vita dhidi ya rushwa itafanikiwa ikiwa ukiritimba wa madaraka utaondolewa, maamuzi ya kiserikali yatafuata taratibu zilizo wazi na zinazoeleweka na kuwaadabisha wanaoshiriki katika rushwa. Mfumo wa rushwa unapunguza uwekezaji wa vitega uchumi ulio makini na kwa hiyo kupunguza ongezeko la ajira na ukuaji wa uchumi. Kwa wawekezaji makini rushwa ni mbaya kuliko kodi kubwa kwa sababu haitabiriki na mtoaji hana uhakika kuwa aliyepokea atatimiza ahadi ya kutoa huduma iliyolipiwa rushwa. Kukithiri kwa rushwa kunaathiri utumiaji mzuri wa vipaji vya ujasiriamali. Wafanyabiashara wenye vipaji vizuri wanatumia uwezo wao kupata utajiri kwa njia rahisi za rushwa badala ya kuwa wavumbuzi wa njia bora za kuongeza uzalishaji, tija na faida katika shughuli halali za kiuchumi. Rushwa inapunguza uwezo wa misaada kutoka nje kusaidia kukuza uchumi na kupunguza umaskini badala yake inachochea nchi na serikali kuwa tegemezi milele. Kwa sababu ya rushwa mikopo na misaada ya nje haijengi miundombinu imara kama vile barabara, ufuaji na ugavi wa umeme, huduma za maji, afya na elimu. Rushwa inafanya gharama za miradi kuwa kubwa mno. Rushwa inasababisha nchi iwe na miundombinu na huduma hafifu. Rushwa inahatarisha afya na maisha ya wananchi. Madawa hafifu au yaliyopitwa na wakati yanaingia nchini na kutumiwa na raia. Vifaa vibovu kama vile nyaya za umeme zinaingizwa nchini na kusababisha ajali zinazoweza kuunguza nyumba na kupoteza maisha ya watu. Maghorofa na madaraja yanajengwa bila kuzingatia viwango. Rushwa inapunguza mapato ya serikali. Wafanyabiashara na makampuni yanatumia rushwa kukwepa kodi na kuipunguzia uwezo serikali kutoa huduma muhimu kwa wananchi kama vile elimu na afya. Rushwa ndani ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa serikali inachangia kuwepo kwa mikataba mibovu katika sekta mbali mbali ikiwemo madini inayoihujumu serikali. Mikataba inaandaliwa kwa makusudi iwe na gharama kubwa kwa serikali kama itaitekeleza na gharama kubwa zaidi ikiwa itaivunja. Upande wa pili ukivunja mkataba haupati gharama kubwa. Rushwa inaendeleza matumizi mabaya ya fedha za umma. Miradi mikubwa yenye mianya ya rushwa inapendelewa zaidi kuliko matumizi yatakayochochea maendeleo ya watu. Uongozi wa Benki Kuu ulichangamkia sana ujenzi wa minara pacha (twin towers) kwa gharama kubwa bila shaka kwa sababu ya rushwa. Inawezekana kuwa robo ya gharama ya majengo hayo ingeweza kukidhi makao makuu yenye taratibu zote za kiulinzi wa Benki Kuu. Serikali ingeweza kutumia robo tatu iliyobaki kuanzisha kama mtaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo na Benki ya Maendeleo ya Viwanda. Athari mbaya zaidi ya rushwa ni mmomonyoko wa maadili ndani ya serikali na katika jamii. Kuwepo kwa rushwa miongoni mwa viongozi waandamizi wa serikali kunaathiri uadilifu kwa watendaji wote wa serikali. Kama Mwanasheria Mkuu wa Serikali amejitajirisha kwa rushwa, kwa nini Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya naye asitafute mbinu za kujitajirisha hata kama rushwa hiyo itaongeza gharama za kupambana na UKIMWI? Kama wakubwa wanakula basi wadogo watataka alau walambe. Mwanasheria Mkuu mmoja wa Serikali inasemekana alitoa agizo lisilo rasmi kwa maafisa wake kuwa kila mtu ale kwenye meza yake mwenyewe. Saratani ya rushwa inaathiri mfumo mzima wa serikali. Najua kwamba hivi sasa kumekuwepo na hisia kwamba Serikali ya Rais Kikwete iko makini katika kupambana na ufisadi kutokana na kesi dhidi ya watuhumiwa wa ufisadi zilizofikishwa Mahakamani. Mimi binafsi siamini kwamba kesi hizo zitafika popote. Naziona kama ni mchezo mchafu wa kisiasa wenye lengo la kuwahadaa Watanzania na jumuiya ya kimataifa waone hatua zinachukuliwa lakini baadaye kusitokee jambo lolote la maana. Inawezekana kabisa zina malengo ya kuifanya Serikali ya CCM ionekane inapambana na ufisadi na hivyo kutumiwa kama kete ya kuombea kura katika uchaguzi mkuu wa mwakani lakini baada ya hapo zife kidogo kidogo. Mfano mzuri wa haya ninayoyaeleza ni kupeleka kesi Mahakamani dhidi ya Sailesh Vithlani ya kupokea rushwa ya dola za Marekani milioni 12 (shilingi bilioni 15.6) kutoka kampuni ya BAE ili Tanzania inunue rada ya bei mbaya ya dola milioni 40 (shilingi bilioni 52.0) badala ya rada ya dola milioni 5 (shilingi bilioni 6.5) wakati mtuhumiwa ameshafanyiwa mipango na kuondoka nchini. Sakata lililojaa utatanishi la dhamana dhidi ya mtuhumiwa Amatus Liyumba lilioibuka wiki iliyopita tu ni mfano mwingine unaoonesha kuna mchezo unachezwa katika kesi hizi zinazoitwa za ufisadi. Waheshimiwa Wajumbe wa Mkutano Mkuu na Watanzania wenzangu, eneo jengine linaloonesha kushindwa uongozi kwa Rais Kikwete na chama chake cha CCM ni kuyumba kwa uchumi. Hadi sasa nchi yetu inategemea zaidi ya asilimia 30 ya bajeti yake kutoka kwa wafadhili. Miaka minne ya utawala wa Rais Kikwete imeshindwa kuchukua hatua zozote za kupunguza utegemezi huu. Rasilimali zilizopo nchini zikitumiwa vizuri na kwa maslahi ya Watanzania zinatosha kabisa kuifanya Tanzania iwe na uchumi imara usiohitaji kutembeleza bakuli la omba omba kila mwaka. Hivi sasa Serikali inapaswa kuwa inatekeleza Mpango wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini Tanzania – MKUKUTA. Madhumuni makubwa ya MKUKUTA yamejikita katika kufanikisha malengo makuu matatu:- Kukuza uchumi na kupunguza umaskini wa kipato Kuimarisha ubora wa maisha na ustawi wa jamii Kuimarisha Utawala bora na uwajibikaji Katika hotuba za Rais anapozungumzia uchumi, huwa hataji kabisa wala kufanya marejeo kwa MKUKUTA kama vile hana taarifa kuwa huu ndio mpango unaopaswa kuiongoza serikali katika utekelezaji wa sera zake za uchumi. Rais alieleza juhudi zake za kutafuta misaada na akasisitiza mbinu anazotumia za kuwasifu wenye fedha ili watoe ahadi za misaada kwa maeneo wanayotaka kusaidia. Maelezo yake yalikuwa kinyume na Mkakati wa Pamoja wa Misaada Tanzania (MPAMITA) ambao unastahiki kuwa mkakati wa serikali wa muda wa kati wa kusimamia misaada ya maendeleo ya wahisani isaidie utekelezaji wa sera na mipango ya serikali ili malengo ya taifa ya kukuza uchumi na kupunguza umaskini yafanikiwe. Rais Kikwete anaonyesha haielewi mipango rasmi ya Serikali yake ikiwa ni pamoja na MKUKUTA, MPAMITA na MKURABITA. Rais hatulii ofisini akasoma na kutafakari. Kila wakati yuko safarini. Wakati mwingine wananchi wanapata hisia kuwa anasafiri kukwepa majukumu. Watanzania wenzangu, migomo ya wafanyakazi ni eneo jingine ambalo linadhihirisha kushindwa kwa uongozi kwa CCM. Mwaka uliopita umeshuhudia kuongezeka kwa migomo ya wafanyakazi. Migomo ya walimu, wafanyakazi wa benki ya NMB, wafanyakazi wa Shirika la Reli, wafanyakai wa viwanda katika sekta binafsi ililitikisa Taifa. Matatizo yaliyopelekea migomo hiyo ikiwemo malimbikizo ya madeni ya malipo na stahiki zao na malipo duni ya mishahara na mazingira mabaya wanayofanyia kazi yangali yapo na hayajatafutiwa ufumbuzi. Hatua za zimamoto zilizochukuliwa haziwezi kuzuia kuibuka kwa migomo kama hiyo kwa siku za mbele. Migomo ya wanafunzi iliyotokana na kupinga kwao mfumo wa utoaji mikopo ya elimu ya juu nayo ilitawala nchi nzima katika vyuo vya elimu ya juu vya umma na vile vya binafsi. Viongozi waliopo madarakani ambao walisomeshwa bure kwa jasho la wananchi masikini wa nchi hii leo wanakataa watoto wa kimasikini wasipate mikopo kwa asilimia 100 ya kuwawezesha kufikia pale walipofikia wao. Badala ya kuchukua hatua za mazungumzo na viongozi wa wanafunzi hawa ili kupata ufumbuzi, Serikali inawapiga mabomu ya machozi, inawakamata na kuwafungulia mashtaka wanafunzi na wengine inawafukuza vyuoni. Viongozi wa CCM wanakipotezea kizazi hiki mustakbali wao kwa kushindwa kuwajibika katika uongozi. Ukiacha ya migomo, hata umoja wa kitaifa umekuwa majaribuni. Kuwepo na kuonekana kuwa kuna utawala wa sheria unaotoa haki kwa wananchi wote ndio msingi imara wa kujenga na kuendeleza umoja wa kitaifa. Wimbi la demokrasia duniani kote na maendeleo ya teknolojia na utandawazi yameongeza changamoto za umuhimu wa uadilifu katika uongozi. Katika miaka ya nyuma dola ilikuwa na uwezo wa kuchuja na kuzuia habari zinazowafikia wananchi. Kwa kutumia propaganda ilikuwa rahisi alau kwa muda, kujenga hisia za kuwepo umoja wa kitaifa hata kama ulikuwa ni wa bandia na haukusimama juu ya msingi wa haki. Muongo wa mwisho wa karne ya 20 na hasa karne ya 21 umeshuhudia kuwepo kwa mapinduzi makubwa ya kupeana habari hata katika nchi maskini kama Tanzania. Umuhimu wa kuwepo na kuonekana kuwa upo utawala wa sheria unaotoa haki umeongezeka na ndio msingi pekee na uhakika unaoweza kujenga na kuendeleza umoja wa kitaifa. Hivi sasa katika nchi yetu kuna mmomonyoko wa umoja wa kitaifa. Ndani ya Chama tawala na hata baadhi ya vyama vya upinzani siasa za vikundi na za kikanda zimejikita. Mwandishi wa habari mahiri ambaye ni kada wa CCM ameeleza masikitiko yake ya kusambaratika kwa CCM. Anasikitishwa kuona kuwa CCM ya Katibu Mkuu Yusuf Makamba siyo CCM ya Anna Kilango Malecela. CCM ya Rais Jakaya Kikwete siyo CCM ya Spika Samuel Sitta. Hivi sasa mwaka 2009, makundi ya CCM yanawekeana mikwara na kukashifiana kwa lengo la kujenga kundi litakaloweka Mgombea wa Urais kwa tiketi ya CCM mwaka 2015. Hawapambani kwa hoja ya kwa nini Watanzania wenye ulemavu wa ngozi (albino) wanaendelea kuuawa na kunyofolewa viungo bila wahusika kukamatwa, kufikishwa Mahakamani na kuhukumiwa. Makundi ya CCM hayajiulizi kwa nini Watanzania milioni 12.9 ni maskini wa kutupwa mwaka 2007 ukilinganisha na Watanzania milioni 11.4 mwaka 2001. Ongezeko hilo la watu 1,500,000 kati dimbwi la umasikini kati ya 2001 na 2007 pamoja na serikali kudai kuwa uchumi unakua kwa wastani wa asilimia 7 kila mwaka haliyashughulishi makundi ya CCM. Mapande ya CCM hayajiulizi kwa nini vifo vya kina mama waja wazito vinazidi kuongezeka katika nchi yetu. Hatari zaidi kwa umoja wa kitaifa ni kwamba mpasuko wa kidini unainyemelea Tanzania. Ilani ya Uchaguzi ya CCM iliwaahidi Waislamu kuwa CCM ikichaguliwa itaanzisha Mahakama ya Kadhi. Na kwa kuwa kampeni za CCM zilifanikiwa sana kiasi cha baadhi ya viongozi wa madhehebu ya Kikristo kunukuliwa wakisema kwamba Jakaya Kikwete, mgombea wa CCM ni chaguo la Mungu, iliaminiwa na Watanzania wengi kuwa Ilani ya CCM imepewa baraka ya Kanisa. Hata hivyo mjadala ndani ya Bunge wa kuanzisha Mahakama ya Kadhi umejikita katika misingi ya dini. Wabunge walio Waislamu wanaunga mkono na wabunge walio Wakristo wanapinga. Kumbe hoja ya kuanzisha Mahakama ya Kadhi iliwekwa ili kugusa na kuwavutia Waislamu wakati wa kupiga kura bila kuwa na nia thabiti ya kuitekeleza. Matokeo yake Ilani ya CCM inakuwa chanzo cha kuchochea mpasuko wa kidini ndani ya jamii. Waheshimiwa Wajumbe wa Mkutano Mkuu na Watanzania wenzangu, wengi tulipewa matumaini na hotuba ya Rais Kikwete ya tarehe 30 Desemba 2005 kuwa ana nia ya kuutafutia ufumbuzi wa kudumu mpasuko wa kisiasa wa Zanzibar. Mazungumzo kati ya CCM na CUF yaliyochukua miezi 14 yalikamilika mpaka kufikia hatua ya kuandikwa rasimu ya makubaliano. Kumbe wakati wote wa mazungumzo na ahadi zake kwa Watanzania na viongozi wa kimataifa Rais Kikwete alikuwa hana nia thabiti ya kuupatia ufumbuzi wa kudumu mpasuko wa kisiasa Zanzibar. Alikuwa anapoteza muda kwa kuwapa matumaini feki Wazanzibari na Watanzania. Kauli zake alizozitoa wakati akifanya ziara visiwani Zanzibar zimeongeza mpasuko na kuweka petroli kwenye moto unaowaka. Ameeleza wazi wazi kuwa chini ya utawala wake, wapinzani wa CCM itawachukua muda mrefu kuongoza Zanzibar na wanaweza wasiipate fursa hiyo kabisa katika uhai wao wote. Ameeleza pia kuwa kwa kutumia kisingizio cha kulinda Mapinduzi, Serikali yake haitoruhusu wapinzani kuongoza Zanzibar. Hizi ni kauli hatari kutolewa na Mkuu wa Nchi na Amiri Jeshi Mkuu wa majeshi ya ulinzi na usalama. Rais Kikwete alipata nafasi adimu ya kuwaunganisha Wazanzibari wayaone matunda ya kisiasa ya kuwa na Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, matunda ambayo yangewawezesha Wazanzibari kujenga misingi imara ya demokrasia na kujipatia maendeleo ya kiuchumi na kijamii kama nchi ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Badala ya kujenga Zanzibar yenye maelewano na inayoelekea kwenye demokrasia ya kweli, udhaifu wa uongozi wake umeibua mjadala usiokuwa na tija wa Zanzibar ni nchi au siyo nchi wakati inafahamika kwamba Tanzania ni muungano wa nchi mbili, Tanganyika na Zanzibar, zilizounda mamlaka ya pamoja inayotambuliwa kimataifa. Waheshimiwa Wajumbe wa Mkutano Mkuu na Watanzania wenzangu, eneo la mwisho ninalotaka kulizungumzia linalodhihirisha kushindwa uongozi kwa CCM lakini ambalo ni muhimu sana ni lile la kuporomoka kwa maadili ya Taifa. Taifa limepoteza mwelekeo kutokana na kukosa dira imara ya uongozi. Siasa na maisha yetu vinaongozwa na kutawaliwa na chuki, wivu, kupikiana majungu, kuchafuana na kulipizana visasi kwa kukomoana. Kuporomoka kwa maadili ya Taifa kumewafikisha Watanzania kuwaua na kuwanyofoa viungo vya miili yao ndugu zetu wenye ulemavu wa ngozi (albino) kwa imani potofu kwamba viungo hivyo vinaweza kuwapa utajiri na vyeo. Badala ya kufanya kazi kwa bidii, juhudi, maarifa na kujituma, tunakimbilia ushirikina. Matokeo ya haya yote ni kwamba Taifa linayumba. Hali hii inatisha na ni wazi kwamba CCM ikiendelea kutawala itaifikisha nchi yetu kule ambako zilitumbukia nchi nyingine za Kiafrika. Hatupaswi kujidanganya kwamba Tanzania ni tofauti. Njia pekee ya kuzuia wimbi hili la kushindwa uongozi kwa CCM na athari zilizotokana na kushindwa huko ni kuiondoa CCM madarakani. CCM imechoka Waheshimiwa Wajumbe wa Mkutano Mkuu na Watanzania wenzangu, katika Kongamano lililoandaliwa na CUF mwezi Agosti 2008 kuzungumzia ukosefu wa uongozi na hatima ya Tanzania nilisema, na nadhani Mkutano Mkuu huu ni mahala muafaka kurejea na kusisitiza, kwamba baada ya miaka 48 ya utawala wa CCM na watangulizi wake, ni wazi kuwa CCM imechoka na imechakaa na haina tena mawazo mapya ya kukabiliana na changamoto mpya zinazohitajika kututoa katika umaskini wa kutupwa na kutupeleka katika maendeleo na ustawi. CCM imechoka, ndiyo maana imeshindwa kuwaongoza Watanzania kutumia neema ya utajiri wa rasilimali tulizo nazo na kuwatoa katika dimbwi la umaskini linalowazonga. CCM imechoka, ndiyo maana inaendelea kuwalisha Watanzania takwimu za kukua kwa uchumi huku wananchi walio wengi wakiendelea kuishi bila hata ya kumiliki mlo mmoja ulotimia kwa siku. CCM imechoka, ndiyo maana imekuja na sera zinazopalilia tofauti kubwa ya kipato kati ya tabaka la matajiri wachache na tabaka la walalahoi wengi. CCM imechoka, ndiyo maana inaimba wimbo wa kupambana na ufisadi huku ikiendelea kuwakumbatia mafisadi. CCM imechoka, ndiyo maana imefikia mahala imesababisha kugawanyika kwa Taifa katika misingi ya kidini. CCM imechoka, ndiyo maana imeshindwa hata kukabiliana na changamoto za kuuimarisha Muungano wetu kwa misingi ya haki na usawa kati ya Tanganyika na Zanzibar. CCM imechoka, ndiyo maana imepoteza dira na mwelekeo ikilipeleka Taifa kusikojulikana. CCM imechoka, ndiyo maana hata yenyewe imegawanyika katika makundi yanayopigana vita na kuumbuana. CCM imechoka, hadi sasa imewachosha Watanzania na Watanzania wameichoka CCM. CCM imechoka, ndiyo maana sasa Watanzania tunapaswa kuipumzisha. Watanzania tunawajibika kujipanga kuleta mabadiliko. Tusipojipanga vizuri na kuwang’oa mafisadi wa CCM, umaskini utaongezeka na nchi inaweza kusambaratika. Lakini agenda ya mabadiliko katika nchi kama Tanzania ambayo watawala wake wamejipenyeza katika kila sekta ya maisha ya wananchi haiwezi kuwa ni jukumu la wanasiasa pekee. Viongozi wa kisiasa wa vyama vinavyoamini katika mageuzi ya kweli tumejitolea kuongoza harakati za kuleta mabadiliko haya. Wengine harakati hizi zimetugharimu sana lakini hatulijutii hilo. Tunaona fahari kwamba tumeweza kujitolea kwa ajili ya kuwaletea mabadiliko Watanzania. Imetuchukua muda mrefu kwa wananchi kuweza kuamini mabadiliko yanawezekana hapa nchini. Lakini sasa Watanzania wameanza kuamka na kuunga mkono kwa nguvu haja ya kuleta mabadiliko. Watanzania wanataka mabadiliko yatakayowapa uongozi wa namna bora ya kutumia neema ya utajiri wa rasilimali tulizo nazo ili kuwatoa katika dimbwi la umaskini linalowazonga na kuwalekeza katika maendeleo na ustawi kwa wote. Watanzania wanataka mabadiliko yatakayomhakikishia kila Mtanzania anamiliki alau milo mitatu ilotimia kwa siku. Watanzania wanataka mabadiliko yatakayomhakikishia kila Mtanzania anaongeza kipato chake kupitia kazi halali na jasho lake na kumhakikishia kwamba gharama za maisha hazipandi kiholela. Watanzania wanataka mabadiliko ili wawekeze kwenye afya ya watoto wao toka wakiwa katika mimba za mama zao kwa kuhakikisha kina mama waja wazito na watoto wachanga wanapata lishe bora. Watanzania wanataka mabadiliko yatakayowapa huduma za msingi za afya zilizo bora, na kuwahakikishia watoto wao wanapata elimu bora ya msingi na sekondari. Watanzania wanataka mabadiliko yatakayowapa maji safi na salama, na miundombinu ya umeme na barabara iliyo imara itakayowezesha sekta binafsi kuongeza ajira kwa vijana wetu. Watanzania wanataka mabadiliko ili kuanzisha utaratibu wa hifadhi ya jamii kwa kuwalipa wazee maskini kiinua mgongo kila mwezi kwa kuanzia na mifano midogo midogo ya kujifunzia (pilot schemes) Watanzania wanataka mabadiliko yatakayosafisha uoza wa ufisadi na rushwa na yatakayoleta uwajibikaji na utawala wa sheria. Watanzania wanataka mabadiliko yatakayojenga misingi imara ya umoja, udugu na mapenzi kati ya wananchi wenye imani tofauti za kidini, wa makabila, rangi, na jinsia tofauti. Watanzania wanataka mabadiliko ambayo yataupa uhai mpya Muungano wetu na kuuimarisha uweze kukabiliana na changamoto mpya kwa kuhakikisha haki na usawa kati ya Tanganyika na Zanzibar, na hivyo kuvutia nchi nyengine kujiunga nasi. Watanzania wanataka mabadiliko yatakayowapa dira na mwelekeo mpya utakaolipeleka Taifa katika jamii inayozingatia haki sawa kwa wote na yenye uchumi imara unaotoa ajira na tija kwa wananchi wote. Watanzania wanataka mabadiliko yatakayowapa uongozi makini, thabiti na wenye uzalendo wa kweli kwa Taifa letu. Watanzania wanataka mabadiliko kwa sababu sasa wako tayari kwa mabadiliko. Nafasi ya CUF kama Chama Mbadala Waheshimiwa Wajumbe wa Mkutano Mkuu na Watanzania wenzangu, kufanyika kwa Mkutano Mkuu huu ni uthibitisho tosha kwamba Chama Cha Wananchi (CUF) ndiyo Chama Mbadala chenye uwezo wa kuwaongoza Watanzania kuking’oa madarakani Chama Cha Mapinduzi (CCM) na pia kutoa uongozi makini na imara utakaoleta mabadiliko ya kweli hapa nchini, mabadiliko yatakayotujengea Tanzania mpya yenye haki sawa kwa wote na ujenzi wa uchumi imara wenye kuleta neema kwa Watanzania wote. Tanzania inahitaji mabadiliko. Watanzania wamechoshwa na miaka 48 ya bakora za CCM na sasa wanadai mabadiliko. Lakini mabadiliko hayawezi kuletwa na chama chochote tu cha siasa kinachodai kutaka kuleta mabadiliko. Mabadiliko ili yawe mabadiliko ya kweli na yenye tija na neema kwa Watanzania ni lazima yawe mabadiliko makini. Mabadiliko makini yanaweza kuletwa na Chama Mbadala makini tu. Watanzania wameshuhudia kwamba CUF katika miaka 17 tokea kuasisiwa kwake imekuwa ikiimarika siku hadi siku, mwaka hadi mwaka, na imeweza kujenga imani katika nyoyo za Watanzania kwamba ndiyo Chama Mbadala makini, ndiyo Chama kiongozi katika kuleta mabadiliko ya kisiasa, kiuchumi na kijamii. Hata hivyo, katika siku za karibuni, kumekuwa na majaribio ya kutaka kuonesha kwamba eti CUF haiwezi kuongoza mageuzi ya kisiasa, kiuchumi na kijamii hapa Tanzania. Wanasema kwamba CUF imeshindwa kuongoza harakati za Watanzania za kuleta mabadiliko kutokana na utawala wa CCM. Wanaosema hivi ni wavivu wa kufikiri na ama wana macho lakini hawataki kuona au wana masikio lakini hawataki kusikia au vyote kwa pamoja. Kufanyika kwa Mkutano Mkuu huu pekee ni dalili ya wazi ya uwezo wa CUF. Ni ushahidi wa CUF kuwa ni Chama kilichojijenga kama taasisi kamili ya kisiasa. Mkutano Mkuu huu unafanyika miaka mitano kamili tokea ule wa Februari 2004 na hivyo kuifanya CUF ijipambanue kwa kuweza kutekeleza sheria ya nchi inayovitaka vyama vya siasa kufanya chaguzi zake kwa vipindi vilivyotajwa ndani ya Katiba zao. Kipimo kingine cha chama makini cha siasa ni jinsi kilivyojengeka katika muundo na mtandao wake katika pembe zote za nchi. CUF imefanikiwa kujenga mtandao wake takriban katika pembe zote za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. CUF ipo kuanzia Dar es Salaam hadi Kigoma, Tanga hadi Mtwara, Bukoba hadi Tabora, Pemba hadi Unguja. CUF imejipambanua kuwa ni Chama cha Kitaifa. Katika maeneo yote hayo, muundo wa Chama unafahamika na umejengeka kuanzia Tawi, Kata/Jimbo, Wilaya hadi Taifa. Kuleta mabadiliko ya kisiasa katika nchi zinazoongozwa na chama dola kinachong’ang’ania kubaki madarakani kwa njia yeyote ile kunahitaji Chama Mbadala kilicho madhubuti na chenye viongozi na wanachama jasiri, wasiotetereka, wasioyumbishwa na wasio na woga. Viongozi na wanachama wa CUF tokea ngazi ya Taifa hadi Matawini wamejipambanua na kujidhihirisha kuwa ni jasiri na shupavu wasioogopa vitisho wala hujuma za chama tawala katika kutetea haki za Watanzania. Viongozi na wanachama wake wamekamatwa, wamebambikiziwa kesi, wamefungwa, wamepigwa, wamebakwa na hata kuuawa lakini hawakurudi nyuma katika mapambano ya kumkomboa Mtanzania. Kufichua ufisadi na maovu ya chama kinachotawala ni sehemu ya wajibu muhimu wa chama cha upinzani. CUF imejipambanua kwa kuongoza mapambano ya kupiga vita ufisadi kwa kipindi chote tokea kuingia kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa hapa nchini. Tuliachiwa peke yetu vita dhidi ya ufisadi katika miradi ya IPTL, ununuzi wa rada na ndege ya rais, utolewaji wa zabuni katika manunuzi ya vifaa vya kijeshi kwa JWTZ, ujenzi wa minara pacha ya BOT na ufujaji wa fedha zilizotokana na misamaha ya madeni kutoka nje. Kwa chama makini cha siasa kinachopigania mabadiliko, kufichua maovu na ufisadi au kwa lugha ya mitaani ‘kuripua mabomu’ pekee hakutoshi kuleta ukombozi wa kweli wa Mtanzania. Kauli za hamasa na jazba ni muhimu kuwapa wananchi ari ya kujiletea mabadiliko katika maisha yao baada ya kuangushwa vibaya sana na Serikali za CCM kwa miaka 48 sasa. Lakini ukombozi wa kweli utapatikana kwa kuwa na Umma uliozindukana na unaotambua kwa nini unataka mabadiliko na ni mabadiliko gani unaoyataka. CUF siku zote imejipambanua kwa kuja na sera mbadala zilizofanyiwa utafiti na kutayarishwa kitaalamu kwa kuzingatia misingi ya ujenzi wa uchumi imara wa kisasa. Ni CUF katika miaka miwili sasa kupitia kwa Kiongozi wa Upinzani Bungeni ambayo imekuja na Bajeti Mbadala zitakazoweza kumkomboa Mtanzania kiuchumi na kuondokana na umasikini walioletewa na CCM ambao hauna sababu. Watanzania wamezindukana kutokana na sera hizi. Tunawashukuru Watanzania kwa kutupa imani zao na kukubali kwamba sisi katika CUF tumeweza kujipambanua kuwa ni Chama makini kinachopambana kuleta Haki Sawa kwa Wote na kujenga uchumi imara utakaoleta neema kwa wananchi wote. Naamini matokeo ya Mkutano Mkuu huu yatawathibitishia Watanzania kwa namna nyingine kwamba bado CUF imejipambanua kuwa ni Chama imara na ambacho kitaendelea kutekeleza wajibu wake wa kihistoria wa kuwaongoza hadi kufikia lengo la ukombozi wa kweli katika maisha yetu na ya nchi yetu. Nawahakikishia kwamba na sisi tumejiandaa kikamilifu kuendelea kuutekeleza wajibu huo kwa Watanzania. Baada ya maelezo hayo, sasa natamka rasmi kwamba Mkutano Mkuu wa Nne wa Taifa wa THE CIVIC UNITED FRONT (CUF – Chama Cha Wananchi) umefunguliwa rasmi. Ahsanteni sana kwa kunisikiliza.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s