Nyumba 600 zabomolewa Zanzibar, CUF yalaani

Date::2/21/2009

Na Salim Said
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) jana iliendesha bomoabomoa inayodaiwa kuwa mbaya katika maeneo ya shehia(kata) za Tomondo na Kisauni ambapo zaidi ya nyumba 600 zilibomoloewa na kuharibu misingi 250 wilaya ya Magharibi .

Watu walioshuhudia matukio hayo walisema yalifanyika kwa kushtukiza, bila notisi na kuendeshwa chini ya ulinzi wa Polisi wa kutuliza ghasia (FFU), Mkuu wa Mkoa huo, Mkuu wa Wilaya, Masheha na baadhi ya Maafisa wa usalama.

Shuhuda na mwathirika Khamis Ramadhan Juma, ambaye kwa kushirikiana na wanakijiji wenzake waliendesha tathmini ya kuhesabu nyumba zilizobomolewa na kugundua kuwa nyumba 600 na fondesheni 250 zilikwishabomolewa hadi kufikia saa 10:00 jioni ya jana huku zoezi likiendelea. Sheha wa Shehia ya Tomondo jimbo la Dimani, Mohammed Ali Kidevu, alipoulizwa juu ya suala hilo jana , alisema kazi hiyo inafanyika kwa amri ya Mkuu wa mkoa na kwamba yeye asingeweza kuzungumza.

“Sikusikii vizuri nipo kazini, unalisikia Burdoza (Tingatinga) hilo linafanya kazi na mimi natakiwa kusimamia, mpigie mkuu wa mkoa huyu ndiye mwenyewe” alisema Kidevu.

Kwa mujibu wa baadhi ya waathirika, hatua hiyo inchukuliwa kwa madai kuwa walivamia maeneo yasiyoruhusiwa na serikali kujengwa yakiwemo ya viwanja vya shule.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi alisema, ana taarifa za kuendeshwa kwa zoezi hilo na kuthibitisha kuwa linasimamiwa na polisi pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Mjini magharibi .

“Mimi sipo katika eneo la tukio ila mpigie mkuu wa mkoa amenipigia muda si mrefu akiwa katika eneo la tukio anasimamia zoezi hilo” alisema.

Aidha alipogiwa simu Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Abdallah Mwinyi alijigamba kuwa ni kweli anasimamia lakini alikataa kueleza sababu za kubomoa bila ya kutoa notisi kwa wananchi.

“Wewe panda ndege tu, uje uchukue habari, kila baada ya dakika 10 ndege zinatua pale uwanja wa ndege, mnakaa juu ya meza mnapiga simu kuandika uongo na kula fedha bure tu. Njoo huku kama unahitaji habari” alidai.

Ali Ali Yussuf, ambaye ni muathirika wa tukio hilo, alisema SMZ imekusudia kuwadhalilisha kwa kuwa wao hawana nguvu ya kupambana.

“Tuliwekewa X jana (juzi) jioni na sheha wa shehia yetu, na leo limekuja tingatinga
kubomoa, lakini wamebomoa hata zilizokuwa hazijawekewa X” alilalamika Yussuf na kuongeza:
“Tumeambiwa nyumba zingine zitawekewa X kesho (leo) na wanabomoa kama waliovuta bangi ,hawana huruma, wengi wamepoteza mali, lakini wepesi wameokoa baadhi ya mali”.

Wakati huohuo Chama cha Wananchi (CUF) kimelaumu hatua ya SMZ kubomoa nyumba za wananchi eneo hilo.

Naibu Mkurugenzi wa Haki za Binadamu na Mwasiliano na Umma wa CUF Salim Bimani, alisema ubomoaji huo umefanyika wakati shauri la suala hilo likiwa mahakama ya ardhi na bado halijatolewa uamuzi.

“Sisi, Chama cha Wananchi (CUF), tunalichukulia suala hili kama ni uvunjaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala wa sheria ambao unahimiza kutokuchukuliwa hatua zozote za kisheria bila kupitia ngazi ya mahakama” alisema Bimani na kuongeza:

“Pia tunatoa wito kwa SMZ, wanasheria na wananchi, kwamba SMZ isitishe mara moja bomoabomoa hiyo na ifidie hasara zilizopatikana kutokana na hatua hiyo.

Advertisements

One thought on “Nyumba 600 zabomolewa Zanzibar, CUF yalaani

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s