“SMZ haikupaswa kutumia msamaha wa madeni kwa anasa”

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI 13 Februari 2009

“SMZ haikupaswa kutumia msamaha wa madeni kwa anasa”

Wapendwa Wanahabari,

Juzi Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kupitia Waziri wa Nchi, Afisi ya Waziri Kiongozi, Hamza Hassan Juma, imetetea ununuzi wake wa magari 80 ‘kwa ajili ya matumizi ya maafisa’ wake, kwamba, kwanza, ulifanywa kwa kutumia fedha ya msamaha wa madeni na, pili, kutokana na ukweli kwamba maafisa wengi wa serikali hawana usafiri wa kudumu na wa uhakika.

Ambapo utetezi wa kwanza unatukumbusha kuhusu dai kama hilo la Serikali ya Muungano juu fedha za Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) kwamba hazikuwa za serikali – dai ambalo limekuja kuthibitika si sahihi – utetezi wa pili unakwenda kabisa na mantiki katika wakati huu ambapo nchi imekabiliwa na hali ngumu ya uchumi huku maisha ya wananchi yakizidi kudidimia.

Kwanza, haikuwa sawa kutumia msamaha wa madeni kununulia magari ya serikali wakati mahospitali yetu yakikosa madawa na huduma muhimu za tiba, wakati maskuli yetu yakiwa hayana vifaa vya ufundishaji na walimu wakiwa hawana mishahara ya kuridhisha, na kwa ujumla mfumo wa huduma za kijamii ukiwa mbovu katika namna tunaoushuhudia.

Pili, si sawa kusema kuwa fedha zinazotokana na msamaha wa madeni si fedha za serikali na, hivyo, si za wananchi. Ukweli ni kuwa serikali inaposamehewa deni huwa waliosamehewa hasa huwa ni wananchi ambao ndio wao waliokuwa wakatwe kodi zao kulipwa deni hilo. Kwa hakika hasa mzigo wa deni la serikali hubebwa na wananchi, kwani serikali husema kwamba zinakopa kwa ajili ya kuwaendeleza au kuwahudumia wananchi hao. Kwa hivyo, kama zilivyo fedha za kodi, fedha za msamaha wa madeni pia ni miliki asilimia mia moja ya wananchi na, hivyo, lazima zitumike ipasavyo kwa ajili ya wananchi ni si kwa starehe na anasa.

Tatu, ukosefu wa usafiri kwa watendaji wa SMZ, kama kweli upo, hauwezi kulinganishwa hata kidogo na ukosefu wa huduma muhimu za kijamii kama vile umeme, afya, maji na elimu – kwa kutaja maeneo machache. Raha ya wakubwa kutembea na Prado na Rav4 haina maana mbele ya dhiki za wananchi walizonazo sasa.

Nne, inakumbukwa kwamba Serikali ya Muungano imezuia mpango kama huu wa SMZ wa kuagiza magari kwa ajili ya watendaji wake. Kwa kila hali, uchumi wa SMT ni mkubwa na imara zaidi ukilinganisha na wa SMZ. Ni kinyume cha mambo kwa SMZ kuendelea na maamuzi haya hata baada ya wenzao wa SMT kung’amua kwamba haukuwa uamuzi sahihi.

Kwa hivyo, sisi CUF, tunataka SMZ iyakusanye magari hayo mara moja na ama kuyarudisha ilikoyanunua au iyauze kwa bei ile iliyonunulia na fedha zitakazopatikana ziingizwe kwenye mfumo wa huduma ya jamii kupunguza machungu ya wananchi.

Imetolewa na Salim Bimani
Naibu Mkurugenzi,
Haki za Binaadamu na Mahusiano ya Umma,
CUF – Chama cha Wananchi
Simu: +255 777 414 112, +255 777 414 100
Weblog: https://hakinaumma.wordpress.com
Website: http://cuf.or.tz

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s