“Waziri Haroun ajiuzulu”

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI 11 Februari, 2009

“Waziri Haroun ajiuzulu”

Wapendwa Wanahabari,

The Civic United Front (CUF – Chama cha Wananchi) kimeyapokea matokeo ya mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne upande wa Zanzibar kwa mshtuko mkubwa. Kama ilivyokuwa kwa miaka mingine ya nyuma, matokeo ya mara hii yameendelea kuwa mabaya na Zanzibar imeendelea kuwa nyuma sana.

Katika hali ya kawaida, uchache wa wanafunzi na skuli za Zanzibar ungelitakiwa uwe kichocheo cha kufanya vyema, ikiwa tu kungelikuwa na walimu wa kutosha wenye uwezo na vifaa vya kufundishia. Kwa muendelezo wa matokeo kama haya, ile kauli kuwa “Watoto wa Kizanzibari hawana uwezo wa kupasi mtihani wa Kidato cha Nne” imefanywa ionekane ni ya kweli. Na hili ni tusi si kwa uwezo wa kiakili wa vijana wetu tu, bali pia – na zaidi – kwa heshima ya Zanzibar na kwa Tanzania kwa ujumla.

Wapendwa Wanahabari,

Sisi, CUF tunasikitishwa sana na tabia kongwe ya SMZ kupuuzia hatima ya Zanzibar kwa kudharau umuhimu wa elimu bora kwa vijana wetu, ambayo matokeo yake yamekuwa ni kuwafelisha vijana hawa na hivyo kulifelisha taifa zima kwa ujumla. Hatua ambazo zimekuwa zikichukuliwa na SMZ, kwa mfano kulundika wanafunzi katika skuli za msingi na kati kwa wingi ili kutaka kujiengea sifa ya kuwa kila mtoto wa Kizanzibari anakwenda skuli, bila ya kujali hali halisi ya upatikanaji na utoaji wa elimu katika skuli hizo, zimekuwa ni kikwazo kwa maendeleo ya kielimu ya Zanzibar na sio msaada kwa watoto wetu.

Wapendwa Wanahabari,

Sisi, CUF, tunataka hatua tatu zifuatazo zichukuliwe haraka kwa upande wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), ambayo ndiyo yenye jukumu la kusimamia elimu na maendeleo ya Wazanzibari, ili kurudisha heshima iliyopotezwa na kuwajenga vijana wetu wasivunjwe moyo na aibu kama hii:

1. Waziri anayehusika na masuala ya elimu, Haroun Ali Suleiman, aombe radhi kwa wazee na vijana wa Zanzibar kwa kushindwa kwake kusimamia vyema jukumu lake la kuinua na kukuza elimu visiwani Zanzibar. Waziri Haroun aueleze umma nini kimekuwa kikitokezea hata watoto wa Kizanzibari wakawa wanafeli mtihani wa Kidato cha Nne kila mara kwa kiwango cha kutisha kama hiki. Mwisho, Waziri huyo awe muungwana kwa kukubali mwenyewe kujiuzulu wadhifa wake kutokana na kufeli kwake.
2. Kwa kuwa mwaka jana, SMZ iliunda Kamati Maalum ya kufuatilia kufeli kama huku kwa wanafunzi wa Zanzibar, tunataka ripoti ya Kamati hiyo iwekwe wazi, mapendekezo yake yatekelezwe haraka iwezekanavyo na hatua kali zichukuliwe ikiwa kuna uzembe wowote ule uliobainika kuwa chanzo cha kufeli kwa wanafunzi miaka iliyopita
3. SMZ iajiri walimu wenye uwezo na iwape mafunzo walimu iliokwisha waajiri, iweke vifaa vya kufundishia kwenye maskuli na iwalipe walimu mishahara inayokidhi matakwa ya maisha ya sasa. Kwa ujumla, iuboreshe mfumo mzima wa utoaji na upokeaji wa elimu, ambao matokeo haya yameuthibitika kutokufaa.

Tunasisitiza kuwa ni lazima SMZ itumie vyema kodi ya wananchi na misaada inayopata kutoka kwa marafiki wa kimaendeleo, sio kwa kujenga mabanda ya skuli yasiyokuwa na elimu, bali kuweka elimu bora kwenye mabanda hayo yanayobeba mustakabali wa taifa letu.

Imetolewa na
Salim Bimani
Naibu Mkurugenzi
Haki za Binaadamu na Mahusiano ya Umma
The Civic United Front
Simu: +255 777 414 112, +255 777 414 100
Weblog: https://hakinaumma.wordpress.com
Website: http://cuf.or.tz

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s