Maalim Seif: “Kikwete akome kutufitinisha Wazanzibari!”

Kauli ya Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, katika Mkutano wa Nane wa Maombolezi ya Januari 2001, uliofanyika viwanja vya Kibandamaiti, mjini Zanzibar, tarehe 31 Januari, 2009

Waheshimiwa wananchi wenzangu, sote tunakumbuka kwamba tarehe 27 Januari 2001 nchi yetu ilikumbwa na maafa makubwa. Watanzania wenzetu, hususan Wazanzibari, waliuawa, wengine wakafanywa walemavu wa maisha, wengine walibakwa, wengine wakafungwa, wengine mali zao zikaharibiwa na kuporwa, na wengine wakakimbilia Mombasa kama wakimbizi, kwa mara ya mwanzo. Huu ni msiba mkubwa kwa taifa la Tanzania.

Na hawa (wahanga wa maafa hayo) kosa lao lilikuwa nini? Kosa lao ni kushiriki maandamano ya amani kudai haki zetu. Kimsingi walidai kwamba uchaguzi wa 2000 ulikuwa ni uchafuzi, wakataka urejewe. Wakadai tuwe na katiba mpya Bara na Zanzibar. Wakadai tume huru za uchaguzi Bara na Zanzibar. Lakini kwa watawala, hiyo ilikuwa ni dhambi; kwa hivyo,serikali chini ya usimamizi wa CCM wakaamrisha majeshi: majeshi wanaolipwa kwa fedha za kodi za Watanzania, watumie risasi na silaha zilizonunuliwa kwa fedha za kodi za Watanzania, wawauwe Watanzania wenzao. Na kama alivyosema, Mheshimiwa Duni, baada ya hayo yote kutokezea, Bwana Mkapa anawatunza wale wauaji – anawapa vyeo zaidi – na Amani Karume anawapongeza majeshi kwa kufanya kazi nzuri.

Waheshimiwa wananchi, mimi napenda tujuwe kuwa msiba huu ni wa wana-CUF peke yao. Msiba huu ni wa Wazanzibari sote. Kuna wengine wenye mtazamo finyu wataona CUF wameshikishwa adabu, lakini wakumbuke ‘Tumbili akisha miti, huja mwilini.’ Mghani Utenzi amesema wazi wazi kwamba kuna viongozi wa chama cha Afro Shirazi wakubwa tu, nao walipoteza maisha yao. Kwa hivyo, tusiangalie mambo hayo kwa ufinyu kwamba ni CUF.

Huu ni msiba kwa taifa. Wajibu wetu Wazanzibari ni kuwakumbuka wenzetu, tusiwasahau, tuwaenzi. Na kuwaenzi wenzetu ni kuendelea na mapambano yale ambayo yalisababisha damu zao zitoke. Hakuna kurudi nyuma. Yeyote yule ambaye atarudi nyuma kwa namna yoyote ile, huyo ni msaliti na muuaji kama wauaji wenyewe, kabisa. Ni lazima, ni lazima, sote kabisa tuungane kuhakikisha kuwa dhulma katika nchi yetu inaondoka moja kwa moja. Lazima dhulma iondoke. Hakuna mizinga, hakuna bunduki, hakuna rupleni ambayo itaturudisha nyuma katika kudai haki zetu. Tutadai haki zetu mpaka zote zimalizike, lakini tutazipata haki zetu. Lazima tuzipate haki zetu, tusiwasaliti wenzetu.

Waheshimiwa, nasema bado yale yaliyowafanya wenzetu wapoteze maisha, bado madai yetu yapo pale pale. Bado tunataka katiba mpya; hili ni dai ambalo mpaka leo ni halali. Tunataka tume huru ya uchaguzi. La kusikitisha, mimi nilidhani yaliyotokea 2001 watawala watajifunza, lakini bahati mbaya watawala wetu wana vichwa vigumu. Kwao kubwa ni kuhakikisha namna gani wataendelea kubakia kwenye madaraka kwa gharama yoyote ile. Maisha ya binaadamu kwao si kitu, kitu ni wao waendelee kubaki na madaraka, basi.

Wamesahau kuwa waliowaua wenzetu 2001, wengi wao na wao weshakufa. Mwenyezi Mungu hana haraka, lakini anahukumu hapa hapa duniani, akhera ni malipo tu. Nao watahukumiwa, huko akhera kutakwenda hisabu tu basi. Sawa sawa!?

Waheshimiwa, nasema tena nasikitika kuwa watawala hawajifunzi. Na ushahidi kuwa watawala hawajifunzi ni kauli alizozitoa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Jakaya Kikwete, katika ziara aliyoifanya Zanzibar katika visiwa vya Unguja na Pemba.

Kikwete alisema mengi, lakini mawili makubwa niliyoyashika mimi ni haya: alipokuwa Pemba anawaambia Wazanzibari, kwamba haki ya Wazanzibari ni kuchagua mbunge, mwakilishi na diwani, basi. Lakini ukija kwa uchaguzi wa kumpata kiongozi mkuu wa Zanzibar, Wazanzibari hawana haki hiyo. Hiyo ndiyo kauli ya Kikwete. Na kwa kweli chaguzi za 1995, za 2000 na za 2005 zimeonesha kuwa huo ndio mtindo. Kwa hivyo Kikwete anatwambia kabisa kuwa na 2010, yeye ndiye ataamua nani awe rais wa Zanzibar. Huo ndio ujumbe wa Kikwete.

Waheshimiwa, na hapa nawaomba ndugu zetu wa CCM waifahamu: ingawa Kikwete kasema wapinzani, lakini kakusudia Wazanzibari. Ndugu zetu wa CCM, nyinyi wenyewe ni mashahidi, mwaka 2000 mlikuwa na mtu mlomtaka, mlomchagua nyinyi wenyewe, wana-CCM wa Zanzibar, lakini watawala wa Bara walikuwa hawamtaki. Wakamuweka mtu wanayemtaka wao.

Kwa hivyo, msidhani kauli ile tunaambiwa CUF peke yetu. Hapana, tunaambiwa Wazanzibari kwa ujumla wetu. Inawezekana kabisa na 2010, CCM mkawa na mgombea wenu, lakini madam hamtaki Bwana Kikwete, basi huyo mgombea wenu asahau. Huo ndio ujumbe wenyewe alioutoa Kikwete, kwamba mwenye haki ya kutupatia rais wa Zanzibar ni Kikwete mwenyewe na CCM yake ya Bara. Huo kwa ufupi ndio ujumbe wa Jakaya wa Mrisho wa Kikwete.

Ujumbe wa pili, ambao kautolea hapa hapa Kibandamaiti, ni kwamba ati wako tayari kupambana na wapinga Mapinduzi na akasema watayalinda Mapinduzi yao kwa gharama zozote. Jamani nataka mnisikie vizuri: kauli ya Kikwete na namnukuu: “Tutayalinda “Mapinduzi Yetu”, kwa gharama zozote!”

Mimi ninavyojuwa – na tunavyoambiwa – ni kwamba Mapinduzi yale yalikuwa ni ya Wazanzibari, kwamba kiongozi wa Mapinduzi alikuwa Mzee Abeid Amani Karume na wenzake kina Said Washoto. Tunaambiwa ni Wazanzibari ndio waliofanya Mapinduzi, au sio? Haya Kikwete ni Mzanzibari? Mimi ninavyojuwa – na Profesa (Lipumba, ambaye ni Mnyamwezi na kimila ni mtani wa Kikwete) – kwamba Kikwete ni Mkwere. Zanzibar haimuhusu shikio wala ndewe. Leo vyereje Kikwete asema: “Tutayalinda Mapinduzi yetu!” Vyereje!?

Hapo pana mambo makubwa Wazanzibari, lakini leo si wakati wake kuyazungumza. Inshallah siku za mbele tutayafunua moja baada ya moja, kwa nini Kikwete katoa kauli ile. Na kwa kweli anaposema kuwa atapambana na wapinga Mapinduzi, anakusudia wale ambao watampinga mgombea atakayeteuliwa na yeye, Kikwete. Usijali kama wewe ni CCM au CUF, madhali unapingana na mtu aliyemleta yeye, wewe ni mpinga Mapinduzi yao. Ndio maana nasema Wazanzibari tuone kuwa hili suala si dogo. Haambiwi CUF, twaambiwa Wazanzibari kwa ujumla wetu.

Wananchi, jambo la kushangaza, wenzetu watawala – hawa watawala wa Bara – jambo wanaloliogopa kwa Wazanzibari ni umoja wa Wazanzibari; kwa sababu ndiyo sera yenyewe. Nguvu zao (watawala wa Bara ni) ‘wagawe uwatawale.’ Mtakumbuka alipokuwa mtawala Mkapa lile linamkera, pale pale hakuweza kujizuia…. Pale pale kwenye jukwaa alipopewa nafasi ya kusalimia, akaanza kusema: “Tunatoa salamu kwa mababu za hao wapinga Mapinduzi, vijukuu vyao, vitukuu vyao hawatawali hapa.” (salamu za Mkapa katika sherehe za mwaka 2002 za Mapinduzi ya Zanzibar. Baada ya Muafaka wa pili wa 2001, CUF ilishiriki katika sherehe hizo kama chama na Mkapa aliogopeshwa sana na namna umma wa Kizanzibari wenye sare za CUF na CCM ulivyokusanyika pamoja kwa mara ya mwanzo kwenye sherehe kama hizo).

Ebo! Wewe badala ya kufurahi kwamba Wazanzibari kwa umoja wao wanasherehekea Mapinduzi kwa mara ya mwanzo, unakasirika. Lakini si ujinga, analijua analolifanya, kwamba lile aliliona inawasogeza Wazanzibari wawe karibu pamoja na hilo watawala wa Tanganyika hawataki kuliona. Na hili, Jakaya Kikwete, kwa hili kashtushwa sana na mshikamano wa Wazanzibari. Kashtushwa sana na umoja wa Wazanzibari. Wazanzibari sasa hivi wamekuja juu kusema kuwa tutalinda nchi yetu, Zanzibar ni nchi na itabaki kuwa nchi mpaka Kiama. Wazanzibari wameshikamana kulinda rasilimali zao, hasa za mafuta. Sasa Kikwete hili linamuuma sana.

Linamuuma sana tu, kwa sababu wao wamo katika kutekeleza mkakati tangu aliouwacha Julius Nyerere kwamba Zanzibar itoweke katika ramani ya dunia. Sasa mshikamano wenu Wazanzibari unawafanya wao wasifanikiwe. Kwa hivyo, alilokuja kufanya Kikwete ni kujaribu kuwagawa tena Wazanzibari kwa kutumia wimbo wa Mapinduzi. Tena, mimi nashukuru Mungu, kasema ‘Mapinduzi yetu,’ katumia wimbo wa Mapinduzi yao. ‘Mapinduzi yao’ si Mapinduzi ya Wazanzibari, jamani. Mujuwe hilo!

Kwa hivyo, anataka kutumia wimbo huo atugawe, lakini kachelewa. Kachelewa. Hatugawiki tena ng’o! Tena namwambia Jakaya wa Mrisho wa Kikwete akome, akome, akome! Akome kutuletea fitna katika nchi yetu. Akome, akome kuja kutugawa Wazanzibari. Fanya chokochoko zako huko huko Bara. Namna gani, bwana!?

Tena anajisifu mwenyewe: “Miye Zanzibar naijuwa!” Waijuwa Zanzibar weye? Wee waijuwa Zanzibar? Ati mwenyewe anaijua Zanzibar kaja ’77 akiwa afisa dawati pale Kisiwandui (ofisi ndogo ya CCM, Zanzibar). Wakati huo Maalim Seif tayari ni mjumbe wa Baraza la Mapinduzi. Wakati huo Maalim Seif ni Waziri wa Elimu wa Zanzibar. Wakati huo Maalim Seif ni mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM. Wakati huu Maalim Seif ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM. Yeye (Kikwete) mtoto mdogo tu, nani Kikwete? Nani huyu, kabisa!? Namwambia Jakaya wa Mrisho wa Kikwete kwamba enzi za kuja na shanga mununue nchi yetu umepitwa na wakati.

Eti CCM imeleta maendeleo. Maendeleo gani? Tumejenga barabara! Barabara ipi mulojenga? Mimi nasema tena, hao vibaraka uliowaweka hawajaleta maendeleo yoyote Zanzibar na sisi Wazanzibari ndio tunaojuwa. Ati umekuja hapa kumtetea Amani Karume kuwa kaleta maendeleo; na mwenyewe bila haya anasema ati Kikwete na Karume ni mama mmoja, baba mmoja, watoto mapacha. Hujasema jipya Kikwete. Na tunajua kwa sababu hiyo, kwa wewe na yeye baba yenu na mama yenu ni CCM – ati leo CCM huyo huyo ni baba, huyo huyo ni mama, ni khuntha.

Khuntha CCM imemzaa Kikwete na Karume, ati wanasema ni mapacha. Hatushangai, ndio maana ufisadi unaotokea Zanzibar, watu wanachukuliwa ardhi zao, Kikwete mhm! Kimya, hasemi kitu. Fedha za serikali, kodi zinazokusanywa kutoka bandarini, kutoka airport, kutoka kila mahali zinakwenda nyumba kubwa. Kimwete mhh! Kimya. Lakini hatushangai, CCM inazaa mafisadi, Bara na Zanzibar.

Kwa hivyo ninalosema, Mheshimiwa Kikwete, ujumbe wako Wazanzibari wameupokea, kwamba 2010 kushamuonea choyo Mkapa, nawe wataka kuua. Keshamuonea choyo Mkapa kwamba mikono yake ina damu, na yeye Kikwete anataka mikono yake iwe na damu vile vile. Basi Wazanzibari tunakusubiri njoo! Njoo! Njoo! Wazanzibari tunakusubiri njoo!

Sisi tulikuamini uliposema 2005 kwamba mpasuko wa Zanzibar unakuuma kweli kweli na kwamba utafanya kila njia ili uumalize. Tukakupa mashirikiano yote Kikwete. Wakati napita kwenye matawi kuelezea suala hili, sehemu nyingi nikiulizwa: “Hivyo Maalim, unamuamini Kikwete?” Nami jibu langu lilikuwa: “Simuamini lakini tumpururie, atajinyonga mwenyewe huyu!” Mwenyezi Mungu hamfichi mnafiki. Lile ambalo lilikuwemo kwenye moyo wa Kikwete, juzi kalitapika. Sawa sawa? Bila ya siye kushiriki, mwenyewe kalitapika. Wazungu wanasema: “the true colors of Kikwete have now come out!” Rangi sahihi za Kikwete sasa hivi zinakuja juu. Sawa sawa?

Sasa anajiandaa kutuua tena Wazanzibari. Tunamwambia aje. Lakini tunakwambia, tunakwambia, tunakwambia: Inshallah mara hii, mara hii, mara hii, utakavyoipiga, tutaicheza hivyo hivyo.

Makamo karibu…

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s