Kama fedha za EPA zipo, ziko wapi? – Hamad Rashid

MAONI YA MHESHIMIWA HAMAD RASHID MOHAMED (MB) KIONGOZI WA UPINZANI NA MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI WIZARA YA FEDHA NA UCHUMI KUHUSU MUSWADA WA SHERIA YA MATUMIZI YA NYONGEZA KWA MWAKA WA FEDHA 2008/2009 [SUPPLEMENTARY APPROPRIATION (FOR FINANCIAL YEAR 2008/09) ACT, 2009]

Mheshimiwa Spika
Napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uzima na nguvu za kuweza kusimama hapa mbele yenu ili kuwasilisha maoni ya Kambi ya Upinzani, kuhusu Muswada wa Sheria ya Matumizi ya Nyongeza kwa Mwaka wa Fedha 2008/09, kwa mujibu wa kanuni za Bunge, kanuni ya 86(6) toleo la mwaka 2007.
Mheshimiwa Spika,
Wakati nikiwasilisha maoni ya Kambi ya Upinzani ya Bajeti ya 2008/09, tuliishauri Serikali kwamba pesa za EPA, shilingi bilioni 131.8, ziingizwe katika bajeti (sisi tuuliita “Commitment ya EPA”), Serikali ilijibu hivi, nanukuu: “Waheshimiwa wabunge na wananchi wote wanaonisikiliza kwamba fedha za EPA hazikuwa fedha za Serikali wala fedha za Benki Kuu. Hizi fedha zilikuwa za wafanyabiashara ambao kwa wakati ule waliilipa iliyokuwa NBC kwa ajili ya kuagiza bidhaa mbalimbali toka nje.” Mwisho wa kunukuu.
Mheshimiwa Spika,
Kwa nukuu hii, Serikali ilikataa kuziingiza pesa katika Bajeti yake. Tunashukuru kwamba yale tuliyosema wakati ule, sasa yameonekana yanawezekana. Ni matumainio yetu kuwa na ushauri mwengine tulioutoa utazingatiwa pia, ili kuwapunguzia mzigo wa maisha Watanzania wakati raslimali zipo, lakini zimekosa usimamizi thabiti. Kama kunatakiwa uthibitiso wa hayo, tuko tayari kuutoa.
Mheshimiwa Spika,
Aidha, Kambi ya Upinzani inasikitika kuwa majibu yaliotolewa na Serikali sio tu yalipingana na ushauri wetu, bali hata Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali, jambo ambalo linaidhalilisha sana Serikali. Ushauri wetu kwa siku za mbele ni kuwa Serikali iongeze umakini katika kutoa majibu na hasa pale ambapo ushauri wa Kambi ya Upinzani na Mdhibiti na Mkaguzi wa Serikali (kwani yeye katika taarifa yake alizionyesha fedha za EPA kuwa ni fedha za Serikali zilizotakiwa zirudishwe na Serikali ikazikana), au taasisi zinazoheshimika maoni yao kwa kiasi fulani yanaoana, maana leo Watanzania watajiuliza hivi ni nani mkweli?
Mheshimiwa Spika,
Hata fedha yako ulioiweka Banki kama utakaa muda wa miaka miwili huiendeshi akaunti hiyo, benki huiita “Dormant account’ na ukizidi muda kidogo tu fedha hiyo huwa mali ya Benki, fedha ya EPA imekaa muda gani bila ya wadai kujitokeza? Hili ni angalizo tu Mhe.Spika. Naamini tumejifunza mengi katika mchakato wa EPA.
Mheshimiwa Spika,
Katika muswada huu inaonyesha kuwa kiasi cha shilingi bilioni 40 kinaongezwa katika mfuko wa ruzuku ya mbolea kwa ajili ya kununulia pembejeo za kilimo, ili kuweza kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula.
Kambi ya Upinzani inauliza hivi hii mbolea ya ruzuku inamnufaisha nani kati ya mkulima au mfanyabiashara? Kutokana na taarifa halisi kutoka kwa wakulima wa mikoa mbalimbali, inaonyesha mbolea hii ya ruzuku haina faida kwa wakulima na badala yake inawanufaisha wafanyabiashara. Hii ni kumuongezea mlipa kodi wa Tanzania mzigo. Tunashauri Serikali isikie kilio cha wakulima ambacho kimewasilishwa vyema na waheshimiwa Wabunge hapa Bungeni juu ya matatizo ya mbolea ya ruzuku, kwanza kuwa kidogo, halafu haifiki kwa wakati na wafanyabiashara ndio wanaofaidi zaidi kuliko wakulima.
Mheshimiwa Spika,
Kutokana na kauli aliyoitoa Mhe. Rais hapa Bungeni, kwamba fedha hii itakwenda kwenye kilimo kupitia TIB, ni vyema Serikali ikaeleza wazi kiasi gani kinaenda TIB, na kwamba hizo nyengine zimekwisha kutumika au bado zilikuwa zinangoja idhini ya Bunge au vipi? Kwa kuwa tunaamini Serikali haiwezi kutumia bila ya idhini ya Bunge, ni vyema basi ikatoa mchanganuo wa matumizi kamili ya fedha hizi – hasa kwa kuzingatia kuwa fedha hizi kwa mujibu wa kauli ya Serikali, huenda wenyewe wakaja kudai – zinahitaji kutumika katika kuzalisha ili ziweze kulipwa zikihitajika.
Mheshimiwa Spika,
Serikali ilikwishatoa tathmini yake ya upembuzi yakinifu juu ya azma yake ya kuufanya mkoa wa Morogoro kuwa ndio ghala kuu la chakula hapa nchini. Kambi ya Upinzani inaona kuwa badala ya Serikali kuendelea kuwanufaisha wafanyabiashara, ni bora ichukue uamuzi wa kuwekeza fedha hizo kwa Mkoa wa Morogoro. Tunaamini mafanikio yake yatajionyesha kwa kipindi cha muda mfupi, na nchi itaondokana na tatizo la njaa nchini.
Mheshimiwa Spika,
Muswada wa sheria hii unapendekeza mgawo wa shilingi bilioni tatu kwenda kuongeza mtaji kwenye Benki ya Rasilimali. Kambi ya Upinzani toka mwanzo ilipendekeza kuwa Benki hii ya Rasilimali, japokuwa imepewa majukumu makubwa ya kutoa mikopo kwa wakulima, bado ilikuwa ni changa kwa dhana kuwa mtandao wake bado ulikuwa ni mdogo mno, na mtaji wake pia ulikuwa ni mdogo na hivyo kutumiwa kama ndiyo benki ya Taifa kutoa mikopo ya kilimo ni kiini macho na hadaa kwa wakulima. Ni vyema Serikali ikaeleza ni namna gani Benki hii itakavyoweza kuwahudumia wananchi vijijini.
Mheshimiwa Spika,
Kambi ya Upinzani kabla haijaunga mkono hoja hii ni vyema tukafahamishwa hizi fedha kabla hazijatumika ziko wapi, kwa sababu Gavana anashindwa kujua ni akaunti ipi yenye fedha hizo. Je ni mamlaka gani inayoweza kulielimisha Bunge fedha hizo ziko katika mfuko gani hata Serikali sasa iwe na mamlaka ya kuzitumia?
Mheshimiwa Spika,
Baada ya kusema hayo, naomba kuwasilisha.
……………………………
Hamad Rashid Mohamed (Mb)
Msemaji Mkuu wa Kambi-Wizara ya Fedha na Uchumi.
Na Kiongozi wa Upinzani Bungeni.
03.02.2009

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s