Hamad: Kikwete acha kutuvuruga

*Akumbushia machungu ya kutemwa kwa Dk Bilali

Na Salma Said, Zanzibar

KATIBU Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad amemtaka Rais Jakaya Kikwete kuacha kutamka maneno ya kuwagawa Wazanzibari kwa vile hawagawanyiki.

Vile vile amesema kutokana na kauli hizo za Kikwete wanachama wa chama chake wataingia katika uchaguzi mkuu wa mwaka kesho, wakiwa wamejitayarisha kupambana na mazingira yoyote yatakayojitokeza.

Kiongozi huyo aliyewania urais wa Zanzibar mara tatu bila mafanikio, alikuwa anazungumzia kauli ya Kikwete akiwa ziarani kisiwani Pemba kuwa, wapinzani wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) itawachukua muda mrefu kupata nafasi ya kuongoza nchi hiyo au wanaweza wasiipate kabisa.

Rais Kikwete alisema, “Tutamwendeleza kila mtu kwa sababu dhamana ya maendeleo ni yetu katika serikali. Hawa wengine hawana serikali. Kazi ya wabunge wao na wawakilishi wao ni kufoka tu. Sisi ndio wenye dhamana ya serikali na wala hatubagui.”

Jana akihutubia mkutano wa hadhara katika Viwanja vya Kibandamaiti Mkoa wa Mjini Magharibi, Maalim Seif alisema kauli hiyo ni ya kuwagawa Wazanzibari wote hata wa Chama Cha Mapinduzi visiwani humo, ambao mwaka 2000 walimchagua Dk Gharib Bilali, lakini chama hicho kilipoketi Dodoma kikawaletea Amani Karume ambaye alikuwa ameshika nafasi ya tisa.

Alisema kwamba viongozi wa CCM Tanzania Bara wamekuwa na utamaduni wa kuwagawa Wazanzibari kwa malengo ya kurudisha nyuma maendeleo ya Zanzibar na kuididimiza kisiasa na kiuchumi.

“Viongozi wa Tanzania Bara wapo katika mkakati wa Mwalimu Julius Nyerere wa kuitokomeza Zanzibar, tunamwambia Kikwete kachelewa Wazanzibari hatugawiki tena ng’o tena namwambia akome akome akome kutuletea fitna katika nchi yetu, afanye chokochoko huko huko bara,” alisema Maalim Seif huku akishangiliwa na umati wa watu waliohudhuria mkutano huo.

Alisema kwamba, Wazanzibari hawapo tayari kuona umoja wa kitaifa ukivurugwa kwa kisingizio cha mapinduzi, kwa vile mapinduzi ya Zanzibar yalifanikishwa na Wazanzibari wenyewe na ndio wanaopaswa kuyalinda na sio yeye Kikwete.

Hamad alisema kauli zilizotolewa na Rais Kikwete wakati wa ziara yake Zanzibar haziashirii kuwepo uchaguzi huru na wa haki Zanzibar, kwa vile wapinzani wasitarajie kukamata madaraka ya dola na wengine wataishia kutafuta nafasi hiyo hadi mwisho wa maisha yao.

Alisema CUF imejifunza mambo mengi tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi, baada ya kuvurugwa kwa uchaguzi mwaka 1995, 2000 na 2005 na sasa umekuwa ni utamaduni wa kudumu wa CCM.

Maalim Seif alisema ameshangazwa na kauli ya Rais Kikwete kwa vile inakwenda kinyume na ahadi yake ya kuhakikisha anawaunganisha Wazanzibari kwa kumaliza mpasuko wa kisiasa aliyoitoa Desemba 30, 2005.

Alisema kauli ya Rais Kikwete kuwa Wazanzibari wana haki ya kuchagua madiwani, wawakilishi na wabunge, lakini hawana haki ya kumchagua rais ni kauli inayokwenda kinyume na misingi ya demokrasia na utawala bora.

“Napenda kuwaambia wananchi sasa rangi sahihi ya Rais Kikwete inakuja juu, lakini tunamueleza kuwa ngoma itakavyopigwa ndivyo tutakavyocheza,” alisema Maalim Seif na kuongeza kuwa Wazanzibari wamechoshwa na matatizo ya kisiasa.

Alisema Wazanzibari hivi sasa wanaishi katika lindi la umasikini na viongozi waliopo madarakani kazi yao kubwa ni kukusanya mapato ya serikali na kutumia kwa maslahi yao binafsi, huku wakiacha wananchi wakiteseka.

Alisema hivi sasa Zanzibar wananchi wanakabiliwa na tatizo kubwa la ufisadi wa ardhi, lakini Rais Kikwete ameshindwa kukemea vitendo hivyo licha ya kuwa ni tatizo kubwa hivi sasa kwa Unguja na Pemba.

“Wazanzibari wamepokea ujumbe wake, lakini tunaamini anataka mikono yake iwe na damu kama Rais Mkapa alivyoondoka na damu mikononi, lakini Wazanzibari tunakusubiri njoo, tulikuamini kwa kauli yako ya kushughulikia mpasuko wa kisiasa, lakini sasa tumekufahamu tunakwambia njoo,” alirudia kusema Maalim Seif huku akishangiliwa.

Akihutubia katika mkutano huo mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba alisema CUF imesikitishwa na kauli ya Rais Kikwete kwa vile inakwenda kinyume na ahadi yake ya kumaliza mpasuko wa kisiasa wa Zanzibar.

Alisema kwamba, tangu mapema alijenga wasiwasi na uwezo wa utendaji wa Rais Kikwete na kumbatiza jina la msanii na alipata matumaini mapya baada ya hotuba yake ya kwanza kuahidi kushughulikia matatizo ya Zanzibar.

Lipumba alisema katika mikutano mitatu ya Rais Kikwete na mabalozi aliyoifanya kuanzia 2006 hadi 2008, alikuwa akiwaeleza kuwa ameshafikia hatua nzuri katika kushughulikia mpasuko wa kisiasa wa Zanzibar kitendo ambacho ni kinyume na kauli zake.

“Tunamshukuru Kikwete kwa kuweka mambo wazi kwa vile sasa katudanganya basi tena, kwa vile wanasema wao ndio wanaoamua na rais atateuliwa na yeye nashukuru ametupa muda wa kuweza kujipanga, tena kujipanga kweli kweli, tumechoka na bakora za CCM,” alisema mwenyekiti huyo huku akishangiliwa.

Aliwataka vijana, wanawake na wazee kujipanga kukabiliana na vitendo vyovyote vinavyozorotesha demokrasia kwa kuanzia na uchaguzi mdogo wa uwakilishi unaotarajiwa kufanyika Mei 23 katika Jimbo la Magogoni .

Mkutano huo ulitawaliwa na vilio vya wanawake kwa vile ulibeba ujumbe wa kuwakumbuka wanachama wa CUF waliouawa Januari 26 na 27 mwaka 2001, hali iliyofanya baadhi ya wanawake kumwaga machozi baada ya kusomewa utenzi kukumbusha majina ya watu waliokufa katika vurugu hizo.

Chanzo: http://mwananchi.co.tz/newsrids.asp?id=9670

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s