CUF kufuta nyayo za JK Zanzibar

Na Exuper Kachenje
CHAMA Cha Wananchi (CUF) kimeandaa mkutano wa hadhara utakaofanyika kesho mjini Zanzibar kujibu hoja za Rais Jakaya Kikwete alizotoa alipokuwa kwenye ziara visiwani humo.

Naibu Mkurugenzi wa Haki za Binadamu na Mawasiliano ya Umma, Salim Biman alisema jana kuwa mkutano huo, utafanyika katika viwanja vya Kibandamaiti ambapo mgeni rasmi atakuwa Mwenyekiti wa chama hicho , Profesa Ibrahim Lipumba.

Biman alisema katika mkutano huo, Profesa Lipumba atajibu hoja mbalimbali za Rais Jakaya Kikwete, zikiwemo za, CUF kufuta ndoto ya kuiongoza Zanzibar, wanaobeza maendeleo ya CCM ni walevi tende na kuzungumzia uchaguzi mdogo wa ubunge jimboni Mbeya vijijini.

“Pia atazungumzia kauli ya Pinda kutaka wanaoua walemavu wa ngozi, wauawe na kujibu hoja mbalimbali alizotoa Rais kuikejeli CUF,” alisema Bimani.

Hivi karibuni akiwa ziarani Zanzibar, Rais Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama Chama Cha Mapinduzi (CCM), alitoa kauli mbalimbali zinazotafsiriwa na CUF kuwa kejeli na dharau dhidi yake.

Katika moja ya mikutano yake ya hadhara visiwani humo, aliyoifanya baada ya kufungua mradi wa maji wa Kengeja, Mkoa wa Kusini Pemba, Rais Kikwete alinukuliwa akisema “Ni muhimu kwa watu kukubali kuwa ipo serikali iliyoko madarakani hata kama wanaikataa jinsi ilivyoingia madarakani:

“Ukweli ni kwamba ipo na ni muhimu kwa watu wote kushirikiana nayo, katika kuleta maendeleo. Maana ukisubiri hiyo serikali yako, inaweza ikachelewa sana ama pengine isije kabisa katika uhai wako,” alisema Mwenyekiti Rais Kikwete.

Kuhusu kauli za wapinzani kubeza na kukejeli kuwa CCM wala SMZ haijaleta maendeleo yoyote kwa wananchi, Rais Kikwete aliwaambia wananchi hao wa Kengeja kuwa “Wananchi, hizi ni fitina tu. Unajua midomo kazi yake ni kusema. Unaweza kusema lolote hasa inapokuwa kwenye kufitini, kudanganya watu ili wakuchague,” alisema na kuongeza,

“Ujumbe wetu kwa wapinzani wetu ni rahisi kabisa, kuwa nyie endeleeni kuwachagua mnaowataka, lakini endeleeni kutukabidhi sisi serikali na dhamana ya kuleta maendeleo.
Wao wache waendelee kutia fitina, kubeza maendeleo, lakini maji safi, wanaendelea kunywa; barabara wanaendelea kupita wakipeperusha bendera zao kwa sababu zinateleza kama mgongo wa ngisi.”

Katika mkutano wake mwingine visiwani humo, Kikwete alisema watu hao wanaobeza maendeleo na serikazi ya Mapinduzi Visiwani humo ni walevi wa pombe ya kienyeji aina ya tende inayotengezwa na kunywewa Zanzibar.

“Watu wengine sijui wanakunywa tende, maana mtu mzima na akili yake anadiriki kusema hakuna maendeleo, wakati anapanda gari hatikisiki kwa sababu ya barabara zilizojengwa na CCM, manawe haugui na hafi kwa kuwa hakuna malaria, lakini mtu huyo anasemaaa, mpaka mapovu ya mdomo yanamtoka kulia na kushoto, wee sema, mfereji unatoa maji, wao watasema mfereji utatoa maziwa, na kila siku wanashangaa, kwa nini hawashindi, jibu ni kwamba hawasemi ukweli,” alisema

Biman alisema Profesa Lipumba atazungumzia kauli hizo kwenye mkutano huo ambao utafanyika kuanzia saa 8:00 mchana ambapo pia atazungumzia chaguzi mdogo wa Jimbo la Mbeya Vijijini uliofanyika hivi karibuni na mgombea wa CCM kuibuka kidedea.

Aidha katika siku za karibuni Waziri Mkuu Mizengo Pinda, akiwa katika ziara mikoa ya kanda ya Ziwa alinukuliwa akisema “Mkimuona mtu akamkata mwingine shingo naye amueni cha kumfanya kwani sasa viongozi wote tumechoka… no more, I can’t tolerate anymore (imetosha, siwezi kuvumilia tena).”

Kuhusu uchaguzi huo, mgombea wa CUF aliishia kupata nafasi ya pili huku chama hicho na vingine vya upinzani walitoa madai mbalimbali kuulalamikia uchaguzi huo, ambao idadi ya watu waliopiga kura ilikuwa chini ya asilimia 45 ya watu waliojiandikisha kupiga kura.

Kwa mujibu wa Biman, Jeshi la Polisi Zanzibar limeridhia na kutoa kibali cha kufanyika Mkutano huo akiwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kuhudhuria mkutano muhimu.
Hata hivyo Pinda aliviomba vyama vya siasa kushirikiana na wananchi kuhakikisha suala la mauji linakwisha kwa kuwa ni rahisi kulimaliza tatizo hilo iwapo watakuwa kitu kimoja katika kuondoa kashifa.

Chanzo: http://mwananchi.co.tz

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s