Kauli za Kikwete, Pinda zaweka ufa

• JK aonekana kuigeuka CUF Zanzibar

na Asha Bani na Edward Kinabo

MWENENDO wa mambo nchini unazidi kuwa tata, baada ya viongozi wakuu wawili wa kitaifa kutoa kauli zilizotafsiriwa na wachambuzi wa mambo kuwa zinaweza kuhatarisha amani na mshikamano uliopo nchini.

Viongozi hao, Rais Jakaya Kikwete na Waziri Mkuu wake, Mizengo Pinda, wiki iliyopita, kwa nyakati tofauti, walitoa matamshi yenye kuashiria kwamba serikali wanayoingoza haiko tayari kuachia madaraka na kuchochea mauaji miongoni mwa wanajamii.

Wa kwanza kutoa kauli iliyoibua hisia nzito mbele ya jamii ni Rais Kikwete ambaye akiwa ziarani Zanzibar, aliwaeleza wananchi wa huko kuwa Chama cha Wananchi (CUF) kisahau kuingia madarakani, labda hadi mwisho wa uhai wake.

Rais Kikwete alitamka maneno hayo wakati akiwasalimia wakazi wa Kijiji cha Kengeja, Mkoa wa Kusini Unguja, ambapo alieleza wazi kuwa wapinzani wasahau kuingia ikulu wakati yeye akiwa hai, labda hadi katika uchaguzi mkuu wa mwishoni mwa 2010.

Katika salamu zake hizo, alinukuriwa akieleza kuwa wapinzani wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) wanaweza kuchukua muda mrefu kupata nafasi ya kuunda serikali, ama pengine wasiipate kabisa hadi mwisho wa uhai wao, na hivyo kuwataka washirikiane na serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kuwaletea maendeleo wananchi.

Kauli hiyo ya Rais Kikwete, imetafsiriwa na baadhi ya wananchi waliozungumza na Tanzania Daima Jumapili kwa sharti la kutotajwa majina yao gazetini kuwa, inaonyesha jinsi anavyofanana na Rais mstaafu, Benjamin Mkapa, kimsimamo na kiimani kuhusu mustakabali wa uongozi wa taifa hii.

Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa walilieleza gazeti hili kuwa kauli ya Rais Kikwete inaweza kuibua upya chuki za kisiasa baina ya wafuasi wa vyama vya CUF na CCM licha ya hali hiyo kuwa imetulia kwa muda sasa.

Wachambuzi hao walieleza kuwa, licha ya chokochoko za kisiasa baina ya vyama hivyo viwili ambazo zimekuwepo katika kipindi cha hivi karibuni, vikao vya kutafuta muafaka wa kisiasa visiwani humo vilivyotokana na kauli ya Rais Kikwete aliyoitoa katika hotuba yake ya kwanza bungeni kuwa anafadhaishwa na mpasuko wa kisisasa Zanzibar, viliwapoza na kuwafanya kuwa na subira mahasimu hao wakisuburi kupatikana kwa suluhisho la kudumu.

Mkurugenzi wa Mambo ya Nje na mjumbe wa kamati ya kutafuta muafaka kati ya CCM na CUF, Ismail Jussa Ladhu, alisema muda wa kuonyeshana uwezo wa kisiasa kwa vyama hivyo sasa umefika, baada ya viongozi wakuu wa CCM kuanza kutoa kauli zenye kila dalili za kugeuza hali ya mambo tofauti na ilivyotegemewa.

“Nakwambia viongozi wetu wamekuwa watu wa kubadilika siku hadi siku, tulimwamini sana Rais Kikwete, hasa baada ya hotuba yake ya ufunguzi wa Bunge jipya mwaka 2005 pale Dodoma alipoahidi kutanzua migogoro ya kisiasa hapa Zanzibar, lakini sasa tunaona ameanza kupoteza mwelekeo kwa kutoa kauli zisizo za kistaarabu,” alisema Jussa.

Alisema Rais Kikwete ameonyesha hasira nyingi pasipo na kosa mbele ya wananchi, jambo linalothibitisha kuwa alidhamiria kufanya hivyo kipindi kirefu.

Wakati Rais Kikwete akiwa amezua mjadala kutokana na kauli yake hiyo, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, naye anaonekana kuwa gumzo miongoni mwa wananchi wa kada mbalimbali kutokana na kauli yake ya kuwataka wananchi kuwaua watu wanaowaua maalbino na vikongwe.

Pinda alitoa kauli hiyo juzi wakati akiwahutubia wananchi wa Tabora, ambapo alisisitiza kuwa wasisubiri uamuzi wa mahakama kuwaua watu wanaoua maalbino na vikongwe.

Alikaririwa akiwaambia wananchi kuwa kuanzia sasa mtu yeyote atakayemuona mtu amemkata shingo au mkono mwenziwe, naye auawe papo hapo.

Baadhi ya wabunge waliozungumzia kauli hiyo, walisema Pinda anapaswa kutumia busara zaidi anapotoa maagizo mazito kwa wananchi na walishauri kuwa ili kuiweka sawa kauli yake hiyo, anapaswa kuitolea ufafanuzi kwa vile inaweza kuleta utata na kusababisha wananchi kujichukulia sheria mkononi.

Walisema kwa Waziri Mkuu Pinda kutamka maneno hayo amevuka mipaka ya cheo chake na kuingilia uhuru wa mahakama.

“Kuna kauli ambazo hazitakiwi kutolewa na viongozi kwa wananchi, kwa tafsiri ya Watanzania wengi, kauli zinazotolewa na rais au waziri mkuu zinaweza kuchukuliwa kama ni msimamo wa serikali.

“Pinda amevuka mipaka yake na kuingilia uhuru wa mahakama, ni busara aitolee ufafanuzi ili kutengeneza mazingira ya kutaka kujua msimamo ulivyo,” alisema Halima Mdee, Mbunge wa Viti Maalumu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Alibainisha kuwa hata hivyo haamini kwamba kauli ya waziri mkuu ina nguvu kuliko mahakama ambazo zina hatua zake za kuchukua kwa watuhumiwa.

Alisisitiza kuwa kauli ya Pinda inaweza kusababisha mkanganyiko kwa maalbino na jamii nyingine, kwani inaweza kutokea albino akafanya kosa kubwa miongoni mwa jamii lakini kutokana na kuwepo kwa kizingiti fulani, akashindwa kuchukuliwa hatua yoyote.

“Tusije tukajikuta badala ya kutatua tatizo la msingi kwa kuwatafuta wauaji na kuwachukulia hatua, tunaweka matabaka kwa maalbino dhidi ya kundi la watu wa kawaida.

“Jambo la msingi kwa serikali ni kutumia vyombo vyake vya dola vilivyopo na ikiwa kuna atatayebainika kuua albino anakamatwa na taratibu za kisheria zinachukuliwa dhidi yake,” alisisitiza Mdee.

Naye Mbunge wa Viti Maalumu (CUF) Mkoa wa Lindi, Mwanawetu Zerafi, alisema haiwezekani mwananchi kujichukulia hatua mkononi bila sheria kufuatwa.

“Kauli yake ni too short (fupi mno), nadhani akikaa akafikiri ataona amepotoka, aliteleza kufanya hivyo, “Suala la kuua halipo kwa albino pekee bali hata binadamu wengine, hivyo ikiwa ataruhusu hali hiyo, itawadhuru pia hata watu wengine,” alisema Mwanawetu.

Naye Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CHADEMA), Zitto Kabwe, alisema haamini kama Waziri Mkuu aliteleza kutoa msimamo huo.

“Haiwezekani iwe hivyo, lazima taratibu za kisheria ziwepo ndipo mtu huyo auawe, siamini kama waziri mkuu aliteleza,” alisema Zitto.

Chanzo: http://www.freemedia.co.tz/daima/habari.php?id=1825

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s