“Serikali ya Jamhuri ya Muungano Iseme: “Basi” kwa Ukandamizaji wa Haki za Binaadamu!”

TAARIFA YA MWENYEKITI WA THE CIVIC UNITED FRONT (CUF – CHAMA CHA WANANCHI) KATIKA KUMBUKUMBU ZA MAUAJI YA JANUARI 2001

Wapendwa Wanahabari na Watanzania Wenzangu,
Leo ni tarehe 26 Januari 2009. Miaka nane iliyopita, siku ya leo ulikuwa ni mwanzo wa mauaji ya kutisha yaliyofanywa na Vyombo vya Dola vya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa wananchi wasiokuwa na hatia. Mauaji hayo yaliambatana na matendo mengine ya uvunjaji wa haki za binaadamu kama vile kupigwa kwa raia, kuwekwa ndani bila ya makosa, kubakwa kwa wanawake na kuibiwa mali za raia. Mpaka maafa haya yanamalizika, tayari Watanzania wapatao 70 walishapotezewa uhai wao, mamia wakiachwa na vilema vya maisha, mamia wakitiwa umasikini kutokana na ama kuibiwa au kuharibiwa kwa mali zao na maelfu ya wengine wakiwa wakimbizi nje ya mipaka ya Tanzania.

Wapendwa Wanahabari na Watanzania Wenzangu,
Hakuna fakhari yoyote kuyakumbuka na kuyakumbushia matukio haya machafu katika nchi yetu ambayo yaliiacha historia iliyotukuka ya Tanzania ikiwa imejeruhika vibaya. Watanzania waliopoteza maisha yao, viungo vya miili yao, ndugu na jamaa zao, na; zaidi ya yote; waliopoteza heshima yao kutokana na ukandamizaji ule uliofanywa na Vyombo vile vile vya dola ambavyo vilitarajiwa kuilinda nchi hii na watu wake, hawana la kufidiwa kwa hayo yote. Na hao ni sote sisi kwa umoja na wingi wetu. Maafa ya Januari 2001 yalikuwa ni aibu kubwa kwa taifa letu na yataendelea kubakia kuwa hivyo daima.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inachukuwa dhamana ya yote yaliyotokezea; na sasa – wakati tukiyakumbuka maafa hayo, tuna wajibu wa kutazama nyuma na kukitathmini kile kilichotokea katikati (baina ya mwaka 2001 na 2008) na kuona ikiwa kweli sote, kama taifa, tulijifunza chochote kwa maafa haya na ikiwa pana dhamira ya kweli ya kutokuyarudia tena yale yale.

Wapendwa Wanahabari na Watanzania Wenzangu,
Inafahamika kuwa chanzo cha maafa yale ni chaguzi zisizozingatia haki, uadilifu na usawa ambazo zimekuwa zikiendeshwa na Tume zetu za Uchaguzi tangu kuanzishwa tena mfumo wa vyama vingi mwaka 1992. Uchaguzi wa mwanzo wa 1995 ulitawaliwa na mapungufu ya makusudi na ukamalizika kwa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kulazimisha ushindi kwa mgombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Salmin Amour. Uchaguzi wa pili wa 2000 sio tu ulikuwa na mapungufu bali pia ulivuuka hata vipimo vya chini vya chaguzi, kiasi ya kwamba waangalizi wa ndani na nje waliuita ‘aibu kwa demokrasia.’ Uchaguzi wa 2005 nao ulifuata mkondo wa chaguzi mbili zilizotangulia.

Maandamano ya amani ya Januari 27, 2001 yalikusudiwa yawe ni kielelezo tu cha wananchi kupaza sauti zao kuonesha kutoridhishwa kwao na namna ambavyo ZEC ilikuwa ikidharau matakwa yao . Matakwa ya wananchi – na ya kikatiba – ni kwamba uongozi wa nchi upatikane kwa njia ya uchaguzi huru, haki na adilifu. Serikali ya Jamhuri ya Muungano ikajibu kilio hicho kwa mtutu wa bunduki na uvunjaji wa haki binaadamu.

Kutokana na maandishi yake, Muafaka uliofikiwa baina ya vyama vya CUF na CCM baada ya maafa haya, ulikusudia kukimaliza kabisa – kama si kukizika – chanzo cha maafa hayo – ukosefu wa demokrasia na uchaguzi usioakisi matakwa ya wananchi. Lakini kwa kuwa CCM ilihisi kuwa utekelezwaji wa Muafaka huo haukuwa na maslahi kwake, viongozi wa Serikali (ambao ndio hao hao wa CCM) wakaanza kuuhujumu hatua kwa hatua na hatimaye wakauvunja kabisa na kufikia mwaka 2005 hapakuwa tena kitu kinachoweza kuitwa Muafaka kwa upande wa CCM.

Hii ni kusema kwamba CCM haikujifunza hata kidogo kwa yale ambayo Serikali yake iliyafanya mwaka 2001. Kiwango cha uvunjwaji wa haki za binaadamu, kujenga khofu kwa raia na mateso yalikuwapo kutoka ama kwa vyombo vya dola moja kwa moja au kutoka kwa makundi ya Janjaweed, ambayo yanamilikiwa na CCM.

Matokeo yake ni kuwa uchaguzi wa 2005 nao ukaongezea hisabu ya chaguzi zetu zisizokidhi vigezo vya kidemokrasia. Na tena, kila ushahidi ulikuwa unaonesha kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano ilikuwa tayari kutumia tena mabavu dhidi ya raia pindi raia hao wangeamua kuingia barabarani kudai haki yao iliyoporwa. Kilichozuia maafa yasitokee mwaka 2005 ni busara za hali ya juu za uongozi wa CUF na sio utotayarifu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakati huo ikiwa chini ya Uamiri Jeshi Mkuu wa Rais Mstaafu, Benjamin William Mkapa.

Wapendwa Wanahabari na Watanzania Wenzangu,
Miaka nane sasa baada ya Maafa ya 2001, na bado Tume za Uchaguzi zimeendelea kujenga mazingira ya kutokuwa na chaguzi za haki, huru na adilifu. Kwa mfano, katika mwezi wa Disemba 2008, Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, alitoa taarifa inayoonesha kuwa tayari ZEC imeanza kushirikiana tena na vyombo vya dola kuhakikisha kuwa inapandikiza wapiga kura katika kisiwa cha Pemba ili waje waisaidie CCM katika chaguzi zinazokuja. Itakumbukwa kuwa kisiwa cha Pemba kiliathirika zaidi na maafa ya Januari 2001 kutokana na ukweli kuwa wananchi wa huko, kwa wingi na umoja wao, wamekataa katakata kuiunga mkono CCM tangu mageuzi ya siasa yaanze miaka 17 iliyopita. Mkakati wa CCM ni kulazimisha kuwa inapata viti vya ubunge na uwakilishi kutoka kisiwa hicho na tuna ushahidi wa kutosha namna ZEC inavyoyaandaa mazingira hayo. SMT, CCM na ZEC hawakutosheka na maafa ya Januari 2001 na sasa wanaandaa janga jingine, ambalo lazima Watanzania walipinge na walizuie kwa nguvu zao zote.

Mambo kama hayo yameendelea katika chaguzi ndogo mbali mbali zilizowahi kufanyika Tanzania Bara: ule wa Tunduru wa 2007, wa Tarime wa 2008 na wa Mbeya Vijijini wa 2009. Kiwango cha utumiaji mbinu na hila chafu kutoka Tume za Uchaguzi na pia maguvu ya vyombo vya dola hakioneshi kabisa kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imedhamiria demokrasia na, kwa hivyo, kuwa imejifunza kutokana na maafa iliyosababisha Januari 2001.

Wapendwa Wanahabari na Watanzania Wenzangu,
Sisi Chama cha Wananchi (CUF) tunachukua fursa hii kuungana na kila raia wa nchi hii kuomboleza maafa haya ambayo yameendelea kuwa aibu kubwa kwa taifa letu. Tunawahakikishia kwamba hichi ni chama cha siasa chenye dhamira ya kutumia njia za kistaarabu kufikia lengo la pamoja la kitaifa – yaani kuwa na Tanzania imara kiuchumi, kisiasa, kijamii na kitamaduni. Tunaamini katika uhuru wa binaadamu na demokrasia kama njia pekee za kufikia lengo hilo la kitaifa.

Kwa hivyo, wakati tukiungana pamoja kukumbuka msiba huu mkubwa kwa taifa, tunatoa wito kwa, kwanza, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, iseme: “Basi, imetosha!” Basi, kuwakandamiza raia wanapodai haki zao. Basi kutumia vyombo vya dola kwa maslahi ya kisiasa. Basi kujenga jamii yenye khofu kila inapokaribia na wakati wa uchaguzi. Pili, tunatoa wito kwa Tume za Uchaguzi zote mbili – NEC na ZEC – kwamba nazo ziseme basi kusimamia na kuendesha uchafuzi wa haki ya raia kuchagua viongozi wanaowataka na badala yake wasimamie na waendeshe uchaguzi utakaoakisi matakwa ya Watanzania.

Kwa kutumia maneno ya Mstaafu Mkapa, ambayo kwa bahati mbaya hakutaka kuyatimiza kwa makusudi, “Tanzania ni yetu sote…Hakuna mwenye hati miliki ya nchi hii.” Hatimiliki ya Tanzania ni ya Watanzania wenyewe. Ni vyema Serikali, kama taasisi iliyopewa dhamana ya kusimamia hatimiliki hiyo, kuona kuwa haki za mwenye mali (Mtanzania) zinachungwa, kuheshimiwa na kudumishwa. Na kigezo kimoja cha kuhakikisha hilo ni kuwa na chaguzi huru, za haki na wazi. Huo ndio wajibu wa SMT na Tume zetu za Uchaguzi.

HAKI SAWA KWA WOTE

PROF. IBRAHIM H. LIPUMBA
MWENYEKITI,
CUF – CHAMA CHA WANANCHI

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s