CUF: JK anaongeza mpasuko zaidi

Date::1/24/2009

Na Exuper Kachenje

KAULI ya Rais Jakaya Kikwete kuwa wapinzani wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) watalazimika kusubiri kwa muda mrefu na pengine wasipate nafasi ya kushika madaraka visiwani humo, imewasha moto mpya baada ya Chama cha Wananchi (CUF), kuielezea kuwa imetonesha vidonda vya kisiasa.

Kikwete alitoa kauli hiyo juzi katika siku ya mwisho ya ziara yake kisiwani Pemba ambako ni ngome kuu ya CUF, aliposema kuwa ni bora wanaouwanga mkono wapinzani wakashirikiana na serikali ya CCM kuweka maendeleo visiwani humo kwa kuwa itawachukua muda na pengine iusiwezekane kabisa kutwaa madaraka.

Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti jana, viongozi wa juu wa CUF- mwenyekiti Prof. Ibrahim Lipumba na katibu wake Maalim Seif Hamad- walisema kauli ya Rais Kikwete itaongeza mpasuko wa kisiasa visiwani Zanzibar na kuendeleza utaratibu wa kuwa na uchaguzi usiokuwa huru na wa haki visiwani humo.

Wakati viongozi hao wakisema hayo, katibu mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Wilbroad Slaa amesema bado haamini kama Rais Kikwete anaweza kutoa kauli hiyo, lakini akasema kama rais ametamka hayo, basi nchi imekosa utawala wa sheria.

Akizungumza na Mwananchi jana, Prof. Lipumba alisema kauli ya rais, ambaye aliahidi kushughulikia mpasuko uliotokana na kutangazwa kwa matokeo ya urais katika uchaguzi wa mwaka 2005, imekivunja moyo chama hicho kwa kuwa inapingana na wajibu wake.

“Kauli ya Rais Kikwete ni tatizo linaloongeza matatizo, rais lazima asimamie demokrasia na nafasi ya uhuru wa nchi na watu wake, lakini badala yake yupo kinyume,” alisema.

“Anatonesha vidonda na majeraha makubwa ya kisiasa… anaonyesha wazi sera yake ni kuendeleza wizi katika uchaguzi visiwani Zanzibar. Hana nia ya kuziba mpasuko wa kisiasa ulio Zanzibar ambao alisema anaushughulikia.

Profesa Lipumba alisema kauli hiyo imemsikitisha kwa kuwa inaonyesha nia ya Kikwete na chama chake kuwanyima wananchi uhuru na haki yao ya kuchagua kile wanachopenda kwa manufaa yao na nchi yao.

Aliongeza kwamba kwa kauli hiyo Kikwete haitofautiani na kiongozi wa utawala wa kikoloni wa Rhodesia (Zimbabwe) Mwingereza Ian Smith ambaye aliwahi kutamka kuwa Waafrika hawawezi kujitawala hadi baada ya miaka 50 au 100, jambo ambalo Lipumba alisema halikuwezekana baada ya wananchi wa Zimbabwe kutokubali na kupigania uhuru wao hadi walipoupata.

“Huko ni kukosa uongozi bora na kuhatarisha amani na uhuru wa kweli wa wananchi kwa njia ya demokrasia ya uchaguzi. Rais hana nia njema na demokrasia,” alisema Profesa Lipumba.

Lipumba alidai kuwa chama chake kilishinda katika chaguzi za mwaka 1995, 2000 (ambao ulirudiwa katika baadhi ya majimbo) na 2005, lakini iliibiwa kura zake na kwamba kauli ya Kikwete inaonyesha mapema nia mbaya kwa Zanzibar, jambo ambalo Lipumba alisema ni hatari.

CUF na CCM zimekuwa zikichuana vikali kwenye chaguzi za urais visiwani humo na tangu kuruhusiwa kwa mfumo wa vyama vingi, CCM imekuwa ikishinda kwa tofauti ndogo, matokeo ambayo yamekuwa yakizusha utata mkubwa na kusababisha ghasia, ambazo zilifanya baadhi ya wananchi wa Pemba kwenda Mombasa kuishi kama wakimbizi mwaka 2000 baada ya watu zaidi ya 27 kuuawa.

Naye katibu mkuu wa CUF, Seif Shariff Hamad alisema Kikwete ameushangaza umma na kuonyesha CCM haikubali Zanzibar kujichagulia rais wake na badala yake rais wa visiwa hivyo atawekwa na Serikali ya Muungano inayoongozwa na CCM.

“Sikutarajia rais aliyeingia madarakani na ahadi ya kuziba mpasuko wa kisiasa Zanzibar kutoa kauli kama hiyo. Kauli hiyo itazidisha mpasuko uliopo kwa kuwa inamaanisha wananchi wa Zanzibar waishie kuchagua, madiwani, wawakilishi na wabunge lakini si serikali,” alisema akirejea kauli ya Kikwete kuwa wabunge hawana serikali hivyo hawawezi kuwajengea barabara wala huduma nyingine za jamii.

“Kikwete anamaanisha serikali itaendelea kuwekwa na wao… Wazanzibari hawana haki ya kujichagulia rais wanayemtaka bali CCM na Serikali ya Muungano ndiyo itawachagulia rais wa kuwaongoza. Basi sasa tusubiri tuone,” alisema Maalim Seif.

Katika hotuba yake baada ya kuingia madarakani Rais Jakaya Kiwete, pamoja na mambo mengine aliahidi kuushughulikia mpasuko wa kisiasa uliopo visiwani Zanzibar, lakini jitihada zake za serikali yake kutafuta muafaka zimeishia kwa CUF kutangaza kujitoa kwenye mazungumzo.

Naye Leon Bahati anaripoti kuwa Dk. Slaa amesema haamini kuwa Rais Kikwete ametoa tamko hilo na kama ametamka basi nchi imekosa utawala wa sheria.

Alisema kama kweli atakuwa ametamka hayo basi nchi itasambaratika kwa sababu kutakuwa hakuna uhuru wa utawala wa sheria.

“Siamini kwamba Rais anaweza kusema hayo… inawezekana walimnukuu vibaya, maana kama nchi imefikia hapo, imeanza kusambaratika,” alisema Dk. Slaa.

Chanzo: http://mwananchi.co.tz/newsrids.asp?id=9470

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s