Viongozi wa CUF kuchaguliwa Feb 23-27

Date::1/18/2009

Na Salim Said

MWENYEKITI atakayeongoza Chama cha Wananchi (CUF) kwa kipindi kingine atajulikana mwezi ujao wakati baraza kuu la uongozi la chama hicho litakapokutana kuanzia Febuari 23 hadi 27 kwenye ukumbi wa Diamond Jublee jijini Dar es Salaam.

Katika uchaguzi huo mwenyekiti wa sasa, Profesa Ibrahim Lipumba atapambana na wanachama wawili; Profesa Abdalah Safari na mwanajeshi mstaafu Koplo Steven Masanja kutoka Kahama

Mkutano huo utamchagua katibu mkuu na naibu wake huku wanaoshikilia nafasi hizo wakiwa hawana wapinzani.

Mkutano huo utafanya uchaguzi wa wajumbe 90 wa baraza hilo kutoka Tanzania Bara na 10 kutoka Visiwani huku kukiwa na nafasi maalum mbili za vijana, mbili wazee na mbili wanawake.

Mkutano huo pia utakuwa na kazi ya kujadili na kupitisha mabadiliko ya katiba ili iendane na mabadiliko ya kidemokrasia duniani na matakwa ya jumuiya za kikanda na kimataifa za kiuchumi.

Kwa mujibu wa mkuu wa Idara ya Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa wa CUF, Jussa Ismail Jussa, marekebisho hayo yatakuwa katika vipengele vya namna ya kupata wagombea wa chama katika chaguzi na kuongeza uwakilishi wa wanawake ndani na nje ya chama kuanzia ngazi ya tawi hadi taifa.

Alisema mapendekezo ya marekebisho hayo tayari yameshaandaliwa na yanatarajiwa kujadiliwa na baraza hilo.

Jussa alisema wanatarajia kuwa mapendekezo hayo ya marekebisho yatapita bila ya kupingwa katika mkutano huo.

Alisema wanatarajia kuongeza nafasi ya uwakilishi wa wanawake ndani ya chama kutokana na lengo lao walilojiwekea kuwa hadi kufikia mwaka 2010, chama kiwe na uwiano wa asilimia 30 ya wanawake kwa mujibu wa mapendekezo ya nchi wanachama wa SADC.

Pia alisema katika kipengele cha namna ya kupata wagombea wa CUF katika chaguzi wa mwaka 2010, maamuzi ya mwisho ya kumpata mgombea yanatakiwa kutoka kwa wanachama badala ya viongozi.

“Tunataka hadi kufikia mwaka 2010 wagombea wa CUF katika chaguzi zote nchini wawe wanapigiwa kura na wanachama majimboni mwao. Lengo ni kuondoa malalamiko na lawama kwa wanaoshindwa,” alisema Jussa.

Jussa alifafanua kuwa baraza litapokea na kujadili taarifa ya utendaji wa kazi chama kwa miaka mitano kuanzia 2004 hadi 2009.

“Sambamba na hilo la kupokea na kujadili taarifa hiyo, pia baraza kuu litaandaa kazi za chama kwa miaka mingine mitano kuanzia mwaka 2009 hadi 2014,” alisema Jussa.

Alisema mkutano utakuwa na wageni kutoka katika taasisi mbalimbali za ndani na nje ya nchi ili kushuhudia demokrasia inavyofanya kazi ndani ya chama chao na kwamba hadi sasa wanatarijia ushiriki wa wajumbe 700 katika mkutano huo.

Chanzo: http://mwananchi.co.tz/newsrids.asp?id=9365

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s