SURA YA NNE

                       

LIPI LA KUFANYA?

 

Mambo mengi yanahitaji kufanywa ili kuzuwia matukio kama haya yasitokee tena katika nchi yetu.

 

(i)                  Ni vyema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali yake wasiangalie suala hili kama pahala tulipoangukia tuu, bali pia jicho lao litazame ni wapi tulipojikwaa hadi tukaanguka hapa.

(ii)                Tabia iliyojengeka miongoni mwa viongozi wa siasa na pia baadhi ya wanachama wao kwamba katika nchi hii wapo wenye haki ya kutawala na wengine daima kuwa ni watu wa kutawaliwa, iondolewe na dhana ya kua nchi hii ni ya Watanzania wote ieleweshwe ipasavyo ili ni ya Watanzania wote ieleweshwe ipasavyo ili kupunguza hisia za chuki na uadui miongoni mwetu.

(iii)               Tuhakikishe kwamba chaguzi huru na za haki ndizo zinazofanyika katika nchi yetu.  Wale wanaochangia kuharibu chaguzi kwa njia yoyote ile ieleweke kwamba wanatupeleka pahala pabaya, hivyo ni maana kua sheria za uchaguzi ziboreshwe na zifuatwe na kwa zile zinazotoa adhabu kwa watu wanaoharibu chaguzi kwa makusudi ziongezwe ukali na hatua zichukuliwe dhidi yao.

(iv)              Wananchi wapewe nafasi ya kutumia haki yao ya kuchagua bila vikwazo na maamuzi yao yaheshimiwe baada ya kuchagua.

(v)                Vyombo vya habari hasa vya Serikali vitumike katika kukuza demokrasia na isiwe kushabikia katika kuleta chuki, mgawanyo na mifarakano katika jamii yetu.

(vi)              Vyombo vya dola hasa jeshi la Polisi (ngunguri kama wanavyojiita), JKU, KMKM, Magereza, Valantia, Usalama wa Taifa na JWTZ kwa upande wa Zanzibar wafundishwe maadili na uwajibikaji wao katika mfumo wa demokrasia ya vyama vingi, kadhalika uajiri wao pia uzingatie kanuni bora za utumisi na paanzishwe jitihada za makusudi za kurudisha mahusiano mema baina ya vyombo vya Dola, wananchi na vyama vya Upinzani

(vii)             Kwa kua muafaka ndio safina (jahazi) la safari hii ya kutokurudi tena kwenye karne ya upotofu, basi ni vyema ukatekelezwa ipasavyo tena kwa wakati uliopangwa, kwani kuchelewa kutekeleza jambo lolote katika muafaka huu kunaweza kuleta hisia mbaya miongoni mwetu.

(viii)           Marekebisho ya katiba ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania, yanahitajika haraka.  Na hapa haja si marekebisho tu lakini pia suala zima la kuiheshimu katiba hiyo kwa ukamilifu wake ndio liwe jambo muhimu hata katiba hio iwe na kasoro kiasi gani.

(ix)              Tume ya Taifa ya Uchaguzi, sheria za Uchaguzi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nazo zirekebishwe kufatana na hali ya mfumo wa vyama vingi vya siasa na muafaka tulionao.  Aidha uanzishwaji wa daftari la kudumu la wapiga kura, na marekebisho ya chaguzi za serikali za mitaa kutolewa chini ya ofisi ya waziri mkuu na kuwekwa chini ya tume huru ya uchaguzi ni mambo muhimu sana.

(x)                Sheria arubiani na tano (45) za ukandamizaji zilizoainishwa na Tume ya Jaji Nyalali na zile zinazofanana nazo ziondolewe haraka.

(xi)              Aidha suala la kero za Muungano kujadiliwa na kuondoshwa pia washika dau kushirikishwa katika hilo kuna umuhimu wake.

(xii)             Suala la kutoa Elimu ya uraia, lizingatiwe upya na kuonekana likitendeka.  Na kwakua hili ni suala la kitaifa kampeni yake iendeshwe na, vikundi visivyo vya kisirekali, taasisi na asasi zote katika jamii pia vyama vya siasa na Serikali kuu yenyewe, na iwe ni lazima na muhimu kwa vyombo vya habari hasa vya serikali kusaidia kazi hio ya kuuelimisha umma na kua na programu maalum zitakazo  shirikisha pia taasisi zilizotajwa hapo juu katika suala hili.

(xiii)           Kama tamko la haki za binaadamu lilivyo ingizwa katika katiba zetu.  Rais asaini Mikataba ya nyongeza ya matamka hayo na isiishie kuweka sahihi mikataba hiyo tu bali utekelezaji wake uonekane ukifanywa kuzuia utesaji.

(xiv)           Tume ya haki za binaadamu Tanzania iliyoundwa na Rais iboreshwe iwe huru katika kazi zake na ipewe nguvu na kinga za kisheria katika kufanya kazi hizo.  Sheria ya kuanzishwa kwake ifanyiwe mapitio na irekebishwe kulingana na mahitaji ya taida kwa ujumla na izingatie suala la Muungano.

(xv)            Ushirikishwaji wa wazi kwa wapinzani katika mambo muhimu ya kitaifa na kijamii hasa katika  shughuli za Kiserikali uongezwe.

(xvi)           Ziandaliwe sera za taifa katika alau yale mambo muhimu ili kuondosha utashi wa vyama katika mambo yenye maslahi kwa Taifa kama vile Sera za mambo ya Nje, uchumi, Hifadhi ya utamaduni, Urithi wetu n.k.

(xvii)         Serikali ikubali ombi la kuanzishwa kwa Taasisi huru za kutetea Haki za Binaadamu na kupiga vita utesaji na sheria kandamizi kwa raia.

 

Tunaamini haya tuliyo yaeleza hapa pia ni baadhi ya kero za wananchi ambazo zikiondolewa hali ya mwenendo wa kisiasa mwenendo ambao unaweza kuathiri uchumi, utamaduni na maendeleo ya jamii yetu nao pia utarekebishika, ingawaje mambo haya yako mengi lakini yanazidiana kwa umuhimu hivyo ni imani yetu kwamba Serikali inaweza kuona umuhimu wa mambo haya na vile yanavyoweza kuchangia au kuliepusha taifa na maafa kama haya yaliyo tokea siku ya tarehe 26 – 27/01/2001 ambayo nia yetu ni kwamba yasitokee tena katika taifa letu.

 

 

SURA YA TANO

 

 

HITIMISHO

 

Ukweli ni kwamba Tume ya Rais ya uchunguzi wa matukio ya tarehe 26 – 27/01/2001 imetusaidia sana Watanzania kwa ripoti yake.  Kwani si kila jambo lililoandikwa katika ripoti hiyo kuwa ni baya yako mambo tume wameyaeleza ambapo hakuna aliyeyafikiria kama wangeyaeleza, wamefanya uchambuzi wa taarifa na wamepitisha jitihada za kibinaadamu, ingawaje hakuna mkamilifu.

 

Vile vile kama binadamu yapo makosa yaliyofanywa na mikono yao ya kulia ambayo yanastahamilika na makosa mengine yaliyofanywa na mikono ya kushoto ambayo ndiyo hayo yanayoitwa kasoro zinazopaswa kuchambuliwa.  Yawezekana kutokana na kutanguliwa kazi hii ya Tume na Muafaka wa Kisiasa Tume ilipata kazi ngumu ya kuandika ripoti yake.  Kadhalika mitazamo ya mamlaka iliyowapa jukumu hili, hisia za Watanzania na walimwengu kwa ujumla, hata zile hisia za waandishi wenyewe na mielekeo yao zinaweza zikawasukuma katika kuandika vitu vinavyoshindana na dhamira zao, kwa nia ama ya kuepusha au kunusuru jambo lisitokee au kutaka kupandikiza fikra Fulani kwa wasomaji.

 

Kwa sababu kazi moja kubwa ya Tume ni kuhakikisha kama wanatushauri Watanzania na serikali yetu, nini kifanyike ili matukio kama yake ya tarehe 27/01/2001 yasitokee tena.  Ni wajibu wetu kuelewa kama kazi hii ilihitaji ustadi mkubwa, ambao Tume imeuonyesha.

 

Ila kasoro kuu ziliyojitokeza katika ripoti ya Tume ambazo kimsingi zimekwenda kinyume na hata zile hadidu rejea zake  ni vyema zikaeleweka, kama ni mafuno kwa Tume nyengine kama hizi:

 

1                    Kuhusu mapendekezo ya Tume: Tume katika hadidu rejea zake ilitakwia kutoa mapendekezo kuhusu hatua za kuchukuliwa katika ama kuwafidia waliopatwa na maafa au kuzuia mambo hayo yasitokee tena, lakini kwa bahati mbaya tume haikutoa mapendekezo ya wazi kwa hatua za kuchukuliwa.  Tume haikutoa mapendekezo ya wazi ya kulipwa fidia.

 

2                    Kutotambuliwa kwa baadhi ya vifo: Tume haikufanya jitihada za kutosha kwa baadhi ya vifo na lau kama ingelifanya jitihada ndogo tu wangelipata taarifa sahihi za vifo hivyo inaonekana zaidi tume ‘ilimangimeza’.

 

3                    Kuhusu matumizi ya nguvu katika kuzima maandamano: Neno la tume kukiri kuwepo kwa matumizi ya nguvu na kuzihalalisha nguvu hizo bila ya kufanya utafiti wa kina na kwa kuzingatia mazingira yaliyotangulia maandamano hayo, na siku ya maandamano hayo ni jambo ambalo lilihitaji kuwana lugha inayofaa zaidi ya ile inayotumika, kwani walio wengi hawakujali juu ya kupotelewa na pesa wala kuharibiwa mali zao.  Lakini walishughulishwa na utu wao na roho za ndugu zao, sasa hili halikuwa suala la mzaha.  Hivyo kauli ya tume haikuwa ya busara na inaweza kuleta hisia mbaya kwa waathirika.

 

4                    Matumizi ya historia: Tume kila mwenye kuijua Zanzibar kadhalika na Tanganyika na mwenye kuelewa chimbuko la maandamano matokeo na athari zake hawezi kukubali kwamba historia ile ilitumika kwa kigezo sahihi.  Hili ni jambo jengine lililoonekana kama ni dhambi ya makusudi kwa tume (ya mkono wa kushoto) kwa maelngo maalum.

 

5                    Kukosekana kwa orodha za Mayatima na Wajane wa Marehemu: katika ripoti ya tume ni kasoro nyengine inayoonyesha kwamba tume haikushughulishwa zaidi na matukio ya vifo, kwani kuwapata hao pia kungeliweza kutoa  taswira halisi ya namna marehemu walivyokuwa wakitegemewa na msaada unaohitajika kwa familia zao na pia ingelipunguza machungu kwao kwa kuona angalau tume iliwajali kama wapo.

 

6                    Makisio ya mali zilizoharibika: Ingawaje tume imetaja uharibifu na upotevu wa mali katika ripoti yake lakini kukosekana kwa makisio japo ya awali ya mali hizo, au pendekezo la kufanywa uchunguzi kwa waliopoteza mali zao kama ilivyoshauriwa kufanyika uchunguzi kwa baadhi ya vifo ni jambo lililoleta simanzi kwa baadhi ya waathirika, kwani suala la kujiuliza tume alau haikuona kwamba baadhi ya madai ya watu yalikuwa na uzito sasa unapoyanyamazia yote haya, maana yake ni kuwafanya wote walioleta malalamiko yao wasiridhike na ripoti ya tume.

 

7                    Mgogoro uliokuwepo: Kila mara tume imejaribu kuonyesha kwamba mgogoro ulikuwa ni wa vyama vya CUF na CCM na ikaondoa fikra kwamba labda Serikali nazo zilihusika kikamilifu pamoja na baadhi ya vyombo vya ulinzi na usalama, hii nayo ni kasoro kwani kila anayejua matatizo ya kisiasa ya nchi hii anaelewa fikra kwamba tatizo kuu ilikuwa ni vyombo vya dola.

 

Mfano, angalia wakati tulionao sasa baada ya vyombo vya dola kuacha kushabikia vyama vya siasa, hali imekuwa nzuri na pindi wakiendelea hivyo itazidi kuwa nzuri zaidi.

 

KAULI YETU

 

Tunatoa shukurani zetu za dhati kwa niaba ya The Civic United Front [CUF – Chama cha Wananchi] kwa wale wote wanao tuunga mkono katika harakati hizi za kupigania demokrasia ya kweli katika nchi yetu na mliotuunga mkono katika kununua na kusoma kitabu hiki ambacho kitakua ni cha mwanzo katika mfululizo wa vitabu vingi vinavyo fuata vyenye maudhui mbalimbali juu ya siasa, uchumi, utamaduni wetu, muungano n.k.

 

AHSANTENI SANA

 

Mkurugenzi wa Vijana na Haki za Binaadamu – CUF

 

 

 

 

 

 

 

 

 

1.                   

 

 

 

 

 

 

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s