SURA YA KWANZA

 

 

UCHAMBUZI WA TAARIFA

 

Baada ya shukrani na utangulizi huo, tunaomba kujaribu kuangalia kwa ufupi katika baadhi ya maelezo ya vifungu vya ripoti ya Tume ya Mbita ili kupata uchambuzi wake.

 

 

Katika (kifungu No. 1) Ripoti hii inazungumzia uteuzi wa Wajumbe wa Tume uliofanywa na Mhe. Rais Mkapa.  Ni kweli kwamba Wajumbe hawa ni watu mashuhuri wenye majina yanayoheshimika kwa mfano; Mwenyekiti wa Tume hiyo Bregedia Jeneral Mstaafu Iddi Hashim Mbia kabla ya uteuzi huu aliwahi pia kuwa Kamanda wa Vijana wa CCM katika Mkoa wa Tabora jambo ambalo lilimpa heshima kubwa, vile vile atakumbukwa pamoja na mambo mengine kwa mchango wake katika kamati ya ukombozi wan chi za Afrika Bw. Mbita hivi sasa ni Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe nafasi aliyotunukiwa baada ya kazi nzito aliyofanya!.  Nae Mwalimu Yussuf Masauni alikuwa Mkuu wa idara ya Uhamiaji Zanzibar, Mjumbe wa Tume ya Uchaguzi ya Taifa (NEC) ambae hivi sasa ni Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) twabaan nae amepata stahiki yake kwa utumishi wake mwema, mwengine ni Bw. Ali Abdalla Suleiman aliyekuwa pamoja na nafasi nyengine mtumishi katika Ofisi ya Waziri Kiongozi Zanzibar, mwengine ni Salama Ahmed Kombo ambae alikuwa Mtumishi wa Ikulu Zanzibar, nae Bw. Kassim Ali aliekuwa kamishna wa Polisi Zanzibar na Mkuu wa Kikosi cha Zimamoto, mwengine ni Bw. Bruno Mpangala aliyewahi kuwa Mkuu wa Mkoa na kiongozi wa Vyama vya Wafanyakazi kwa muda mrefu, mjumbe mwengine wa Tume hii ni Prof. Hasa Mlawa wa Chuo kikuu cha Dar es Salaam na wa mwisho ni Katinu wa Tume Bw. Philip Mkamanga ambae amechukua LLB yake hapo Dar es Salaam mwaka 1986 pamoja na kazi nyengine alizowahi kufanya hivi sasa ni Mfanyakazi katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu Tanzania.

 

Si jambo linalogomba kwa Rais kuona kwamba watu hawa tuliowataja hapo juu wangelifaa kwa uteuzi wake kwa jambo lolote lile lakini ingekuwa vyema kabla ya uteuzi angeangalia aina na uzito wa majukumu anayowateulia.  Pia maoni ya watu kwa suala hilo.

 

Chama cha CUF kiliwahi kupendekeza baadhi ya majina kwa Rais ili afikirie katika uteuzi wake majina ambayo chama hicho kiliamini yanaweza yakawa ni yenye kukubalika kwa watu waliowengi katika jamii ya kitanzania na kimataifam kutokana na mchango wao wa mambo mbali mbali kwa taifa hili na heshima waliojijengea na uzowevu wao katika shughuli za uchunguzi na kitaaluma lakini rais akakataa ushauri huo kwa asilimia mia moja.  Ni vyema tukaelewa kwamba heshima ya chombo unachokiunda, ufanisi wake na kufanikiwa kwake hutowa taswira ya uwezo wa kufikiri na usahihi wa maamuzi hata pia ukweli wa imani na uthabiti wa malengo kwa ALIYE UNDA CHOMBO HICHO.

 

Je! Tujiulize Rais etu anapokataa ushauri wa kuwateua watu kama Profesa Issa Shivji, wa Chuo kikuu cha Dar es Salaam mtu ambaye ni Mwanasheria aliyebobea na ambae ameshashiriki katika kufanya uchunguzi wa migogoro kadhaa Nchini petu likiwemo suala la mgogoro wa Ardhi ambao ulishapelekea kuwepo kwa hisia za kugombana baina ya Watanzania.  Tume yake aliyokuwa akiiongozza (Tume ya Shivji) iliyoteuliwa na Rais Ali Hassan Mwinyi ilifanya kazi nzuri.  Mwengine aliyependekezwa na CUF ni Profesa Haroub Othman ambae pamoja na utaalam wake wa Sheria na uzoefu alionao wa kuangalia Chaguzi ni Mwenyekiti wa Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar, pia alikuwa Mwenyekiti wa kundi la Watazamaji wa ndani wa uchaguzi wa Zanzibar (ZEMONG) katika Uchaguzi wa mwaka 1995 ambapo ripoti yao haikuwa tu ripoti ya Uchaguzi bali pia unaweza kusema ulikuwa ni utafiti wa Siasa za Zanzibar.  Prof. Huyu apia alikuwa ni muangalizi wa kundi la watazamaji wa ndani la (TEMKO) katika uchaguzi wa mwaka 2000 aidha Haroub amewahi kuwa muangalizi katika Uchaguzi wa Liberia.  Mwengine ni Jaji W. Daurado alllliyewaji kuwa Mwanasheria Mkuu wa SMZ, mwendesha mashtaka Mkuu wa Kesi ya Uhaini ya mauaji ya Kiongozi wa kwanza wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Sheikh Abeid Aman Karume aidha Bw. Huyu atakumbukwa sana kwa msimamo wake wa uwazi, ukweli na utetezi wa demokrasia bila ya woga.  Mtu mwengine alie pendekezwa na CUF ni Mheshimiwa Jaji R. Kisanga huyu ni yule ambae alipewa kazi ya White paper na Mhe. Rais ili kukusanya maoni ya wananchi pa atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa katika taifa hili hasa kuhusu masuala ya haki za binaadamu na mambo ya kisheria.

 

Hiii ndiyo tofauti ya mapendekezo ya CUF ikiwa kama sehemu ya mgogoro uliokuwepo na uteuzi wa Rais.  Tunawaachia wasomaji wetu muamue wenyewe juu ya suala hili.  Na imani za kila mmoja wetu katika kuwa na nia njema, wakweli, waaminifu na wawazi juu ya yaliyotokea.

 

Aidha (kifungu No. 2) cha taarifa hii kinazungumzia uteuzi wa Sekreterieti ya Tume, ingawaje haikuelezwa ni nani aliyeteuwa Sekreterieti hiyo, lakini hii ni Sekreterieti ya Tume ya Rais hivyo nayo ni sehemu ya Tume kwani katika maseketeri hawa wamo wataalamu wanaoweza kushawishi mambo mengi katika Tume kwa ujuzi wao na kazi waliokabidhiwa zaidi ya hata hao Wajumbe kwani wao ndio watendaji na ndio waandishi wa shughuli za Tume.

 

Cha kushtua zaidi katika uteuzi wa Sekreterieti hii walioteuliwa kusaidia Tume ni Maafisa wenye nyadhufa mbalimbali katika utumisho wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

 

Hii ingaliweza kufanywa ikajenga imani zaidi kwa Watanzania kama wangeliteuliwa zaidi ya robo tatu ya watumishi hawa kutokana na jamii ya Watanzania wasiopungua milioni thelathini (30,000,000), ambao si watumishi wa serikali lakini wenye uwezo wa kazi uliyokusudiwa.

 

Katika (kifungu No. 3), pamoja na maelezo ya tume yanayoeleza kwamba, Tume ilielewa uzito wa jukumu walilopewa hivyo wakazingatia sana hadidu rejea za kazi yao bali Tume katika kifungu hicho inasema “ilianza kazi zake kwa kuelewa kikamilifu kwamba itawajibika kufanya kazi yake kwa uaminigu na uadilifu mkubwa”.

 

Hata hivyo, tume ya Mbita haikueleza wala kuweka wazi kuwa kuwajibika huko ni kwa ajili ya wananchi au ni kwa yule aliyewateuwa.  Uchambuzi unaonyesha kuwa taarifa ya tume haimpi tabu sana msomaji kujua iliwajibika kwa nani.

 

Mfano mwengine.  Kama utasoma (Fungua Namba 4) la taarifa ya Tume linaeleza kwamba ilitambua kua “kazi yake kuu ni kupata taarifa, ushahidi, malalamiko, maoni na ushauri” hapa kumbe ndio msingi wa tatizo kumbe Tume haikuelewa kuwa ilitakiwa pia kuishauri Serikali nini cha kufanya baada ya uchambuzi wa hayo watakayoyapata ili Serikali ijue cha kufanya katika kuhakikisha matukio kama hayo hayatokei tena nchi mwetu, kadhalika katika kufidia waliopatwa na maafa, kuleta umoja wa kitaifa na kusimamisha utawala ulio bora na mambo kama hayo.

 

Kwa maoni yetu ni kwamba tume ikiwa haikufahamu kwamba huu pia ulikuwa wajibu wake basi hiyo ni kasoro tena kubwa hata kama iliyafanya hayo kwa bahati mbaya; yaani kuishauri Serikali lakini ikihisi kuwa haikuwa wajibu wake.

 

(Fungu Jengine ni lile la 22) linalozungumzia kuundwa kwa jopo la madaktari.

 

Ni kweli limeundwa kwa kushirikiana na madaktari wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) na Serikali ya Muungano ya Tanzania (SMT) kama tume ilivyoeleza, hii ilikuwa ni kasoro kubwa kwani hao madaktari wa Mnazi mmoja baadhi yao ndio wanaolalamikiwa kwa kushindwa kutimiza wajibu wao kisheria na kuzingatia maadili ya kazi yao wakati wa kuwahudumia wagonjwa wa matatizo ya kisiasa.

 

Mfano waliopatwa na matatizo ya tarehe 27/1/2001 si siri kwamba wengine hawakupokelewa walipopelekwa hospitali.

 

Kwa mujibu wa taarifa zilizochapishwa katika ripoti ya tume kuna baadhi ya majeruhi walikataliwa hospitali nap engine lau wasingekataliwa yawezekana wasingepoteza maisha au kupatwa na madhara makubwa ya ulemavu kwa sababu ya kukosa tiba wakati unaostahiki.

 

Wengine wakafa katika mazingira ya kutatanisha  wakiwa hospitali na wengine kutolewa Hospitali wakiwa mahatuti kwa amri ya Madaktari hao hao wa hospitali ya Mnazi Mmoja kwa Unguja na Hospitali za Wete, Chake na Mkoani kwa Pemba katika visiwa vya Zanzibar na wakakabidhiwa kwa vyombo vya Dola yaani (Polisi) na baadae wakarudishwa tena Hospitali baada ya kupata kipigo chengine.

 

Kwa mfano tarehe 2/2/2001 majeruhi waisopungua watano (5) walitolewa katika hospitali ya Mnazi mmoja chini ya usimamizi wa polisi wakiongozwa na kamanda Goerg Kizuguto wakati wa saa 1:00 usiku, kinyume na taratibu za utoaji wagonjwa.

 

Wagonjwa hao walipelekwa kituo cha polisi Madema hadi tarehe 5/2/2001 ambapo walifikishwa mahakamani na kuachiwa kwa dhamana.

 

Mfano mwengine ni wa Bwana Juma Ngwali, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa kusini Pemba ambaye kwa sasa ni Mjumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa – CUF pale alipochukuliwa Hospitali akiwa mahututi hana fahamu huku amewekewa dripu na akapelekwa korokoroni.

 

Kwa rekodi ya Madaktari wetu hao, leo Tume inapotueleza imechukua madakrati kutoka Hospitali za Serikali, Hospitali ambazo madaktari wake kwa wakati huo pamoja na kuwa na sifa tulizozitaja hapo juu lakini pia ufanyaji kazi wao ulikuwa na dosari nyengine kubwa miongoni mwao (si wote) inataka tueleweje?

 

Haya si mageni kwa Zanzibar.  Dhahiri imebainika kuwa hata ukiwa na ujuzi wa kiasi gain kama hufuati matakwa ya wakubwa unatimuliwa kazi.  Zipo kesi nyingi za watu kama hao.

 

Kwa mfano, Dk. Juma Ameir Muchi aliyekuwa mtaalamu muhimu wa Malaria na akatambuliwa na WHO (shirika la Afya duniani) kwamba anaweza kuwa dhamana wao katika kupambana na kuitokomeza malaria katika visiwa vya Zanzibar lakini kutokana na misimamo yake ya kisiasa SMZ ikahiari kumtoa kikoa.

 

Mradi wa kupambana na malaria ukafa kwa kukosa wasimamizi wazuri na leo gonjwa hili ndilo lililoshika nambari wani Chambilecho CCM kwa kuuwa watu Zanzibar.

 

Ukiachilia mbali Dk. Muchi hebu muangalie Dk. Sheha.  Sheha aliyekuwa daktari bingwa wa maradhi ya macho katika hospitali kuu ya Mnazi mmoja.  Shutuma za kisiasa  zilimsakama pale aliposhtumiwa  kuwa eti alitaka kuiunguza moto hospitali anayoifanyia kazi ya Mnazi mmoja.

 

Hii ni kichekecho kikubwa.  Ni sawa na mkulima kuvunja mpini wa jembe analolimia.  Akasimamishwa kazi na kupandishwa Mahkamani kwa kosa hilo watu wakaendelea kukosa huduma katika hospitali kuu ya serikali ambayo wakiipata kutokana na daftari huyo.

 

Wapo wengi kama hao ambapo si nia yetu katika sura hii kueleza matatizo yanayowakabili madaktari wetu wanaoitumikia Serikali.

 

Swali linabaki kwa nini madaktari wengi wanaoheshimu kazi na fani zao, wakaikimbia Zanzibar?  Suala hili halina maana kwamba waliopo hawaheshimu taalum zao lakini labda tuwaite majasiri.

 

Sasa Tume ya Mbita, hiyo imani ya Mzanzibari na Mtanzania kuambiwa Madaktari hawa wa serikali hii wamchunguze afya yake kutokana na ugonjwa aliopewa na Serikali iliyomuajiri yeye na atatendewa haki ataitowa wapi?

 

Madaktari ambao katika ripoti hiyo ya Tume ya Rais wameripotiwa katika maelezo ya baadhi ya mashahidi kwamba hata ripoti, vyeti na taarifa za ugonjwa zikiwemo picha za X – ray za baadhi ya wagonjwa zilizuiliwa na mamlaka ya Mnazi mmoja tena kwa jambo dogo tu wagonjwa hao walihitaji kwenda kupata tiba zaidi mbele ya safari.

 

Lakini tunalazimika kuheshimu uteuzi huu wa jopo la madaktari uliofanywa na tume labda ulikuwa na undani zaidi ya huu tuliouona.

 

Kwa nini Tume kama ilikusudia kuona ukweli na kuleta hisia za maelewano isiondoe shaka ya waathiriwa kwa kuwashirikisha madaktari wa kujitegemea na ikiwezekana japo wastaafu ama wawe wa ndani na japo mmoja kutoka nje?

 

Kama hiyo haitoshi! Tume inapoamua kuikalia ripoti ya kitaalamu ya madaktari hao na ikatueleza kwa maneno machache katika ripoti yao kwamba madaktari hao “waliwasilisha ripoti iliyosaidia sana tume” katika kujua ukweli wa waathirika na kuona ni kwa kiasi gain walipatwa na maafa hasa wanawake waliobakwa na kudhalilishwa kijinsia.

 

Kwa kweli inaonekana madaktari wetu walijitahidi kufanya kazi yao kwa uadilifu lakini si ajabu tume ikawa imechagua la kuchukua katika ripoti ya madaktari.  Na kama si hivyo kwa nini ripoti yao isiwe katika viambatisho vya taarifa ya tume?

 

Jambo jengine muhimu kuhusiana na shughuli za wataalamu hawa wa kiafya ni pale tume ilipotangaza orodha maalum kwa watu kukaguliwa afya kama vile wameomba kazi kwani inashindwa kujulikanwa ni kigezo gani kilichotumika katika kuwaita watu kupima afya zao na wengine kati ya waathirika wasiitwe.

Je, hawa tume inakusidia kutufahamisha kwamba iliridhika na maelezo yao mia kwa mia; au kinyume chake kwamba yamekataliwa mia kwa mia?  Hata iwe moja kati ya hayo mawili basi ingepaswa maamuzi yake kutolewa na wataalamu wanaohusika, kwani kwa bahati mbaya kati ya Wajumbe wa tume walioteuliwa na Rais Mkapa hakuna mwenye Taaluma ya udaktari kisheria anayetambulika.

 

(Katika fungu No. 36) ripoti hiyo imeanza na maneno yasemayo “yaliyotokea nchini Tanzania mwezi wa Januari, 2001 kama yanavyoelezwa katika sehemu ya nne ya taarifa hii yanahistoria.  Ili kuyaelewa matukio hayo vizuri inabidi kuelewa japo kwa muhtasari historia ya kisiasa ya Tanzania.  Hivyo basi sehemu hii ya taarifa, itaelezea historia ya kisiasa ya Tanzania Bara na Zanzibar”.

 

Kwa maelezo haya haimpi taabu msomaji kuelewa kwamba dhamira ya tume ni kuwaeleza wasomaji wa taarifa yake kwamba matukio ya tarehe 26 – 27 yametokana na historia ya Tanzania ingawaje katika maelezo yake mambo mawili makubwa yamejitokeza kwanza kuhusishwa matokeo hayo zaidi na historia ya Zanzibar na sio Tanzania.

 

Pili, kuhusishwa kwa matukio maalum ya kihistoria yaliyoonekana kama ni matukio ya kiupinzani kwa chama cha ASP na baadae CCM, matukio mengine yoyote kinyume na hayo hayakupewa umuhimu si kwa Tanganyika wala Zanzibar.

 

Suala la kujiuliza hapa ni kwamba Je, matumizi ya historian a kuhusisha matukio ya tarehe 26 – 27 yalihitajika kiasi yalivyo tumika katika ripoti ya tume?

 

Ni kweli kwamba kila kitu kina chanzo chake.  Lakini Je! Ni kweli kua kila tukio jema au baya alitendalo mwanadamu wa leo huhusiana na historia ya maisha yake ya kale?  Taarifa yetu ya upembuzi, imeona kuwa tukio la Januari 26 – 27, 2001, halina uhusiano – ama na vyama vya zamani vya siasa au historia yeyote ile ya Zanzibar, hasa kisiasa.

 

Ni kipindi gain katika historia ya Zanzibar, polisi iliwahi kutumia nguvu, ushupavu wa kuchupa mipaka ya ubinaadamu au kuwapiga watu kwa kutumia “helicopter gunsfire”?

 

Iwapo ni hivyo basi wanadamu hawa wasingelibadilika milele na milele.

 

Maisha wangelikuwa watumwa wa historia zao na kamwe leo mwarabu na muafrika wa Zanzibar wasingelipata kuonana kwa ridhaa zao tena kwashangwe na vigelegele vya familia husika, kamwe Wana – Afro na wale wa vyama vyengine wasingelipatapo kushiriki siasa za upande mmoja kama ilivyo leo katika CUF na CCM Zanzibar.

 

Kwa mfano, watu maarufu kama Dr. Salmin Amour aliyewahi kushikilia nyadhifa za juu nyingi katika CCM na Serikali zake ikiwemo Urais wa Zanzibar kwa vipindi viwili; Umakamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano na hata Umakamo Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi lakini historia yake kisiasa na kiitikadi ni kwamba baba yake alikuwa Hizbu.

 

Kadhalika Jaji Mkuu wa Zanzibar Mhe. Hamid Mahmoud.  Hamid amekuwa mtumishi mzuri wa (SMZ na CCM).  Kihistoria, baba yake mzazi alikuwa Hizbu.

 

Katibu Mkuu wa Baraza la Mapinduzi aliyestaafu juzi juzi Bw. Mohammed Abdulrahman Machungwa, ambaye pia alikuwa mjumbe wa Tume ya Uchaguzi iliyosimamia na kuvuruga uchaguzi wa mwaka 1995 na wa mwaka 2000 ambapo matokeo yake hapana asiyeyaelewa.  Maalim Machungwa, kuna maneno ambayo hayajapata kukanushwa kwamba alikuwa Hizbu.

 

Kadhalika hata aliyekuwa Mwanasheria mkuu wakati wa Dr. Salmin Marehemu Ali Omar (maarufu kwa jina la Baba Ali) ukisoma historia aliwahi kuwa wakili wa kuitetea Hizbu Mahakamani ili kuinyang’anya Afro Shirazi kiti cha Uwakilishi.

 

Historia hiyo hiyo inatueleza kwamba hata baadhi ya Mawaziri ndani ya Serikali ya awamu ya sita, chini ya Amani Karume, inadaiwa kuwa wamo watendaji wenye chimbuko la U – hizbu.

 

Wanahistoria ya kiarabu na ki-hizbu lakini vile vile kwa upande mwengine hata baadhi ya wapiga debe wakuu wa kampeni za CCM kwa wananchi walikuwa ndio hao hao wapiga debe wa Hizbu wakati wa siasa za nyuma na wakitumia kauli au mbinu/mbiu za Hizbu katika majukwaa ya CCM na kamwe katika muda wote wa kuitumikia kwao CCM hawajapatapo kusikika juu ya majukwaa wakisema kidumu chama cha Mapinduzi.

 

Kila mara wakisema Kwaaaaacha!  Huku wana CCM na viongozi wao wakiitikia Kweupeee!  Hii ni kauli mbiu ya Hizbu ndani ya CCM miaka hii tuliyonayo.

 

Kwa upande wa pili katika Chama hicho hicho cha Mapinduzi, wapo watu waliotokana kimsingi na African Asossiation, Shirazi Asossiation, Comoro Asossiation, Umma Party n.k.  Umma Party ni chama kilichogawanyika kutokana na HIzbu”.

 

Na baada ya Viongozi wake ambao wamependeza mno ndani ya CCM na kushikilia nafasi kadhaa ni Mhe. Salim Ahmed Salim ambae aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa Chama hicho cha Umma Party.  Salim amewahi kuwa Waziri wa ulinzi na jeshi la kujenga Taifa, pia amewahi kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

 

Kwa kusema kweli hivi sasa hisia hizo za U – afro Shirazi, U-hizbu, Umma Party, U-afrika, Ushiriazi, Ungazija, Uwarabu, Uhindi, Ubwana na Utwana na mambo kama hayo yamebaki ni porojo za nganu za kale; kamwe hazipo na wala hazitokuwepo katika siasa za Zanzibar tena hazina nafasi na kuzikumbusha ni uchuro.

 

Kwani hata ukiangalia safu ya Uongozi katika chama kikuu cha Upinzani cha The Civic United Front (CUF – Chama Cha Wananchi) utaweza kuona ujenzi wa safu zake hauna tofauti na huo wa CCM wako waliotokana na Hizbu, Afro shirazi, Umma Party nk.

 

Wengi kati ya hao viongozi wa juu wametokana na Afro Shirazi na CCM kwani chimbuko la viongozi hao la kuanzisha harakati za upinzani visiwani lilianza ndani ya CCM yenyewe kutokana na kutokuheshimu misingi ya haki za usawa pia suala la Muungano kwa wakati huo lilikuwa na nafasi kubwa ya kuleta upinzani ndani ya CCM kama linavyoonekana kuendelea hivi sasa miongoni mwa wajumbe wa chama hicho tawala.

 

Na hili si kwa Wazanzibari pekee kwani lilichukua nafasi katika chama cha Mapinduzi na Serikali yake hadi kufikia Bunge la Jamhuri kwa ushawishi wa hoja za wale waliojiita G-55.  G-55 ni kundi lililoundwa na baadhi ya Mawaziri wa sasa na Wabunge mashuhuri wa chama cha Mapinduzi kutokea bara waliodai Bungeni Serikali tatu”.

 

Suala hili lilizuiwa na Chama cha Mapinduzi kwa hoja ya kwamba si sera yake ingawaje mambo hayo hayo yalikuwa yakilalamokiwa kama ni matatizo ya muungano leo yanatekelezwa chini chini kwa jina la kuimarisha muungano wakati huko nyuma kuzungumzia hayo ilikuwa ni uhaini.

 

Viongozi hawa wa CUF walioonekana kwamba ni wapinzani ndani ya CCM kiasi ya kamba Mwenyekiti wa CCM wa wakati huo J.K.Nyerere alipokuwa akihutubia Taifa juu ya ufukuzwaji wao katika CCM alitamka kwamba ni vyema wakafanye upinzania nje ya CCM.  Sasa leo unapowaita hawa Mahizbu unazungumzia nini?

 

Je, CCM kumbe ni Hizbu? Kwani hawa walitokea CCM.

 

Maana ya CCM kutumia neon UNITED FRONT katika jina lake ni kumaanisha kwamba ni muunganiko wa watu walio mstari wa mbele katika harakati za kudai ukombozi na maendeleo ya Mtanzania ambapo katika visiwa hivi, liliwajumuisha watu tofauti katika Serikali kwa wakati huo.

 

Kusema kweli kuna dalili zote au madai kuwa hata baadhi ya mawaziri wa sasa na viongozi wa CCM walikuwemo katika gurupu hili la FRONT LINERS wakati wa kuanzishwa kwake ndani ya CCM, na ni vyema tukawataja baadhi ya viongozi hao ili Tume ya Mhe. Mbita pamoja na Rais Benjamin Mkapa ambaye labda kwa wakati huo alikuwa Balozi Nje ya nchi wawaelewe.  Hii pia ni kwa faid ya Taifa ili kuondoa upotoshwaji wa historia ya kweli ya harakati za kisiasa ya visiwa hivi vya Zanzibar, baadhi katika hao alikuwemo Dr. Salmin Amour (Rais Mstaafu wa Zanzibar), Bregedia Adam Makanjuki (Waziri wa Sheria Pandu Hassan (Mwanasheria Mkuu wa SMZ hivi sasa), Mhe. Omar Ramadhan Mapuri (Waziri wa mambo ya ndani katika Serikali ya Muungano hivi sasa), Moh’d Mwinyi Mzale (Balozi wa Tanzania nchini Misri), Mhe. Abraham Issac Sepetu (Mbunge wa Jumuiya ya Afrika mashariki kwa tiketi ya CCM) ambae amewahi kuwa Balozi na Waziri katika wizara kadhaa za SMZ na wengine wengi ambao sitomaliza kuwataja hapa.

 

Suala lilikuwa ni mapambano ya Wazanzibari katika kudai hifadhi ya Utaifa wao na si venginevyo na ndio maana likawajumuisha watu wa pande zote za visiwa vya Zanzibar na dini zote na kwa upande wa wenzetu wa Bara G55 ilikuwa ni kudai heshima ya Tanganyika yao, hivyo maana ya hoja hii ni kwamba kila upande ulikuwa na hisia za kukandamizwa katika Muuungano uliokuweko baina ya Tanganyika na Zanzibar.

 

Swali zito linajitokeza, kwa kundi la G – 55, likiongozwa na akina Njelu Kasaka, Philip Marmo – haikuonekana kuwa ni upinzani  au uasi mbele ya macho ya Watanzania; lakini kitendo kama hicho, kinaonekana ni “uasi”, “usaliti” au “uhaini” wanapodai Wazanzibari.

 

Kwa Wazanzibari, hatukuona ajabu kubaini kuwa mtu kama Njelu Kasaka alipatiwa tunzo ya U- waziri badala yake au Philip Marmo kuwa Msaidizi wa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, lakini akina Maalim Seif Sharrif Hamad, Shaaban Khamis Mloo, Khatib Hassan, Ali Haji Pandu, Soud Yussuf Mgeni, Maalim Masoud  Omar na baadae wakafatia akina Hamad Rashid, Maulid Makame, Machano Khamis Ali na wenzao wengi, walifukuzwa CCM, na hatimaye baadhi yao kuwekwa Gerezani.

 

Kitu chengine muhimu cha kuzungumza hapa kuhusiana na maelezo ya historia yaliyotolewa na Tume ya Bregedia Jeneral mstaafu Hashim Iddi Mbita katika taarifa yao ni kujiuliza kwamba hivi utawezaje kuzuknguzia matokeo muhimu yaliyohusiana na harakati za  siasa kabla ya 26 – 27, 2001, ifike hatua ya kutaja kifo cha A. A. Karume (Rais wa kwanza wa Zanzibar), kuchaguka kwa hali ya hewa ya kisiasa Zanzibar wakati wa Rais Aboud Jumbe aliyekuwa Rais wa awamu ya pili Zanzibar, lakini Tume ikasahau walau basi kuwa katika historia hiyo hiyo mara baada ya Mapinduzi kwamba kuna watu kama kina Abdalla Kassim Hanga aliyekuwa Makamo wa Rais katika Serikali ya Afro Shirazi, Abdul – Aziz Twala aliyekuwa Waziri wa Fedha wa A.S.P au Jaha Ubwa; na Othman Sharifu aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini  Uengereza mara tu baada ya Mapinduzi ya 1964 ambao walipotea katika mikono ya Serikali.

 

Saleh Sadalla, Mdungi Ussi na hata Sheikh Mohammed Shamte aliyekuwa Waziri Mkuu wa mwanzo wa Zanzibar ambaye Serikali yake ilidumu kwa mwezi mmoja tu na kupinduliwa na Chama cha Afro Shiraz, wengine ni Muhammed Salim Jinja (babu yake Shadiya Karume), Jimmy Ringo. N.k.

 

Wakati wa Sheikh Mohammed Shamte, Zanzibar ilikuwa na Bendera yake, ilikuwa na kiti cha Uwakilishi Umoja wa Mataifa ambacho ndicho kinachotumiwa leo kwa jina la Tanzania, Zanzibar hiyo hiyo ilikuwa na Mabalozi wanaowakilisha nchi zao hapa kwetu zikiwemo ncho za Uengereza na Marekani, Ufaranza nayo Urusi kadhalika Uchina, India na Egypt pia Mabalozi wa Zanzibar katika nchi za nje walikuwepo.  Kwa mfano nchi ya Ufaransa ilianzisha ubalozi wake Zanzibar mwaka 1840.

 

Hata wakati wa utawala wa Karume (1964 – 72), Zanzibar ilikuwa na kadi za Uraia zilizokuwa zikitolewa kwa kila raia wake leo ukiuliza hayo utakuwa hupendi Muungano.

 

Ah! Zanzibar ilikuwa na mengi zaidi ya hayo.  Sasa utazungumziaje historia ya Zanzibar uyasahau hayo.

 

Nikifikiri watwani                   Zenjibari kuitaka

Nimepita Barani                      nchi nyingi nikafika

Nimebaki ziarani                     Unguja kuiepuka

Kila Nchi nipitayo                   Zenjibari yasifika

 

Sasa yachafusha moyo           Karibu tutatapika

 

Yanini kujionyesha                  Na kizuri hujulika

Japo ndani ya makasha          Na kufuli kubandika

Imekuwa fawahisha                Hakuna la kufichika

Zenjibari yashitusha               Mambo yanayofanyika

 

Wamegeuka kelbu                  hawana wanokumbuka

 

Wakasahau vitabu                  mola alivyotamka

Ikiwafika Ikrab                       Kipindupindu pinduka

Si mweusi si mwarabu            hapana ate epuka

Yaoneni yaoneni                      chonde chonde wahusika

 

AH! ZENJIBARI                   WAPI INAPOPELEKWA?              

 

Kuna wengin kati ya wana Afro Shirazi ambao kwamba walipotea na hadi hii leo Serikali yao wakati huo Afro Shirazi na sasa hivi CCM imeshindwa sit u kuwatunza jamaa zao kwani hawa walikuwa watumishi wakubwa katika Serikali na chama lakini hata taarifa juu ya vifo vyao zimeshindwa kutolewa hadi sasa.

 

Aidha kuna watu waliolewa kwa nguvu (hapa kwetu tukiita ndoa za vijiwe) ajabu ni kwamba watoto wao hivi sasa ni watu wazima na wengine wana madaraka makubwa Serikalini, vile vile wako watu walioekwa kizuizini kwa dahari ya miaka na kupata mateso makali na wengine kufia huko huko.

 

Kwa mfano, ukiwacha hao tuliowataja hapo juu hata aliyewahi kuwa mume wa Muwakilishi maarufu wa CCM kama Mvita Kibendera Bwana Suleiman Salim Suleiman alifia huko huko kiinuwa miguu, wakati maiti ya Baba watoto wake huyo inatolewa ndugu wa marehemu Bwana Moh’d Salim Suleiman alipishana nayo mlangoni akiingizwa machinjioni alikokufia kaka yake.  Kwa unyonge ulioje maskini nae hakutoka mzima.  Aidha Ami wa ndugu hao wawili aliyewahi kufungwa kwenye gari la Land Rover na kubururwa hadi kituo cha Polisi cha Mwera na baadae kupelekwa gerezani kwa kesi kama iliyowahusu wanawe hao alitoka gerezani na kukuta harakati nyingi za kisomo cha Arobaini ya marehemu mwanawe aliyekuwa mume wa Mwakilishi Mvita.  Maskini Bw. Huyu hakujuwa kwamba kule gerezani alikokuweko yeye alikuwa na wanawe wawili ambapo mmoja alifariki na ndiye huyo anayesomewa arobaini leo siku aliyotaka yeye gerezani unyonge ulioje!

 

Watu namna hii ni wengi hata kwa kuwataja huwezi kuwamaliza katika nafasi hii, lakini ndio historia hiyooo!!!  Wengine mpaka leo hii wako hai ingawa si wazima tena na wanavilema vya maisha pindi wakikusimulia mambo ya gereza kuu la Zanzibar, kwa Bamkwe kama waitavyo wenyewe (mlango wa nyuma au maarufu kwa Mandera) utashangaa kama watendaji na watendwaji baadhi yao sasa hivi ni maswahiba hiyo ndio Zanzibar.  Yote hayo hayakufanywa na mwarabu wala mzungu.

 

Wazanzibari ni weledi wa mambo na waungwana wa kusameheana sasa leo Tume ya Mzee Mbita inapotwambia mambo haya ni ya kihistoria mbona haikutueleza ni nani dhidi ya nani kwa sababu Mkoloni wa Ki sultani hayuko tena walioko ni hao hao Mussa Haji Kombo na Omar Ali Juma (hayati) ndo hao hao Said Rashid na Hamad Rashid Baba mmoja Mama mmoja vyama mbalimbali wakagombania kiti kimoja cha Ubunge katika Jimbo la Wawi huku wapiga kura wakiwa ni Ndugu zao wa damu na ukoo.

 

Mzee Mbita na wajumbe wenzako, mnayafahamu haya, na kuyaweka katika akili zenu?  Sasa hiyo historia ya chama alichokiwakilisha Hamad Rashid na Said Rashid itaathiri vipi kwa wapiga kura ambao ni damu yao ndugu zao wa ukoo.

 

Tunao wengi kama hawa katika visiwa vya Zanzibar kwa Mfano:

Watoto wa Mzee Mati katika Uchaguzi wa mwaka 1995 waliogombea kiti kimoja cha Uwakilishi katika Jimbo la Matemwe kupitia bwana Mun’go Mati Wadi chama cha CUF, Bw. Ame Mati Wadi aliyeshinda wa chama cha CCM, na bwana Dodo Mati Wadi wa chama cha TADEA.

 

Katika mazingira haya hatuone hiyo, historia ya Mzee Mbita na wajumbe wake impe hisia Mmatemwe za kumuona Mun’go Mati Wadi wa CUF anawakilisha Wakoloni wa Kiarabu nae Ame Mati Wadi wa CCM anawakilisha Wana wa Afro Shirazi.  Ni upumbavu ambao Wazanzibari hawatokubali kupakaziwa nao.  Tunaamini kwamba maelezo haya ya historia yaliyotolewa katika ripoti ya bwana Mbita na ambayo yamekuwa ni kawaida kutolewa katika kila ripoti zinazohusu serikali na chama cha Mapinduzi juu ya hali ya kisiasa ya Zanzibar na ambayo yalikuwa yakisemwa katika makongamano, katika semina, warsha na mikutano mbali mbali ya hadhara ya chama cha Mapinduzi yana ajenda nyengine zaidi ya yaliyoelezwa kwa Wazanzibari.

 

Kwani ukirejea maelezo ya hapo juu utaweza kuona kwamba siasa za mgawanyo kwa misingi ya vyama vya zamani basi zinaweza kuleta hisia za chuki hata miongoni mwa viongozi wa chama kimoja, kwa mfano CCM kwa CCM, CUF kwa CUF n.k. na wakatazamana kwa macho ya U-Hizbu na U-Afro, Umma Party, ZPPP n.k. zinaweza kuleta mifarakano baina ya wanandoa waliokwisha tukuu, watoto na wazazi wao ama wa kuukeni au wa kuumeni kama alivyo lielezea baraza la wawakilishi kwa uchungu mheshimiwa Mansour motto wa hayati Yussuf Himid hivi majuzi ambae Wazanzibari wanamuelewa vilivyo kwa namna anavyo chukia ubaguzi hasa huu wa Uuunguja na Upemba.

 

Kwa ufupi wa maneno tukiendekeza hayo itakua huyu “si mwenzetu” na yule “si katika sisi” kuanzia katika Siasa, biashara, familia, majirani, marafiki n.k.

 

Hali hii inatufanya tujiulize kwamba kumbe haja ya kuwagawa Wazanzibari kwa historia ya hadaa hata wakiwemo ndani ya CCM bado ipo na inaonekana kama ni sehemu ya ajenda ya falsafa  ya CCM?  Naam! Siasa ya “wafawe” na “uwatawale” inaendelea vizuri kumbe!

 

Kitu kimoja tunachoomba kukumbusha ni ule msemo maarufu unaosema kuwa Mtu mmoja anaweza kuudanganya Umma kwa mara moja lakini hatoweza kumdanganya mtu mmoja tu kila siku.  Aidha ni muhimu pia kujikumbusha ile kauli ya baba wa Taifa Mwalimu J. K. Nyerere kwamba mbaguzi ni sawa na mtu alie zowea kula nyama ya mtu, akianza kamwe hatoacha kula nyama ya mtu mpaka atiwe kaburini.  Pia maoni ya walimwengu wenye elimu zao juu ya falsafa za viumbe wanatueleza kwamba ukitaka kumsoma mtu mtazame vitendo vyake au kutokana na maneno yake.  Hivyo nadhani kwa hili Watanzania tumejifunza mengo juu ya dhamira ya tume na serikali yetu.

 

Kwa ujumla hayo ni baadhi ya mambo ya wakati huo unaoitwa muda mrefu kwa maelezo ya Tume ya Bwana Mbita lakini haya ya juzi jee?  Nayo pia tume haikuyaona au historia ni lazima ipitiwe na awamu tano za uongozi ndio iwe historia, maana masuala ya kuvunjiwa watu nyumba, kesi za kubuni, hasa ile ya uhaini, kwa viongozi waandamizi 18 wa CUF; watu kulishwa mavi, kunajisiwa kwa watoto wa kike, kufukuzwa kazi, migomo ya wanafunzi na mengineyo, kuwa haya kwa uoni wa Tume ya Bwana Mbita hayana mchango wowote katika Maandamano ya Januari 2001 ni kichekesho kikubwa!!!

 

Ukitaka kuzungumzia historia kuhusiana na jambo lolote ni lazima ukubali ukweli japo kuwa unachoma.  Lakini pamoja na hayo yote kitu muhimu chengine cha kujiuliza hapa ni kuwa matokeo haya yaliyohusiana na harakati za kisiasa kabla ya tarehe 26 – 27/01/2001 Zanzibar, pia yanamahusiano na kuandamana kwa Watanganyika.

 

Kukataa hayo, ni kubainisha kuwa kwa nini Tume haikueleza matukio kama hayo ambayo pia yalichochea hisia za Watanganyika kuandamana tarehe hiyo.  Au hawa ilikuaje hata wakaandamana?  Hapa inazidi kutia shaka Mzee Mbita na Tume yako.  Hivi ni kweli kuwa katika kumbukumbu za Tume yenu matukio yaliyotokea Tanganyika hayakuweza kuwa na uzito kama haya ya Zanzibar katika maelezo yenu?

 

Kwani kumbukumbu zinaonyesha kwamba:-

 

Katika mwaka 1964 huko Tanganyika kulitokea Uasi wa jeshi dhidi ya Serikali pia mpango mwengine wa kutaka kuipindua Serikali ya Julias Nyerere ulikuwepo mwaka 1969 – 1970, uliowakilisha Mejar Wiliam Makori Chacha, Bibi Titi Moh’d, Alfred Millinga, Elia Chipaka, Dunson Lifa Chipaka na wenzao, kadhalika mpango kama huo ulikuwepo tena mwaka 1974 wa kutaka kuipipndua Serikali kabla ya ule wa mwaka 1982 uliowashirikisha Khatib Ghandi, Mohammed Tamimu na wenzao bila ya kusahau kwamba katika mwaka 1971 kulichawanywa makaratasi ya kuipinga Serikali wakati wa maadhimisho ya miaka kumi (10) ya uhuru wa Tanganyika tena kwa ndege.

 

Haya ni baadhi ya mambo yaliyokuwa juu ya kutolewa hadharano.  Yapo tele ambayo yamefichika lakini.  Lakini Tume imeona suala la kuchafuka kwa hali ya hewa ya kisiasa ya Zanzibar (1984) wakati wa Aboud Jumbe tena ndani ya Chama kimoja kuwa ni katika mambo muhimu yaliyochochea hisia za watu kuandamana na yakasahauliwa yale yote yaliyotokea bara labda kwa vile yametokea Tanganyika; lakini si Tanzania?

 

Vile vile, ili kukamilisha japo kwa wastani historia ya matukio ya kisiasa kabla ya tarehe 27 Januari 2001 kwa upande wa Tanganyika kama ilivyoandikwa katika ripoti ya Tume ya Bregedia Jeneral mstaafu Hashim Mbita ni vyema pia ripoti hiyo kwa maoni yetu japo kidogo ingeliyaeleza mambo yafuatayo ambayo tunayaamini yanamahusiano na matukio ya kisiasa ya muda mrefu kwa Tanganyika kabla ya maandamano ya tarehe 27/01/2001

 

Kwa mfumo katika mwaka 1967 watu kadhaa akiwemo Bwana John Rupia, Bwana Said Chaurembo na wenzao walinyang’anywa mali zao wa kisingizio cha kutekeleza Azimio la Arusha, kadhalika katika mwaka 1983 Operesheni kama hiyo ya Serikali ya kuwanyang’anya watu mali na wakati mwengine kuwaweka hata kizuizini kwa kisingizio chengine cha wahujumu uchumi yalitokea.

 

Vile vile, kati ya mwaka 1976 – 1977 wakati wa zoezi la kuanzishwa kwa vijiji vya ujamaa, maarufu kwa jina la (Operesheni Vijijini) watanzania kadhaa walipoteza maisha wakati wa zoezi hilo tena kinyama kwa kuliwa na samba, kufa kwa njaa, maradhi n.k.

 

Hapana atayesahau kauli ya marehemu Baba wa Taifa, Julius Nyerere, alipokuwa Rais wa Tanzania  ya kufunga mkanda kwa miezi kumi na nane (18) ili kufufua na kuinua uchumi wa Tanzania ulioanguka na kudorora baada ya vita vya Uganda vya kumuondoa nduli Amin na katika vita hivyo pamoja na vita vingi vya Ukombozi wa Afrika ndugu zetu kadhaa walipoteza maisha na wengine kubakia vilema.  Malipo yao yalikuwa “ahsante”.

 

Mhe. Mbita, kwa sababu ulikuwa ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ukombozi Afrika unalielewa sana suala hili, ingawa katika ripoti yenu hamkuona umuhimu wa kulieleza kama ni moja kati ya matukio muhimu ya kisiasa kabla ya 27 Januari 2001.

 

Mambo mengine ambayo hisia zake kwa watu mpaka leo zimo ndani ya mishipa yao ya hisia na damu na kila inapochemka ama kuja juu wanaitazama Serikali ya CCM kwa kuhusika na hayo ni pamoja na vifo vya baadhi ya viongozi muhimu wa taifa na ambavyo vilitatanisha katika kutokea kwake, na au maelezo yaliyotolewa na Serikali yasikidhi haja kwa wananchi.

 

Kwa mfano, wakati wa vita vya kupambana na rushwa vilivyoendeshwa na aliyekuwa Waziri mkuu wa zamani wa Tanzania Hayati Edward Moringe Sokoine ambaye alifariki kwa ajali ya gari akitokea Dodoma.

 

Mazingira ya kifo cha Sokoine, yamebakia kitendawili, na kutatanisha.  Pamoja na kumtoa machozi Julius Nyerere , bado machozi yake hayajaleta jawabu kidogo.

 

Vita hivyo vya rushwa hadi leo ni donda ndugu kwa nchi yetu wasiwasi wetu ni juu ya usalama wa watu kama Mbunge wa Makete Bwana Hastine Kitine alivyoamua kujitokeza hadharani kukemea vitendo vya rushwa kwa wazito kwamba ataweza kuhimili matoke yake akiwa ndani ya CCM?  Vita iliyoshinda wenye mbawa.  Pia tupige jicho katika ripoti ya jaji Jaseph Warioba kuhusu rushwa hadi leo imebakia ni kumbukumbu kwenye mafaili isiyofaa kufanyiwa kazi wala kutolewa hadharani.

 

Kuna kifo cha Marehemu Horace Kolimba aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM ambaye alitamka wazi kwamba, “CCM haina Dira” na imepoteza muelekeo ghafla akaitwa Dodoma kuhojiwa tukasikia nae kupasuka mshipa wa damu na akafariki.

 

Kwa sababu serikali yetu ilitoa taarifa “sahihi” zilizotokana na uchunguzi wa kitaalamu juu ya kifo chake, na zaidi Chama chake mwenyewe ambacho alikuwa anakiongoza, hatukuweza kupinga kitu.

 

Lakini kuna kifo cha David Mwaikambo aliyekuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM ambaye nae pia alifariki kwa ajili ya gari siku chache baada  ya mkutano wake wa hadhara hapo Mwembe Kisonge Mjini Unguja.

 

Bwana David Mwaikambo aliwaambia wakereketwa wa CCM Zanzibar, kwamba ikiwa hawaelewi Sera za CCM basi wajue kwamba CCM nia yake ni Serikali mbili kuelekea moja maskini Mwaikambo alipotea katika mazingira yenye utatanishi mkubwa!

 

Mwengine ni Jeneral Imrani Kombo aliyekuwa mkuu wa usalama wa Taifa Tanzania aliyeuliwa na Polisi “Kwa bahati mbaya” kwa kile kilichoelezwa kuwa alidhaniwa kuwa ni “mwizi wa gari” Jambazi Sugu.

 

Vifo hivyo vyote vinamahusiano mazito na matukio ya kisiasa kwa sababu vimewahusu watu na wanasiasa wazito wenye nafasi kubwa katika jamii, tena wengine baada ya matamshi au matukio mazito waliyoyatenda.  Mazingira ya vifo vyao, yana wasiwasi kuwa yalitokana na kauli au matendo yao ya awali.

 

Sasa haya hayawezi kuwa kichocheo kwa wapenzi na wafuasi wao kuipinga Serikali iliyoko madarakani na kuwaona kuwa ni wauwaji wanaostahiki kuondolewa?

 

Ukiachilia mbali mauwaji kama ya Mwembe Chai, Bulyanhulu, Mirerani, Mbeya [vifo vya mahabusu] na vifo kama vya M.V Bukoba, ajali ya treni na vifo vyengine kadhaa vinavyosababishwa na uzembe wa Serikali au mabavu yake hata view si vya kisiasa haviwezi kuwapelekea watu kuichukia serikali hiyo na kutamani kuibadilisha?

 

Matukio mengine ni kama yale ya kukimbilia nje ya nchi Bwana Oscar Kambona, aliyekuwa waziri wa mambo ya nje awamu ya kwanza ya serikali ya Tanzania (Tanganyika) katika Serikali ya Nyerere, kukimbia huko kwa Kambona kulinasibishwa na vituko vya Azimio la Arusha.

 

Wananchi walifundishwa kuimba nyimbo kadhaa za kumkashifu Kambona kama vile “KAMBONA AMEOLEWA..!  WAPI…! HUKO ULAYA..! WIVU… WAMKEREKETA” na mambo kama hayo.

 

Nako kuwekwa ndani watu kama Bibi Titi Moh’d, James Kabalo Mapalala, Christoper Kasanga Tumbo, Chief Abdalla Said Fundikira na wenzao wengi na hata baadhi yao kuhamishiwa magereza tofauti wakati wa utumishi wao wakiwa gerezani kama alivyofanyiwa Mzee Mandela wa Afrika ya Kusini na Makaburu.

 

Haya nayo ‘ni matukio ya kisiasa kabla ya tarehe 27 Januari 2001 yaliyotokea huko Tanganyika ambayo Tume ya Bwana Mbita hawayakuyaona wala hawakuhisi umuhimu wake.  Kwamba nayo yanaweza yakawa na mchango wa mabadiliko kwa mwenendo wa siasa za nchi yetu hasa Tanganyika?

 

Nayo mambo ya uendeshaji Serikali ukizingatia mabadiliko ya Katiba, utoaji haki katika vyombo vya Sheria na Muungano kwa jumla kwa yakini hayawezi kupuuzwa.

 

Kwa mfano, suala la kukiuka misingi ya Muungano na kufikia mambo zaidi ya ishirini na saba (27) likiwemo lile la kuondoshwa Rais wa Zanzibar, kuwa Makamu Rais wa Jamhuri ya Muungano, chini ya mabadiliko ya kumi na moja (11) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, kwa kisingizio cha kutengeneza protokali.

 

Aidha mawazo ya utatu, uwili au umoja wa Serikali yaliyofikia hata Wabunge wa CCM kupitisha Azimio la kuanzisha Serikali tatu ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano na likapigwa na aliyekuwa Baba wa Taifa katika Chama nayo ni matukio muhimu ya kisiasa kabla ya tarehe 27 Januari 2001 yaliyotokea Tanganyika ambayo hayawezi kuyahakikisha CCM imani na mapenzi ya watu juu yake hata viongozi waliomo ndani yake.

 

Sasa iwe yote haya hayana hisia zozote kwa Watanganyika katika siasa za Tanzania nap engine kuhusika na matokeo ya tarehe 26 – 27 kama ilivyo Zanzibar?  Au ndio kusema zumari ikipulizwa Zanzibar watimkao ni watu wa Ziwa Tanganyika?

 

Inawezekana sana ikawa hivyo iwapo Tume itakubaliana nasi kua Watanganyika wawe ni watu wenye  sahau na wanaodanganyika haraka.  Labda iwe hivyo! Na Wanzania wawi ni watu wenye visasi, na wanaopenda wapigano?  Labda iwe  hivyo pia! INGAWA HATUFIKIRII HASA KWA WAKATI TULIONAO.

 

Kama si hivyo hakuna sababu ya kueleza kuwa historia ndio chanco miongoni mwa vyanzo muhimu vya maandamano na matukio yake kwa upande wa Zanzibar.  Lakini historia hiyo hiyo na ikawa kwa Tanganyika haina umuhimu wala mahusiano na maandamano hayo.

 

Mwenyekiti Mbita na tume yako munapotueleza kuwa historia imechangia kuwepo kwa maandamano ya matukio yake hivyo pia mnataka tuelewe kwamba kwa upande wa pili wa shilingi serikali katika kuzima maandamano hayo nayo ilikuwa ikijua kwamba inapambana na mabaki ya wakoloni na historia ilikuwa mbele ya Macho yao? Alaa ndio maana Zanzibar wakauliwa watu kama kuku?  Na huku kusikokuwa na historia ambapo watu waliandamana kwa bahati mbaya Serikali hiyo hiyo ikaona hapana haja ya hayo ya kuuwana!

 

 

Nadhani Mtanganyika na Mzanzibari wa leo kumpa sifa hizo za kushiriki jambo kwa hisia za kale ambazo yeye alikuwa hajazaliwa ni kumdhalilisha tena kumdhalilisha sana na ndio kusema katika suala hili  historia haikuhitajika.

 

Zaidi ni kwamba Bwana Hashim Mbita na tume yako mwakumbusha kilio matangani tena mbaya zaidi wafiwa wengine wamo serikalini hivi kweli tutafika kwa kufufua makaburi, na kufikia vilivyokufa?

 

Kwa maneno mengine Bwana Mbita na wajumbe wenzako hamkuwatendea haki pia Watanganyika kwa kutokuwaeleza yale muliyoyaona huko kama ni miongoni mwa sababu za muda mrefu.  Napia mumewadhalilisha Wazanzibari wao kwa kuwahusisha na mambo yasiyowahusu mambo ya kale.

 

Mbona katika maandamano hayo kuna watoto ambao wazee wao kwa asili na hata wao wenyewe ni wana wa Afro, waliandamana na wakafa?

 

Hivi huyu Ali Haji Kombo ndugu yake Mussa Haji Kombo – baba/mama mmoja waijua nasaba yao na Afro Shirazi au ndio maana Tume ikapata kigugumizi katika kukitambua kifo chake maana huyu ndio mtu wa mwanzo aliolimbua risasi ya polisi katika mji wa Chake chake hapo Machomane, Pemba mbele ya hadhara ya watu kwenye kina cha maandamano ya watu wasiopungua alfu tano (5000), maiti yake ilifikishwa katika hospitali ya Chake kabla ya mazisho.

 

Kwa bahati mbaya ripoti ya Tume haituonyeshi ni wakoloni wangapi walioandamana?  Maana haya kwa maelezo ya tume yalikuwa ni maandamano ya ukombozi kwa watu kutaka kurudisha utawala wa zamani kutokana na hisia zao za kale.

 

Sasa hawa akina Said Miraj (Wangoni), Machono Khamis, Juma Duni (Watumbatu) na Waafrika  wenzao hivi tuseme nini juu ya kuandamana kwao.

 

Nao akina Ali Haji Pandu na Shaaban Khamis Mloo leo hawa si Waafrika tena ? wala si wana wa Afro asili?  Acha huko, huyu Mwenyekiti Lipumba, Profesa wa Uchumi kumbe nae ni Mnyamwezi wa Kiarabu?  Hili lilikuwa halijulikani kabla ya ripoti hiii ya Tume ya Mbita.

 

Leo huoni ajabu kama utasikia Ali Haji Pandu aliekuwa jaji Mkuu Zanzibar na wakati mmoja kuwahi kusikiliza kesi ya uhaini alipouliwa Karume mwaka 1972 wakati Jaji  W. Dorado akiwa mwanasheria wa serikali na mwendesha mashtaka Mkuu kwamba wanaweza kuketi meza moja na mtu ambaye wakati huo akiitwa haini na alihukumiwa kifo kama Mzee Miraj Mpatani?

 

Basi hayo ndiyo yaliyopo Mzee Mirah Mpatani, Baramia (kikono), Mussa Shaaban (marehemu) na wenzao wengi leo ni maswahiba wakubwa katika CUF na kina Mzee Ali Haji Pandu.

 

Wote hao wanaipinga CCM?  Nadhani siasa za Zanzibar bado hazijaeleweka hata kidogo.  Na ilifikiriwa kwamba Tume ya Bregedia Mbita labda ingeiweza kusaidia lakini ndio imekuwa kichocheo cha kupotosha matumizi yake.

 

Na hii historia ambayo hufichwa fichwa kwa makusudi kwa ajili ya kupotosha ukweli sasa imefika wakati wa kuisema wazi kwani utazungumzaje historia ya Zanzibar na usherekee Mapinduzi matukufu ya Januari 12/1964 lakini usahau tarehe 10 Disemba mwaka 1963, wakati Wazanzibari walipopewa Uhuru wao kutoka Mkoloni kabla ya Tanganyika tena bila ya kumwaga damu au kwa kuwa ulipatikana katika mikono ya watu ambao ukiwaita unatumia neon Sheikh akina Sheikh Mohammed Shamte na wenziwe? Lakini huo ndio ukweli wenyewe!

 

Kila mwaka Watanganyika wanasherekea tarehe ya uhuru wao lakini uliza kuhusu Wazanzibari utadhani jambo hilo muhimu halikupita katika historia ya maisha yao wameuduna duu!  Kwa kumridisha “Bwana mkubwa” labda kwa hii “kejeli” ripoti ya Mbita NDIO SUALA HILO LITAANZA KUZUNGUMZWA SASA KINAGA UBAGA.

 

Aidha utazungumzaje hayo Mapinduzi ya mwaka 1964 na usimtaje mtu kama John Okelo ni kichekesho!

 

Jambo jengine katika historia ambalo ni muhimu kulizungumza katika uchambuzi huu ni pale ripoti ya Tume inapoeleza kwamba miongoni mwa sababu za kupigwa marufuku kwa vyama vingi katika visiwa vya Zanzibar na kuifanya Afro Shirazi kiwe ni Chama pekee cha siasa kwamba ilikuwa ni kwa nia ya kufuta hisia za kikabila na ubaguzi wa rangi pamoja na mambo mengine ambayo yalitajwa.

 

Shaka inayoyojitokeza katika hoja hii ni kwamba, Bwana Mwenyekiti na wajumbe wa Tume mumepata kujiuliza juu ya vitendo vya Chama hicho cha Afro Shiraz kuwagawa Wazanzibari katika masuala ya ajira ndani ya vyombo vya ulinzi na usalama, mgawanyo wa madaraka kwa misingi ya uzawa na hata suala nyeti la Elimu kwani iligaiwa kwa kuzingatia asili ya mtu na kabila lake kulikuwa na asilimia za waafrika mbali, wangazija mbali, wahindi mbali na waarabu mbali, hapana asiyelewa kwa mujibu wa visiwa hawa wote kwao ni Zanzibar.  Tena haya ya kugawana asilimia yalitokea wapi?

 

Jee haikuwa kuwabagua?  Au ubaguzi ni mbaya ukifanywa na Mkoloni tu?  Sawa na

Mfano wa hadithi ya raiya anapouwa Simba huitwa “jangiri” na kuambiwa ameuwa mnyama pori anayeifadhiwa hata kama samba huyo alitaka kuhatarisha maisha yake, lakini kinyume chake “Bwana mkubwa” anapouwa mnyama huyo huyo huambiwa kuwa ameuwa mnyama hatari na amenusuru maisha ya watu wengine ah, ni miujiza!

 

Ukweli ni lazima tuukubali kwamba polisi wetu wamezoea kutumia risasi mara kadhaa na kuua, ama kujeruhi watu kwa visingizio mbali mbali lakini haya ya tarehe 27 maji yalizidi unga.

 

Kwani katika historia ya Zanzibar Polisi wameshawahi kuuwa watu mara kadhaa na ukweli usio katalika ni kwamba rekodi ya vifo vilivyo tokea katika mikono ya dola katika Zanzibar tokea mwaka wa 1964 hadi leo mwaka wa 2003 ni kubwa zaidi kuliko hata ya wale waliokufa kwa ujambazi.

 

Kwa mfano katika mwaka 1988, wakati wa harakati za Maandamano ya kupinga kauli ya mama Sophia Kawawa ya kutaka kitabu kitukufu cha QUR’AN kibadilishwe katika baadhi ya mambo yanayohusu wanawake wa kiislam na mirathi, polisi Zanzibar, waliuwa na kujeruhi baadhi ya watu wengine hadi hii leo ni vilema.

 

Ubingwa wa polisi ulionekana zaidi kule Shumba Mjini walipomuua Marehemu Omar Ali Haji mwaka 1992, kwa madai ya kupachika bendera ya CUF baada ya Chama hicho kupata usajili rasmi na kusingizia kwamba risasi ilipigwa hewani lakini ikarudi na kumpiga yeye tumboni na mwanawe katika sehemu za siri, na baadae kuuwa.  Hii ni sawasawa na ripoti yako Mhe. Mbita juu ya mauaji ya tarehe 27 Januari 2001 unatueleza kwamba ufundi huu ulitumika tena wa kupiga risasi juu na kuuwa watu chini ufundi ambao huwezi kuupata mahali pengine duniani.

 

Kwa maneno mengine, suala lote la kuhusisha historian a matukio ya tarehe 26 – 27, 2001.  Hasa kwa Zanzibar ni sawa na kutafuta kisingizio cha hadithi ya Simba na mwana wa kondoo ili apate amle nyama.

 

Tukirudi katika uchambuzi wetu hebu na tuangalie (fungu no. 145) la ripoti ya Tume ya Bwana Mbita ambapo anaeleza kwamba Chama cha CUF katika kuonyesha ubingwa wake wa kukataa matokeo ya Uchaguzi iliyakataa matokeo ya Uchaguzi ya mwaka 1995, jambp ambalo lilileta mgomo kwa Wawakilishi wa CUF kuingia katika Baraza la Wawakilishi.

 

Kama Tume ya Bwana Mbita ilikusudia kueleza ukweli juu ya suala hili katika ripoti yake mbali na CUF na taasisi kadhaa za uangalizi kupinga matokeo hayo lakini pia katika barua yake kwa MWenyekiti wa Tume ya Uchaguzi wa Zanzibar kwa wakati huo Bwana Zuberi Juma Mzee, Naibu Katibu Mkuu wa CCM kwa wakati huo ambaye pia alikuwa ni Waziri wa Mambo ya Ndani wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Bwana Ali Ameir Moh’d kwa barua yake yenye Ref. No. CCM/AKZ/U.30/21 ya tarehe 25 October 1995 iliyonakiliwa kwa Jaji Lewis Makamo Mwenyekiti wa tume ya Taifa ya Uchaguzi, Mabolozi wote wanaowakilisha Nchi zao Tanzania, waangalizi wa Uchaguzi wa ndani na nje ya nchi na waandishi wa habari, Mheshimiwa Ali Ameir alieleza matokeo yake na hivyo kutokana na kasoro walizozitaja katika barua hiyo wakakataa matokeo yatakayotangazwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kwa wakati huo.

 

Hii ni kwa sababu CCM ilishaarifiwa au kupata fununu juu ya kushindwa kwake vibaya na CUF katika Uchaguzi huo, cha kushangaza baada ya Tume kubiruwa mambo mpaka yakenda kinyume na matakwa ya Katiba ili kuipa ushindi CCM.

 

CCM hiyo hiyo ikayakubali matokeo hayo, hapa kama Tume iliona ni vyema kuelezea kwamba CUF ilkataa matokeo ya uchaguzi ya mwaka 1995 na kukataa kwake huko kukapelekea kasoro kubwa katika siasa za Zanzibar basi katika msingi wa mizania ya haki, tume ya Bwana Mbita, ilipaswa pia kueleza katika ripoti yake hiyo kwa kina kwa nini CUF hawakuutambua uchaguzi huo kuliko kuitupia mzigo kwamba CUF ilikataa tuu, na tunasema haya kwa sababu tume wakati ilipoonana na baadhi ya Viongozi wa CUF ilikabidhiwa taarifa ya maandishi inayo elezea kwa nini CUF haikuitambua serikali ya Salmini Amour na matokeo yaliyo tangazwa na tume kuhusu uchaguzi huo wa mwaka 1995.

 

Kadhalika katika (fungu la 148, 149 na 150) la ripoti “yetu” kutoka kwa Bwana Mbita na wajumbe wenzake inaeleza kwamba kuliwahi kuundwa na kutolewa ripoti ya wataalamu iliyoandikwa katika mwaka 1998 kufuatia haja ya kurekebisha kasoro zilizotokea katika Uchaguzi Mkuu 1995.  Serikali hiyo hiyo mwaka 1998 iliunda kamati ya kuratibu maoni kuhusu katiba ambayo kazi yake ilikuwa ni kuwasilisha kwa Watanzania maudhui ya waraka wa Serikali No. 1 wa mwaka 1998.

 

Miongoni mwa mapendekezo ya Kamati ya Wataalamu ni pamoja na kuanzisha daftari la kudumu la wapiga kura, kuanzisha Tume ya Haki za Binaadamu na Utawala bora kwa ajili ya kuhamasisha nchini hifadhi ya Haki za Binaadamu lakini hayo nayo kwa wakati huo yalipuuzwa.

 

Jee! Kudharau haya Tume haikuona kama kuemchangia matatizo ya Uchaguzi wa Zanzibar 2002 ambayo baadaye yameleta majanga ya Januari 2001?

 

Kitu kingine kilichopaswa kutupiWA macho na kuangaliwa kwa undani katika ripoti ya Bwana Mbita ni juu ya suala la Muafaka wa Juni 1999 ambao umeelezwa kwa paragrafu mbili tu (151 na 152) na kuhitimishwa kwa (kifungu cha 153) chenye maneno kumi na mbili (12) yenye herufi sitini na nane (68) na tarakimu nne (4) tuu.

 

Yanayosema hivi Muafaka huu haukuweza kutekelezwa kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2000”.  Tofauti na historia iliyochukua mafungu tele katika ripoti hiyo labda ni kutokana na umuhimu wake! lakini mtazamo wetu sisi ni kwamba Muafaka huu ulipaswa kuelezwa kwa kina kuanzia chanzo na chimbuko lake hadi kumalizia na kukwama kwa utekelezaji wake kwani lau kama Muafaka huu ungelitekelezwa ni imani yetu kwamba ya 2001 yasingelitokea kamwe.

 

Kwa sababu Tume haikuyaeleza hayo tena si kwa bahati mbaya ili kwa kusudio la kuwafanya watu wasielewe kinachoendelea na kwa kuondosha uzito wa suala hili basi katika uchambuzi huu japo kwa maneno machache tumeamua kulizungumzia suala hili ili yale yote yaliyoelezwa na tume kuwa ni vyanzo vya matukio ya tarehe 27 Januari 2001 yawe ni ya muda mrefu ama mfupi mazito au mepesi kuonyesha kwamba yangeliweza kumalizika na kusahauliwa kabisa iwapo Muafaka huu ungetekelezwa.

 

Ushahidi wa hayo ni huu ufuatao:

 

(1)               Katika uongozi wa Zanzibar wa awamu ya tatu (3) iliyoongozwa na Sheikh Ali Hassan Mwinyi, akiwa Rais wa Zanzibar na Maalim Seif Shariff Hamad, Waziri Kiongozi wake katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika uongozi wao viongozi hao pamoja na hayo yote yaliyodaiwa na Tume ya Mhe. Mbita kama ni vyanzo vya muda mrefu na yale tuliyo kumbusha sisi baada ya wao kuyasahau yalikuwa yameshatokea lakini Wazanzibari waliweza kuishi vizuri kwa mapenzi na mashirikiano bila ya tofauti zozote za dini, rangi, kabila, kipato, mahali mtu alipotoka, jinsia au vyengine vyovyote.

 

(2)               Hata baada ya utawala wa awamu ya tano wa Dr. Salmini Amour utawala wa vishindi, kejeli, kiburi, majivuno, manyanyaso, maonevu na vituko kadhaa wakadhaa katika utawala ambao watu walidhulimiwa, wakauliwa, wakiteswa, wakaharibiwa mali, wakawekwa vizuizini na mambo kadhaa wa kadhaa.  Wazanzibari hawa hawa huku wenzao kumi na nane wakiweko gerezani kwa tuhuma za kubuni za Uhaini walishirikiana pamoja katika kunywa kahawa na chai huko Ikulu na kutia saini za kuwafikiana.  Haya si zamani ni juzi tu Juni 1999 baada ya usiku mmoja tu nchi ilibadilika watu wakasahau yaliyopita nuru ikazagaa na upendo ukachipua tena.  Sasa iweje kwa kutokutekelezwa Muafaka huo na hali ikachafuka kuliko mwanzo waliozuia muafaka huu usitekelezwe wasiwajibishwe lakini hili Tume ya Mhe. Mbita haikuliona kama ni sababu na badala yake wakaona ya mwaka 1964 ambayo yalifutwa 1999 na Muafaka wa mwanzo.  Hii inadhihirishwa wazi kwamba chuki baina ya wazanzibari ni jambo la kupandikizwa na sio suala la kudumu kwao.

 

(3)               Lakini kama ni jambo la kumfunza mtu basi Tume ya Bwana Mbita ingejifunza na huu muafaka wa 2001.  Je, ni nani aliewalazimisha Wazanzibari washirikiane?  Ni  nani aliyewalazimisha Wazanzibari wapendane?  Ni nani anayewaongoza Wazanzibari kuheshimiana?  Pamoja na masuala mengine mengi ambayo majibu yake yanaweza kusaidia kufafanua kwa nini yalijiri mambo ya watu kutokuzikana, kutokuendeana harusini, kugomeana katika biashara, kutukanana, kuonana maadui n.k.

 

Katika (fungu la 151) ambapo Tume inaarifu kwamba pamoja na Wawakilishi wa CUF kugomea vikao vya Baraza, CUF (1995 na 2000) pia walifanya kampeni ya kusimamisha misaada ya wafadhili kwa Zanzibar kauli kama hii si ngeni masikioni mwa watu na wanajulika ni kina nani wanaopenda kuitumia lakni inashangaza unapoona tume kama hii, kuona kwamba ni maneno yafaayo kuandikwa katika ripoti yake kwani watumiaji wa mwanzo wa maneno haya waliyatumia kama propaganda ya siasa, lakini fikra zetu ni kwamba wenye akili zao timamu wanaelewa kama misaada kwa nchi haizuiwi kwa maneno ya watu tu, Wahisani na wafadhili wanavigezo vyao katika kutoa na kuzuia misaada yao.

 

Pamoja na tume katika taarifa yake kueleza athari ya Wawakilishi wa CUF kugomea vikao vya Baraza kua ni pamoja na wananchi wengi kukosa uwakilishi lakini hawakueleza juu ya sababu za msingi za uamuzi huo na hata kama wangelishiriki ni faida gain ambayo wangeliipata wananchi hao katika mfumo huu wa utawala tulionao leo.

 

Je, tume hii ina maoni gain kuhusu kitendo cha Bunge la jamhuri ya Muungano wa Tanzania pia Baraza la Wawakilishi la Zanzibar cha kupitisha sheria ya kuwanyima wananchi hao hao wa Pemba waliosiitikiwa na tume kwa kutokuwakilishwa na wajumbe wao waliowachagua kwamba wakae nje ya vyombo hivyo vya kutunga sheria kwa miaka miwili ndio uchaguzi urudiwe?

 

Hivi ni nani asiyejua kwamba sheria hio ilitungwa kwa kuwakomoa CUF na si kwa maslahi ya wananchi?  Au hili halina athari kwa wananchi ya kukosa uwakilishi katika vyombo vya kutunga sheria?  Au tume haikutaka watu walielewe hilo?

 

Kimsingi uamuzi huu wa CUF ulitokana na kupigania demokrasia katika nchi na kudai mabadiliko kwa njia za amani na ustaarabu.

 

Katika (kifungu cha 164) tume imeandika kuwa muelekeo wa wananchi wa kawaida kuhusu kurejewa kwa uchaguzi wa mjini magharibi peke yake kulitegemea mwelekeo wao kisiasa hii ni hoja isiyo na msingi kwa maisha ya kikwetu vyama vilivyojitokeza awali kulumbana ni CCM na CUF labda kwa kua ndio waliokua washiriki wkauu wa uchaguzi huo lakini pia mbona hata waangalizi wa ndani na nje ya nchi kama vile TEMCO, Common wealth, FIS walitoa misimamo yao juu ya uchaguzi huo na wakatamka bayana kwamba uchaguzi huo umevurugwa na inapaswa urejewe upya tena kwa nchi nzima.

 

Jee hawa nao walikuwa ni washabiki wa vyama vilivyokua vikishindana yaani  CCM na CUF.  Jee! Vyombo vya habari vya nchini na nje ya nchi ambavyo pia viliripoti na kutoa maoni yao kuhusu uchaguzi huo huo na kutaka urudiwe Je, hawa nao maoni yao yalizingatia msimamo ya vyama vya CUF na CCM?

 

Kwa nini tume pia haikutueleza kitu kuhusu maoni ya mabalozi na nchi wahisani (wafadhili) waliyoyatoa kuhusu uchaguzi huo na kasoro zake kua nayo yanamisimamo na mielekeo ya vyama vya CCM na CUF au laa?

 

Ukweli utabaki ni ule ule kwamba uchaguzi uliharibiwa na haikumuhitaji yeyote kati ya mwenye akili timamu kukosa kulijua hilo labda asitake au iwe ndio hao wenye msimamo wa kukubali tuu kama wasemavyo waswahili “wamaa kala l- balozi fahuwa l- muafaka” tafsiri yake ni kuwa kila analolisema Bw. Balozi ndio sahihi.

 

Hoja ya kuwa watu waliunga mkono ama kukataa kitu katika uchaguzi huo kulitegemeana na misimamo ya kisiasa ya Wazanzibari ni vyema tume ya Bwana Mbita ikaelewa ikaelewa kwamba wanachama wa CUF na CCM Zanzibari hawawezi kufika hata asilimia hamsini (50%) ya wapiga kura wote.  Kuna Wazanzibari wengi ambao si wanachama wa vyama vya siasa kama ilivyokuwa Tanganyika wapiga kura kutokufika milioni kumi na tatu (13,000,000) kati ya watu zaidi ya milioni thalathini na tatu (33,000,000).  Wapo ambao kwa kazi zao hawaruhusiwi kuwa wanachama wa vyama vya siasa, wapo ambao kwa shughuli zao hawapendi kunasibishwa na vyama vya siasa, kadhalika wapo watu kwa mapenzi yao wasiopenda tu kujiunga na vyama vya siasa, lakini wote hao wanatumia haki yao ya kikatiba kuchagua viongozi wanaowataka ijapokuwa wanatokana na vyama vya siasa.  Watafanyaje wakati katika nchi hii hakuna wagombea binafsi?

 

Ama wale wote walio kataa na kupinga maharibiko hayo ya kura ya Mjini Magharibi na kutaka uchaguzi wote urudiwe tuonavyo sisi walikuwa na hoja zao kama Wazanzibari na wapiga kura na hio ni haki yao ya kimsingi na kikatiba, kama raia.  Imani yao imewafanya waamini hivyo hakuna wa kuwazuia.

 

 

Katika (kifungu cha 167) taarifa inaeleza kile kinachodaiwa kuwa ni msingi wa chama cha CUF kuitisha maandamano hii ni kutokana na tamko la Baraza Kuu la Chama hicho lililotolewa tarehe 30 Novemba 2000, tunadhani CUF wanajua wenyewe zaidi ni kitu gain kilichowapelekea kuitisha maandamano hayo.

 

Hapa kwanza ieleweke kuwa CUF haikuandamana ila iliiitisha maandamano.  Pili, ni busara tume ingalisema kuwa CUF iliiitisha maandamano kwani wito wa maandamano si msingi wa maandamano bali ni baada ya kuridhika kwamba kuna haja ya kuitisha maandamano.  Kwani “msingi” na “mwito” ni mambo mawili mbali mbali ambayo tume ingelipaswa kujifunza.

 

Kinacho sikitisha hapa ni Tume kuwa haikuona umuhimu wa kueleza kwa kina matokeo yaliyotokea baina ya uchaguzi na maandamano au mara baada ya uchaguzi wa 2000 na maandamano na baadae ndio CUF wakakataa matokeo ya uchaguzi na Baraza Kuu likaitisha maandamano hayo.

 

Hivi tume hiii haiyaelezi hayo au haina habari ya kuwa askari wetu kubeba visanduku vya kura kwa nguvu kabla ya kuhesabiwa, kuwa kutokuhesabiwa vituoni, polisi kupiga watu na wengine kuwekwa kizuizini, askari jeshi (JWTZ) kuranda mitaani na silaha nzito kama RPG na magari ya dereya na mambo mengine kadhaa wakadhaa ya vitisho kwa raia kabla ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi.

 

Katika  (kifungu 169) taarifa ya Tume inaeleza kwamba Serikali iliyakataza maandamano ya CUF lakini hawakusikia na katika (fungu la 170) inaelezwa kwamba “ili kuyazuiya maandamano hayo yaliyopigwa marufuku, serikali ilibidi kutumia nguvu.

 

Katika mapambano hayo, watu waliumia, wengine kupoteza maisha na baadhi kukimbia kwenda katika hifadho ya ukimbizi, nchi Kenya.  Lakini tume imekataa kata kata kueleza taratibu za uzuiwaji wa maandamano ya amani katika nchi jambo ambalo inalielewa vyema kutokana na uwezo wa kisheria waliokuwa nao baaadhi ya masekeretari wa Tume hio na hizo nguvu zilizo tumika kama zilistahili au zilizidi.

 

Na badala yake katika kuorodhesha vyanzo vya maandamano hayo katika (fungu la 239 [d]) Tume imeeleza kwamba “viongozi na wafuasi wa chama cha CUF kukiuka sheria na kukaidi amri ya Serikali iliyowataka kuwacha kuandamana”.  Eti kuwa ni moja kati ya vyanzo vya muda mfupi vya maandamo haya na hii inakuja baada ya Tume kufanya tathmini na kuafiki kwamba hiyo ni sababu ya maandamano.  Hivyo kwa maelezo haya ya Tume inaonyesha kwamba Tume ilikwisha amua kwamba chama cha CUF kilikiuka sheria, sasa ni vyema hapa tukatumia fursa hii si kuanzisha mjadala na mabishano ya kisheria lakini kueleza vile sheria inavyosema juu ya masuala haya ya kuandamana.

 

Sheria ya vyama vya siasa, ya mwaka 1992 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kifungu cha 11 (6) kinaeleza kwamba “ iwapo chama cha siasa kitatoa taarifa kwa mujibu wa ibara ndogo ya (4), basi chama hicho kinaweza kufanya mkutano au maandamano kama ilivyopangwa, isipokuwa tu kama chama hicho kitapokea amri (ambayo katika sheria hii inaitwa  “amri pingamizi”) kutoka kwa afisa wa Polisi mfawidhi wa eneo linalohusika inayoagiza kwamba mkutano usifanyike au maandamano yasifanyike kama ilivyoelezwa kwenye taarifa ya chama hicho”.

 

(7) Afisa wa Polisi aliepelekewa taarifa kwa mujibu wa ibara ndogo ya (4), haruhusiwi kutoa amri pingamizi kuhusu taarifa hiyo kwa mujibu wa ibara ndogo ya (6), isipokuwa tu kama ameridhika

(a)        Kwamba taarifa ya namna hiyo ilikwisha tolewa mapema na chama cha siasa kingine au na mtu mwingine kwa ajili ya kufanya mkutano, maandamano au shughuli nyingineyo mahali hapo hapo na wakati huo huo kama ilivyokusudiwa na huyo aliyetoa taarifa yake baadaye;

(b)        Kwamba shughuli za mkutano huo au maandamano hayo zinakusudiwa kutekelezwa au kutumiwa kwa ajili ya kutimiza lengo ambalo si halali kwa vile litakiuka au kuvunja sheria;

(c)        Kwamba shughuli za mkutano huo au maandamano hayo zinaashiria au zinakusudiwa kuvuruga amani au kuathiri usalama wan chi katika eneo linalohusika;

(d)        Kwamba chama cha siasa au kikundi cha watu kilichotoa taarifa si chama cha siasa kilichosajiliwa au kwamba taarifa imewasilishwa na Jumuiya isiyotambulika au mtu binafsi asiyetambulika kuwa ni wakala rasmi wa chama cha siasa chenye usajili kinachohusika.

(8) Amri yenye pingamizi inayotolewa kwa mujibu wa ibara ndogo ya (6) ni lazima iwe kwa maandishi na iandikwe kwa namna ambayo inaonyesha bayana sababu za kutolewa hiyo amri pingamizi na ieleze wazi kama chama kinachohusika kinaweza au hakiwezi kufanya mkutano wake mahali hapo hapo na katika eneo hilo hilo wakati mwengine au siku nyengine inayofaa zaidi.

 

Maelezo haya ni katika kifungu kinachozungumzia haki za vyama vya siasa vilivyosajiliwa na utaratibu wa mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa.

Sasa suala la kujiuliza hapa ni pahala gani  polisi walitoa amri pingamizi kisheria?  Tume inapoeleza kwamba serikali ilipiga marufuku maandamano hayo kwa amri ya Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), waziri wa mambo ya ndani, waziri mkuu au mwengine yeyote huyo katika sheria ya vyama vya siasa ni karata isiyo na nguvu yaani ni sawa sawa na “Joker” katika mchezo wa karata, na wacheza karata hawawezi kuitumia.

Turufu pekee katika suala hili ilikuwa ni kuwaachia maafisa wafawidhi wa polisi yaani OCD wa kila wilaya atumie nguvu zake kisheria kuweka pingamizi.

Lakini hata pale OCD walipojaribu kuzuia maandamano hayo hawakufuata taratibu za kisheria.  Kwa mfano, katika ripoti hii hii ya Bwana Mbita inaeleza kwamba:-

(kifungu cha 274) kinaelezea majibu ya mkuu wa Polisi wa wilaya ya Wete, ambayo katika majibu hayo ilitolewa sababu za “kiusalama” zisizokuwa na maelezo ya kina na barua yake ambayo CUF inayo nakala yake haikuzingatia kamwe pingamizi kisheria kwa kutoa maelekezo ya kufanyika mkutano au maandamano hayo siku nyengine au pahala pengine kama wanavyotakiwa.

 

Kadhalika, Mkuu wa Polisi wilaya ya Micheweni sababu zake zilikuwa ni kuhusu kuwepo kwa “vitendo vingi vya hujuma”  za kuchoma moto majengo na taasisi mbali mbali za CCM na Serikali na vile vile nchi kuwa katika hali ya tahadhari.  Hivi tukijiuliza wakati ule kulitangazwa hali ya hatari au “stand by”?

 

Suala la kuchoma moto majengo na vitendo vyengine vya hujuma vinahusiana nini na kuzuiwa kwa mikutano ya hadhara ya CUF katika sheria ya vyama na haki ya vyama vya siasa; pamoja na ile haki ya kimsingi ya kukusanyika au kuandamana ya kikatiba?

Kwa upande wake, Afisa wa Polisi wilaya ya Chake chake sababu alizotoa ni kwamba “hali ya hewa ya kisiasa haikuwa nzuri”, dalili nyingi zilijitokeza za miripuko ya mabomu na zaidi ni kwamba kulikuwa na amri ya Waziri wa Mambo ya Ndani (Moh’d Seif Khatib) ya kukataza kufanyika kwa maandamano.

Katika wilaya ya Mkoani ilitolewa sababu ya tamko rasmi la Jeshi la Polisi lililokaririwa na vyombo vya habari la kukataza kufanyika kwa maandamano nchi nzima nako wilaya ya Mjini na Wilaya ya Magharibi Unguja zilitolewa sababu ya Jeshi la Polisi kukabiliwa na kazi mbali mbali kiasi cha kuwa na ugumu wa kutoa ulinzi kwa maandamano na mkutano.

Sasa suala la kujiuliza hapa: Je, maelezo haya yanakidhi haja ya sheria na anayeyakataa ameharifu sheria?  Tume haikutaka kufafanua suala hili vyema.  Kinyume chake, waliitupia mzigo chama cha CUF kwamba haikutii amri ya Serikal ya kuzuia maandamano.

Lakini amri gani isiyokuwa halali kisheria ambayo inapaswa kufuatwa?  Tatizo ni kwamba sheria hizi zilitungwa na Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano;

Wakiwemo CCM peke yao; hivyo, walipaswa wao na Serikali yao kuzielewa vyema na kuziheshimu.

Cha kushangaza zaidi ni kwamba hukumu iliyotolewa kwa waandamanaji ya kuwapiga risasi na kuwauwa au kuwajeruhi ndio ilistahili?  Iwapo========== hukumu yake ni kifo katika Tanzania toka huko tunakotoka mpaka leo.  Je, mwenye kuua atafanywa nini? Iwe itakavyokuwa, hakuna sheria inayomruhusu askari polisi kufyatua risasi na kuua raia, kwa mazingira yeyote.

 

Vile vile namna suala hili lilivyochukuliwa na Serikali mara baada ya kutokea kwake ingekuwa vyema tume kama ilivyoripoti kauli zilizokuwa zikitolewa na viongozi wa kisiasa kabla ya maandamano hayo pia wakaeleza na kauli zilizokuwa zikitolewa na viongozi wa Serikali.

Baada ya maandamano hayo itakumbukwa kwamba Mhe. Rais Benjamini mkapa alipokuwa akizungumza katika kipindi cha Hard Tallk katika idhaa ya kingereza ya BBC aliwabeza sana waandamanaji na hata kufika kusema kwamba amesikitishwa sana na kifa cha askari polisi mmoja na kukejeli raia wake kama alivyoita mwenyewe kumi na saba tu (17) waliokufa.

 

Kadhalika kauli ya Rais wa Zanzibar A. A. A. Karume alipo wapongeza polisi kwa kudhibiti maandamano hayo, vile vile kauli za watu kama Suleiman Ligora kwa niaba ya Wenyeviti wa Mikoa CCM Tanzania na namna zilivyoathiri nyoyo za Watanzania.  Suala la wauwaji kupandishwa vyeo au kupewa uhamisho.  Je, tume haikuona kama zilipaswa kuzungumzwa katika ripoti yake?

Si nia yetu hapa kueleza uhalali na uharamu wa maandamano hayo ila ni vyema tukajaribu pia kutoa dondoo zifuatazo:-

1.                  Vyombo mbali mbali vya ndani na nje ya nchi vililaani wazi wazi mauwaji yaliyofanywa na Serikali katika kuzima maandamano hayo; hizi nguvu ambazo katika ripoti ya Bwana Mbita anasema zilihitajika zimeelezwa kwamba zilikuwa ni za ziada tena ziada isiyofaa na inayopaswa kulaumiwa.

(i)                 Mama Maria Nyerere na Taasisi ya Mwalimu Nyerere katika taarifa yake kwa vyombo vya habari iliyotiwa saini na Mkurugenzi mtendaji Bwana Joseph W. Butiku pamoja na kusikitishwa na mauwaji hayo amesema, “ Askari wetu ni walinzi wa Watanzania.  Ni walinzi wa mali na usalama wa Watanzania.

(ii)                Nayo kamati ya msaada wa kisheria ya Chuo kikuu cha Dar es Salaam katika taarifa yake ya tarehe 28 January 2001 kwa vyombo vya habari iliyosainiwa na Mwenyekiti wake, Profesa Chris Maina Peter, pamoja na kulaani mauwaji ya raiya yaliyofanywa na Polisi tarehe 26 – 27/01/2001 pia ilieleza kuwa CUF wanahaki na uhuru wa kuafanya maandamano ya amani na kuwa haki hiyo imo katika mikataba ya kimataifa ya Haki za Binaadamu ambayo Tanzania imetia saini, hivyo basi hatua za Polisi kuwazuia hazikuwa halali (The Guardian la tarehe 29/01/2001)

(iii)               Kitivo cha sheria cha Chuo kikuu cha Dar es Salaam katika taarifa yake kwa vyombo vya habari tarehe 31 Januari 2001 iliyotiwa saini na Mkuu wa kitivo hicho, Dk. Sengondo Mvungi, kimeeleza kuwa kwa mujibu wa kifungu cha 20 (1) cha katiba ya Jamhuri ya Muungano maandamano haya yalikuwa halali.  (Tazama Gazeti la Majira la tarehe 1 Februari 2001).

(iv)              Mjadala juu ya Mauaji ya Zanzibar uliofanyika Chuo kikuu cha Dar es Salaam tarehe 1 Februari 2001 umethibitisha yafuatayo:-

(a)               Serikali haikuwa na msingi wowote wa Kikatiba wa kuzuia maandamano hayo.

(b)               Si kazi ya Polisi kutafsiri Sheria; hiyo ni kazi ya Mahkama kwa mujibu wa Katiba ya Nchi.

(c)                Kilichofanywa na Polisi ni mauaji na uvunjaji wa haki za binaadamu na vitendo hivi vinapaswa vichunguzwe.  (Tazama The Guardian la tarehe 13 February 2001 na An – nuur la 2 February 2001)

(v)                Katika kongamano hilo hilo, mwanasheria wa kikatiba aliyebobea (a leading constitutional lawyer) hapa nchini, Profesa Issa Shivji alifafanua kwamba iwapo Polisi waliridhika kuwa maandamano hayo yangehatarisha amani kama wanavyodai, wangepaswa kwenda Mahkamani kuiomba itoe amri ya injection ya kuizuia CUF kutofanya maandamano hayo.  Polisi hawakufanya hivyo.

(vi)              Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari ya tarehe 29 January 2001 iliyotiwa saini na Mwenyekiti wake Profesa Haroub Othman, kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar kimeeleza kwamba “Haki ya kukusanyika, kufanya maandamano … ni vitu ambavyo vinatambuliwa katika katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 pamoja na sheria nyengine za nchi.  Hakuna katika sheria zetu au ibara yoyote ya katiba zetu mbili ambapo chama cha siasa kinahitajika kupata kibali cha Jeshi la Polisi kabla ya ama kukutana au kufanya maandamano.  Kituo cha Huduma za sheria Zanzibar kinasikitishwa zaidi na vitendo vya Jeshi la Polisi ni kinyume na Katiba na Sheria….”

(vii)             Ikitoa tafsiri ya haki ya vyama vya siasa kufanya maandamano na mikutano ya hadhara  chini ya Political Partied Act No. 5 of 1992 na Polisi Force Ordinance of 1953 zinazokitaka chama cha siasa kuomba kibali cha Polisi kabla ya kufanya hivyo, Mahkama Kuu ya Tanzania chini ya hayati Jaji Kahwa Lugangikira katika kesi ya Re. Christopher Mtikila v. Attorney General ya 1993 ilitamka kwamba “sharti la kuomba kibali ni kinyume na Katiba na ni bati”.  Na kwa sababu Serikali haikukata rufaa Mahkamani dhidi ya hukumu hii wala Bunge halikufanya marekebisho ya Sheria hizo kufuatia hukumu hiyo, hukumu hii bado inasimama hadi leo.  Kwa hiyo, maandamano ya CUF ya tarehe 27 Januari 2001 ni halali.

(viii)           Ufafanuzi zaidi wa sheria umetolewa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Barnabas Samatta alipohutubia Semina ya Wabunge kwamba Polisi hawana uwezo wa kisheria wa kuvizuilia vyama vya siasa haki yao ya kikatiba na kisheria ya kuandamana na kufanya mikutano ya hadhara. Ifahamike kwamba Jaji Mkuu huyu ndiye anayeongoza Mahkama ya juu kabisa nchini.

 

Madhumuni ya kueleza maoni ya wataalamu, taasisi na dondoo hizi za kisheria ni pia kuonyesha upande wa pili wa hoja za wale wanaotetea msimamo wa kwamba maandamano hayo yalikuwa halali na polisi hawakupaswa kisheria kuyavunja kwa kutumia nguvu, na haingelikuwa hivyo bali taratibu walizotumia wao na Serikali si halali katika kuyazima maandamano hayo tumeyaeleza haya kusudi kwani tume pamoja na kuyaelewa hawakupenda kuyataja.  Wao wametosheka na kuwaeleza wananchi katika ripoti yao kwamba serikali ilipiga marufuku maandamano hayo, CUF hawakutii agizo la serikali na ikawa ni sababu ya matatizo yaliyotokea.

 

Wapenzi wasomaji tukirudi nyuma katika kuangalia undani wa maelezo ya Tume ya Tais inashangaza mno kuwa katika (fungu la 185)  la ripoti hiyo tume inaeleza kwamba “sababu za muda mrefu za matukio ya tarehe 26 – 27 Januari 2001 ni nyingi na zinagusa maeneo mengi ya jamii katika nyanja za siasa, uchumi, utamaduni na ustawi wa jamii”.

Sasa hili suala la “historia” ambalo tume ya Mbita imechukua muda wake mrefu kulieleza, na kulipa uzito mkubwa, lilianzia kwa nani wakati mambo yaliyotajwa ni yale yanayohusu siasa, uchumi, utamaduni na ustawi wa jamii lakini Tume hiyo hiyo ikashindwa kutoa maelezo katika tathmini yake vipi ustawi wa jamii, utamaduni na hata uchumi kwamba umechangia kuwepo kwa maandamano hayo.

Kwa lugha ya uchambuzi, tunaweza kusema kuwa tume ya Mbita inaamini kuwa “ni sehemu ya utamaduni wetu Wazanzibari” kuuwana; kitu ambacho hakijawahi kutokea katika historia ya Zanzibar.

Kwa mfano katika (fungu la 183) kama ifuatavyo:-

 

a.         Udhaifu

b.         Vyama kutokubali kushindwa

c.         Uchaguzi mbaya – sio wa haki na huru

d.         Vyombo vya dola kujiingiza katika siasa

e.         Serikali kutoheshimu maamuzi ya wananchi

f.          Kutotekelezwa kwa Muafaka wa 1999

g.         Kutoeleweka vyema kwa mfumo wa vyama vingi

h.         Kukosekana haki. Bila haki amani haiwezi kutawala

i.          Maendeleo duni hususan kisiwani Pemba.

j.          Kutokuwepo matayarisho ya kutosha juu ya kuendesha siasa katika mfumo wa vyama vingi

k.         Kuwepo kwa dhana ya kwamba wapinzani wanaleta vurungu

l.          Uunguja na Upemba; hisia kwamba Mpemba hawezi kutawala

m.        Vyama kuhoji uhalali wa Muungano

n.         Nia ya CUF na kutqaka kurudisha kwa wenyewe mali zilizochukuliwa na Serikali baada ya Mapinduzi

0.         CCM ilipenda Msajili wa Vyama awadhibiti wapinzani

p.         Polisi kuhisi wana uwezo wa kutoa vibali vya mikutano

q.         Vyama kudai haki bila ya kufuata Katiba na sheria za nchi

s.          Vyama vya siasa kutotii amri za Serikali

t.          Viongozi wa baadhi ya vyama vya siasa kushindwa kuwadhibiti wafuasi wao.

u.         Kauli zilizodai Chama cha CUF kifutwe

v.         Uchaguzi wa Rais wa Zanzibar mwaka 1995

w.        Kauli zinazokera; za CCM

           Vyama visivyo na historia ya ASP na TANU haviwezi kutawala.

           Nchi imepatikana kwa bunduki haiwezi kutolewa kwa kura/karatasi

           Mapinduzi daima

 

za CUF

           Ngangari

           Jino kwa jino

           Kukaa vizuka

           Kulala barabarani

           Kuwa vilema

           Damu kumwagika

 

za Jeshi la Polisi

           Ngunguri

 

Itakapokuwa haya ndio maelezo ya wananchi na viongozi waliopata fuursa ya kuzungumza na tume juu ya chanzo cha maandamano.  Haya hili suala la historia lilitokea wapi mpaka likachukua nafasi zaidi ya haya maelezo yaliyotajwa hapo juu.

 

Ingawaje ni vigumu kwa tume kuorodhesha kila waliloambiwa lakini inashangaza kwa jambo ambalo tume imetumia muda wake mwingi kulieleza lakini ikasahau kuliorodhesha kama ni miongoni mwa mambo yaliyotajwa na wananchi.

 

Kama vile Tume ilivyosahau kauli za baadhi ya viongozi wakuu wa CCM na Serikali ambazo zilidaiwa kuchochea kuwepo kwa maandamano hayo kwa mfano kauli ya Rais Benjamin Mkapa ya kuwakatisha tama wapinzani na wafuasi wao aliyoitoa katika viwanja vya Lumumba Mjini Unguja kwenye mkutano wa hadhara kwamba wapinzani wakome kumuandikia kuhusu matendo yanayotendeka Zanzibar na kwamba wana CCM wasikubali kuzitoa Serikali zote mbili ya Zanzibar na Jamhuri ya Muungano kwa watu wasio na histroia ya ASP na TANU.

 

Huku akisahau kwamba sheria ya vyama inakataza vyama viliopo kujihusisha na vyama vya zamani ingawaje baadhi ya wafuasi wa Chama chake mara kadhaa wamechapisha kanga zenye nembo na bendera za Afro Shirazi na TANU na hapana aliyethubutu kuwauliza chochote kwa kuogopa kuambiwa anapinga Mapinduzi na anataka kurejesha ukoloni.

 

Kama suala ni historia ya vyama vya zamani walivyotokea viongozi wetu iwe ndio njia ya kupatia uongozi sasa basi kama pana mtu asiyestahiki mmoja Mkapa kwa sababu wakati TANU inawapigania Ukombozi wao Watanganyika Bwana Mkubwa alikuwa ni mvaaji wa suruali kipande (kaptura), stokingi refu, shati nyeupe, tai, buti iliyokolezwa kiwi na kiko yake mdomoni kudhihirisha kwamba yeye ni motto wa Wazungu hao tunowaita Wakoloni, kwani wakati huo alikuwa ni mwanafunzi katika chuo cha Makerere.

 

Na itakapokuwa sababu ni mtu anapotokea basi kitabu cha historia ya TANU kilicho andikwa na ULOTU ABUBAKER ULOTU kinatupa jibu kwa kusema yafuatayo:

 

Kwanza kwamba kulikuwa na vyama kabla ya Uhuru wa Tanganyika jambo ambalo wana historia wetu wanakwepa kulisema baadhi yake ni UTP (United Tanganyika Party), Tanganyika Asian Assosiation (TT), Ukaguru Student Assosiation (USA), Hindu Concil, Asian Assosiation, Tanganyika National Society, Tanganyika (ANC) All Muslim National Union of Tanganyika (AMNUT)n.k. kwa ufupi hadi mwaka 1950 kulikuwa na vikundi 87 vya siasa Tanganyika.

 

Kadhalika kulikuwa na Vyama vya Makabila vilivyoipinga TANU, (kwa mfano Tambarare Citezens Union – Cha Korogwe, Mlezi – cha Masasi, “Kwao Bwanamkubwa Mkapa”, Masasi Democratic Union – cha Masasi (MADU), Chagga Congress – Cha Kilimanjaro n.k.

 

Pia, viongozi wa makabila ambao zamani wakitambulikana baadhi yao kwa majina ya WATEMI wapo walioiunga mkono TANU wale walioipinga.

Sasa na tujaribu kuangalia namna viongozi hao na Makabila yao ama walivyoipokea na kuikubali au kuikataa TANU.  Mfano mdogo ni  huu ufuatao:

 

WILAYA

WALIOUNGA MKONO

WALIO PINGA

Bagamoyo

0

6

Handeni

3

7

Korogwe

0

8

Biharamulo

3

0

Geita

0

2

Iramba

3

7

Manyoni

2

5

Mbinga

3

7

Masai

0

4

Newala (kwao Rais Mkapa)

0

4

 

“Imenukuliwa katika kitabu cha historia ya TANU ukurasa wa 27”

 

 

sasa iwapo kauli ya Rais wetu itaheshimiwa na wananchi kwa kusema wachaguliwe watu kutokana na historia zao za kuikubali au kuikataa ATNU na Afro Shiraz haoni kwamba mwanzo anaepaswa kukataliwa angekuwa yeye?  Kwa sababu TANU ilikataliwa huko kwao na wala mchango wake yey binafsi katika harakati za kudai uhuru haujuilikani kwani walioisimamisha TANU Masasi ni akina Eliasi Mmuni, Moses Kente, Bi B. Ling’ande, A. Chigombo, E.Yakobo, Yustine Mpunga, S. Chitwangwa, Sandali haji, Issaka Kambona, M. Chidyanga, Bi Mtaka, Bi Viole Bushiri na baadhi ambao hatukuwataja hapa lakini wale muhimu ndio hao wakati huo ben hakuwepo yeye wala jamaa zake La msingi hapa ni kumkumbusha Rais wetu kuwa tukiangalia historia za watu hatutofika kwani binaadamu kila leo anabadilika na hayo ndio tuliyoyaeleza huko nyuma katika kitabu hiki.

 

Katika maelezo yetu tumejaribu kufafanua mahusiano ya viongozi wa siasa hapa Zanzibar na vyama vya zamani na tukaona kwamba mchanganyiko mkubwa wa wanachama wa vyama hivyo umo ndani ya vyama vya sasa kiasi ya kwamba hapana chama kinachoweza kujinasibisha kwa usahihi na mchango wa vyama vilivyopita katika maendeleo ya Wazanzibari kama tutakubali ukweli; kwani ndani ya vyama vyote viliopo Zanzibar kuna wana wa Afro, ZNP, ZPP, ZPPP n.k.  Suala la kujiuliza:  Je, maneno haya ya Rais wetu yalikuwa ya jazba kama yalivyoambiwa ya Ligora?  Alipotoshwa na washauri wake?  haelewi histori za siasa za nchi hii au kitu gani haswa?

 

Aidha kauli nyengine aliyoitoa katika Hotuba yake ya kuuaga mwaka 2000 na kuukaribisha mwaka 2001 alipopinga marufuku mikutano na maandamano ya vyama vya upinzani hadi wakati wa kampeni kwa madai kwamba CCM iachiwe itekeleze ilani na sera zake za kuwaletea maendeleo wananchi.

 

Lakini Tume ilisahau pia kama katika kauli zilizotajwa mbele yake kuwa ni kali na zenye kuchochea hamasa kwa wananchi ni pamoja na zile za aliyekuwa Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Dr, Salmini Amor alizozitoa nyakati tofauti ya Mwembe Kisonge alisema “Dola ni Dola na ni lazima iheshimiwe Dola inao uwezo wa kutoa amri yoyote na amri hiyo ikatimizwa kwa hivyo Dola haioni taabu kupoteza mtu mmoja, wawili, watatu, mpaka kumi kwa ajili ya maslahi ya wengi”.  Pia kauli aliyoitoa katika viwanja vya Malindi kwamba wapinzani wanatemvea na vitanzi vyetu shingoni na kama wanataka Uchaguzi wasubiri mwaka 2000 kama watafika kwani hapa kati kati pana mambo mengi.

 

Na ni kweli tuliyaona ya watu kusingiziwa kesi za uhaini, kufukuzwa kazi, kupigwa na Polisi, kuvunjiwa nyumba na mambo kadhaa wakadhaa, vile vile wazanzibari hawatosahau maneno yake aliyoyatoa kule Sishel wakati akizungumza na waandishi wa habari kwamba Serikali hii haingepatikana kwa vikaratasi anayetaka na apindue kama walivyopindua wao.

 

Kauli ambayo ilikuwa kama urathi kwa viongozi wa Chama cha Mapinduzi kwani kauli hiyo ilisikika mara kadhaa ikitumiwa na viongozi wa CCM kwa Mfano muasisi wa mwanzo wa Mapinduzi wa Zanzibar Sheikh Ambeid Amani Karume alikaririwa kutamka miaka hamsini (50) kauli ambayo katika taarifa ya Bregedia Mbita imenukuliwa katika kifungu cha 195.

 

Kauli hiyo ilirudiwa tena na Marehemu Sheikh Idrisa Abdul Wakil aliyekuwa Rais wa awamu ya nne wa Zanzibar wakati wa kumrithisha madaraka kamandoo katika viwanja vya Kisiwandui CCM ambaye yeye na Waziri Kiongozi wake wa wakati huo Marehemu Dr. Omar waliifanya ni wimbo wa kuchombezea mwana ili alale usingizi mnono.  Kauli mbiu hii ilitumiwa kama kipandisha mori cha wana CCM pale wanapoonekana kupungua nguvu na imani kwa chama chao zama hizi za chinja chinja kama alivyoitwa na Sheikh Ali Hassan Mwinyi, Dr. Salmini Amour Juma, zilishika kasi na kushamiri hata wasojua Mapinduzi wakazungumzia kuipata Serikali kwa mtutu wa bunduki hapo tena ngoma ikawa haina mwenyewe.

 

Asha Bakar, hafidh Ali, Mvita Kibendera, Castico (ambapo baada ya matusi yake yote kwa Wazanzibari ikabainika kwamba mbali ya kuwa hayajui Mapinduzi kamwe si raia wa Tanzania! Ajabu iliyoje mtu huyu kufikilia hatua ya kuwa msemaji wa chama cha Mapinduzi (mwenezi) na wenyewe wanaoshikilia hatamu za uongozi wan chi hii wasimjue kama si raia wan chi hii.  Je, hapo pana usalama?)n.k.

 

Au tunawatizama CUF tu?  Ali Vuai, Mussa Takrima na wengine kadhaa wakadhaa tena baadhi ya wakati ndani ya Baraza la Wawakilishi wakiungwa mkono na watu kama kina John S. Malecela waliotungiwa kitabu na Nyerere kuitwa “wahuni” na wenzao wengine.

 

Kauli hizi pamoja na kejeli nyengine mbalimbali ziliwapa mashaka sana wapinzani juu ya usalama wa maisha yao kutoka kwa serikali.  Mfano, mwengine ni kauli ya aliyekuwa Katibu Mkuu Umoja wa vijana Sukwa Said Sukwa aliyoitoa katika viwanja vya Kijangwani  miaka hiyo katika mkutano wa hadhara na kusema kwamba wakiruhusiwa watawakamata wapinzani na kuwakata kata kasha nyama zao wazitie katika pakacha na kukabidhi kwa viongozi wao; kuna kauli za watu kama Sleman Ligora Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Dar es Salaam aliyoitoa kwa niaba ya Wenyeviti wote wa CCM wa Mikoa ya Tanzania zikiwa ni salamu zao kwa viongozi wakuu wa chama cha Mapinduzi mkolongo wa kauli kama hizi ni nyingyi mno lakini Tume haikuweza hata kuonyesha sampuli kwa kuichelea nambari wani.

 

Sasa jambo la kujiuliza hapa wataalamu wetu kina Mbita hawakupatapo kusikia kauli hizi?  Waliokwenda mbele ya Tume hawakuzieleza?  Au kwa utashi wao waliona afadhali kuzungumzia “ngangari”; “jino kwa jino”, kukaa vizuka, “kulala barabarani”, “kuwa vilema”, “damu kumwagika” kwa sababu tu zimetolewa na CUF ama kweli mnyonge mnyongeni!!! Lakini haki zake mpeni!

 

Kauli ya baba mwenye mamlaka ya nyumba kwa mwanawe na mwana kwa babae ipi yaweza kupewa uzito?  Hivi kauli ya Serikali yenye dola na kauli ya Rais mmliliki wa Serikali ipi ingeweza kutisha?

 

Ukiangalia ripoti ya Tume kuanzia (fungu la 280 hadi 285) unaweza kuona kwa kiasi gani vyombo vya ulinzi na usalama vilivyoshughulika, kuweka vikao na kutoa maagizo ya kila aina katika kuzuia maandamano hayo.

 

Inaarifiwa na ripoti ya Tume katika (fungu la 282) kwama Polisi katika Mkoa wa Kusini Pemba pekee waliazimia kutumia Askari 500 idadi kamili ya Askari waliotumika katika Operesheni hiyo kama ilivyoripotiwa na tume ni kama ifuatavyo wilaya ya Wete 160, Micheweni 85, Chake chake 85, Mkoani 117, Mjini 114, Magharibi 246 kwa wastani katika Wilaya hizi Askari wasiopungua 807 walitumika na hao ni wale waliopangiwa kazi katika vituo mbalimbali hujatia hesabuni waliobakishwa akiba; vikosi maalum kama vile KMKM, Valantia, JKU, Magereza, Usalama wa Taifa, Askari Wastaafu UMAWA na Wanajeshi wa Jeshi la Wananchi Tanzania.

 

Gharama zot zilizotumika kwa maandalizi ya kuzuia maandamano haya zisingelikuwa na haja zaidi ya busara na maelewano.  Ni dhahiri kwamba Serikali ilitanguliza mbele ushindani na kukubali lolote litakalokua na liwe lakini isishindwe nah ii inathibitishwa na kauli ya IGP Mahita kwamba yakifanyika maandamano ya CUF angejiuzulu ingawaje alishindwa hata baada ya maandamano hayo kufanyika na watu kupoteza maisha kwa maandalizi yaliyofanywa na Jeshi lake na matumizi ya nguvu za ziada.

 

Kauli nyengine ni ile ya Mkuu mmoja katika wakuu wa Jeshi la Wananchi alipoeleza wakati akizungumza na wapiganaji na kunukuliwa na magazeti kwamba fujo ikitokea wao Jeshi watawauwa viongozi muhimu wa CUF ingawaje hawakufanikiwa kufanya hivyo.

 

Suala la kjiuliza hapa iwapo Jamhuri yetu inaweza kutumia zaidi ya Askari 1000 wa vikosi mbali mbali u Maandamano ya kisiasa katika kisiwa cha Pemba tuu je itatumia askari wangapi na shilingi ngapi na maandalizi yepi katika kupambana na wimbi la ujambazi na wizi wa kutumia nguvu Tanzania nzima, ambao unafanyika kila siku?

 

Ni juzi tuu tarehe 25/05/2003 askari wetu wameuliwa na majambazi tena kwa silaha nzito, badala ya kusikia maandalizi ya vyombo vya ulinzi na usalama namna watakavyo pambana na wimbi hili la ujambazi kama vile ni halali kwa Polisi kuua Majambazi.  Mwenendo huu ukiachiwa kuendelea wa askari kuua watu ovyo kwa kisingizio cha ujamgazzi watatumaliza Watanzania na yale ya Imrani Kombe yatawapata wengine.

 

Na kwa upande mwengine tunasikia taarifa za mkuu wa Mkoa wa DSM Luteni Yussuf Makamba kwamba watu wa DSM waanzishe ulinzi wa sungusungu, hivi tujiulize iwapo Polisi na silaha, utaalamu, uzowefu, nguvu ya dola na mambo kadha wakadhaa wameulwa na Majambazi na wameshindwa kukomesha ujambazi kila siku ndio unaongezeka, jee hawa sungusungu na rungu wataweza kukomesha ujambazi?  Halalfu wawakamate na wala rushwa, eti kasha wawafichuwe na wauza madawa ya kulevya na bangi?  Tunahitaji kutafuta dawa na kama ngungur wetu wameshindwa basi ni vyema tuelezwe.

 

Tukirudi nyuma na tuangalie sasa uchambuzi wetu katika (kifungu cha 311) cha ripoti ya tume ambacho kinaeleza kuwepo kwa matumizi ya helikopta [helicopter gunfire] katika maandamano hayo ya tarehe 27/01/2001.

 

Taarifa za wananchi zinalilalamikia jeshi la polisi kwa kutumia helikopta katika kuwatawanya waandamanaji na hata kutiliwa shaka ya waliokuwemo kwenye helikopta hiyo kwamba waliwapiga risasi na kuwauwa baadhi ya waandamanaji jambo ambalo polisi kwa upande wake walilipinga sana.

 

Katika kifungu hiki ripoti ya tume inasema hivi “maandamano yalitawanywa kwa helikopta ya Polisi iliyoleta vifaa Wete na hatimae Micheweni.  Helikopta hiyo wakati ikituwa iligandishwa angani na hivo kutimua vumbi.  Waandamanaji waliingiwa na hofu na hatimae walikimbia mwituni.  Polisi walifanikiwa kuwatia nguvuni watu 40”.

 

Kwa utaratibu wa uandishi kifungu hiki kina taarifa nne ambazo zote zinajitosheleza.

 

Ya kwanza ni kwamba “maandamano yalitawanywa kwa helikopta ya Polisi iliyoleta vifaa Wete na hatimae Micheweni”.

 

Ya pili ni kwamba “Helikopta hiyo wakati ikituwa iligandishwa angani na hivyo kutimua vumbi”

 

Ya tatu ni kwamba “Waandamanaji waliingiwa na hofu na hatimae walikimbilia mwituni”.

 

Ya nne ni kwamba “Polisi walifanikiwa kuwatia nguvuni watu 40”.

 

 

Uchambuzi wa taarifa hii kwa uoni wa kawaida taarifa inatoa ukweli wa kilichotokea katika maandamano hayo kuhusiana na matumizi ya Helikopta.  Kwa mfano unapoambiwa maandamano yalitawanywa kwa helikopta vitu unavyoweza kujiuliza ni jee helikopta hiyo ilitumika kuwafukuza waandamanaji, ilitumia vipaza sauti kuwatawanya waandamanaji? Ama ilidondosha kitu kuwatawanya waandamanaji?

 

Pili suala jengine unaloweza kujiuliza inaelezwa kwamba helikopta hiyo iligandishwa angani na hivyo kutimua vumbi.  Huku ikielezwa kwamba baadae waandamanaji waliingiwa na hofu na kukimbilia mwituni! Jambo la kujiuliza hapa ni kwamba je waandamanaji hao wanaodaiwa katika baadhi ya vifungu  katika taarifa hii kuwa kabili polisi na kupambana nao huku polisi wakiwagyatulia risasi hawakurudi nyuma waje wakimbie na kuingia huku polisi wakiwafyatulia risasi hawakurudi nyuma waje wakimbie na kuingia hofu kwa kugandishwa helikopta angani?

 

Ni dhahiri kwamba helikopta hiyo yenye uwezo wa kubeba maafande wasiozidi sita isingelikuwa na la kutisha na kutia hofu kama haikufanya jambo la ziada ambalo lilipelekea kupatikana  maiti watatu katika eneo hilo kwa mujibu wa taarifa ya tume.

 

Hivyo hoja ya kwamba helikopta hiyo ilitumika katika kutawanya maandamano inabakisha suala ilitumika vipi?  Na hawa maiti watatu katika msitu mkuu ambao msitu huo ndio uliotajwa kuwa waandamanaji walikimbilia huko katika (kifungu cha 348) cha ripoti ya tume inaeleza kwamba watu watatu walikufa katika eneo hilo.  Je, walikufaje?

 

Kadhalika katika (kifungu 313) taarifa ya tume inaeleza kwamba taarifa za kipolisi zimeiambia tume kwamba waandamanaji wa Chake chake walikuwa wamebeba mapanga, visu, mawe, manati, marungu na mabomu ya petrol na ushahidi inaeleza kwamba vitu ambavyo vinadaiwa kutumiwa na waandamanaji hao.  Taarifa hizi zimeripotiwa na polisi pia katika wilaya za wete, micheweni na mjini Unguja lakini jambo la kushangaza kwamba mwahala mwote polisi walimodai kushambuliwa wameeleza kushambuliwa kwa mawe na pale ilipotokea kifo cha polisi mwenzao ikadaiwa kwamba amechinjwa kwa kisu.

 

Suala la kujiuliza hapa mapanga, manati, marungu na mabomu ya petroli waandamanaji waliyabebaje na wakashindwa kuyatumia?  Jengine zaidi nini kimetokea kati ya waliokamatwa hata mmoja asishitakiwe kwa kukutwa na vifaa hivyo?  Wote ikawa ni kushiriki maandamano haramu, kuandaa maandamano na watu watatu wakashtakiwa kwa mauwaji.

 

Lakini majibu ya taarifa hii yanajieleza katika (fungu la 432)  la taarifa ya tume linalosema hivi “mmoja wa waandamanaji alijaribu kumshambulia askari mwenzake kwa panga.  Waandamanaji walikuwa wanasonga mbele na kurusha mawe.  Alifyatua risasi tatu hewani halafu akapiga goti na kujaribu kupiga risasi  kuelekea kwa waandamanaji kwa kulenge miguu.  Alipokuwa anafyatua risasi, ilitolewa amri kutoka miongoni mwa waandamanaji ya kuwataka waandamanaji walale chini.  Wakati huo huo alipiga jiwe mkononi na aliumia”.

 

Kwa taarifa hiii ni dhahiri kwamba madai ya CUF kwamba katika maandamano hayo kulikuwa na makundi ya askari ambao hawakuvaa sare waliobebeshwa silaha za kienyeji kama vile mapanga, marungu na silaha nyengine ili wafanye vitendo vya uharibifu na baadaye kuwasingizia waandamanaji hao yalikuwa na ukweli na hilo ndilo liliotokea kwa mujibu wa taarifa hii ya tume ingawaje baadhi ya askari wenye yunifomu haikuwa rahisi kwao kuweza kutambua wenzao au watu wao walio andaliwa kwa kazi hio.

 

Na hili linapata nguvu katika taarifa za kipolisi ya kwamba waliwakamata baadhi ya watu na baadae kuwaachia, maelezo haya yanaelezwa na tume katika mafungu yafuatayo kwa mfano (kifungu cha 314)  cha ripoti ya tume kinaeleza kwamba “Aidha, watuhumiwa 62 walikamatwa na kati yao 26 walifikishwa mahakamani” katika (kifungu cha 321) cha ripoti hii kinaeleza kwamba “tume ilielezwa kwamba tarehe 27 Januari, 2001 polisi ilipata taarifa kwamba watu wanaosadikiwa kuwa ni wafuasi wa CUF walijikusanya katika msikiti wa Jumuiya ya Waarabu eneo la Komba wapya tangu saa 11:30 asubuhi tayari kwa maandamano.

 

Na kwamba watu hao walikuwa wamebeba mapanga, visu, mashoka, vipande vya nondo, majambia, mikasi, patasi, maji yaliyodhaniwa ni tindi kali nk.  Mara baada ya kupata taarifa hizo, polis walikwenda kwenye eneo hilo la msikiti na kuuzingira.  Waliwakamata waandamanaji 35 na ambao kumi na nne walifikishwa mahakamani”.

 

Eneo hili la Komba wapya ndilo lililoelezwa kwamba askari alimshambulia askari mwenzake kwa jiwe yumkini baada ya waandamanaji hawa kukamatwa gurupu hilo la watu 21 ambao hawakufikishwa mahakamani na mambo yao kumalizia polisi wakawa ndio hao wabeba patasi, nyundo na misumeno kama vile mafundi seremala kwani kwa mujibu wa kesi zilizokuwepo mahakamani kutoka eneo la Msikiti wa Jumuiya ya Waarabu na kwa Biziredi kuishia Michenzani wote walioshtakiwa kwa kukamatwa huko hawakushtakiw akwa kukutwa na silaha suala la kujiuliza hapa orodha hii ya vifaa iliyotajwa na polisi alikamatwa navyo nani?  Na kwa nini hao watu 21 waliachiliwa na hawakufikishwa mahakamani au tuseme palikuwa na mazingira tata ya rushwa?  Au walikuwa ni watoto wa wakubwa?

 

Wakati wengine walitolewa majumbani, hata baada ya kutii amri ya serikali kwamba wasiandamane lakini haikuwasaidia kitu, wengine wakashushwa katika madaladala, wakapigwa, wakatiwa ulemavu na wakisha wakashtakiwa.  Inakuwaje Polisi wasiokuwa na haya kuiambia tume kwamba kati ya watu 35 ni kumi na nne tu waliopelekwa mahakamani.  Je tume haikuelezwa ni kwa nini hawa wengine hawakupelekwa mahakamani?

 

Aidha suala jengine hapa la kujiuliza ni juu ya hii taarifa waliyopokea Polisi kwamba saa 11:30 Asubuhi wamepokea taarifa ya kwamba kuna watu katika eneo la Komba wapya wanadhaniwa kwamba ni CUF wamkusanyika na silaha kama hizo zilizotajwa hapo juu.  Jee ingelizekanaje kuonekana wakati huo wa kiza (Alfajiri) na kutambuliwa kwamba watu hao walibeba Bisibisi, Nyundo, Patasi, Misumeno, Tindi kali n.k.  Kama mtu huyo aliypeleka taarifa (ingawaje hakutajwa na Polisi) asiwe miongoni mwa walioandaa silaha hizo?  Kwani wakati wa kiza kama hicho na udogo wa silaha zilizotajwa hakueleweki kwamba ni vitu vinavyoweza kuonekanwa kwa mara moja na mpita njia.  Suala jengine la kujiuliza hapa ni mahusiano ya msumeno na maandamano, hata waandamanaji hao wangeliamua kubeba silaha kwa ajili ya kufanyia fujo katika maandamano basi isingekuwa za aina hiyo.

 

Hii inaonyesha dhahiri kwamba hizi zilikuwa ni lugha za kusukuma ili Polisi waweze kujikosha kwa yale waliyofanya.

 

Fungu jengine ambalo tumejaribu kuliangalia katika uchambuzi wetu huu ni (fungu la 375) linalozungumzia taarifa za kifo cha Hassan Omar Hassan, katika fungu hili  tume inaeleza yafuatayo:

 

“walijitokeza watu kadhaa waliosema kwamba walimuona Hassan Omar Hassan akipigwa risasi.  Mmoja wa watu hao ni Katibu wa CUF wilaya ya Wete, ambaye alieleza kwamba alimuona Marehemu akipigwa risasi, wakati yeye mwenyewe akiwa amejificha katika nyumba ya jirani.  Shahidi mwengine aliieleza Tume kwamba yeye alimuona Hassan Omar Hassan akipigwa risasi katika eneo la jingo la Sunda, Mtemani Wete na akafariki.  Alimtaja pia Askari aliyempiga risasi.  Kifo hiki kingeweza kuoanishwa na moja ya maiti ambayo haikutambuliwa katika hospitali ya Wete”.

 

Kasoro kubwa iliyopo katika fungu hili si taarifa ya kifo cha Hassan bali ni namna Tume ilivyoripoti tukio hili katika taarifa yake itakumbukwa wazi kwamba Tume iliahidi kwamba maelezo yote atakayoyatoa shahidi ni siri baina yake na Tume si vibaya kwa Tume kuwataja watu kwa ujumla wao, kuwataja majina walioathirika, kuwataja majina waliopokea majeruhi au maiti lakini imekiuka maadili kutaja mtu aliyetoa taarifa za kuuliwa mtu ni vyema tukajiuliza mbona wale wote waliotoa taarifa vyeti kama hizi hawakutajwa kwa mfano waliodaiwa kunajisi au kunajisiwa, waliodaiwa kupiga na kuua ijapokuwa matendo yao yameripotiwa hata baadhi ya taarifa nyengine muhimu mbali mbali kwa mfano; Tume imeeleza baadhi ya viongozi wa CUF katika wilaya ya Mjini walivyoitaarifu juu ya vile Kamanda wa Polisi aliyekuwa akiongoza kikosi alivyoamuru kuuliwa Ustadh Juma kwa kupigwa risasi ya kichwa hapana aliyetajwa kutoa ripoti hiyo wala kamanda aliehusika na mauwaji hayo hakutajwa.

 

Kulikoni Tume kumtaja Katibu wa wilaya ya Wete pekee kwamba ni mtoa taarifa ya mauaji lakin hapo hapo shahidi mwengine aliyetoa taarifa za kifo hicho hicho asitajwe?  Wala Muuwaji ambae alitajwa na mashahidi hao.

 

Katika (fungu la 407) la ripoti ya tume inaripoti kwamba kuna madai ya wafuasi wa CUF kabla ya maandamano kuchoma moto ghala la karafuu, ZSTC na nyumba ya Mkuu wa Polisi wilaya ya Mkoani.  Isingeshangaza kuona tume inaripoti matukio haya kama ni matukio ya zamani lakini yanapohusishwa na maandamano inabidi kidogo tume tuikumbushe kwa faida ya wasomaji kwamba ghala la karafuu, ZSTC na nyumba ya Mkuu wa Polisi wilaya ya Mkoani zilidai kuchomwa moto zaidi ya miaka mitatu kabla  ya maandamano hayo na siyo siku ya maandamano.

 

Waliotuhumiwa kuhusika na madai haya walipelekwa mahakamani kesi zao ziliamuliwa na wale viongozi wa CUF waliokamatwa na kuhusishwa na tuhuma hizo kwa misingi ya kisiasa hawakupatikana na hatia na wakaachiliwa huru.

 

Serikali haikukata rufaa juu ya maamuzi hayo ya mahakama kwa sababu ilielewa wazi kwamba waliokamatwa hawakuwa wahalifu na kamwe wasingeliweza kuwafanya kuwa wahalifu.  Sasa hizi tuhuma za viongozi wa CUF kuhusishwa na vitendo hivyo zimetokea wapi?  Tunaamini wengi kati ya Wajumbe wa Tume na Sekreteriati yao hasa wana Sheria waliotolea Zanzibar wanalielewa hilo lakini kukubali kwao kuandikwa kama lilivyoandikwa ni katika mwenendo ule ule wa kuisukumizia CUF sifa ya ukorofi ambayo haina.

 

Hivyo maoni yetu ni kwamba suala hili halikuwa na uzito wowote wa kuingizwa katika ripoti ya T ume hata kama limesemwa na mashahidi, kwani yappo mengi yaliyosemwa tena mengine matatizo kuwatuhumu CCM na Idara ya Usalama ya Taifa lakini katika mizania yake tume haikuthubutu kutamka kwamba Usalama wa Taifa Zanzibar walitajwa kuhusika na vitendo vya kutia vinyesi katika visima, kuchoma moto shule na mambo kadhaa wakadhaa.

 

Ingawaje hoja zilijengwa juu ya suala hili.  Kwa mfano, itakuwaje wakaazi wa eneo ambalo wote ni CUF watie kinyesi katika kisima ambacho wao wenyewe wanatumia maji yake na ikawa hawana pengine pa kupata maji hayo kwa karibu, au shule iliyojengwa na wananchi kwa nguvu zao na ambayo watoto wao wanatumia shule hiyo na eneo hilo wakaazi wake wote wakawa ni CUF halafu waichome moto skuli hiyo walioijenga wenyewe na wanayosoma watoto wao?

 

Ni ajabu ya kweli lakini tume iliarifiwa kwamba tarehe 03 Januari 1996 kwa barua yenye Ref No. KAS/P/SO.7/2/A/119 iliyoandikwa na kamanda wa polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba SACP, marehemu Ahmada Juma Chum kwenda kwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kaskazini Pemba na Mratibu wa CUF Mkoa wa Kaskazini Pemba, iliyowataka kuweka ulinzi wa kienyeji ili kuzuia vitendo vya uchomaji moto na upakaji vinyesi katika mkoa wao, ambapo pia ilielezwa katika barua hii kwamba polisi wataendelea kufanya doria kama kawaida katika maeneo ya mkoa huo.

 

Katika kutekeleza agizo hili ambalo tume ilipewa nakala ya barua hiyo:  wananchi wa Shengejuu walifanikiwa usiku wa manane siku moja kuwakamata maafisa wa usalama wa taifa wakiwa na gari lao lenye namba za usajili za kiraia wakichoma moto kwa petroli shule ya Shengejuu.

 

Wakati wa kujihami wanausalama hao inadaiwa kunyang’anywa bunduki moja aina ya SMG. Siku ya pili Televisheni Zanzibar (TVZ) ilibahatika kuonyesha gari hilo Alfajiri yake likisafirishwa kwa meli ya MV.  Jitihada kutokea Wete kurudishwa Unguja, pia walionyeshwa majeruhi wakiwa katika hospitali ya Mnazi Mmoja, kwa haraka wananchi waliwatambuwa kuwa baadhi yao walikuwa si wana wa usalama, bali walikuwa ni wakereketwa maarufu wa CCM huko Jang’mbe.  Kwa mfano, alikuwemo Ngurwa  Ngurwa na wenzake.  Ngurwa Ngurwa ni mwana maskani maarufu, picha hiyo haikuoneshwa tena katika TVZ hadi leo.

 

Kadhalika kilichowashangaza watu mara baada ya tukio ni gari hilo la Wanausalama, kukimbiziwa Unguja kabla ya hata kufunguliwa faili ya kesi.  Pili, ni polisi kuanza kazi ya kuingia majumbani kupiga watu, kuharibu mali, kuiba na kubaka.

 

Kijiji kizima cha Shengejuu kikahamwa na watu  wake wakakimbilia katika miji nyengine na misitu ya kaibu, kadhia hiyo ilidumu kwa muda mrefu. Watu wasiopungua ishirini na moja wakawekwa ndani akiwemo Mwakilishi wa jimbo la Pandani Mhe. Salim Yussuf aliyetangazwa na Rais wa Zanzibar kwa wakati huo Dr. Salmini katika mkutano wa hadhara hapo katika viwanja vya Malindi Unguja kwamba Mwakilishi huyo na aruke apae lakini wakimpata ataozeana ndani jambo ambalo walilitekeleza.  Mahabusu walikaa ndani zaidi ya miezi sita na wakapata mateso makubwa.

 

Nae Hakimu wa Mkoa aliewapa dhaman mahabasu hao baada ya muda mrefu kupita Mhe. Adam Salim Abdulla alifukuzwa katika kisiwa cha Pemba kwa notice ya masaa 24 na aliyekuwa Mkuu wa Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Marehemu Salim Nassor.  Kwa barua yenye Ref No. MKP.4/2/VOL. 1/139 ya tarehe 18/03/1996 ambapo katika barua hiyo kuna kifungu kinachosema “kwa barua hii nakupa muda wa wiki moja uwe umeshahama katika Mkoa huu”, baada ya kuwa hakimu huyo hakutii amri hiyo aliandikwa barua ya ukumbusho tarehe 28/031996 yenye Ref No. MKP.4/2/VOL.11/149 ambapo sehemu ya barua hii ilisema “nimekupa muda wa wiki moja uhame katika mkoa huu, lakini inaonekana kuwa bado hutaki kuhama.  Na kuletea barua ya mwisho kukutaka uhame kabla ya muda niliokupa haujamalizika”.  Barua zote hizo zilinakiliwa kwa Jaji Mkuu wa Zanzibar Bwana Hamid Mahmoud ambaye hakusema lolote kuhusiana na suala hili, hata ile heshima ya Mahkama kuwa ni chombo kisichoingiliwa haikuwepo.  Mkuu wa Mkoa alibeba mamlaka ya kumfukuza Hakimu wa mkoa kwa Notice ya masaa 24 tena katika Mkoa aliozaliwa Hakimu huyo.

 

Mhe. Adam alikuwa Hakimu pekee wa Mkoa katika Mkoa wa Kaskazini Pemba aliyehamishiwa huko kutoka Mahkama Kuu ya Vuga.  Hadithi hii ya kuwapa dhamana watuhumiwa hao ukieleza ni refy mno lakini tume pamoja na kuelezwa kwa mdomo, kupewa nyaraka na ukanda wa video unaoionyesha shengujuu na madhila yake hili hawakuona kuwa ni jambo la kuripoti zaidi ya uchomaji wa ghala la Karafuu la ZSTC na Nyumba ya Mkuuk wa Polisi.  Kesi hiyo ya shengejuu pamoja na mateso yote waliyopata watuhumiwa ilifutwa kwa watuhumiwa hao kutokupatikana na hatia na wakaachiwa huru.

 

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s