Rais Kikwete jua linatua lini?

Date::12/31/2008

Na Eunice Kanumba

DESEMBA 30, 2008 ilitimia miaka mitatu kamili tangu Rais Dkt Jakaya Kikwete atoe hotuba yake ya kulizindua Bunge kwa mara ya kwanza toka atawazwe kuwa Rais wa awamu ya nne wa Jamhuri yetu.

Hotuba yake ilikuwa dira kwa Watanzania ambayo ilioonesha mambo yaliyopewa kipaumbele kutekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano

Kimahesabu muda huo aliokalia kiti cha Urais sasa ni asilimia 60 ya muda wa muhula wa uongozi wa miaka mitano Mafanikio yaliyopatikana katika sekta mbalimbali yanachapishwa na kutangazwa na Wizara mbalimbali kupitia vyombo vya habari lakini yale ambayo hayajatekelezwa hayachapishwi na kutolewa sababu za kukwama kwake.

Muda uliobaki ni mfupi mno na kuna dalili za kutotekelezwa yale aliyoyaahidi kwenye hotuba yake Desemba 30, 2005 ambayo wengi wanaitumia kama kipimo.

Ingawaje Rais mwenyewe amekuwa akipita na kujigamba kuwa wananchi wasiwe na hofu itakapofika 2010 yote aliyoyaahidi yatatekelezwa lakini muda umeshakuwa kikwazo kwake.

Rais Kikwete kupitia hotuba yake hiyo alisema kuwa amedhamiria kumaliza kabisa mpasuko wa kisiasa katika visiwa vya Unguja na Pemba ambapo alisema kuwa unatokana na sababu za kihistoria za wananchi wa kisiwa hicho kusimama kwenye mistari yao ya kihistoria wakati wa mapambano ya kujitawala. Ikiwa hilo kweli litatimia katika muda uliosalia, basi utakuwa ni muujiza.

Shinikizo lilipotoka kwenye vyombo vya habari Rais Kikwete aliwasukuma atendaji katika chama chake CCM kuanza mjadala na viongozi wa Chama Cha Wananchi CUF kufikia mwafaka utakaoondoa mpasuko huo, ambao umeweka dosari kubwa ya Tanzania machoni mwa walimwengu ambao nao walidhani ufumbuzi wa kudumu utapatikana.

Mazungumzo hayo yalichukua muda mrefu huku ahadi zikitolewa za kuwataka Watanzania kuwa na subira. Hatimaye mazungumzo hayo yakikwama mbele ya Rais Kikwete pale Butiama na waliokwamishwa ni wanaCCM wenzake ambao wamesimama kwenye mstari ule ule alioubainisha Rais Kikwete kuwa ni chanzo cha mgogoro huo.

Toka mazungumzo yaliposimama hadi leo si kipaumbele tena kwa Rais mwenyewe wala wasaidizi wake hakuna anayekerwa na tatizo hilo. Hata maandalizi ya pendekezo la CCM la Wazanzibari kupiga kura za maoni kuhusu uundwaji wa serikali ya mpito hazioneshi dalili kuwa zinaweza kufanyika haraka na kuzaa matunda kabla ya mwaka 2010.

Kukwama kwa mazungumzo hayo kumezaa mazingira mapya ya Watanzania kuanza kuhoji juu ya dosari za muungano na serikali kutoa majibu rahisi kwa maswali magumu. Mazingira ya mwafaka wa kisiasa ni ajenda inayopuuzwa kila mara lakini matokeo ya uchaguzi mkuu ndiyo yanayotuumbua na wanasiasa hutumia mwafaka kama mtaji wao kisiasa.

Mgogoro wa Zanzibar si wa kubeza, mabilioni ya fedha na muda mrefu vimetumika kuwezesha mwafaka kufanikiwa. Ahadi ya Rais Kikwete bungeni tunadhani haikuwa porojo, ndio maana wanahabari walishinikiza kutekelezwa mwanzoni mwa muda wa uongozi. Kadri muda unavyokwenda ukingoni lisipotekelezwa na kuzaa machafuko basi Kikwete atalaumiwa.

Ajenda nyingine muhimu ya kisiasa inayongojewa na Watanzania wengi itekelezwe ni kauli ya Rais Kikwete siku hiyo hiyo huko Bungeni mjiini Dodoma iliyohusu matumizi makubwa yanayofanywa na vyama vya siasa wakati wa kampeni za uchaguzi. Hakuna hata harufu ya kuanza kwa mchakato wa kudhibiti vyama kutotumia fedha nyingi.

Badala yake vyama hivyo vimezidisha matumizi. Uchaguzi mdogo wa Tarime na huu wa Mbeya Vijijini ni ithibati kuwa ndani ya kipindi cha uongozi wa Rais Kikwete kichosalia haitawezekana kukamilisha mchakato wa kisheria wa kuzuia vyama visimwage fedha ovyo kwani athari zake ni kuinyima demokrasia haki ya kutawala

Matumizi makubwa ya fedha ndio chimbuko la ufisadi serikalini ingawa serikali inalipinga hili lakini historia na matukio toka turejee kwenye demokrasia ya vyama vingi inathibitisha kuwa fedha nyingi huchotwa ndani ya serikali kwa kutumia makada wa CCM ambao hupewa dhamana na kukubali kutumia madaraka yao vibaya.

Watanzania wanajiuliza kwanini kila baada ya uchaguzi mkuu kumalizika hujitokeza kashfa zinazowahusu mawaziri na viongozi waandamizi serikalini. Mara baada ya Uchaguzi mkuu wa 1995 waliokuwa mawaziri wa fedha Simon Mbilinyi na Naibu wake Kilontsi Mporogomyi walilazimika kung’oka kwa kilichodaiwa kutoa misamaha ya kodi.

Sambamba nao Waziri Juma Ngasongwa pia alituhumiwa kuhusika na upotevu wa mamilioni ya fedha kwa kutoa misamaha kwa minofu ya samaki. Uchaguzi mkuu wa mwaka 2000 aliyekuwa Waziri wa Biashara na Viwanda Iddi Simba aliondolewa madarakani baada ya kubainika alitoa ovyo vibali vya uagizaji sukari nje ya nchi.

Mwaka 2005 tuhuma za ufisadi katika akaunti ya madeni ya nje ya Benki Kuu ya Tanzania, EPA na miradi ya ujenzi na ununuzi wa majengo ya mifuko

ya hifadhi ya jamii ya NSSF na PSPF mabilioni ya fedha hizo yanadaiwa kutumika kwenye Uchaguzi Mkuu uliopita, Watanzania wanajiuliza inakuwaje hayo hutokea kila baada ya uchaguzi mkuu?

Matumizi makubwa ya fedha yanayofanywa na vyama vya siasa wakati wa kampeni za uchaguzi ni matumizi mabaya ya rasilimali za umma. Kudhibiti suala hili kama alivyoahidi Rais Kikwete ilikuwa faraja kwetu tulitegemea fedha hizo badala ya kumwagwa ovyo kuelekezwa kwenye uzalishaji au kuimarisha huduma za kijamii.

Kama ambavyo wanasiasa wamekuwa wakisisitiza kuwa viongozi wanaoingia madarakani kwa rushwa au ghilba zozote ni dhahiri serikali watakayoiunda haitaweza kuwa na ujasiri wa kupambana na rushwa na ufisadi kwani ni lazima iwe sehemu ya maisha na ni shamba la wanasiasa kuvuna mamlioni ya fedha kila wakati wa uchaguzi unapofika.

Kuchelewa kwa serikali kushughulikia suala hili kumeleta matatizo ya uendeshaji serikalini na hasa baada ya kashfa ya mradi wa kufua umeme wa dharura ulioihusisha kampuni ya Richmond. Rais Kikwete alibaini na kutamka wazi ni lazima viongozi watenganishe biashara na siasa na kuahidi kuanza mara moja kushughulikia suala hili.

Ahadi hizi mbili za kisiasa za Rais Kikwete zilitakiwa zianze kwa kufanya pestroika ndani ya CCM kwani waliokwamisha mwafaka wa kisiasa ni viongozi waandamizi wa CCM. Akiwemo Makamu wake upande wa Zanzibar ambaye amesimama kwenye mistari ya kihistoria ambayo ndio chimbuko la kuendelea kwa mgogoro huo wa muda mrefu.

Matumizi makubwa ya fedha wakati wa kampeni chama kinachoongoza ni CCM na kwamba ni lazima Rais aanzie ndani ya chama chake kuweka utaratibu utakaodhibiti matumizi makubwa. Hivi kutumia shilingi billioni moja kwenye uchaguzi mdogo wa jimbo la Mbeya vijijini wakati wa kampeni ni matumizi madogo?

Chanzo: http://mwananchi.co.tz/newsre.asp?id=8942

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s