Zanzibar kama Marekani, Umoja wa Kitaifa unawezekana!

Farewell Remarks
Serena Hotel, Unguja Zanzibar
January 8, 2009
Hotuba ya Mheshimiwa Mark Green, Balozi wa Marekani Tanzania

Wazanzibari na Wamarekani ni marafiki kwa miaka mingi. Uwepo rasmi wa Marekani katika ardhi ya Zanzibar ulianza tangu mwaka 1833 ambapo mkataba kati ya Marekani na Oman ulitoa fursa kwa Marekani kufungua Ubalozi mdogo hapa.Tumekuwa washirika wenu wa kibiashara tangu meli ya kwanza ilipotia nanga kwa mara ya kwanza hapa, ikitafuta mafuta ya nyangumi kwa ajili ya kumulika mitaa ya miji ya Marekani. Baadaye, walileta nguo za pamba na bunduki, kwa kubadilishana na pembe na gundi.

Leo karibu miaka 200 baadaye, tumebaki kuwa wanunuzi wakubwa wa mazao yenu ya kilimo, hasa zao la mwani. Watalii wa Kimarekani wametoa mchango mkubwa katika mafanikio ya biashara ya utalii. Kitu kimoja nilichojifunza katika uhusiani wetu na Tanzania ni kwamba, kibiashara na hasa mahusiano ya kibinafsi siku zote hutangualia kwanza, na ya Serikali hufuata baadaye kuja kuyafanikisha haya. Kabla kufika na kuondoka kwangu hapa uhusiano wa kudumu wa wananchi wetu utaendelea kubaki.

Tunaiheshimu historia ya Zanzibar, mafanikio yake kiutamaduni na muungano wake wa kipekee na Tanzania bara. Zanzibar imechangia kwa kiasi kikubwa maendeleo na uanzishwaji wa lugha na utamaduni uliosambaa eneo lote la Afrika Mashariki na zaidi. Muziki wenu, uchoraji, fasihi yenu, sanaa zenu za mikono na busara iliyomo katika methali zenu zimechangia urithi wa utamaduni duniani kwa kiasi kikubwa kuzidi idadi yenu ya watu.

Ninawasihi kuuenzi na kuuheshimu urafiki huu wa muda mrefu kadiri ninavyotoa maangalizo kuhusu historia yetu. Ninatoa nasaha hizi kama mwakilishi wa watu ambao walishakuwa na uzoefu kama wenu.

Historia ni utambuzi wa yaliyotokea zamani ili tuweze kuyadhibiti yanayotokea sasa. Maoni yetu ya kilichotokea zamani yanatofautiana toka kwa mtu mmoja hadi mwingine, toka nyakati hadi nyakati, lakini kitendo cha kujitathmini mwenyewe ni muhimu katika kuboresha hali zetu.

Nimeshanya safari nyingi hapa Zanzibar, zikiwemo za kibinafsi, na marafiki na pia na familia yangu. Nimeshafika kaskazini na kusini mwa visiwa hivi na kufanya mazungumzo na Watanzania katika miji ya Pemba na Unguja.

Huwaomba marafiki zangu wa Kizanzibari kukumbuka kwamba ninaongea kama rafiki na msamaria mwema. Marafiki huzungumza kwa uwazi, ukweli bila kufichana. Ningependa kuongea nanyi kuhusu uzoefu wa nchi yangu katika kupambana na masuala ya kisiasa yanayofanana na haya yanayoukabili uongozi wa Zanzibar leo.

Ningependa kuongea nanyi jioni ya leo juu ya vipengele vichache vya historia ya Marekani na kupendekeza hoja kadhaa kwa viongozi wa Zanzibar kuzifikiria, wakati huu wanapofanya mashauriano ya pamoja katika kutafuta suluhisho la masuala muhimu ya sasa, ili hatimaye kuja kuipata Zanzibar yenye maendeleo kesho.

Hasa ningependa kuwaelezea juu ya uvumilivu wetu wa kisiasa, na kugawana madaraka na ustawi unaopatikana kutokana na usuluhishi. Labda mnaweza kujifunza kutokana na makosa kadhaa ambapo Marekani ilikwishayafanya zamani.

Historia ya nchi yangu inafanana na ya Zanzibar katika namna kadhaa. Sisi pia tulikuwa na mapinduzi dhidi ya ufalme. Ni muhimu ieleweke kwamba mwishoni mwa miaka ya 1700 sio Wamarekani wote waliokubaliana na mapambano ya uhuru dhidi ya Mfalme wa Uingereza. Vita yetu ya uhuru toka Uingereza, kwa kiasi fulani, ilikuwa ni vita ya wenyewe kwa wenyewe miongoni mwa Wamarekani. Wakati majeshi ya mapinduzi yalipoteka eneo fulani, ilikuwa kawaida kwa mali za waliomtii Mfalme kutaifishwa na Serikali ya Mapinduzi. Walio watiifu walikamatwa na kuchukuliwa kama majasusi. Baada ya kushindwa kwa Uingereza maelfu ya waliomtii Mfalme waliyakimbia makoloni hayo ya zamani. Wengi wao waliomba hifadhi nchini Kanada, ambapo siku hizi ni nchi mojawapo ya nchi za Jumuia ya Madola.

Kimsingi, sisi Wamarekani tunaamini kwamba kila mtu anayo haki ya kutoa maoni yake. Hatahivyo, wakati wa mapambano ya kufa au kupona dhidi ya dola iliyokuwa na nguvu duniani wakati huo, viongozi wetu hawakuruhusu haki hiyo itolewe kwa wale walioamini kwamba ilikuwa wajibu wao kuwa watiifu kwa Mfalme. Baada ya kupata uhuru, tulikabililiwa na mtihani mwingine wa uvumilivu wa kisiasa, ambapo makundi mawili yaliyopingana vikali yaliibuka ndani ya jamii ya Kimarekani. Rais wetu wa awamu ya pili, John Adams, alihofu kwamba makundi haya yangeisambaratisha nchi. Aligundua kwamba kila kundi lilikuwa likiungwa mkono na mojawapo na mataifa makubwa yenye nguvu wakati huo, Uingereza na Ufaransa, yalikuwa yakishiriki katika vita kuu ya dunia. Alitaka kuiendeleza sera ya kutofungamana na upande wowote ya Baba wetu wa Taifa, George Washington. Alileta sheria ziliyojulikana kama sheria za uchochezi na ugeni, ambazo pamoja na mambo mengine, zilizuia kwa kiasi kikubwa haki ya uhuru wa kujieleza. Alizitetea sheria hizi kwamba zilikuwa za lazima katika kuzuia makundi ya kisiasa kutolibomoa taifa.

Wanahistoria walilipima suluhisho lake hili kwa ukali, kama walivyomfanyia wapiga kura wa Kimarekani. Juhudi zake za kutaka kuchaguliwa tena zilishindikana. Sheria hizi zilikuja kufutwa baadaye na mrithi wake kwa misingi kwamba zilionekana kama ni tusi kwa haki za binadamu. Kurejeshwa kwa haki ya uhuru wa kujieleza na kutoa maoni kisiasa kumechangia kurejea kwa utulivu katika jamii. Hatari ambazo Rais John Adams alizihofia zilikuwa za kweli, lakini suluhisho bora lingekuwa kwa Rais John Adams kutumia ushawishi wake kupooza mlipuko wa hasira na kutoa wito kwa viongozi wote kuweka mbele maslahi ya muda mrefu ya Taifa dhidi ya maslahi ya muda mfupi ya kisiasa.

Tukirudi upande wa Zanzibar, Nimegundua kwamba kuna majibizano makali kutoka kwa baadhi ya wafuasi kwenda kila upande wa siasa dhidi ya wapinzani wao. Tofauti za kweli za kisiasa, zinaweza kuwepo, na ni budi zijadiliwe kwa heshima miongoni mwa raia wenye lengo sawa la ustawi na maslahi kwa jamii yao. Hali ya hewa kisiasa hapa visiwani itaimarika iwapo viongozi wa vyama vikuu vya kisiasa watatangaza hadharani kwamba wanawaheshimu wapinzani wao kama ni Wazanzibari na Watazania walio wazalendo.

Demokrasia ni majadiliano na majadiliano huhitaji heshima toka kila upande. Kwa namna yoyote ile, fanyeni majadiliano, midahalo na ikibidi bishaneni katika kutafuta njia sahihi kwa ajili ya Zanzibar, lakini ikumbukwe kwamba wapinzani wa kisiasa sio maadui. Viongozi wana wajibu wa kuwaelekeza wafuasi wao juu ya ukweli huu na kuwasahihisha wafuasi wao wanaoweka maslahi ya chama mbele badala ya maslahi ya wananchi. Viongozi wenye kuwajibika huwakemea wafuasi wao wasiowajibika.

Katika miaka ya1860 Marekani ilipigana vita ya wenyewe kwa wenyewe. Tulipigania kwa kiasi gani uhuru ulikuwepo ndani ya Serikali ya Kitaifa. Tulipambana dhidi ya utumwa. Vita hiyo ilileta machafuko dhidi ya raia wasio na hatia na uharibifu wa mali zao. Baada ya kumalizika kwa vita hiyo ilituchukua miaka mingi kupata ahueni. Miongo kadhaa baadaye, katika kipindi hicho hicho cha kihistoria tumeibuka na kuwa taifa kubwa lenye nguvu duniani, pia tulianza kuijenga upya jamii yetu na kuleta maendeleo makubwa kwa kuleta mapatano kati ya watu weusi na weupe katika namna ambayo haikushughulikiwa kwa miaka 100 baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe. Maeneo yaliyotawaliwa na kiwango kikubwa cha ubaguzi ndio yalikuwa maskini zaidi, yenye kiwango duni cha elimu, na ndio maeneo yaliyotawaliwa vibaya nchini. Mara tu hatua nzuri ilipofikiwa katika usuluhishi, maeneo haya yaliimarika zaidi kiuchumi, kijamii na na kisiasa.

Zanzibar inafanana na historia yetu ya huzuni na machafuko ya kisiasa, utumwa na athari mbaya za migawanyiko kisiasa na kijamii. Sote tunajua kwamba mwisho wa utawala wa kikoloni hapa Zanzibar ulifuatiwa na machafuko dhidi ya Serikali huru wakati huo. Kwa bahati mbaya, machafuko haya yalileta machafuko kwa raia kama ilivyotokea wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Marekani. Inahitaji moyo wa uvumilivu wa kisiasa, uwazi na kufanya mijadala ya wazi juu ya matukio mabaya ya kihistoria ili kuweza kuikubali historia yenye machungu ili hatimaye nchi iweze kuendelea mbele. Nchi yangu inalijua hili, kwasababu tulifanya hivi ili kuweza kukabiliana na maumivu yaliyobaki, yaliyosababishwa na matukio yetu ya zamani.

Kwa ruhusa yenu sasa niongelee juu ya dhana ya kugawana madaraka. Katiba yetu, chombo cha juu kabisa kisheria nchini Marekani, imegawa madaraka kati ya Serikali kuu na Serikali ya majimbo. Katika ngazi zote madaraka yamegawanywa zaidi kati ya Serikali kuu, Bunge na Mahakama. Ni kawaida nchini Marekani kwa chama kimoja kuongoza Serikali kuu wakati chama kingine kikiongoza Bunge. Ni kawaida kwa Rais kuteua baadhi ya mawaziri kutoka chama cha upinzani. Rais Bush ameyafanya haya, kama alivyofanya aliyemtangua Rais Clinton. Rais Mteule Obama naye amefanya hivyo hivyo kwa kwa kuwateua wanachama wawili wa chama cha upinzani kuongoza wizara mbili za Serikali yake, ikiwemo Wizara ya Ulinzi. Vivyo hivyo, Bungeni ni kawaida kwa wabunge wa chama kimoja kuungana na wa chama cha upinzani kuiunga mkono sheria inayopingwa na uongozi wa chama chao wenyewe. Hakuna kiongozi atakayeweza kuendesha kila kitu anavyotaka yeye milele. Hakuna chama kinachoshinda madaraka kwa asilimia 100%. Hakuna chama kilicho nje kabisa ya mfumo wa madaraka. Mpinzani wa leo anaweza kuwa rafiki wa kesho. Haipaswi kundi moja la kisiasa lijisikie limetengwa na Serikali.

Nashawishika kusema kwamba kiasi kikubwa cha maumivu ya kisiasa ya Zanzibar yamechipuka kutokana na kutengwa kisiasa. Enzi za utawala wa Omani, Ureno, Sultani na Uingereza, madaraka yalikuwa mikononi mwa wachache. Hakukuwa na mashauriano au kufikiria maslahi ya Wazanzibari walio wengi, au kama kulikuwepo ni kwa kiasi kidogo sana. Upande mmoja ulikuwa na madaraka yote na upande mwingine haukuwa na kitu. Kupoteza madaraka ilikuwa ni kupoteza kila kitu. Kwa kiwango fulani utamaduni huu bado upo hadi leo. Ingawa mfumo wa Serikali umebadilika na sura ya namna ya utawala imebadilika, dhana ya kukosa ama kupata, utamaduni wa kisiasa wa mshindi kujitwalia kila kitu haujabadilika. Ninaamini kwamba ili nchi ya Zanzibar na uchumi wake viweze kustawi, na ili Zanzibar iweze kuzitumia raslimali zake kiukamilifu, utamaduni huu inabidi ubadilike kwa kuwepo maafikiano, heshima kwa kila upande na kugawana madaraka.

Kama wengi wenu mjuavyo, kabla utumishi wangu wa kuwa mwanadiplomasia, nilikuwa mwanasiasa. Nilifanya kazi katika ofisi ya umma kama mwanachama wa chama cha Republican. Watanzania wengi wana wasiwasi na kuendelea kwa shughuli mbalimbali kuu za Marekani hapa nchini. Rais Bush amefanikisha mpango mkubwa wa kupambana na ugonjwa sugu — UKIMWI — ambao dunia imepata kuushuhudia. Mpango wa Rais wa kupambana na Malaria umewezesha kupungua kwa kiwango kikubwa idadi ya vifo vinavyosababishwa na ugonjwa huu hapa visiwani. Mpango wa Millennium Challenge, unaofadhili mradi wa kuboresha na kuunganisha umeme hadi bara na barabara za Pemba, ni kielelezo kingine muhimu cha dhamira yetu hapa. Nawahakikishieni kwamba shughuli hizi za kati ya watu na watu zinaondoa uhasama wa kisiasa nchini Marekani. Mwezi Agosti nilipata bahati ya kuwa jijinini Washington wakati Rais Kikwete alipokuwa na mkutano na Rais Bush katika ikulu ya Marekani. Rais wangu alimuhakikishia Rais wenu kwamba ushirikiano wetu uliopo utaendelea hata katika utawala mpya ujao – bila kuja Rais wa Marekani ni nani.

Katika ziara hiyo, nilifuatilia mwenyewe mipango ya misaada hii katika Bunge letu la Marekani – Bunge linalodhibitiwa na chama cha Democratic chini ya Rais ambaye ni Rebublican. Viongozi kutoka vyama vyote vikuu walishirikiana na hatimaye kuidhinisha fedha kwa ajili ya miradi yetu muhimu hapa nchini Tanzania kwasababu wameona busara ya kuimarisha ushirikiano wetu na watu wa Tanzania. Huu ndio mfano wa tabia ninayoizungumzia. Wapinzani kisiasa? Sawa! Maadui? Kamwe, hapana! Kinachotuunganisha ni kikubwa na kina nguvu zaidi kuliko kinachotutenganisha.

Mwanachama wa kwanza wa chama changu aliyechaguliwa kuwa Rais wa Marekani Abraham Lincoln aliwahi kusema, “Karibu wanadamu wote wanaweza kuivumilia dhiki, lakini ukitaka kupima tabia ya mmoja wao, mpe madaraka.” Nimepata heshima ya kukutana na viongozi wa Zanzibar na ninaamini kwamba wanaweza kuushinda mtihani kama huu. Pia, naomba niweke wazi kwa viongozi wa pande zote kwamba uhusiano wetu na watu wa Zanzibar ndio kimaumbele kuliko uhusiano wetu na kiongozi wa yeyote au chama fulani.

Ni pale tu ushindani wa kisiasa Zanzibar utakapofanyika ndani ya mfumo, na utaratibu utakaowakikishia raia wote kwamba haki zao zote zinaheshimiwa, hata wapinzani wao kisiasa wako madarakani, ndipo utawala utaimarika, tofauti kubwa za rasilimali zilizopo visiwani kwa sasa zitaondoka na fursa za kiuchumi visiwani zitatumika ipasavyo. Hili ni jambo la kimaadili kulifanya. Ni jambo la kutumia akili ya kawaida. Pia ni jambo zuri kibiashara kulifanya. Kila mmoja anashinda. Wawekezaji, watalii wanavutiwa na maeneo yenye utawala mzuri na yaliyotulia. Wanakaa mbali na maeneo yenye majanga ya vita na utawala mbovu. Kugawana madaraka sio suala la upande mmoja kupoteza kitu fulani na upande mwingine kujipatia kitu fulani. Kugawana madaraka ni namna bora kwa Wazanzibari na vyama vyote vikuu vya kisiasa kujihakikishia usalama na ustawi visiwani. Hiki ndicho tunachowatakia marafiki zetu wote wa Zanzibar. Hiki ndicho sisi wenyewe tulikishuhudia wakati maeneo ya nchini kwangu yaliyoathirika kwasababu ya migawanyiko mibaya ya kijamii ilipoanza kupatana. Matokeo ni kupata jamii iliyotengemaa, utawala ulioimarika na ustawi mzuri.
Viongozi lazima wawasaidie wafuasi wao kuona kwamba Wazanzibari wanashuhudua siasa ambazo hakuna anayejiona ameshinda kabisa na wala hakuna aliyeshindwa kabisa. Katika siasa za aina hiyo walio wengi watagundua kwamba wanahitaji kuwafanyia kazi nzuri wapigakura, vinginevyo watajikuta wako katika kundi la wachache. Wapiga kura huvipima vyama vya siasa na wanasiasa kwa kazi nzuri wazifanyazo, na sio kwa kitu chochote kingine kama utambulisho wao kimakabila au kimikoa wanayotoka au kwa uaminifu na utiifu wao kihistoria.

Rais Kikwete alipoingia madarakani, alitangaza kwamba mwafaka visiwani Zanzibar ni kipaumbele katika masuala ya ndani ya nchi. Alisema, “Najua kwamba uamuzi wa mwisho kuhusiana na mustakabali wa kisiasa na uongozi wa Zanzibar unategemea na Wazanzibari wenyewe. Lakini tuna Jamhuri moja, nchi moja. Kitakachotokea Zanzibar kinatuathiri sisi sote.” Sera ya nchi yangu ni kuunga mkono juhudi za Rais Kikwete kwa kushirikiana na viongozi wa Zanzibar hatimaye kuleta mwafaka hapa visiwani.

Rais wa Marekani John F. Kennedy, rafiki wa Afrika aliwahi kusema,” Kamwe tusifanye mazungumzo kutokana na hofu, bali kamwe tusihofu kufanya mazungumzo” Tukiwa kama marafiki wa Tanzania, tena marafiki wa miaka mingi, naomba niwashauri kwamba hivi vyama viwili visiogope kufanya mazungumzo. Mazungumzo ambayo kila upande utatoa… na kila upande utanufaika.

Nina hakika kwamba viongozi wa kisiasa wa Zanzibar waliopo sasa wana uwezo wa kufikia makubaliano ya kugawana madaraka na kuyatekeleza makubaliano hayo kwa moyo wa dhati kwa maslahi ya Wazanzibari wote. Ninaamini kwamba viongozi hawa watakubaliana juu ya utaratibu utakaojenga imani kwa watendaji wote kisiasa ili uchaguzi wa Zanzibar wa mwaka 2010 uwe huru, wa haki na amani. Hili ni jambo muhimu sana kwasababu Zanzibar haiwezekani kuruhusu uchaguzi mwingine wenye utata na mabishano. Uundwaji wa Serikali yenye kugawana madaraka ifikapo mwak 2010 ni lazima utokane na ridhaa ya wananchi wa Zanzibar kama watakavyoonyesha katika uchaguzi utakaokuwa wa amani, huru na wa haki. Uhakika wangu unatokana na imani kwamba viongozi wa vyama vinavyopingana mioyoni mwao wanaitakia maslahi mema nchi yao ya Zanzibar, na kwa uelewa wangu kwamba viongozi wa Zanzibar wanatakiwa kila la heri na wanaweza kupata msaada kutoka kwa Watanzania wenzao walio katika Serikali ya Muungano na watu wa Marekani.

Asanteni kwa kunipa heshima hii na kuwepo hapa jioni hii. Nimefarijika kupata nafasi ya kufanya kazi hapa, na nawatakia kila la heri.

Asanteni

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s