Hamad atoa uthibitisho wa ZEC kupewa maelekezo

Na Mwanne Mashugu, Zanzibar

Maalim Seif Sharif, Katibu Mkuu wa CUF

Maalim Seif Sharif, Katibu Mkuu wa CUF

HATIMAYE Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharrif Hamad, ametoa ushahidi kuhusu tuhuma alizozitoa kuwa Tume mpya ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) imekuwa ikitekeleza majukumu yake kwa kufuata maelezo ya Idara ya Usalama wa Taifa.

Maalim seif alitoa ushahidi huo jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari siku chache tangu atakiwe kuthibitisha tuhuma alizotoa mwezi uliopita na mwenyekiti wa ZEC, Khatib Mwinyichande.

Hamad, alisema kwa mujibu wa ripoti ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar ya mwaka 2005, iliyotolewa mwaka 2006, ukurasa wa 66, imeelezea matatizo ya uchaguzi mkuu wa 2005, ikiwemo vitendo vya vikosi vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kukiuka sheria za uchaguzi na viongozi wa serikali ya mitaa (masheha) kuingilia kazi za uandikishaji na kukataa maelekezo ya tume hiyo yaliyokuwa yakitolewa katika uandikishaji.

Aidha, alisema ukurasa wa 68 wa ripoti ya uchaguzi kifungu (g) kimeelezea matatizo ya tume hiyo ilivyokuwa ikingiliwa katika shughuli zake hasa katika uandikishaji wa wapiga kura kulisababishwa na vikosi vya SMZ mfano kuandikisha askari bila ya kufuata utaratibu wa sheria.

Hamad alisema vikosi vilitembelea vituo vya uandikishaji bila ya indhini ya Tume ya Uchaguzi wala taarifa kabla ya kufanya hivyo.

‘‘Katika maelezo ya vifungu nilivyovinukuu hapo juu, ZEC inathibitisha kwa maandishi yale kwamba vyombo vya SMZ vinaingilia utendaji wa Tume kama ilivyotajwa katika ripoti zote mbili,” alisema Hamad.

Alisema mwenyekiti wa tume hana njia ya kukwepa kwa sababu wakati hayo yakitendeka alikuwa ni Kamishna wa Tume ya Uchaguzi na ameweka saini katika ripoti zote za tume.

“Uthibitisho huo, ambao yeye mwenyewe amethibitisha kwa saini yake, namtaka mwenyekiti wa ZEC Mwinyichande awajibike kwa kujiuzulu kama alivyoahidi,” alisisitiza Hamad.

Alisema kwamba utendaji wa ZEC umekuwa haupo wazi kwa kuwa sekretarieti ya tume hiyo inafanya kazi kwa maelekezo ya Usalama wa Taifa ndiyo maana haijafanyiwa marekebisho licha ya ripoti ya wataalamu wa muafaka kushauri sekritarieti ifanyiwe marekebisho kuzingatia viwango vya elimu na uzoefu wanaopaswa kuwa nayo kabla ya kuteuliwa.

Alibainisha kuwa watendaji katika sekritarieti hiyo ni wale wale wanaolalamikiwa kuhusika na kuchafua chaguzi zote tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1995.

Alisema Tume ya Rais wa Zanzibar ya kusimamia utekelezaji wa muafaka wa 2001, iliwateua wataalamu wa kushauri mfumo bora wa kuwa na sekritarieti iliyoongozwa Profesa Chris Maina Peter na Ron Gould kutoka Canada, lakini mapendekezo yao hayajafanyiwa kazi.

Aliongeza kuwa CUF inaamini kuwa ZEC imekuwa ikifanya kazi kwa maelekezo ya Usalama wa Taifa kwa kuwa Kampuni iliyoteuliwa kufanya kazi ya kubadili kadi za kupiga kura kutoka analogue kwenda digital ni kampuni ya On Track Innovations (OTI) ya Israel, wakati kampuni hiyo hiyo ndiyo iliyopewa kazi ya kutengeneza vitambulisho vya Mzanzibari mkaazi mwaka 2005.

Alisema CUF hivi sasa inafuatilia kupata ukweli kuhusu taarifa kwamba Kampuni ya OTI ilihusika na uvurugaji wa daftari la wapiga kura nchini Guinea, Afrika Magharibi wakati wa utawala wa Rais Lansana Conte.

“Mkurugenzi wa Idara ya Uandikishaji na utoaji vitambulisho vya Mzanzibari, Mohammed Juma Ame, anafahamika kuwa ni afisa wa ngazi ya juu wa Usalama wa Taifa,” alisema Hamad.

Naye Mkurugenzi wa vitambulisho, aliyetambukika kwa jina moja la Ame, amekanusha madai ya Hamad na kuyaita hayana msingi wowote kwa vile vitambulisho vya Mzanzibari mkazi vilitengenezwa na Kampuni ya SUPER.COM kutoka nchini Israel.

Chanzo: http://www.freemedia.co.tz/daima/habari.php?id=1509

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s