Lipumba: Mkapa hana kinga

Na Asha Bani, Masasi

Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, amesema Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, hana kinga, hivyo anastahili kushtakiwa kwa mujibu wa katiba ya nchi.

Alisema hayo jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari walioko kwenye msafara wa ziara ya kukagua uhai wa chama chake mjini Masasi.

Profesa Lipumba alisema kutokana na kifungu namba 46(3) cha katiba ya nchi, Mkapa anastahili kushtakiwa kama ushahidi wa kosa litabainika.

Alisema maovu mengi yalifanyika wakati wa utawala wake, hivyo kuna haja ya kuangalia kwa makini na kufanya uchunguzi endapo itagundulika kuna mkomo wake katika kuliingizia taifa hasara kutokana na mikataba mibovu; na ubinafsishaji usiofuata taratibu, anastahili kushtakiwa.

Alisema kifungu hicho cha sheria kinasema kinga ya rais ni pale ambapo amefanya jambo lililofuata taratibu za nchi.

“Kwa mfano, kama sehemu ina fujo, halafu Rais ameamuru jeshi kwenda kutuliza na kuua, hapo rais hatashtakiwa, lakini si kuipa nchi hasara, kuliingiza taifa kwenye umaskini kwa kushiriki kwenye makosa ya ufisadi na rushwa inabidi ashtakiwe!

“Rais hayuko juu ya sheria na kinga yake ni sheria, hivyo naye achunguzwe endapo itabainika kama alihusika kwenye rushwa katika ununuzi wa rada ambao umeliingizia taifa hasara ya sh bilioni 40, basi hana budi kushtakiwa,” alisema.

Profesa Lipumba alisema hakuna haja ya kuumiza kichwa kwani katika utawala wa Mkapa wizi wa fedha kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), ulifanyika kwa kuchota mabilioni ya fedha na kutafunwa na wachache.

Katika hatua nyingine, chama hicho kimesema Mkapa haheshimu haki za binadamu kama ilivyodaiwa na Askofu wa Kanisa la Anglikan, John Ramadhan, katika ujumbe wake wakati wa mkesha wa ibada ya Sikukuu ya Krismasi iliyofanyika katika Kanisa la Mkunazini, mjini Zanzibar.

Taarifa iliyotolewa na Naibu Mkurugenzi wa Haki za Binaadamu na Mawasiliano ya Umma, Salim Bimani jana, ilisema kumbukumbu za utawala wa Rais Mkapa zinaonyesha kulitokea mauaji ya kutisha yaliofanywa na vikosi vya ulinzi na usalama dhidi ya raia wasiokuwa na hatia visiwani Zanzibar.

“Wakati mauaji hayo yanafanyika si tu Rais Mkapa alikuwa ndio Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, bali pia alithubutu kuwapandisha vyeo askari waliohusika na mauaji hayo,” alisema Biman.

Alisema CUF haikubaliani na kauli ya askofu huyo kuwa Mkapa alikuwa kiongozi aliyeheshimu utu wa mtu wa kuishi kwa vile hakupitisha adhabu hata moja ya kifo katika utawala wake licha ya watu kadhaa kupatikana na hatia na kuhukumiwa kifo.
Alisema kwamba wananchi wa Zanzibar kila Januari 26 na 27 wamekuwa wakiadhimisha kumbukumbu ya mauaji ya kutisha yaliofanywa na vikosi vya ulinzi na usalama chini ya amiri Jeshi Mkuu Benjamin Mkapa.

Akitoa mahubiri katika ibada ya mkesha wa sikukuu ya Krismasi katika Kanisa la Anglikana Mjini Zanzibar, Askofu alisema Rais Mstaafu, Mkapa, katika uongozi wake atakumbukwa kwa kuheshimu haki ya mtu ya kuishi kwa vile hakuidhinisha adhabu ya kifo licha ya watu kadhaa kupatikana na hatia wakati wa uongozi wake.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s