Mauaji ya 2001: Uchaguzi wa Oktoba 1995

SURA YA NNE

UCHAGUZI WA KWANZA VYA VYAMA VINGI – OKTOBA, 1995

Uchaguzi huu ulifanyika baada ya miaka mitatu tokea kuja kwa mfumo wa vyama vingi.  Kwa kuwa mazingira yalioulea mfumo wa vyama kwa kipindi hicho yalikuwa machagu, hakuna alietarajia kwamba haki ingetendeka katika chaguzi zilizofuatia.  Hivi ndivyo ilivyokuwa, kwani pamoja na ukandamizaji mkubwa uliofanywa kwa CUF, bado chama hiki kilifanya vizuri sana na kuashiria kwamba kulishinda majimbo yote ya Dar es salaam na kupelekea  Serikali kufuta matokeo yote na kuurejesha upya.  Ama kwa Zanzibar, hakuna bishar CUF iliibuka mshindi katika kiti cha Urais ingawa wizi wa dhahiri ulifanywa ili kukusanyiwa ushindi.  Mgogoro wa kisiasa ulioambatana na mgawiko mkubwa wa kijamii ulianza, na jaribio la kwanza la kutafuta suluhu lilizimwa katika muafaka wakwanza.  Katika sehemu hii tunazingatia zaidi kueleza dosari za uchaguzi huo, ili tuone kwa kiasi gani tulijifunza na kurekebisha hali hiyo kwa uchaguzi mwengine uliofuata miaka mitano baadae.

Sehemu ya 1: Uchaguzi, Kipimo cha Demokrasia

Wataalamu wengi wa masuala ya siasa wamekubaliana kwamba katika uchaguzi ndipo penye kipimo cha demokkrasia.  Kwa mfano, Pateman (1985) anasema, ushiriki katika mchakato wa kisiasa unachangia katika kasi ya maendeleo na ubora wa demokrasia.  Joseph  Schhumper (1976) anaeleza, kwa ufupi demokrasia ni utaratibu wa kisiasa unaotoa njia ya kuchagua kiongozi wa kisiasa.  Na kwa maneno yake (1976:260), njia ya kidemokrasia ni mpangilio wa kitaasisi wa kufikia katika maamuzi ya kisiasa, ambayo kwayo, watu wanapata uwezo wa kuamua kupitia vuguvugu la ushindani wa voti (kura) za watu.  Na kwa maneno yetu uwezo wa watu wa kufanya maamuzi wapendavyo hauwezi kupatikana bila ya Serikali kutoa fursa isiyo na masharti ya kimatakwa.  Musambichame (1998) akikubaliana na baadhi ya maoni ya hapo juu anaamini kwamba sifa muhimu za kuwepo kwa deemokrasia hujengwa iwapo Serikali inatoa fursa pamoja na kukubaliana na matakwa na maamuzi ya watu.

Ama kwa kuungana na maelezo yaliotangulia Dahl (1971:3) anataja fursa hizo zitokane miongoni mwa:

?          Uhuru wa kuunda na kufanya jumuiya

?          Uhuru wa kujieleza;

?          Haki ya kuchagua;

?          Kufaa katika Ofisi za Serikali;

?          Haki za Viongozi wa kisiasa kushindana kwa kutafuta kukubalika na kura ;

?          Ruhusa ya kukaribia, kutumia na kusema na katika vyombo vya habari;

?          Kufanya uchaguzi huru na haki;

?          Kukubalika kwa chaguo la watu

?          Na kwa maneno tena ya Dahl (1971:4), fursa hiyo hutegemea masharti ya msingi yafuatayo:

?          Kuwepo kwa ushindani wa hali ya juu kabisa lakini ulio huru na wa haki miongoni mwa watu na makundi yaliyojiunda (hasa vyama vya siasa) kwa nafasi zote za madaraka ya kisiasa kwa kipindi maalum;

?          Pawepo na ushiriki wa hali ya juu wa kisiasa katika kuchagua viongozi na sera kupitia chaguzi za haki kwa kipindi maalum;

?          Pawepo na kiwango cha kuridhisha cha haki za kiraia na kisiasa, kama uhuru wa kujieleza, kuzungumza na vyombo vya habari, kufanya na kujiunga na jumuiya; pamoja na hayo kuhakikisha sifa za ushindani wa kisiasa na ushiriki wa watu na vyama vya kisiasa.

?          Kuondoa au kutokuwepo matumizi ya nguvu ama kwa majeshi ya vita, polisi au mtu yeyote mwenye silaha au jumuiya ya chama cha siasa.  Mwisho wa kunukuu.

Kabla ya kueleza hali ya chaguzi za 1995 na 2000, tulidhani tutangulize nadharia hizi kwa sababu mbili.  Kwanza kupata kigezo cha maana katika maelezo yetu.  Pili, kuwapa wasomaji nafasi ya kupima uhalisi wa baadhi ya mambo yalivyokuwa hasa kwa vile hatutanafasika kueleza kila kitu kilichotokea katika chaguzi hizo.

Sehemu ya 2: Hali kabla ya kupiga kura

Hiki ni kipindi cha uandikishaji, kuelekea kampeni na kampeni zenyewe.  Katika kuanza na hatua za uandikishaji hapa ndipo palipoanza vituko.  Watu wengi wenye haki ya kupiga kura hawakupewa haki hiyo na wale wasiostahiki ndio waliopewa fursa ili kupunguza idadi ya kura za mgombea wa upinzani na kumuongezea ashikae hatamu ili aendelee.  Sheria ya ukaazi ilikuwa kwamba kwa Zanzibar, mtu yamlazimu kukaa pahala miaka mitano mfululizo ili awe na haki ya kupiga kura.  Sheria hii ilitumiwa vibaya na Masheha na kila mtu akienda kujiandikisha ilibidi Sheha awe na maamuzi ya mwisho.  Akisema tu huyu si mjui ndio haki inapotea.  Hata mtu akisema basi nipe haki ya kumchagua Rais tu ambapo sheria inakubali [Kifu. 12 – 6 (c) (ii) basi pia alikataliwa.

La kushangaza ni kwamba sheria hii ilikuwa inawapa haki wanajeshi, wafanyakazi wa serikali na jumuiya ya kimataifa pamoja na baadhi ya wanafunzi katika vyuo vyengine.  Hata hivyo, kwa makundi mengine hakukuwa na shida kwani iliaminika yalikuwa na utiifu kwa CCM na Serikali yake.  Vikwazo vingi viliwekewa kwa baadhi ya wanafunzi hasa walioko masomoni Unguja kutoka Pemba.  Wanafunzi wa aina hii walinyimwa haki ya kupiga kura na pale walipojaribu tu kuulizia haki yao walifukuzwa.  Tunaishukuru CUF ilibeba mzigo mzito kuwasaidia waathirika wasome.  Wako miongoni mwao waliofuzu vizuri zaidi kwani walipelekwa Tanzania Bara katika shule ambazo viwango vya elimu ni vikubwa kulinganisha na skuli walizotoka.

Katika hali ya kuhakikisha kwamba CCM inawanyima watu haki zao, tulishuhudia watu wenye umri wa zaidi ya miaka 18 wakipingwa na Masheha, lakini wenye umei mdogo, (maadam tu wanaunga mkono CCM) wao waliruhusiwa.  Tumeshuhudia vijana wa familia moja, yule mkubwa kwa umei akikoseshwa haki na yule mdogo akipewa.  Waandishi wengi wa wapiga kura na Wasimamizi ni watumishi wa Serikali lakini wale tu wanaoweza “siri kali“.  Wengi wa wale ambao hawana uwezo wa kuandika ndio waliopewa kazi za ukarani wa kuandikisha wapiga kura mule mwahala mwenye wafuasi wengi wa CUF.  Baada ya kasoro zote hizo, mwishowe tulipokea ripoti kutoka Tume yetu ya Uchaguzi ya ndani ya Chama kwamba, takriban wastani wa vijana 550 (kwa kila jimbo) katika majimbo 21 ya Pemba walikosa haki ya kuandikishwa kama wapiga kura.  Katika majimbo ya Mkoa wa Mjini/Magharibi, takriban vijana 350 (kwa kila jimbo) katika majimbo 18 walikosa haki ya kujiandikisha.  Hii haina maana kwamba sehemu nyengine zilikuwa shwani, lakini humu ndimo mlimokithiri kwa sababu muna wafuasi wengi wa CUF.

Katika kipindi cha kampeni haki hapakuwa na usawa hasa katika matumizi ya vyombo vya habari.  Kila chama kilipewa muda mdogo, lakini CCM iliyohodhi vyombo hivyo ilivitumia itakavyo kuwatangaza wagombea wake na sera zake.  Tunamshukuru Mwalimu aliposema kwamba “watu hawatapigia vyama kura kwa rangi za viongozi wao, lakini watapiga kwa uzuri wa sera zao“.  Huu ndio ukweli uliotiwa dosari kwa maksudi ili sera za vyama vingine zisipate nafasi ya kusikika.  Siyo kuvinyima uhuru vyama  vya upinzani tu, bali wakati mwingi vyombo hivyo vya habari vilitimika kukashfu, kuponda na kugeuza ile taswira na maana halisi ya sera za vyama vya upinzani.

Polisi waliweza kuzuia mikutano ya hadhara mwahala mwingi na kuna baadhi ya sehemu walisema hasa kwamba huko hakuruhusiwi kwa mpinzani kufanya siasa.  Huu ndio wakati ambao rungu za dola zilinolewa na zikifanya kazi kuliko wakati mwengine wowote.  Wapinzani wengi walipigwa kwa marungu iwapo walisema linaloudhi watawala.  Tuna kumbukumbu na tunawajua watu waliopewa silaha kutishia maisha ya watu.  Siku moja tulikuwa katika kampeni Pemba.  Siki hiyo, kikundi cha vijana wa CCM walipita katika kijiji cha Kuyuni wakielekea Wambaa.  Mmoja wao, ambae alitambuliwa wazi kuwa ni askari wa usalama alichomoa bastola na kuwatishia watu waliokuwa katika mkutano wa hadhara ila watishike na watawanyike.  Katika sehemu moja ya Mkoani watu hao walishikwa siku moja, lakini walipopelekwa Polisi waliachiwa na siku ya pili waliokamata ndio waliowekwa ndani kwa wiki mbili na kufunguliwa kesi.

Kama tulivyosema kwamba katika kipindi hiki kwa kawaida vyombo vya dola navyo hugeuzwa matawi ya CCM.  Polisi walikamata watu wengi na kuwekwa ndani na wakesha maliza kazi yao ya kupeleka Mahakamani, huko na kulikuwa na mtindo wa wiki mbili unawekwa ndani ili eti usiharibu ushahidi.  Watu wengi wakati wa kupiga kura walikuwa ndani.  Walinyimwa haki kwa kutumia mahkama ambayo tunaambiwa ndio uwanja wa haki.  Ili kuyafanya mambo yende kama yalivyopangwa mahakimu wenye asili ya Kipemba au mzaliwa wa Unguja anaetiliwa mashaka walitimuliwa ama kwa kuhamishiwa katika Idara za Serikali au kuwadhalilisha kisaikolojia ili waache kazi.  Nafasi zao kwa bahati njema walipewa ndugu zetu wa Tanzania Bara.

Ama kwa Bara mambo ya kule yalikuwa ya kikalamu zaidi kuliko ya kifimbo ya huku Zanzibar.  Maana tunakumbuka, hadi ilipofika bado siku chache za tareje ya mwisho ya kuandikisha watu wengi walikuwa hawajaandikisha kwa sababu kwamba hawaoni haja ya kuchukua tabu kujiandikisha na kupiga kura ambayo haibadilishi maisha ya wapiga kura.  Maoni kama yalimaanisha kuwa wengi wakisema wamechoshwa na CCM, ingawa walikuwa hawajui taathira ya kuiwacha CCM iendelee kwa kutoandikisha na kukipigia chama cha upinzani.  Lakini ilipokuja siku ya kutoa takwimu za waliojiandikisha ikaonekana watu wamezidi sana makisio ya awali.

Sehemu ya 3: siku ya Voti

Ilikuwa ni tarehe 26 Oktoba, 1995 wakati watu wamekwishajipanga kwenye mistari mirefu, kuanzia saa nane za usiku kusubiri kuwa wapige.  Matatizo yalikuwa ni dhahiri, kwa kuwa matatizo ni mkakati wa CCM na Serikali yake ili wapate mwanya wa kufanya watakavyo.  Mtu atashangaa kwamba watu waliowakipiga kura Malindi au tuseme Mkunazini hadi saa nne za asubuhi (siku ya kura) walikuwa hawana karatasi za kura za kutosha eti kutokana na matatizo ya usafiri.  Vituo hivi vipo mita chache kutoka sehemu zilipohifadhiwa vifaa.  Kwa Pemba ambako kuna masafa marefu na bara bara mbovu kupita kiai, hili lilikuwa mashuhuri.

Wakati huo, ule mkakati wa kibabe wa kuchukuwa vijana kutoka Bara na kupeleka Pemba ulikuwa haujaanza kwa sababu CCM haikufikiria kwamba ingepata kipigo cha mbwa dume Pemba.  Hali hii ilitokana na ushauri wa wanamikakati wao na wadadisi (wakereketwa) wa siasa ambao bila shaka waliwaambia kuwa ufahamu mdogo wa siasa za upinzani ungeanzia Pemba.  Pengine pia, ndio walitegemea historia ni mambo kujirudia.  Kwa majimbo kama ya Mkoani, Mkanyageni, Wawi na Vitongoji walishakuwa na yakini kwamba ni yao toka nitoke kwa vile eti kulikuwa na Afro wengi miaka ya nyuma.  Hawakujuwa kwamba kulikuwa na Afro wengi kwa kuwa walikuwa wakishiba.  Kama ni nchi walishagomboa na bado hawatimizi mkate, leo wakae wafanye nini !  Ndio kama tulivyokwishaona kuwa hata mwanafalsafa mashuhuri, Maliyamkono alikwishawaeleza kwamba eti sehemu hizo ni za kwao CCM kwa eti kuna Waafrika wengi wa asili ya Bara.  Hii ndio maana ya wagawe uwatawale dhana iliyokwishapitwa na wakati siku nyingi sana.

Siku ya uchaguzi, tuligundua kwamba kura haikuwa siri baadae kwani karatasi za kura zilikuwa na vishina ambavyo ukipewa kura na jina lako linarekodiwa.  Ilifanywa hivi maksudi ili baadae ajulikane nani kapiga kura wapi, hasa miongoni mwa wafanyakazi wa Serikali, ili  iwe rahisi kuwafuatilia na kuwafukuza waliopigia upinzani.  Naam, hivi ndivyo ilivyokuwa baadae kwani watu wengi walifukuzwa kazi kwa misingi hiyo.  Kama tulivyosema makarani wa siku ya kupiga kura walifundishwa kupoteza muda kwa zile sehemu zenye CUF wengi ili ifike saa kumi na mbili wakate tamaa au kiza kiingie na kulifanya zoezi liwe gumu.  CUF tuliyajuwa yote hayo ndio maana tukajitahidi kupata taa za akiba ingawa uwezo wetu mdogo wa kifedha haukuweza kufanikisha hili kwa sehemu kubwa ya nchi.

Kwa mikakati kama hiii ilitokea mwahala mwingi watu hawakupiga kura.  Sababu nyengine ni kwamba mtu aliweza kukaa kwenye mstari na akifika kwenye kisanduku anaambiwa jina lako halimo.  Kupotea kwa majina kulijitokeza hata katika kipindi cha pingamizi.  Tulikagua majina yaliyoandikishwa na tukaona mengi hayamo.  Wapi utapeleulikagua majina yaliyoandikishwa na tukaona mengi hayamo.  Wapi utapeleka malalamiko yako ndio kazi; kwani mambo yote yalikwisha pangwa yawe “danadana“.  Ndani ya vituo vya kupiga kura askari wenye silaha walikuwa mara nyengine wanawaonesha watu midomo ya bunduki ili kuwatia hofu.  Sehemu za makambi ya Jeshi la Ulinzi na Polisi huko ndio CCM wakifanya watakavyo kwani mawakala wa upinzani hawakuruhusiwa hata kuchungulia.  Demokrasia kule imo ndani ya mdomo wa bunduki sehemu hizi ndizo zilizotumiwa na walinzi wa nchi kuongeza ushindi wa chama tawala kwa kuwaingiza watu makambini kutokna kokote kwa kadiri walivyopenda.  Kwa hivyo, iliwezekana katika majimbo yalio na kambi kuiba kiasi chochote cha kura na hakuna lolote ungefanya.  Baadhi ya majimbo yaliothirika sana ni Jang’ombe, Mfenesini, Mwera, Dimani, Vitongoji n.k.

Baada ya kupiga kura, matatizo yaliendelea katika kuhesabu na kutangaza matokeo ya kura.  Tuliweza kugundua kwamba kila kituo cha kura kulikuwa na kura mifukoni mwa watu wao waliowapanga ili kutafuta mwanya wa kuzipenyeza kuongeza kura za CCM hasa kwa yale majimbo mazito kwao.  Kwa mfano, Jimbo la Mlandege Unguja lilikwisha nyakuliwa kwa madaha na CUF.  Walichofanya CCM ni kuhakikisha linarudiwa kuhesabiwa mara mbili na kugundua ni la CUF, mawakala wa CCM walikataa kutia saini.  Waliomba kura zilale na hesabu ifanyike siku ya pili kwa kisingizio cha usiku na pia ndio tayari kulikuwa na pingamizi.  Kwa kuwa Mgombea wetu alihisi ‚alikwishapeta’ aliona bora akajipumzishe.  Mawakala wetu walibaki ngangari lakini hawakuweza kuwa na udhibiti nzuri wa kura.  CCM walijipenyeza na wakazichezea kura nyingi za CUF zikiwa zimeharibiwa maksudi.  Nyengine zimeandikwa matusi na  baadhi zimeandikwa “I love you dear”.  Kabla ya hapo kura za aina hiyo hazikuwepo kwenye visanduku.  Jimbo lilichukuliwa kwa mipango hiyo.

Tatizo jengine lilihusu utangazaji wa matokeo.  Chombo pekee cha habari kkilichopewa uwezo wa kutoa matokeo ni Sauti Tanzania Zanzibar (STZ) kwa Zanzibar.  Kazi ya kumtangaza mshindi ni ya Tume ya Uchaguzi ambayo yote ilikuwa ya CCM.  Kilichofanywa ni kwamba Tume ilikuwa ikitoa matokeo ya Mbunge na Mwakilishi wa Jimbo, bila kusema Mgombea wa Urais kwa kila jimbo kapata kura ngapi.  Jambo kama hili linashida gani hata lionekane ni kikwazo kufanyika!  Hili likidanyika basi hupunguza wasiwasi (tension) nchi nzima na hata ile hali ya kutoaminiana ambayo hujengeka tokea mwanzo wa kura basi hushuka polepole.

Hili pia huongeza uwazi kwenye kuta ya Urais ambayo ndio yenye “mbinde”.  Hata kama hapana mizengwe iliyopangwa na Tume lakini pia hapana mantiki kwa nini kura za Rais zisitajwe ili kuipunguzia Tume lawama.  Bila shaka Tume ilikuwa inafanya hayo kwa sababu ilikuwa ni sehemu ya mkakati na kwa kweli, kila Taasisi ilikwishapangiwa jukumu lake.  Tumeshuhudia kwa mfano katika uchaguzi wan chi jirani, Kenya ambapo wakitaja kura zote kwa wakati mmoja, hili lilisaidia sana kupunguza joto la uchaguzi nchini humo na hivyo kuondokana kabisa  na mizozo baada ya uchaguzi wao wa tatu wa vyama vingi mwaka 2002.

Tukirudi nyuma kidogo, tulishuhudia pia kampeni za uchaguzi zilizohutubiwa na mgombea wa CCM wa Urais wa Muungano, Benjamin Mkapa ambae aliwaambia Watanzania kwamba iwapo chama kilicholeta uhuru hakikupigiwa kura na kurejea madarakani, basi kuna hatari kwamba wapinzani watawarudisha wakoloni.  Sisi tunawasubiri wakoloni warejee Kenye kwanza kwani sasa upinzani umeingia madarakani baada ya vipindi viwili vya madhila ya demokrasia kama ilivyo Tanzania hadi leo.  Kwa ufupi, matokeo ya uchaguzi yalibadilishwa na mtu aliechezea maisha ya watu na akapewa madaraka ya kuwa Katibu Mkuu wa Wizara nyeti.  Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi iliyovurunda nae akapata chake na anaendelea kutanua.  Hivyo ndivyo demokrasia inavyokuzwa Tanzania ambapo kila siku, pamoja na kasoro zote hizi, Jumuiya ya Kimataifa inasema imeridhika na hatua Tanzania inazochukuwa kuendeleza demokrasia.

Kwa Tanzania Bara, matokeo ya wizi wa kura yalikuwa ni ya wazi wazi, kwani inajulikana kabisa kwamba kwa vile masafa ambayo kura zinasafirishwa na kwa kuwa vyama vya upinzani havina uwezo wa kusindikiza masanduku ya kura, basi njia inayotumiwa na Tume ya Uchaguzi ya Taifa ni kuweka utaratibu ambao mawakala wa vyama wasiingie kwenye magari ya kura.  Kwa kuwa Tume ilikuwa dhahiri inaisaidia CCM, basi ndani ya safari ya kura ndio kulikokuwa na kazi ya kuchezea kura na kuiba kwa manufaa ya chama tawala.  Hivyo walifanikiwa sehemyu nyingi na wataendelea kuanikiwa kila uchaguzi iwapo ambamo wapinzani hasa CUF ilipata viti vya ubunge baada ya kuhesabiwa kura, lakini wasimamizi wa uchaguzi kwa kiburi kabisa wakakataa.  Kondoa ni sehemu moja wapo.  Katika Jimbo la Kagera Mjini tulimpita Mbunge wa CCM sana lakini likafanyiwa njama na CCM kuchukuliwa kirahisi.  Jimbo hilo ingawa lilibakia kwa CCM kwa miaka mitano ya kwanza lakini mwaka 2000 wananchi wa Kagera Mjini wakashinda ile mbinu ya CCM.  Dar es Salaamu ndipo palipokuwa na vituko.  Majimbo ya pale yote yalichukuliwa na upinzani na ikaonekana ni abu Ikulu kuwa ndani ya upinzani.  Walichofanya ni kufuta matokeo ya Mkoa mzima na kuurejesha uchaguzi mdogo na “wakafanya vitu vyao”.  Huu ndio mkakati wa CCM waliourejea kwa majimbo ya Mjini Unguja mwaka 2000 baada ya majimbo yote kuchukuliwa na CUF.  Tuliyotaja ni baadhi tu ya matukio ya vituko vya siku ya kura.  Jee baada ya matokeo mambo yalikuwa vipi?  Haya ndio maelezo yatakayofuata sehemu ijayo.

Sehemu ya 4: Matokeo Baada ya Uchaguzi

Matokeo ya uchaguzi wa 1995 yalitolewa tarehe 26 Oktoba, 1995.  hii ilikuwa ni siku ya nne baada ya uchaguzi.  Nchi ndogo kama Zanzibar, hili latia mashaka.  Ikilinganishwa na Kenya ambayo ni nchi kubwa mata karibu 300 ya Zanzibar, ilitoa matokeo baada ya siku 3.  Kwa Zanzibar matokeo ya Madiwani hayakuulizwa kabisa.  Kenya walikuwa wanayotoa angalau kwa kusema idadi ya viti vilivyochukuliwa na chama.  Hii ni kawaida kwa Zanzibar kuwadharau Councillors na hata baada ya uchaguzi bado hawajathaminiwa katika majukumu yao.  Kwa ufupi basi, CUF ilikataa matokeo ya uchaguzi wa rais baada ya kutangazwa kwa misingi ifuatayo:

?          Kuchelewa kutangazwa matokeo ya rais kwa siku nne,na matokeo yalitakiwa yatangazwa pamoja na yale ya Wabunge, Wawakilishi na Madiwani.

?          Uhakiki (Verification) wa kura ulifanywa na Tume ya Uchaguzi pekee bila ya kuwaruhusu Waangalizi wa ndani na nje paoja na mawakala;

?          Fomu za kujaza matokeo hazikuwepo kwa baadhi ya vituo;

?          Waangalizi wengine hawakuruhusiwa na Tume kuona takwimu za matokeo;

?          CUF haikupewa takwimu za matokeo ilipoziomba kutoka Tume;

?          Baadhi ya vituo vilikuwa na tafauti za wazi kama vile Kwahani ambapo wapiga kura walioandikishwa ni 6,035 lakini kura zilizopigwa ni 6,838;

?          Kwa Jimbo la Mlandege, matokeo ya kwanza ya Tume yalikuwa 3,248 (CCM) na 2,319(CUF).  ZIlipohesabiwa mara ya pili kwa maombi ya CUF zilikuwa 2,775 (CCM) na 2,792(CUF);

?          Takwimu za Tume zilitafautiana na ZEMONG (Wasimamizi wa ndani);

?          CUF na baadhi ya waangalizi walionya kwamba kura zitabadilishwa lakini hakuna chombo kilichotilia maanani;

Baada ya matokeo kuchelewa kote nchini Tume ya Uchaguzi ilimpa Mgombea wa CCM Dr. Salmini kura 165,271 (50.2%) na Mgombea wa CUF Maalim Seif kura 163.706)49.8%).  Haya yalikuwa ni mapishi ya tume na CUF haikukubaliana sio tu na matokeo lakini zaidi na kuchezewa demokrasia.  Msimamo wa CUF wa kutotambua matokeo ulikuja baada ya kuapishwa Dr. Salmini.  Baada ya hapo sherehe zilipangwa za kumuapisha Dr. Salmin na hazikuwa za furaha kuanzia awali.  Hata uwanja wa Amani ulionekana uko mbali.  Sherehe zilikuwa Kizingo.  Jambo moja la ajabu ni kwamba wakati huu wote CUF ilikuwa haijatoa msimamo wake juu ya uchaguzi lakini hata Wawakilishi wa CUF hawakualikwa kwenye sherehe za kumuapisha huyu tulieambiwa ndie angekuwa mwenzetu kwenye Baraza.  Kwa hivyo, kwa kweli ilikuwa ni CCM ilioanza kuwagomea CUF na haukuwa CUF iliyoanza na mgomo.  Ah! Ndio historia kujirudia; “CCM kwenda pekee”.

Kilichofuata baada ya hapo ni agizo la chama cha CUF kuwataka Wawakilishi wake wasichangie miswada na mazungumzo yote ya Baraza la Wawakilishi kama njia ya kuonesha kuchukizwa na kuvurugwa kwa demokrasia.  Hata hivyo, Wawakilishi walitakiwa wabakie katika Baraza ili wasipoteze Uwakilishi wao kwani ulalamikiaji matokeo ulielekezwa kwa matokeo ya Urais.  Kazi hii ilifanywa vizuri na wajumbe wetu lakini baadae Spika wa Baraza Pandu Ameir Kificho aliamua kuwafukuza ili CCM ibakie pekee itunge Sheria kadiri wapendavyo. Wako miongoni mwa Watanzania waliojaribu kukebehi msimamo huu wa CUF na kusema kwamba usingetusaidia chochote katika madai yetu.

Hawa walikuwa ni baadhi ya wadadisi wa siasa na CCM wenyewe.  Lakini tukasema ndio maana ya muhanga, siku zote ajitoae huondoka lakini hali hubadilika kwa wengine.  Kama si muhanfa kusingekuwa na maendeleo, na muhanfa si kujiuwa tu kwani hata kusamehe maposho ni muhanga.  Nyerere na Abdul Wakil waliingia kwenye siasa kwa kuacha mishahara bila ya kujua kuwa wangefaulu au la.  Na sisi ndivyo ttulivyofanya.  Lililopatikana kwa msimamo huu  na lililokosekana wananchi ni wajuzi zaidi, lakini msimamo wetu ulijulikana dunia nzima na kila mara ulikuwa hai (live).

Hawakuwa wawakilishi tu waliosikitika kwa kuvurugwa demokrasia lakini na makundi mengine hasa wanafunzi.  Hawa nao waligoma kwa kuwa wenzao wengi walinyimwa haki na kufukuzwa.  Mgomo ulikuwa mkubwa na baadae Serikali ikawafukuza vijana wengi zaidi ya 1500 ambao walikuwa wafanye mitihani yao ya kidato cha nne.  CUF iliwasaidia kufanya mitihani hiyo Bara kwani Zanzibar waliwazuia kabisa hata kucukuwa fomu za “Private candidate”.  Tulikuwa tunamsubiri Mmuya atasema nini kuhusu vijana kunyimwa elimu.  Kimyaa, Profes wa siasa.

Mambo ya manyanyaso yakaanza sasa.  Wafuasi wa CUF wa Unguja na Pemba kufukuzwa makazini.  Wapemba kufukuzwa Unguja.  Na hata Bara Makamo Mwenyekiti wa CCM Jonh Samwel Malecella alitoa hutuba Tanga (Mkoa ambao idadi ya Wapemba ni kubwa) na kusema “hapa Wapemba si pao, hawana haja ya kujiingiza kwenye siasa, kazi yao kubwa ni kuuza mchele”.  Darajani palikuwa peupe, kwani ukionekana CUF unanyimwa leseni za kufanyia biashara.  Wafanyakazi nao walifukuzwa wengi na kila Mpemba au mtu mwengine ambae taarifa zilipelekwa kuwa anatiliwa mashaka basi akirudi masomoni hata kama hakupiga kura hapangiwi kazi hata kama ana digirii tatu.  Katika Mji mkongwe waliodhaniwa CUF na Wapemba walifukuzwa wengi na leo unaona nani anakaa huko.  Ndugu zetu wa “Jua Kali’, wengi wao wakiwa CUF, walikuwa wakinyang’anywa vitu vyao, akina mama ntile walikuwa wakimwagiwa vyakula vyao na mara nyengine mtu akiweza kuambiwa kula hadi uvimalize pale chini mithili ya mbwa na nguruwe.

Huku bado mambo, sherehe za ushindi zilichukuwa zaidi ya miaka mitatu, majumba mwengi ya wana CUF yalichomwa moto ili wahame waende kwao.  Ikaja amri ya kuwavunjia majumba sehemu ote ya Mtoni karribu na anapoishi Maalim Seif.  Yeye aliambiwa ahame nyumba akaayo ende kwao Mtambwe.  Simu akakatiwa.  Akiwindwa kama ngedere, kila mahala kuna askari wa JKU na Polisi wakipiga watu virungu.  Mahkama zilijaa, watu hawana furaha ya roho.  Haya yote yakitokea hakuna msomi wa siasa aliependekeza kwamba jamani sasa yatosha, wamekoma hao! “Waso haya wana mji wao” ndizo nyimbo za wakati huo STZ.

Watu walipoteza mali, viuongo vya mwili na uhasam baina ya Mpemba na Muunguja ndio uliokuwa ukitafutwa lakini hasa ulipatikana baina ya CUF na CCM.  Kule Pemba ulionekana dhahiri kuwa CUF ndio wengi zaidi.  Haya yalifanywa na CCM na Serikali zake lakini ukipekuwa vitabu vya Mmuya anasema yalitokea kwa sababu wananchi walikuwa na elimu ndogo na hawakuelea mfumo wa vyama vingi.

Sehemu ya 5: Jitihada za Ufumbuzi wa mgogoro

Wakati haya yakitendeka hatukuwa na muombezi ndani ya nchi.  Vyombo vyote vya dola vilikumbizwa kutushughulikia CUF.  Hapo ndio viongozi wetu walianza kutafuta tafuta watu mashuhuri na jumuiya za kimataifa zinazohusika na masuala ya haki za binaadamu na demokrasia.  Kejeli zikaanza kwamba Maalim Seif anakwenda akionana na Jemshid.  Eti Maalim anakwenda Ulaya kuzuia misaada ya Zanzibar.  Haya ni maneno baada ya Uchum wa Zanzibar kushuka sana.  Tunakumbuka katika mwaka 1998 uchumi ulikuwa kwa asilimia zero nukta nane.

Ndivyo wengine walivyosema ni heri tule udongo, lakini wengine wakajiuliza; itakuaje mwenye dola ashindwe kuwashawishi wahisani afaulu mwenye ndevu tupu.  Ukweli ulikuwa ukifichwa, kwani wananchi hawakuambiwa kweli kwamba, taasisi za fedha na maendeleo ya kiuchumi za dunia zimeweka masharti kwamba nchi yoyote isiyoheshimu haki za binaadmu haiwezi kupata misaada ya kimaendeleo.  Hili ndilo lililoathiri siku ya mwanzo mara tu baada ya demokrasia kuathirika  na kufuatiwa na uuvunjaji wa haki za binaadamu kwa kiwango cha hali ya juu.  Shukrani za pekee ziende kwa Taasisi za ulimwengu za haki za binaadamu kama vile Human Right Watch na Amnesty International.  Vyomvo hivi vilithibitisha kila tukio la kuvunjwa kwa haki za binaadamu.

Juhudi za kutafuta ufumbuzi wa mgogoro wa kisiasa hazikufanyika nje tu, lakini zilianzia ndani ya nchi kwa kila kiongozi kujishughulisha na mazungumzo ya mtu mmoja mmoja na wenzetu wa CCM.  Mara nyingine Chama chetu kilitangaza kwenye mikutano michache tulioruhusiwa, nia yetu ya kutaka mazungumzo ili kufafuta ufumbuzi wa kudumu wa matatizo ya chaguzi.  Tunakumbuka ujumbe ulioongozwa na Katibu Mkuu wa wakati ule Mheshimiwa Shaaban Khamis Mloo uliwahi kumfuata Mwalim Nyerere Butiama ili asaidie.  Hata hivyo, juhudi hizi ziligonga mwamba ingawa hatukutarajia sana nyani kumhukumu tumbili lakini ilitulazimu kwa kuwa Mwalim ndie aliepachikwa cheo kwa Baba wa Taifa.

Huku mambo ya mapatano yakizorota, haki za binaadamu ziliendelea kuvunjwa siku hasi siku.  Hata pale palipoonekana  hakuna matata basi mpango ulifanywa ili kupata kisingizio cha kuwagombanisha watu au cha kuwakamata watu na kuwaweka kizuizini ili kuwafungulia mashitaka.  Kwa mfano, katika majimbo ya CUF mpango ulifanywa ili kutoa maji vinyesi na baadae kuita vyombo vya habari na kutangaza kuwa vile vilikuwa vitendo vya CUF.  Hii ilitokea sehemu nyingi za Kaskzini Pemba na Bumbwini kwa Unguja.  Na itakuwaje CUF ambao wanatumia visiwa hivyo hivyo wawe ndio wahusika katika utiaji wa vinyesi! Pia iwaje vinyesi vitiwe katika majimbo yaliyokuwa chini ya CUF tu?

Sio tu wenzetu kukubali kutaka kuzungumza, lakini walikuwa wakisema hakuna mgogoro kabisa.  Hatukujuwa kwamba maana ya mgogoro kwa CCM ni kumwaga damu.  Ndugu zetu wa barani Afrika nao hawakuwa wa msaada wowote na kilichoendelea.  Walikuja viongozi watatu katika kipindi hicho akiwemo Rais Muluzi wa Malawi, Chiluba wa Zambia na Mbeki wakati huo Makamo wa Rais wa Afrika Kusini.  Kila wakija wanafikia Ikulu halafu wakitembezwa kwenye fukwe na hatimae hayaumani“.  Ndio umoja wa kiafrika ulivyo, si kwa ajili ya Waafrika bali ni kwa ajili ya viongozi wa Afrika.  Tulisikitika sana na wenzetu, hasa Afrika Kusini, Nchi ambayo tafsiri ya neno mateso, unyanyasaji na ubaguzi vimo ndani ya vichwa na nyoyo zao.  Baada ya muda mkubwa sana kupita; yaani kuanzia mwaka 1995 hadi 1999 ikiwa bado mwaka mmoja tu kabla ya uchaguzi wa pili wa vyama vingi, tena tulipata kitu kilichoitwa muafaka.  Huu tunauita muafaka wa kwanza lakini hasa ni muafaka uliovia.  Ulivia kwa kuwa ulikubaliwa shingo begani na wenzetu na kwa hivyo hawakuwa na nia thabiti ya kisiasa ya kuutekeleza.

Sehemu ya 5: Muafaka Viza, wa 9 Septemba, 1999

Muafaka uliokuwa utekelezwe baina ya CUF na CCM na ambao ulipigwa vita kwa ushawishi wa Serikali ya Muungano ulikusudiwa kuleta suluhu ya mgogoro wa kisiasa uliosababishwa na matokeo haramu ya uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi.  Uendeshaji mbovu wa uchaguzi, unyanyasaji na utesaji wa raia waliotaka kutumia haki yao ya kuchagua ulimalizika kwa chama cha CUF kuporwa ushindi wa Urais.  Baadae furaha ya ushindi usio wa haki iligeuka mtafaruku, purukushani na kuanzisha mgogoro wa kisiasa Zanzibar na hata baadae kubadilisha hali ya Tanzania kisiasa na kiuchumi.  Watu maarufu wa mataifa ya nje na kupitia mabalozi  wao walishangaa kuwa Tanzania iko mstari wa mbele kusuluhisha migogoro ya nchi nyingine ilhali yenyewe ina mgogoro Zanzibar na wanaunyamazia kimya.

Kwa upande wetu muafaka huu ulitutaka sisi CUF tuutambue ushindi wa Dr. Salmini na hapo hapo Wawakilishi wetu warudi katika Baraza.  BUF ilitekeleza hatua kwa hatua kila kipengele kilichotuhusu.  Serikali chini ya CCM ilitakiwa kuunda Tume mpya ya Uchaguzi kulingana na mfumo unaokubalika katika Tume za nchi za Jumuiya za Madola na vile vile kurekebisha Katiba na Sheria za Uchaguzi.  Haya yote yalikusudiwa kuondosha machafuko katika uchaguzi wa pili kwa kujenga mazingira bora ya chaguzi.  Ingawa CCM ilikubali kila kipengele na baadae muafaka kutiwa saini lakini katika utekelezaji ilikataa kila kipengele.  Kutokana na hali hiyo, Muafaka sio ulififia tu, lakini ulivia kabisa.  Yaliyokuwemo katika Muafaka huo hatuyataji hapa kwani ndio miongoni mwa ambo ya msingi ya Muafaka wa Pili wa tarehe 10 Oktoba, 2001 uliokuja baada ya mgogoro kuzaa damu iliyomwagwa tarehe26/27 Januari, 2001.

Tukirudi nyuma kidogo, tutaona kuwa baada ya mgogoro kudumu kwa miaka mitatu na nusu (yaani kuanzia 1995 adi Septemba 1999), hatimae Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola Chief Emeka Anyauku alikuja Zanzibar nae kujaribu kusuluhisha.  Wenzetu wa CCM mara hii walisema sasa tuko tayari“ tuzungumzie matatizo yetu.  Baada ya kukubali huko kwa wenzetu (japo shingo begani), Anyauku alimteuwa msaidizi wake Moses Anaf kufuatilia na kutengeneza waraka wa makubaliano.  Waraka huu ulikamilika na kila chama kutakiwa kupendekeza majina ya watu saba ambao wangeunda kamati ya usimamizi yaani Inter Party Committee.

Kwa mara ya mwanzo CUF na CCM walikutanishwa katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi tarehe 9 Juni, 1999 ili kutiliana saini makubaliano hayo.  Katika mambo ya utekelezaji CUF ilitakiwa kuwaruhusu Wawakilishi wake Barazani mara tu baada ya kutiwa saini. Wiki ya pili tu agizo hili lilikubaliwa ndani ya CUF na wakaenda ili kuhudhuria kikao cha kwanza.  La ajabu ni kwamba CCM hawakuwapokea ila kwa masharti kwamba waandike barua waombe radhi ili ionekane kwamba CUF walifanya makosa na CCM siku zote wako juu ya kweli na sheria na hawashindwi na kitu.

Wawakilishi wa CUF hili walilikataa, lakini kwa busara za viongozi wetu walinasihiwa na kuandika barua.  Huu ni ubishi wa kitoto ambao hatungefikiria kufanywa na Spika ambae ni mtu anaefahamu sheria, hakimu na Al haj.  Ilionekana kwamba mtu kama yeye asingekubali baada ya saini ndani ya Baraza mkataba uchezewe.  Mambo hayakuwa hayo lakini, kwani pamoja na kutiliana saini na kukubaliana, CCM ilikataa kutekeleza hata kipengele kimoja.  Kati ya mambo waliokuwa wayafanye ilikuwa ni kuwafutia kesi wanachama 18 wa CUF ambao walikuwa wamo rumande kwa miaka 3 kuongejea ushahidi wa kesi ya uhaini juu yao ukamilike.

Zaidi ya yote sheria za uchaguzi zilifanywa kuwa mbaya zaidi ili kuhakikisha kwamba CCM inaendelea na kiti cha enzi katika uchaguzi uliofuata wa 2000.  Uchaguzi huu utapewa nafasi yake kuelezewa kwani ndio uliokuwa wa kishindo hasa kwa vile mshindo wake ulisikika kwa mara ya mwanzo msikitino ukimuangamiza Ustadh Juma Mohammed na mwenzake wawili hapo tarehe 26 Januari, 2001.  kishindo kilizidi kushindia wengine kwa mamia waliomwagiwa damu, wengine kunajisiwa na baadhi kukimbilia Kenya kujificha kama wakimbizi wa madhila na mateso ya kisiasa.  Ukisikia‚ushindi wa kishindo“ maana yake ni ushindi na mauaji na umwagaji damu.  Naam, mauaji yalitokea Tanzania nzima, lakin Pemba yalitia fora.  Kama kuna sababu maalum tutaona tukiendelea kusoma.

SURA YA TANO

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s