Sijawahi kushindwa uchaguzi – Maalim Seif

Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, (kulia) akipokea fomu ya kugombea nafasi hiyo kutoka kwa Mshika Fedha wa Tawi la Mtoni, Fatma Ali Omar, leo 7 Novemba, 2008

Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, (kulia) akipokea fomu ya kugombea nafasi hiyo kutoka kwa Mshika Fedha wa Tawi la Mtoni, Fatma Ali Omar, leo 7 Novemba, 2008

Na Ripota Wetu, Zanzibar

Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, amesema hajawahi kushindwa katika chaguzi zote zilizowahi kufanyika nchini tokea kurudhishwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini Tanzania.

Maalim Seif amesema hayo muda mfupi mara baada ya kujaza fomu ya kugombea nafasi ya ukatibu mkuu wa chama hicho katika tawi la CUF Mtoni, nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

Amesema anachukua fomu ya kugombea tena nafasi hiyo siyo tu kwa kuwa ana haki hiyo kikatiba, lakini pia anaamini kuwa bado anao uwezo wa kukiongoza chama chake na kwamba hali yake ya kiafya inamruhusu kuendelea kukitumikia chama na nchi yake.

“Hii ni haki yangu ya msingi. Mimi bado uwezo wangu wa kuwaongoza wananchi ninao na uwezo wa kusaidiana na wenzangu wa kukiimarisha chama chetu ninao, akili zangu bado ni nzuri sana kwa kukitumikia chama changu na nchi yangu.”

Kuhusu nafasi ya chama chake na upinzani kwa ujumla kuchukua madaraka ya nchi, hasa kwa kuwa Katiba ya Tanzania ina mapungufu makubwa panapohusika na mfumo wa kidemokrasia wa vyama vingi, Katibu Mkuu huyo amesema pamoja na mapungufu hayo anaamini kwamba upinzani unaweza kushinda mwaka 2010 kutokana na uongozi mbovu uliooneshwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) hasa katika kipindi hiki cha karibuni.

Akiyataja mambo ambayo yamejitokeza katika siku za hivi karibuni ni pamoja na masuala ya fedha za nje EPA, sakata la Richmond na migomo isiyokwisha ambayo yote hayo yanjidhihirisha kwamba nchi inayumba na imekosa uongozi imara.

“Nchi yetu sasa inayumba kwa kukosa uongozi thabiti. Mambo mengi yameanza kujitokeza na inajidhihirika hivi sasa kama chini ya uongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) nchi imewashinda na ipo haja ya uongozi bora na imara,” amesema Katibu Mkuu huyo ambaye anasubiri chama chake kimuidhinishe kuwa Katibu Mkuu mpya.

Amesema wakati wapinzani wakiendelea kudai katiba mpya, mikakati madhubuti inapaswa kuchukuliwa na kujiweka sawa ili kuiondosha madarakani CCM ambayo “imeonesha kushindwa na uongozi unaokwenda sambamba na maisha ya Mtanzania wa leo.”

Maalim Seif ameeleza kwamba viongozi wa Kiafrika wamekuwa na kawaida ya kung’ang’ania madarakani na kupuuza matakwa ya wananchi ambayo wakati wa kampeni waliahidi kuyatimiza.

Amesema kwamba sio rahisi kwa viongozi wa Kiafrika kujipiga kisu wenyewe kwa kutaka kubadilisha katiba kwani jambo hilo litawasafishia njia wapinzani ya kushika madaraka kwa haraka.

“Kukubali katiba mpya ni sawa na kujipiga kisu mwenyewe. Hawawezi hata siku moja kukubali mabadiliko, lakini dawa ni kujipanga vizuri katika uchaguzi.”

Amesema kwamba katika chaguzi zinazofanyika mara zote jimbo la Mji Mkongwe na kisiwa cha Pemba chama chake huwa kinashinda kwa asilimia kubwa licha ya kuwapo kwa katiba ‘mbovu’, hivyo hata pamoja na katiba hii hii upo uwezekano wa chama chake kuingia madarakani ikiwa kitajipanga vyema kukabiliana na vitimbi na hila za CCM.

“Pamoja na katiba yetu mbovu na tume ya uchaguzi, lakini mbona Pemba tunashinda vizuri? Na mbona Mji Mkongwe pamoja na kuwa wanatumia nguvu kubwa lakini tunachukua jimbo? Mimi nasema ni kujipanga vizuri tu.”

Maalim amewaambia wanachama wa CUF waliofurika katika tawi hilo kuja kumshuhudia wakati wa akichukua fomu hiyo, kwamba bado uwezo wake ni mkubwa wa kukiongoza chama chake na anaamini kwamba CUF bado ipo imara chini ya uongozi wa Mwenyekiti wake Profesa Ibrahim Lipumba.

Akizungumzia uchaguzi wa Marekani, Katibu Mkuu huyo amesema uchaguzi huo umetoa funzo kubwa kwa viongozi wa Kiafrika ambao hung’anga’nia madaraka kwa misingi ya kikabila na rangi.

Amesema kwa muda mrefu nchini Marekani, wengi miongoni mwa watu weupe walikuwa wakiamini kwamba mtu mweusi hana uwezo wa kuongoza taifa hilo, lakini sasa dhana hiyo imeondoka kutoka na umahiri mkubwa uliooneshwa na kiongozi aliyeshinda katika uchaguzi huo, Barrack Obama.

Amesema pamoja na kuwa Rais George Bush alirithi matrilioni kutoka kwa kiongozi aliyemtangulia, Bill Clinton, lakini fedha hizo hazikuweza kumsaidia chochote na matokeo yake uchumi wa Marekani umeporomoka kwa kiwango kikubwa.

Amesema wakati Waafrika wakitafakari uchaguzi wa marekani wanapaswa kufahamu kubwa suala la kung’ang’ania madaraka halina nafasi katika siasa za wakati huu na wanapaswa kuiga mfano wa mpinzani wa Obama, John McCain, ambaye alisoma upepo unapoelekea akajijua mapema kwamba hana nafasi ya kutwaa madaraka na akakiri hilo.

“McCain mapema alisoma upepo alianza kukubali mapema sana kuwa ameshindwa na uchaguzi wao hakukuwa na mizengwe lakini kwetu hilo halipo hasa. Zanzibar mwananchi hapewi haki ya kupiga kura akijulikana kama ni mpinzani.”

Amesema uchaguzi wa marekani uwe funzo kwa nchi za Afrika kutokana na kutokuwepo mizengwe wowote licha ya wananchi wa marekani kuwa ni wengi wanapiga kura lakini uchaguzi huo umekwenda kwa salama bila ya vurugu wala wizi wowote na matokeo ya uchaguzi yametoka mapema tofauti na uchaguzi unaofanyika hapa nchini ambapo matokeo huchezewa kwanza kabla ya kutangazwa.

Rais mteule wa Marekani, Obama, anatoka chama cha Democratic ambacho kina itikadi ya kiliberali kama kilivyo chama cha CUF. Umoja wa Kiliberali wa Kimataifa, Liberal International, juzi ulitoa taarifa ya kumpongeza Obama na kuwapongeza Wamarekani kwa kukipa ushindi chama hicho, kwani huko kunaonesha imani waliyonayo kwa sera, falsafa na itikadi ya kiliberali.

Maalim Seif amekuwa Katibu Mkuu wa CUF tangu mwaka 1999 na anagombea tena nafasi hiyo, ambayo kama atachaguliwa, ataishikilia kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s