CUF yashiriki maandamano ya Maalbino

Mwenyekiti wa CUF, Prof. Ibrahim Lipumba (wa pili kushoto) katika maandamano ya kupinga ukatili dhidi ya maalbino

Mwenyekiti wa CUF, Prof. Ibrahim Lipumba (wa pili kushoto) katika maandamano ya kupinga ukatili dhidi ya maalbino

Akiwa ameandamana na mamia ya watetezi wa haki za binaadamu, wanachama wa chama chake na maalbino, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Prof. Ibrahim Haruna Lipumba, ameshiriki katika maandamano ya amani kupinga mauaji na unyanyasaji dhidi ya jamii ya maalbino nchini Tanzania.

Maandamano hayo ambayo yalianzia makutano ya Samora Avenue na Independence na kuishia kwenye viwanja ya ukumbi wa mikutano wa Karimjee, jijini Dar es Salaam, yalipokewa na kuhutubiwa, pamoja na wengine, na Rais Jakaya Kikwete, leo Jumapili ya 19 Oktoba, 2008.

Wasanii wa Albino Cultural Troupe wakiwasilisha kilio chao kwa njia ya wimbo

Wasanii wa Albino Cultural Troupe wakiwasilisha kilio chao kwa njia ya wimbo

Akizungumza baada ya maandamano hayo, Prof. Lipumba alisema kwamba chama chake kimejengwa juu ya msingi wa haki za binaadamu na kinaamini kwamba maalbino ni wanaadamu kama wanaadamu wengine, ambao lazima walindwe kama inavyoagiza Katiba ya Jamhuri ya Muungano na Tamko la Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Binaadamu, ambalo Tanzania imesaini.

“Suala la maalbino ni suala letu sote. Maalbino ni ndugu zetu, watoto wetu, marafiki zetu – kwa ufupi maalbino ni sisi wenyewe. Hivyo, lazima tuwalinde kama tunavyojilinda wenyewe, na Katiba zetu zinaagiza hilo. Pia Tanzania ni mwanachama wa Umoja wa Mataifa na imesaibi tamko la kimataifa la kulinda na kuheshimu haki za binaadamu. Lazima ilitekeleze kwa vitendo kwa kuwahahakishia usalama wao maalbino.” Amesema Prof. Lipumba.

Wana-CUF wakiwaunga mkono maalbino katika kupaza sauti dhidi ya ukatili

Wana-CUF wakiwaunga mkono maalbino katika kupaza sauti dhidi ya ukatili

CUF ina kurugenzi maalum ya Haki za Binaadamu na Mahusiano ya Umma na pia ina sera maalum kuhusu watu wenye ulemavu, maalbino wakiwa miongoni mwao. Kaimu Mkurugenzi wa Kurugenzi hiyo, Mbaralah Maharagande, ambaye aliongozana na Prof. Lipumba katika  maandamano hayo, amesema kwamba ni jukumu la kuwalinda na kuwatetea maalbino maana wao ni sehemu ya raia wa nchi hii.

“Inaonekana Serikali haijafanya vya kutosha kuhusu tatizo hili. Ni karibuni mwaka wa pili tangu mauaji na ukatili dhidi ya maalbino utangazwe wazi. Bado umekuwa ukiendelea kwa kuwa hatua za haraka hazijachukuliwa kuusimamisha. Sasa maalbino wanajihisi hawako salama ndani ya mipaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambapo Katiba imewahakikishia usalama wao.” Amesema Maharagande.

Mapema katika ngonjera iliyotambwa na watoto maalbino, vitoto hivyo vidogo viliifananisha jamii ya maalbino Tanzania kama watoto wa kambo ambao hawana haki katika nyumba ya baba wa kambo. “Kwenye nyumba ya baba wa kambo, mtoto wa kambo sina haki!” kilisema kibwagizo cha ngonjera hiyo iliyopandisha hisia kali, machozi na vilio.

Pia wasanii kutoka kikundi cha Albino Cultural Troupe nao waliomboleza kilio chao mbele ya waandamanaji wakihoji ilipo salama yao na kwamba kama wao hawatakiwi kwenye ardhi ya Tanzania, basi wapewe nchi nyengine ya kuishi. Katika wimbo huo ambao nao ulikuwa na kila aina ya hisia kali za unyonge na maumivu, maalbino waliuliza kulikoni wafyekwe kama miti msituni au wachinjwe kama wanyama buchani na jamii iendelee kubakia kimya!

Wanachama wa CUF walishirikiana vyema na maalbino na wanaharakati wengine katika maandamano hayo ili kupaza sauti ya kupinga mauaji na ukatili dhidi ya jamii hiyo Tanzania. Mmoja wa wanachama hao, Shaweji Mketto, amesema kwamba hajisikii salama wala huru ikiwa albino wa Tanzania hajisikii huru na salama.

Prof. Lipumba amesema kwamba hakuna sababu wala kisingizio cha kushidnwa kudhubiti mauaji na ukatili dhidi ya maalbino na ameyaita mapambano hayo kama vita vinavyopasa kupiganwa na kila Mtanzania. “Hivi ni vita vyetu sote. Ni lazima tushinde kama Watanzania, ni lazima tushinde kama taifa.”

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s