Tendwa ana haki kuipinga CUF, si kuipotosha

  • Vipi ameamua kutia ulimi puani dakika hii?
  • Au ndio kujaribu kumpoka Yussuf Makamba nafasi

Na Mustakim Ali

John Tendwa ni mmoja wa maofisa wa ngazi ya juu katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Si hivyo tu. Huyu ni mtendaji mkuu wa ofisi adhimu ndani ya jamhuri yetu. Tendwa, msomi aliyebobea katika kada ya sheria, anaongoza Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini.

Kutokana na kuongoza kwake ofisi hiyo, wadhifa wake umepewa jina la Msajili. Kwa hivyo Tendwa ni Msajili wa Vyama vya Siasa nchini. Kila chama kinapotaka kusajiliwa kuwa kimoja ya vyama halali, basi lazima viongozi wa chama hicho, wapeleke maombi kwake.

Kwa mujibu wa sheria ya uanzishaji vyama vya siasa nchini iliyopitishwa na Bunge mnamo mwaka 1992, chama huanza kuomba kutambuliwa rasmi kwa kupatiwa hati ya usajili wa muda inayoshurutisha viongozi kuendeleza taratibu za kupata hati ya usajili wa kudumu.

Chama kikishatimiza masharti ya kisheria ya kuanzishwa kwake, kitakuwa kimekwenda kwa wananchi na kujitambulisha huku kikitumaini kupata wanachama wa kukiwezesha kuandikishwa kama chama chenye usajili wa kudumu. Kinakuwa na hati ya kusajiliwa rasmi kama chama cha siasa.

Basi kwa namna Ofisi ya Msajili ilivyoanzishwa, madhumuni ya kuanzishwa kwake na kazi zake, si uongo nikisema kwamba huyu Msajili ndiye mlezi mkuu wa vyama vya siasa. Yeye, kama mzazi, ndiye pia mlezi wa vyama hivi. Sasa kama mzazi na mlezi wa vyama vya siasa, Msajili lazima itakuwa amefungwa na kushabikia chama kimojawapo ya vile alivyovisajili na kupaswa kuvilea.

Msajili anakuwa mlezi wa vyama vyote kwa usawa na kwa haki. Haimjuzu yeye Msajili kuona chama fulani ni chama bora kuliko kingine. Anaweza akakiona chama kimoja kina sifa nzurinzuri kuliko vingine, lakini kukiona kwake hivyo, hakumuwajibikii kukipa umbele kisheria, kiusawa na kihaki kuliko vyama vingine.

Vyama vyote vinakuwa sawa kwake na mbele ya sheria. Na hii inatambulika hivyo hata kama inaeleweka kuwa kipo chama kimoja kinatawala dola. Kwa kuwa dhamira muhimu ya kuanzisha chama cha siasa ni kushika hatamu ya kuongoza dola, basi kinakuwepo kimojawapo huwa chama tawala. Kina haki zake lakini hakipaswi kushindana na vingine pasina kuzingatia usawa, haki na sheria. Chenyewe ni chama tu cha siasa kama vilivyo vile vingine visivyo madaraka ya dola.

Msajili, kwa maana hiyo, anabaki kuwa ni mtumishi wa serikali kupitia pale alipokabidhiwa dhamana na mteuzi wake, ya kuongoza. Bila ya shaka, ofisa huyu anawajibika kumtii Rais kwa kuwa; kwanza ndiye mteuzi wake na pili, ndiye kiongozi mkuu wa serikali ambayo kwayo, ofisi yake Msajili inawajibika.

Tunakubaliana kuwa katika utendaji wake wa kazi kama Msajili wa Vyama vya Siasa, Msajili ana wajibu wa kutenda kulingana na sheria ya usajili wa vyama isemavyo, kulingana na sheria za nchi zisemavyo na zielekezavyo na kulingana Katiba ya nchi isemavyo na ielekezavyo.

Lakini hatutarajii hata siku moja Msajili akawa Msajili wa Vyama na papo hapo akawa yeye Rais au Kiongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM). Hiki ndio chama dola, chama kinachoshika hatamu ya kuongoza dola, chama ambacho kwayo ndiko Rais wa Jamhuri ya Muungano, mteuzi wa Msajili Tendwa, atokako.

Ni imani ya kila Mtanzania kwamba Msajili ni mtu mahiri na makini kwa namna zote. Yeye Msajili anatarajiwa kuwa mtiifu kwa Katiba na Sheria za Nchi, ikiwemo Sheria ya Usajili wa Vyama vya Siasa inayomuongoza yeye kufanya kazi alizokabidhiwa dhamana kuzifanya. Msajili anatakiwa kuwa mtiifu kwa Rais kama mteuzi wake na mkuu wa nchi.

Kutokana na kuteuliwa kuongoza Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Tendwa ana wajibu wa kuwa muadilifu mbele ya umma anaoutumikia. Akiwa muadilifu, anajenga imani kwa mteuzi wake, Rais, na pia kwa umma. Basi ninaamini kwamba Tendwa ana jukumu la kuwa mkweli na kutembea kwenye maneno yake.

Haiingii akilini pale umma unapobaini kuwa Msajili wa Vyama vya Siasa, ameanza kuwa kichwa maji: leo anaamka na kauli hii, lakini kesho anaamka akiwa ameibadili. Kwa nafasi yake, Msajili ana ruhusa ya kufanya ziara kuangalia shughuli za vyama vya siasa. Jukumu hili ni muhimu kwa sababu kazi ya kulea vyama, haifanikiwi kwa kukaa ofisini tu.

Msajili anapelekewa barua za malalamiko, matatizo na maendeleo ya vyama vya siasa, kwa hivyo anapaswa si tu kutafuta utatuzi wa malalamiko na kusaidia kuondoa matatizo kwa kukaa na maofisa wake wasaidizi wakiwa kwenye viyoyozi. Lazima atembee kwenye ofisi za vyama ili ashuhudie kama aliyoandikiwa kwenye barua ni ya kweli.

Tofauti na Msajili aliyemtangulia, George Liundi, ambaye ameshafariki dunia, Tendwa amejitahidi kujitofautisha kiutendaji. Mara tu baada ya kuingia ofisini na kuzoea hali nzuri ya hewa humo ndani, aliamua kuzunguka kwenye wadau wake wakuu kikazi; vyama vya siasa. Ziara hizi zilimuwezesha kujifunza mambo mengi na ikawa kwake rahisi kutatua matatizo yaliyomfika au aliyoyabaini.

Moja ya mambo anayoweza kujivunia Tendwa, ni kufanikiwa kufungua ofisi kuu Zanzibar. Haya ni mafanikio makubwa kwake kama Msajili, lakini pia kwa vyama vya siasa vyenyewe. Vyama vilipunguziwa mzigo mkubwa wa kuifikia Ofisi ya Msajili Makao Makuu jijini Dar es Salaam. hata naye, tangu hapo, amekuwa akipata unafuu wa kufanya kazi zake anapokuwa Zanzibar.

Ndiyo maana Tendwa amefika Zanzibar mara kadhaa tangu kuteuliwa kwake. Amekagua shughuli za vyama na kujionea uhai wa vyama, akipata nafasi pia ya kubaini udhaifu wa vyama hivi. Wakati fulani alipata thubutu ya kutamka kuwa ukiacha vyama vichache mno, vilivyobaki vipo vipo tu Zanzibar, maana havina hata ofisi. Alivionya na kuvitaka vijirekebishe.

Lakini Tendwa anabadilika. Mabadiliko kwake yanatokana na kuyumba. Amekuwa akitoa kauli hii leo na baada ya muda kupita, pengine akidhani watu wamesahau alisema nini nyuma, anabadilisha. Ipo kwenye rekodi kwamba baada ya uchaguzi wa 2005, alipofanya ziara Zanzibar, aliahidi kumshauri Rais, mteuzi wake, kuiangalia kwa makini hali ya mambo ilivyo visiwani Zanzibar baada ya kuiona hairidhishi.

Vyombo vya habari vilimkariri akisema kuna matatizo ya kisiasa Zanzibar kutokana na matokeo ya uchaguzi yalivyokuwa. Na kwa kuwa yeye ni msaidizi wa Rais kwa upende wa ulezi wa vyama vya siasa, aliahidi kumshauri Rais njia za kuondokana na tatizo hilo.

Msajili Tendwa alisema ameona nchi ilivyogawika na kwamba itakuwa vizuri kukatafutwa namna ya kuundwa serikali itakayoziba mgawanyiko huo. Hayo aliyasema baada ya kuwa amekutana na viongozi wa juu wa CCM na Chama cha Wananchi (CUF), vyama vinavyovutana kila kimoja kikijitahidi kuwa na udhibiti wa siasa.

Juzi tumemsikia tena Msajili akizungumzia suala la Zanzibar. Kwa bahati mbaya tumemsikia kama mtu mwingine, si yule tunayemfahamu na tuliyewahi kusikia kauli zake za matumaini kila anapofanya ziara Zanzibar. Leo anasema ni hoja dhaifu CUF kutaka serikali ya mseto na pia wanajisumbua kutaka uchaguzi urudiwe.

Ninasikitika kwanza kufikiria ni vipi Tendwa alifikia kutoa tamko hili jipya. Sijui aliomba kutoa habari au aliombwa kutoa habari. Ni aibu kwa sababu mara ngapi atajitokeza kusema kila chama cha siasa kinapofanya maandamano au mkutano wa hadhara? Lakini upande mwingine inaonyesha kuwa Msajili anakitazama chama hiki vinginevyo tofauti na vingine. Sababu anazijua mwenyewe.

Tumemuona Tendwa akitoa maoni baada ya CUF kufanya maandamano na mkutano wa hadhara kuzungumzia matatizo ya kisiasa ya Zanzibar. Chama hiki kilitumia haki ya kikatiba kuandamana na kuhitimisha maandamano kwa mkutano wa hadhara Novemba 12 kwa lengo la kulaani kauli za Rais Amani Abeid Karume za kupinga kuwepo mgogoro wa kisiasa na kwamba hakuna mazungumzo ya kuyatatua.

Cha kutia uchungu ni kuona maelezo ya Msajili yanabeza hatua hiyo na kuhoji ina mantiki gani. Anajenga hoja kwa kusema Rais Jakaya Kikwete hajasema iundwe Serikali ya Mseto. Lakini Msajili ameyapata wapi haya? Hivi ni nani amepata kumsikia akisema Rais Kikwete ataunda Serikali ya Mseto au kwamba amesema hiyo ni moja ya njia anazozifikiria katika kutafuta ufumbuzi wa alichoiita mpasuko wa Zanzibar?

Anaposema Rais hajasema suluhisho la matatizo ya kisiasa Zanzibar ni kurudiwa uchaguzi au kuwa na serikali ya mseto, anakusudia nini wakati upande wa CUF hakuna kiongozi aliyenukuliwa akisema hivyo? Maana yake nini Msajili kuhoji kama CUF walielewa hoja? Au kwamba labda wana hoja wanazotaka wananchi wazielewe kama ni hoja za Rais? Hii maana yake Msajili anawafanya viongozi wa CUF ni wazushi.

Pia kwa kushikilia madai yao, haina maana kuwa CUF wanamuamrisha Rais, isipokuwa wanamhimiza atimize ahadi aliyoitoa kwenye Bunge. Ni hivyo kwa sababu kusema kwake amefikia pazuri, si kuwaeleza wananchi hatua anazochukua na angefanya hivyo kwa kuzingatia hali tata ya kisiasa Zanzibar. Ndio tuamini asemayo kuwa tatizo ni ugombanishi wa uongozi katika serikali? Wanaogombana ni nani, CCM wanaotofautiana kauli? Au CUF na CCM?

Walio makini, na ambao wamemuona Tendwa akitamka haya, wanaamini amebadilika haraka. Kwa bahati mbaya, Tendwa amegeuka na kuwa kama vile ni Msemaji wa CCM. Matamshi aliyoyatoa kuhusu hatua ya CUF yamemaanisha kuwa hana tofauti na Luteni Yussuf Makamba, Katibu Mkuu wa CCM. Kiongozi wa CCM ni kawaida yake kutoa kauli za kubeza kila kinachofanywa na CUF, lakini Tendwa si kiongozi wa CCM, ni Msajili.

Kwanza amesahau kuwa alitoa maoni ya matumaini kwa watu alipotembelea Zanzibar; amesahau kuwa yeye ni mlezi wa vyama vya sisasa kikiwemo CUF, na amesahau yeye ni Msajili wa vyama vyote nchini. Hakuna aliyemtarajia kuwa atatoa kauli za kuiunga mkono CUF kwa hoja yake, lakini angalau angeshikilia yale yale aliyowahi kuyasema miezi kadhaa michache iliyopita baada ya kubaini matatizo ya Zanzibar.

Msimamo wa CUF ni ule ulioelezwa kwenye mkutano pale Uwanja wa Demokrasia, Kibandamaiti. Msajili anaweza kuwa na msimamo wake ukiwa wa kupingana na CUF, lakini pia umma hautarajii kamwe, msimamo wake uwe wa kupotosha ukweli. Msajili ajue kwamba ukweli utabaki kuwa ukweli tu.

UKURASA 11 – NI VIPI KARUME ALIYEKO JIKONI ASIUONE MPASUKO?

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s