Siku Moja Itakuwa Kweli

  • Nakutana na Nyerere

Na Ali Nabwa

Nilipofika London nikijiringia kiakiba changu kutoka Manchester. Nikapanga East Africa House, karibu na Marble Arch. East Africa House ilikuwa ni mahala pazuri pa kukutania wananchi wote wa Afrika Mashariki, na hata Waingereza waliofanya kazi katika serikali za kikoloni huko na walitaka kuendeleza mahusiano yao binafsi walifika hapo. Ilikuwa nyumba safi yenye vyumba vya kulala,ukumbi wa chakula mzuri na mahala pa vinywaji na kuzungumzia.

Nakumbuka siku moja tulikuwa tunajiburudisha kwa vinywaji, na walikuwa mtu na ami yake. Jamaa aliyekuwa akisimamia meza akamuuliza kijana atakunywa nini,akasema Coca Cola, akamuuliza ami, naye akasema hivyo hivyo, lakini yeye akiwajuwa uzuri, hivyo akaenda kuchanganya madawa akawaletea. Ikawa hivyo duru ya pili, lakini duru ya tatu kijana akasema, “Mimi ile ile Coca Cola na Whisky,” na ami naye akaona potelea pote, akasema, “Na mimi ili ile Coca Cola na Gin.” Tangu hapo ukuta ukaporomoka baina ya mzee na mwana mambo yakawa shahir dhahir.

East Africa House ilikuwa karibu na Hyde Park, uwanja maarufu wa kila mtu kwenda kujisemea alitakalo. Kuna mzee mmoja akipendwa na wengi. Yeye akianza na kusema, “I am not, yaani, Mimi si…” Akiendelea hivyo hivyo mpaka amezungukwa na watu wengi ndipo anamalizia, “a speaker.” Yaani yeye si msemaji. Watu wanacheka, wanampigia makofu na wanamtunza. Wengi wao weshamsikia mara nyingi, lakini bado wakihusudu uchale wake, hasa kuzingatia umri wake. Uingereza ilikuwa hairuhusiwi kuomba moja kwa moja, lazima ufanye kitu watu wakutunze, na hii ndio ilikuwa kitu yake huyu mzee.

Baadae nikahamia Golder’s Green,lakini mwishowe sahibu yangu marehemu Dr Said Himid akanishauri nikakae na mama mmoja wa asili ya Austria ambaye aliwahi kukaa naye yeye huko Shaphard’s Bush. Aliniambia ana shahada ya Ph.D. na anawapenda sana Waafrika.

Lakini hatimaye Serikali ilipojuwa nimekatisha masomo nikazuiliwa malipo na ndipo nilipotumbukia katika dimbwi la ulofa. Nilipata kazi ya mhudumu katika hospitali moja ya East End,wakati huo likiwa eneo la kutisha kweli. Kulikuwa na mzee mmoja wa ki-Cockney akiitwa Cook. Alikuwa mnene sana na alikuwa na ugonjwa wa moyo,hajiwezi kwa lolote.

Nikiwa zamu hataki kuhudumiwa na yoyote isipokuwa mimi,sijui hii ilikuwa na maana kwamba alinichunuka au aliona mtu mweusi ndio kazi zake hizi. Nakumbuka siku moja nilikuwa zamu usiku,muuguzi akaniambia anakwenda kunywa chai saa sita. Kurudi nikaona ananiamsha kwa kishindo na kuniambia kuna mgonjwa amefariki kitambo na yuko kinywa wazi. Tukashirikiana kumfunga kinywa,akamuwekea mto na akaniambia nishikilie vizuri wakati anakwenda kumuita daktari.. Kurudi akanikuta nimemlalia maiti nakoroma, wa juzi.

Baadae nikapata kazi ya kurekodi vipindi vya Central Office of Information,COI,kwa ajili ya Afrika Mashariki na Kati kwanza chini ya mzungu kutoka Rhodesia,Dampster,na baadae Mtanzania, Wagi. Mimi nilikuwa kiongozi msaidizi.Baadhi ya viongozi mashuhuri wa Tanzania leo walishiriki katika vipindi hivyo. Vibarua hivi vya muda vilivyopita,nikaanza mradi mpya..Sijui ilianzaje,likini nilikuja kugundua kwamba watu wanapoteza pesa nyingi wanapokaa kwenye makochi ya kudidimia.

Nilitembea Jiji la London usiku kucha, Oxford Street, Picadily Circus,Trafalgar Square,usingizi ukinishika nakwenda kulala steshen ya gari la moshi Charing Cross nikifanya kama nangojea gari la mwanzo. Sio kama nikiwachezea akili askari. Hasha. Lakini hiyo ilikuwa London ya Waingereza, ambao wakisifiwa kuwa ndiwo wenye askari polisi pekee wasiobeba silaha za moto.

Waliniona,walinitambuwa na kunipima kuwa sina madhara yoyote hivyo wakiniacha nijitese mwenyewe.Asubuhi mapema milango ya East Africa House ilipofunguliwa, nilikuwa wa kwanza kuingia na kwenda kujitupa kwenye kochi ukumbini na kulala. Lakini sio kabla sijachovya mikono yangu mgongoni na kuitumbukiza ndani kabisa mwa kochi. Mbizi mbili-tatu kama hizo na sikosi chai ya asubuhi na chakula cha mchana.

Jioni moja,nikiwa peke yangu ukumbini nikiendeleza shughuli yangu ya kusafisha makochi,alitokea Oscar Kambona, Katibu Mkuu wa Tanganyika African National Union, TANU, aliyekuwa masomoni London. Kambona alikuwa rafiki mkubwa wa Salim Rashid na Abdalla Kassim Hanga,ambao wote wawili walikuwa watu wa karibu sana na mimi.

Sasa Kambona alikuwa amefuatana na jamaa mwembamba aliyevaa suti nyeupe na sharubu za Hitler. Nilimtambuwa kuwa ni Mwalimu Julius Kambarage Nyerere anatoka kwenya mkutano wake maarufu Umoja wa Mataifa mwaka 1959. Aliniuliza taarifa ya habari ya jioni inakuwa saa ngapi,nikamuambia saa kumi na mbili, akaangalia saa yake kisha wakatoka. Ilikuwa mara yangu ya kwanza kukutana na Mwalimu Nyerere. Nilikuwa maarufu East Africa House kwa kuwaelekeza watu njia,route,za mabasi ya London kwa vile nikilitembea Jiji zima kwa miguu,sasa nilikuwa namuelekeza Mwalimu saa za kusikiza taarifa ya habari.

Kama nilivyosema, East Africa House ilikuwa karibu na Hyde Park. Kina dada wakijipanga Bayswater yote kuanzia Marble Arch hadi Nottinghill Gate station na upande mwengine ikinyosha Park Lane mpaka Hyde Park Corner.Akipita mtu wanamwita, “Unataka starehe? Muda mfupi? Muda mrefu?”

Kama ni muda mfupi, wanaingia bustanini, anampa pauni moja na wanakwenda kwenye mti usiokuwa na mtu. Hawawahi hata kukohoa mti ushazungukwa na jamaa weusi, warefu na makofia makubwa kutoka Caribbean kama watu waliokata tiketi ya mpira wanangoja kushangiria.

Siku moja walikuja watunga sheria wawili, LEGCO, kutoka Tanga, mmoja wa umri, mwengine kijana mfupi, maji ya kunde, damu inamchemka. Kufika tu akataka nimpeleke kwa mwanamke wa kizungu. Nikamuambia atulie mpaka tule chakula cha usiku, asiwe na wasi wasi, yuko Ulaya, wamejaa tele. Wakati ulipowadia nikamuongoza. Kama kawaida walizungukwa na jamaa zetu wa West Indies. Alichukuwa mama kubwa. Mara nasikia makofi na hoi hoi kutoka kwa watizamaji. Kutupa jicho namuona jamaa yuko chini na yule mama kama chozi aliyepanda mbuyu. Kutoka pale yule mama akasema waende nyumbani kwake, kawaida pauni tatu, kila kitu juu yake, pamoja na chai ya asubuhi.

Kina Kambona walikuwa na mwenzao akiitwa Dennis Pombea. Alikuwa Mkoministi mkubwa na akiheshimiwa sana katika ‘nchi za nyuma ya pazia la chuma’. Maji yalipozidi unga niliwaomba wanipatie fursa ya kwenda kusoma huko. Baada ya muda mfupi tu nikapatiwa nafasi ya kwenda kusomea udaktari Rumania. Nikaondoka London Victoria Station na gari la moshi la Ostende, Ubelgiji, kisha nikaelekea Berlin Mashariki.

Kufikia huko ilikuwa lazima upite miji ya Ujerumani Magharibi na ulihitaji viza,mimi sikuwa nayo. Nilipita, sijuwi vipi. Nafikiri Kijarumani changu nilichopata kwa yule mama wa Kiaustria kilisaidia kidogo.

Kivumbi ilikuwa baada ya kuingia Berlin kwenyewe, kwani mji huo ulidhibitiwa na dola nne, Muingeeza, Mfaransa, Marekani na Mjarumani. Sema kitu kimoja kikisaidia – ukiona stesheni chafu,haina matangazo,unajua hapo ni German Democratic Republic, GDR, Ujarumani Mashariki.Nilielekezwa kuwa baada ya Zoo Garten,ambayo ni sehemu ya Muingereza,nishuke stesheni ya pili. Kutoka pale nikaelekea Unter den Linden, moja katika mabarabara makubwa aliyojenga Hitler,autoburn,ambapo ndipo yalipokuwa makao makuu ya umoja wa vijana, FDJ, na ambapo ndipo ulipojengwa Ukuta wa Berlin baadae,ambao mimi mwenyewe nilikuja kuushuhudia.

Nilimkuta kijana wa Kialgeria analia machozi baada kuambiwa arudi magharibi. Mimi kumtaja Dennis Pombea tu nikapokelewa kwa mikono miwili na kuwekwa katika moja ya hoteli wanazofikia vigogo. Jioni nikamuona Said kafika kutoka Leipzig. Nafikiri aliitwa kuja kunitambuwa, kwani nilimtaja pia. Siku ya pili tukaondoka kwenda Karl Max University, Leipzig, ambapo nilikaa siku tatu nikitayarisha safari yangu ya Rumania. Nilipita Czechoslovakia, Hungary mpaka mpakani mwa Rumania. Nilikuwa nimechanganyika na wanawake wanene, waliojizongeresha maguo kuepuka baridi. Walikuwa na ‘miche’ ya salami, sausage nene, na mikate meusi. Walinigaia, hivyo sikukaa na njaa.

Kufika mpakani nikateremshwa na askari waliovalia makoti mazito,mikanda minene na mabuti yaliyofika magotini na kofia za manyoya. Nilitambuwa sasa niko mbali na ‘ulimwengu wa kiingereza’. Nilihojiwa hapo na nilijibu jinsi nilivyoweza kwa Kijerumani changu kibovu, mbele ya taa ya kandili. Niliona treni niliyokuja nayo inaondoka,lakini mimi nikazuiliwa mpaka asubuhi. Baada ya kukorokochwa simu ukafanywa mpango nikaondoka na treni iliyofuata. Kuanzia hapo safari ya kuelekea Bucharest, mji mkuu wa Rumania ilikuwa nyepesi.

Nilifikia kwenye nyumba ya wanafunzi wa Technical College, lakini kila mtu alinionya kuwa atakuja mwanafunzi mmoja wa Sudan, Osman Hassan Sorkati, kutaka kunichukuwa nikaishi naye kwenye hosteli ya wanafunzi wa Chuo cha Udaktari, nisikubali. Nikawauliza kwa nini,wakaniambia nitaishia madeni. Masikini, hawakujuwa yatakayofuata. Osman alikuwa kaka yangu wa kweli, na aliniokoa na ‘scandal’ nyingi. Yeye na Msudani mwenzake, Suleiman, walikuwa wanachama wa Communist Party ya Sudan na hivyo wakipendeza kwa uongozi wa George Georgescu na Osman alitumia umaarufu wake kuniokoa.

Siku ile niliyofika, mwanafunzi mmoja wa Tunisia alinichukuwa chumbani kwake akanikaribisha chai, lakini alisema bahati mbaya hakuwa na kijiko, hivyo ilibidi akoroge sukari kwa msuwaki.

UKURASA 5 – CUF INAPOKARIBIA TURUFU YA KISIASA ZANZIBAR, CCM WANAUWANGIA MUUNGANO

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s