Kikwete amezungukwa na wahafidhina – Lipumba

  • Ni akina Karume, Shein na Shamuhuna
  • Asisitiza hoja ya CUF ni uchaguzi chini ya UN
  • Amtaka Kikwete aone kuwa subira ina mipaka
  • Machano: CCM inaamini juu ya vurugu
  • Mrema: Watu hawa watakuharibia
  • Bimani: Tutadai haki hata mbele ya mizinga na vifaru

Na Mustakim Ali, Zanzibar

Chama cha Wananchi (CUF) kimekamilisha ratiba yake ya
maandamano na mikutano mitatu ya kulaani vikali kile inachokiita kauli za uchochezi zilizotolewa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Amani Abeid Karume, juu ya mpasuko wa kisiasa Zanzibar na kuunga mkono jitihada za Rais Jakaya Kikwete katika kuupatia ufumbuzi wa kudumu mpasuko huo, kwa kufanya maandamano makubwa mjini Wete kisiwani Pemba, juzi Jumamosi.

CUF imekamilisha ratiba hiyo kwa kurejea wito wake wa kumtaka Rais Kikwete akamilishe haraka mpango wake alionao kwa mpasuko huo hasa ikizingatiwa kwamba kuna njama za makusudi za kumfelisha kutoka ndani cha Chama chake mwenyewe Cha Mapinduzi (CCM), ambacho yeye (Rais Kikwete) ni mwenyekiti wake.

Ikiwataja kwa majina na nafasi zao, CUF imesema kwamba Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk. Ali Mohamed Shein, Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Amani Abeid Karume na Naibu Waziri Kiongozi, Ali Juma Shamhuna, wameutumia ukimya wa Rais Kikwete katika suala la Zanzibar, kuvuruga hatua yoyote iliyopigwa au inayokusudiwa kupigwa katika utafutaji wa suluhu kutokana na ubinafsi wao.

Katika hatua iliyoonesha kuwa hao ndio viongozi wanaomharibia Rais Kikwete umakini wa utekelezaji wa ahadi ya kuondoa mpasuko huo aliyoitoa kwenye hotuba yake ya Disemba 30 ndani ya Bunge, mjini Dodoma, wasemaji wakuu wa mkutano wa hadhara wa Chama cha Wananchi (CUF) uliofanyika mjini Wete, walisema hawana isipokuwa ubinafsi tu.

Kuonesha ukorofi wa viongozi hao, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alimuhimiza tena Rais Kikwete kuchukua hatua za kumaliza mgogoro wa Zanzibar, maana kadiri siku zinavyozidi kwenda “subira ya CUF inashuka sana.”

“Tunataka uchaguzi huru na wa haki chini ya Umoja wa Mataifa kwa sababu ni wao tu watakaowaleta uchaguzi huu baada ya serikali ya CCM kushindwa mara tatu kutuhakikishia uchaguzi huru na wa haki.

“Rais Kikwete ukitaka kumaliza tatizo, itisha uchaguzi na waombe Umoja wa Mataifa kusimamia. Hili si jambo jipya. Yametokea Liberia, yametokea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Tatizo la Zanzibar ni kushindwa kwa uongozi wa CCM kufanya kazi. Sera mbovu ndio zinazoivuruga nchi. Tatizo ni CCM tu,” alisema.

“Watanzania wanakuunga mkono katika ahadi yako ya kushughulikia suala la Zanzibar, lakini wao ni binadamu si malaika. Wazanzibari ni binadamu, wamefanya subira sana sasa ina mwisho. Chukua hatua,” alisema Profesa Lipumba aliyekuwa mgeni rasmi wa mkutano uliotanguliwa na maandamano makubwa ya wana CUF wa mikoa miwili ya Pemba yakianzia Weni na kuishia viwanja vya Mnazimmoja.

Majina ya viongozi hao watatu wa CCM yalikuwa mdomoni mwa Profesa Lipumba kila wakati alipozungumzia hoja ya kuharakisha hatua za ufumbuzi wa mgogoro wa Zanzibar akiwaita kuwa ni la wahafidhina wanaomzunguka Rais Karume ambaye mwenyewe ndiye mhafidhina namba moja.

Profesa Lipumba alisema suala la kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar si geni, kwani lilijadiliwa kwa kina na Kamati ya Makatibu Wakuu ya CCM na CUF na kutolewa pendekezo kuwa baada ya uchaguzi, chama kilichokosa mgombea wake kuchaguliwa rais, kitapewa nafasi ya Waziri Kiongozi na kusimamia kuundwa kwa serikali ya pamoja.

“Kamati ya CCM iliongozwa na Philip Mangula na ya CUF ikaongozwa na Maalim Seif. Wajumbe wa CCM ni Mzee Kingunge (Ngombale Mwiru), Omari Mapuri, Mohamed Aboud na Dk. (Masumbuko) Lamwai na yetu CUF wajumbe ni Ali Haji Pandu, Hamad Rashid, Abubakar Khamis na Khamis Hassan. Tuliandika rasimu ya namna ya kuendesha siasa Zanzibar. Sisi tulizitia baraka kwa Baraza Kuu la Uongozi lakini CCM hawakuipeleka (rasimu) Kamati Kuu yao .

“Sasa Karume anaposema hajui haya simuelewi; na ningedhani alikuwa katika kinywaji chake cha John Walker maana alisherehekea sana siku iliyotangulia Novemba Moja,” alisema.

Majina ya Rais Karume, Dk. Shein na Shamhuna yalitajwa pia na Makamu Mwenyekiti wa CUF, Machano Khamis Ali, ambaye alisema kauli za Rais Karume, Dk. Shein na Shamhuna zinamaanisha kuamini kuwa vurugu kwa viongozi hao wa CCM ni kuona watu wanauliwa, kwa hivyo wanataka kuwe na hali kama hiyo ndipo waseme Zanzibar kuna matatizo ya kisiasa.

Machano alisema si CUF waliomtuma Rais Kikwete kuzungumzia hali mbaya ya kisiasa ya Zanzibar, bali ni yeye mwenyewe baada ya kuona kweli ipo hali hiyo na akaahidi mbele ya wabunge kuiondoa.

“Hatukumtuma sisi aseme yale. Aliyoyasema yametokana na uoni wake baada ya hali iliyosababishwa na CCM chini ya uongozi wa Rais Mstaafu Benjamin Mkapa.

“Tuna ushahidi. Jeshi walituambia baada ya matukio ya mwaka 2001 walilalamika kutumiwa kuwaua ndugu zao, ndio mwaka jana wakaleta jeshi la kigeni… kwa Dk. Shein vurugu ni watu kuuawa kama ilivyotokea Burundi walikouliwa watu 800,000. Sisi tunasema serikali ya CCM haina uwezo wa kuzuia vurugu kama hili likija. Inashangaza wanachochea vurugu ili tuuane,” alisema.

“Rais Kikwete alisisitiza tatizo la Zanzibar na kuahidi kulitafutia ufumbuzi. Akarudia mote alimofanya ziara nchi za nje. Tunajiuliza hawa wana CCM wenzake kawatuma, wanamuasi au nini?” alihoji na kuwasihi wana-CUF kutafakari jibu la swali hilo na wakishalipata huo ndio msimamo wa CUF.

Alisema kama hakuna mpasuko Zanzibar, ina maana gani serikali kubagua watu wa Pemba katika ajira na nafasi za masomo.

“Eti leo Mpemba lazima abadilishe cheti cha kuzaliwa kioneshe anatoka sehemu za Unguja ndipo apate anachokitaka serikalini. Waziri mmoja tu kutoka Pemba yumo katika serikali, mwalimu mkuu na msaidizi wake katika maskuli ni waliokuwa wametoka Unguja. Bado hapana mpasuko Zanzibar!?” Alihoji Machano kwa mshangao.

Makamu Mwenyekiti huyo wa CUF alisema, “CUF itaendelea kumuonesha imani Rais Kikwete kwamba hiki si chama cha fujo, si chama cha Pemba peke yake wala si chama cha kidini, ndio maana kipo mpaka Musoma. Chama cha vurugu ni CCM na watu wakishafahamu hivyo na dunia wakishafahamu hivyo na kukubali hali hiyo, hapo ndipo itakapoonekana kama CUF ni chama cha vurugu.”

Lakini, kama alivyofanya Prof. Lipumba, Machano pia alimpa indhari Rais Kikwete kwamba akiendelea kukaa kimya bila ya kusema hatua alizofikia katika kutafuta ufumbuzi wa mgogoro wa kisiasa Zanzibar, CUF itachukulia kuwa wale viongozi wengine wa CCM wanaungwa mkono naye.

Alikuwa ni Mwenyekiti wa Taifa wa Tanzania Labour Party (TLP), Augustine Mrema, aliyehudhuria kikamilifu na sambamba na Profesa Lipumba katika mapokezi ya maandamano pamoja na mkutano wa hadhara, ndiye aliyeanza kuwataja na kuwachambua viongozi hao watatu wa CCM (Shein, Karume na Shamhuna) kuwa kikwazo kwa jitihada za kuijenga Zanzibar mpya na akamshauri Rais Kikwete atahadhari nao.

Akitumia saa nzima kurusha shutuma dhidi ya wasaidizi hao wanaoelezewa kuwa wanamdhihaki waziwazi Rais Kikwete, Mwenyekiti huyo wa TLP alisema wakati umefika kwa Rais Kikwete kusema hasa nini anaona ni ufumbuzi muafaka wa tatizo la Zanzibar.

“Rais Kikwete namwambia kwamba, sasa lazima aseme, yeye ndiye daktari wa kubainisha dawa kwa mgonjwa huyu Zanzibar. Hali ni mbaya na yatakayotokea huku Pemba ni makubwa kuliko anavyofikiria.

“Sisi TLP tunakupa ushauri, tena huu ni ushauri wa bure. Kwamba acha mzaha dhidi ya watu wako hawa wanaokukwamisha. Tatizo hapa ni kigenge kidogo sana cha watu fulani wanaotaka wao kuhalalisha kuwa ndio watawale milele. Hebu chukua hatua na uamue kuwashirikisha hawa walioamua kuchagua CUF, waingize katika serikali waijenge Zanzibar,” alisema.

Mrema alisema tatizo kubwa kwa Pemba ni kubaguliwa kwao kwa sababu ya msimamo wao wa kupigania haki. “Zaidi ya watu 30 waliuawa Januari 26 na 27 kwa sababu ya kudai haki za kidemokrasia. Halafu anatokea mtu wa Pemba anapenda CCM, hakuna sababu ya kupenda CCM nyie na anayesema CCM nambari wani ni fal… mkubwa,” alisema.

Aliisifu CUF kwa kuwa makini kisiasa na jasiri katika harakati zake za kudai haki yake, na akakieleza kuwa ni chama tofauti na vyama vingine nchini. “Mna historia nzuri ya ukombozi wala msituangushe, maana tunaona huku ndiko kuna njia ya kuikomboa Tanzania ,” alisema.

Alisema kinachoisibu CUF ni kampeni za kutaka kukivuruga kwamba kionekane eti kina nguvu Pemba tu. Alisema chama hicho kimepata bahati nzuri ya kuwa na Maalim Seif Sharif Hamad aliyemtaja kama mwanasiasa makini aliyemfahamu tangu yeye akiwa Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania .

“Mtamchukua kila mpinzani baada ya kumchukua yule Tambwe, lakini wapi, hamumpati Maalim Seif. Kwanza hamjui hata bei yake,” alisema katika kauli iliyozidi kuwatia hamasa wana-CUF waliohudhuria mkutano huo.

Mrema alisema CCM wanajaribu kwa mbinu nyingi kumchonga Maalim Seif mwingine Pemba lakini wameshindwa. Alisema walianza kwa Dk. Omar Ali Juma, aliyekuwa Makamu wa Rais na kufariki dunia mwaka 2000.

“Wakamleta Dk. Shein na sasa wanamtafuta Maalim Seif wa kuchonga ambaye atakuwa hana madevu. Watashindwa tu. Hizi ni chuki za makusudi za kuvuruga msimamo wenu wa umoja na mshikamano kwa chama chenu hiki. Haiwezekani katika serikali ya Karume hakuna Mpemba isipokuwa yule mama mmoja. Inakuaje marais sita wote wanatoka Unguja peke yake?,” alihoji.

Alisema ubaguzi unaofanywa na CCM ni mbaya hata kuliko ule uliofanywa na Makaburu nchini Afrika Kusini. Kwamba hawa Wapemba ni watu wa kupigwa tu, ni watu wa kuuliwa tu.

“Rais wetu lazima tukwambie hawa ni kigenge kidogo mno kinachotumia Mapinduzi ya Zanzibar kujinufaisha. Wanatumia raslimali zote kwa maslahi yao wakiendeshwa na ufisadi mkubwa… mafisi wakubwa hawa,” alisema.

Itakumbukwa kuwa Mrema amekuwa pamoja na CUF katika ratiba hii nzima ya maandamano haya iliyoanzia Dar es Salaam tarehe 11 Novemba, yakaendelea Unguja tarehe 12 Novemba hadi katika haya ya mwisho ya tarehe 18 Novemba. Katika kila mkutano, amekuwa akipewa muda mrefu wa kuzungumza na wananchi na kuwasilisha salamu za chama chake ambacho, amekuwa akisema, kinaunga mkono kikamilifu jitihada za CUF na za Rais Kikwete katika kuupatia ufumbuzi wa kudumu mpasuko wa Zanzibar.

Risala ya wana CUF yenyewe ilikuwa nzito, wakisema kauli za Rais Karume na Dk. Shein siyo tu zimefufua hasama, bali pia zimekumbusha makovu ya yaliyotokea mwaka 2001.

Katibu wa Wilaya ya Chake Chake, Saleh Nassor Juma, alisema: “CCM hawaaminiki hata mara moja kiasi kwamba wakikwambia wanakwenda Wete, basi kawasubiri Mkoani.” Wete iko Kaskazini ya kisiwa cha Pemba wakati Mkoani iko Kusini mwa kisiwa hicho.

Wana CUF pia walishutumu mwenendo wa Sauti ya Tanzania Zanzibar (STZ) na Televisheni ya Zanzibar (TvZ) kwa kile kilichoelezwa kuwa ni vyombo vinavyoeneza chuki mfano wa redio ya Interahamwe iliyokuwa nchini Burundi.

“Vyombo hivi vinajisahau hasa kwamba ni vya serikali vinavyokwenda kwa kodi yetu wananchi, ni ajabu kubwa mambo wanayoyafanya ni sawa na Interahamwe wanataka tuuane tu basi,” alisema Saleh akikazia hoja iliyoanzishwa na msoma utenzi katika mkutano huo, Said Hamad.

Utenzi uliotungwa na Kombo Khamis Kombo ulisisimua kama ambavyo ulikuwa ukitia huzuni watu. Ulisema kauli za Rais Karume ni za kishetani zisizoashiria mema hata chembe.

Ni utenzi huo huo uliowakumbusha viongozi wakorofi wa CCM yaliyotokea kwa Rais wa Kwanza wa Zanzibar baada ya Mapinduzi, Mzee Abeid Amani Karume aliyeuawa kwa risasi mwaka 1972, Dk. Omar Ali Juma, Mwalimu Nyerere aliyefariki mwaka 1999 licha ya kusema angeishi zaidi ya hapo na Balozi Ahmed Hassan Diria aliyefariki mwaka 2002 akiwa pia alitamba kabla kuwa hali yake ya afya ilikuwa makini.

Walitakiwa viongozi wa CCM kufuata mwenendo aliouonesha kiongozi wa tatu kwa Zanzibar, Dk. Idris Abdulwakil, ambaye aliachia madaraka baada ya kuona wakati umempita ili aachie vijana kuongoza. Mzee Idris aliachia ngazi kabla ya uchaguzi wa mwisho wa chama kimoja mwaka 1990.

Naibu Mkurugenzi wa Habari, Haki za Binadamu na Mawasiliano ya Umma, Salim Bimani, alisema hakukuwa na uchaguzi huru na wa haki 2005 kwa sababu kigezo kikuu cha uchaguzi huo ni kulindwa kwa haki za binadamu, jambo ambalo lilikosekana.

Alisema CUF itadai haki kwa nguvu zote ikiwemo ya kurejewa kwa uchaguzi na kwamba katika hilo, hakutakuwa na woga kwa mzinga.

UKURASA 3 – JUHUDI ZA KUSHUGHULIKIA ‘MPASUKO’ ZIWEKWE WAZI

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s