Ardhi ya Watanzania yagaiwa kwa wageni – Jecha

1.0    UTANGULIZI

 

1.                   Mheshimiwa Spika awali ya yote nachukuwa nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu, Mwenye kupasa kushukuriwa ambaye ni Rahimu, Mwenye nguvu mwenye ukarimu na Mwingi wa hekima Ambaye ametupa uhai na afya njema siku ya leo tukaweza kukutana kutekeleza wajibu wetu tuliokabidhiwa na wananchi kwa manufaa yao na kwa manufaa ya Taifa letu.

 

2.                   Mheshimiwa Spika, kadhalika nikushukuru wewe binafsi kwa kunipa nafasi ya  kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu kuwasilisha maoni ya Kambi ya Upinzani kuhusu Bajeti ya Wizara ya Maendeleo ya  Mifugo na Uvuvi  kwa mwaka wa fedha 2008/2009 kwa mujibu wa Kanuni za Bunge Kifungu cha 99 (7) toleo la 2007.

 

3.                   Mheshimiwa Spika nitakuwa mchache wa fadhila kama sikuchukuwa nafasi hii kukishukuru chama changu cha CUF kwa kuniteuwa na hatimae kuchaguliwa kuwa Mbunge. Nakishukuru sana Chama changu kwa hatua hiyo. Aidha napenda kuwapongeza wananchi wa Jimbo langu la Wete kwa kuendelea kuniunga mkono katika  kutekeleza wajibu wangu. Nawaahidi kwa uwezo atakaonipa Mwenyezi Mungu nitawatumikia vyema na kwa juhudi zangu zote, na sitowaangusha.

 

4.                   Mheshimiwa Spika, Aidha natoa shukrani zangu za dhati kwa Waheshimiwa Wabunge wote wa Kambi ya Upinzani kwa mashirikiano yao makubwa wanayonipa yanayonipelekea kuifanya kazi zangu kwa wepesi na kwa ufanisi zaidi. Bila ya kuwasahau wabunge wote wa Bunge lako Tukufu kwa uswahiba na urafiki tulionao unaonifanya kujiona ni miongoni mwao.

 

5.                   Mheshimiwa Spika, napenda pia kuchukuwa fursa hii kuwashukuru viongozi wangu wa Kambi ya Upinzani kwa kutuongoza, kutuelekeza na kutusimamia vyema katika shughuli zetu za kila siku. Ufanisi mkubwa unaoonekana katika Kambi yetu ni kutokana na Uongozi wao mahiri.

 

2.0    HALI  HALISI YA MIFUGO NCHINI .

 

6.                    Mhesshimiwa Spika, mwaka 2007 ,shughuli za kiuchumi za mifugo ziliathiriwa na ugojwa wa homa ya  bonde la ufa, hata hivyo idadi ya mifugo iliongezeka kiasi, ng’ombe walifikia 19.1 milioni ikilinganishwa na 18.5 milioni mwaka 2006, mbuzi walikuwa 13.6 milioni ikilinganishwa na 13.5 milioni mwaka 2006, kondoo 3.6 milioni ikilinganishwa na 3.5 milioni mwaka 2006. Jumla ya idadi ya kuku ilikuwa 30 milioni ambao ni sawa na mwaka 2006, hii inaonyesha kuwa kwa kipindi cha mwaka mzima kuku hawakuongezeka na wala hawakupungua.

 

7.                   Mheshimiwa Spika, ugonjwa wa homa ya bonde la ufa uliathiri uzalishaji wa nyama ya ng’ombe,mbuzi,kondoo,nguruwe na kuku. Kupungua kwa asilimia 9.3 toka tani 388,294 mwaka 2006 hadi tani 370,566 mwaka 2007 hali hii lilisababisha ulaji wa nyama kupungua kwa wastani wa kilo 11.5 kwa mwaka hadi kilo 10.5 kwa mwaka. Kambi ya Upinzani inataka kujua serikali imechukua hatua gani madhubuti ili kukabiliana na maambukizo ya magonjwa ya wanyama kama vile Homa ya bonde la ufa, mafua ya ndege n.k ili kutoathiri sekta hii muhimu kwa ajili ya ukuaji wa uchumi hapa nchini.

 

8.                   Mheshimiwa Spika, takriban asilimia 99% ya mifugo hapa nchini inamilikiwa na kutunzwa kienyeji. Kwa bahati mbaya mifugo yetu ya asili uzalishaji wao ni mdogo. Kiwango cha kuzaa (calving rate) ni chini ya asilimia 40%; muda wa mzao (calving interval) ni miezi 18 – 24, na hivyo kuzaa ndama 4 – 5 katika uhai wao. Vifo vya ndama ni zaidi ya asilimia 25%. Aidha uzalishaji wa maziwa uko chini ya lita 500 kwa mwaka. Matokeo ya haya yote yamesababisha ukuaji wa National herd kubaki katika kiwango cha asilimia 0.02%.

 

9.                   Mheshimiwa Spika, Pamoja na rasilmali kubwa ya mifugo tuliyonayo, takriban zaidi ya asilimia 63% ya wafugaji wetu bado ni masikini.  Hii ni changamoto kubwa, inatupasa tukae na kutafakari nini la kufanya kuondokana na hali hii.

 

10.               Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2006/07 ukuaji wa Sekta ya Mifugo ulishuka kwa asilimia 1.2, kutoka 5.2% hadi kufikia 4.0%.Kushuka huku kwa asilimia 1.2 si jambo dogo, athari zake katika Sekta kuu ya Kilimo na uchumi wa nchi kwa ujumla ni kubwa.

 

11.               Mheshimiwa Spika, wafugaji wanakabiliwa na tatizo la kuyafikia masoko na kukosekana taarifa za masoko (limited access to market outlets and market information). Kwa kawaida wafugaji nchini mwetu huwa hawazalishi kwa sababu ya kibiashara. Mara nyingi huzalisha kwa ajili ya matumizi ya nyumbani, hutafuta soko pale tu wanapokuwa na ziada. Wanapokosa kuuza hiyo ziada huwa ni sababu ya kupunguza uzalishaji.

 

12.               Mheshimiwa Spika, Serikali kwa muda mrefu haijawekeza ipasavyo katika kukuza masoko, kadhalika upatikanaji wa taarifa za masoko ya mifugo na mazao yake. Hali hii inaathiri kwa kiasi kikubwa juhudi ya kuongeza uzalishaji. Ipo haja basi kwa Serikali kuongeza juhudi za makusudi kuwashajiisha wafugaji kuzalisha zaidi ili kuuza katika masoko. Juhudi hizo zinaweza kuzaa matunda iwapo tu utunzaji wa mifugo, kukuza masoko, upatikanaji wa taarifa za masoko na usindikaji wa mazao ya mifugo utaendelezwa.

 

13.               Mheshimiwa Spika, suala la uwezeshaji kwa wafugaji wadogo wadogo halijapewa kipaumbele cha kutosha kwani hakuna mkakati wa kuhakikisha kuwa wafugaji hawa wanapewa mikopo, mafunzo, wanatafutiwa masoko, miundombinu na nyenzo nyinginezo ili kuweza kuboresha mifugo yao kwa minajili ya kuongeza kipato na tija.

 

 

14.               Mheshimiwa Spika, tatizo jengine kwenye sekta hii muhimu  ni uwezo na utaalamu wa watendaji wa idara husika katika kuratibu na kusimamia sekta hii ndogo maeneo ya vijijini hususani ukosefu wa vitendea kazi, utafiti, uchache wa  watumishi na malipo  madogo kwa watumishi wetu.  Kambi ya Upinzani inamtaka Waziri kutueleza Wizara ina mikakati gani ya kuhakikisha kuwa watumishi hawa wanapatiwa nyenzo na vitendea kazi ili kuweza kuboresha sekta hii kwa manufaa ya Watanzania masikini.

 

15.               Mheshimiwa Spika, kuna tatizo ambalo limekuwa likifukuta hapa nchini katika maeneo mbalimbali, nalo ni migogoro kati ya wakulima na wafugaji. Tatizo hili linakuzwa zaidi na usimamizi mbovu kwenye sekta ya ardhi na ukosefu wa mikakati ya kujenga mahusiano mazuri baina ya wakulima na wafugaji. Kwa mfano, upo uwezekano wa kuzuka migogoro baina ya wakulima na wafugaji katika mkoa wa Pwani na hata maeneo mengine kutokana  na uhaba wa ardhi ambao unatokana na kwamba hivi sasa ardhi inatengwa kwa wawekezaji wa kilimo cha mazao ya miwa na mibono pasipo kuzigatia sheria na mahitaji ya ardhi kwa wakulima na wafungaji wadogo.

 

16.               Mheshimiwa Spika, Kuna taarifa kwamba kiasi kikubwa cha ardhi kimegawiwa kwa makampuni makubwa ya nje hasa katika wilaya za Rufiji, Kisarawe na Bagamoyo. Kambi ya Upinzani inaitaka serikali kuhakikisha kuwa inaandaa sera na mikakati kabambe ya kulinda haki za ardhi za wafugaji wadogo dhidi ya udanganyifu wa wawekezaji wakubwa katika kilimo hasa kilimo cha mazao ya nishati. Vile vile Kambi ya Upinzani inaishauri serikali kurekebisha sheria za ardhi ili uamuzi wa kugawa na kusimamia raslimali za ardhi uwekwe mikononi mwa wananchi kupitia vyombo vyao vya uwakilishi.

 

17.               Mheshimiwa Spika, Kambi ya upinzani inaamini kwamba rushwa, ufisadi katika sekta ya ardhi na hususan migogoro isiyoisha baina ya wakulima na wafugaji vinasababishwa zaidi na udhaifu wa sheria za ardhi ambazo zinatoa mamlaka makubwa kwa watendaji wa serikali kusimamia ardhi pasipo na udhibiti wa kutosha kutoka kwenye vyombo vya uwakilishi wa wananchi. Vile vile serikali inashauriwa kuchukua hatua mara moja pindi viashiria vya migogoro vinapoanza kuonekana ili kuweza kunusuru yasije yakatokea machafuko baina ya Wakulima na Wafugaji na kusababisha umwagaji damu hapa nchini.

 

·        Usindikaji wa Mazao ya Mifugo:

 

18.               Mheshimiwa Spika, usindikaji wa mazao ya mifugo hasa maziwa na nyama unaongeza thamani ya mazao hayo na hivyo mahitaji kwa mlaji huongezeka na hatimae kupanuka uzalishaji.  Kwa bahati mbaya hapa nchini viwanda vingi vya kusindika maziwa vilivyokuwa vinaendeshwa na Serikali vimekufa. Hali hii ilitokana na utaratibu mbaya ulokuwepo kwamba Serikali ndiyo pekee iliyokuwa inasimamia na kuendesha viwanda vya maziwa nchini. Kwa upande mwingine viwanda vya kusindika nyama navyo ni vichache, hali inayopelekea kukwaza biashara ya nyama na bidhaa zitokanazo na nyama nje na ndani ya nchi.

 

19.               Mheshimiwa Spika, ukiangalia takwimu zilizopo kwenye Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa katika mwaka 2007, jedwali namba 60 linalohusiana na idadi ya watu walioajiriwa kwenye sekta ya viwanda, utaona kuwa takwimu zinazoonyesha idadi ya watu walioajiriwa kwenye viwanda vya  kusindika ngozi pamoja na bidhaa za ngozi. Takwimu hizo zinatia mashaka makubwa sana. Kwa mwaka 2003 walikuwepo waajiriwa 68, mwaka 2004 walikuwepo 20, mwaka 2005 walikuwepo 20, mwaka 2006 walikuwepo 20 na hali kadhalika mwaka 2007 walikuwepo waajiriwa 20.

 

 

20.               Mheshimiwa Spika, kwa Takwimu hizi inaonyesha kabisa kuwa Tanzania hainufaiki na ngozi ambazo zinapatikana nchini na viwanda vilivyopo havitoi ajira  ya kutosha kwa watanzania. Kambi ya Upinzani inamtaka Waziri kuelezea watanzania nini maana ya takwimu hizi kama kwa miaka minne mfululizo viwanda vinavyosindika vya ngozi nchini vimeajiri watu 20 tu. Hii haileti maana kwa nchi ambayo ina jumla ya ng’ombe milioni 19.1, mbuzi 13.6 na kondoo 3.5. Hivi ngozi za wanyama hawa huwa zinaenda wapi? Ama tunawafuga Ng’ombe, Mbuzi na Kondoo ambao hawana ngozi?

 

21.               Mheshimiwa Spika, kwenye taarifa hiyo hiyo ya hali ya uchumi wa Taifa ukiangalia viwanda vinavyohusika na utengenezaji wa viatu idadi ya watu ambao wameajiriwa kwenye viwanda hivyo waliongezeka kama ifuatavyo, mwaka 2003 walikuwa waajiriwa 851, mwaka 2004, walikuwa 1,130, mwaka 2005 walikuwa 1,146, mwaka 2006 walikuwa 1,157 na mwaka 2007 walikuwa 1,169. Kwa takwimu hizi ni dhahiri kuwa ngozi ilikuwa inatumika kwa wingi kwa ajili ya utengenezaji wa viatu hivyo na ndio maana sekta hii imekuwa ikitoa ajira ambazo zimekuwa zikiongezeka kila mwaka.  Kambi ya Upinzani inamtaka Waziri aweze kutupatia majibu kuwa je? Ngozi hizi ambazo zimekuwa zikitengeneza viatu kwenye viwanda vyetu zimekuwa zikiagizwa kutoka nje ya nchi au hali ikoje huko?

 

3 .0     MIFUGO NA MAZINGIRA.

 

22.               Mheshimiwa Spika, tatizo la upatikanaji wa maji na malisho limekuwa kwa kiasi kikubwa linaathiri mwenendo mzima wa ufugaji hapa nchini. Kutokana na hali hii wafugaji wanalazimika kuhama kutoka sehemu moja kwenda nyingine kufuata maji na malisho pale yanapopatikana. Kadhalika sehemu kubwa ya nyanda zilizokuwa zinatumika kwa kuchungia mifugo zimekuwa zinavamiwa na kutumika kwa matumizi mengine kama sehemu za Kilimo, hifadhi za wanyama pori, machimbo ya madini n.k. Katika hali kama hii, wafugaji hulazimika kuhama kutafuta maeneo mengine ya kulisha mifugo yao. Kutokana na kuhamahama huko kwa wafugaji, na kwa sababu hakuna utaratibu maalum ulioandaliwa katika uhamaji huo ndiko wakati mwengine kunakopelekea mazingira kuharibiwa.

 

23.               Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaona kwamba njia mahususi ya kupunguza ufugaji wa kuhamahama ni kuongeza maeneo yanayotumika kwa malisho; Wafugaji wapatiwe ardhi ya kutosha na kupewa hati ya kumiliki maeneo hayo; kujenga mabwawa na malambo yanayoweza kuhifadhi kiasi kikubwa cha maji. Aidha majosho ya kutosha yajengwe na yale yaliyoharibika yafanyiwe ukarabati wa kina.

 

·        Wafugaji waliohamishwa Ihefu.

 

24.               Mheshimiwa Spika, tatizo la wafugaji waliohamishwa kwenye bonde la Ihefu, Mbarali Mkoani Mbeya. Unyanyasaji wa Wafugaji uliotokea Ihefu mwezi March, 2006 kwa kuwaondoa bila utaratibu wala mipango mathubuti.  Vitendo walivyofanyiwa wafugaji Ambavyo ni kinyume na Haki za binadamu bado vimeacha makovu mengi. Wananchi wengi waliopoteza mali zao, mifugo, familia na kuumia kisaikolojia.  Tume ya Rais, iliyotumia mamilioni ya fedha za Watanzania iliyoongozwa na Mhe. Jaji Chande hadi leo taarifa yake imewekwa kabatini, na wala Watanzania hawakujulishwa kilichojiri katika ripoti hiyo na wala hatua izilizochukuliwa kwa watendaji waliotekeleza vibaya agizo la Serikali. Kambi ya Upinzani inamtaka Mhe. Waziri atoe Tamko la Serikali kuhusu Taarifa ya Tume/Kamati ya Rais iliyochunguza matukio ya Ihefu ili Watanzania waamini kuwa Serikali yao inawajali.

 

4.0 HALI HALISI YA UVUVI NCHINI.

 

25.               Mheshimiwa Spika, Kiwango cha ukuaji wa shughuli za kiuchumi za uvuvi katika mwaka 2007 kilikua asilimia 4.5 ikilinganishwa na asilimia 5.0 mwaka 2006. Sababu kuu za kushuka kwa ukuaji wa shughuli za uvuvi kulitokana hasa na kuendelea kwa vitendo vya uvuvi haramu, kupungua kwa mahitaji ya samaki na mazao ya samaki nje ya nchi. uharibifu wa mazingira katika mazalia ya samaki ,na matumizi ya zana duni za uvuvi. Mchango wa sekta ya Uvuvi katika pato la Taifa uliendelea kuwa asilimia 1.6 mwaka 2007 kama ilivyokuwa katika miaka ya 2005 na 2006.

 

26.               Mheshimiwa Spika, Katika mwaka 2007 idadi ya wavuvi waliosajiliwa nchini iliongezeka na kufikia 163,037 ikilinganishwa na 156,544 mwaka 2006. Wavuvi hao walivuna samaki wenye uzito wa tani 327,807.5 wakiwa na thamani ya shilingi 292.7 bilioni mwaka 2007 ikilinganishwa na tani 341,109.2 zenye dhamani ya shilingi 285.7 bilioni mwaka 2006.

 

27.               Mheshimiwa Spika, Katika mwaka 2007 mapato yatokanayo na mauzo ya mazao ya uvuvi nje ya nchi yalikuwa shilingi 7,589 milioni ikilinganishwa na shilingi 6,236 milioni mwaka 2006. Kati ya mapato hayo mauzo ya Sangara nje yaliingizia nchi mapato ya shilingi 6,660 milioni mwaka 2007, ikilinganishwa na shilingi 5,491 milioni mwaka 2006;

 

28.               Mheshimiwa Spika ,ukiangalia takwimu hizi utaona ya kuwa Sangara ambao wanatoka ziwa Victoria na Tanganyika ndio pekee ambao wanaongoza kwa mauzo kwa zaidi ya asilimia 87.8%, Kambi ya Upinzani inataka majibu kutoka serikalini ni kwa nini samaki ambao wanapatikana na /au kuvuliwa  Bahari ya Hindi wanachangia kiasi kidogo sana cha mauzo nje ya nchi, ilhali meli nyingi za uvuvi zinaendelea kuvua na kupata vibali kila wanapohitaji ila uvuvi huo hauonekani ukileta faida ya kutosha kwenye mapato.

 

29.                Mheshimiwa Spika, kutokana na jinsi ambavyo Sangara wamekuwa wakiliingizia Taifa fedha nyingi kama ilivyoonekana kwa kipindi cha mwaka jana 2007 ,kuna kila sababu ya kuhakikisha kuwa panawepo mkakati kabambe wa kuvuna Sangara ambao wanapatikana ziwa Tanganyika. kwa kuwa mpaka sasa uvunaji wa sangara waliopo ziwa Tanganyika hawavuliwi kwa wingi pamoja na ukweli kuwa sangara hao ndio chimbuko la sangara waliopo ziwa Victoria. Kuvuliwa kwa sangara waliopo ziwa Tanganyika itaongeza ukuaji wa mauzo ya sangara nje na kuongeza ukuaji wa pato la taifa na wakati huo huo kipato cha wananchi wa mkoa wa Kigoma kitaongezeka mara dufu kutokana na kupanuka kwa shughuli za kiuchumi na pia sekta ya viwanda itaweza kukua kutokana na ujenzi wa viwanda vya samaki kwenye mkoa huo. Aidha hatua hii itapelekea kuimarishwa kwa uwanja wa ndege wa Kigoma ili kuruhusu ndege kubwa za mizigo kuweza kutua na kuruka kwa ajili ya biashara ya minofu ya samaki.

 

30.               Mheshimiwa Spika, kama tulivyosema kwenye hotuba yetu ya Bajeti Mbadala kuhusiana na vyanzo vya mapato kutokana na Uvuvi wa Bahari Kuu naomba kusisitza tena yale ambayo yalisemwa na kuitaka Wizara husika itilie maanani hoja zetu hizi ili kuweza kuongeza mapato ya Serikali na kukuza uchumi wa taifa letu.

 

31.               Mheshiwa Spika, Uvuvi katika Bahari Kuu ni moja ya maeneo ambayo kama Serikali ingelikuwa makini na kuchukua maamuzi ambayo Kambi ya Upinzani ilipendekeza, mapato yatokanayo na uvuvi yangeliongezeka marudufu kutokana na kusimamia vyema shughuli za uvuvi . Maeneo yenyewe ni kama haya yafuatayo:-

 

                    i.            Kuongeza ada ya leseni kwa meli za nje zinazovua katika bahari kuu hadi kufikia USD 50, 000, kutoka inayotozwa sasa ambayo ni USD18, 000 kwa mwaka. Kulingana na takwimu zilizopo ni kuwa kuna meli 140  za nje zilizopatiwa leseni za uvuvi katika bahari kuu ya Tanzania.  Kwa maoni haya mapato ya yangelifikia Tshs 9.5bn. ambayo Serikali ingelikusanya.

                   ii.            Kuongeza tozo la mrahaba wa mauzo la asilimia 10 katika bidhaa za Samaki zinazovuliwa katika Bahari Kuu. Kila meli kwa mwezi inavua wastani wa tani 2000 za samaki, kwa makisio ya chini sana. Bei ya soko kwa kilo ya samaki ni USD2.5 . Kwa  tozo hilo Mapato yangelifikia shs. 370 bn. ambayo Serikali ingelikusanya.

                  iii.            Katika kuhakikisha kuwa Sekta Uvuvi inaleta mabadiliko ya kiuchumi kwa nchi na wananchi kwa ujumla, inashauriwa bandari za Mtwara, Dar es Salaam,Tanga  na Zanzibar zitenge maeneo ya  bandari za  samaki (Fish Ports and Fish Processing plants) ili  meli zote za uvuvi  wa bahari kuu zilazimike   kununua mahitaji yao yote ya mafuta ,maji,chumvi na vyakula wanapo kuja kukaguliwa kwa ajili ya kukusanya mapato. Kwa uamuzi huu mapato yanakisiwa kuwa Tshs.3bn. ambayo Serikali ingelikusanya.

 

                 iv.            Uvuvi katika ziwa Victoria na ziwa Tanganyika, haujadhibitiwa vizuri. Hivi sasa kuna uvunaji haramu wa samaki wastani wa Tani 36,000 kwa mwaka. Kama uvunaji huu haramu ukidhibitiwa Serikali inaweza kujipatia kiasi cha shilingi 45 bn kwa mwaka. Kutokana na uvunaji huu haramu katika maziwa hayo kunasababisha viwanda vyetu vinakosa mali ghafi ya kutosha kuzalisha minofu. Tunaitaka Serikali kuchukua hatua za  dharura kuikabili hali hii  kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na TRA ili kuongeza mapato na  ajira. Zoezi hili litaongeza wingi wa samaki hivyo viwanda vya samaki vitaongeza uzalishaji na hatimae kodi itaongezeka

 

 

32.               Mhe. Spika, Maoni haya Kambi ya Upinzani sio tu yamepanua wigo wa kodi, lakini pia kwa hatua hizo tutakuwa tumedhibiti uvunaji endelevu wa raslimali zetu ambapo sasa hazivunwi kikamilifu.

 

   5.0      HALI HALISI YA WAVUVI WADOGO WADOGO.

 

33.               Mheshimiwa Spika , hali ya wavuvi wadogowadogo hapa nchini kwetu ni ya kusikitisha sana kwani hakuna juhudi zozote za kina zinazochukuliwa na serikali kuhakikisha kuwa wavuvi hawa wanasaidiwa kupata mitaji ya kuweza kujiendeleza na kupata nyezo na vifaa vya kisasa kwa ajili ya kukuza shughuli za uvuvji hapa nchini.

 

34.               Mheshimiwa Spika, Ukiangalia kwa kina utaona kuwa badala ya Serikali kuwawezesha wavuvi hawa wadogo wadogo wanachofanya ni kuwawekea vikwazo vinavyopelekea washindwe kufanya kazi zao kwa ufanisi. Pia yapo malalamiko mengi kutoka kwenye jamii za wavuvi wadogowadogo kuhusu vitendo vya unyanyasaji wanavyofanyiwa na baadhi ya maafisa wa idara ya uvuvi kwa visingizio vya kuthibiti uvuvi haramu. Kambi ya upinzani inaishauri serikali kuimarisha mikakati yake ya kudhibiti uvuvi haramu na kufanya hivyo kwa mujibu wa kanuni za utawala bora na haki za binadamu.

 

35.               Mheshimiwa  Spika, pamoja na ukweli kuwa wavuvi wadogo wadogo huchangia kwa kiasi kikubwa sana kwenye mapato ya serikali lakini bado wananyanyasika sana. Mfano halisi ni barua iliyoandikwa na Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi Makao Makuu yenye kumbukumbu namba KA/594/01/87 ya tarehe 13 Mei 2008 inayowaagiza kwa Wakurugenzi Halmashauri kote nchini Tanzania Bara na ninanukuu“waraka huu unawapa uwezo maafisa walio chini yenu na vyombo vya dola kuthibiti na kuhakikisha kuwa matumizi ya nyavu za aina ya mtando na ringnet, juya au juya la kojani au kokoro na uvuvi wa kuzamia kwa kutumia mitungi ya gesi aina ya oxygen ,viatu vya kuogelea na au miwani ya kiupiga mbizi yanapigwa maraufuku kuanzia sasa”  Kambi ya Upinzani inamtaka Waziri alieleze Bunge hili na wananchi wote kwa ujumla ni jinsi gani vifaa hivyo vinahusika na kuharibu mazingira. Kadhalika tunamtaka Waziri achukue hatua ya kuifuta barua hiyo ya Mkurugenzi wake kwani kwa kiasi kikubwa itaathiri  kipato chao kutokana na shughuli zao za uvuvi. Aidha hatua hiyo itapunguza mapato ya Halimashauri za wilaya ambazo shughuli za uvuvi zinafanyika kutokana na kukosa ama kupungua kwa mapato yatokanayo na shughuli za uvuvi, kwani wavuvi hawa wamekuwa wakilipa mpaka zaidi ya shilingi 100,000 kwa siku kama ushuru wa mauzo ambapo wanakatwa asilimia 5 ya mauzo ya samaki.

 

36.               Mheshimiwa Spika ,Kambi ya Upinzani inataka maelezo ya kina kutoka serikalini ni kwa nini serikali inawawekea vikwazo wavuvi wadogowadogo na huku ikiwapa uhuru mkubwa wavuvi wa bahari kuu wenye meli kubwa na ambao hawalinufaishi taifa hili;

 

a.       Mheshimiwa Spika, hali ya usalama wa wavuvi wetu wawapo kwenye shughuli zao ni mdogo sana kwani zimekuwa zikitolewa taarifa mara kwa mara kuwa kuna wavamizi wanawavamia na kuwanyanganya vifaa vyao na hata wakati mwingine wavuvi hawa hupoteza maisha yao. 

b.      Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kuhakikisha kuwa panawepo mpango maalumu na shirikishi wa kuhakikisha kuwa ulinzi unaimarishwa na haswa katika maeneo yale ambayo vitendo hivi vya kiharamia vimekuwa vikitokea mara kwa mara ili kuhakikisha kuwa tunayalinda maisha ya watanzania wenzetu wawapo kwenye shughuli zao za kujitafutia riziki.

 

37.               Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani imesikitishwa na kustushwa sana na taarifa iliyopo kwenye Randama ya mpango na bajeti ya Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi kwa mwaka 2008/2009 (kifungu 1003 Sera na Mipango) iliyowasilishwa kwenye kikao cha kamati ya kudumu ya Bunge kuwa miongoni mwa kazi za kipindi hiki cha bajeti ya mwaka 2008/2009 nanukuu “Kupitia sera ya Taifa ya Uvuvi (1997) na kuandaa mkakati wa kutekeleza sera hiyo”. Hivi tujiulize kwa kipindi cha zaidi ya miaka kumi inawezekana vipi serikali haikuwa na mkakati wa kuitekeleza Sera ya Uvuvi? Huu si uzembe? na kuna kila sababu ya wahusika waliofanya uzembe huo wachukuliwe hatua mara moja kwani wanarudisha nyuma juhudi za kukuza uchumi wa Taifa letu hili, Tunamtaka Waziri atupe majibu ya kina juu ya hili.

38.               Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inahoji hivi ni kweli kwa zaidi ya miaka 10 sera hiyo haijawahi kutekelezwa? Ama walikuwa wanafanya kazi kwa kutumia muongozo gani kama hakuna mkakati wa kutekeleza sera ambayo ndio muongozo na dira ya utekelezaji wa shughuli za Uvuvi hapa nchini? Kama sera inasema kuwa “the overall goal of the National Fisheries Policy is to promote conservation, development and sustainable management of the fisheries Resources for the benefit of present and future generations” .Kambi ya Upinzani inamtaka waziri kuelieza Bunge na wananchi je lengo hili limeweza kufikiwa kwa kiasi gani kama hakukuwa na mkakati wa kutekeleza sera husika? Na ni vigezo gani vinatumika kupima utekelezaji wa sera hii kama mkakati haukuwepo tangu miaka kumi iliyopita?

 

                 HITIMISHO.

 

39.               Mheshimiwa Spika, nichukuwe nafasi hii kutoa shukurani za dhati kwa wake zangu, Bi Asha Mohammed Haji na Mhe. Mkiwa Adam Kimwanga, watoto wetu na familia yangu kwa ujumla kwa kunipa moyo na kuniunga mkono kwa muda wote, nikifanya shughuli zangu za kuwakilisha wananchi katika Bunge lako Tukufu.

 

40.               Naamini kabisa kuwa Waziri ataweza kutupatia majibu ya kina juu ya mambo yote ambayo Kambi ya Upinzani imeyauliza au kutaka ufafanuzi juu ya mambo kadhaa kwa masilahi ya Taifa.

 

41.               Mheshimiwa Spika,  baada ya kusema hayo na kwa niaba ya Kambi ya Upinzani naomba kuwasilisha.

 

                          ……………………………

Mwadini Abbas Jecha (Mb),

MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI.

WIZARA YA MAENDELEO YA MIFUGO NA UVUVI

31 JULY 2008.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s