IMF inachochea ufisadi -Prof. Lipumba

Na Kizitto Noya

 

MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF) Profesa Ibrahim Lipumba amelituhumu Shirika la Fedha Duniani (IMF) kwamba linachochea na kuendekeza rushwa na ufisadi nchini.

 

Profesa Lipumba alitoa shutuma hizo nzito upitia barua yake aliyomwandikia Mkurugenzi Mtendaji wa IMF, Dominique Strauss-Khan.

 

Katika barua hiyo ambayo jana aliamua kuigawa kwa vyombo vya habari, Profesa Lipumba alidai amebaini kwmba IMF ambayo imekuwa ikiheshimika kwa miaka mingi, ina mkono katika matukio ya ufisadi yanayoendelea hapa nchini.

 

Alisema amebaini hilo kutokana na shirika hilo kufumbia macho matukio kadhaa ya ufisadi nchini na kitendo chake cha kumpongeza Rais Jakaya Kikwete kwa hatua ya kuwapa muda wa kurejesha fedha mafisadi wa EPA badala ya kumponda.

 

“Sikusoma popote zaidi kujiridhisha kwamba ulisema, niliamini kwamba taarifa iliyotolewa na gazeti la serikali hapa nchini, The Daily News kuhusu mazungumzo yako na Rais Kikwete ni sahihi. Kauli yako inachochea rushwa na kuendekeza ufisadi Tanzania,” alisema Profesa Lipumba katika barua hiyo ya Septemba 26, mwaka huu yenye kumbukumbu namba CUF/AK/ DSM/MKT/001/IMF/2008.

 

Septemba mosi mwaka huu, gazeti la Daily News lilimkariri Mkurugenzi Mtendaji wa IMF akimsifia rais Jakaya Kikwete kwa hatua alizochukua dhidi ya watuhumiwa wa ufisadi wa EPA.

 

Kwa mujibu wa gazeti hilo, katika mkutano wao uliofanyika kwenye hoteli ya Omni Shoreham, nchini Marekani, Mkurugenzi huyo wa IMF alisema “Tumeridhirika sana na kukupongeza jinsi ulivyoshughulikia suala la EPA. Suala hilo linaweza kutokea popote duniani lakini cha msingi ni jinsi ulivyolishughulikia. Na umelishughulikia vizuri kwa umahiri na utalaam wa hali ya juu. IMF sasa imefunga suala la EPA,”

 

Profesa Lipumba alisema kauli hiyo ya IMF, inachochea rushwa kwani ni ukweli usiofichika kwamba serikali imeshindwa kushughulikia suala hilo kwa umahiri wala utaalam wa hali ya juu kama mkurugenzi huyo anavyodai.

 

Akifafanua alisema: “Serikali haikuwa wazi kuueleza umma jinsi fedha hizo zilivyochotwa, watuhumiwa bado hawajulikani kwa majina na makampuni hayajafikishwa mahakamani,”

 

Kwa mujibu wa Profesa Lipumba kitendo cha Rais Kikwete kutaka watuhumiwa wa ufisadi wa EPA warejeshe fedha, kinaleta shaka kuwa hatawafikisha mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili, kitendo ambacho ni kinyume na utawala bora na sheria.

 

Alisema rais Kikwete amewasamehe watuhumiwa wa EPA na kauli yake haionyeshi nia thabiti ya serikali kuwafikisha mahakamani hivyo kumsifu kwamba amelishughulikia suala hilo kwa umahiri sio sahihi.

 

Aliitaka IMF kuongeza umakini katika kupitia hali ya uchumi wa Tanzania katika vikao vyake vijavyo na kuishikiza serikali kusimamia mapendekezo ya ripoti ya awali iliyokagua akaunti ya EPA mwaka 2006 iliyotaka nchi iache kuendelea kulipa madeni hayo kwa kuwa yamepitwa na wakati.

 

Katika hatua nyingine Profesa Lipumba jana ameeleza kuwa msimamo wa chama chake kuandamana kwa lengo la kuishinikiza serikali itaje majina ya watuhumiwa wa EPA na kuwafikisha mahakamani, uko palepale.

 

Aliwaambia waandishi wa habari kuwa maandamano hayo yamepangwa kufanyika Oktoba 6 mwaka huu kuanzia Buguruni kupitia barabara ya Uhuru hadi viwanja vya Mnazi Mmoja ambako viongozi wakuu wa CUF watahutubia.

 

Profesa Lipumba alibainisha kuwa ingawa polisi wameshajulishwa kuhusu maandamano hayo, baadhi ya watendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala wameanza kuyawekea mizengwe kwa kuzuia viwanja hivyo.

 

Alisema baada ya CUF kumwandikia barua mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala kumjulisha juu ya maandamano hayo kuishi katika viwanja vya Mnazi Mmoja, aliwajibu kwa barua kwamba viwanja hivyo haviruhusiwi kwa shughuli za kisiasa.

Chanzo: http://www.mwananchi.co.tz/newsrids.asp?id=7321

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s