Msimamo wa Wawakilishi wa CUF kuhusu mafuta ya Zanzibar

Tarehe 18 Septemba, 2008, Wizara ya Maji, Ardhi, Nishati na Mazingira ya Zanzibar iliitisha semina kwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kujadili ripoti ya Mshauri Muelekezi, David Reading, aliyeteuliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano na ya Zanzibar, kushauri namna bora ya kugawana gharama na mapato ya utafutaji na uchimbaji wa mafuta katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, huku ikijuilikana wazi kwamba taarifa zilizopo zinaonesha kwa hakika kuwa nishati hiyo inapatikana kwa wingi katika mwambao wa visiwa vya Zanzibar tu. Ifuatayo ni michango ya wajumbe wa CUF katika semina hiyo baada ya Bwana Reading kumaliza kuwasilisha ripoti yake.

SAID ALI MBAROUK, CUF GANDO

SAID ALI MBAROUK, CUF GANDO

Said Ali Mbarouk (CUF, Gando): Mhe. Mwenyekiti, naomba nianze kwa swali moja halafu nitoe mchango wangu mfupi. Swali langu liko katika maelezo yake (Mshauri Muelekezi, Bwana David Reading) au labda tuseme utafiti wake, kwamba uwezekano wa kugundua mafuta Zanzibar ni mdogo. Sasa mimi naomba ni-quote (ninukuu) kipande kidogo cha maelezo halafu yeye ataweza kutufafanulia nini maana yake maelezo haya na ikiwa yanalingana na maelezo yake au la.

Maelezo yenyewe, Mhe. Mwenyekiti, ni haya; naomba kunukuu (anasoma kipande cha taarifa ya kampuni ya Antrim Energy ambacho kinaeleza uwezekano wa kuwepo akiba kubwa ya mafuta katika eneo la Mashariki la Bahari ya Zanzibar ifikiayo matangi bilioni 7 na ambayo, kwa hivyo, yanaweza kuwa ya kibiashara, na sio kiwango kidogo ambacho Bwana Reading aliwaeleza wajumbe wa semina hiyo)

Taarifa hii haimo katika document yake (mshauri muelekezi), isipokuwa source yake ni watu wengine waliofanya utafiti Zanzibar na wakagundua hii hali. Swali langu ni je, maelezo hayo niliyoyatoa, yanapingana vipi na kauli yake kwamba uwezekano wa kugundua mafuta Zanzibar ni mdogo sana na je, authenticity, uhakika wa maelezo haya, ukoje? Hayo ndiyo maswali yangu.

Mhe. Mwenyekiti, baada ya maswali hayo, sasa mimi ushauri ninaoweza kusaidia katika suala hili ni kwamba, kwa kuzingatia hali halisi ya kiuchumi ya watu wetu, suala hili linahitaji kuzingatiwa kwa mapana sana na, kwa hivyo, tulenge kuona kuwa maslahi ya Zanzibar yamezingatiwa sana. Na katika kuangalia hilo, basi ushauri wangu ni katika masuala matatu manne yafuatayo:

i. TPDC (Shirika la Maendeleo ya Mafuta la Tanzania), chombo ambacho kilianzishwa mwaka 1969 kikiwa si chombo cha Muungano na mpaka hivi leo hakijawa chombo cha Muungano, lisijishugulishe kabisa na masuala ya mafuta Zanzibar. Badala yake, Zanzibar nayo ianzishe kampuni yake iitwe Zanzibar Petroleum Development Corporation (ZPDC). Hii (ZPDC) ijishughulishe na utoaji wa leseni na usajili wa makampuni na shughuli nzima ya utafutaji na uchimbaji wa mafuta kwa Zanzibar. Utaratibu utafanywa ionekane kwamba kampuni yetu ZPDC inashirikiana na TPDC katika ama masuala ya kimataifa au masuala mengine, lakini bado Zanzibar iwe na kamandi ya kutosha katika masuala mazima ya mafuta.

ii. Suala jengine Mhe. Mwenyekiti, ni kuhusu mambo yanayohusiana na kodi. Kodi ilipwe moja kwa moja katika vyombo vinavyohusika na ukusanyaji kodi kwa Zanzibar. Pia masuala ya royalty (mrahaba) na mengine, nayo yakusanywe na kuingia moja kwa moja kwenye Hazina ya Zanzibar. Mhe. Mwenyekiti, suala hili ni muhimu sana kwa sababu kama alivyosema mwenyewe (Mshauri Muelekezi), kwamba uchimbaji wa mafuta una athari nyingi za kimazingira, na kijamii ambazo hatimaye Hazina ya Zanzibar italazimika kushughulikia mambo hayo. Kwa hivyo, tuone kwamba kwa mambo haya, Hazina inapata fedha za kutosha kuyashughulikia. Na jambo hili si geni, kwa sababu Statistics (Takwimu), kwa mfano, ni jambo la Muungano lakini bado Idara yetu ya Statistics ya Zanzibar ina uwezo wa kufanya shughuli zake kwa upana na kwa undani bila ya kuingiliwa na ile Bureau of Statistics ya Muungano.

iii. Mwisho Mhe. Mwenyekiti, ningetahadharisha mambo mawili: kwamba masuala haya ni muhimu sana kuyaangalia katika upeo mkubwa. Pamoja na Mshauri Muelekezi kutwambia kwamba tunaweza sisi tusipate chochote, sawa! Sisi hatukuzoea kupata: almasi inachimbwa, dhahabu inachimbwa, tanzanite inachimbwa na hatupati wala hatulalamiki. Na gesi saa hizi inachimbwa, watu wanatumia, sisi hatupati kitu, wala hatulalamiki. Kwa hivyo hivi kukosakosa sisi tushazowea sana, bwana muelekezi aambiwe kwamba si tatizo ikiwa sisi hatutapa kitu, tushazowea kukosa. Aambiwe. Lakini mheshimiwa mgeni rasmi (Waziri Kiongozi wa SMZ, Shamsi Vuai Nahodha) kasema kwamba mambo haya ya mafuta katika Afrika yamezua matatizo mengi. Hivi leo kuna Oil War (Vita vya Mafuta), Nigeria, kuna Oil War, Sudan. Tunaomba sana busara itumike, musije mukawafikisha Wazanzibari wakaanzisha Oil War. Tunawaomba sana.

Nakushukuru Mwenyekiti.

RASHID SEIF SULEIMAN, CUF ZIWANI

RASHID SEIF SULEIMAN, CUF ZIWANI

Rashid Seif Suleiman (CUF, Ziwani): Mhe. Mwenyekiti, kuhusu suala hili, sina tatizo na huu ushauri wa kushauri namna gani ita-deal na makampuni, kwa sababu hayo ni mambo ya kimataifa. Kwa hivyo, hayo yatashughulikiwa na wataalamu wa kiuchumi, baada ya kupata ripoti hiyo watalinganisha na nchi nyengine.

Suala lililonishitua mimi, katika mwanzo wa maelezo yake, Mshauri Muelekezi, pale aliposema kwamba hawakuruhusiwa kuingilia chochote katika suala la Katiba ya Jamhuri ya Muungano. Kwa sababu, Mhe. Mwenyekiti, sisi tuna nchi mbili, na ndivyo tulivyoungana, lakini kumetokezea matatizo mengi ndani ya Muungano na karibu dunia nzima inayajua. Kwa sababu kama Muungano wetu ungelikuwa ni mzuri, tungepata na marafiki zetu wakaunganisha, lakini tangu siye tulipoanza miaka 40 iliyopita, hatukupata mwengine yeyote wa kutuunganisha nasi.

Sasa nafikiri washauri waelekezi walipunjwa kuambiwa wasiangalie huko, kwa hivyo hadidu rejea yao haikuwafanya watizame nini matatizo ya Muungano – ni kipi kilichopo katika matatizo ya Muungano. Kwa hivyo, katika hawa washauri wenzake aliotutajia, ilikuwa awepo mmoja wa kisiasa wa kutizama ndani ya Muungano muna matatizo gani kabla hatujagawana haya mafuta na utafutaji wake. Kwa hivyo, kungelikuwa na political consultant wa Muungano. Hiyo ingelisaidia kidogo katika hilo. Na kwa hapa, kabla sjaondoka pointi hii ningependa kumuuliza huyu consultant, kama kuna makontrakta wawili, mmoja akajenga foundation, wewe wa pili unapoambiwa ukajenge jengo, je waambiwa ujenge jengo lako bila ya kuangalia foundation ilivyojengwa? Au utataka kujua foundation imejengwa vipi ili (kufahamu) kuwa jengo utakalojenga liwe lita-support ghorofa mbili, tatu, kumi au kumi na tano?

Kwa hivyo, unapotueleza sisi kwamba hamuna constitutional considerations katika mambo haya, tunayachukua kama yalivyo, tunaona kuwa kuna kasoro sana, kama ulivyosema mwenyewe: “within the current constitution of Tanzania lakini we are telling you that the constitution is full of problems. So if we are considering it in the present current situation, we will fail. Hiyo ya kwanza.

Lakini ya pili, Mhe. Mwenyekiti, ni kwamba kitabu hichi tulichopewa, Petroleum Exploration and Production Act 1998, kulifanywa makusudi kabisa Kifungu cha 3 kipo juu hapa: “No right to search for or find any mineral as defined in Section C of the Mineral Act of 1978 shall be granted or exercised under this Act.” Sasa kulizuiwa kabisa, kwamba Muungano huu maadini yote hayamo.

Kwa hivyo, mimi narudia kusema aliyoyasema Mhe. Said Ali Mbarouk, ikiwa siye hatuna hayo mafuta, basi siye tuko tayari kuchukua hiyo risk ya kuwa tukose, lakini yetu yawe yetu yasiwe ya wengine. Siye tuko tayari kuchukua hiyo risk, kwa sababu ndivyo tulivyoumbiwa – lazima kuna kitu kitatupa faida: kama si haya mafuta, ni kitu chengine.

Juzi imetolewa ripoti Mhe. Mwenyekiti, maadini yaliyoko Tanzania hayajawahi kugunduliwa katika Bara lote la Afrika in terms of quality, in terms quantity and in terms of samples. Sasa leo Muungano huu ni muungano gani? Kwa nini maadini yote hayo yawe ya upande mmoja, lakini mafuta tu ndiyo yawe ya pande mbili? Haiwezekani! Siye tunasema hapa full stop.

Tatizo ni kwamba consultant hakupewa information ya kutosha na kazuiwa, kawekewa kitanzi. Si kosa lake. It’s not your mistake; it’s the authority’s mistake. Hilo la pili.

La tatu, hata misguiding inatokea. Bahati mbaya siye tumepewa muda mdogo, lakini mimi nimetazama humu kwenye ile ripoti ya Antrim, imeandikwa kuwa TPDC ni kitengo cha Muungano. Iko wapi TPDC (kwenye Mambo ya Muungano?), lakini kwenye ripoti imeandikwa. Kwa hivyo kuna mambo mengi, kama tutayapitia, yametajwa kuwa ni ya Muungano wala si ya Muungano. Na ile lugha ilitomika vile vile katika kurekebisha TPDC, hata kama tungekuwa twataka (hilo la TPDC na mafuta kuwa jambo la Muungano, tuseme), lakini haiwezekani to employ, to change to nini… Kitu kama hichi ambacho si cha Muungano, lazima utumie neno lenye uzito unaofaa – restructuring. Sisi tunasema, kama mafuta yapo ni yetu, kama hayapo basi. Tunasamehe!

Mwisho, Mhe. Mwenyekiti, mimi nasema hivi: suala hili la mafuta kwanza lirejeshwe katika hali ya kisiasa – lijadiliwe katika hali ya kisiasa kwanza (kujuwa) je, watu wako tayari? Kwa sababu tangu Muungano ulipofanywa mwaka 1964, mpaka likaja likaingizwa katika katiba 1980, bila ya kujali zile Articles of Union zilizounganisha.

Tulisikia zamani kulikuwa hadithi za Juha na Abunuwas, (Juha) akilima viazi, avuna mboga, yule (Abunuwas) achukuwa viazi. Basi na siye tushakuwa majuha? Mhe. Mwenyekiti, hatukubali. Suala hili hatukubali na wananchi wote hawakubali. Miye najivua mbele ya Mwenyezi Mungu, suala hili sikubali hata siku moja na niko tayari vyoyote itakavyokuwa; (lakini siko tayari) kusikia kuwa suala la mafuta linapelekwa kwenye Muungano lakini maadini yote ni yao wao.

Na hapa pana ujanja mmoja, Mhe. Mwenyekiti, hapana Muungano wa kweli, kwa sababu Tanganyika ndiyo iliyofanywa Tanzania, Zanzibar haina chake sasa. Kwa hivyo Muungano huu ndio umepelekea Tanganyika kuitwa Tanzania…..

Ahsante sana, Mhe. Mwenyekiti.

ZAKIA OMAR JUMA, CUF VITI MAALUM

ZAKIA OMAR JUMA, CUF NAFASI MAALUM

Zakia Omar Juma (CUF, Nafasi Maalum): Ahsante sana, Mhe. Mwenyekiti, kunipa nami nafasi niweze kutoa mawazo yangu kuhusiana na suala hili muhimu lililopo mbele yetu. Awali ya yote, napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu kujaalia hayawi hayawi leo yamekuwa. Lakini pamoja na kuwa kwake, mimi nataka nitangulize masikitiko yangu – kwa dhati kabisa nasema ni masikitiko – kwamba suala kama hili tumekuja kuletewa ma-documents haya, mengi tu, na yote ni muhimu yanahitaji kupitiwa, lakini sidhani kama kuna mwenzangu yeyote amepata muda, wasaa, wa kutosha kupitia ili aweze kuona hasa kilichomo humu ndani. Na huenda hii – sijui ni makusudi, labda niseme, au kutaka tufanye tu haraka haraka – lakini nasema kwamba mara zote tunaambiwa haraka haina baraka. Lakini pamoja na hilo, Mhe. Mwenyekiti, tutajitahidi twende katika lengo kuu si la kwenye makaratasi, bali lile lililomo ndani ya vifua vyetu, ndani ya vifua vya Wazanzibari wote.

Mhe. Mwenyekiti, mimi kwanza nataka nitangulize kwa kuuliza swali, maana yake mwenzangu alokaa kitako alishasema kabisa kwamba Muelekezi alikatazwa kabisa kuangalia masuala ya katiba. Sasa hili linaonesha jinsi gani upande huo wa pili – nami sitaki niite Tanzania Bara kwa sababu tutakuwa tunawa-confuse hawa wenzetu, hususan ambao si Watanzania, lakini nitasema “Tanganyika” na naomba munistahmilie – upande wa Tanganyika, sioni kama una nia njema na Zanzibar. Na kadiri ya uelewa wangu na umri wangu nilionao, kila panapogusa kuwa na maslahi ya Zanzibar, hasa kiuchumi, basi Katiba zinaonekana – hasa ya Jamhuri au upande huu ambo unajihisi kwamba una status, una mamlaka – ndio unakuwa wa mwanzo kutusemea au kutuzuilia zile nafasi za riziki.

Mhe. Mwenyekiti, nasema hivyo kwa sababu, kwanza, hili suala zima la huyu mshauri muelekezi kuzuiliwa kuangalia Katiba ni moja ya yanayoashiria ukosefu wa nia njema dhidi ya Zanzibar. Pili, nashangaa (kazi alizopewa mshauri) – na simshangai mshauri kwa kuwa yeye amekuja kwa ajili ya kazi na kazi zake ni hizi kama zilivyoelezwa, moja ni ugavi baina ya kampuni na serikali ya Zanzibar na pili ni ugavi baina ya Zanzibar na Serikali ya Tanganyika, the so-called Muungano. Mimi sikubaliani na hii kazi ya pili, ya kufanya ugawaji baina ya Serikali ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano, ambayo ni Tanganyika. Hii sikubaliani nayo, na sikubaliani nayo kwa sababu – kama wenzangu walivyotangulia kuzungumza na wengi tunazungumza hivyo – kuna maadini mpaka mengine hayajaguswa kama inavyoelezwa hapa, na katika Bara la Afrika imepigiwa mfano na nashangaa bado nchi hiyo inaambiwa ni katika nchi masikini, lakini hapana mahala popote ambapo Zanzibar imefikiriwa pamoja na Muungano ambao una miaka 44.

Mhe. Mwenyekiti, wenzetu hivi sasa wanatumia pesa ya gesi ambayo imevunwa hapa karibuni, nafikiri kuanzia 2003 kama sikosei – na nataasaf kama nimekosea, mtanisamehe na niko tayari kukosolewa – lakini sijaona serikali hiyo inayosema ya Muungano (kutaka) kuwe na mshauri; akatafutwa mshauri muelekezi wa kuona jinsi gani gesi hiyo ambayo na Zanzibar inafaidika kwa shares yoyote ambayo wangeliamua kufanya.

Lakini leo mafuta ambayo tunaambiwa huenda hayapo, ndiyo tunakuja kuletewa muelekezi ambaye na Serikali ya Jamhuri nayo inatarajiwa kupata chochote. Hili si haki na si hapa duniani tu lakini hata huko tunakokwenda. Na kama mwenzangu alivyosema, nami hili silitilii baraka. Baraka yangu inaishia tu katika uelekezi baina ya Serikali ya Zanzibar na hayo makampuni ambayo yatachimba. Inaishia hapo, si vyengine. Vyenginevyo na sisi tupate shares za hayo madini yaliyoko upande wa pili ikiwa kweli tunao Muungano na tuna nia njia na Muungano huo.

Mhe. Mwenyekiti, suala la mafuta si suala la Muungano, kwanza. Na katika masuala haya, Articles of Union ni International Agreement ambayo kiilivyo Mkataba huu ni mkubwa kuliko hiyo Katiba ya Jamhuri ambayo imeambiwa isitiwe mkono au katiba nyengine yoyote katika nchi husika kwa ule Mkataba wake. Kwa hivyo, ninaamini kabisa ingelikuwa ni vyema ukaangaliwa ule Mkataba – ambao bado unawekwa siri, sijui kwa sababu zipi – akapewa huyo mshauri, akajuwa kwamba hayo mambo yenyewe yakoje katika suala hili, ili akaona kazi yake inarahisika vipi. Kama mfano ambao Mhe. Rashid ameutoa, huwezi kwenda mahala pana foundation imejengwa ya nyumba pengine very simple, ukaambiwa ujenge sky scraper. Huo usalama utakuweko wapi?

Sasa, kwa kweli Mhe. Mwenyekiti, mimi kwanza napenda mshauri angefahamishwa kwamba katika suala hili la nchi mbili, Zanzibar kama nchi na Tanganyika tumeungana na Muungano hivyo ndivyo unavyoitwa – Muungano wa Tanganyika na Zanzibar – haukubadilishwa; na Mkataba kama watataka kuuleta uko hivyo hivyo. Na mambo (ya kwenye Mkataba huo) ni 11 na napenda niyasome kwa faida ya muelekezi wetu, nitayasoma kwa Kiingereza. (Hapa anasoma Kifungu cha IV cha Mkataba wa Muungano. Tembelea https://hakinaumma.wordpress.com/2008/09/29/whither-zanzibar-appendix-the-article-of-union-between-the-republic-of-tanganyika-and-the-peoples-republic-of-zanzibar/).

Sasa hapa hakuna suala la madini wala hakuna suala la mafuta. Kwa hivyo, kadiri ya mambo yetu yote tunayofanya – na muelekezi wetu atuelekeze vizuri – ni mgawanyo baina ya Serikali ya Zanzibar na kampuni tu, sio Serikali ya Jamhuri ya Muungano. Hawahusiki. Kama ambavyo wametaka katiba yao isiguswe; basi isiguswe, sawa, lakini na wao hawamo kwenye suala la mafuta. Na hii ni yangu binafsi lakini na watu wetu wote tunasimamia hapo.

Mhe. Mwenyekiti, miye nilikuwa naomba sana, kama wenzangu walivyotangulia kusema, kwamba suala la Muungano bado lina kero nyingi na kadiri siku zinavyokwenda bado mambo yanazidi na kadiri linavyonyamaziwa kimya, mambo yanaongezeka. Sasa katika masuala muhimu kama haya ya kiuchumi, serikali yetu ifanye moja kwa moja kwa mujibu wa Mkataba kwamba kuna mambo si ya Muungano, hayamo kwenye mkataba, basi hatuna haja ya kuvuuka maji kwenda kutafuta ushauri wa mtu yeyote. Tufanye wenyewe hapa kwa mujibu wa Mkataba kama ulivyo. Vyenginevyo, tukae kitako tuyajadili mambo ambayo yanahusiana na Muungano wetu, ikiwa tunautaka, kwa sababu Mhe. Marehemu Baba wa Taifa (Mwalimu Julius Nyerere) aliulizwa kuhusu suala hili la kuwepo au kutokuwepo kwa Muungano, na akasema kwamba pahali popote penye Mungano lazima kuwe na washiriki zaidi ya mmoja.

Na Mwalimu alisema hayo alipohojiwa na gazeti la Observer la Uingereza tarehe 20 Mwezi wa Nne, 1968 na alisema kwamba – nitasema kwa Kiingereza halafu nitafasiri: “If the mass of people of Zanzibar should, without external manipulation, and for some reasons of their own, decide that the Union was predjucial to their existence, I will not bomb them into submission. The Union will have ceased to exist when the consent of its constituent members was withdrawn.” By Nyerere, London Observer, 1968. Yaani Muungano wa Tanganyika na Zanzibar hautokuwepo kama wale walioungana watatoweka au watakuwa hawapo. Sasa tuna mashaka na huu Muungano kwa sababu Tanganyika inafanywa haipo; na ikiwa haipo maana yake – wakati sisi tuliungana na Tanganyika – kwa hivyo inaonekana na huo Muungano nao haupo.

Mhe. Mwenyekiti, bado mimi nasisitiza kwamba umuhimu wa suala hili ni lazima suala zima la Muungano liangaliwe, kero zake zishughulikiwe, na tusitiliwe viraka. Kuna mambo yanafanywa ndani ya Jamhuri ya Muungano, kunatungwa masheria za kuingilia mambo ya Zanzibar na yanakiuka Mkataba ambao tangu ulipofanywa haujawahi kukaliwa kitako cha kurekebishwa pahali popote, lakini bado yanapitishwa bila sisi kushauriwa. Katika ziara zetu za kamati, jana tumekuta kuna mamkala zimeanzishwa, hazivunji sheria lakini Baraza hili halina habari.

Kwa hiyo, Mhe. Mwenyekiti naona nikiendelea kusema hayeshi kwa sababu kero ni nyingi, nazungumzia suala la mafuta si suala la Muungano kwa hivyo hatuna haja ya kuiingiza hapa SMT.

Nakushukuru Mhe. Mwenyekiti kwa kunipa nafasi.

HAJI FAKI SHAALI, CUF MKANYAGENI

HAJI FAKI SHAALI, CUF MKANYAGENI

Haji Faki Shaali (CUF, Mkanyageni): Ya kwangu mimi Mhe. Mwenyekiti ni maswali tu. Suala la kwanza nauliza, lipo katika Kifungu cha 8, Applicable Law. Tukiangalia huu mkataba unasema kwamba sheria zitakazotumika katika mkataba huu au zitakazoutafsiri mkataba huu ni sheria za Jamhuri ya Muungano. Lakini sasa huu mkataba, clients wake ni wawili – Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Zanzibar. Sasa kwa nini sheria zitakazotumika katika huu mkataba ziwe za upande mmoja tu wa Jamhuri ya Muungano? Hilo naomba kufahamishwa kwa sababu mimi si mwanasheria, kazi yangu ni mwalimu.

La pili katika huu mkataba vile vile, kuna kifungu cha 19, Termination of Contract. Sasa hapa kwenye Termination of Contract imeeleza tu kwamba, baada ya kutia saini mkataba, ikiwa mkataba utakuwa haukutekelezwa, mjumbe mmoja anaweza kumuandikia mwenzake kujitoa ndani ya siku 21. Sasa suala langu, huu mkataba ikiwa haukutekelezwa kwa sababu zipi: ikiwa pametokea frustrations au kwa sababu mjumbe mmoja tu hakutekeleza majukumu yake? Kwa sababu mkataba unaweza ukavunjika kwa njia mbili: ama ikatokea frustrations, jambo ambalo linazuia mkataba kutekelezeka naturally bila uzembe wa upande wowote, au mkataba haukutekelezwa kwa sababu upande mmoja umezembea. Sasa hapa tuelewe vipi: kwamba huu mkataba termination yake inaweza ikatokezea kwa frustrations au mjumbe mmoja kutokutekeleza wajibu wake?

Yalikuwa masuala yangu mawili ambayo yamo kwenye huu Mkataba.

Sasa nije katika hii Section Report. Ukenda katika ukurasa wa 8, paragraph ya 3, 4 … (hapa anasoma aya hiyo kwa Kiingereza)… Kwa mujibu wa walivyoona hawa, TPDC ni ya upande mmoja. Wao wanapendekeza sheria irekebishwe ili iwe inatumika pande zote mbili. Kwa maana hiyo, huyu muelekezi anatu-convince tukubaliane hili suali la mafuta liwe la Muungano, kwa sababu asingelipendekeza ifanyiwe maekebisho ili iweze kufanya kazi kisheria na Zanzibar. Hayo madaraka ya kutushawishi sisi kapewa na nani? Hilo suala langu.

Halafu suala la tatu, hapa hapa, paragraph ya 3, ndogo ya 5… (hapa anasoma aya hiyo kwa Kiingereza)… Hapa pia anarekebisha sheria ile ya mafuta ya Tanzania Bara ili iweze na sisi kutunufaisha. Sasa suala linakuja: hapa ndipo hadaa ilipotumika katika Muungano. Katika Muungano wa 1964 ulipofanyika, ilichukuliwa ile Katiba ya Tanganyika ikarekebishwa ili kutoa nafasi kwa Zanzibar nayo kuwemo. Sasa nadhani hii ni wrong. Miye nadhani, kama hata hayo makubaliano yatakuwepo, basi sheria iandikwe upya na sio ukachukua sheria ya upande mmoja, ukairekebisha ifanye kazi pande mbili. That is wrong!

Halafu kuna suala moja nataka nimpongeze huyu bwana. Anasema katika ukurasa wa 4 wa ripoti yake hii kwamba hawakupewa taarifa TPDC. Kwa hivyo mimi nakupongeza kwa kusema ukweli kwamba mulikwenda kule na hamukupewa taarifa. Kwa hivyo, hiyo ndiyo hali halisi ya TPDC ambayo munapendekeza irekebishwe itusaidie siye. Ikiwa nyinyi mulinyimwa baadhi ya ripoti, hapo kuna marekebisho gani yatakayofanyika sisi tukayakubali?

Halafu jengine, Mhe. Mwenyekiti, linanikanganya kidogo: huyu mtaalamu anasema hawakutakiwa kuingia masuala ya katiba, lakini ukiangalia wamefanya legal analysis kubwa, ambayo wameangalia zile sheria pamoja na katiba yenyewe. Sasa kama wewe hukupewa uwezo wa kuangalia mambo ya katiba, kwa nini umefanya legal analysis ambayo inajumuisha pamoa katiba yenyewe, ya Zanzibar pamoja na Jamhuri ya Muungano?

Mheshimiwa nakushukuru sana.

SOUD YUSUF MGENI, CUF WAWI

SOUD YUSUF MGENI, CUF WAWI

Soud Yussuf Mgeni (CUF, Wawi): Mhe. Mwenyekiti, ahsante sana kunipa nafasi ambayo nitazungumzia mambo mawili kwa ufupi sana.

Kwanza ni kauli ya mshauri kwamba uwezekano wa kupata mafuta Zanzibar ni mdogo. Hii taarifa sijui kapewa na nani au ameambiwa aje atuambie hivyo, kwa sababu katika mwaka 1980, alikuja mtaalamu aitwa Mr. John, kuja kufanya utafiti wa maji chini ya ardhi. Akafanya kazi hiyo, baadaye akaomba ruhusa ya kwenda Uingereza kukamilisha shughuli ambayo ameifanyia utafiti. Aliporudi, akaja akanipa taarifa ifuatuyo – wakati huo nilikuwa mimi waziri wa maji – akanambia kwamba katika kazi aliyokwenda kuifanya ya underground water, amepata document ambayo inaelezea taarifa ya mafuta ya Zanzibar. Na katika document hiyo, tarifa iliyomo ni kwamba Zanzibar ina mafuta mengi ya kibiashara. Sasa leo kuja kusikia kuwa Zanzibar uwezekano wa kuapata mafuta ni mdogo, miye nashangaa sana na si kweli.

Kwa taaraifa hii ni kwamba Zanzibar kuna mafuta ya kutosha, lakini kuna njama njama kidogo zinataka kufanywa ili na siye tuamini kwamba hayapo halafu watu waje wachukuwe. Twasema hilo hatulikubali.

Mhe. Mwenyekiti, kama alivyosema Mhe. Waziri, suala la mafuta limeingizwa katika Muungano katika mwaka 1980. Jana nilipata taarifa kwamba sheria iliyopitishwa katika Buge kuhusu mafuta, Mhe. Marehemu Karume aliidhinisha. Kumbe taarifa ile ilikuwa siyo kweli. Marehemu Karume ameondoka duniani mafuta ni mali ya Zanzibar. sasa katika nchi hii, hakuna mtu wala chombo chenye mamlaka ya kubadilisha Mkataba wa Muungano. Makubaliano ya Muungano ni makubaliano ya nchi mbili. Wanaobadilisha ni wale wale ambao waliounda Mkataba wa Muungano. Si chombo. Bunge la Jamhuri ya Muungano, kisheria, halina mamkala ya kubadilisha Articles of Union. Baraza la Wawakilishi halina mamlaka ya kubadilisha Articles of Union. Articles of Union hubadilishwa na wale wale ambao walianzisha Articles of Union, nchi mbili Tanganyika na Zanzibar. Kwa hivyo, mambo yote yale ambayo Bunge lilichukuwa mamlaka ambayo si yake ya kuingiza mambo katika Articles of Union kuwa ni ya Muungano, mimi nasema yale yote ni batili na hatuyakubali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyokwishasema, mafuta ni mali ya Zanzibar. Na nina hakika, Wazanzibari tukikazana, mafuta yatakuwa mali ya Zanzibar. Tukilegea, yatachukuliwa. Naamini kwamba tutakazana, sote kwa pamoja, kuhakikisha kuwa mafuta ni mali ya Zanzibar kwa maslahi ha Wazanzibari.

Lakini harakati za shughuli ya kutafuta mafuta hivi sasa ni kubwa, mpaka kufika kutafutwa mshauri elekezi. (Ingawa wao) wanatwambia mafuta hakuna, lakini kazi ya kutafuta mshauri muelekezi wa kuja kutuambia tugawanye vipi, na bado hakuna mafuta? Wazi ni kwamba mafuta yapo.

Nasema kwamba asiilimia 100 ya mafuta ni mali ya Zanzibar kama iliyokuwa asilimia 100 ya dhahabu ni mali ya Tanganyika. Lakini mambo yakienda vibaya – na naomba yasiende vibaya – tukabakia na hali hii hii ya sasa, basi nashauri (kwamba) katika mapendekezo ya kugawana rasilimali hii ya mafuta, pale ambapo yanatoka wapate asilimia kubwa kuliko sehemu nyengine. Yakitoka Bara, wapate wao zaidi; lakini yalitoka Zanzibar, ipate zaidi Zanzibar.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.

HAMAD MASOUD HAMAD, CUF OLE

HAMAD MASOUD HAMAD, CUF OLE

Hamad Masoud Hamad (CUF, Ole): Mhe. Mwenyekiti, kwanza Waziri katimiza ahadi yake. Kwa hili yafa tumpongeze. Na katimiza ahadi yake wakati ndio. Sote tuna swaum na tuayoyasema hapa hayana toa. Hamna uongo mule maana ukisema uongo saumu inakwenda na maji. Na si hayo tu, mimi nilipopewa hili kabrash, halafu nikapewa parcel hii, niliitikisa kidogo. Inaonekana humu muna juisi maalum – au ni maji haya, sina hakika – lakini inaonekana leo futari ni hapa. Kwa hivyo hii ratiba ya kumaliza saa nane kasoro, itabidi irekebishwe. Mheshimiwa Waziri, nakushukuru kwa futari!

Mheshimiwa Mwenyekiti, semina hii leo hawajajuilishwa watu waliotoka Tanzania Bara, lakini ingenoga sana ikiwa Waziri anayehusiana na Mafuta – Waziri wa Madini na Nishati wa Serikali ya Muungano – angelikuwepo hapa, kwa sababu yatakayoripotiwa kwenye magazeti hayatakuwa exactly yale ambayo yeye kama angelikuwepo angeliyasikia. Na sijui haya ambayo tutayasema hapa yeye atayapataje kama yalivyo na hayupo. Naomba apelekewe hansard. Hansard itasema na atasoma kila ambacho kimezungumzwa na kila mtu. Sasa angelikuwepo Waziri, mimi ningefurahi sana. Lakini kwa kuwa hayupo, haya tutakayoyasema hapa, naomba apelekewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri Kiongozi alitoa njia mbili za kuchangia hili: alisema ya kwanza, tunaweza kung’unika wee na kulalamika mpaka pengine muda ukesha lakini mshauri ikawa hakunufaika na michango yetu. Akasema hiyo si rai nzuri. Rai aliyotoa yeye ni kuwa tuwe watulivu, tusikilize vizuri na tuchangie ili mshauri aondoke hapa na michango ambayo itamsaidia yeye kufanya kazi yake vizuri, lakini vile vile kazi yake ikiwa nzuri maana yake na hii kazi ambayo tumeitwa sisi nasi tutanufaika kwa manufaa yetu. Sasa mimi naomba ngoma zote mbili tupige: hii ya kunung’unika, ya kulalamika, ya kusikitika na hii ya kuchangia ili akiondoka hapa, mshauri ajue ameondoka na kitu gani kutoka kwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi.

Kazi aliyopewa mshauri ni kuangalia namna bora ya mgawanyo wa gharama na faida katika utafutaji na uvunaji wa mafuta na gesi asilia. Hiyo ndiyo kazi miongoni mwa kazi kubwa ambazo mshauri amepewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi Rais Kikwete katika hotuba yake katika masuala ya Zanzibar ni nchi au si nchi, alisema hivi: “Zanzibar ni nchi katika mambo ya ndani ya Zanzibar. Zanzibar si nchi katika mambo nje ya Zanzibar.” Hivyo ndivyo nilivyomsikia akisema au ndivyo nilivyofahamu miye akusudia nini! Ili Zanzibar iwe ni nchi madhubuti, imara na ikiwezekana inayojitegemea, kwa hivyo ile undani wake – hiyo mipaka aliyo-define yeye Rais Kikwete – nayo iwe imara; na moja katika mambo imara ni uchumi wa nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Muungano huu ni Muungano ambao tunataka uwe wa haki, usiokuwa na ulalamifu, usiokuwa na ubabamizi, wala kudanganyana wala kusingiziana. Tunataka uwe Muungano wa haki: kila upande uridhike. Ndio Muungano huo. Kwa hivyo, maisha sisi tungelitaka Muungano huu udumu, lakini udumu ukiwa Muungano imara ambao pande zote mbili za muungano zitafaidika na hakutakuwa na malalamiko makubwa kama yalivyo sasa hivi.

Kila nchi ilikuwa na ghala yake. Waheshimiwa, waasisi wa Muungano huu, wakachukua mambo kutoka ghala moja ya kila nchi – mambo 11 – wakayaweka katika ghala moja. Mheshimiwa, kutokea hapo kila kinachochukuliwa kutoka ghala moja, ni kutoka ghala ya Zanzibar na linaingizwa katika ghala ya Muungano kiasi ambacho sasa yamefikia mambo 23 wa ushei. Ninavyoona mimi ni kwamba itakuja siku ghala yetu haina kitu kwa sababu kila kinachochukuliwa, kinachukuliwa kutoka kwetu…

ABOUBAKAR KHAMIS BAKARY, CUF MGOGONI

ABOUBAKAR KHAMIS BAKARY, CUF MGOGONI

Aboubakar Khamis Bakary (CUF, Mgogoni): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ningependa niombe kwamba haya mazungumzo tunayozungumza, kwa faida yetu na kwa faida ya wetu wengine ambao hawajui Kiswahili, basi hii hansard itafsiriwe na wataalamu wetu wa Baraza ili mshauri huyu apewe tafsiri halisi ya haya tuliyoyazungumza. Miye sikubaliani na tafsiri ambayo wanatoa tu pale – adhoc tafsiri – kwamba iwe ndiyo tafsiri ya maelezo yetu. Naomba hansard itafsiriwe na wataalamu wetu halafu akabidhiwe kwamba hii ndiyo tafsiri hasa ya yale ambayo tumeyazungumza. Na hapo ndio ile tafsiri hasa, au ile maana hasa ya shughuli hii, ndiyo ataipata mtaalamu huyu.

Baada ya kusema hayo, Mhe. Mwenyekiti, kwanza naomba niulize: pengine sikufahamu hii hoja ya leo, lakini nilivyoambiwa ni kwamba semina hii itazungumzia suala la mapato na mgawanyo wa gharama hizi za uchimbaji wa mafuta. Sasa kama hivi ndivyo – na sijui ripoti ilivyokuja imekuja namna gani, kwa sababu kwanza sikuona huo mtiririko wa mgawanyo wa mapato katika uchimbaji huo wa mafuta. Hilo ni la kwanza.

Lakini la pili, wenzangu wengi walisema kwamba suala la mafuta ni suala ambalo lina matatizo, na mimi nakubaliana nao. Lakini hata tuseme – na mimi nakataa – kwamba suala na mafuta na gesi ni suala la Muungano. Sasa kama hivyo ndivyo, mbona katika ripoti hizi au ushauri huu tunaopewa, haujazungumzia chochote kuhusu gesi? Na kwa nini hawa wenzetu wakakarupuka tu wakasema sisi tunataka kuwe na mshauri elekezi ambaye atazungumzia mgawanyo wa mapato ya uchimbaji na utafutaji wa mafuta? Ni kwa sababu mafuta haya yanatoka Zanzibar tu lakini kwa gesi ambayo haiko Zanzibar hawashughuliki?

Hicho ni kitawi kimoja tu ambacho nahisi kuna ajenda ya siri; na ajenda ya siri yenyewe ni dhahiri kwa sababu ikiwa gesi ambayo karibu tangu 2000 inachimbwa na inatumiwa kwenye viwanda – ripoti niliyonayo ni kwamba takriban viwanda 20 hivi sasa katika Bara wanatumia gesi inayochimbwa katika maeneo mengine. Fedha ambazo zimeshakusanywa ni zaidi ya shilingi bilioni 100. Sasa kama kweli hili ni suala la Muungano, kwa nini hawa wenzetu hawakusema kwamba suala hili nalo liingizwe katika mchakato huu, likazungumziwa suala la mafuta ambayo hata kuanza kuchimbwa hayajachimbwa?

Sasa huu ni wasiwasi wangu wa pili, ambao unaonesha dhahiri – hii ni circumstantial evidence – ambayo ukiziunganisha unaona kuwa hawa wenzetu ni majambazi na wanataka kuchukua mafuta yetu kwa maana sisi tunayo mafuta na wanaona choyo. Yote hayo waliyonayo kule – dhahabu, almasi, gesi – yote hayo hawaoni kitu, lakini haya mafuta yanawatoa roho. Kwa Kipemba tunasema wachechenka mate. Sasa huu nafikiri si ushirikiano mzuri wa kidugu.

Mhe. Mwenyekiti, ripoti hii ambayo imeletwa, mshauri anasema kwamba bahati mbaya hakupata yale mambo muhimu – basic issues – ambayo alitakiwa ayafanyie kazi. Na basic issues hizi walikuwa watoe Serikali ya Jamhuri ya Muungano kwa kupitia TPDC. Sasa kama huyu ni mtu wetu wa pamoja, na tumempa kazi kwa pamoja, lakini wenzetu wanazuia ripoti muhimu ambazo zingaliweza kumsaidia kutoa ripoti nzuri, sasa hao wenzetu tutawafikiria vipi? Wana ajenda ya siri. Circumstantial evidence nyengine hiyo.

Na Mhe. Mwenyekiti, mimi nina ripoti ya mwaka 1958 inayosema kwamba Pemba na Zanzibar kwa pamoja kuna mafuta mengi sana ambayo ni commercial. Na ripoti hiyo ipo na documents ninazo. Na wataalamu ni hao hao waliotoka Uingereza. Hao hao ndio waliosema kuna commercial production ya mafuta katika ripoti za mwaka ’58 na archives ziko. Sasa leo huyu, kwa kughilibiwa, anasema kwamba mafuta Zanzibar yanaelekea kwamba ni kidogo. Si kweli hata kidogo. With due respect to him, this is a blantat lie. Kwamba mafuta hamna hapa Unguja na Pemba si kweli. Ripoti zilizopo mafuta yapo.

Lakini, naamini, pengine ni hawa hawa TPDC waliofanya mambo wakajaribu kumshawishi huyu ili ionekane kwamba hakuna mafuta, sisi tukubali kujiingiza katika mtego huo. Sasa kama walivyosema wenzangu, kama hapa kweli hapana mafuta, wao TPDc wana hamu ya nini ya kuja hapa kutafuta haya mafuta na wamekwishasema kwamba hamna? Yote hayo ni mambo ya kujiuliza ambayo conclusion yake inaonesha kwamba hawa ni watu ambao wanatudanganya. Wanatudanganya ili tukubali halafu vizazi vyetu vije vijute. Hicho ni kitu ambacho hatukikubali.

Mhe. Mwenyekiti, suala muhimu ambalo limezungumzwa ni kwamba mshauri katika ripoti yake hii – na ukisoma katika hizi documents tulizopewa kuanzia page 28, Advice on the Government of Zanzibar of Petroleoum Sharing – anasema “exploring licence covering Zanzibar, TPDC has marked 11 possible prospects na katika hizo 5 prospects around and on Zanzibar, 3 around and on Pemba na 3 in the waters closed to the Mainland.” Kwa hivyo, in total utaona kwamba prospects 8 ziko katika visiwa vya Zanzibar, 3 ziko katika Mainland. Na halafu ukisoma chini hapa, utaona kwamba maelezo yake yanaonesha kwamba prospects za mafuta zilizopo ni commercial. Ni kwamba yanawezekana yakapatikana, yakachimbwa na yakatumiwa katika commercial basis. Lakini ripoti hii ya mtaalamu inasema kwamba production ni ndogo.

Sasa ukisoma hizi documents, Mhe. Mwenyekiti, zinatu-confuse. Na confusion hii inatokana la suala zima la TPDC kutaka ku-confuse Serikali ya Zanzibar ili waone kwamba mafuta katika maeneo ya Unguja na Pemba si commercial, kitu ambacho si kweli.

La pili, Mhe. Mwenyekiti, utaona katika Inception Report hii, page 5 item 3 ndiyo subject matter katika hii Contract Agreement. Ni kufanya study ya ugawaji wa mapato na gharama za utafutaji na uchimbaji wa mafuta baina ya Mainland na Zanzibar. Halafu tuje katika paragraph ya pili wanazungumzia kuhusu relevant petroleoum exploration and production.

Kwa hivyo issue hapa ni petroleoum exploration na production. Sasa huyu mshauri – mimi nilikuwa najiuliza – kweli amekuwa assigned katika masuala ya petroleoum tu au amekuwa assigned katika both petroleoum and gas? Kwa sababu mara nyengine hapa tulikuwa tunaambiwa ni suala la petroleoum na gas, sasa which is which? Ni petroleoum peke yake au ni petroleoum na gas? Na ikiwa si petroleoum peke yake, mbona hatukuzungumzia masuala yanayohusu exploration na production ya gas na namna gani Zanzibar itafaidika na gesi hiyo?

Mhe. Mwenyekiti, ukija katika Contract Agreement, utaona vile vile kwamba inakuja pale pale, kwamba huyu consultant amekuwa requested ku-carry out a study on measures zinazohusiana na petroleoum exploration and production. Hizi ndizo issues ambazo zimeelezwa katika mkataba huu. Sasa mimi napenda nielezwe suala la gas exploration, production na sharing costs hizo ziko namna gani? Na ikiwa issues hizi ni za Muungano, je zitatizamwa vipi kwa maslahi ya Zanzibar?

Lakini, Mhe. Mwenyekiti, kitu cha kufanya hapa ni kwamba masuala yote hayo ya petroleoum na gas yalikuja katika mwaka 1988. Katika mwaka huo ndipo suala la mafuta na gesi lilipoingizwa katika katiba ya Jamhuri ya Muungano. Huko nyuma, kwenye Mkataba, lilikuwa halimo. Na nasema haya kwa ushahidi kamili nilionao. Mimi wakati huo ni Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar. Na 1988 ndipo katiba ilipobadilishwa baada ya wajumbe wa Halmashauri Kuu kwenda Dodoma na tukakubaliana kubadilisha baadhi ya mambo. Suala la petroleoum na gesi halijazungumzwa wala halikuzungumzwa. Na mnaweza kwenda kwenye archives za CCM Dodoma, mukatizama, haliko.

Yaliyozungumwa, Marekebisho ya Katiba, ni masuala mengine ambayo yaliingizwa katika katiba. Bahati mbaya, katiba ilipokuwa drafted baada ya marekebisho hayo, alo-draft katiba alikuwa Lushajalo, ameshakufa – alikuwa Chief Parliamentary Draftsman. Sasa yeye baada ya kudraft katiba ile, akaniletea mimi kama ni mwanasheria mkuu wa Zanzibar, noisome niitazame. Suala la petroleoum na gesi tulilisema kwamba hili halikuzungumzwa. Na mimi nikawazungumza authorities wangu wa juu – Waziri Kiongozi na Rais, Mzee Idrissa Abdul Wakil, marehemu (Mwenyezi Mungu amrehemu). Tukakubaliana twende tukazungumze kwamba suala hili halimo. Mimi na Waziri Kiongozi tukenda, tukaonana na Waziri Mkuu, Waziri Mkuu akamwita mwanasheria wake. Tukawaambia hili halimo wala halikuzungumzwa katika Halmashauri Kuu.

Tukenda kwa Marehemu Nyerere, nyumbani kwake Msasani. Mimi nikamwambia kwamba suala hili halimo wala halikuzungumzwa katika Halmashauri Kuu. Alivyonambia: “Aah, basi hili limekwishatiwa, basi tutapeleka tu katika Bunge na kufanya utaratibu kwamba lifutwe.” Nikamwambia, Mwalimu hivyo sivyo kwa sababu jambo hili limeandikwa kimakosa, Mwanasheria Mkuu ana uwezo kisheria kufuta yale ambayo yameingia kimakosa. Hayo nimemwambia mimi na Warioba yupo, aliyekuwa Mwanasheria Mkuu. Baada ya kusema hivyo, Nyerere akawa hana la kusema pale. Akasema basi nendeni tutafanya hivyo ili lirekebishwe. Sasa mkubwa anaposema ndio mkubwa kashasema. Tukarudi kwa kuamini kuwa ata-instruct lakini haku-instruct. Kila siku tukisema ndio hivyo hivyo. Kumbe kuna nia nyengine na nia ndio hii.

Sasa we are talking under authority, kwamba hii ni issue ambayo imeingizwa kinyemela, just kwa kuona kuwa Zanzibar kuna mafuta. Na mimi nilisema kwamba hawa walikuwa kama waliovugwa, maana yake waliona kwamba under Chemistry penye mafuta lazima pawe na gesi. Kwa sababu Zanzibar kuna mafuta, wakasema petroleoum and gas products, lakini hawakujua kuwa wakati mwengine kunaweza pakawa na gesi si lazima kuwe na petroli kama ilivyotokea kwao, kuna gesi lakini hakuna petroli. Sasa gesi waliyonayo ni nyingi, wanaona tabu kutugaia sisi hicho wanachotaka kwa sababu ni cha kwao, wanataka haya mafuta yetu na wao tuwagaie. Sasa huu ujambazi sisi hatukubali hata siku moja. Over our dead bodies, mafuta ni suala la Zanzibar, na si la nchi nyengine.

Mafuta ni ya Zanzibar na ni ya Wazanzibari. Na huyo mshauri tumwambie: kwamba there is no way utakuja utwambie hapa suala la mafuta kuna cost sharing between Zanzibar and Mainland. No way. Petroleoum products are for Zanzibar and that is all, not for Tanzania Mainland. You have to bear that in mind.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ndiyo history ya suala hili la petroli. Ndio maana nasema kwa ushahidi huu huu, nenda kwenye hansard za CCM Dodoma utazame kama hili utaliona. Kuna marekebisho mengine ya Katiba ya 1988 yaliyozungumzwa. Yako marekebisho ambayo tumeyapitisha wakati huo tuko Dodoma, suala la mafuta halikuzungumzwa hata siku moja. Lakini iliporekebishwa Katiba, Lushagana – naye huko aliko Mungu atamuhukumu kwa kutuibia mafuta yetu – pamoja na hao wengine wakafanya hivyo. Sisi tulikuwa tunapiga kelele, lakini sisi tufanye nini wakati mkubwa anaposema nendeni sisi tutarekebisha, huna njia nyengine wewe mdogo, lazima uamini. Lakini kuamini kwetu ndio kukawa hivi.

Sasa ili kuyatatua matatizo haya ni kuona kwamba Zanzibar inabakia na mafuta yake na Tanganyika wabakie na gesi zao, wabakie na almasi zao, na dhahabu zao – wabakie na kila kitu chao. Kwa sababu ikiwa ni Muungano mulioungana, kwa nini ukasema saa yangu miye tu ndiyo tuitie katika Muungano lakini saa yako wewe wasema ni yako peke yako? Kama ni kudumisha Muungano, ziletwe basi dhahabu ziwe za Muungano, almazi ziwe za Muungano. Hiyo gesi waliyosema ni ya Muungano, mwaka wa nane huu wanatumia, siye Wazanzibari tuna faida gani? Tunafaidika lipi hata tuseme na mafuta nayo ni ya Muungano? Hatuwezi kusema hivyo kwa sababu hawana nia njema.

Mhe. Mwenyekiti, mimi sitaki niseme mengi, lakini ninachosema ni kwamba hii ndiyo history ya mafuta. Ninayo ripoti ya 1958, anayetaka nitampa, inayosema kwamba Zanzibar kuna mafuta. With due respect, ripoti ya mtaalamu huyu aliyesema Zanzibar hakuna mafuta, siikubali. Na hiyo ripoti (ya 1958) iliandikwa huko huko Uingereza anakotoka yeye, na ni ripoti inayosema mafuta yaliyopo ni commercial. Sasa leo ukisema si commercial, sijui ikiwa hayo mafuta yaliyoko kwenye ardhi yatakauka. Sijui.

Mhe. Mwenyekiti, sijui hao hawakumpa hizo ripoti au ametumwa aseme hivyo, lakini sisi hatukubali. Mafuta yapo, na ni ya Zanzibar, na yatabakia kuwa ya Wazanzibari kwa faida yetu na vizazi vyetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.

NAJMA KHALFAN JUMA (CUF NAFASI MAALUM)

NAJMA KHALFAN JUMA (CUF NAFASI MAALUM)

Najma Khalfan Juma (CUF, Nafasi Maalum): Kule kwetu Pemba kuna hadithi ya mtu akila na akawa ananenepeana tu. Basi alikuwa akiambiwa: “Mjenga kando waumia” akisema “aah, sina ‘ta!” Sasa sisi Wazanzibari tulidhani hawa ni wenzetu, tukawaamini kweli. Tukajikaza kibwewe. “Eeh, mjenga kando waumia we!” “Aah sina ‘ta!” Naye kashika pakachu pakachu pakachu. Matokeo yake tulipofunguliwa kibwebwe, Wazanzibari tumebakia kile Upembani tukiitacho ‘ukilini.’ Ujuzi mwembamba ambapo ukiufanya hivi, basi utakatika.

Sasa hayo yameshapita. Wajuwe wenzetu kwamba tumeshapita katika karne hizo. Sasa sisi si wajenga kando tena. Sasa wajuwe kuwa sisi Wazanzibari ni nyuki – wadogo, tukiungana tunatengeneza asali, na mtu akija hivi hivi tu tunaungana pamoja tunampiga. Wasikaribie mafuta ya Wazanzibari.

Toka zamani mimi nasema, jamani haya mafuta ni ya Wazanzibari. Sasa muelekezi hapa anasema haya mafuta ni kidogo. Mimi nasema hata yakawa kinibu – kwa wale wenzangu mie wa zamani watakuwa wanajuwa kile kiglasi kidogo kilichokuwa kinapimiwa mambo – kinibu, basi hichi kinibu kitakachopatikana Zanzibar ni cha Wazanzibari. Tutapakana. Ikiwa hatuwezi kufanyia mambo mengine, tutachuliana mishipa, lakini ni yetu. Wasijaribu kutuhadaa na kutaka kutuibia.

Kwa sababu Mwenyezi Mungu, Mhe. Mwenyekiti, alitupa karafuu siye na na nazi. Zimekwenda karafuu na nazi, nazi zimetoweka – tunazo za kupikia tu. Karafuu ziko katika hali mbaya, maana yake hatuzalishi tena kama tulivyokuwa tukizalisha. Lakini kuwa sisi ni wanaadamu tupo juu yah ii ardhi, Mwenyezi Mungu katupa jambo jengine – katupa mafuta ambayo yalivumbuliwa miaka khamsini na khamsini na ngapi iliyopita. Mwenyezi Mungu katupa kitu kingine cha kutumia, sasa madam Mwenyezi Mungu kaondoa hili kaweka hili, wasituingilie wala wasitutilie mkono.

Twawaomba wenzetu wa Tanzania Bara, Muungano tunautaka, lakini usiwe Muungano wa chetu. Isiwe ile khadithi ya zamani – chetu chao, chao chao. Hiyo hatutokwenda. Chambilecho maneno yako, Mhe. Mwenyekiti, Msegeju ana ng’ombe. Wala tusichezeane kibafte katika mchezo huu. Kibafte nipe mbili zangu nkufte. Haya hayapo.

Tena wataalamu munaomuandikia huyo mtaalamu hapo, mumuambie kuwa Wazanzibari wanasema mafuta yao hawataki na ni yao wenyewe. Waandishi wa habari, wahariri wenu wasije wakageuza lugha wakasema kwamba Wazanzibari wamekubali kwamba mafuta yagaiwe. Hatukubali. Mafuta ni yetu wenyewe kama ilivyokuwa almasi, dhahabu, tanzanite, chuma, rubi, na mengine mengi yanayovumbuliwa huko Bara hivi sasa ni yao wenyewe. Siye hatuwaingilii. Twenda na shida zetu, alhamdulillah, tukipata twala, tukikosa twashukuru Mungu, alhamdulillah. Tukipata twafanya, tukikosa twacheza upatu. Maana yake Zanzibar uchumi wetu mdogo, huwa tunacheza upatu. Serikali vile vile huwa inacheza upatu. Anaweka, anaweka, anapata pesa anafanyia jambo hili. Siye hautukeri utajiri wao, wao kwa nini wakereke na wetu, Mungu anaotaka kutujaalia nao?

Basi miye naomba, wataalamu mumwambie mtaalamu alokuja: Zanzibar hata kama mafuta ni kinibu ni ya Wazanzibari. Waandishi habari waambieni huku katika magazeti ya kesho, kwamba wawakilishi wa Wazanzibari, wa wananchi wa Zanzibar, nchi ya Zanzibar, mafuta yao hawataki, ni ya Wazanzibari kwa ajili yetu tuliopo hivi sasa, watoto wetu wetu walioko nyuma yetu, wajukuu wetu wajao, vitukuu, vilembwe, vinying’inya mpaka Zanzibar itakapokwisha. Wasije wakatugeuza Nigeria, vita vya kila siku. Hatuviwezi wala hatuvitaki. Siye ni wachache na watuwache na utajiri ambao Mwenyezi Mungu atatujaalia.

Musitowane roho jamani kwa mali ya Wazanzibari.

Ahsante mwenyekiti.

Advertisements

One thought on “Msimamo wa Wawakilishi wa CUF kuhusu mafuta ya Zanzibar

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s