Hotuba ya Prof. Lipumba kukubali uteuzi wa kuwa mgombea urais, 2005

Waheshimiwa Wananchi,

Hii ni mara ya tatu kuteuliwa na Mkutano Mkuu wa Chama chetu kuwa Mgombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia The Civic United Front (CUF-Chama Cha Wananchi) Niliamua kujaza fomu ya kuomba kuwa mgombea Urais kwa kuamini kuwa nina nia, sababu, na uwezo wa kutoa ushawishi kwa Watanzania kunichagua kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuunda serikali itakayopambana na saratani ya rushwa, kusimamia upatikanaji wa haki sawa kwa wananchi wote, kukuza uchumi utakaokuwa na manufaa na kuleta neema kwa wananchi wote, kuharakisha maendeleo yetu na kuondoa umasikini. Kama mnavyojua mzigo mzito hupewa Mnyamwezi.

Mwaka 1995 nilikubali kugombea Urais kupitia tiketi ya CUF katika saa za majeruhi kwa sababu mbili kubwa. Mosi, mfumo wa demokrasia ya vyama vingi ulikuwa ndio unaanza kufanya kazi katika nchi yetu. Baada ya miaka karibu 35 ya uhuru wa Tanzania maendeleo yetu yalikuwa madogo. Sera za kuondoa ukiritimba wa dola katika uchumi zilizokuwa zikitekelezwa na Rais Mwinyi hazikuungwa mkono kikamilifu na Chama chake. Baada ya kufanya kazi kama Mshauri wa Uchumi wa Rais Mwinyi, na kushuhudia vizingiti vilivyowekwa na CCM katika utekelezaji wa sera za kurekebisha uchumi, niliamini kuwa CCM haina uwezo wa kufanya mageuzi ya kimsingi yatakayojenga uchumi imara wenye manufaa kwa wananchi wote.

Nilikubali kugombea Urais kwa tiketi ya CUF ili niitumie nafasi hiyo kuwazindua wananchi waelewe kuwa wakiichagua CCM, hali zao za maisha zitaporomoka.

Nilivutiwa na sera za msingi za Chama cha CUF za “HAKI SAWA KWA WANANCHI WOTE” na itikadi ya UTAJIRISHO yenye madhumuni ya kujenga uchumi imara utakaoleta NEEMA KWA WOTE.

Sababu ya pili ilikuwa kujenga umoja wa kitaifa kwa kukiimarisha chama cha CUF Tanzania Bara. Nilikuwa na uhakika kuwa CUF itashinda Zanzibar. Vile vile niliamini kuwa kwa mwaka ule Chama chetu kisingeweza kushinda Uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano. Niliingia katika kugombea Urais kwa nia ya kukiimarisha Chama chetu Bara ili kulinda Umoja wa Kitaifa na Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Kama chama chetu kingekuwa imara Zanzibar peke yake na kuwa kibovu Tanzania Bara, umoja wa kitaifa ungeathirika. Chama cha CUF sasa kimeimarika sana Tanzania Bara.

Baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2000 CCM ilijitangazia ushindi wa kishindo. Haukuwa ushindi wa kishindo ulikuwa wizi wa kishindo. Tanzania Bara ni eneo kubwa na hatukuwa na mawakala katika vituo vyote. Ilikuwa rahisi kwa CCM wakishirikiana na Usalama wa Taifa, Watendaji wa Kata na Wakurugenzi wa Halmahauri kutuibia kura.

Zanzibar tuna mtandao mzuri wa Chama na tuliweza kulinda kura zetu. Viongozi wa CCM walipoona wanaelekea kushindwa waliamrisha Polisi wapore masanduku ya kura na kuyapeleka walikojua. Watazamaji wa uchaguzi wa ndani na nje walishauri uchaguzi wote ufutwe na urejewe baada ya kuunda Tume Huru ya Uchaguzi ya Zanzibar. Chama chetu kilikubaliana na ushauri huo lakini Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na CCM waliupuuza wakarudia uchaguzi katika majimbo 16 na kujitangazia ushindi wa kishindo.

CUF – Chama Cha Wananchi kiliitisha maandamano ya amani yanayoruhusiwa na Katiba ya nchi na sheria ya vyama vya siasa ya 1992 yafanyike tarehe 27 Januari 2001. Madhumuni ya maandamano yalikuwa kudai Katiba mpya yenye misingi imara ya demokrasia, Tume huru ya uchaguzi – Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Uchaguzi wote wa Zanzibar urejewe baada ya kuirekebisha Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar. Kuhakikisha kuwa maandamano yatakuwa ya amani tulieleza tutafunga vitambaa vyeupe katika bega la kulia na viongozi wa CUF watayaongoza.

Mimi binafsi nilieleza nitaongoza maandamano hayo jijini Dar es Salaam. Serikali iliamua kupinga maandamano haya kwa njia yeyote ile. Tarehe 25 Januari 2001, mimi, Mbunge wetu wa Kigamboni, Mheshimiwa George Frank Magoba, baadhi ya Wakurugenzi na wanachama tulikamatwa na polisi tukapigwa na kuporwa saa, simu za mkononi na fedha na kuwekwa mahabusi.

Serikali ya CCM ilianza kuua raia wasio na hatia Zanzibar tarehe 26 Januari 2001 na tarehe 27 waandamanaji zaidi ya 45 waliuawa Pemba na Unguja. Pamoja na kuuliwa wanachama na wapenzi wa CUF na mimi binafsi kupigwa, kudhalilishwa na kubambikiwa kesi, niliweza kushawishi Chama na kukiongoza kiingie katika mazungumzo ya kutafuta suluhu ya kisiasa katika mgogoro wa Zanzibar mpaka tukafanikiwa kutia sahihi Muafaka tarehe 10 Oktoba 2001.

Kama Muafaka ungetekelezwa kikamilifu, maendeleo ya demokrasia Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yangekuwa makubwa na tungekuwa na matumaini ya uchaguzi ulio huru na wa haki zaidi mwaka 2005 kuliko ilivyokuwa mwaka 2000 na 1995. Hata hivyo serikali ya CCM haikutekeleza vipengere muhimu vya Muafaka na hasa kile kinachokataza matumizi ya vyombo vya dola kwa manufaa ya Chama tawala. Rais Mkapa bila kuona haya ameeleza hadharani dhamira yake ya kutumia vyombo vya dola kuhakikisha CCM inashinda uchaguzi mkuu mwaka 2005.

Tunamjulisha Rais Mkapa Tanzania ya 2005 siyo Tanzania ya 2000. Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla hawatakubali wizi wa kishindo wa CCM. Kwa nia safi namshauri Rais Mkapa ajijengee heshima na astaafu salama usalimini kwa kuhakikisha uchaguzi wa Zanzibar na wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania unakuwa huru na wa haki.

Waheshimiwa wananchi, kwa mara ya tatu katika uhai wangu nimeomba ridhaa ya chama changu na mmekubali kunitwika mzigo mzito wa kuwa mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano. Sababu kubwa za kuhiari kubeba jukumu hili ni tatu. Mosi, Chama chetu kimeimarika. Sera zake za msingi : Haki sawa kwa wote na ujenzi wa uchumi imara wenye neema kwa wote zinakubaliwa na Watanzania wote. Changamoto wanayoitoa wananchi ni kutafsiri misingi hii kwa vitendo ili kujenga nchi inayoheshimu haki za binadamu, inayoendeshwa kisheria, inayopambana kwa dhati dhidi ya saratani ya rushwa na inayoweka mazingira ya kuboresha hali ya maisha ya wananchi wote mwaka hadi mwaka.

Sababu ya pili ni kwamba baada ya kutawala kwa muda wa miaka 43, CCM imechoka, inanuka rushwa na haina uwezo wa kusimamia maendeleo ya Tanzania. Uongozi wa CCM wa sasa hauna huruma na hauyajali matatizo yanayomkabili mtu wa kawaida. CCM haina dira. Viongozi wake wanang’ang’ania madaraka kwa manufaa ya watu wachache. Wamepoteza uzalendo na wanaiuza nchi bei poa. Hawana mtazamo wa kujenga demokrasia ya kweli au kutetea maslahi ya wananchi wa kawaida. Viongozi wa CCM hawana haya wala aibu. Wako tayari kutumia dola na propaganda yeyote ile ili wabaki madarakani. Mbinu hizi zinahatarisha umoja wa kitaifa. CCM ni sawa na kapu la samaki waliooza. Hata samaki msafi akiwekwa katika kapu hilo naye ataoza.

Waheshimiwa wananchi, sababu yangu ya tatu ni ya binafsi. Toka nikiwa kijana mdogo katika shule ya sekondari ya Tabora nilipendelea sana kusoma uchumi na namna nchi zinavyoendelea kiuchumi. Nilipomaliza kidato cha nne nilikuwa katika mchepuo (sub stream) wa sayansi. Masomo niliyofanya vizuri sana yalikuwa Hisabati, Fizikia na Kemia. Kwa kupenda kuelewa maendeleo ya uchumi niliamua kuomba kuchukua masomo ya Hesabu, Uchumi na Jiografia katika kidato cha tano (5). Kwa muda wa miaka 35 nimekuwa najifunza na kutafiti sababu zinazofanya nchi ziendelee kiuchumi. Shahada zangu zote nne, mbili za Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, na mbili za Chuo kikuu cha Stanford Marekani ni za uchumi. Miaka 44 baada ya uhuru Tanzania ni miongoni mwa nchi maskini sana duniani. Nahitaji kutumia ujuzi na uzoefu wangu wa maendeleo ya uchumi kushirikiana na Watanzania wenzangu kujenga uchumi imara utakaoleta neema kwa wananchi wote.

Ilani yetu ya Uchaguzi inafafanua kwa undani zaidi azma yetu na mikakati tutakayoitumia kujenga uchumi imara wenye manufaa kwa wote. Hapa nitazungumzia mambo machache ambayo nikiwa Rais nitayasimamia kwa karibu.

1. Kujenga Uchumi Imara Unaoongeza Ajira

Iwapo nitachaguliwa kuwa Rais lengo kuu la sera litakuwa kujenga uchumi unaokua kwa kasi kubwa ya wastani wa asilimia 8 na kuongeza ajira. Haiwezekani watanzania kuondokana na umaskini bila kukuza uchumi unaoongeza ajira. Katika suala la kukuza uchumi hakuna miujiza. Uchumi unakua kwa kuongeza elimu, ujuzi na utaalamu wa wafanyakazi, ongezeko la raslimali na vitendea kazi, na kuongezeka kwa ufanisi na tija katika uzalishaji na utoaji huduma. Dira ya maendeleo na sera za kutekeleza dira hiyo ni jambo la msingi katika kuleta maendeleo ya muda mrefu. Sera za ukiritimba wa dola katika mambo ya uchumi na kuwabana wananchi, kuwanyang’anya motisha wa kujiendeleza, na kufumbia macho rushwa ya hali ya juu inayoendelea nchini zimeporomosha uchumi wetu. Kwa muda mrefu uchumi wetu umetumikia siasa, badala ya siasa kuweka mazingira mazuri ya kukuza uchumi.

Dira yetu ya maendeleo itakuwa ni kujenga uchumi wa soko wenye ushindani halali na unaowashirikisha na kuleta maendeleo kwa wananchi wote. Majukumu makubwa ya dola yatakuwa ni:-

 1. Kuasisi utawala unaolinda kikamilifu haki za wananchi, unaozingatia kanuni na kufuata sheria.
 2. Kuasisi mapinduzi ya kilimo yatakayohakikisha Tanzania inaondokana na baa la njaa na uksefu wa lishe bora.
 3. Kujenga mazingira yatakayotuhakikishia ongezeko kubwa la ajira mwaka hadi mwaka.
 4. Kuweka mazingira yanayolinda ushindani halali wa biashara, kuepuka mfumuko mkubwa wa bei, na kulinda ushindani wa bidhaa zetu katika soko la dunia.
 5. Kuboresha huduma za msingi za jamii na hasa elimu na afya.
 6. Kujenga au kusimamia ujenzi wa miundombinu mizuri kama vile barabara, reli, nguvu za umeme, simu na maji.
 7. Kulinda na kuhifadhi mazingira.

2. Ajira

Ukosefu wa ajira ni tatizo kubwa linaloathiri maisha ya vijana, kuongeza umaskini na kuchangia katika kuongezeka kwa kasi ya mmomonyoko wa maadili. Kila mwaka vijana 700,000 wanaingia katika soko la kutafuta ajira. Kila mwaka ajira mpya inayopatikana nchini haizidi watu 40,000.

 1. Lengo la serikali nitakayoingoza itakuwa alau kuanzisha ajira mpya katika sekta rasmi ya watu 500,000 kila mwaka.
 2. Kuongeza ajira kwa kujenga mazingira ya kuwezesha viwanda vinavyoajiri vijana kwa wingi kama vile viwanda vya nguo na mavazi, viatu, bidhaa za ngozi, vifaa vya umeme na electronics.
 3. Kutumia jiografia ya Tanzania kuongeza ajira katika sekta mbali mbali ikiwa ni pamoja na utalii, usafirishaji, mawasiliano, kilimo na ufugaji wa kisasa.
 4. Kutenga na kuyapa huduma maeneo ya kuanzisha viwanda ikiwa ni pamoja na viwanda maalum vya kuuza bidhaa nchi za nje.
 5. Kujenga mazingira ya kuwezesha kuanzishwa na kushamiri viwanda na biashara ndogo ndogo na za kati (small and medium scale enterprises) kwa kuvipatia mikopo, utaalam, utafiti, teknolojia na masoko ili viweze kutoa ajira kwa wingi

3. Kilimo

Njaa na ukosefu wa lishe bora ni matokeo ya umasikini lakini pia ni kichochea kinachokuza na kudumisha umasikini. Watu wenye njaa hawawezi kuwa wazalishaji wazuri na wenye tija ya juu. Watoto wenye njaa hawafundishiki na kwa hiyo hawanufaiki kikamilifu wakiwa shuleni. Watu na hasa watoto wanaokosa chakula bora na cha kutosha wanapoteza kinga ya mwili na kwa hiyo huugua mara kwa mara. Malaria huua kwa haraka watoto wasiokuwa na lishe bora.

Nusu ya Watanzania hawana usalama wa chakula. Usalama wa chakula unakuwepo ikiwa watu wote, wakati wote, wana uwezo wa kupata chakula na lishe ya kutosha na salama kwa mahitaji yao kuwaweza kuishi maisha yenye afya na tija. Serikali itahakikisha katika miaka mitano ijayo Watanzania wote wana usalama wa chakula. Ili Tanzania ijinasue katika dimbwi la umaskini ni lazima pawepo na mapinduzi ya Kilimo. Kuendeleza kilimo tunahitaji:-

 1. Kuongeza motisha kwa wakulima wapate bei nzuri ya mazao yao. Hatua za makusudi zahitajika kuboresha huduma za kilimo na kuweka usimamizi wa kuwalinda wakulima wasinyonywe na wafanyabiashara wanaoshirikiana kupunguza ushindani katika soko huria na kwa lengo la kuangusha bei za mazao.
 2. Kuendeleza kilimo kwa kuwawezesha wakulima ikiwa ni pamoja na wakulima wadogo wadogo kuongeza tija na uzalishaji kwa kuwapatia zana na pembejeo bora, masoko ya mazao na kurahisisha usafirishaji kwa kutengeneza barabara ziendazo vijijini.
 3. Katika kipindi cha miaka mitano ijayo tutaanzisha mapinduzi ya kilimo kwa kupenyeza sayansi na teknolojia katika kilimo. Kuongeza utumiaji wa mbolea ya samadi na kemikali, mimea na miti inayorudisha rutuba katika ardhi, mbegu bora na mifugo bora; miradi midogo midogo ya umwagiliaji maji, mafunzo kwa wakulima na jitihada za maksudi kuwafikia na kuwawezesha wakulima wanawake.

Upatikanaji wa umeme vijijini ni muhimu katika utoaji wa huduma za afya, kuendeleza viwanda vidogo vidogo vya kusindika vyakula, karakana za zana za kilimo, mawasiliano na matumizi ya kompyuta na mtandao. Serikali itatekeleza mpango kabambe wa usambazaji wa umeme vijijini na kuhamasisha matumizi ya vianzio endelevu vya nguvu za umeme kama vile mionzi ya jua, gesi ya samadi na mimea na upepo.

Katika awamu ya tatu 1995/96- 2004/05 serikali imetenga chini ya asilimia tano ya bajeti yake katika sekta ya kilimo. Ili kuboresha kilimo serikali itatumia asilimia 10-15 ya bajeti yake kutoa huduma za kuwasaidia wakulima

4. Elimu

Kukua kwa uchumi wa kisasa wenye uwezo wa kuboresha maisha ya wananchi kunategemea sana wafanyakazi wenye ujuzi na maarifa. Kwa hakika utafiti unaonyesha kuwa kukua kwa uchumi wa taifa lolote kunashabihiana kwa karibu na kiwango cha kuwekeza katika sekta ya elimu. Hivi sasa dunia inashuhudia mapinduzi ya teknologia ya mawasiliano ya habari (Communication and Information Technology) ambayo yanaleta mageuzi makubwa ya uchumi na biashara ya kimataifa. Uchumi wa kisasa unatumia kompyuta na mtandao (internet). Kwa hakika mtandao umeondokea kuwa ni kisima kilichojaa kila aina ya habari, taarifa, na data ambazo kila mmoja wetu anaweza kujichotea kwa matumizi yake kwa gharama nafuu kabisa. Ili Tanzania ishiriki kikamilifu na ifaidike na uchumi wa ulimwengu inatulazimu kuweka mkakati wa kuboresha na kupanua elimu toka elimu ya msingi mpaka vyuo vikuu. Pamoja na mambo mengine, iwapo nitachaguliwa kuwa Rais serikali itachukua hatua za makusudi ikishirikiana na taasisi za kimataifa kusambaza matumizi ya kompyuta na mtandao (internet) katika mashule yetu.

Nitahakikisha watoto wote wanapata elimu bora ya msingi. Serikali itafuta malipo na michango iliyobakia inayowazuia watoto wa familia maskini kwenda shule. Juhudi maalum, ikiwa ni pamoja na kupambana na unyanyasaji wa kijinsia zitaelekezwa kuhakikisha kuwa wasichana wote wanapata fursa ya kwenda shule na kumaliza masomo yao.

Mtoto mwenye njaa hafundishiki. Serikali Kuu itashirikiana na Halmashauri za wilaya, manispaa na jiji, na kamati za shule kuhakikisha kuwa watoto wote wanapata alau mlo mmoja wakiwa shuleni. Kila shule itatumia vyakula vinavyopatikana katika eneo husika.

Nitahakikisha kuwa shule zinakuwa vituo vya kuboresha afya ya watoto kwa kuweka utaratibu wa kuwagawia watoto virutubisho muhimu kama vile Vitamin A inayoongeza kinga ya mwili na kuboresha uwezo wa macho, dawa za kuua minyoo, elimu ya afya bora na kinga dhidi ya maambukizo ya maradhi hatari ya Ukimwi

Serikali itagharimia elimu ya sekondari kwa watoto wote waliopasi mitihani na ambao wazazi wao hawana uwezo wa kulipa ada. Kuanzisha Mpango Kabambe wa serikali wa kupanua na kujenga shule za sekondari na kuwapa mafunzo walimu. Kuna vijana wengi waliomaliza vyuo vikuu na kidato cha sita ambao hivi sasa hawana kazi. Vijana hawa watahamasishwa kupata mafunzo ya Ualimu ili waajiriwe katika shule za sekondari.

 1. Kushirikiana na Jumuia ya Kimataifa, UNESCO, Massachusetts Institute of Technology, ComputerAid, na Serikali marafiki kuingiza mafunzo ya kompyuta na matumizi ya internet katika shule za msingi, sekondari na vyuo.
 2. Kuimarisha michezo tokea shule za chekechea, shule za msingi, shule za sekondari na vyuo vya elimu ya juu ili kujenga miili ya watoto, kuwafundisha nidhamu na kujenga hazina ya wanamichezo wanaoweza kushindana kimataifa. Michezo na mazoezi ya viungo ni muhimu sio tu kwa kujenga afya bora ya mwili bali pia kuimarisha ubongo na uwezo wa kufikiri.
 3. Serikali itaboresha mishahara ya walimu, kuwajengea nyumba bora na kwapatia mafunzo ya kujiendeleza ili wawe na ari na motisha wa kufundisha vizuri

5. Afya

Kuwa na afya bora ni lengo muhimu la binadamu kufurahia maisha na ni nyenzo ya kukuza uchumi kwani watu wenye afya bora ni wazalishaji wazuri na wabunifu. Kusambaratika kwa sekta ya afya nchini siyo kitu cha bahati mbaya, ni matokeo ya sera. Vigogo wa CCM na serikali hawaoni sababu yoyote ya kuipa sekta hii msukumo kwa sababu wao na familia zao wanapimwa afya zao na kutibiwa nje ya nchi, kwa fedha za walipa kodi.

Lengo letu ni kwa kila Wilaya kuwa na mfumo kamili wa huduma za afya ya msingi. Kila kijiji kiwe na Zahanati iliyokamilika inayotoa huduma za msingi za afya na ina dawa muhimu ya maradhi yanayowaathiri wananchi waliyowengi hasa watoto na wanawake wajawazito. Maslahi ya wahudumu wa afya yazingatiwe na walipwe vizuri ili wawe na motisha na ari ya kuwahudumia wananchi.

Huduma za msingi za afya kuwa haki ya kila Mtanzania. Kufuta malipo kwa huduma za msingi za Afya za Zahanati zote za serikali na zahanati za taasisi zisizo za kiserikali zitakazotoa huduma hizo kama mawakala wa serikali. Serikali itashirikiana na Jumuia ya kimataifa kuhakikisha kuwa malengo ya milenia ya kupunguza vifo vya watoto na kina mama waja wazito yanafikiwa.

Tanzania inaongoza kwa vifo vya kinamama wajawazito duniani. Kwa kushirikiana na taasisi zisizo za kiserikali za wanawake za nchini na za kimataifa:

 1. Tutahakikisha kina mama wanapata huduma za afya na za ukunga kupunguza vifo vya kina mama waja wazito.
 2. Kuhakikisha kupatikana kwa maji safi na salama kwa wananchi wote kwani maradhi mengi yanasababishwa kwa kutokuwepo kwa maji safi na salama
 3. Kusambaza bure vyandarua vilivyowekwa dawa kwa kina mama waja wazito na wenye watoto wachanga ili kupunguza matukio ya malaria, ungojwa unaoongoza kwa kuua watoto wengi Tanzania.
 4. Kuhamasisha serikali za vitongoji, vijiji na mitaa na taasisi zisizo za kiserikali kuanzisha vituo vya kulelea watoto wakati kinamama wako katika shughuli za kiuchumi. Vituo hivyo viwezeshwe kutoa chakula chenye lishe bora na virutubisho muhimu kwa watoto.

6. Kupambana na Ukimwi

Ukimwi hivi sasa ni tishio kubwa linaloashiria maangamizi si kwa taifa letu tu, bali pia katika nyingi ya nchi zinazoendelea hususan katika bara letu la Afrika. Inakadiriwa kuwa nchini mwetu katika kila watu mia moja waishio mjini, 25 wana virusi vya Ukimwi. Hata huko Vijijini hali si shwari. Inakadiriwa kuwa vijijini kuna wananchi 10 wenye virusi vya ukimwi katika kila wanakijiji 100. Tukiendelea kuuonea haya ukimwi utatumaliza.

Waheshimiwa wananchi, wanawake wanaathirika vibaya zaidi na ukimwi. Kimaumbile ni rahisi zaidi kwa wanawake kuambukizwa virusi vya ukimwi kuliko wanaume. Katika kila watanzania watano wenye virusi vya ukimwi, watatu ni wanawake na wawili ni wanaume. Naomba tuelewe vizuri kuwa wanawake wengi wanaoambukizwa ukimwi sio kwa sababu za uasharati bali ni kutokana unyonge na umasikini wao. Uhuru wa ukombozi wa wanawake na kuongezeka kwa uwezo wao wa kupata ajira na kujiendesha kimaisha utasaidia sana kupunguza ongezeko la ugonjwa huu kwa wanawake.

Utafiti katika nchi nyingi umeonyesha wazi kuwa vijana wanaofahamu vizuri athari na jinsi ukimwi unavyoenea, wanajikinga na hawaambukizwi virusi vya ukimwi ukilinganisha na wale ambao hawana elimu ya ugonjwa huu. Kuwapa elimu vijana wetu kuhusu ugonjwa huu ni kuwapa kinga ya radhi hili hatari. Kuanzia mwaka 1985 hatua na mikakati kadhaa imechukuliwa yote ikilenga katika kuelimisha na kuhamasisha jamii juu ya athari za maambukizo ya ukimwi na njia za kudhibiti kuenea kwa maambuki mapya. Hata hivyo pamoja na kampeni hizi, maambukizi ya ukimwi bado yameshika kasi na wanaougua maradhi haya wanazidi kujitokeza. Ni dhahiri kabisa kuwa hatua za ziada zinahitajika.

Waheshimiwa wananchi, nikichaguliwa kuwa Rais tutaweka mkakati wa kitaifa utakaolenga kupunguza kwa kiasi kikubwa uwezekano wa mtu ambaye hivi sasa hana virusi vya ukimwi, kuambukizwa ugonjwa huu. Pamoja na mambo mengine mkakati huu utalenga katika kuishirikisha jamii katika mjadala wa kutunga sera mahsusi ya nchi itakayosimamia mapambano dhidi ya Ukimwi kwa nia ya kufanikisha malengo yafuatayo:

 1. Kuondoa utaratibu wa sasa unaofanya taarifa za maambukizi ya ukimwi kuwa ni siri na badala yake taarifa hizi ziwe za wazi kama ilivyo kwa magonjwa mengine.
 2. Kufikia makubaliano ya kitaifa ni nini kifanyike ili kudhibiti kwa kiwango cha juu kabisa uwezekano wa maambukizi kwa wananchi wetu ambao bado kuambukizwa.
 3. Kuweka taratibu na mikakati rasmi ya kukinga maambukizi mapya katika sehemu za kazi, mashule, vyuo vya elimu, majeshi, na taasisi nyingine.
 4. Kuweka taratibu na mikakati rasmi ya kukinga maambukizi mapya kutokana na tendo la ndoa.
 5. Kuweka taratibu za kuwahudumia walioambukizwa virusi vya ukimwi kwa kuwapa dawa zinazoongeza muda wa kuishi kwa wale wenye virusi katika hospitali na vituo vya afya vilivyopo nchini.
 6. Kuanzisha utaratibu wa makusudi wa kuziunga mkono na kutoa kila aina ya msaada unaowezekana, juhudi za watafiti wa kizalendo ikiwa ni pamoja na waganga wa jadi katika kutafuta tiba au kinga dhidi ya maambukizo ya virusi vya Ukimwi.

Waheshimiwa wananchi, nikichaguliwa kuwa Rais serikali itaanzisha uhusiano wa karibu na taasisi zisizo za kiserikali kama vile Bill and Melinda Gates Foundation na Shirika la Afya Ulimwenguni, WHO, utakaolenga katika kufungua vituo maalum vya kuzuia kuenea kwa ugonjwa huu na kutoa tiba inayopunguza athari na kuongeza muda wa kuishi kwa wale wenye virusi.

7. Kuboresha Makazi ya Wananchi Masikini

 1. Kuwahakikishia haki miliki za nyumba za wananchi wanaoishi katika maeneo ambayo hayajapimwa rasmi.
 2. Kuwapa sauti wananchi katika kupima na kupanga miji.
 3. Upatikanaji wa mikopo ya ujenzi wa nyumba bora vijijini na mijini
 4. Kujenga miundombinu kama vile barabara, mifereji ya maji machafu, masoko safi katika maeneo ya miji ambayo hayajapimwa rasmi

8. Barabara

Mawasiliano mabovu ya barabara ni kikwazo kikubwa cha maendeleo ya uchumi na hivyo ni kizingiti katika vita yetu dhidi ya umaskini.

Tutaasisi mpango kabambe wa miaka kumi wa kujenga barabara muhimu za kitaifa zitakazounganisha mikoa yote ya nchi yetu. Katika mpango huu tutaazimia kujenga kilomita 400 za barabara safi za lami kila mwaka

Kila wilaya kuhamasishwa kutayarisha na kuutekeleza mpango wa muda mrefu wa kujenga na kukarabati barabara ziendazo vijijini. Asilimia 50 ya fedha za ushuru wa barabara unaotozwa mafuta ya magari utatumiwa kuimarisha barabara za vijijini.

Ili mali asili na nguvu kazi iliyoko mikoa ya kanda ya ziwa na mikoa ya kusini itumike kikamilifu kuinua maisha ya wananchi wa mikoa hii na Watanzania kwa ujumla, barabara kuu ya Mwanza mpaka Dar es Salaam na Barabara ya kusini inayounganisha Mikoa ya Lindi na Mtwara na Dar es Salaam ni lazima zikamilishwe haraka iwezekanavyo.

9. Utawala Bora na Kupambana na Rushwa

Maendeleo ya Uchumi yatakayoinua hali ya maisha ya wananchi kwa muda mrefu yanahitaji utawala bora wenye sera zilizo wazi na zinazotabirika. Kila mwananchi awe na uhuru wa kumiliki mali aliyoipata kwa njia za halali. Ni wajibu wa serikali kujenga mazingira yatakayomwondolea mwananchi hofu kuwa mali yake aliyoichuma kihalali haitapokonywa na serikali au majambazi kwa kisingizio chochote kile. Sera na utendaji wa serikali uweke mazingira ambayo yatatoa motisha kwa wananchi kufanya kazi kwa bidii na kwa ufanisi ili kujiendeleza kiuchumi na kibiashara.

Rushwa ni adui wa haki, na pia ni adui mkubwa wa maendeleo. Rushwa ni saratani (cancer) inayoua uchumi na kuwanyima wananchi haki ya maisha mazuri na maendeleo.Chanzo kikubwa cha rushwa ni ukiritimba wa madaraka, mishahara midogo ya watendaji serikalini, maamuzi yasiyofuata taratibu zinazoeleweka na kutowajibishwa kwa wanaoshiriki katika vitendo vya rushwa. Vita dhidi ya rushwa itafanikiwa ikiwa ukiritimba wa madaraka utaondolewa, maamuzi ya kiserikali yatafuata taratibu zilizowazi na zinazoeleweka na kuwaadabisha wanaoshiriki katika rushwa.

Nitahakikisha kuwa “SAMAKI WAKUBWA-Sangara na Mapapa” wanaoshiriki katika rushwa wanashughulikiwa kwanza kabla ya kuwashughulikia ‘dagaa’.

Viongozi na watendaji serikalini waliojilimbikizia mali isiyoelezeka kwa vipato vyao halali watafikishwa mahakamani kwa mujibu wa sheria.

Nitateua Mwanasheria mkuu wa serikali na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Jinai (DPP) mwenye usongo dhidi ya rushwa.

Taasisi ya kubinafsisha mahirika ya umma itafanyiwa uhakiki wa utendaji (management audit) wa kina. Mashirika yaliyobinafsishwa katika misingi ya rushwa yatarejeshwa serikalini na kubinafsishwa kwa mujibu wa sheria. Makampuni ambayo hayakutimiza mikataba ya ubinafsishaji yatachukuliwa hatua za kisheria.

Nyumba zote za serikali zilizouzwa kwa viongozi wa serikali bila kufuata utaratibu wa kisheria wa kuuza kwa mnada wa wazi mali ya umma zitarudishwa serikalini.

10. Tanzania Kuingia Fainali ya Kandanda Afrika ya Kusini 2010

Serikali itashirikiana na Tanzania Football Federation (TFF) kuanda Mpango kabambe wa kuifanya Tanzania ifuzu kuingia fainali za kombe la dunia la kandanda (mpira wa miguu) 2010 huko Afrika ya Kusini. Mpango huo utaanza kwa kuimarisha mashindano ya timu za vijana nchini na kuijenga vizuri timu ya taifa ya vijana wa chini wa umri wa miaka 17 (Serengeti Boys) na ile ya vijana wa chini wa umri wa miaka 21.

11. Fedha za Kugharamia Huduma za Jamii na Mipango ya Maendeleo Zitapatikana Wapi?

Mambo yote haya yanahitaji fedha; Je, fedha zitapatikana wapi kuinua viwango vyetu vya elimu, kuongeza huduma za kilimo, kuimarisha huduma za afya na kupambana na ukimwi, kujenga barabara, na kuweka mazingira bora kwa wawekezaji wa ndani na nje ili kuanzisha shughuli za kiuchumi zitakazoongeza ajira?

Kwanza kabisa inatupasa tuelewe kuwa pamoja na majigambo ya serikali ya awamu ya tatu kuwa imeongeza ukusanyaji wa kodi, mfumo wetu wa kodi bado ni mbaya, ambao unawabana wafanyabiashara wadogo na wale wa kati kulipa kodi na wakati huo huo kusamehe makampuni makubwa kwa kisingizio kuwa wao ni wawekezaji. Sehemu ya pato la Taifa linalokusanywa kama kodi limepungua toka asilimia 13.4 mwaka 1996 mpaka kufikia asilimia 11.2 mwaka 1999. Makusanyo ya kodi yameongezeka kidogo kufikia asilimia 12.1 mwaka 2004. Tanzania inakusanya sehemu ndogo ya pato la taifa kama kodi ukilinganisha na wastani wa asilimia 15 wa nchi nyingine za Kiafrika. Kwa kuongeza uwajibikaji wa mamlaka ya kodi, kuondoa misamaha ya kodi isiyo ya lazima, kupunguza viwango vya kodi na kuongeza adhabu ya kukwepa kodi, Tanzania pia inaweza kukusanya alau asilimia 18 – 20 ya pato la taifa kama kodi.

Pili, serikali inawajibika kubana matumizi kwa kuondoa matumizi yote ambayo siyo ya lazima, ikiwa ni pamoja na kupunguza ukubwa wa serikali yenyewe. Tutapunguza safari za nje za viongozi. Serikali yetu itakuwa na wizara chache zisizozidi kumi na tano. Misaada yote toka nje kusaidia elimu, afya, ujenzi wa barabara na mawasiliano haitanyofolewa na kutumiwa kwa matumizi ambayo hayakukusudiwa. Tatu, tunatarajia vita yetu dhidi ya rushwa iwe na msukumo mkubwa katika kupunguza matumizi hewa ya serikali, kuongeza ukusanyaji kodi na kupata malipo ya haki kwa mali ya umma inayobinafsishwa. Nne, tutaweka mazingira mazuri sana kwa wawekezaji kutoka nje na ndani kuweza kuwekeza mitaji yao kwenye huduma za maji, barabara, reli, na mawasiliano.

Pamoja na haya yote, nikichaguliwa kuwa Rais, Serikali itaacha kutumia utaratibu wa sasa wa cash budget. Katika upande wa matumizi udhaifu mkubwa wa bajeti ya Tanzania ni kwamba siyo dira ya utaratibu wa matumizi ya serikali. Ukiondoa malipo ya mishahara na sekta zinazosaidiwa na wafadhili toka nje, matumizi katika sekta nyingine yanapangwa kwa kutegemea kupatikana kwa fedha na siyo kwa kufuata bajeti. Kwa mfano matibabu ya vigogo nchi za nje yanapewa kipaumbele kuliko ununuzi wa madawa ya kuwatibu wananchi waishio vijijini. Utaratibu wa cash budget unakwamisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Hazina wanaupendelea utaratibu wa cash budget unawapa madaraka zaidi ya kugawa fedha baada ya bajeti kupitishwa. Zoezi la kutayarisha bajeti halipewi uzito unaostahili kwani maamuzi ya matumizi yatafanyika baadaye kwa kutegemea mapato yaliyopatikana katika mwezi au robo mwaka. Kwa miaka kumi iliyopita bajeti inayoidhinishwa na Bunge na matumizi halisi katika wizara na sekta mbali mbali ni vitu viwili tofauti kabisa.

Bajeti ya serikali ya CUF itazingatia gharama halisi, na makadirio makini ya mapato. Mapengo ya muda mfupi kati ya matumizi na mapato yatazibwa na mikopo toka Benki Kuu ya Tanzania.

Ili kutekeleza programu ya kutoa huduma za jamii na za kiuchumi serikali itaelekeza matumizi yake katika mambo muhimu na kuacha matumizi ya anasa. Kuthibitisha nia thabiti ya serikali ya kuachana na matumizi ya anasa serikali itaipiga mnada ndege ya kifahari ya Rais Gulf Stream G 550 inayoweza kutua katika viwanja vitano tu hapa nchini.

Serikali itawajibika kubana matumizi kwa kuondoa matumizi yote ambayo siyo ya lazima, ikiwa ni pamoja na kupunguza ukubwa wa serikali yenyewe. Tutapunguza safari za nje za viongozi. Serikali yetu itakuwa na wizara chache zisizozidi kumi na tano.

Tutaongeza mapato ya serikali kwa kufuta misamaha ya kodi inayotolewa kiholela kwa makampuni makubwa.

Sekta ya madini itachangia kwa kiasi kikubwa katika mapato ya serikali. Tutahakikisha katika kila mauzo ya shilingi 1000/- serikali inapata alau shilingi 300/-.

Tutaongeza ukusanyaji wa kodi kwa kuweka viwango vya kodi vya wastani lakini kila anayestahili kulipa kodi atailipa.

Kituo cha uwekezaji – Tanzania Investment Centre kinatumiwa kukwepea na wawekezaji bandia. Uhakiki wa kina wa miradi yote iliyopitishwa na TIC utafanywa na wale wote waliotumia hati zao za uwekezaji kukwepa kodi kinume cha sheria watawajibika kulipa kodi hizo.

12. Serikali ya Umoja wa Kitaifa

Ili kupambana na matatizo makubwa ya rushwa, umaskini na ujenzii wa demokrasia nitaunda serikali ya Umoja wa Kitaifa. Demokrasia ya kweli na ushindani wa kisiasa unaotoa haki sawa kwa washiriki wote, uhuru wa kusema na uhuru wa vyombo vya habari, ni msingi wa utawala bora. Demokrasia ni lengo la maendeleo ya kisiasa lakini pia ni nyenzo ya kujenga uchumi kwani inasaidia sana kuzuia kuenea kwa sarakani ya rushwa. Demokrasi ya kweli inawafanya viongozi wawajibike kwa wananchi. Ili kujenga misingi imara ya demokrasia ya kudumu tunahitaji Katiba nzuri inayowapa uhuru wa kweli watanzania wa kuchagua na kuchaguliwa. Muungano wetu utaimarika ikiwa Watanganyika na Wazanzibari watahisi wana haki sawa katika Muungano huo. Katiba ya sasa haikidhi maendeleo ya demokrasia nchini mwetu. Serikali ya umoja wa kitaifa itaandaa utaratibu wa kupata Katiba ya wananchi yenye misingi imara ya demokrasia.

Katika uchaguzi wa mwaka 1995, kati ya wagombea wanne nilikuwa mtu wa tatu kwa wingi wa kura. Mwaka 2000 nilikuwa wa pili kati ya wagombea wanne. Sina shaka mwaka 2005 itakuwa zamu yangu kuwa mtu wa kwanza na hasa ukizingatia kikwazo changu kikubwa mwaka 2000 kilikuwa ni Mheshimiwa Rais Benjamin William Mkapa. Yeye hawezi kuwa mgombea wa kiti hiki mwaka 2005. Ninawaomba viongozi na wanachama wa vyama vyote vya mageuzi vyenye nia thabiti ya kuing’oa CCM waniunge mkono katika mapambano haya ya kumaliza udhalimu wa CCM na kuleta serikali itakayosimamia Haki Sawa kwa Wananchi Wote na kujenga Uchumi imara wenye maslahi kwa Wananchi wote.

HAKI SAWA KWA WOTE

PROF. IBRAHIM HARUNA LIPUMBA, APRILI 25 2005

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s