Maendeleo ya Jamii: Wanawake

Ingawa wanawake ni asilimia hamsini na moja (51%) ya wananchi wote wa Tanzania, mila na desturi, matatizo ya kihistoria na uzembe wa muda mrefu wa Serikali vimesababisha kuwe na tofauti kubwa ya kifursa kati ya Watanzania wanaume na Watanzania wanawake. Kipaumbele katika fursa zinazogusa masuala mengi muhimu katika jamii kimekuwa kikitolewa kwa wanaume zaidi. Hali hii imewajengea wanawake kutojiamini iwe ni katika masuala ya uongozi, elimu, kazi, na hata katika masuala ya kifamilia. Kwa upande mwingine, hali hii imewajengea wanaume wengi mtazamo hasi juu ya uwezo wa wanawake. Wanaume wengi waliokumbatia mila na desturi, na hasa wale ambao hawakubahatika kupata elimu ya kutosha wamejenga mazoea ya kuwachukulia wanawake kama viumbe duni na wasiokuwa na mchango wowote kifikra na kimaendeleo zaidi ya kuzaa watoto, kutafuta mahitaji ya familia, na kuwatumikia wanaume.

Kwa muda sasa kumekuwa na juhudi za makusudi, na hasa kutoka kwa kina mama wenyewe zenye mwelekeo wa kujaribu kurekebisha hali hii. Sehemu kubwa ya juhudi hizi zimelenga zaidi katika kuhimiza kuwe na upendeleo maalum kwa wanawake. Pamoja na uzuri wa jitihada hizi, ni dhahiri kuwa hazitoshi na bado kazi kubwa inahitajika kufanyika ili hatimaye tofauti za kijinsia zisiwe ni tatizo tena katika upatikanaji wa fursa za kujiletea maendeleo.

Kasoro za CCM

 • Serikali ya CCM imeshindwa kubuni mbinu sahihi zitakazotuhakikishia kuwa matatizo ya ubaguzi dhidi ya wanawake katika upatikanaji wa fursa yanapatiwa ufumbuzi wa kudumu.
 • Serikali ya CCM imeshindwa kuielimisha jamii katika ngazi zote juu ya umuhimu wa kukumbatia haki sawa kwa jinsia zote, na hivyo kuwa ni kikwazo katika kuwaendeleza wanawake.
 • Pamoja na uwakilishi walionao hivi sasa wanawake katika bunge – ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa nafasi za upendeleo – ushiriki wao mdogo katika vyombo mbalimbali vya kutoa maamuzi, unaonyesha kuwa bado hakuna nia ya dhati ya kuleta usawa wa kijinsia katika jamii. Hali hii isingetarajiwa ikizingatiwa kuwa hivi sasa idadi ya wanawake wenye elimu ni kubwa inayotosheleza kuweka uwiano mzuri wa kijinsia katika vyombo mbalimbali vya kufanya maamuzi.
 • Pamoja na kuwepo kwa mifuko mbalimbali kwa ajili ya mikopo ya wanawake, uendeshaji wa mifuko hiyo ni wa kisiasa zaidi na hivyo kufanya wanawake walio wengi, hasa wa vijijini wasinufaike na mikopo hiyo.

Ajenda ya CUF ya Kuleta Mafanikio

Msingi mkuu wa sera za CUF ni ‘Haki Sawa kwa Wote’. Hii inamaanisha kwamba pamoja na CUF kutambua tofauti za makundi mbalimbali ya watu katika jamii, inayatambua makundi yote kuwa ni sawa kutokana na uwananchi wa kila kundi. Wanawake na wanaume ni makundi yenye kutegemeana na hakuna linaloweza kuwa endelevu bila ya jingine. Kwa maana hii basi mfumo dume uliojikita katika kila nyanja ya maisha nchini si chochote zaidi ya kuwa ni ‘kidhibiti mwendo’ katika maendeleo ya taifa letu. Sera za chama chetu kuhusu elimu, afya, na kuondosha umasikini kama zilivyoainishwa katika ilani hii ni kichocheo kikubwa katika suala zima la ukombozi wa mwanamke wa Kitanzania.

Lakini pamoja na sera hizi nzuri, Serikali ya CUF pamoja na mambo mengine itachukua hatua zifuatazo ili kuboresha mazingira ya kujenga usawa wa kijinsia katika uwiano unaofaa:

 • Itatunga sheria itakayotoa adhabu kali kwa mtu yeyote atakayetumia mamlaka yake kumdhalilisha kijinsia, na kumsababishia madhara ya namna moja ama nyingine Mtanzania mwenye jinsia tofauti na ya kwake; ili kujinufaisha binafsi kwa njia moja ama nyingine. Pamoja na manufaa ya sheria hii katika maeneo mengine, sheria hii itasaidia hasa katika suala zima la kupambana na rushwa ya ngono, hususan kwa wanafunzi na waajiriwa wa kike.
 • Itauboresha utaratibu uliopo hivi sasa ambao unatoa nafasi maalum za upendeleo kwa wanawake ili kuongeza ushiriki wao katika ngazi mbalimbali za maamuzi ya kisiasa, utawala, menejimenti na uongozi.
 • Ili kuwanyanyua wanawake kiuchumi serikali ya CUF itaiimarisha mifuko mbalimbali ya mikopo na kuisimamia kusudi iwanufaishe wanawake walio wengi wa mijini na vijijini bila kujali itikadi zao za kisiasa.
 • Serikali ya CUF itawaunganisha wanawake wote bila kujali itikadi zao, kuunda chombo chao huru ambacho kitasimamia maslahi yao.
 • Hata hivyo kwa kuwa CUF inaelewa fika kuwa suluhisho la kudumu la matatizo ya kijinsia nchini liko katika kubadilisha mtizamo wa jamii kuliko katika kuweka mashinikizo ya kisheria na kutoa upendeleo, basi hatua zifuatazo za ziada zitachukuliwa:
 • Kwa kuwa tafiti zinaonyesha kuwa mabinti wanaosoma katika shule za peke yao mara nyingi wanajenga kujiamini kuliko wale wanaosoma katika shule mchanganyiko, serikali itahakikisha kuwa kunakuwa na marekebisho katika mashule ambapo mkazo mkubwa utakuwa kulifundisha kila kundi peke yake.
 • Mitaala ya somo la uraia mashuleni itafanyiwa marekebisho ili pamoja na mambo mengine somo hilo lilenge katika kufifisha mitizamo ya vijana wa kiume dhidi ya wenzao wa kike kuwa ni viumbe duni, dhalili, na wasio na mchango wowote wa maana kifikra katika jamii.
 • Serikali itaanzisha na kuhimiza mjadala wa kina na wa wazi kitaifa katika ngazi mbalimbali za jamii kuhusu mgawanyo wa wajibu, majukumu, na haki katika mahusiano ya kijinsia, kwa nia ya kuboresha mahusiano hayo.

PREVIOUS… NEXT…

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s