Huduma za Uzalishaji Mali: Umeme

Nishati na maji ni muhimu katika maendeleo ya uchumi wa kisasa. Matumizi ya mashine, iwe ya viwandani, matrekta ya mashambani, au vyombo vya usafirishaji, n.k. hutegemea nishati na maji kujiendesha. Hivyo basi ili uweze kupata ufanisi wa juu kutoka kwenye mashine ni sharti kwanza kuwepo na uwekezaji wa kiasi cha kutosha kwenye sekta za nishati na maji ili kuhakikisha huduma hizi zinapatikana kwa bei ya kuridhisha. Tanzania ina udhaifu mkubwa sana katika sekta za nishati na maji.

Umeme – ambayo ndiyo nishati kuu kwa matumizi ya mitambo viwandani (na inapaswa kuwa na majumbani pia ili kupunguza matumizi ya kuni na mkaa kwa lengo la kulinda mazingira) unazalishwa kwa kiwango kidogo, kwa ufanisi mdogo na bei yake ni kubwa sana.

Uzalishaji umeme nchini Tanzania kwa asilimia 90 unategemea maji ya mvua. Hili lisingekuwa ni tatizo sana kama hifadhi ya maji haya kwenye mabwawa ya kuzalishia umeme ingekuwa ni ya uhakika. Kwa bahati mbaya sana uhakika huo haupo. Zaidi ya maji, TANESCO pia huzalisha umeme kwa kutumia mafuta ya dizeli na hivi karibuni gesi ya Songosongo. Mitambo inayotumia dizeli ya kampuni ya IPTL ambayo ilijengwa mwanzoni mwa miaka ya tisini kwa ajili ya kuzalisha umeme wa kuiuzia TANESCO siyo tu kwamba haijasaidia kuondoa tatizo la umeme, lakini pia imekuwa ni mzigo mkubwa kwa watumiaji. TANESCO inailipa kampuni ya IPTL mabilioni ya fedha kila mwezi na kuhamishia gharama hizo kwa wateja wake.

Ilitarajiwa kuwa tatizo la umeme lingepungua sana baada ya TANESCO kuanza kutumia gesi ya songosongo. Hata hivyo pamoja na kuanza kuitumia gesi hiyo matatizo ya umeme kwa wateja yamebaki palepale, kama siyo kuongezeka. Pamoja na serikali ya CCM kuifukuza menejimenti ya wazalendo ya TANESCO na kuiajiri kampuni ya NET GROUP SOLUTIONS katika mazingira yaliyojaa utata ili kuliendesha shirika hilo, kukatika hovyo kwa umeme kumekuwa ni jambo la kawaida. Ni vigumu kusema tatizo hili linatokana na nini hasa, lakini tunadhani sababu kubwa ni uchakavu wa mitambo ya TANESCO. Kama ni hivyo inabidi tujiulize ni kwa nini uchakavu huu haupatiwi dawa ikizingatiwa kuwa TANESCO inauza umeme wake kwa kwa bei za juu mno ikilinganishwa na nchi zote za jirani, na kwa muda mrefu shirika hilo lilikuwa likinufaika kwa ruzuku iliyokuwa inatoka kwenye mfuko wa NISHATI.

Mpaka miaka mitatu iliyopita, kila mwaka kupitia katika manunuzi tunayofanya ya bidhaa za petroli, Watanzania tulikuwa tunaichangia serikali kiasi cha wastani wa Dola za Kimarekani zaidi ya milioni Kumi kuingia kwenye mfuko wa nishati. Sehemu kubwa ya fedha hizi ilikuwa inakwenda TANESCO kama ruzuku kuiwezesha kuimarisha miundombinu yake. Sasa kama hivi ndivyo, kulikoni TANESCO?

Kasoro za CCM

  • Bila ya shaka makucha ya UFISADI ambayo yamejikita kila mahala chini ya Serikali ya CCM, hadi kuteketeza takriban kila nyanja ya maisha ya Mtanzania yanaiparua na TANESCO pia mitambo chakavu ya TANESCO inayosababisha umeme ukatike ovyo ni kielelezo tosha kuwa siyo tu kuwa fedha za mfuko wa nishati zilikuwa zikitafunwa kwa miaka mingi bila kufanyia kazi iliyokusudiwa, lakini pia kuwa kuna ubadhirifu mkubwa katika shirika hilo.
  • Uchambuzi unaonyesha kuwa pamoja na TANESCO kuwa na matatizo mengi tangu wakati ikiwa chini ya menejimenti ya umma, matatizo hayo yameongezeka kwa kiasi kikubwa baada ya menejimenti hiyo kufukuzwa na nafasi yake ikachukuliwa na menejimenti ya kigeni. Hali hii inaonyesha kuwa serikali ya CCM iliiajiri menejimenti hii ya kigeni bila kuwa na uhakika wa uwezo wake.
  • TANESCO imekuwa na malalamiko ya muda mrefu kuwa baadhi ya wateja wake wamekuwa wakiliingizia shirika hilo hasara kwa kuwa na malimbikizo ya bili ya muda mrefu. Kwa upande mwingine wateja nao wamekuwa wakilalamika kuwa bili wanazoletewa na TANESCO ni kubwa mno na kuwa hazilingani na matumizi halisi ya umeme. Serikali ya CCM imeshindwa kufanya uchunguzi na kutoa kauli juu ya madai ya pande hizi.
  • Malalamiko ya TANESCO kwa upande mmoja, na malalamiko ya wateja kwa upande mwingine yangeweza yakapatiwa suluhisho kupitia matumizi ya mita za LUKU. Uchunguzi unaonyesha kuwa gharama za umeme wanazolipa wateja wenye LUKU ni nusu au chini zaidi ya nusu ya zile wanazolipa watumiaji wa mita za kawaida. Aidha uchunguzi unaonesha kuwa chanzo cha tofauti hizi ni wasoma mita wa TANESCO kukadiria matumizi ya umeme ya juu zaidi kuliko yale halisi yanayosomeka kwenye mita za wateja. Haieleweki ni kwa nini TANESCO iliamua kusimamisha utaratibu wa usambazaji wa mita za LUKU, lakini kwa vyovyote vile inatia shaka iwapo uamuzi huo ni kwa manufaa ya shirika hilo au wateja wake.

Ajenda ya CUF ya Kuleta Mafanikio

Ili kuondoa matatizo sugu ya umeme yanayoikabili nchi yetu, Serikali ya CUF, pamoja na mambo mengine itachukua hatua zifuatazo:

  • Uzalishaji na ugavi wa umeme. Shirika lililopewa kuiendesha TANESCO la NET GROUP SOLUTIONS inavyoekekea halijui linachokifanya kwani hivi sasa matatizo ya umeme nchini ni makubwa kuliko hata wakati TANESCO ilipokuwa chini ya menejimenti ya wazalendo. Serikali ya CUF itaupitia upya mkataba ulioiingiza kampuni hiyo kwenye menejimenti ya shirika hilo na iwapo yatabainika mapungufu yoyote mkataba huo utasitishwa mara moja. Aidha serikali itatafuta wabia miongoni mwa makampuni yanayoaminika ulimwenguni kwa ajili ya kushirikiana nao kuliendesha shirika hilo kwa nia ya kuvuta mitaji mipya, tekinolojia mpya na utaalamu. Hata hivyo pamoja na TANESCO kuwepo, serikali itaweka huru shughuli za uzalishaji wa umeme, ili pamoja na kuongeza ushindani katika soko huduma hii muhimu iweze kusambaa kwa wananchi wengi zaidi kwa haraka na kwa gharama nafuu.
  • Uanzishaji wa vyanzo vipya vya umeme. Pamoja na serikali kuendelea na mpango wa kuibadili nishati ya kemikali iliyomo kwenye gesi ya SongoSongo kuwa nishati ya umeme, serikali pia itatafuta wawekezaji watakaowekeza kwenye ujenzi wa vinu vya kuzalisha umeme kutokana na vyanzo vingine, mathalan kwa kutumia mali ghafi ya makaa wa mawe kutoka katika mgodi wa Kiwira. Hili ni muhimu ili kutuhakikishia kuendelea kupata umeme wa kutosha hata kama kutakuwa na tishio la ukame litakaloathiri uzalishaji wa umeme wa maji.
  • Matumizi ya fedha za mfuko wa nishati. Mwaka 2000 serikali ya CCM ilifuta kodi ya nishati iliyokuwa ikitozwa kwenye bidhaa za petroli. Nia ilikuwa kujaribu kudhibiti mfumuko wa bei katika bidhaa za petroli ulioanzia kwenye kupanda kwa bei ya bidhaa hizo kwenye soko la ulimwengu, na kukaziwa na hatua ya serikali ya kutoza VAT kwenye bidhaa hizo. Hata hivyo kusudio hilo limefeli, kwani hivi sasa bidhaa za petroli zinauzwa kwa bei ya juu kuliko wakati mwingine wowote wa historia ya nchi yetu. CUF inaamini kuwa bado kuna umuhimu wa mfuko wa nishati katika uimarishaji wa sekta ya nishati nchini. Sehemu ya kodi ya VAT katika bidha za petroli itawekwa katika mfuko wa nishati. Fedha zote za mfuko wa nishati zitatumiwa kupelelekea huduma ya umeme vijijini.
  • Nishati ya jua, upepo na samadi na mabaki ya mimea. Serikali itahamasisha matumizi ya nishati mbadala kwa kufuta ushuru wote kwenye vifaa vinavyotumika kuzalisha umeme kutokana na nishati ya jua, upepo na samadi na mabaki ya mimea ili kuharakisha usambazaji wa umeme katika maeneo ya vijijini.

PREVIOUS… NEXT…

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s