Seif aitaka CCM iige Zimbabwe

2008-09-17 09:20:56

 

Na Mwinyi Sadallah, Zanzibar

 

Chama cha Wananchi (CUF) kimesema mgawanyo wa madaraka Zanzibar kati yake na Chama cha Mapinduzi (CCM) ndilo suluhisho pekee la kumaliza mpasuko wa kisiasa uliozuka visiwani humo tangu mwaka 1995.

 

Kauli hiyo ilitolewa jana na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Shariff Hamad, alipokuwa akizungumza na Nipashe katika mahojiano maalum, kufuatia mwafaka wa kisiasa nchini Zimbabwe kati ya vyama vya Zanu-PF na Movement for Democratic Change (MDC).

 

Hamad alisema iwapo rais atatoka chama tawala, msaidizi wake ambaye ni Waziri Kiongozi atoke chama cha upinzani, kama utaratibu wa kugawana madaraka uliotumika Zimbabwe na Kenya.

 

Alisema CUF haina tatizo na mfumo wa kugawana madaraka kwa sababu ni njia kugawana madaraka kwa sababu ni njia pekee ya kumaliza mitafaruku ya kisiasa na kuleta umoja wa kitaifa.

 

Mpasuko wa kisiasa Zanzibar ulilipuka baada ya kufanyika Uchaguzi Mkuu wa kwanza chini ya mfumo wa vyama vingi mwaka 1995, ambapo mgombea wa urais wa CCM, Dk. Salmin Amour alishinda kwa asilimia 50.2 dhidi ya Hamad aliyegombea kwa tiketi ya CUF na kupata asilimia 49.8.

 

Matokeo hayo yalikataliwa na CUF kwa madai kuwa kura za mgombea wao ziliibwa na CCM na hivyo kusababisha mpasuko mkubwa wa kisiasa.

 

Jumuiya ya Madola kupitia kwa aliyekuwa Katibu Mkuu wake, Chifu Emeka Anyauku na mjumbe wake, Dk. Moses Anafu iliingilia kati kuvisuluhisha CCM na CUF na kufanikisha kusainiwa kwa mwafaka uliosainiwa na vyama hivyo Juni, mwaka 1999 katika Ikulu ya Zanzibar.

 

Hata hivyo, mwafaka huo haukudumu kutokana na viongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kukaidi kutekeleza baadhi ya mambo yaliyokubaliwa.

 

Matokeo ya hali hiyo ni kuzuka kwa machafuko mengine makubwa ya kisiasa Januari 26 na 27, mwaka 200, wakati polisi walipowaua wafuasi wa CUF zaidi ya 30 waliokuwa wakiandamana kupinga ushindi wa CCM baada ya kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000, ambao Rais Amani Abeid Karume alimshinda Hamad.

 

Waandamanaji hao pia walikuwa wakishinikiza kurudiwa kwa uchaguzi huo.

Baada ya machafuko hayo yaliyosababisha mamia ya wafuasi wa CUF kukimbilia Shimoni, Mombasa nchini Kenya kutafuta hifadhi

 

Makatibu wakuu wa CCM na CUF walianzisha mchakato wa mazungumzo ya kuacha uhasama na kuzaa mwafaka wa pili uliosainiwa na makatibu hao, Philip Japhet Mangula kwa upande wa CCM na Hamad kwa upande wa CUF na kushuhudiwa na wenyeviti wao, Benjamin Mkapa na Profesa Ibrahim Lipumba

 

Hata hivyo, mwafaka huo nao ulikwama baada ya CUF kulalamikia na kutoyatambua matokeo ya urais wa Zanzibar katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005, hali iliyomlazimisha Rais Jakaya Kikwete kuvitaka vyama hivyo kurejea katika mazungumzo ya kusaka mwafaka chini ya makatibu wakuu, ambayo yalikamilika kwa makubaliano ya kugawana madaraka.

 

Hata hivyo, mazungumzo hayo yamekwama baada ya CCM kutoa azimio la Butiama Machi, mwaka huu likitaka Wazanzibari kuamua mgawanyo wa madaraka kupitia kuundwa kwa serikali ya mseto kupitia kura ya maoni.

 

Katika mahojiano ya jana, Hamad aliwataka viongozi wa kisiasa kutoka CCM kujifunza kutoka Zimbabwe kwa kuweka maslahi ya taifa mbele badala ya maslahi binafsi ili kumaliza mivutano inayodumaza demokrasia na kukwaza maendeleo

 

“Hakuna lisilowezekana, tatizo wenzetu wa CCM hawana nia njema ya kumaliza mpasuko wa kisiasa uliojitokeza na ndio maana mazungumzo yamekwama,” alisema.

 

Alisema mapendekezo yaliyofikiwa katika Kamati ya Mazungumzo ya CCM na CUF, kama yangepitishwa na Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) huko Butiama kama yalivyo bila ya kukwamishwa, basi mwafaka wa Zanzibar ungefikiwa.

 

Alieleza kwamba kimsingi, Kamati ya mazungumzo iliyokuwa ikiongozwa na mwanasiasa mkongwe wa CCM, Kingunge Ngombale-Mwiru na Hamad Rashid Mohamed wa CUF ilishamaliza kazi yao na kilichobaki ni utekelezaji wa mambo yaliyokubaliwa.

 

“Naungana na wote wanaompongeza Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika Rais Jakaya Kikwete, lakini napenda kukumbusha asiwe ngariba wa Kilwa,” alisema Hamad.

 

Alisema inashangaza kwa kuwa Rais Kikwete amekuwa mstari wa mbele kushughulikia migogoro ya nje kama ya machafuko ya uchaguzi yaliyotokea Kenya na Zimbabwe wakati tatizo la Zanzibar linawekwa kiporo.

 

Rais Kikwete,ambaye ni Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU) alishiriki kusaka mwafaka kati ya vyama vya ODM na PNU nchini Kenya Februari mwaka huu na kuwezesha kuundwa kwa serikali ya kitaifa, ambapo Rais Mwai Kibaki alichukua urais na Raila Odinga akachukua uwaziri mkuu.

 

Rais Kikwete pia amehusika katika kuhimiza mwafaka wa kisiasa Zimbabwe ambao ulisainiwa juzi na Rais Robert Mugabe na Morgan Tsvangirai, ambaye sasa atakuwa waziri mkuu.

 

Alisema matatizo ya kisiasa ya Zanzibar kwa kiasi kikubwa yamechangia kuzorotesha hali ya uchumi na uimarishaji demokrasia na kuonya kwamba bila ya mwafaka wa kweli, Zanzibar inaelekea kubaya.

 

Alisema iwapo serikali ya umoja wa kitaifa itaundwa Zanzibar, itaweza kuweka mazingira mazuri hasa ya sheria za uchaguzi na hivyo chaguzi zijazo kuwa huru na haki.

Hata hivyo, alisema kwamba CUF haiko tayari kurudi katika mazungumzo ya mfumo wa Kamati ya Kingunge na Hamad Rashid kwa vile kamati hizo zimeonekana hazina nguvu ya maamuzi yanayofikiwa.

 

Agosti 21 wakati Rais Kikwete, alipokuwa akihutubia Bunge, alisema kuwa mazungumzo ya mwafaka wa CCM na CUF yamekwama kutokana na viongozi wa CUF na CCM kutokuaminiana.

 

Hata hivyo, alisema kwamba nia yake bado iko pale pale kuhakikisha mpasuko wa kisiasa Zanzibar unapatiwa ufumbuzi kwa lengo la kuimarisha umoja wa kitaifa.

 

SOURCE: Nipashe

 

 

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s