CUF na Umma

The Civic United Front (CUF - Chama cha Wananchi)

UANACHAMA: HAKI NA WAJIBU WA MWANACHAMA NDANI YA CUF

Mtu anayeweza kuwa Mwanachama wa CUF

7 (1) Mtu yeyote yule:

(a)  ambaye ni raia wa Tanzania, na

(b)  ambaye amefikia umri wa miaka 18 au zaidi,

(c)  ambaye anakubaliana na madhumuni, imani, itikadi na sera za chama; na

(d)  ambaye si mwanachama wa chama kingine cha siasa, anaweza kuomba kujiunga na chama hiki na ikiwa atakubaliwa na vikao vinavyohusika, atakuwa ni mwanachama wa chama hiki.

Namna ya Kuomba Uanachama

(2)  Mtu yeyote anayeomba kuwa mwanachama:

(a)  atajaza fomu ya maombi na kuiwasilisha kwenye tawi lililoko katika eneo lake.

(b)  ataorodheshwa katika daftari la wanachama la tawi hilo pindi ikiwa amekubaliwa.

(c)  mara baada ya kukubaliwa ombi lake atalipa kiingilio na kupewa haki ya uanachama na baadaye atalipa ada ya kila mwezi kama zitakavyopangwa na Baraza Kuu la Uongozi  Taifa la Chama.

Mamlaka na Ruhusa ya Kuwa Mwanachama

(3) Mtu yeyote aliyeomba kuwa mwanachama na akakataliwa anaweza kuomba tena baada ya kipindi cha miezi sita kupita akikataliwa mara ya pili, ataweza kukata rufaa kwenye ngazi ya kata au jimbo ambalo tawi lake limo, na kama atakataliwa ataweza kukata rufaa katika ngazi ya wilaya kwa uamuzi wa mwisho.

(4) Mamlaka yote ya kuingiza mwanachama mpya katika chama hiki yako chini ya tawi ambalo mwanachama huyo anaishi au ameomba kuwa mwanachama wa tawi hilo.

Masharti ya Uanachama

8. Mtu yeyote atakayekubaliwa kuingia katika chama au kuendeleakuwa mwanachama atatakiwa atimize masharti yafuatayo na yale ambayo mara kwa mara yatawekwa na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa au chombo chengine chochote cha chama kinachohusika:

(1) awe ni mtu anayelinda na kuitetea Katiba ya chama na kanuni zake pamoja na kuineza kuieleza na kuitekeleza itikadi ya Utajirisho ya chama na sera za chama zitokanazo na itikadi hiyo.

(2) awe ni mtu mwenye kuheshimu watu na uhuru wao wa kibinadamu, serikali halali za nchi, Bunge au Baraza la Wawakilishi pamoja na mahakama zilizowekwa kwa mujibu wa Katiba za nchi.

(3) awe ni mtu anayependa mashirikiano na wenzake,

(4) awe ni mtu mwenye uchu wa kuleta maendeleo nchini.

Kusita kuwa Mwanachama

9 (1) Mwanachama yeyote atasita kuwa mwanachama ikiwa:

(a) atajiuzulu mwenyewe, au

(b) atafukuzwa au kuachishwa uanachama na tawi lake kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii, au

(c) atafukuzwa au kuachishwa uanachama na Mkutano Mkuu wa Taifa au na Baraza Kuu la Uongozi kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii, au

(d) atasita kulipa ada ya chama kwa kipindi cha mwaka mmoja mfululizo, au

(e) atashindwa kuheshimu Katiba ya Chama au kutoheshimu masharti ya uanachama, au

(f) atachukua uraia wa nchi nyingine, au

(g) atakuwa mwanachama wa chama chengine cha siasa.

(2) Mtu yeyote aliyeacha uanachama chini ya kifungi 9(1) (b), (c),(d) au (e) ataweza kukata rufaa kwa ngazi ya juu yake ila ijulikane tu kwa wale waliofukuzwa au waliothibitishwa kufukuzwa kwao na Mkutano Mkuu wa Taifa basi hakuna chombo chengine chochote kitacho zungumzia uamuzi huo.

(3) Mtu yeyote anayepoteza uanachama wake chini ya kifungu 9(1) atapoteza haki zake zote za uanachama na hatorudishiwa ada, zawadi, au ruzuku yoyote aliyokwisha itoa kabla ya kupoteza uanachama huo.

(4) Uwezo wa kumuachisha uanachama mwanachama yeyote wa kawaida au kiongozi wa chama wa tawi umo mikononi mwa tawi lake na au Baraza Kuu la Uongozi la Taifa .

(5) Mwanachama yeyote ambaye ana wadhifa katika chama au serikali anaweza kuachishwa uanachama na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa au Mkutano Mkuu wa Taifa kwa kadiri ya katiba inavyoeleza.

(6) Mwanachama yeyote aliyefukuzwa, kuachishwa au kujiuzulu uanachama kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii hatoweza kugombea nafasi ya uongozi wowote ule wa chama au serikali kupitia chama mpaka ipite miaka miwili kuanzia siku aliyofukuzwa au aliyojiuzulu au aliyoachishwa.

(7) Mwanachama yeyote aliyeachishwa au aliyefukuzwa uanachama anaweza kujiunga tena na chama baada ya kupindukia miaka miwili tokea aachishwe ikiwa atapeleka maombi yake kwa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa na kukubaliwa.

Haki za Mwanachama

10. Kila mwanachama atakuwa na haki zifuatazo:

(1) kushiriki kwa ukamilifu katika shughuli zote za chama zinazomuhusu.

(2) kuhudhuria, kushiriki katika mijadala ya vikao vya chama na kupiga kura pale anapohusika katika vikao vinavyomhusu ambavyo ana wajibu wa kuhudhuria.

(3) kuchagua na kuchaguliwa katika uongozi, ujumbe au uwakilishi wa chama, au serikali kwa kupitia chama.

(4) kuonana na kiongozi yeyote wa chama kwa kufuata taratibu zilizowekwa.

(5) kujitetea mbele ya chombo chochote cha Chama kinachotaka kumchukulia hatua za nidhamu dhidi yake, na kuomba kukata rufaa hadi kufikia ngazi ya mwisho ikiwa hataridhishwa na uamuzi uliokwishatolewa. Taarifa ya kukata rufaa itolewe na muhusika ndani ya siku 14 tangu mwanachama huyo kuchukuliwa hatua au rufaa yake kukataliwa na kusikilizwa kwa rufaa hiyo iwe katika kikao chochote kinachofuatia cha ngazi ambayo inasikiliza rufaa hiyo.

(6) kumkosoa kiongozi, mwanachama au mfanyakazi wa Chama kwa kufuata taratibu zilizowekwa.

Wajibu mwa Mwanachama

11. Kila mwanachama atakuwa ana wajibu ufuatao:

(1) kuijua, kuikubali, kuilinda na kuitetea imani ya chama pamoja na madhumuni yake.

(2) kuyafahamu malengo ya chama na kuweza kuyajadili, kuyaunga mkono, kuyasahihisha au  kuyapinga  kwa nguvu za hoja thabiti katika vikao vya chama.

(3) kukieneza chama kwa kushiriki kuingiza wanachama wapya na kueneza siasa za chama kadiri ya uwezo wake wote.

(4) kukiunga mkono chama kwa kuwapigia kura wanachama wanaogombea nafasi yoyote katika uchaguzi wa nchi utakaohusisha vyama vingine vya siasa.

(5) kulinda heshima ya Chama kwa kuwa na tabia njema, kutekeleza masharti ya Katiba ya chama, kutii kanuni za chama, kutii sheria na sheria ndogo ndogo za serikali iliyoundwa kihalali na pia, kwa busara, kukosoa utekelezaji mbaya wa serikali kwa hoja za msingi ili kuendeleza maslahi ya chama, yake mwenyewe, ya wanachama wenzake, ya nchi na ya raia wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

(6) kuwa mwaminifu kwa chama na Serikali zilizoundwa kihalali na kwa ridhaa ya wananchi na kuwa tayari kuwatumikia watu kwa juhudi na vipaji vyake vyote.

(7) kuhudhuria vikao vya Chama vinavyomhusu na vile alivyoalikwa kwa barua au kwa simu au fax au kwa ujumbe wa afisa wa chama.

(8) kuimarisha umoja na kujenga mapenzi baina ya wananchi kwa kuwa raia mwema, kuwaheshimu watu na kuwasaidia wasiojiweza, wazee na watoto kila inapowezekana.

(9) kuwa tayari kupambana na namna yoyote ya uonevu, ukandamizaji, udhalilishaji na ubaguzi.

(10) kujielimisha zaidi ili aweze kukabiliana na dhamana zote atakazopewa na chama au Dola ili azitekeleze vyema kwa maslahi ya wanachama na wananchi wote wa Tanzania.

(11) kulinda na kutetea haki za binadamu na haki za watu popote duniani pale wanapoonewa au kudhulumiwa na dola au serikali zao.

(12) kutumia uhuru na haki zake bila ya kuingilia uhuru na haki za mwenzake na kuheshimu maoni ya wengine.

(13) kushirikiana na serikali ya nchi na kujitolea muhanga  nafsi yake pale adui wa nje anapoivamia nchi yetu kwa uhasama au ubabe wa aina yoyote ile.

(14) kupambana na serikali yoyote ya nchi kwa njia za demokrasia na hoja ikiwa serikali hiyo imeanza au itaanzisha mfumo wa utawala wa ubabe na mabavu kwa raia wake.

(15) kukilinda chama kutokana na maadui wa ndani au wa nje wanaokusudia kukiua, kukigawa au kukidhoofisha


KWA MAWASILIANO ZAIDI, TAFADHALI WASIALIANA NASI:

1. Mbaralah Maharagande

Kaimu Mkurugenzi Haki za Binaadamu na Mahusiano ya Umma

Simu: +255 773 062 577

2. Salim Bimani

Naibu Mkurugenzi Haki za Binaadamu na Mahusiano ya Umma

Simu: +255 777 414 112

3. Ismail Jussa

Msaidizi Maalum wa Katibu Mkuu

Mambo ya Nje na Mahusiano ya Kimataifa

Simu: +255 777 414 100

Ama tunakuomba utuandikie kwa kutumia hakinaumma@yahoo.co.uk au wacha maoni yako kwenye kisanduku cha CUF Maoni.

Kurugenzi ya Haki za Binaadamu na Mahusiano ya Umma inakushukuru kwa kutembelea Web Blog hii.

Tafadhali tutumie maoni yako. Tunakuomba usisahau kuandika mada ya kile unachokitolea maoni.

(c) 2008, Kurugenzi ya Haki za Binaadamu na Mahusiano ya Umma, CUF

Wajanja wote sasa wamejiunga na CUF kuwa sehemu ya mabadiliko ya kweli ya taifa hili. Kwa nini wewe uwe sehemu ya mafisadi na usije kwa wajanja wenzako kuikoa Tanzania yetu?

Wajanja wote sasa wamejiunga na CUF kuwa sehemu ya mabadiliko ya kweli ya taifa hili. Kwa nini wewe uwe sehemu ya mafisadi na usije kwa wajanja wenzako kuikoa Tanzania yetu?

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s