Zanzibar yawaka tena

Na Mwinyi Sadallah, Zanzibar

Naibu Mkurugenzi wa Haki za Binaadamu na Mahusiano ya Umma wa CUF, Salim Bimani

Naibu Mkurugenzi wa Haki za Binaadamu na Mahusiano ya Umma wa CUF, Salim Bimani

Hotuba iliyotolewa bungeni mjini Dodoma Agosti 21 mwaka huu na Rais wa Jamhuri ya Muungano, Bw. Jakaya Kikwete, kufafanua kuhusu hadhi ya Zanzibar inaonekana kuwa haijasaidia kuzima mjadala uliozuka kuhusu Zanzibar ni nchi ama la. Hali hiyo imethibitishwa na kusambazwa kwa vikaratasi katika mitaa ya Unguja juzi, vinavyozidi kudai kwamba Zanzibar ni nchi.

Katika hotuba yake, Rais Kiwete alisema kimsingi katika mambo ya nje, Tanzania na Zanzibar zinatambulika kama nchi moja ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliyoundwa Aprili 26, mwaka 1964 baada ya nchi hizo kuungana.

Lakini Rais Kikwete aliliambia Bunge kuwa, katika mambo ya hapa nchini Zanzibar inatambulika kama nchi kama ilivyo kwa Tanganyika.

Rais Kikwete alilazimika kuzungumzia jambo hilo kufuatia kuibuka kwa mjadala uliokuwa umeigawa nchi huku kundi moja likisema kuwa Zanzibar ni nchi na lingine likisema siyo, bali ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano.

Mjadala huo uliowahusisha wanasiasa, wabunge, wawakilishi na vigogo kadhaa wa Serikali ya mapinduzi Zanzibar (SMZ) uliibuka baada ya Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda, kusema bungeni katika mkutano wa Bunge ulioahirishwa Ijumaa iliyopita kuwa, Zanzibar siyo nchi yenye mamlaka kamili, bali ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Bw. Bakari Khatibu Shaaban, alithibitisha jana kusambazwa kwa vikaratasi hivyo na kusema kuwa uchunguzi wa polisi umeanza ili kubaini waliohusika na vitendo hivyo ili kuwachukulia hatua za kisheria.

“Ni kweli, tumepata vikaratasi hivyo na tumeanzisha uchunguzi,” alisema Kamanda huyo alipozungumza na Nipashe kuhusu vikaratasi hivyo vilivyopigwa chapa kwa kutumia mashine ya kompyuta.

Kamanda Shaaban alisema ni mapema kufahamu ni kikundi gani kilichohusika na vitendo hivyo na kuongeza kwamba sio vizuri kuanza kunyooshea kidole chama cha siasa au vikundi vingine kabla ya uchunguzi.

Vikaratasi hivyo vilikuwa na kichwa cha habari “Heri Muungano uvunjike, tubaki na Zanzibar yetu” na kuonya kwamba hawatokuwa tayari kuona viongozi wa Zanzibar wakiadhibiwa kutokana na mjadala wa hadhi ya Zanzibar uliojitokeza kuhusu hadhi ya Zanzibar katika Muungano wa Tanzania.

Sehemu nyingine ya vikaratasi hivyo inasema: “… yeyote atakayewaadhibu viongozi wetu sisi Wazanzibari hatutokubali na Zanzibar ni nchi kamili na ina mambo yake kamilifu.”

Vikaratasi vilizidi kusema: “Tanganyika ina mambo kumi na mbili tu, sisi Wazanzibari tunasema turejeshewe mamlaka yetu kama zamani, yanayohusu sisi Wazanzibari. Mbona nyinyi mambo yenu hatuwaingilii?”

Vikaratasi hivyo ambavyo Nipashe ina nakala zake, vilizidi kusema: “Mabadiliko ya kumi na moja ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya 1977 yalifanyika kwa malengo ya kutaka kuwaburuza Wazanzibari kwa kuanzisha nafasi ya Makamu wa Rais badala ya Rais wa Zanzibar kwa wadhifa wake kuwa moja kwa moja Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano.”

Aya nyingine kwenye vikaratasi hivyo inasema: “Na hao wanaotaka iundwe serikali moja sisi Wazanzibari hatutaki na haiwezekani, bora tubaki na Zanzibar yetu. Tumechoka kuburuzwa na Watanganyika.”

Katibu Mwenezi wa CCM Zanzibar, Bw. Vuai Ali Vuai, alisema kwamba CCM haihusiki na vikaratasi hivyo kwa sababu ni chama cha heshima na ustaarabu na wanachama wao wana utaratibu mzuri uliowekwa na chama wa kutoa maoni au malalamiko yao kuanzia ngazi ya shina mpaka ngazi ya Taifa.

Naibu Mkurugenzi wa Haki za Binadamu na Mawasiliano ya Umma wa CUF, Bw. Salum Bimani, alisema kwamba CUF haihusiki na vikaratasi hivyo lakini alisema kwamba inawezekana kitendo hicho kimefanywa na wananchama wa CCM waliokasirishwa na kauli iliyotolewa na Bw. John Chiligati, Katibu Mwenezi wa CCM Taifa.

Bw. Chiligati alikaririwa katika vyombo vya habari hivi karibuni akisema kwamba, mjadala wa suala la Muungano umefungwa na mwanachama yeyote wa CCM atakayeendelea kujadili suala hili atachukuliwa hatua za nidhamu.

Aidha, Bw. Bimani alisema: “CUF haina tabia ya kuzungumza mambo kwa milango ya nyuma. Liwe jambo chungu au tamu litasemwa hadharani.”

Naye Katibu Mkuu wa National Reconstruction Alliance (NRA), Bw. Suleiman Gaddafi, alisema kwamba chama chake hakihusiki na vikaratasi hivyo licha ya polisi kuzuia maandamano yao yaliyopangwa kufanyika wiki iliyopita kwa ajili ya kupinga kauli iliyotolewa na Waziri Mkuu kwamba Zanzibar sio nchi.

Hata hivyo, alisema kwamba ni vyema wananchi wakaachiwa kujadili suala la Muungano kwa uwazi na Serikali ikayafanyia kazi maoni yatakayotolewa ili kuuboresha Muungano wa Tanzania ulioasisiwa mwaka 1964 na aliyekuwa Rais wa Tanganyika, marehemu Mwalimu Julius Nyerere na aliyekuwa Rais wa Zanzibar, marehemu Abeid Amani Karume.

Vijikaratasi hivyo vilitawanywa baada ya maandamano ya CCM yaliyopangwa kufanyika jana mjini Zanzibar kupongeza hotuba ya Rais Kikwete kuvunjwa ghafla na waandaaji wake wa Mkoa wa Mjini Magharibi na hakuna sababu yoyote iliyotolewa.

Mjadala huo ulichukua sehemu kubwa katika vikao vya Baraza la Wawakilishi Zanzibar na Bunge huku wajumbe wakigawanyika kwa misingi ya upande wa Tanzania Bara na Zanzibar na kuzua hofu kubwa kwa wananchi kutokana na kuwahusisha pia viongozi waandamizi wa SMZ, ambao hawakusita kutamka kuwa Zanzibar ni nchi kwa mujibu wa katiba yake.

Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Shariff Hamad, alidai kwamba Zanzibar ni nchi kamili ndani ya Muungano na katika ngazi za kimataifa.

Kauli ya Katibu Mkuu huyo aliitolewa juzi alipokuwa akihutubia mkutano katika viwanja vya Chaani, Mkoa wa Kaskazini, Unguja.

Alisema kwamba Serikali ya Zanzibar ina mamlaka ya kuzungamza na mashirika ya kimataifa kama vile FAO na WHO moja kwa moja bila ya kuwakilishwa na Serikali ya Muungano na kwamba kitendo cha Serikali ya Muungano kuiwakilisha Zanzibar katika mashirika ya kimataifa ya FAO na WHO ni ukiukwaji wa mkataba wa awali wa Muungano na kuinyima Zanzibar fursa ya kusimamia mambo yake wenyewe.

Katibu Mkuu huyo pia alisema kwamba Zanzibar ilikuwa na haki kujiunga na Jumuiya ya Kimataifa ya Kiislamu (OIC) bila ya kupitia Serikali ya Muungano kwa vile suala la ushirikiano wa kimataifa sio miongoni mwa mambo kumi na moja ya awali ya Muungano.

Maalim Seif aliwapongeza mawaziri wote wa Serikali ya Zanzibar wailosimama imara kutetea Zanzibar ni nchi hususan Naibu Waziri Kiongozi wa Zanzibar, Bw. Ali Juma Shamuhuna, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Kiongozi Bw. Hamza Hassan Juma, Waziri wa Maji Ujenzi na Nishati Bw. Mansour Yussuf Himid na wabunge na wawakilishi wote wa CCM waliotetea hadhi ya Zanzibar kuwa ni nchi.

Chanzo: Nipashe, 1 Septemba, 2008

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s