Watawala wanacheza na haki za watu

Hivi ndivyo Vikosi vya SMZ vinavyowatendea Wazanzibari. Picha hii ilichukuliwa katika harakati za uchaguzi wa 2005

Hivi ndivyo Vikosi vya SMZ vinavyowatendea Wazanzibari. Picha hii ilichukuliwa katika harakati za uchaguzi wa 2005

Moja ya maeneo ambayo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imefeli kabisa ni heshima yake kwa haki za binaadamu. Rikodi ya serikali hii katika uwanja huo ni mbaya sana kiasi ya kwamba taasisi nyingi , za ndani na nje, zimewahi kubainisha mara kadhaa kwamba Zanzibar kuna tatizo kubwa la haki za binaadamu. CUF ni chama kilichoundwa katika msingi wa kulinda, kutetea na kudumisha haki za binaadamu na ndio maana katika hotuba yake kwa Baraza la Wawakilishi, Msemaji wa Kambi ya Upinzani kuhusu Katiba na Utawala Bora, Haji Faki Shaali (MBLW), anaonya juu ya ucheleweshaji wa makusudi wa kesi katika mahakama za Zanzibar kwamba ni dalili kuwa serikali haijali haki za raia na hivyo kuwa miongoni mwa sababu za raia kutokuwa na imani na serikali…

UTANGULIZI

Mheshimiwa Spika, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kuandika hotuba  hii na hatimaye kusimama mbele ya Baraza lako tukufu kuchangia Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Nchi Afisi ya Rais Katiba na Utawala Bora.

Mheshimiwa Spika, pia nakushukuru wewe  kwa kunipa fursa hii muhimu na nawashukuru wajumbe wenzangu wote kwa kukaa kwa makini kunisikiliza. Kupitia Baraza lako tukufu natoa shukrani zangu za dhati kwa wananchi wote wa Jimbo la Mkanyageni kwa mashirikiano wanayonipa katika utekelezaji wa majukumu yangu. Nitakua mchache wa fadhila ikiwa nitasahau   kumshukuru Mheshimiwa Abubakar Kiongozi wa Kambi ya Upinzani kwa uongozi wake wa busara ambao unatusaidia sana sisi ambao uzoefu wetu katika uongozi ni mdogo.

MAANA YA UTAWALA BORA

Mheshimiwa Spika, sikusudii kutoa ainisho la kitaalamu juu ya Utawala Bora lakini ili nieleweke vizuri katika mchango wangu nalazimika kutaja misingi ya dhana hii ili nitakapojenga  hoja zangu juu ya kuwepo au kutokuwepo kwa utawala bora iwe rahisi kwa wanaonisikiliza kunielewa.

Mheshimiwa Spika, kutokana na makala mbali mbali nilizozipitia nimejifunza kwamba ili pahala paweze kuambiwa kuwa pana utawala bora ni lazima pawe na mambo yafuatayo:

 • Uwazi
 • Uwajibikaji
 • Ufanisi
 • Kutabirika kwa watendaji na vitendo vyao
 • Katiba inayowakilisha matakwa ya watu
 • Mgawanyo wa madaraka unao heshimiwa
 • Utawala wa Sheria
 • Haki za binadamu na Haki za Watu
 • Kanuni za maadili n.k

Mheshimiwa Spika, muda hautoshi kutoa maelezo ya kina kwa kila kanuni iliotajwa lakini nitajaribu kuelezea baadhi tu tena kwa ufupi sana.

UWAZI

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa kanuni hii ya utawala bora shughuli zote za umma zinatakiwa zieleweke na wananchi ukiachilia mbali baadhi ya mambo ya kiutawala na ulinzi. Ni haki ya raia kuelewa shughuli za nchi yao kwa mapana na marefu na kamwe haki hiyo siyo ya watawala peke yao. Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 Toleo la mwaka 2003 katika ibara ya (18) (2) imeliweka wazi jambo hili lakini linakuja katika utekelezaji.

Mheshimiwa Spika, hali halisi ya mambo hapa petu sote tunaijua. Bado SMZ ina utamaduni wa kuficha mambo mengi ambayo wananchi wanapaswa kuyajua. Mfano mojawapo wa hoja hii ni suala la mazungumzo ya kuondoa kero za Muungano. Wananchi hawaelezwi juu ya hatua iliofikiwa, Jambo hili ni siri ya wakubwa tu. Katika nchi zenye utawala bora kweli kweli mijadala ya mambo kama haya hutangazwa moja kwa moja.

Mheshimiwa Spika, Hata wajumbe wa Baraza lako Tukufu mara nyengine tunanyimwa taarifa wakati wa ziara za kamati ingawa kufanya hivyo ni kosa la jinai. Mwaka jana Mheshimiwa Muhunzi alipolalamikia juu ya kunyimwa taarifa ambayo kamati ya PAC ilihitaji katika Wizara moja, Waziri aliehusika alijibu hawawezi kutoa taarifa kwa wapinzani. Je, Utawala Bora unataka hivyo?

Mheshimiwa Spika, Kanuni ya uwazi inahitaji uhuru wa vyombo vya habari. Taarifa ya Tume ya Haki za Binadamu Tanzania ya 2007 ambayo imezinduliwa wiki chache zilizopita imetamka wazi kwamba uwazi na haki ya wananchi ya kupata habari haieleweki na taasisi nyingi za serikali ya SMZ. Taarifa hiyo imeendelea kusema kwamba maofisa wengi wa   serikali wanapoendewa na waandishi wa habari ili watoe maelezo kuhusu matukio muhimu katika nchi mara nyingi wanakataa.

Taarifa inaeleza kwamba katika mwaka jana waandishi wa habari waliokwenda Micheweni kujionea hali ya njaa ili waripoti kwa uhakika katika  vyombo vya habari walikamatwa na kupelekwa Polisi lakini baadae waliachiwa. Sheria ya Usajili wa vyombo vya habari na vitabu ya mwaka 1988 pamoja na kufanyiwa marekebisho mwaka 1997 bado ni kikwazo katika ujenzi wa utawala bora.

2:2 UWAJIBIKAJI

Kanuni ya uwajibikaji inataka kila mtumishi wa umma atimize wajibu wa kuwatumikia watu kwa nidhamu na unyenyekevu. Inataka huduma zitolewe kwa haraka bila urasimu usio wa lazima. Inataka wafanyakazi wa umma wafike kazini kwa wakati na kuondoka kwa wakati uliopangwa. Inataka nidhamu ya kujituma na kuelewa mipaka ya kazi. Penya uwajibikaji wa kweli panatakiwa Kanuni za Utumishi zifuatwe.

Mheshimiwa Spika, SMZ haya yapo kwa kiwango cha chini sana. Katika taasisi nyingi za umma ukenda utaona wafanyakazi wengi wakipiga porojo: utaona wafanyakazi wengi wasioelewa majukumu yao: utaona wafanyakazi wanaoingia na kutoka kazini wakati wapendao: utaona viongozi wa kazi wanaoogopa wafanyakazi wanaowasimamia. Utaona watumishi wanaofanya kazi wasioelewa kanuni za utumishi. Je utawala bora utajengeka?

2:3 KATIBA INAYOKIDHI MATAKWA YA WATU

Mheshimiwa Spika, Utawala Bora unasimama pale penye Katiba yenye kukidhi matakwa ya watu. Nchi zote katika ulimwengu wa leo zina katiba ilioandikwa au isioandikwa. Kuna nchi zenye katiba zinazolinda Haki na maslahi ya wananchi walio wengi na zipo nchi ambazo zenye Katiba zinazolinda maslahi ya kundi dogo la watu.

Mheshimwa Spika, Zanzibar tunayo Katiba ya mwaka 1984 Toleo la 2003 ambayo kimaandishi sio mbaya sana ingawa haifuatwi ipasavyo na watawala. Kwa mfano ibara ya 66 ya Katiba inatamka wazi kwamba katika wajube 10 wa Baraza la Wawakilishi wa kuteuliwa na Rais wajumbe wawili watoke katika Upinzani lakini hadi hotuba hii inaandaliwa bado wajumbe hao hawajateuliwa. Iko mifano mingi ya ukiukwaji wa katiba ukiacha huo nilioutaja na zaidi ukiukwaji huo uko katika Sura ya Pili  na Sura ya Tatu ya Katiba.

Mheshimiwa Spika, Sisi katika kambi ya Upinzani tunahisi katiba iliopo ina mapungufu mengi na ni kikwazo kwa demokrasia ya kweli. Tunapekeza ifanyiwe marekebisho ili ikidhi matakwa ya walio wengi, mambo ambayo tunahisi yanapaswa kuangaliwa ni pamoja na:-

Suala la kuweka utaratibu mzuri wa kugawana madaraka makubwa ya nchi kati ya Unguja na Pemba. Kuna haja katiba itamke wazi kwamba Rais akitoka Kisiwa cha Unguja Waziri Kiongozi atoke Pemba na kinyume chake. Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika ibara ya 47 (3) imeweka utaratibu kama huu ili isitokee Rais wa Jamhuri na Makamo wake wote kutokea upande mmoja.

Kupunguza madaraka ya Rais ili yasiwe makubwa mno kama ilivyo sasa. Katiba ya sasa inampa uwezo Rais kutekeleza shughuli zake bila ya kulazimika kufuata ushauri wa mtu yoyote (ibara ya 52) jambo ambalo ni hatari sana. Chini ya ibara hii ikitokea nchi kupata Rais asie na busara anaweza kufanya mambo ya kuwachukiza raia badala ya matarajio yao. Vile vile ibara ya 53 ya katiba inampa uwezo Rais kuanzisha au kufuta ofisi  bila hata kuridhiwa na Baraza la Wawakilishi. Ikitokea nchi kupata Rais asie na busara inaweza kuwa na idara nyingi kuliko mahitaji ya nchi. Yako maeneo mengi yenye mapungufu lakini nimechagua mifano miwili tu.

Suala la kuimarisha madaraka ya umma kwa kuzipa meno Halmashauri za Wilaya, Mabaraza ya Miji, pamoja na Manispaa.

Kuweka mfumo mzuri wa uchaguzi ambao utazingatia kuimarisha demokrasia zaidi na ambao utalifanya Baraza la Wawakilishi lionekane kweli ni chombo cha Wananchi. Baraza letu la sasa lina wateule wengi wa Rais ambao jukumu lao kubwa ni kulinda maslahi ya muhimili wa utawala (Executive) wala sio Baraza.

Kuweka mazingira mazuri zaidi ya kuwadhibiti wavunjaji wa katiba. Katiba ya Jamhuri wa Muungano ibara ya 104 hadi ibara ya 113 imeweka masharti ya fedha lakini yanahitaji maboresho zaidi.

Kuweka mazingizra mazuri zaidi ya kuwadhibiti wavunjaji wa katiba. Katiba ya Jamahuri wa Muungano ibara ya 132 imeweka Sekreterieti ya maadili ya viongozi ambayo ina uwezo wa kuchunguza tabia na mwenendo wa viongozi wa umma.

Kuboresha mfumo wa utumishi wa umma. Katiba katika ibara ya 116 hadi ibara ya 118 imeeleza juu ya Tume ya Utumishi Serikali lakini ipo haja mfumo wa utumishi wa umma ukaangaliwa upya na katiba ikawa wazi zaidi.

Kuweka utaratibu wa kuwathibitisha wateule wa Rais katika Baraza la Wawakilishi wenye kushika nafasi nyeti kama vile Waziri Kiongozi, Jaji Mkuu, Mwanasheria Mkuu n.k.

Mheshimiwa Spika, nimetaja maeneo machache sana lakini yapo maeneo mengi zaidi ambayo wataalamu wakipewa fursa ya kutoa maoni yao watatoa na kutumika.

2:4 UTAWALA WA SHERIA

Mheshimiwa Spika, Utawala wa Sheria unajengeka kwa misingi lakini nitataja misingi michache tu na kuangalia inavyotekelezwa hapa petu. Nimeamua kutaja misingi ifuatayo:

 • Sheria iwe ndio msingi wa utawala (the supremacy of law), yaani  kila mtu lazima awajibike kufuata sheria na anapokiuka aadhibiwe kwa mujibu wa sheria.
 • Haki itolewe bila ubaguzi wa aina yoyote kwa kufuata taratibu ziliopo.
 • Viongozi hawatakua na mamlaka ya kuamua watakavyo wenyewe bali kwa mujibu wa Sheria.
 • Sheria ziangalie maslahi ya umma na sio maslahi  binafsi

Mheshimiwa Spika, hapa petu msingi wa kufuata sheria ziliopo na kwamba ataekiuka sheria aadhibiwe kwa mujibu wa sheria haufanyi kazi. Kwa mujibu wa taarifa a Tume ya Haki za Binadamu Tanzania ya mwaka 2007 ambayo imezinduliwa hivi karibuni katika mwaka wa 2007 hakuna mauaji yaliyoripotiwa ambayo yamefanywa na vikosi vya SMZ kinyume na ripoti ya mwaka 2006 ambayo yamefanywa na vikosi hivyo katika matukio mbali mbali.  Hata hivyo hakuna dalili kwamba kuna askari yoyote aliepelekwa mahkamani kati ya hao waliohusika na mauaji  ya miaka ya nyuma.

Mheshimiwa Spika, msingi wa haki kutolewa bila ubaguzi nao una mashaka kibao, kwa mfano, katika uchaguzi ulliopita wa mwaka 2005 wananchi wengi walinyimwa haki yao  ya kujiandikisha na kupiga kura kwa sababu tu masheha hawakutaka watumie haki yao hiyo. Ripoti ya Tume ya Uchaguzi mkuu wa Zanzibar ya mwaka 2005 (uk.66) inakiri kwamba masheha waliingilia kazi za uandikishaji kinyume na utaratibu na kukataa maelekezo ya Tume ya Uchaguzi. Kwa mujibu wa taarifa niliopata katika chama changu cha CUF kiasi ya wananchi wapatao 12,000 waliyimwa haki ya kujiandikisha na kupiga kura kwa kuzuiliwa na masheha ambao kwa mujibu wa kifungu cha 11a (2) na (3) ya  sheria ya uchaguzi ya mwaka 1984 kama ilivyorekebishwa kwa sheria ya 2004 ni mawakala wa uandikishaji. Je, kwa hali hii utawala bora utajengeka?

Mheshimiwa Spika, suala la viongozi kufanya maamuzi yasiozingatia sheria lakini yanayojali utashi wao nalo lipo. Kwa mfano, Sheria ya wafanyakazi kushiriki  katika siasa ya mwaka 2003 (Act No 3 of 2003). Imeweka mambo mengi wazi lakini bado viongozi wengi hufanya maamuzi yanayopingana na sheria hiyo. Kwa mfano, ibara ya 7 ya sheria hii inakataza muajiri kumlazimisha mtu kujiunga na chama cha siasa ili apate ajira lakini masheha wengi hukataa kuthibitisha barua za maombi ya kazi  zinapowapitia ikiwa muombaji si mfuasi wa CCM. Pia ibara ya 5 ya sheria hii imeweka masharti kwa mfanyakazi wa Serikali anaetaka kujiingiza katika uongozi wa kisiasa ambayo ni pamoja na kuchukua likizo bila malipo au kuacha kazi.

Mheshimiwa Spika, katika mwezi wa Januari mwaka huu baadhi ya viongozi wa utumishi wa umma Pemba waliwalazimisha wafanyakazi wao wajaze fomu za kumdhamini Mwenyekiti wa CCM Mheshimiwa Kikwete katika matembezi ya kuchangia CCM wakati wa sherehe za kuadhimisha kuzaliwa kwa chama hicho. Mbali na hilo lakini pia wapo maofisa wa serikali ambao waliwalazimisha wafanyakazi washiriki katika matembezi ya mshikamano na maandamano kinyume na kifungu cha 5 cha sheria hii.

Mheshimiwa Spika, msingi wa kutunga sheria zenye kuzingatia maslahi ya umma hauzingatiwi sana na SMZ na kinachoangaliwa zaidi ni maslahi ya Chama cha Mapinduzi. Kwa mfano, Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 Toleo la 2003 Ibara  ya 66 inampa uwezo Rais kuteuwa wajumbe 8 kati ya 10 wa Baraza la Wawakilishi  kutoka chama  chake  upande  wa upinzani wajumbe  wawili tu. Aidha ibara ya 64 (d) ya Katiba inawapa uhalali wakuu wa Mikoa kuwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi ili kuongeza nguvu za Chama Tawala ndani ya Baraza.

KANUNI ZA MAADILI

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa Fedha wa 2003/2004 Wizara ilikuja na habari njema ya uundaji wa Taasisi ya maadili ya viongozi na shilingi 55,909,000 zikaombwa kwa ajili ya kukamilisha jengo hilo. Tulifarijika sana kwani utawala bora bila ya kanuni za maadili hasa kwa viongozi ni mtihani mkubwa.

Mheshimiwa Spika, pia katika mwaka huo wa 2003/2004 ziliombwa shilingi 71,830,000 kwa ajili ya uundaji wa taasisi ya kupambana na rushwa. Katika miaka iliofuatia taasisi hizo ziliunganisha na kuwa na mamlaka ya kupambana na rushwa na Maadili ya Viongozi. Tokea kipindi hicho fedha zinaombwa lakini leo ndio kwanza tunaambiwa kwamba Idara ya Uratibu wa Utawala Bora ndio imeanza kazi ya kuratibu mapitio ya Rasimu ya Sheria ya kupambana na Rushwa. Hatujui mwaka gani rasimu hiyo itamalizika na kuletwa Barazani.

Mheshimiwa Spika, Kwa kuwa Waziri wa Nchi anayeshughulikia Fedha na Uchumi Mhe. Dr Mwinyi alilihakikishia Baraza wakati alipokua akifanya majumuisho ya Bajeti ya Serikali kwamba kwetu Alhamdulilah ni waadilifu, tuko wazi na tena tuko safi basi tuache maandalizi ya uundaji wa mamlaka ambayo itakuwa haina kazi.

3:0 MAHKAMA

Mheshimiwa Spika, Muhimili wa Mahkama upo kwa mujibu wa ibara ya 5A ya katiba ya Zanzibar Toleo la 2003 na jukumu lake la msingi ni kusimamia utoaji wa haki.

Mheshimiwa Spika, lalamiko kubwa kwa upande wa mahkama ni ucheleweshaji wa kesi. Sisi katika kambi ya upinzani hatujaelewa sababu zipi hasa zinazopelekea  kesi kukaa miaka   mingi bila kutolewa uamuzi. Kuna mashauri yaliofunguliwa zaidi ya miaka mitano sasa lakini bado uamuzi haujatolewa wakati mahkama inajua wazi kwamba haki inayocheleweshwa ni haki inayonyimwa Lord Simon katika kesi ya Central Asbestos Co Ltd v. Dodd (1972) 2 All ER 1135 alisema yafuatayo katika umuhimu wa kuharakisha kesi: Speedy rough justice will, there fore be better justice than justice worn smooth and fragile with the passage of time.

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa hotuba ya Mheshimiwa Waziri ni kesi moja tu kati ya kesi kumi na sita zilizofunguliwa katika Mahkama ya Rufaa ndio iliotolewa maamuzi katika mwaka huu wa fedha. Vile vile katika kesi 38 zilizofunguliwa katika Mahkama Kuu kanda ya Pemba hapana hata moja iliotolewa uamuzi na sisi kila mwaka tunapendekeza apelekwe Jaji Mkazi Pemba lakini ushauri huu hautakiwi. Je, wananchi wa Pemba wawe na imani gani na seriakali juu ya jambo hili?

Mheshimiwa Spika, Mahkama ya Kadhi Mkuu nayo kati ya kesi 37 zilizofunguliwa ni kesi 7 tu ndizo zilizotolewa uamuzi. Mahkama ya Mkoa Vuga ni kesi 49 tu ndizo zilizotolewa uamuzi kati ya kesi 249 zilizofunguliwa. Je huku si kucheza na haki za watu?

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri amejitetea katika hotuba yake kwamba suala la ucheleweshaji kesi si la Mahkama pekee bali pia linahusisha Polisi, Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka, Mawakili na mashahidi. Utetezi huu haukubaliki hata kidogo kwani vyombo hivi havina maamuzi isipokuwa Mahkama yenyewe ndio yenye maamuzi.

4:0 AFISI YA MKURUGENZI WA MASHTAKA

Kuwepo kwa Mkurugenzi wa Mashtaka kumetajwa katika Katiba ya   Zanzibar  ibara ya 56 A (1) (a) Majukumu yake  yametajwa katika ibara ndogo ya 3 na 8 ya ibara hii ambayo ni:

 • Kufungua na kushughulikia mashataka yoyote ya jinai dhidi ya mtu yoyote mbele ya mahkama yoyote (isipokuwa ya kijeshi) kuhusiana na kosa lolote ambalo mtu huyo anashtakiwa nalo.
 • Kuchukua na kuendeleza mashtaka yoyote ya jinai ambayo mwanzoni yalifunguliwa na mtu au chombo chengine.
 • Kusitisha mashtaka yoyote ya jinai ambayo yalianzishwa na mtu yoyote au chombo chochote.
 • Kuzuia matumizi mabaya ya vyombo vya sheria.

Mheshimiwa Spika, Kutokana na uwezo mkubwa aliopewa na katiba wa kuzuia matumizi mabaya ya vyombo vya sheria wananchi walijenga matumaini makubwa kwamba matatizo yaliokuwepo yangeondoka. Wananchi walitarajia kwamba suala la watuhumiwa wa makosa ya jinai hawatatendewa kama vile wameshatiwa hatiani kama inavyoagiza katiba ibara ya 12(6)(b). Wananchi walitarajia tatizo la Polisi kukamata watuhumiwa na kuwafungulia kesi lakini ushahidi wa kesi hizo ukakaa miezi na miezi haujakamilika lingefikia mwisho. Wananchi walitarajia suala la watu kukamatwa na kuwekwa ndani muda mrefu bila kwenda mahkamani lingeondoka kabisa. Wananchi walitarajia unyanyasaji wa mahabusu katika vyuo vya mafunzo ungesita.

Mheshimiwa Spika, kwa kiasi fulani bado vyombo vya dola havijajirekebisha ipasavyo kwani bado Polisi inaendelea na utamaduni wa kukamata watu na kuwaweka kizuizini muda mrefu bila kuwapeleka Mahkamani. Pamoja na Mheshimiwa Waziri kutueleza kwamba Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka  imeanza hatua ya kukamilisha lengo la kuimarisha mfumo wa Uendeshaji Mashtaka kwa utaratibu wa kukamilisha Upelelezi  kabla ya kufungua Mashtaka na kwamba mwezi Machi Mwaka huu imekutana na wahusika wa upelelezi kukamilisha azma hii, matendo hayaonyeshi mabadiliko makubwa.

Mheshimiwa Spika, Sheria ya nyendo za jinai nambari 7 ya mwaka 2004 imeweka utaratibu wa kutumikia jamii kwa wakosaji wa makosa madogo madogo na kanuni za mpango huo zilianza kutumika tarehe 1 Febuari 2005.Kwa nini utekelezaji wake ikawa haujashika kasi wakati tunaambiwa Chuo cha mafunzo kuna msongamano wa mahabusu na nafasi ni finyu sana. Kwa bahati mbaya sana hata katika hotuba za bajeti Mpango huu siku hizi hautajwi tena.

5:0   KAMISHENI YA WAKF NA MALI YA AMANA

Mwaka jana nilipokuwa nachangia hotuba ya bajeti ya Wizara hii nilieleza lalamiko la baadhi ya misikiti kwamba nyumba za wakf za misikiti hiyo zimechukuliwa na Serikali kinyume na malengo ya wakf. Pia nilieleza lalamiko la msikiti mmoja la kutopewa pesa za matengenezo ya msikiti kutoka kamisheni wakati nyumba hiyo iko chini ya kamisheni ya wakf. Kwa taaria niliyonayo bado hakuna hatua yoyote iliochukuliwa juu ya nilioyasema.

Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa  taarifa nilizozipata na baadhi ya viongozi wa misikiti kuna misikiti ambayo ilikuwa na mashamba kabla ya Mapinduzi ya 1964 lakini mashamba hayo yakataifishwa bila fidia yoyote. Ningependa kuishauri kamisheni kutafiti taarifa hizi na kuchukua hatua muafaka.

Mheshimiwa Spika, hivi karibuni kamisheni imepandisha bei za nyumba zilioko chini yake kwa kiwango kikubwa sana. Kwa mfano, kuna mpangaji aliekua akilipa Shilingi 20,000 kwa mwezi na sasa anatakiwa alipe shilingi 120,000 kwa mwezi. Ningeshauri wakaweka bei ambazo ni muafaka kwa pande zote hasa ukizingatia  kwamba kamisheni haina utamaduni wa kufanya matengenezo  na jukumu hilo linafanywa na wapangaji kwa gharama zao wenyewe.

6:0 AFISI YA MUFTI

Mheshimiwa Spika, Afisi ya Mufti imetoa muongozo wa uundwaji wa kamati za kutatua migogoro katika kila shehia. Kwa mujibu wa muongozo huo kamati ina wajumbe wafuatao:

 • Sheha
 • Wajumbe sita Waislamu
 • Wajumbe watatu kutoka dini ya Kikristo

Mheshimiwa Spika, baadhi ya waumini hawaridhishwi na suala hili. Baadhi ya Waislamu wanadai Kitabu chao cha Kur-an kinajitosheleza, hivyo hawahitaji kushirikiana na viongozi wa dini nyengine katika kutatua migogoro ya Waislamu. Pia wapo Waislamu wanaoziona kamati hizi kwamba zina agenda ya kisiasa na wao tayari walikwishaambiwa kwamba wasijishirikishe na siasa na kwamba watakao sasa wavue vilemba. Mashekhe wengi wanasema hawawezi kuvua vilemba, hivyo kamati hizi haziwafai.

Mheshimiwa Spika, katika Visiwa vyetu vya Unguja na Pemba mashekhe ni watu wenye kuheshimika sana. Kwa msingi huo wa kuheshimu mashehe wao Waislamu wa Pemba wanamuomba Mufti amtafutie gari naibu wake aliyeko Pemba ambae hulazimika kupakiwa kwenye vespa kwa ajili ya kwenda na kurudi kazini.

7:0 AFISI YA MDHIBITI NA MKAGUZI MKUU WA HESABU ZA SERIKALI

Mheshimiwa Spika, Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali yupo kwa mujibu wa ibara ya 112 ya katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 Toleo la 2003. Majukumu yake yametajwa katika ibara ndogo ya 3 hadi ya 7.

Mhesimiwa Spika, Ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu kila mwaka zimekuwa zikiripoti juu ya mambo yafuatayo:

 • Ufinyu wa bajeti
 • Upungufu wa nyenzo za kufanyia kazi
 • Upungufu wa wataalamu

Mheshimiwa Spika, bila matatizo haya kupatiwa  ufumbuzi kikamilifu tusitarajie ufanisi mkubwa.

Mheshimiwa Spika, nina wasiwasi kwamba sheria ya Fedha za Umma (Publuc Finance Act, 2005) pamoja na sheria ya manunuzi (the Public Procurement and disposal of public assets act, 2005) hazijafanyiwa kazi ipasavyo. Kifungu cha 9 cha sheria ya Fedha ya mwaka 2005 kinampa uwezo Waziri kuwachukulia hatua za sheria watumishi wasiofuata sheria hii lakini sijui kwa nini Waziri anaehusika na Fedha hatumii sheria hii ipasavyo.

Mheshimiwa Spika, nasikitishwa sana jinsi ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu zinavyocheleweshwa kufanyiwa kazi na Baraza letu tukufu. Siku za nyuma sisi tulikua tunalaumu ucheleweshwaji wa taarifa lakini hivi sasa zipo taarifa za miaka mitatu ambazo hatujazifanyia kazi. Hivyo Serikali ina umaskini wa kiasi gani hata ikashindwa kuiwezesha PAC kushughulikia taarifa hizi.

8.0 AFISI YA MRAJISI MKUU

Mheshimiwa Spika, Afisi ya Mrajisi Mkuu wa Serikali inaonekana ina wafanyakazi wasio waaminifu. Nimelazimika kusema hivi kutokana na tatizo lililoibuka la baadhi ya watu kumiliki hati za mali zisizokuwa zao. Tayari yamekwishajitokeza matatizo ya watu kuuza nyumba zisizokuwa zao lakini walikuwa na hati miliki za kughushi. Je, watu wamezipata wapi hati hizi?

Mheshimiwa Spika, kuna kilio cha watu wa Pemba kuhusu usumbufu wanaoupata katika usajili wa NGO. Afisi ya Mrajisi Pemba haina uwezo huo na hivyo lazima Wapemba waje Unguja kuomba usajili wa NGO wanazotaka kuanzisha. Utawala bora hautaki usumbufu usio wa lazima kwa wananchi hivyo kwa nini Wizara isiweke utaratibu maofisa wa Idara hii wakaweka utaratibu wa kwenda Pemba kushughulikia mambo kama haya.

Mheshimiwa Spika, tatizo jengine liliopo katika Afisi ya Mrajisi Mkuu ni kushindwa kudhibiti utoaji holela wa vyeti vya kuzaliwa. Katika ripoti ya Tume ya Uchaguzi ya mwaka 2005 imekiri kuwepo kwa watoto wengi waliokuwa na vyeti vya kughushi wakati wa uandikishaji katika daftari la wapiga kura.

CHANGAMOTO

Mheshimiwa Spika, Ujenzi wa Utawala bora Zanzibar umekabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo zifuatazo:

 • Kukosekana utashi wa kisiasa kwa watawala. Nafikiri watawala wanaimba wimbo wa utawala bora ili kuwavutia washirika wa maendeleo tu lakini moyoni hawana dhamira ya kweli.
 • Uhafidhina kwa kiasi kikubwa nao unarejesha nyuma jitihada za ujenzi wa utawala bora. Baadhi ya viongozi wa kisiasa na watendaji katika serikali hawako tayari kubadilika na hutumia kisingizio cha kudumisha Mapinduzi ili kukwepa utekelezaji wa utawala bora.
 • Baadhi ya sheria za nchi nazo ni kikwazo cha ujenzi wa utawala bora. Bado kuna sheria  za ukandamizaji na sheria ambazo zipo kwa maslahi ya chama tawala tu.
 • Vyombo vya dola hasa vikosi vya SMZ navyo ni kikwazo cha utekelezaji wa dhana ya uatawala bora. Kama ilivyoripotiwa na Tume ya Haki za Binadamu katika ripoti yake ya mwaka 2006 vitendo vingi vya uvunjaji wa Haki za Binadamu hufanywa na vikosi hivi.
 • Wananchi wanaojichukulia hatua mikononi mwao mwenyewe nao ni kikwazo cha utekelezaji wa ujenzi wa uatawala bora. Pamoja ba udhaifu wa vyombo vya dola wa kuwashughulikia wahalifu lakini sio sahihi kumuua mtu kwa sababu tu ameiba kuku au nazi mbili.

10:0 HITIMISHO

Wananchi katika Bara la Afrika waliunga mkono harakati za kupigania Uhuru kwa matarajio kwamba madhila yaliokuwepo wakati wa ukoloni yataondoka. Matarajio yao yalikua kufaidi rasilimali zao ambazo zilikuwa zikiwafaidia wachache, walitarajia kufanyiwa haki na vyombo vya dola, walitarajia hawatabaguliwa na  viongozi wao, na matarajio mengineyo jukumu kubwa la viongozi kwa sasa ni kurejesha matarajio hayo ya wananchi.

Mheshimiwa Spika, Mohamed Seif Khatib muandishi maarufu wa Kiswahili hapa Zanzibar aliuona udhaifu wa viongozi wa Afrika na katika shairi lake juu ya viongozi wa Afrika kuwasaliti wananchi wao anasema hivi katika beti mbili za shairi hilo ambalo limo katika kitabu chake cha FUNGATE YA UHURU.

Viongozi wa Afrika,

Wanaotawala kwa mabavu,

Kujifanya ni mashupavu,

Wao wachache ni werevu,

Na umma wote ni mpumbavu,

Wanafiki,

Wazandiki.

Viongozi wa Afrika,

Wapendao lao kabila,

Kulijaza kila mahala,

Kwa kuwatafutia kula,

Wengi kuwapa madhila,

Wahaini,

Wa watani.

Mheshimiwa Spika, nataraji tutafakari maneno ya kiongozi mwenzetu ili pale tulipotetereka tujirekebishe tuweze kujenga Taifa lenye furaha.

Nashukuru kwa utulivu wenu.

Mheshimiwa Spika, Naomba kuwasilisha.

Tafadhali tutumie maoni yako kuhusu hotuba hii

(c) 2008, Kurugenzi ya Haki za Binaadamu na Mahusiano ya Umma, CUF

Advertisements