Bunge lamalizika kwa kishindo kizito cha Muungano

Bendera ya Zanzibar.

Bendera ya Zanzibar.

Bunge la Bajeti la mara hii limemalizika mjini Dodoma Ijumaa iliyopita ya terehe 29 Agosti, 2008, huku likiwa limeiwacha nchi imejeruhika vibaya, hasa katika masuala ya Muungano, mahkama ya kadhi na kashafa ya EPA. Kuhusu Muungano, ambapo kauli ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda kwamba Zanzibar si nchi ndiyo iliyochochea yote, hali ilikuwa ni ngumu na mbaya zaidi kwa kuwa wabunge waligawanyika baina ya Uzanzibari na Utanganyika. Wakati wa Zanzibar walipigania hadhi ya nchi yao ndani ya mipaka ya Muungano, wa Tanganyika walipigania kuidhibiti zaidi Zanzibar. Fuatilia sehemu ifuatayo ya majadiliano katika michango ya wabunge kwa Ofisi ya Makamo wa Rais (Muungano)….

Sehemu ya Majadiliano ya Bunge (KUTOKA HANSARD) ya tarehe ya  19/08/2008.

Mkutano wa 12. Kikao cha 44

MHE. ALI SAID SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kupata nafasi jioni hii ya leo, ili kutoa maoni yangu kuhusu suala zima la Muungano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, nichukue nafasi hii nimshukuru Mwenyezi Mungu, kunijaalia mimi pamoja na sisi sote, afya njema tukaweza kushiriki katika shughuli za Bunge jioni hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende moja kwa moja kwenye makusudio, kabla sijaingia katika yale niliyokusudia kuzungumza, naomba nami nianze kwa utangulizi wa hotuba yangu kwa kusema maneno machache kuhusu kauli ambayo aliitoa Mbunge wa Kyela, Mheshimiwa Mwakyembe, wakati akichangia Hotuba ya Waziri wa Sheria na mambo ya Katiba.  Mheshimiwa Mwakyembe, alieleza kwamba, baadhi ya Mawaziri wa Zanzibar au Viongozi wa Zanzibar, wamekosa nidhamu na kwamba ni watovu wa nidhamu na wanahitaji kuadhibiwa kwa kitendo chao cha kumpiga hadharani Waziri Mkuu, Mheshimiwa Pinda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme kwamba, kwa kutumia Katiba hii ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, kifungu cha 103 (3), ukurasa wa 89, naomba ninukuu inasema kwamba: “Pamoja na madaraka yake mengine, Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ndiye atakayewateua na kuwakabidhi madaraka Mawaziri na Manaibu Mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi ya Zaznibar.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nadhani Mheshimiwa Mwakyembe ni Mwanasheria, lakini hapa kateleza.  Angeangalia kwanza kwa mujibu wa kifungu hiki, Mawaziri wa Zanzibar hawawajibiki kwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; kwa hiyo kauli yao ya kueleza hisia zao kwa mujibu wa hisia za Wazanzibar walikuwa sahihi na kwa vyovyote vile akitaka ama asitake, lakini Mheshimiwa Mwakyembe hapa alitekeleza na ni vyema sasa kama ni muungwana, awaombe radhi Mawaziri wa SMZ lakini pia Wazanzibari.  (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tumefikia hatua hii ya Muungano, matatizo kila siku yanaongezeka, kero au kasoro, lakini yote haya ni  kutokana na msingi wa jambo lenyewe; kwa sababu kwa vyovyote vile kama msingi ni mbovu, vyumba hata uweke vigae na tiles lakini at the end of the day itabomoka tu.  Kwa hiyo, mapambo yote utakayofanya yatakuwa ni batili kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukitazama tangu asili ya Muungano huu, ulikuwa na dosari kadhaa na maana yake ni kwamba, haukusimama katika nguzo madhbuti.  Ukiangalia, ninyi mnaungana nchi mbili zenye mamlaka na hadhi na kila kitu chake, Jamhuri ya watu wa Zanzibar na Jamhuri ya watu wa Tanganyika, inakuwaje katika Muungano huo Serikali moja inakufa, nchi moja inakufa na moja inabaki ndani ya Muungano?  Hilo peke yake ni tatizo tutake tusitake hilo ni dosari.  Kwa hivyo, kwanza kabisa, kama tuna nia njema na tunataka kweli Muungano huu udumu na  uendelee, bado haja ya kuwa na Serikali ya Tanganyika peke yake na haja ya kubaki na Serikali ya Zanzibar peke yake na Serikali ya Shikirishi ina umuhimu wa aina yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu tuangalie namna yenyewe hasa ya Muungano kwa kweli ni kichekesho, maana yake tuchukue mfano; kuna mambo karibu manane ambayo yanatajwa kwamba hayawezi kutolewa maamuzi isipokuwa kwa ridhaa ya theluthi mbili ya kila upande; upande wa Zanzibar na upande wa Bara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kichekesho nilichokikusudia ni hiki, ukifungua ukurasa wa mwisho wa Katiba kuna mambo hayo manane, Mahakama Kuu ya Zanzibar kwa shughuli zake zote, inahitaji ridhaa two third ya majority ya Wabunge wa Zanzibar na two third ya majority ya Wabunge wa Bara, lakini katika mambo haya manane Mahakama Kuu ya Tanzania haimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni haki yenu tu upande wa bara; sisi Zanzibar mpaka mkubali nyinyi lakini yenu nyinyi sisi tusikubali; inakuwaje hiyo?  Haiwezekani, hakuba utaratibu huo popote duniani, lakini kama hiyo haitoshi katika hayo mambo manane ambayo yanataka ridhaa ya pande zote mbili; la nane linasema, idadi ya Wabunge kutoka Zanzibar ni lazima ipatikane ridhaa ya pande zote mbili lakini idadi ya Wabunge kutoka Tanzania Baraza hahitaji ridhaa hii; kwa nini?  Tunaomba maelezo hapa Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti nilitaka niulize, dizaini hii ya Muungano mfano wake upo wapi hapa duniani; nyinyi mmeuona kweli duniani?  Mimi katika utafiti wangu mpaka dakika hii sijaona Muungano wa aina hii tulionao sisi, kama upo naomba Mheshimiwa Waziri atakapofanya majumuisho atuambie na kutupa mfano kama ilivyo ni wap na isiwe tofauti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi toka niingie katika Bunge hili mwaka 2003, kwa bahati nilikuja wakati wa bajeti nikakuta mgawo wa Zanzibar katika fedha za Muungano na misaada ni asilimia 4.5 Toka muda ule nilikuwa nauliza na kuchangia nikiuliza na tukaambiwa kwamba, suala hili ni kweli kero lakini linafanyikwa kazi, kamati nyingi zimeundwa, mikutano mingi imefanywa lakini mpaka leo tunapozungumza 2008; bajeti hii ambayo tunayo bado kima ni hicho hicho asilimia 4.5, kwa kweli mchakato huu kwa maoni  yangu utamaliza kiama ndipo utakapopatikana ufumbuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa tupo katika mchakato wa kutafuta Shirikisho la Afrika Mashariki, lakini kwa nini tusiwashawishi hawa wenzetu Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi?  Sisi tuna Muungano mzuri tu; kwa nini tusiwashirikishe katika Muungano huu tulionao na wote wakaja katika Muungano wetu huu badala yake tunataka tuunde shirikisho lingine mbali?  Huu mnasema kwamba ni mfano wa kuigwa; ni mfano mzuri duniani; kwa nini sasa hawa wenzetu wa Kenya,  Uganda tusiwashawishi kwamba na nyinyi nyote njooni katika Muungano wetu huu wa Zanzibar na Tanganyika ni Muungano mzuri tu?

Kwa hiyo, dada kupata gharama yote hiyo ya kufanya mashirikiano mengine, njooni moja kwa moja katika hii na tufanye shirikisho.  Najua kwamba, hamkubali.  Hapa juzi mlisema shirikisho bwana hili halina maana, sisi tutakuwa tumepoteza hiki, kumbe mkuki mbaya kwa samba tu na nguruwe lakini kwa binaadamu mchungu.  Sisi kule kwa sababu mamlaka kadhaa mnayachukua hamjali.

Baya zaidi, haya marekebisho ya 11 kwa kweli ilikuwa ni risasi ya mwisho.  Makubaliano ya awali ya Muungano; Rais wa Zanzibar anabaki kuwa Makamu wa Rais, lakni mkafanya mlivyofanya mkaondoa kiepengele hiki.

MHE. SIRAJU J. KABOYONGA:  Mhe. Mwenyekiti kuhusu utaratibu.

MWENYEKITI: Kuhusu utaratibu Mheshimiwa Kaboyonga kanuni gani?

MHE. SIRAJU J. KABOYONGA:  Mhe. MwenyekitI, Kanuni ya 68.

MWENYEKITI: Hebu tusomee kifungu cha ngapi?

MHE. SIRAJU J. KABOYONGA:  Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati mbaya kitabu chenyewe cha kanuni sina labda unisaidie.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mbunge, Kiti changu hapa mezani si maana yake kusaidia Wabunge kukumbuka kanuni na kuzishughulikia. Unapotaka kueleza jambo lolote Bungeni ni lazima uwe unajua kanuni unayoihitaji na ndipo utaomba huo utaratibu na mwongozo wangu.  Mheshimiwa Mbunge, naomba uendelee, Mheshimiwa Kaboyonga kwa kweli leo amesahau kanuni aliyokuwa naihitaji. (Akofi)

MHE. ALI SAID SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa ufafanuzi huo; msimamo mzuri.  Loo!  Nilikuwa nikizungumzia nini , sijui ilikuwa habari gani?

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mbunge, tuendelee kama umesahau unaweza ukamaliza.

MHE. ALI SAID SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nazungumzia suala la mabadiliko ya 11 kwamba, kwa kuondoa mamlaka ya Rais wa Zanzibar kuwa Makamu wa Rais sasa anaingia katika Baraza la Mawaziri kama Waziri asiye na Wizara maalum.  La zaidi ni kwamba, kikao kile cha Baraza la Mawaziri, Mwenyekiti wake anakuwa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano, ikiwa hayupo kwa dharura yoyote anakuwa ni Makamu wa Rais, lakini kama wote hawapo Waziri Mkuu anakuwa ndiyo anashikilia kiti kile.

Sasa tujiulize; pana Muungano hapo, kwa nini Rais wa Zanzibar asiwe ndiyo mwenye kuongoza kikao kile wakati yeye anawakilisha Jamhuri ya watu wa Zanzibar?  Kwa hivyo dosari hiyo ni kubwa, mkubali au msikubali ni dosari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoke hapo moja kwa moja; mimi nina mambo kama sabab, naomba Waziri atakapofanya majumuisho anifafanulie.  La kwanza ni kuhusu mamlaka ya nchi, ukurasa wa 15 wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.  Naomba ninukuu kifungu cha 4 (1) kinasema: “Shughuli zote za mamlaka ya nchi katika Jamhuri ya Muungano, zitatekelezwa na kudhibitiwa na vyombo viwili vyenye mamlaka ya utendaji, vyombo viwili vyenye mamlaka ya kutunga sheria na kusimamia utekelezaji wa shughuli za umma.

Mheshimiwa Waziri nataka ufafanuzi kifungu hiki cha Katiba kilikusudia kitu gani hasa, maana mimi sijaelewa hapa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni kufungu cha 64 (3).

MHE. SIRAJU J. KABOYONGA:  Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu utaratibu.

MWENYEKITI: Kuhusu utaratibu Mheshimiwa Kaboyonga.

MHE. SIRAJU J. KABOYONGA:  Mhe. MwenyekitI, KIFUNGU CHA 68(3); Msemaji anayeendelea alipokuwa anaongea kuna wakati alisema kwamba, mkuki kwa nguruwe kwa mwanadamu mchungu. Sasa humu ndani nani nguruwe nani mwanadamu? (Makofi/kicheko)

MWENYEKITI:  Mheshimiwa Kaboyonga, sehemu ya tatu uliyoisoma inasema: “baada ya kutaja sehemu ya Kanuni ya Bunge iliyokiukwa.  Mbunge aliyesimama kuhusu utaratibu ataketi mahali pake kusubiri maelezo ya Mheshimiwa Spika.”  Kwa hiyo, hapo ulitakiwa pia useme kanuni iliyovunjwa sasa ni ipi.  Hata hivyo, maneno hayo uliyoyasema yametumiwa na Mbunge aliyekuwa anachangia hoja kama mifano.  Sasa ungetumia kanuni inayosimamia maneno ndiyo ingeku- guide katika kuomba utaratibu na kuomba mtoa hoja aweze kuindoa kauli yake.(Makofi)

MHE. ALI SAID SALIM:  Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa ufafanuzi.  Naomba Mheshimiwa Waziri atakapofanya majumuisho anipe ufafanuzi wa kifungu cha 68(3); naomba ninukuu:  Endapo sheria yoyote iliyotungwa na Baraza la Wawakilishi inahusu jambo lolote katika Tanzania Zanzibar, ambalo lipo chini ya mamlaka ya Bunge, sheria hiyo itakuwa batili na itatenguka.” Endapo sheria yoyote iliyotungwa na Bunge inahusu jambo lolote ambalo lipo chini ya mamlaka ya Baraza la Wawakilishi, sheria hiyo itakuwa Batili na itatenguka. Naomba ufafanuzi.

Kifungu kingine ambacho nilikuwa nataka ufafanuzi ni kifungu cha 103 ukurasa wa 89 (3) kinasema hivi: “Pamoja na madaraka mengine, Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ndiyo atakayewateua na kuwakabidhi madaraka Mawaziri na Naibu Mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Kifungu 115(2) kinasema hivi: “Bila ya kuathiri masharti ya Katiba hiyo au sheria nyingine yoyote iliyotungwa na Bunge, iwapo sheria yoyote iliyotungwa inayotumika Tanzania Baraza na vile vile Tanzania Visiwani, imekabidhi madaraka yote kwa Mahakama Kuu, basi Mahakama Kuu ya Zanzibar yaweza kutekeleza Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.”

Ufafanuzi mwingine kifungu cha 116(1): “Bila ya kuathiri masharti ya ibara ndogo ya pil, Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania hatakuwa na madaraka juu ya jambo lolote linalohusu muundo na uendeshaji wa shughuli za siku hadi sikuw za mahakama zilizoundwa kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar au sheria yoyote ya Tanzania Zanzibar.”

Pia naomba ufafanuzi mwingine, kifungu cha 127(1) ukurasa 107: “Mahakama Maalum ya Katiba itakuwa na Wajumbe ambapo nusu ya Wajumbe wote watateuliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano na nusu nyingine ya jumla hiyo watateuliwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.”

Kifungu cha mwisho ni kifungu 128(3)

(Hapa kengele ililia kuashiria muda wa mzungumzaji kwisha)

MHE. ALI SAID SALIM:  Afanaleki! Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi/Kicheko)

MHE. SIRAJU J. KABOYONGA:  Mhe. Mwenyekiti kuhusu utaratibu.

MWENYEKITI: Kuhusu utaratibu Mheshimiwa Kaboyonga.

MHE. SIRAJU J. KABOYONGA: Kama nilivyoanza pale mwanzo, sasa nakwenda kwenye kifungu cha 64(1)(g) kwamba, Mbunge hatatumia lugha ya kuudhi au inayodhalilisha watu wengine.  Sasa nimeonekana kulifuatilia hili jambo kwa maana tu ya kumbukumbu zetu kwamba, mzungumzaji aliyemaliza sasa hivi kusema kweli yale maneno ya kwamba mkuki kwa nguruwe kwa mwanadamu mchunge, huo ni usemi lakini hapa ndani tunapaswa kuzungumza kistaarabu.  Hakuna nguruwe humu ndani au wapo?  Kwa hivyo, ndiyo nilikuwa nataka mwongozo wako kama lugha hii inastahili kutumika humu ndani . (ndani)

MWENYEKITI:  Waheshimiwa Wabunge, Mheshimiwa kaboyonga, ametumia kanuni hiyo namba 64, ambayo inazungumzia mambo yasiyoruhusiwa Bungeni na kifungu (g) kinamtaka Mbunge asitumie lugha ya kuudhi au inayodhalilisha watu wengine.  Waheshimiwa Wabunge, nafikiri lugha iliyotumiwa ni usemi wa kawaida.  Naomba utulivu ndani ya ukumbi.

Kwa kuwa lugha hiyo mahali ilipotumiwa na wakati ilipotumiwa inaoanisha na masuala yanayoweza kuudhi Wabunge wengine ndani ya Ukumbi wa Bunge; kwa maana hiyo, Mheshimiwa Salim maelezo yako yalikuwa na maana na mantiki, lakini lugha uliyoitumia na msamiati ulioutumia kwa wakati ulioutumia umeudhi watu wengine.  Ninaomba uondoe msamiati huo na maelezo yako mengine yabakie katika utaratibu unaotakiwa.

MHE. ALI SAID SALIM:  Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kama ulivyosema Mheshimiwa Kaboyonga kwamba, nimeudhi katika kutumia msamiati huu ambao ni kawaida kutumiwa, basi naondoa maneno hayo. (Makofi)

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, URATIBU NA BUNGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu utaratibu.

MWENYEKITI:  Kuhusu utaratibu Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera Uratibu na Bunge.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, URATIBU NA BUNGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nilikuwa nasubiri Mheshimiwa Mbunge amalize hotuba yake bila kusumbuliwa ili baadaye nimrejeshe kwenye kanuni hiyo hiyo ya 64(1)(a) kuhusu utaratbu.  Lakini twende pale pale ….

MWENYEKITI: Naomba ili twende sawasawa, unatumia kanuni gani Waziri?

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, URATIBU NA BUNGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, Kanuni ya 64(1)(a).

MWENYEKITI: Ndiyo.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, URATIBU NA BUNGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, bila kuathiri masharti ya ibara ya 100 ya Katiba yanayolinda na kuhifadhi uhuru wa maawazo na majadiliano katika Bunge, Mbunge hatatoa ndani ya Bunge taarifa ambazo hazina ukweli na hatazungumza jambo lile ambalo halipo kwenye mjadala.  Hili ni la kwanza.

Mheshimiwa Mbunge amesema kwamba, mabadiliko ya mwaka 1994, mliyafanya nyinyi kwa maana ambayo inaonekana ni Waheshimiwa Wabunge wa upande wa Tanzania Bara, upande mmoja ndiyo uliopitisha mabadiliko yake ya mwaka 1994 ambapo Waheshimiwa Wabunge wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndiyo waliopitisha Katiba ile. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mbunge, Mheshimiwa Waziri ametumia tena Kanuni hiyo namba 64 na amegundua kwamba, katika maelezo yako umekiuka kanuni namba 64(1)(a); hukusema ukweli kuhusu mabadiliko ya Katiba kwamba yalipitishwa tu na Kambi ya Upinzani na siyo Bunge zima. Kauli hiyo haina ukweli; ni kwamba Katiba ile ilipitishwa na Bunge zima. Kwa hiyo, baada ya kukusikiliza na kugundua pale hapakuwa sahihi, basi pia ameomba uondoe ile ili kuweka kumbukumbu sawa.

MHE. ALI SAID SALIM:  Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nadhani wakati ule ilikuwa ni chama kimoja na jambo zito kama lile lingehitaji maamuzi au maoni ya wananchi wote.  Lakini kama hiyo imekuwa kimantiki kwamba ndiyo iliamuliwa na Zanzibar kwa tafsiri yenu nyinyi ni sawa. Kwa kweli jambo kama hilo, lilihitaji maamuzi ya nchi nzima na kwa hapo ninaondoa usemi wangu.

MHE. PETER J. SERUKAMBA:  Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa. Kwanza lililopo mbele yangu.

MHE. ALI SAID SALIM:  Mheshimiwa Mwenyekiti, nafuta usemi wangu.

MWENYEKITI: Waheshimiwa Wabunge, ameondoa usemi na kwa kuwa ameondoa usemi, ningeomba tutumie muda uliobaki kumsikiliza Mbunge aliyebakia kuliko kuendeleza tena hilo ambalo lipo mezani.  (Makofi)

MHE. PETER J. SERUKAMBA:  Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI:  Taarifa Mheshimiwa Peter Serukamba.

MHE. PETER J. SERUKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo ibara ya 64(1) ya kanuni nilitaka kuweka record clear.

MWENYEKITI: Ibara gani”

MHE. PETER J. SERUKAMBA: Ibara namba 64(1) (a).

MWENYEKITI: Ya Kanuni?

MHE. PETER J. SERUKAMBA: Ya Kanuni

MWENYEKITI: Ndiyo

MHE. PETER J. SERUKAMBA: Nilitaka kusema il kuweka record clear; mwaka 1994 kweli lilikuwa ni Bunge lla Chama kimoja, lakini katika Bunge hilo walikuwepo pia Wazanzibari.  Kwa hiyo, naamini mabadiliko yale yaliwahusu pia na Wazanzibari. (Makofi)

MWENYEKITI:  Nakushukuru kwa taarifa, kwa maana ya kwamba, pande zote mbili za Muungano zilishiriki katika maamuzi hayo. Mhe. Lucas Selelii.

 

Advertisements

One thought on “Bunge lamalizika kwa kishindo kizito cha Muungano

  1. Nashindwa kuelewa ni kwa nini Tanzani wameweka kijibendera cha Muungano kwenye bendera ya Zanzibar. Zanzibar sio koloni la Tanzania bali ni sehemu ya Muungano. Makoloni ya Uingereza kama vile Kanada na Australia ndio yna kijibendera cha UK, lakini nchi zinazotendeneza Munungano wa Uingereza kama vile Scotland na Ireland hazina kijibendera hichi.

    Hizi dharau dhidi ya Zanzibar na Wazanzibari haziwezi kuisha mpaka Muungano utakapomalizika.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s