SMZ haikuwatendea haki vijana wa Jua Kali

Mwezi uliopita, Julai 2008, SMZ ilitekeleza amri yake ya kuwaondosha wafanyabiashara ndogondogo katikati ya mji wa Zanzibar, Darajani, wanaojuilikana kama ‘vijana wa Jua Kali’ na kuwalazimisha kwenda katika eneo la Saateni, ambako hata hivyo hakuna na matayarisho ya kuwaweka vijana hao waliojiajiri wenyewe. Kikiwa chama kinachosimamia misingi ya haki za binaadamu na uhuru binafsi wa kujiendeleza, CUF inaiunga mkono Jua Kali kama sekta binafsi na inalaani kitendo cha kuwafukuza vijana hawa katika maeneo yao ya kazi bila ya kupewa eneo mbadala na la kibiashara. Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani kwa Wizara ya Kazi, Maendeleo ya Vijana, Wanawake na Watoto katika Baraza la Wawakilishi, Bi Aziza Nabahan, anabainisha msimamo wa CUF katika hotuba hii ya kuchangia makadirio ya matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2008/2009.

Saateni, Mjini Unguja. Hapa ndipo vijana wa Jua Kali walipokuja kutupwa na serikali ili wafanye biashara zao.

Saateni, Mjini Unguja. Hapa ndipo vijana wa Jua Kali walipokuja kutupwa na serikali ili wafanye biashara zao.

Utangulizi

Mheshimiwa Spika,

Awali ya yote, kwa niaba yangu na kwa niaba ya Kambi ya Upinzani namshukuru Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema na Utukufu, mwenye Uwezo kuliko vyote duniani kwa kutujaalia uzima na afya njema kuweza kujadili masuala ya nchi ya Zanzibar.

Mheshimiwa Spika,

Pia nawashukuru wanawake wote wa Tanzania na zaidi wale wa Chama Changu cha CUF chini  ya Mwenyekiti Prof. Ibrahim Lipumba walioshiriki kunileta katika Baraza hili ili niwasilishe maoni yao juu ya mambo mbalimbali ya maendeleo ya nchi pamoja na matatizo wanayokabiliana nayo katika maisha ya kila siku.  Pamoja na hao, nakushukuru wewe Mhe. Spika kwa kunipa nafasi hii.

Hali ya Ajira Nchini

Mhe. Spika,

Masuala ya kazi ambayo ndiyo yanayoshughulikiwa na Wizara hii hayawezi kuelezewa kwa umakini na kupimwa kwa uhakika bila ya kuelezea hali ya ajira katika nchi. Katika suala zima la ajira tuliitarajia Wizara hii angalau kwanza itueleze kiwango cha wasio na ajira katika nchi ya kuwa Sekta za uzalishaji, biashara, kilimo, utalii na uwekezaji chini ya Wizara husika pamoja na Sekta binafsi ndizo zilizopewa dhamana ya kushughulikia ajira chini ya Mpango wa Kupunguza Umasikini Zanzibar (MKUZA).  Ukosefu wa ajira katika nchi yetu ya Zanzibar hasa kwa vijana wanaomaliza masomo yao katika ngazi mbali mbali bado ni mkubwa na unatishia hata usalama wa kawaida wa maisha ya watu.

Mhe. Spika,

Katika hali ya kawaida unaweza kupima ukosefu wa ajira kutokana na kuongezeka kwa watu wanaozurura ovyo mitaani hasa mijini, vijana waliokata tamaa na kutumbukia katika matumizi ya madawa ya kulevya, waombaji waliokithiri na kila rika na jinsia, ongezeko la ajira ya watoto pamoja na uhalifu wa kutumia silaha.  Mambo yote haya hapa Zanzibar yameongezeka kwa kazi inayodhihirisha kushindwa kwa Serikali katika kuidhibiti.  Mhe. Spika, si katika hotuba ya Bajeti ya Serikali wala Bajeti hii ya Wizara inayoratibu masuala ya kazi zilizoweza kutueleza kiwango cha ukosefu wa ajira nchini.  Na kwa hivyo, ni dhahiri kuwa hali hii ni mbaya na pengine ndio sababu serikali inaogopa kuitaja.

Mhe. Spika,

Katika ajira inayotolewa na Serikali, bado kunaonekana kuwa na ongezeko kubwa la ajira katika vikosi vya ulinzi ambavyo havionekani kusaidia hata katika kudhibiti uhalifu. Kwa mfano, wafanya biashara ambao ndio tegemeo kubwa la Serikali katika mapato na pia tegemeo la watu katika upatikanaji wa bidhaa, huduma na ajira, wanaendelea kupotezewa maisha yao kwa wizi wa silaha ambazo kisheria humilikiwa na Serikali tu. Hali hii ya kutisha katika nchi ndogo kama hii inarejesha nyuma matumaini ya Sekta binafsi tuliyoipa dhamana ya kuongeza kasi ya uchumi nchini.

Mhe. Spika,

Katika hali ya kawaida, nchi hupungukiwa sana na uwekezaji kutoka ndani na nje panapokuwa na hatari za kiuchumi (economic risks). Uhalifu ni sehemu moja ya hatari hizo na nimeamua nizipe nafasi ya awali kwani maslahi ya kazi katika sekta binafsi ni pamoja na usalama wao na mali zao. Ni matumaini yangu kuwa Serikali italingalia upya suala hii sambamba na kutoa ulinzi wa kutosha kuzuia uhalifu usiongezeke kama njia ya kushajiisha uwekezaji na ajira kwa vijana wetu.

Mhe. Spika,

Wakati ajira katika sekta ya utawala ikiongezeka, imedhihirika kuwa ajira katika sekta ya umma inayoshughulikia uzalishaji na utoaji huduma inazidi kuzorota kutokana na kasi ndogo ya kupanuka kwa sekta hizo.  Sasa hivi uwekezaji hasa wa majenzi katika sekta ya utalii umepungua licha ya kuwa sekta ya ujenzi yenyewe inaongeka. Makampuni ya kigeni yalikuwa yakitoa hudhuma katika kandarasi za miundombinu ya barabara na uwanja wa ndege yameondoka katika hali ya utata na kuwaacha vijana bila kazi.  Maslahi madogo katika kilimo yanapunguza imani ya watu kuendelea na ajira hiyo muhimu.

Mhe. Spika,

Unyeti wa taarifa ya kukatika kwa kandarasi nyingi nchini unaweza kusababishwa na mikataba isiyozingatia sheria au cheche za ufisadi ambazo kwa kuwa hazijaripuka ndio tunaona mambo yote Serikali ni sawa kumbe sivyo kabisa. Mhe. Spika, zaidi ya hayo, bado kuongezeka kwa vijana wanaomaliza masomo katika fani mbalimbali bila ya kazi ni dalili nyengine kuwa Sekta ya umma ya huduma za uchumi nayo haipanuki kwa kasi. Mhe. Spika, tunaamini kuwa wakati Sekta binafsi ikipanuka Sekta ya Umma inapungua lakini kupungua huku hakumaanishi kupungua kwa ufanisi kazini. Kwa sekta binafsi kukosa uwezo wa kupatia kazi vijana wenye ujuzi huku maofisa na watendaji wengi Serikali wakiendelea kutegemea uzoefu usiozingatia mabadiliko ya teknologia ya kileo ni kielelezo cha kupungua kwa Sekta ya Umma hata katika ufanisi.

Ajira za Watoto

Mhe. Spika,

Wakati Serikali ikisema inaendelea na matayarisho ya Sera na mikakati ya kudhibiti ajira za watoto, ukweli ni kwamba ajira hizi bado zinaendelea kukithiri nchini. Suala kubwa tunalotakiwa kulipatia jibu kabla ya sera hiyo ni jee, nini sababu kubwa ya ajira ya watoto? Kwa maoni yangu, ajira ya watoto kwa kiasi kikubwa inasababishwa na umasikini wa wazee wao na kwa kiasi kidogo umasikini wa watoto wasio na makao maalum na ya kutegemea. Kwa Zanzibar, kwa kuwa hili la awali ndio sababu kubwa na kwa kuwa hata MKUZA haujaweza kuutukusa umasikini na sasa Serikali inazungumzia ufukara kuliko hata umasikini, ni dhahiri basi sera ya kudhibiti ajira ya watoto itabakia kuwa ni nadharia isiyo na mbinu ya utekelezaji.

Mhe. Spika,

Sisi katika Baraza hili tuna wasiwasi kuwa kuporomoka kwa maadili malezi katika nchi yetu pia kunaendeleza ajira ya watoto kwani miaka ya nyuma wazee wote walikuwa walezi wa watoto katika jamii jambo ambalo leo ni hadithi. Napenda nimuulize Mhe. Waziri, jee hili atalitanyia mbinu gani ili sera yake ifanye kazi? Mhe. Spika, ili tuamini kuwa Wizara inaweza kutengeneza sera itakayotekelezeka tena kwa mafanikio, basi tunaiomba Wizara hii itupatie utafiti angalau tujifunze juu ya ukubwa na sababu za ajira za watoto katika nchi yetu ya Zanzibar. Mhe. Spika, pamoja na ajira ya watoto, pia wapo watoto wasio na ajira lakini waliokosa uhifadhi na matunzo bora katika sehemu wanazoishi hasa kutokana na hali mbaya ya maisha ya walezi wao.  Tunaamini kuwa watoto hawa ambao athari ya umasikini kwao ni kubwa zaidi pia watazingatiwa katika sera inayowahusu wale wenye ajira.

Sekta isiyo Rasmi

Mhe. Spika,

Huku sekta binafsi na ile ya umma zikionesha matatizo mbali mbali katika suala la ajira na maslahi ya kazi, kambi ya upinzani ina masikitiko makubwa na namna Serikali inavyolishughulikia suala la vijana wanaojishughulisha kupunguza umasikini katika Sekta isiyo Rasmi.  Ni miaka kadhaa sasa tokea Serikali ilipotoa ahadi kupitia Baraza hili kuwa ingeliwapatia vijana wa Jua Kali sehemu ya Saateni ili waendeleze biashara zao. Sisi tulidhani Serikali ilikuwa na nia njema na ya dhati lakini tumesikitishwa sana tunaposhuhudia katika utekelezaji kkuwa kumbe Serikali ilikuwa na nia ya kuwavunjia kazi zao kabisa kabisa.

Mhe. Spika,

Kitendo cha Serikali kuwahamisha bila ya kukamilisha majenzi katika sehemu hizo za Saateni hakikubaliki licha ya kuwa ni kitendo cha ajabu na aibu kufanywa na Serikali inayojinadi kwa kuwa na utawala wa sheria na utawala bora. Haiwezekani hata kidogo umma wote wa Jua Kali upangiwe sehemu ndogo kama ile banda moja la Saateni kumbe kama Serikali ingekuwa na nia njema ingeweza tu kuwapatia viwanja hivyo ili wajijengee wenyewe. Hata hivyo, kama kawaida inasikitisha kuwa viwanja vingi vimechukuliwa na baadhi ya watu wenye uwezo kwa maslahi yao ya kibinafsi kuliko kuzingatia jamii inayoisaidia Serikali katika vita dhidi ya umasikini. Baada ya hayo, kinachoshuhudiwa ni matumizi ya nguvu yanayofanywa na askari wa Manispaa katika kuwahamisha. Hii si njia nzuri hata kidogo na zaidi ni njia ya vitisho ambayo kwa kawaida haitumiwi na Serikali inayojinadi kwa demokrasia.

Mhe. Spika,

Wizara imesema inategemea mikakati shirikishi katika mipango na sera zake, lakini vitendo vyake ni tafauti na sera zake. Katika hali kama ile ya Jua Kali inaonesha wazi kuwa ukosefu wa kazi katika nchi hii unachangiwa na kukosekana kwa mipango madhubuti ya Serikali inayolenga ushirikishwaji wa kweli wa wananchi katika shughuli zao za maisha. Lakini, iwapo Serikali  inajiamini katika mipango yake, ni dhahiri basi usimamizi wake unatia dosari adhman na utekelezaji wa mipango hiyo; hasa kwa vile utekelezaji unahusisha Wizara na Idara nyengine isiyokuwa hii inayopanga. Hii ndio maana wakati katika hotuba hii panahubiriwa ushirikishi, Darajani kwenye walengwa wa ushirikishi kunatembezwa marungu kuvuruga ushirikishi huo. Hata pale Serikali inapojitetea kuwa inasimamia sheria, lazima pia ielewe kuwa hata sheria na taratibu katika nchi ya kidemokrasia huwa ni shirikishi.

Mhe. Spika,

Ni matumaini yetu kuwa Serikali italiangalia upya suala la vijana wa Jua Kali na hatua za kistaarabu na za kiungwana zitatumika katika kuwaondosha katika makazi yao sambamba na kuwapatia sehemu bora kwa ajili ya kuendeleza kazi zao.  Serikali kivuli inaiomba Serikali Kuu kuingilia kati na kuwaongezea muda vijana hawa hadi itakapokamilisha mpango wake wa kuwahamisha.  Tunaamini kuwa mpango nzuri ni kuwapatia viwanja kwa vikundi na kuwapatia plan za majengo hata ya ghorofa moja ili sehemu hiyo ndogo iweze kuchukua vijana wengi katika mazingira mazuri ya kibiashara.

Uhamiaji holela katika Nchi

Mhe. Spika,

Zanzibar iwe ni nchi au si nchi na bila shaka kama ilipotakiwa kuunganishwa ilikuwa ni nchi na leo tena haiwezi kuwa si nchi labda iwe wenzetu wanahamu isiwe nchi.  Kwa mnasabab huo basi, Zanzibar ina chimbuko la historia, mila, silka, utamaduni wake, tena kwa kiwango kikubwa vikitafautiana na sehemu nyengine za dunia, tena hata Tanzania Bara ambao tun udugu wa kimuungano wa miaka 44 sasa.  Kionjo kimoja katika Historia kinachoithibitisha kuwa Zanzibar ina historia ya kipekee ni kule kutawaliwa na wageni kwa dahari bila ya watawala kuzifanya lugha zao kuwa ndio za Taifa la Zanzibar.

Mhe. Spka, katika mfano huo huo Zanzibar ikizungukwa na Mataifa makubwa wakati huo kama Tanganyika, Kenya na Uganda katika mashirikiano ya kikanda, lakini haikuwezekana pamoja na udago wake kuiba lugha yoyote ya mataifa hayo ikawa ndio lugha rasmi ya Zanzibar.

Mhe. Spika,

Kiswahili kinachoelezwa leo kuwa ni kiungo cha Watanzania, hakikuwa na mbadala Zanzibar kwa karne zilizopita hadi leo ambapo eti tunaambiwa sasa chetu sisi kimepitwa na wakati na tunatakiwa kusoma kwengine.

Mhe. Spika, katika hali ya uungwana akutukanae hakuchagulii tusi na wala akufukuzae hakwambii toka ila hufanya vitendo ili mwenye kufahamu afahamu. Hata hivyo, nataasaf kusema kuwa hatafahamu mtu ila awe ana uchungu na yale yatokeayo. Mhe. Spika, moja katika sababu kubwa zinazopelekea wengine waseme kuwa Zanzibar si nchi ni kutokana na maamuzi ya Serikali ya kuiwachia nchi hii ihamiwe na kila mtu tena kutoka popote bila kuulizwa. Mhe. Spika, hii kweli kuwa katika mantiki na maana ya kinchi hili halifanyiki katika nchi nyengine duniani, isipokuwa Zanzibar.

Mhe. Spika,

Uhamiaji holela unaendelea kwa kasi ya aina yake hapa Zanzibar unapunguza uwezo wa Serikali kumudu utekelezaji wa mipango yake ambayo bila shaka ilizingatie idadi ya watu. Sambamba na hili, ongezeko la watu hapa Zanzibar limejidhihirisha katika suta tatu kubwa. Kwanza, wahamiaji hawawezi kuishi bila ya kufanya kazi na kwa hivyo, nafasi nyingi za ajira zilizotarajiwa kuwanufaisha watu wetu zinaangukia katika mikono ya watu wasiohusika. Pili, baadhi ya wageni hujiingiza katika wahamiaji wanapokosa  kazi za kufanya na soko la kufanyia ukahaba, kinachoendelea ni biashara haramu na wizi wa kutumia nguvu na silaha.

Mhe. Spika, kuna msemo kuwa “mgeni hachomi pweza akanuka” na wageni kwa kufahamu haya huendesha vitendo vyao haramu kwa mashirikiano na watu wetu ambao wengi ni vijana waliokata tamaa ya maisha kwa ukosefu wa kazi. Mhe. Spika, matokeo yake ni kuwa uhamiaji holela unapunguza nafasi za kazi na pia unaambukiza maradhi ya kiroho na kimwili. Hali hii inazidi kutuongezea umasikini na maisha bora kwa Mtanzania hayajafika Zanzibar na ingawa hakuna dalili ya kufika kwengine kokote kamwe. Haya yakitokea, wasio na nia njema wanayo sababu ya kusema Zanzibar si nchi hasa kwa vile malengo yao ya siri ya siku nyingi sasa yanakamilika.

Wanawake na Walemavu

Mhe. Spika,

Nakusudia kuwasemea wanawake sambamba na walemavu kwa kuwa makundi haya yanahitaji msaada mkubwa wa Serikali ili yajikwamue katika matatizo yao. Kwa upande wa wanawake, ni kweli sasa kuna ongezeko la elimu na taaluma hasa kwa vile idadi ya wale wanaomaliza masomo ya juu inaongezeka. Hata hivyo, bado kuna sehemu ya jamii ambayo haijaweza kuondosha makucha ya unyanyapaa yaliyodumu kwa karne nyingi dhidi yao. Wanaume ambao ndio mabosi katika sekta nyingi za ajira hawajasafisha tamaa mbaya kwa wanawake wanapotaka ajira. Wako wanaopata ajira huku wakishirikishwa katika vitendo vya ufuska kinyume na maadili kwa kuwa tu kufanya hivyo na mabosi kunaweza kumpatia mwanamke nafasi ya kusomea zaidi au kuongezwa cheo.

Mhe. Spika,

Sisemi hivi ili kinababa walioruhusu wake zao wafanye kazi waanze kulia wivu, lakini nasema hivi kuwatanabahisha wanawake kuwa wanayo haki sawa na wanaume katika masuala ya nchi na kwamba hawastahiki kuyumbishwa kimaadili kwa tamaa ya ajira, cheo au fedha.

Aidha nasema hivi pia kuwatanabahisha kuwa mabosi wenye tabia hii katika sehemu za kazi hawana tafauti na makahaba wowote wanaozurura katika mitaa na chochoro za mijini. Bila shaka, hiki ni chanzo kikuu cha kueneza Ukimwi ambao sote tumeamua kuupiga vita. Ukimwi haupigwi vita kwa kuwa unauwa tu, lakini zaidi unawaacha watoto na wazee wanaotegemea nguvu na msaada wa vijana ambao ndilo kundi kubwa la waathirika.

Mhe. Spika,

Serikali imeamua kuwakusanya wanawake ili washirikiane katika harakati za kujilletea maendeleo, lakini bado viko vitendo vinavyofanyiwa wanawake vinavyorudisha nyuma juhudi hizi za Serikali. Kwa mfano, katika wilaya ya Kusini – Makunduchi, wanawake wanaojishughulisha na kilimo cha mwani walidanganywa na mwekezaji wa hoteli ya kitalii kuwa wangelipwa fidia kutokana kuondoshewa vifaa vyao ambavyo ni pamoja na mawe wanayotumia katika mradi. Mhe. Spika, hata hivyo, tokea kuondoshwa mawe hayo, huu sasa ni zaidi ya mwaka mmoja malipo ya fidia yaliyofanywa kwao ni ya mwezi wa kwanza tu, miezi iliyofuata wameambukia matusi na kejeli za mwekezaji huyo.

Mhe. Spika,

Inasikitisha kuwa wakati uondoshaji wa mawe hayo ulisimamiwa na Sheha, sasa kiongozi huyo wa Shehia anashirikiana na mwekezaji kuwanyima wanawake hao haki yao. Huu ni ushahidi ulio wazi kuwa sera, mipango na mikakati ya Serikali hii ni tafauti na vitendo katika utekelezaji wake.

Mhe. Spika,

Sambamba na wanawake, walemavu nao wanakumbwa na matatizo makubwa ya kimaisha na misaada michache wanayopata baadhi yao haitoshi kumudu maisha.  Pamoja na matatizo ya kiuchumi kwa walemavu, pia wao ni waathirika wakubwa na matatizo ya kijamii sehemu nyingi za nchi yetu.

Mhe. Spika,

Katika sehemu za mashamba ambako miundombinu ya barabara ni mibaya, walemavu hawawezi kusaidiwa na kigari ambacho mjini hukitumia kuendea skuli na hata katika masoko na kwenye hafla nyengine za kijamii. Katika ajira, walemavu wengi hawana fursa ya kutumia visaidizi vinavyotumiwa na wengine nchi nyengine kuhakikisha kazi zao za maisha.  Mhe. Spika, nina imani kuwa Waziri ataweka katika sera za Wizara yake njia bora za kuwasaidia walemavu waongeze kipato na huduma za jamii kutokana na fursa za ajira ambazo wengine wnazitegemea.

Maslahi ya Kazi Nchini

Mhe. Spika,

Maslahi ya kazi ni kiungo muhimu cha ufanisi kazini. Bado kuna hali mbaya katika Sekta za umma na binafsi kutoka na wafanyakazi kukosa maslahi ya kazi. Kwa mujibu wa wanafalsafa wa fani ya utawala kama vile Abraham Maslow, motisha ya kazi zinatokana na malipo yanayolingana na ajira pamoja na wadhifa anaostahiki mfanyakazi. Si hayo tu, lakini ziko motisha nyengine tafauti na fedha na wadhifa na hizi ni mazingira bora na salama pamoja fursa za kupumzika na kutembea kuburudika baada ya kazi.

Mhe. Spika,

Kwa upande wa maslahi ya kifedha, bado mishahara na marupurupu mengine kwa wafanyakazi wengi hasa wa ngazi za chini midogo. Na hii si Serikali tu, lakini hata katika Sekta binafsi hasa katika mahoteli ya kitalii ambayo yanaendelea kupata faida kubwa ya kazi zao kwa jasho la watu wetu.

Mhe. Spika, katika hali nyengine ya kusikitisha ni kupitana kwa maslahi kusikolingana na ujuzi na uzoefu aliona mfanyakazi. Hali hii inazidi kupata nguvu hasa kwa vile Serikali haina Mfumo wa Utumishi (Scheme of Service) ulio bora. Tanzania Bara kwa ndugu zetu, kuna mfumo mzuri wa utumishi katika ualimu na kwa hivyo, mwalimu hunasibika na daraja mbalimbali kabla ya kupandishwa ngazi na kuwa msimamizi au mwalimu mkuu. Hapa Zanzibar, hadi leo wako walimu wakuu wenye elimu ya UPE ambao wanawasimamia walimu wenzao wenye elimu ya Chuo Kikuu.

Mhe. Spika, vile vile wako wahasibu wakuu wana Ordinary Diploma wanaowasimamia wasaidizi wahasibu wenye CPA, na hivyo hivyo hali ni sawa katika sekta nyengine.

Mhe. Spika,

Katika siku za nyuma mfanyakazi alikuwa akifahamu lini ataongezwa mshahara na lini atachukua likizo na kusafiri kwa posho ya safari ya likizo. Sidhani kuwa mambo haya bado yanaendelezwa kazini leo katika karne ya sayansi na teknolojia.

Mhe. Spika, ziko sehemu nyingi za sekta binafsi ambazo mishahara ni chini ya hata kiwango cha Serikali na wizara hii imekaa kimya. Wafanyakazi kuajiriwa bila ya mikataba ya kudumu ili ipatikane nafasi (loophole) ya kuwafukuza kiholela.  Zimo sehemu nyingi za kazi, hamna vifaa vya kujikinga na ajali kama vile gloves na viatu, lakini bado wananchi wanachapa kazi kutumisha maslahi ya wawekezaji.

Mhe. Spika,

Tunapata malalamiko ya wafanyakazi wanaokaa zaidi ya maa 10 kazini bila ya chakula cha kutosha cha kukifu tumbo moja tu.  Nyingi ya kazi hizi ni za mabavu na ulinzi.  Mhe. Spika, hivyo unafahamu kuwa katika nchi hii ya kimapinduzi, bado wananchi wake hawana uzoefu wa ulinzi kiasi kwamba makampuni mengi yanayota huduma za ulinzi zinatoka nje ya Zanzibar! Hii ni aibu nyengine na haiwezi kutokea katika nchi iwapo hakuna harufu ya rushwa na ufisadi.  Kama hili la ulinzi ni kubwa, nini kinachowafanya watu kutoka bara jengine la Afrika kuruhusiwa kugawa chakula katika maholi?  Mhe. Spika, hizi zote ni changamoto ambazo Wizara hii haina budi izishughulikie ili kuinuwa kiwango cha ajira kwa wazalendo ambao wakinyimwa fursa hii, pakukimbilia ni kwa madawa ya kulevya na ujambazi.

Vita dhidi ya Ukimwi

Mhe. Spika,

Kama wizara nyengine za Serikali ya Mapinduzi, Wizara hii inatumia fedha kwa kuhamasishwa wafanyakazi wajikinge na ukimwi.  Sisi hatuoni choyo kwa hilo, ila vita hii ambayo iko kwa wananchi wasio chini ya Wizara inahitaji nyenzo pia.  Naishauri Serikali sasa idhinishe matumizi ya fedha hizi kwa Wawakilishi wako ili wakahamasishe umm uliowachagua. Hili litatoa ufanisi mkubwa zaidi tena kwa matumizi madogo zaidi ya fedha.

Mhe. Spika, hili sisemi kwa mzaha ila sote n mashahidi kuwa walengwa ni vijana na watu ambao hapana awezae kupinga kuwa wako karibu zaidi na Wawakilishi wako kuliko maafisa wa Serikali waliaminiwa kufanya kazi hii.

Miradi Shirikishi katika Jamii

Mhe. Spika,

Serikali imeamua kuwa na miradi shirikishi katika kuwaletea wanancho maendeleo yao.  Sisi katika Kambi ya Upinzani tunaamini kuwa huu si mpango mbaya, lakini tunasikitishwa na namna ugawaji wa nyenzo hizi usivyokuwa na uiano Kimajimbo, Kiwilaya na ha Kimikoa. Mhe. Spika, imesadifu kwamba, kwa kuwa Serikali huwa inatangaza kuwa inatekeleza Ilani ya Chama chake ya Uchaguzi, basi hata walengwa wakuu wa ruzuku na mikopo nafuu hupelekwa zaidi kwa hao wanaominika kuwa wananasibika na Ilani yenyewe. Hiki si kilio changu peke yangu ila ni cha Wawakilishi wako hasa katika kambi ya Chama changu cha CUF ambacho Ilani yake itaanza kutekelezwa mwaka 2010.

Mhe. Spika,

Sisi tunaomba sana kuwa uadilifu utumike katika suala hili na wananchi bila ya kujali imani na itikadi zao za kisiasa wanufaike na fedha ambazo ama chanzo chake ni kodi inayolipwa na kila mtu au misaada na mikopo ya wahisani ambayo pia haikukusudiwa kuwabaguwa watu kwa misingi yoyote ile.

Mhe. Spika, katika makundi ambayo yanashajiishwa sana na Serikali za awamu hii ni kupitia vyama vya kukopa na kulipa SACCOS. Tayari katika mbwembwe zote za nchi kuwa SACCOS zilizoanza kufanya kazi na ingawa ziko nyengine zinasubiri Mapesa ya JK na AK ndiyo yaanze kazi.

Mhe. Spika ilivyokuwa, zote zipo kisheria, hatuna sababu kwa nini tusiziunge mkono, lakini ni matumaini yetu kuwa zilizotangulia utekelezaji hazitoachwa nyuma katika kupewa msukumo wa kuziimarisha zaidi.

Hitimisho

Mhe. Spika,

Nachukua nafasi hii ya mwisho kuishauri Wizara kujitahidi kusimamia masuala ya kazi ili kuongeza ufanisi na tija katika sekta za umma na binafsi.  Naamini kupatikana kwa viojo hivi kutatokana na usimamizi thabiti wa sheria za kazi zinazokataa kumdhalisha mwanamke kijinsia, zinahimiza maslahi bora kazini, zinazojali mazingira ya afya na usalama kazini, zinazoshajiisha vita dhidi ya ajira kwa watoto, zizizotoa mwanya wa upungufu wa ajira nchini na zisizozorotesha ushiriki wa wananchi katika kujiletea maenedeleo yao.

Mhe. Spika,

Ili Wizara hii ifanikishe malengo yake, Sheria za kazi, sera na Mipango ya Serikali lazima iepukane na kila chembe ya unyanyapaa ama wa kijinsia, kimaumbile au wa imani na itikadi ya kisiasa.  Hata hivyo, Mhe. Spika, kwa ujumla malengo na maamuru ya kiuchumi yatakayosimamia kazi yenye tija katika nchi hii yatapatikana kwa wasaa, urahisi na ufanisi zaidi iwapo Wazanzibari wataacha kila tafauti isiyowasaidia kwa sasa ili kusimama kidete kwanza kuitambua na baadae kusimamia mipaka ya nchi ya Zanzibar, sio tu angani na baharini lakini hasa katika Sheria mama ya makubaliano ya Muungano wetu na halafu ndani ya Sheria zilizofuata baada hapo.  Bila shaka kwa kuwa penye nia iko njia na kwa kuwa “inawezekana, basi tutimize wajibu wetu”

Mwisho kabisa, nakushukuru tena, Mhe. Spika, kwa ruhusa hii adhimu na pia nawashukuru Wajumbe wako kwa kunivumilia na kunisikiliza kwa makini.

Kwa niaba yangu na kwa niaba ya Kambi ya Upinzani, naomba kuwasilisha.

Aziza Nabhan Suleiman (MBLW)

Waziri Kivuli, Wizara ya Kazi,

Maendeleo ya Vijana, Wanawake na Watoto

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s