Kuna harufu ya ufisadi mkubwa Zanzibar

Tangu ile Orodha ya Mafisadi (List of Shame) itangazwe hadharani na vyama vya Upinzani nchini, macho na masikio yote yameelekezwa katika taasisi za Serikali ya Muungano tu, huku chochote kikiwa hakisemwi, hakiandikwi wala hakisikiki kuhusu ufisadi ndani ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Kimya hiki cha umma na hasa vyombo vya habari kimewahi kumpa juburi Amani Karume kudai kwamba serikali yake haina mafisadi. Lakini CUF imenusa harufu ya ufisadi mkubwa Zanzibar kupitia zabuni za ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Zanzibar, gati ya Malindi, barabara, Shirika la Meli na katika fursa za usimamizi wa Bajeti kwa visiwa viwili vya Unguja na Pemba; na sasa, kupitia msemaji wake wa Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi kwenye Baraza la Wawakilishi, Said Ali Mbarouk (CUF, Gando), inataka Tume huru iundwe kuchunguza zabuni hizo. Serikali ina majibu?

Gati ya Malindi, Zanzibar, ikiwa katika ujenzi unaondelea sasa ambao CUF inaamini kwamba una harufu ya ufisadi

Gati ya Malindi, Zanzibar, ikiwa katika ujenzi unaondelea sasa ambao CUF inaamini kwamba una harufu ya ufisadi

Mhe, Spika,

Ninaanza kwa kumshukuru Subhanahu Wataala na kumshukuru kwa neema ya uhai na uzima aliotupa na pia kuijaalia nchi hii ya Zanzibar ikiwa salama na watu wake. Naomba ukubali kupokea shukrani zangu kwa kunipa nafasi ndani ya ukumbi huu kutoa maoni ya kambi ya Upinzani juu ya hotuba ya Wizara hii. Naomba pia niwashukuru wananchi wa Jimbo la Gando kwa kuendelea kunipa mashirikiano katika utumishi wangu kwao.

Mhe. Spika,

Kwa niaba ya Kambi ya Upinzani ya Baraza lako tukufu, ninaomba nimpe pole Waziri wa Wizara hii Mhe. Brigedia Jenerali Mstaafu, Adam Mwakanjuki, kwa ugonjwa alionao, na kwa  baraka ya Ijumaa ya leo na siku ya 21 ya mwezi mtukufu  huu wa Rajabu, Mwenyezi Mungu amuondolee uzito wa maradhi na amjaalie apate nafuu apone. AMIN!

Mhe. Spika,

Wakati Waziri wa Wizara hii ni mgonjwa, inaelekea kiuendeshaji wizara yake nayo iko mahtuti, pengine I.C.U. Hii ni kutokana na kuyumba kwa shughuli na taasisi nyingi zinazofanya kazi chini yake.

USIMAMIZI WA ZABUNI ZA UJENZI

Mhe. Spika,

Katika maoni ya Kambi ya Upinzani ya miaka ya nyuma, nimekuwa nikionesha mashaka yangu juu ya mikataba ya ujenzi na usimamizi wa makampuni mbali mbali yanayosimamiwa na Wizara hii.

Nilionesha wasiwasi wangu wa namna usimamizi  wa Ujenzi wa Uwanja wa Ndege  wa Zanzibar ulivyokuwa dhaifu na wakizembe hali iliyosababisha nchi kupata hasara kubwa, huku hakuna ofisa hata mmoja aliyewajibishwa kwa uzembe au ufisadi, na hakuna uchunguzi wowote uliofanywa kujua tatizo lilikuwa wapi. Nchi imebakia na uwanja wa ndege usiokidhi haja, huku waliohusika wakiendelea kutanua.

Nilionyesha wasiwasi wangu pia juu ya danadana ya zabuni ya ujenzi wa Gati ya Malindi – mara gati ya nguzo, mara gati ya tuta, mara athari za mazingira, mara kampuni ya ujenzi sio. Alimradi ucheleweshaji mkubwa. Wafanyabiashara  wakaingia hasara, bidhaa  zikapanda bei, mfumuko wa bei ukapaa;  na pia hakuna yeyote  aliekemewa  na kuwajibishwa kwa uzembe au ufisadi na hakuna uchunguzi wowote uliofanywa kujua tatizo lilikuwa nini na nani mhusika.

Nilionesha wasi wasi wangu wa uwezo wa Kampuni ya Prismo juu ya ujengaji wa Barabara za Unguja baada ya matokeo ya udhaifu wa ujenzi wa barabara za Pemba. Pamoja na Wajumbe wa Baraza lako tukufu kukemea kwa kauli kali, bado Kampuni ya Prismo ilipewa zabuni ya ujenzi, na amelipwa mapesa mengi ya mkopo wa ADB pamoja na fedha za ndani. Mwishowe ameiacha kazi bila ya kufika popote, huku wananchi wakisumbuka kwa usafirishaji wa bidhaa na abiria. Nchi nayo ikiwa imepata hasara sana  kwa mkopo unaohitaji kulipwa na pesa iliotolewa na Serikali. Uendeshaji wa nchi wa namna hii hauonekani mwahala mwingi sasa. Hivi katika Wizara hii niulize anaetia hasara nchi namna hii na kuachiwa bila kuhojiwa, analindwa na nani?

Mhe.Spika,

Kwanza katika suala hili la Prismo, kwa maoni yangu inaonekana pamoja na udhaifu wa Kampuni ya Prismo, lakini pia usimamizi wa Serikali unaonekana ulikuwa na kasoro kubwa. Kwa hivyo, naomba kupata majibu kutoka kwa waziri:

  • Hivi kulikuwa na Mpango wowote ulioandaliwa wa utekelezaji wa kazi (Design for Execution), ambao Prismo alitakiwa kuufata? Kama upo, naomba kuuona.
  • Hivi kulikuwa na hati ya kukabidhiwa saiti ya kazi (Site Possession), kama ipo naomba kuiona.
  • Hivi hakukuwa na uchelewaji mkubwa wa kuondoa vikwazo kwenye kazi zenyewe (obstruction), kwa mfano nguzo za umeme, paipu za maji, waya wa radio ambao ulichelewesha utendaji kazi na Prismo na akapata mwanya wa kututega, na kutupiku?
  • Hivi Consultant – Black and Veatch South Africa Ltd – alikuwa na uhalali wa kufanya kazi hapa Zanzibar kisheria? Je, Kampuni ilisajiliwa katika msajili wa makampuni hapa Z’bar, au huwa hakuna umuhimu kisheria?

Mhe. Spika,

Ni kwa vipi Wizara hii ilizembea au niulize kulikuwa na ufisadi katika shughuli nzima wa mkataba na Prismo hata Prismo akapata nafasi ya kuvunja mkataba? Kwa sababu  hiyo, naomba  Tume ya Baraza lako iundwe kuchunguza  utaratibu wa usimamizi wa zabuni  katika Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi, na Tume ijikite katika zabuni za Uwanja wa Ndege na Kampuni ya Kichina, zabuni ya  Gati ya Malindi na Kampuni ya Phil na zabuni ya Barabara  ya Mazizini – Fumba, Amani – Dunga, Mfenesini – Bumbwini na Kampuni ya Prismo.

Mhe. Spika,

Naamini uundwaji wa Tume katika suala hili ni muhimu sana katika  kuona kwamba katika usimamizi wa zabuni na utekelezaji  wake siku za usoni, maslahi ya nchi yanalindwa, vyenginevyo itakua ni kulea uzembe na pengine ufisadi jambo ambalo ni hatari  sana kwa maendeleo ya wananchi.

BANDARI

Mhe. Spika,

Eneo  jengine, ambalo bado ni kitendawili kwa uchumi wa Zanzibar, ni uekezaji wa maana na uendeshaji wa shughuli  za Bandari. Kungekuwa  na umakini wa sera, sheria na uendeshaji ulio madhubuti kwenye sekta hii kwa jiografia ya Zanzibar ilipo, ingalikuwa ni tegemeo  kubwa kwa nchi nyingi za Afrika, hali ambayo ingelikuza uchumi wetu. Kinyume chake Zanzibar inategemea Bandari ya nchi jirani.

Ni kweli ujenzi wa gati ni jambo linalohitaji pesa nyingi, lakini siku hizi duniani kuna utaratibu wa Jenga, Endesha na Kabidhi (Build, Operate na Transfer) ambapo nchi hukubaliana na wenye pesa kwa utaratibu maalum ya kuwa na ubia wa kujenga, kuendesha na kukabidhiana gati. Hivi sasa nchi ya Djibouti imo njiani kujenga gati kubwa sana katika Bahari ya Hindi, na wenzetu Tanzania wana mpango wa kujenga Gati kubwa katika mji wa Bwagamoyo, kwa ubia na kampuni moja ya Ghuba. Sisi, Zanzibar, sera zetu ni za kibabaishaji mno, ambazo hazilengi kuondokana na umaskini wa kweli.

Mhe. Spika,

Jambo jengine linalotia wasiwasi katika Shirika la Bandari, ni kutokuwa na uwazi katika shughuli za uendeshaji wa shirika. Mwaka jana nilipokuwa natoa maoni ya Kambi ya Upinzani juu ya shughuli za bandari, nilimsihi waziri atoe mchanganuo wa kibajeti unaohusu mipango ya maendeleo na matumizi yake. Bahati mbaya hakuzingatia; na mara hii mchanganuo umekuwa wa mistari minne tu: “Kwa upande wa miradi ya maendeleo, Shirika linatarajia kuendelea na kuikamilisha miradi iliyoanzishwa mwaka wa fedha unaomalizika,” (uk. 39, aya 93). Kwa mtazamo wangu hii ni dhihaka.

Hii ni Bajeti ya Nchi. Ni muhimu kuainishwa kila kazi vizuri na fedha yake itayotumika ili Baraza lipime, lihoji au lishauri. Mimi kwa hapa sijaridhika.

Mhe. Spika,

Wafanyakazi wengi wanalalamikia menejimenti juu ya maslahi na fursa zao za kazi. Kwa mfano, hadi leo sehemu ya utumishi ya wafanyakazi imevungwavungwa. Ikiwa kuna waliofaidika, basi ni wachache. Nimearifiwa hata nyongeza ya mishahara ya wafanyakazi iliyotangazwa mara ya mwisho na Serikali kwa watumishi wake, bado katika Shirika la Bandari halijawa na utekelezaji ulio wazi. Katika hili, naomba ufafanuzi wa Mhe. Waziri: analielewa vipi suala hili,  na  ikiwa ni kweli ni kwa sababu ipi? Mbali ya hilo, naomba kufahamishwa gharama yote ya ujenzi wa gati mpya ya abiria, iligharimu shilingi ngapi, na Kampuni ngapi na zipi zilishindana?

Mhe. Spika,

Naomba kupata ufafanuzi na maelezo, ni lini Shirika la Bandari litapatiwa Bodi yake? Na hatuoni Shirika hili kufanya kazi bila ya Bodi kunazorotesha ufanisi wa kazi na kunaweza kusababisha matumizi ambayo yamefanywa bila ya utaratibu?

GATI YA WETE

Mhe. Spika,

Kwa muda mrefu sasa Wizara imekua na kauli ya ujenzi wa gati ya Wete, na kwamba lugha iliyokuwa ikitumika ni kuongeza mita 15-20 mbele. Kwa  lugha hii, mtu angefikiri kwamba kuongeza mita 15-20 mbele, maana yake ni kuanzia pale alipoacha mkoloni mwaka 1963, ujenzi utaofanywa ni kuongeza mita 15-20 ndani ya maji.

Mimi ni mtumiaji mkubwa wa gati ya Wete katika safari zangu za ndani ya jimbo la Gando. Kwa mtazamo wangu, ujenzi uliofanywa ni ujenzi wa kuinyanyua juu gati kwenye ‘foundation base’ ile ile, sasa hilo halikusaidia sana. Linalohitajika, na hicho ndio kilio cha wananchi kama ilivyoahidiwa, ni kuongeza mbele gati mita 15 – 20 ndani ya maji, ili kusogea kwenye kima kikubwa cha maji, ili vyombo vidogo vidogo viweze kufunga bila ya kutegemea kutoka na kupwa kwa maji.

BANDARI YA MKOANI

Mhe. Spika,

Bandari ya Mkoani bado haijapewa umuhimu unaostahili, uamuzi wa kuitangaza kuwa ni ‘Lango la Kimataifa’ la kuingilia, umefanywa kuwa wa kisiasa kuliko wa kimaendeleo. Ingalikua Wizara ilikuwa makini wakati bandari ya Unguja inatengenezwa ambapo wafanyabiashara walisumbuka sana na msongamano wa makontena bandari ya Dar es Salaam, na mtafaruku wa uchaguzi kwenye bandari ya Mombasa, bado serikali ilishindwa kuandaa mazingira ya kutumika bandari ya Mkoani. Pamoja na hayo, kutowaka kwa minara ya Kigomasha na Matumbini kunaleta udhia mkubwa. Hivi imeshindwa kutengenezwa au vipi? Bora zinadishwe zile taa za zamani.

SHIRIKA LA MELI

Mhe. Spika,

Wananchi sasa wamekata tamaa ya unafuu wa huduma za usafiri kutoka kwenye serikali yao. Ahadi za ununuzi wa meli nyengine, tena za kasi, zilizokuwa zikitolewa, imeonekana ni usanii tu, hakuna kilichotekelezwa. Baraza lako limekuwa likisubiri kwa hamu khatma ya Shirika la Meli, lakini mambo yanaenda mwendo wa konokono. Huu ni mwaka wa nne kamili, hadithi ya utafiti wa Shirika la Meli inaletwa hapa Barazani kila mwaka, huku meli ya M.V Mapinduzi ikiendelea kuharibika zaidi baharini. Itafika pahala isiuzike tena kwa ubovu (beyond depreciation limit). Ikiwa utafiti tu tena wa wataalamu wa ndani, ndio kwanza ripoti yake imefika wizarani sasa; baada ya miaka minne (angalia bajeti ya 2005 aya 78, bajeti ya 2006 aya 79, bajeti ya 2007 aya13, bajeti ya 2008 aya 13) je, utekelezaji wake utachukua miaka mingapi?

Mhe. Spika,

Jambo jengine ambalo lina utata ndani ya Shirika la Meli ni ukodishwaji wa meli zake. Inaonekana ama kuna mizengwe au wanasheria hawashirikishwi katika kutengeneza mikataba ya ukodishwaji wa meli zake. Mfano, MV Maendeleo imekodishwa kwa Kampuni moja ya hapa Zanzibar, ambapo ukodishwaji wenyewe unalilazimisha Shirika la Meli kugharimikia mishahara na posho ya wafanyakazi wa meli hiyo, na matengenezo ya meli hiyo inapoharibika. Je, faida itapatikana? Si gharama za uendeshaji zitapindukia faida ya ukodishwaji?

Kwa kuondoa wasiwasi, namuomba Waziri anipatie mchanganuo wa gharama za uendeshaji na matengenezo yanayogharamiwa na Shirika lake na mapato yanayolipwa na mkodishwaji kwa angalau mwaka mmoja uliopita. Na je, meli imekodishwa dola ngapi kwa mwezi? Ni dola 37,200 au 30,000 kwa mwezi?

VIWANJA VYA NDEGE

Mhe. Spika,

Katika jambo la kulionea aibu, ni hali ya Uwanja wa Ndege wa kimataifa wa Zanzibar. Jengo lake halifanani na jina lake, njia yake ya kurukia ndege ni nzuri kidogo kuliko njia ya Wete – Gando. Na tokea mwaka 2001, awamu hii ilipoingia madarakani, imekuwa na riwaya ya matengenezo ya uwanja huu. Hali inaonesha awamu ya Sita itakwisha, hali ikiwa haijatengamaa. Na hapa napo, ni eneo ambalo Build, Operate na Transfer inaweza kufanya kazi vizuri, lakini wapi?

Mara huambiwa matengenezo ya jengo la abiria, mara huambiwa panataka kujengwa kenopi, mara huambiwa panataka kujengwa uzio, mara lugha ya kununua vifaa vya kisasa vya kurushia ndege. Alimradi maneno mengi ya kubabaishababaisha bila ya vitendo vyovyote. Mambo ni mabaya zaidi uwanja wa ndege wa Pemba, ambako achilia mbali jengo, hata taa za kurukia ndege usiku au wakati wa mvua kubwa, matengenezo yake yameshindikana, mwaka wa nane sasa!!! Tukisema Wizara hii iko mahtuti katika uendeshaji wake ndiko huko.

Mhe. Spika,

Kuna nchi zilioko kwenye Muungano mfano Dubai, ambazo hazichimbi mafuta, gesi wala madini, hazina mikarafuu wala minazi, wameekeza kwenye Uwanja wa Ndege, Gati na Bandari huru, basi lakini hivi sasa ‘per capital income’ yao inakisiwa kuwa dola milioni 4.8, sisi bado tunacheza na rasilimali tulizonazo na wananchi wakiwa ombaomba.

Mhe. Spika,

Wizara ilituletea mpango mkuu wa usafiri, ambao ndani yake kuna mpango mzima wa matengenezo ya barabara, Gati na Viwanja vya Ndege chini ya utaratibu wa public private partnership. Mara nyingi ninapouliza hapa Barazani, huambiwa mpango ule uko kwa kamati  ya makatibu wakuu, mara nyengine huambiwa uko Serikalini. Ikiwa hivyo  ndio utaratibu wa kushughulika na mambo ya maana katika nchi hii, basi maendeleo bado yako mbali nasi

Mpango huu umetajwa humu Barazani tokea 2005/06, hadi leo unapigwa danadana namna hii. Sijui Wizara hii inasimamiaje kazi? Mimi nilitegemea sana mpango ule, kwani ulionesha mchupo wa makusanyo ya viwanja vya ndege mara 5 zaidi ya kile kinachokusanywa. Kwa nini unacheleweshwa? Je pana nia njema? Au mpango uliopo wa makusanyo unawaneemesha nani?

UJENZI WA BARABARA

Mhe. Spika,

Shughuli za ujenzi wa barabara ni muhimu sana katika kurahisisha huduma kwa wananchi kupuguza umaskini na kuleta maendeleo. Pahala ambapo barabara yake haifikiki kwa miongo yote, wananchi wake huwa na dhiki sana. Serikali imekuwa na mpango wa matengenezo ya barabara katika maeneo ya Visiwa vyetu, lakini hali ya matengenezo ya barabara katika kisiwa cha Pemba imekuwa kwenye makaratasi zaidi kuliko kwenye njia zenyewe, hali inayopelekea kisiwa cha Pemba barabara zake nyingi kubaki kuwa mbovu na kupitika kwa dhiki sana

Mhe. Spika,

Katika Awamu hii ya Sita iliyoko madarakani, kupitia bajeti za Wizara hii, Serikali imekua ikidhamiria matumizi ya bajeti katika Sekta ya Barabara kama ifuatavyo;

MWAKA

UNGUJA (BILIONI SH)

PEMBA(BILIONI SH)

2001/02

15

4.4

2002/03

15

7.73

2003/04

21.7

7.8

2004/05

63

4

2005/06

20

9

2006/07

36

20.5

2007/08

33

8.7

2007/08

33

8.6

Chanzo: Vitabu vya Bajeti 2001/2002 – 2008/2009

Mhe. Spika,

Pamoja na mlinganisho huo wa kinadharia, kuonesha dhamiri ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi wa CCM kibajeti, utekelezaji wake halisi unatafsirika kivitendo kwa kwenye mchanganuo unaofuata:

MAFANIKIO YAUJENGAJI WA NJIA KATIKA VISIWA VYA UNGUJA NA PEMBA BAINA YA 2001/02 HADI 2008/09

UNGUJA

NJIA

UREFU

IMEANZA (√)

HAIJAANZA (×)

IMEKWISHA(√ )

HAIJESHA (×)

1

Kidimni – Kitope

29 km

2

Tunguu – Makunduchi

43.9km

3

Mahonda/Donge/Mkokotoni

14 km

4

Amani – Mtoni

4 km

5

Mfenesini – Bumbwini

13 km

×

×

6

Jang’ombe – Mpendae

1.2 km

7

Mazizini – Fumba

13.2 km

×

8

Amani  – Dunga

13 km

×

9

Paje – Makunduchi

17 km

10

Kinyasini – Tunguu

27 km

11

Mkwajuni – Nungwi

18 km

12

Pongwe – Matemwe

20 km

13

Paje  –   Pingwe

18 km

14

Mshelishelini

Pwani Mchangani

7.5 km

×

15

Mpendae – Nyumba ya Mungu

1.2 km

×

×

16

Pale  – Kiongele

11 km

×

×

251 km

224 km (√ )

191 km (√ )

27 km (×)

60  km (×)

90% (√ )

76%

PEMBA

NJIA

UREFU

IMEANZA (√ )

HAIJAANZA (×)

IMEKWISHA(√ )

HAIJESHA   (×)

1

Mkoani  – Chake

30 km

2

Chake   –  Wesha

6 km

3

Kilindini – Micheweni

6 km

4

Chokocho – Mtuhaliwa

14 km

5

Wete  –  Chake

24 km

×

×

6

Wete  – Gando

13 km

×

×

7

Wete – Konde

15 km

×

×

8

Mtambile – Kengeja

6.6 km

×

×

9

Kenya – Chambani

3.2 km

×

×

10

Mizingani – Wambaa

10 km

×

×

11

Tundaua  – Pujini

14.9 km

×

×

12

Mtambile – Kangani

6.2 km

×

×

13

Mkoani – Makombeni

6.5 km

×

14

Mgagadu – Kiwani

6.5 km

×

×

15

Mkanyageni – Kangani

6.5 km

×

×

16

Bahanasa – Mtambwe

13 km

×

×

17

Chwale – Kojani

3 km

×

×

18

Mzambarauni – Mapofu

8 km

×

×

19

Ole  – Kengeja

35 km

×

×

20

Finya – Mzambarauni

7 km

×

×

21

Kipangani – Kangagani

3 km

×

×

242 km

62 km (√)

52 km  (√)

180 km (×)

190 km (×)

25% (√ )

21% (√ )

Chanzo: Vitabu vya Bajeti 2001/2002   – 2008/2009

Mhe. Spika,

Mie sitaki nitoe hukumu, lakini hukumu itatolewa na Ilani ya Chama cha Mapinduzi yenyewe kuhusiana na ujenzi wa barabara ukurasa wa 104 aya ya 86. Naomba nigusie kwamba ile orodha ya barabara za kisiwa dada cha Unguja; ingekuwa si kasoro ndogo ya Prismo, basi zilitakiwa tangu Januari iliyopita ziwe zimemaliza zote kilomita 156 kwa lami, achilia mbali na zile zilizoongezwa, lakini kwa kisiwa cha Pemba hakuna hata kilomita moja ya ujenzi wa lami uliotekelezwa katika utekelezaji wa Ilani hii ya 2005 – 2010, na chache sana zilitengenezwa katika awamu ya awali ya 2001 – 2005.

Mhe. Spika,

Hii ni kasoro mbovu inayohitajiwa kukemewa na kurekebishwa, ikiwa umoja wetu unahitajika hasa  kipindi hichi ambapo UINCHI wa Zanzibar unapewa mtihani na wenzetu wa Bara. Fursa ya usimamizi wa bajeti isivigawe visiwa, ni hatari kubwa.

USAJILI WA MELI

Mhe. Spika,

Katika eneo ambalo nchi yetu ya Zanzibar inaweza kujifaragua na kuipatia nchi maendeleo makubwa ya mapato ni suala la usajili wa meli za kigeni, lakini tunahitaji kujiimarisha kwa majengo, kusomesha wataalamu na kujiamini katika kufanya kazi zenyewe bila ya kumtegemea mwengine. Kazi zote zinazohusu sekta hii ziwe zinafanywa hapa hapa Zanzibar, sio kazi nyengine hapa na kazi nyengine Bara.

Na pia kuna suala zima la bendera ya nchi ya Zanzibar: kwa nini hatuchangamki ikapepea kwenye vyombo vinavyosajiliwa? Na lini usajili wa meli kubwa utaanza? Na je nini hadhi ya nchi ya Zanzibar kwenye International Maritime Organization? Na hili jina la “Tanzania Zanzibar International Register of Shipping” walilichagua wenyewe wizara au walichaguliwa?

Mhe, Spika,

Katika para, 16 ya kitabu cha hotuba ya Waziri, anataja haja ya kulipachika suala la UOKOZI katika Mambo ya Muungano. Mie nahisi tuachiwe tutute kidogo kwanza. Hamuwachi kutupelekapeleka? Hivi hatuwezi kuazisha sheria yetu ya uokozi? Hebu tuachiwe kwanza tutatue hili tulilonalo!!

OFISI KUU PEMBA

Mhe. Spika,

Kazi za Wizara Pemba zinasimamiwa na Ofisi Kuu Pemba, ambayo ina matatizo yafuatayo:

(1) Ukosefu mkubwa wa magari ya wizara hata kuazimwa magari ya taasisi nyengine

(2) Ukosefu wa zana nzito: boldozer, grader na Escaveta

(3) Tatizo sugu na la siku nyingi linalogharimu sana ni la kukosekana kwa kifaa cha ‘low loader’

(4) Kupewa mgao mdogo na pengine kuchelewa sana kwa fedha za matumizi mengine, hali inayosababisha Wizara Pemba kukosa mafuta ya kuekea kifusi kwenye barabara mbaya kama vile Gando, Mtambwe na Wambaa.

ZANTEL

Mhe Spika,

Kampuni ya Zantel imekuwa ni kampuni yetu na inajitahidi, lakini kuna mapungufu yanayohitaji kurekebishwa.

Uondoaji wa ofa umewavunja moyo sana wanyonge. Zantel ilishakuwa kimbilio la wanyonge, lakini sasa haishikiki kwa ughali, na watu wengi sasa wamegeuka wapiga missed calls wakubwa. Ninaiomba ufanywe utaratibu wa kurudishwa ile ofa japo kwa maeneo ya visiwa vyetu au ukipiga katika maeneo ya Unguja/Pemba. Ukitoka nje ya hapa, hapo shauri nyengine.

Mtandao haujaenea vizuri katika maeneo ya mashamba hasa Pemba, licha ya ahadi nyingi ya kujenga minara.

Hadhi ya Makao Makuu inaonekana ni nadharia zaidi kuliko vitendo.

Mhe. Spika,

Pamoja na hayo naipongeza Kampuni ya Zantel kwa:

  • Kuwa ni mlipaji mzuri wa kodi kwa Zanzibar
  • Kuanzisha huduma ya upatikanaji wa huduma ya simu ya Zantel popote ulimwenguni bila ya kufuata utaratibu wa Roamming. Hii ni hatua nzuri sana.

TTCL, POSTA NA TCAA

Mhe Spika,

Niruhusu nitoe pongezi kwa mashirika ya TTCL, Posta na TCAA, kwa huduma zao hapa Zanzibar. Pamoja na changamoto wanazozipata, bado wanaendelea kutoa huduma kwa wananchi na bila shaka kulipa kodi kwa hazina ya SMZ, katika utekelezaji wa shughuli zao. Namuomba Mhe. Waziri anipatie mchanganuo wa mchango wao wa kodi kwa Zanzibar zilizopatikana kutoka kwa kila shirika kati ya hayo matatu kwa mwaka unaomalizika.

BARABARA YA WETE – GANDO

Mhe. Spika,

Hii ni barabara mbovu sana miongoni mwa barabara zilizopo Zanzibar. Urefu wake ni kilomita 13 tu, wananchi wake wana dhiki kubwa ya usafiri tokea enzi zile. Pamoja na ahadi za siku nyingi na ahadi za awamu zote – kuanzia awamu ya kwanza hadi hii awamu ya sita – bado barabara ya Gando haijaanza kutengenezwa. Pamefanywa uchambuzi sanifu mpaka uchambuzi yakinifu, na kila siku habari ile na hii.

Mhe. Spika,

Kuna wakati, karibu miezi 30 imepita, tuligaiwa Press Releases kwamba mkopo tayari, barabara itajengwa. Hadi leo bado.

Mhe. Spika,

Nimepata wasiwasi kwamba Kampuni ya BLACK AND VEATCH ya Afrika Kusini ndio iliyojigeuza jina na kujiita John Barrow Ltd ya Afrika Kusini. Kampuni iliyokuwa ikisimamia ujenzi wa barabara ya Fumba, Dunga na Bumbwini kama ‘consultant’, ndiyo kampuni inayofanyia usimamizi mchoro na ‘design’  barabara ya Wete, Gando na Konde, kwa jina la John Barrow Ltd.

  • Kwanza kwa habari niliyonayo, hakuna usajili wa kufanya kazi zake Zanzibar. Sasa ilikuwaje akapewa kazi?
  • Pili, keshafanya udhaifu katika barabara za Unguja, iweje anapewa tena kazi barabara za Pemba?

Mhe. Spika,

Kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Gando, nimevunjika moyo sana na hatua hii ya wizara na kwa kweli sifichi nina wasiwasi kwamba panaweza kuwa pana mchezo mchafu, na nataka Mhe. Waziri anitoe wasi wasi nilionao kuhusiana kufanya na kazi Zanzibar kwa Kampuni hii ya BLACK AND VEATCH, je taratibu za tenda zinafuatwa?

Mhe. Spika,

Ikiwa hali ya ujenzi wa barabara ya Gando utaendelea kuchelewa, kama dalili zinavyoonesha, ninaomba ili wananchi waondokane na usumbufu wa usafiri ile barabra iwekwe kifusi hasa sehemu za milima na kwenye michanga. Na kwa sababu mandhari ya Gando ni ya vilima, kifusi kitachoekwa kishindiliwe ili kukinusuru kisikokolewe na mvua kwa urahisi.

BARABARA YA BAHANASA-MTAMBWE

Mhe. Spika,

Eneo la Mtambwe ni eneo lenye matatizo makubwa ya usafiri; usafiri wake ama ni wa kutumia madau au kwa kupitia kwenye barabara mbaya sana. Ninaishukuru serikali kwa kuiombea ufadhili kupitia MCC, lakini matengenezo yake lazima yafike kwenye maeneo wanayoishi watu wengi kama vile Daya – Nyali, Daya Kinazini, Kivumoni na barabara ya Kele – Bwagamoyo.

Mhe. Spika,

Nimetumwa pia na mwakilishi wa Jimbo la Tumbe, Mhe. Ali Mohd nimuulize Waziri, anaifahamu njia inayotoka Finya kupitia skuli ya Shumba Vyamboni hadi Sizini yenye urefu wa kama kilomita 7? Anafahamu Waziri kwamba ile barabara ni mbaya sana, na inatumiwa na wananchi wa shehia kama 4 hivi, na imesahauliwa sana? Je, ana mpango wa kuihami kwa greda na kifusi halafu kuombewa ufadhili?

Mhe. Spika,

Naomba nimshukuru sana kiongozi wa Kambi ya Upinzani  kwa maelekezo aliyonipa katika kumsaidia shughuli zake kuhusiana na wizara hii, na pia naomba niusifu sana msaada wa Mhe. Salum Abdallah, Mwakilishi wa Jimbo la Mtambwe, katika kutayarisha maoni haya ya Kambi ya Upinzani.

Mhe. Spika,

Kama nilivyoanza  kukushukuru kwa  kwa kunipa nafasi hii, nakushukuru  tena kwa kunivumilia hadi mwisho kwa maelezo yangu na nawashukuru wajumbe wa Baraza lako tukufu kwa kunisikiliza.

Ahsante.

Said Ali Mbarouk

Mwakilishi Jimbo la Gando

Msemaji Kambi ya Upinzani

Wizara ya Mawasiliano/Uchukuzi

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s