Serikali yaupuuza mkarafuu

Kwa takribani karne mbili mutawaliya, historia ya imeonesha kuwa Zanzibar imeendelea kutegemea karafuu kama zao lake la kibiashara. Lakini ni bahati mbaya kwamba, licha ya kuwa tegemeo la kiuchumi kwa visiwa hivi, Serikali ya Zanzibar imeshindwa kuchukuwa hatua madhubuti na za makusudi kuliimarisha zao hili, badala yake imekuwa iking’ang’ania udhibiti wake tu. “Mkarafuu unakabiliwa na hatari ya kupotea kutokana na matatizo yanayoukabili ikiwa hatua za haraka za kuhami hazikuchukuliwa. Lakini kwa bahati mbaya Serikali bado inafanya utani juu ya kuliokoa zao la karafuu. Hivyo ni kweli kama serikali imekusudia kuuhami mkarafuu ingetenga shilingi milioni 40 kwa mradi wa kuimarisha mikarafuu? Huu ni utani na serikali haistahiki kufanya utani na maendeleo ya nchi.” Anasema Muhiddin Mohammed, mwakilishi wa CUF kutoka jimbo la Mtambile.

Karafuu za Zanzibar, zao kuu la biashara ambalo licha ya umuhimu wake, Serikali imepuuza ukuzwaji wake na inang'ang'ania udhibiti tu. Sera ya CUF kuelekea zao hili ni kuondoa mkono wa serikali na kuliingiza katika biashara huria

Karafuu za Zanzibar, zao kuu la biashara ambalo licha ya umuhimu wake, Serikali imepuuza ukuzwaji wake na inang’ang’ania udhibiti tu. Sera ya CUF kuelekea zao hili ni kuondoa mkono wa serikali na kuliingiza katika biashara huria

Mhe, Spika,

Kwanza kabisa nachukua nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu Muumba mbingu na Ardhi na vyote viliomo ndani yake, kwa kutuweka hai na kutupa uzima na kuweza kutukutanisha tena baada ya kipindi cha mwaka mzima. Pili ninakushukuru wewe, Mhe. Spika, kwa kunipa nafasi hii adhimu ya kusimama mbele ya Baraza lako Tukufu kutoa maelezo machache yahusuyo Bajeti ya Wizara yaUtalii, Biashara na Uwekezaji.

Tatu ninawashukuru sana wapiga kura wangu wote wa Jimbo la Mtambile kwa kushirikiana  nami katika kuendeleza mapambano dhidi ya hali ngumu ya maisha na mfumko wa bei unaendelea kutukabili bila ya kuwa  na muelekeo wa ufumbuzi, kwani tumekosa msumko katika kapambana nao.

Mhe.Spika,

Ilituweze kupambana na mfumko wa bei ni budi kongeza uzalishaji wa chakula katika kilio. Ili uzalishaji katika kilimo uongezeke hatuna budi sekta hiyo kupewa msukumo na kipaumbele lakini Mhe. Spika, ni bahati mbaya sana kwamba SMZ haioni umuhimu wa sekta ya kilimo na badala yake inaweka msukumo kwa majeshi ya SMZ. Lakini sishangai kwani hii ina maana yake ambapo yatajitokeza baada ya miaka miwili na nusu ijayo.

Mhe. Spika,

Biashara ya namna hii haikidhi ile haja ya kukuza  uchumi na kupunguza umaskini. Kwa hivyo kuna haja ya kukaa chini na kutafakari nini kifanyike kuondokana na hali hiyo. Mimi nadhani ni muhimu kuongeza uzalishaji wa bidhaa zenye bora na kutosheleza ndani na  kusafirisha nje. Ni vyema wakati zinapojitokeza fursa za uwekezaji kwa wawekezaji wa nje na wa ndani ya nchi tuwache ubinafsi na tuwape wawekezaji nafasi ya kuekeza kwa faida ya wote.

Mhe. Spika,

Miongoni mwa taasisi muhimu kwa Wizara ni Idara ya Mipango na Sera.Idara hii ndio inayosimamia na kuongoza shughuli zote za Wizara. Idara inasimamia na kuratibu rasilimali watu na rasilimali nyengine za Wizara. Kutetereka kwa Idara hii ni kutetereka ni kutetereka kwa Wizara yote. Ili Wizara iweze kuendeleza shughuli zake vyema ni umuhimu Idara kuwa na watendaji wenye ujuzi wa uendeshaji na mipago ikisimamiwa na Katibu Mkuu. Kufanikiwa kwa Idara kunategemea sana uwezeshaji  kwa kupatiwa fedha kwa wakati na kwa kima kilichoombwa na kuidhinishwa.

Mhe, Spika,

Pamoja na kwa Serikali kupitia Wizara haiendeshi  biashara moja kwa moja, lakini ina wajibu mkubwa wa kuweka mazingira bora yatakayo wawezesha wadau wa biahara kufanya na kuendesha biashara zao katika mazingira mwanana kwa faida yao na kwa manufaa ya wananchi kama hivyo ndivyo basi ni vyema serikali ingefikiria kutekeleza yafuatayo:

  • Kupunguza viwango vikubwa na vituo vingi vya kodi. Hili ni suala muhimu sana katika kuamsha ari ya biashara ya usafirishaji na uagiziaji. Lakini kwa muono wangu ni jambo lisilowezekana kwa Zanzibar kwa vile kodi limefanywa suala la Muungano  linalosimamiwa na TRA.
  • Kuwa na viwango vya udhibiti wa ubora wa bidhaa. Mhe, Spika, hatua hii itawezekana ikiwa tu Zanzibar itakuwa na chombo chake cha kuendesha shughuli hiyo. Kwa hivyo imefika wakati sasa Zanzibar kuanzisha chombo hicho badala ya kutegemea TBS.
  • Kuanzisha mashirika ya kibiashara ya kitaifa ya kiserikali au ya kibinafsi.
  • Maeneo huru ya uzalishaji na Bandari huru yaendelezewe kwa kuekewa miundo mbinu muwafaka ili yaweze kutumika na kuleta tija. Maeneo hayo yafanyiwe tahafifu na kufanyiwa upendeleo wa kodi kwa vitengo vya uzalishaji.
  • Itayarishwe mipango ya kuinua usafirishaji nje kwa kutoa huduma ambazo zitawawezesha wasafirishaji nje katika masoko ya kimataifa ambayo mazingira yake  ya ushindani mkubwa.
  • Kuongeza wigo wa mazao ya kusafirisha nje, vile mazao ya baharini, viungo, matunda na mazao kadhaa ya kilimo.
  • Kuweko na urahisi wa upatikanaji wa habari za kibiashara.
  • Serikali ijaribu kila iwezavyo kupunguza gharama na kurahisisha taratibu za kibiashara.
  • Serikali ivutie na kushawishi kuanzishwa taasisi za kifedha kufunguliwe na kutoa mikopo nafuu kwa wafanyabiashara wa usafirishaji nje na wazalishaji katika kilimo na Viwanda.
  • Zanzibar kama sehemu ya dunia isibaki nyuma katika kuanzisha ushirikiano wa kikanda na wa kimataifa katika kukuza biashara yake na kuingia katika masoko na mikataba mbali mbali ya kibiashara.

Mhe. Spika,

Waziri amelieleza Baraza lako tukufu kwamba kwa mashirikiano ya SMZ na SMT, Idara imewezesha kuendelea na zoezi la utayarishaji wa mikakati ya usafirishaji bidhaa, Jee zoezi hili limefikia wapi na limeleta tija gani kwa wasafirishaji na usafirishaji nje kwa Zanzibar. Pia tumeelezwa kwamba, Idara kwa kushirikiana na UNIDO imefanikiwa kuanzisha mradi wa kuziongozea thamani bidhaa zinazozalishwa Zanzibar kwa lengo la kukuza usafirishaji. Je, ni bidhaa za aina gani zinazozalishwa Zanzibar kwa lengo la kukuza usafirishaji? Je, ni bidhaa za aina gani zilizoongezewa thamani na usafirishaji umekuwa kwa kiasi gani na nini muelekeo wa baadae? Kwani mwanzoni mwa hotuba yake Mhe. Waziri kalieleza Baraza lako tukufu kwamba usafirishaji nje na Tanzania Bara umepungua.

Mhe.Spika,

Miongoni mwa shughuli nyengine muhimu za Idara hii ni kuangalia mwenendo wa biashara na kumlinda mtumiaji. Kwa maoni yangu kazi hii ya kumlinda mtumiaji haijapata ufanisi unaohitajika kwani bidhaa zilizo chini ya viwango zinaonekana katika soko. Kwa hivyo  kuna haja kubwa ya kuimarisha kitengo ili kifanye kazi kwa ufanisi zaidi.

Mhe. Spika,

Takriban mara zote ninapochangia hotuba ya Wizara hii huwa ninaishauri ifikirie kuanzisha maeneo ya maonyesho ya biashara. Lakini bado ninaona Wizara haijalipa umuhimu eneo hili, kwani  sikuona popote wazo hilo lilipo angalau kutajwa. Mimi ninadhani wataalamu wa biashara waliopo Wizarani wanaelewa umuhimu wa shughuli hii na pia ni imani yangu kwamba wanaishauri vizuri Wizara kuhusiana na suala hilo. Nadhani imefika wakati wa kutotegemea maonesho ya saba saba kwani huwa yanawatia hasara na kuwapa usumbufu mkubwa hao wachache wanaoweza kushiriki na Wizara imeiona faida ya kushiriki kwao.

Mhe, Spika,

Ikiwa kweli, tunakusudia kuongeza tija, kukuza pato la taifa na kupunguza umaskini basi ni budi kuimarisha na kusimamia vyema sekta hii ya viwanda. Mhe. Spika, ninasema hivyo sababu tuna nia ya kuongeza usafirishaji nje, ili tuweze kuongeza usafirishaji ni budi kuwa na cha kusafirisha, tuzalishe bidhaa zenye  ubora wa kimataifa na kwa wingi sasa basi, viwanda ni sehemu moja ya uzalishaji mbali ya ile ya Kilimo.

Mhe, Spika,

Uanzishwaji viwanda  vya  aina yoyote kunahitaji kupatikana kwa mali ghafi. Mali ghafi hii inaweza, kupatikana hapa hapa nchini au kuagizwa kutoka nje kutegemea na aina gani ya kiwanda  kitachoanzishwa. Uagizaji wa mali ghafi ambazo zingeweza kutumika katika viwanda vilivyoanzishwa katika maeneo Huru  imekabiliwa na vikwazo na matatizo ya  utaratibu  yaliyosababishwa na Mamlaka ya Forodha ya Tanzania ya kuingiza  mali ghafi  kulingana na muongozo wa sera  za Zanzibar. Tatizo hili pia linazikabili bidhaa zilizozalishwa katika  viwanda kusafirishwa nje. Ninayo taarifa kwamba kuna kiwanda kimesimamisha uzalishaji na kufunga virago Zanzibar na kuhamia Tanzania Bara kutokana na vikwazo walivyovipata kwa usafirishaji wa bidhaa zao. Je, Mhe. Spika, Mhe. Waziri analieleza nini Baraza hili juu ya utatuzi wa masuala  kama haya ili kupata ufumbuzi wa kudumu kwa nia ya kuimarisha viwanda kwa lengo la kuongeza uzalishaji  na kuwavutia wawekezaji wengine.

Mhe. Spika,

Wizara ya Utalii, Biashara na uwekezaji ni miongoni mwa Wizara zenye sera nyingi za utekelezaji wa shughuli mbali mbali, kama vile sera ya utalii, sera ya Biashara sera ya viwanda na Biashara ndogo ndogo na kati. Kwa hiyo Wizara inakabiliwa na changamoto kubwa juu ya ufanisi  wa sera hizo sera moja kuelezwa kwa sentensi moja katika hotuba hii, nadhani haikidhi haja. Mhe. Waziri ingefaa akaeleza kwa kina juu ya ufanikishaji wa sera hizo na Baraza hili likaweza kunisaidia pale kwenye matatizo.

Mhe. Spika,

Sekta ya Utalii katika utekelezaji wa mpango mkuu wa kupunguza umaskini imeelezwa kuwa ni sekta kiongozi, mbali ya hilo faida na tija inayopatikana katika utalii imeonekana, lakini ni bahati mbaya sana kwamba serikali haijashughulikia ipasavyo sekta hiyo. Imeelezwa mara nyingi katika Baraza hili kwamba wawekezaji wa sekta ya utalii wanakabiliwa na matatizo mengi hata wengine wanafikiria kufunga miradi yao.

Mhe. Spika,

Hata kwenye ripoti ya kamati ya PAC, ya kipindi kinachomalizika hilo limeelezwa kwa ufasaha kabisa miongoni mwa matatizo makubwa ni tatizo la upatikanaji wa maji safi, umeme wa uhakika n.k, la kusikitisha zaidi ni kwamba sikuona katika bajeti ya Wizara ya Maji, Nishati na Wizara yenyewe inayosimamia utalii maelezo juu ya namna gani tatizo la maji litashughulikiwa japo kwa awamu kwa wawekezaji wa mahoteli. Hii inaonesha  jinsi gani Serikali inavyopuuza na kubeza sekta kiongozi ya utalii. Ni matarajio yangu kuona vipi matatizo hayo yanashughulikiwa kwa kukuza utalii.

Mhe. Spika,

Mbali na matatizo ya maji na umeme, pia kuna tatizo kubwa la maeneo ya kutupia taka  zinazotoka mahotilini. Tatizo hili nalo linazipatisha hasara kubwa za uendeshaji pamoja na uchafuzi wa mazingira. Ni vizuri wizara ya Utalii ikishirikiana na Wizara ya Maji na Ardhi  pamoja na Wizara inayoshughulikia  mazingira kukaa pamoja kutafakari  njia ya kutafuta ufumbuzi wa tatizo hili. Mhe. Waziri Kiongozi wakati wa kufanya majumuisho ya  yake alisema kwamba amewapa muda  mpaka Septemba 2008, wamiliki wa mahoteli wawe wameshaeka majiko ya kuchomea taka mahotelini mwao, Jee wale ambao watashindwa ifikapo muda huo hatua gani  zitachukuliwa dhidi yao.

Mhe. Spika,

Kwa mujibu wa maelezo ya Mhe. Waziri idadi ya watalii walioingia Zanzibar imeongezeka kwa asilimia 9.5, ukilinganisha na mwaka uliopita Jee, ni kiasi gani cha mapato kimeongezeka, au kimebaki pale pale au kuongezeka kidogo tu. Mhe. Spika, nimesema  hayo kwa sababu bado kunaonekana hakuna umakini wa ukusanyaji wa mapato yanayotokana na Utalii.

Mhe. Spika,

Kamisheni ya Utalii ambacho ndicho  chombo kikuu kinachosimamia, kuendeleza na kukuza Utalii bado kinakabiliwa na matatizo mengi. Miongoni mwa matatizo hayo ni – uhaba na uduni wa vitendea kazi, upungufu wa wataalam wa mafunzo maalum na katika viwango vya juu, hasa  masoko, mipango na uendeshaji, ukosefu wa majengo ya afisi Unguja na Pemba, migogoro  ndani ya sekta ya Utalii na Zanzibar kutokuwa na Shirika lake la Ndege.

Mhe. Spika,

Ninayo taarifa ambayo bado sijaithibitisha kwani nimeipata punde tu, kwamba Pemba kuna muwekezaji ambae aliomba kibali cha kujenga mkahawa (Restaurant) katika maeneo ya Vitongoji. Mwekezaji huyo amepewa eneo hilo lakini alikaa kwa muda mrefu hajalitumia, baada ya muda amefanya ujanja na kuliuza eneo hilo kwa muekezaji mwengine kwa thamani duni kwa makubaliano kitendo ambacho kinaikosesha Kamisheni na ZRB mapato yanayostahiki. Muekezaji mpya ameanza ujenzi ambao si wa mkahawa lakini ni wa hoteli. Jee Mhe. Spika, suala hili Mhe. Waziri analielewa na Wizara imechukua hatua gani dhidi ya mjanja mkorofi huyo.

Mhe. Spika,

Mamlaka ya Ukuzaji Vitega Uchumi ni chombo muhimu katikakuendeleza uwekezaji wa nyanja mbali mbali nchini, ni matumaini yangu kwamba mamlaka ina wataalamu wa aina mbali mbali wazalendo kwa hivyo kuna haja ya kupewa uwezo na imani ya kutekeleza shughuli zake.

Mhe. Spika,

Chuo cha Maendeleo ya Utalii ni taasisi iliozaliwa upya baada ya Baraza lako tukufu kupitisha Sheria ya uanzishwaji wa chuo hicho. Ni muhimu sana iyonekane tofauti kubwa kati ya chuo cha sasa na kile kilicho kuwepo kabla ya kupitishwa sheria. Utaratibu wa vifaa duni vya kufundishia na wanafunzi wengine kusubiri  chini ya miarubaini uepukwe na kuwa na vifaa bora, madarasa ya kutosha na wanafunzi wenye sifa na uwezo bora wa kufundisha.

Mhe. Spika,

Kabla ya Mapinduzi ya mwaka 1964  zao la karafuu lilikuwa huru, na wakulima wa karafuu waliweza kuuza karafuu zao  wapendapo. Baada ya Mapinduzi, Serikali  ilibadilisha utaratibu wa uuzaji wa karafuu kwa serikali  kuanzisha Shirika la Taifa la Biashara  –  ZSTC ambalo jukumu lake kubwa ni kununua mazao ya kilimo pamoja  na usafirishaji nje  wa mazao hayo na hasa karafuu.

Mhe.Spika,

Serikali ilifanya hivyo kwa kuwaonea huruma  wakulima wa karafuu wasinyonywe na mabepari wachache, pia kwa kuwaonea huruma wavunaji (wa chumaji) wa karafuu, serikali hiyo hiyo ya Mapinduzi ya wakati huo iliweka utaratibu wa kuwalipa fidia wavunaji wa karafuu ambao kwa bahati mbaya walipata ajali ya kuanguka mikarafuu.

Mhe. Spika,

Baada ya miaka mingi kupita hali hii imebadilika sana shirika hivi sasa limekuwa ndio mnyonyaji mkubwa wa wakulima wa zao la karafuu kutokana na hali  inavyojionesha katika mwaka 2007 hadi kufikia Machi 2008, Shirika limenunua tani 1,349.192 za  karafuu zenye thamani ya Shs. 3.86 bilioni. Kati ya hizo tani 1,271 zenye thamani ya Shs. 5.505 bilioni zimeuzwa. Mhe. Spika, utaona kwamba idadi ya karafuu ilionunuliwa ni kubwa lakini thamani yake ni ndogo. Wakati idadi ya karafuu iliouzwa ni ndogo lakini thamani yake ni kubwa. Kama inavyoonekana hapa chini:-.

MWAKA

MANUNUZI

THAMANI

MAUZO

THAMANI

2005/2006

3,343.30

7.459

3,186.31

10.444

2006/2007

3050.8

8.06

2877

11.68

2007/2008

1,349,192

3.86

1271

5.505

2005/2006

2006/2007

2007/2008

3,343.30

3050.8

1,349,192

3,186.31

2877

1271

156.99

173.8

78.192

2005/2006

2006/2007

2007/2008

10.444

11.68

5.505

7.459

8.06

3.86

2.985

3.62

1.645

Ni kweli kwamba kuna gharama za uendeshaji lakini faida inayolimbikizwa na ZSTC ni kubwa na imeweza kuwa na vitega uchumi vya thamani kubwa. Sasa tumuangaliemkulima wa karafuu siku hadi siku anavyokuwa duni na kuwa masikini baya zaidi Mhe. Spika, ni wa shirika kuondoa fidia  kwa wanaoanguka mikarafuu wakati wa uvunaji wa karafuu.

Mhe Spika,

Ni kweli kwamba bei ya karafuu katika soko la dunia imeshuka sana, lakini bado faida inayopatikana kutokana na uuzaji wa karafuu ni kubwa ndio maana serikali imepatwa na kigugumizi juu ya ubinafsishaji wa biashara ya zao la karafuu na iko tayari kuua na inaua mtu akifanya mzaha na hata kilo 5 za karafuu.

Mhe. Spika

Waziri amelisifu Tawi la ZSTC la Dar es Salaam kwamba limefanya biashara nzuri katika kipindi hichi na kuvuka lengo kwa asilimia 25 ya makadirio. Lakini Mhe Waziri  anajua kuwa tawi linafanya kazi katika mazingira magumu hasa ya sehemu ya kuendeshea biashara, yaani makaazi. Kama anajua hali hiyo ipo, jee Wizara yake inafanya nini kulisaidia Tawi kuondokana na tatizo hilo. Ninaomba maelezo yake na hatua zenye muelekeo.

Mhe. Spika,

Mkarafuu unakabiliwa na hatari ya kupotea kutokana na matatizo yanayoukabili ikiwa hatua za haraka za kuhami hazikuchukuliwa. Lakini kwa bahati mbaya Serikali bado inafanya utani juu ya kuliokoa zao la karafuu. Hivyo ni kweli kama serikali imekusudia kuuhami mkarafuu ingetenga shs 40 milioni kwa mradi wa kuimarisha mikarafuu, huu ni utani na serikali haistahiki kufanya utani na maendeleo ya Nchi.

Mhe. Spika,

Shirika la Utalii, ni shirika lilioko chini ya sekta kiongozi ya Utalii kwa mnasaba huo basi, lingetarajia kuwa shirika lenye ufanisi mkubwa katika shughuli zake. Lakini mambo siyo yalivyo kutokana na hali hiyo, basi shirika linahitaji kutazamwa upya na  kupewa nyenzo za kuweza kujipanga upya na kuendeleza shughuli za utalii likiwa na nguvu tosha ya kupambana na sekta binafsi katika kuwahudumia watalii.

Mhe. Spika,

Ni muda mrefu sasa Serikali ina nia ya kuifanya Hoteli kuwa shirika linalojitegemea au kubinafsisha lakini bado imepatwa na kigugumizi juu ya utekelezaji wa moja kati ya masuala mawili hayo, sasa sielewi kigugumizi hicho ni kwa faida ya nani. Ni kweli kwamba ili kufikia maamuzi kunahitaji umakini wa kutosha, lakini pia tungezingatia na wakati.

Mhe. Spika,

Kama hoteli ikiendelea katika hali kama ilivyo sasa, sijui nini itakuwa hatima ya wafanyakazi ambao wanastahiki pongezi kwa juhudi za hoteli kujiendeleza kutokana na ufinyu wa mtaji? Kwa hiyo ninatoa mwito kwa wadaiwa wote wa hoteli walipe madeni yao haraka.

Mhe. Spika, naomba nimuulize Mhe. Waziri nini hatima ya ukumbi wa Komba Disco?

Mhe. Spika,

Zanzibar ni sehemu ya dunia  kwa hivyo haiwezi kujitenga kama inataka kupiga hatua mbele katika shughuli zake za biashara na nyenginezo sasa basi, ni muhimu sana Zanzibar kujiunga na jumuiya mbali mbali  za kikanda na za kimataifa, ushirikishwaji katika jumuiya hizo ingefaa na kupendekeza Zanzibar ikajiunga moja kwa moja kuliko kupitia juu ya mgongo wa kaka. Nadhani tukifanya hivi faida itakayopatikana itakuwa kubwa  na manufaa zaidi kuliko njia ya kupitia mgongo wa kaka.

Mhe. Spika,

Mhe, Waziri katika hotuba yake kwenye kifungu 13.2 ameeleza kwamba, baada ya kuanzishwa kwa umoja wa Forodha wananchi wa nchi wanachama watakuwa na fursa ya kutembea na kufanyakazi, uhuru wa kuanisha kampuni na kusafirisha bidhaa pamoja na kuweka mitaji katika nchi wanachama.

Mhe. Spika,

Zao la karafuu kwa Zanzibar bado linadhibitiwa na serikali, bado kubinafsishwa. Je, ikifika wakati huo wafanyabiashara wa ndani na wa kutoka nchi wanachama, wataruhusiwa kununua karafuu kwa wakulima na kusafirisha? Pia wafanyabiashara wa Zanzibar wanaagiza bidhaa mbali mbali nje na kuziuza ndani na kuzisafirisha tena – re-export. Jee, bidhaa hizo zikisafirishwa tena katika soko huria la Afrika Mashariki na SADC zitakuwa na msamaha wa kodi. Ikiwa zitatozwa kodi, Zanzibar itanufaika vipi?

HITIMISHO

Mhe. Spika,

Hali ya uchumi wa dunia imebadilika na inaendelea kubadilika kutokana na kupanda sana kwa bei za mafuta na kupungua mazao ya chakula. Mambo yote mawili hayo yamesababisha upandaji mkubwa wa bei za bidhaa mbali mbali ikiwemo ile ya chakula, kwa vile Zanzibar ni muagizaji mkubwa wa chakula, mafuta na bidhaa nyengine kama vile za matumizi ya nyumbani na ujenzi, itakuwa imeathirika sana. Kutokana na hali hiyo wananchi pamoja na Serikali   wanalalamikia hali hiyo, anaelalamikiwa hajulikani.

Mhe. Spika,

Mwanadamu kulalamika anapopata matatizo ni maumbile yake, pamoja na kwamba malalamiko hayamsaidii kitu. Hali hiyo ya mwanandamu kulalamika imeelezwa katika kitabu kitukufu kwa kusema:

19) Hakika ya mwanandamu ameumbwa hali ya kuwa na papatiko. (20) Inapomgusa shari huwa mwenye fazaa. (21)  Na inapomgusa kheri huwa anajizuilia.

Kwa hivyo Mhe. Spika, tumelalamika vya kutosha. Sasa imefika wakati kwa Serikali pamoja na wananchi kuacha kulalamika na tufanye kazi. Ni jukumu la Serikali kwa upande wake kuandaa mazingira mazuri yatakayowawezesha wananchi kuzalisha zaidi katika sekta ya kilimo kwa mazao ya chakula hasa mpunga na kutanua wigo wa mazao ya biashara kama vile viungo mbali mbali kwani vinastawi vyema nchini na pia vina bei maridhawa katika soko la dunia. Halikadhalika, kuandaa mazingira mazuri na endelevu katika viwanda ili nako uzalishaji wa bidhaa zenye ubora wa kitaifa na kimataifa uongezeke kwa lengo la kusafirisha. Na kwa upande wa wananchi nao baada ya serikali yao kuandaa ubabaishaji kwani vyote hivyo havitasaidia ili tujipinde tuzalishe zaidi na tuuze starehe zaitafuata baadae. Tusipotanabahi hasara kubwa inatukabili na haiko mbali pale litakapoanza soko huria la pamoja la Afrika Mashariki.

Mhe. Spika,

Changamoto iko kwetu sote tuzinduke, twende pamoja ndio tutafanikiwa, pamoja na kuzingatia ugawaji wenye uwiano mzuri wa rasilimali za nchi kwa pande zote mbili Unguja na Pemba.

Mhe. Spika,

Ninashuru kwa mara nyengine kwa kunivumilia kwa muda wako adhimu, ambao ninajua ndio tatizo lako kubwa kuliko fedha. Fedha kwa vile uko karibu sana Dk. Mwinyi Haji Makame si tatizo kwako. Pia nawashukuru Waheshimiwa, Wajumbe wako kwa kunisikiliza. Naomba tuichangie hotuba ya Mhe. Waziri kwa maendeleo ya wote.

Ahsanteni

Mhe. Spika, naomba kuwasilisha.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s