Mbona SMZ inawaangalia hadi wagonjwa kwa jicho la U-unguja na Upemba?

Suala la mpasuko wa kisiasa Zanzibar linachangiwa kwa kiasi kikubwa na tabia ya serikali iliyopo madarakani, ambayo kwa makusudi hukitenga kisiwa cha Pemba kwa kila kitu kinachomaanisha maisha ya watu: elimu, miundombinu, uongozi na sasa hata afya. Katika hotuba hii ya Waziri Kivuli wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Mhe. Rashid Seif Suleiman (Mwakilishi wa CUF, Jimbo la Ziwani), aliyoitoa kuchangia makadirio na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2008/2009 katika Baraza la Wawakilishi, Zanzibar, CUF inahoji na inataka maelezo ya kwa nini SMZ inafikia kiwango cha kuwabagua hata wagonjwa waliolazwa hospitalini kwa misingi ya U-unguja na Upemba, ambapo ingawa wagonjwa waliolazwa Pemba kwa mwaka 2008 ni asilimia 83 ya wagonjwa wote wa Zanzibar, walitengewa shilingi milioni 84 tu huku asilimia 17, ambao ni wagonjwa waliolazwa Unguja, wakipangiwa shilingi milioni 196!

Mhe. Rashid Seif Suleiman (CUF - Ziwani)

Mhe. Rashid Seif Suleiman (CUF – Ziwani)

Mhe. Spika,

Kwanza sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu (ALLAH S.W) kwa kutuweka hai na kutupa afya tukaweza kusimama katika Baraza lako tukufu na kuwasilisha maoni ya Kambi ya Upinzani juu ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Afya 2008/2009.Pili napenda nitoe shukrani kwako kwa kuniruhusu kutoa maoni hayo.

Mhe. Spika,

Ili nisiwe mpungufu wa fadhila, naomba nichukue fursa hii kuendelea kuwashukuru wapiga kura na wananchi wote wa Jimbo la Ziwani kwa kuendelea kuniunga mkono bila kusahau viongozi wote wa Chama changu cha CUF, nawaomba tuwe makini katika kutetea maslahi ya NCHI YETU bila ya kutetereka.

Mhe. Spika,

Mbali na matumizi ya kawaida ya mishahara na matumizi ya kila siku katika WIzara na taasisi zake, bajeti inategemewa itowe ufumbuzi juu ya kutoa mahitaji muhimu ya Wizara na taasisi pia kutoa ufumbuzi juu ya matatizo mbali mbali yaliyokabili Wizara.  Bajeti hii huchukua sura ya Ujenzi, Ununuzi, kutoa taaluma kwa wafanyakazi mbali mbali na matengenezo mengine mbali mbali.  Hii ndiyo inayoitwa Bajeti ya Maendeleo.

Mhe. Spika,

Hivyo napenda kuendelea kutetea msimamo nilioueleza katika kujadili bajeti ya mwaka 2007/2008 kuwa SMZ na Wizara zingechukuwa msimamo ule wa bara la  Africa  Abuja declaration 2002 ya kutumia 15% ya Bajeti ya Serikali katika Wizara hii ya Afya na Ustawi wa Jamii.

Mhe. Spika,

Wakati Bajeti yetu ya Afya ni 3.5% ya Bajeti ya Serikali, Tanzania Bara ni 11% Kenya ni 12%,Uganda ni 9.5% ya Bajeti ya serikali. Mauritius kisiwa kama sisi wanatumia 8.55 % ya ba jeti ya serikali katika hudma za Afya.

Nidhahiri kuwa hali ya Bajeti ni finyu sana hasa ukitilia maanani kuwa pato la nchi  pato la nchi haliridhishi hata kidogo.  Bajeti ya maendeleo ambayo  ni 1.5billioni. ambayo ni 14.1% ya Bajeti ya Wizara, hali inayokatisha tamaa ya kupata maendeleo halisi katika nyanja za matibabu, kinga na ustawi wa jamii.

Mhe. Spika,

Unapoambiwa kuwa Bajeti hii kwanza ni tegemezi na ni asilimia 14% tu ya Bajeti hii ya Wizara ya Afya, ndiyo ya maendeleo basi ni dhahiri hutegemei kupatikana hatua muafaka ya kimaendeleo. Na kama hakuna hatua ya maendeleo maana yake sekta hii itadorora na kurudia kule kule katika visingizio vingi vinavyofuatiwa na hudma dhaifu au kukosekana kabisa kwa hudma nyingi

Mhe. Spika,

Wakati Zanzibar inapanga kutumia Tshs. 10,000/- tu kwa kila mtu kwa matibabu, kinga na ustawi wa jamii ambacho ni sawa na USD 0.1, Mauritius kisiwa  kinachofanana  na Zanzibar lakini kina maamuzi yake katika nyanja za uchumi ,uhusiano wa nje na ustawi wa jami inapanga kutumia   zaidi ya USD 180 kwa kila raia 2008/2009.  Tunataraji miujiza gani itokee ambapo sekta hii itatoa huduma zinazohitajika.

Mhe. Spika,

Upatikanaji wa fedha hiyo iliyokadiriwa nayo ni mtihani na kikwazo kukubwa katika hudma za Afya.  Hadi Macih 2008 (miezi 9) ni asilimia 65.43% ya bajeti yote wastani wa 7.27% kwa mwezi ambapo hadi kufika Juni isingetarajiwa kuzidi 87%.

Mhe. Spika,

Hata hivyo jaduali kiambatisho Na. 24 inaonesha kuwa sehemu za UTAWALA ndiyo inayochukua fungu kubwa la ugavi. Siyo tu hujipaqngia fungu zao kubwa lakini hata kile wanachokipata ni asilimia kubwa ya viwango walivyoomba.

Angalia:  mipango na Sera hadi Machi 2008 imepewa 71.77% wakati

Mnazi Mmoja    46.77 %

Tiba Unguja      42.77 %

Tiba Pemba       50.54 %

Naomba Mhe. Waziri atueleze ni kwa nini hutokea hali hii?

Mhe. Spika,

Kwa mujibu wa kitabu hiki Idara TIBA inajumuisha.  Hospitali za Wilaya ambazo kwa Unguja ni mbili Makunduchi na Kivunge na kwa Pemba ni hospitali za Wete, Chake Chake, Mkoani na hospitali za Vitongoji na Micheweni.  Kwa hapa napenda kuipongeza Wizara kwanza kuliweka bayana hili lakini pia kuonesha katika Jadueli ya kiambatanisho Na. 24 Bajeti ile ya Idara ya Tiba Unguja na ile ya Pemba.

Mhe. Spika,

Jambo ambalo sikubaliani nalo kabisa ni ule uwiano wa mgao wenyewe wa Bajeti.  Mbali ya kuwa Pemba kuna hospital 5, na Unguja 2, bali hata idadi ya waliohudumiwa inaonesha tofauti kubwa na wengi zaidi wako Pemba.

Mhe. Spika,

Katika jadweli ya kiambatanisho No. 14 katika uk. 57. Idadi ya wagonjwa wa nje waliohudumiwa katika hospitali 5 za Pemba ni 56,157 wakati huo huo wale wa hospitali 2 za Unguja 12,286. Kwa wagonjwa waliopata huduma za ndani yaani wale waliolazwa, kwa hospitali 5 za Pemba ni 13,909 na kwa hospitali 2 za Unguja 2,309.

Mhe. Spika,

Wakati wagonjwa wote waliohudumiwa na hospitali 7 hizi hadi kufikia Machi 2008 ni  84,661, Pemba ambayo ilihudumia wagonjwa 70,066 ambayo ni asilimia 83% ya wagonjwa wote, ilipangiwa kutumia milioni 84 na zile hospitali 2 za Unguja ambazo zilihudumia wagonjwa 14,595 asilimia 17% ya wagonjwa wote ilipangiwa milioni 196 zaidi ya mara mbili ya ile ya Pemba.

Mhe. Spika,

Kwa kweli itabidi Mhe. Waziri aje na fomula nzuri ya kutueleza ni kipengele gani na utaratibu gani ulitumika kufanya mgao huu.

Mhe. Spika,

Suala hili mimi nimeshalizungumzia tokea bajeti ya 2006/2007 lakini bado halijarekebishwa. Haitoshi hiyo, bajeti ya mara hii 2008/2009 Tiba ya Unguja imepangiwa milioni 499 wakati Tiba ya Pemba millioni 110 tu.  Hii ya mara hii ni kubwa zaidi maana ni mara 4.5 au asilimia 450 ambayo ni kinyume kabisa.

HOSPITALI

IDADI

YA WAGONJWA

ASILIMIA

FEDHA

ILIYOTENGWA

2007/2008

FEDHA

ILIYOTENGWA

2008/2009

2  Unguja

14,595

17%

196 milioni

499 milioni

5  Pemba

70,066

83%

84 millioni

110 millioni

Mhe. Spika,

Ni suala hata haliingii akilini kuwa kule kunakohudumiwa wagonjwa wengi kupewe fungu dogo tena dogo sana na kule kunakohudumia watu kidogo kupewe fungu kubwa.

Mhe. Spika,

Naomba hapa Wizara na Baraza lako tukufu lilione hili kwani hospitali za Mnazi Mmoja, Rahaleo na ile ya wagonjwa wa akili, Kidongo Chekundu zinakusanyika katika Idara ya Hospitali ya Mnazi Mmoja ina bajeti yake wenyewe na mimi sina tatizo na hilo.

Mhe. Spika,

Hali hii inasikitisha sana siyo tu kupanga mipango kinyume nyume lakini suala zima la matumizi ya takwimu ambalo linaripotiwa hata na mtakwim Mkuu wa Serikali kuwa lina nafasi ndogo katika maamuzi ndani ya Maidara na Mawizara. Jambo la kusikitisha zaidi hizi ni takwimu zao wenyewe lakini hazifui dafu mbele ya maamuzi. Mheshimiwa Waziri aje na jibu la kutosheleza.

Mhe. Spika,

Napenda pia niwapongeze Wizara kwa kuleta mabadiliko katika kitabu hiki cha bajeti 2008/2009 kwa kuweka malengo katika kila Idara na kitengo. Ni sehemu ya mafanikio na muelekeo mzuri. Lakini ni bahati mbaya sana kuwa malengo haya si mahsusi kama wanavyotaka wataalamu.

Mhe. Spika,

Kwa kutumia herufi tano unapata neno SMART ambapo malengo yanatakiwa yawe Specific, Measurable, Attainable, Realistic, and Time bound, yaani yawe mahsusi, yanapimika, yanafikika (kiuwezo), na yamewekewa muda. Wizara inafaa ifanye jitihada ya ziada ya kurekebisha hayo hata kama ni bajeti ijayo. Mwanzo mgumu.

Mhe. Spika,

Katika kitabu cha Bajeti 2006/2007 Wizara ilipanga malengo 13 katika ukurasa 44 na 45 lakini tena ni bahati mbaya sana hatukuelezwa utekelezaji wake, yale yaliyokamilika, yale yanayoendelea na yale yaliyokwama na sababu zake.  Hii ni kasoro.  Mhe. Waziri  atueleze basi malengo yale yalifikia hatua gani?

Mhe. Spika,

Pamoja na hayo Bajeti hii 2008/2009 katika ukurasa 41 na 42, tumetajiwa tena malengo 16 ya Wizara.  Lengo lililonivutia zaidi ni lile la 12: “Kujenga nyumba 40 za wafanyakazi (20 Unguja na 20 Pemba) katika vituo vya Afya.

Mhe. Spika,

Suala ambalo najiuliza hapa je, nyumba hizi zitajengwa ndani ya kipindi hiki 2008/2009 au uanzishaji wa ujenzi ndiyo utakuwa ndani ya 2008/2009.  Naomba Mhe. Waziri afafanue.

MATIBABU

Mhe. Spika,

Wizara haina budi kutoa msukumo wa kipekee katgika kuimarisha eneo hili la Matibabu(Tiba)  Upatikanaji wa madaktari mahiri, manesi waliobobea na wafanyakazi wengine katika vitengo mbali mbali hutegemea na umakini wa Serikali na Wizara katika kutoa maslahi mazuri, kuwapatia elimu ya kiwango cha juu na kuwatengezea mazingira mazuri ya kazi ikiwa ni pamoja na hudma za usafiri na nyenginezo.

Mhe. Spika,

Mapungufu makubwa yaliyo katika eneo hili kunapelekea madaktari wetu kupewa maslahi madogo na mazingira ya kazi yasiyoridhisha ambayo huathiri kwa kiwango kikubwa huduma hii ya TIBA na hata  kupelekea kuhama kwa madaktari wetu na wataalamu wengine kwenda maeneo yenye maslahi zaidi.

Mhe. Spika,

Katika kuwapata wataalam hususan madaktari ni muhimu sana kuzingatia ubora wa taaluma hiyo.Jambo ambalo linatia wasiwasi mkubwa ni ile taaluma wanayopewa vijana wetu na madaktari kutoka Cuba.

Mheshimiwa Waziri aje atueleze kama  vijana hawa katika  mazingira wanayosomea inawapa fursa ya kujifunza mafunzo ya kimsingi ya “Medicine” kwa mfano kama microbiology, pathology, pharmacology na mengineyo? Je, wanapata kukabiliana (exposure) na maabara? Mheshimiwa Waziri atueleze bajeti iliyotajwa kwa ajili ya kozi hii inatolewa yote na Serikali au kuna msaada wa kifedha kutoka Serikali ya Cuba. Ni chuo kikuu gani kitawatunukia vyeti?

Mhe. Spika,

Kama ingekuwa taaluma hii ni kwa ajili ya kunyanyua viwango vyao vya ufahamu juu ya fani hii (Preliminary Course) ingelikuwa ni jambo la maana sana, lakini kwa kuambiwa wanasomeshwa kikamilifu na madaktari hawa mpaka kuhitimu ni jambo la kutazamwa upya ingefaa wizara kupitia jopo lake la madaktari waliopo wakalikalia kitako mapema na hata kuwaalika wengine ili kupata ushauri wa pamoja nini kifanywe kabla ya kufikia wakati hao vijana wameshatumia muda mrefu lakini ikawa hawakufikia kiwango na sisi wakati huo tuna mahitaji makubwa ya madaktari katika  hospitali zetu.

Mhe. Spika,

Hali hii ilishawahi kutokea katika miaka mwisho wa miaka ya 60 kwa madaktari wa kichina waliwafundisha watu wetu hapa lakini hakuna aliyefikia kiwango cha daktari (MD) na wengi walikataliwa hata kufanya “internship” hapo Muhimbili.

Mhe. Spika,

Jambo jengine ambalo linakwamisha na kulalamikiwa sana katika eneo hili la TIBA ni suala zima la uchunguzi na zana za uchunguzi, ukosefu wa baadhi ya zana za uchunguzi, uchakavu au kukosekana kwa matengenezo au upatikanaji wa zana hizi pamoja na kukosekana utaratibu madhubuti wa kumfanyia mgonjwa uchunguzi kunapelekea baadhi ya wagonjwa kupewa matibabu siyo na matokeo yake maradhi huzidi na kumalizia kuanza safari za kufuata matibabu kwengineko. Hao ndiyo waliobahatika wengi huingia maradhi mengine na kuiaga dunia.

Mhe. Spika,

Kutokana na kupatikana kwa wagonjwa wengi wa saratani za aina mbali mbali na siyo ile ya shingo ya uzazi tu ni mara ngapi tushazungumza na kulieleza ndani ya Baraza lako tukufu kuwa Zanzibar umefika wakati sasa ipate Maabara na wataalamu wake wa Pathology,  nini  Mhe. Waziri anatueleza kuhusu suala hili? Au wagonjwa wetu waendelee kuteseka na wengine kupoteza maisha yao hali familia zao zikijikamua katika tone lao la mwisho la uwezo kufuatilia uchunguzi huo Tanzania Bara na kwengineko.

Mhe.Spika

Wataalam wa Afya wanaandika kuwa: Pathologists are essential members of the patient’s primary health care team, and not only monitor the effects of therapy but also practice preventive medicine ruling out diseases or detecting them EARLIER”

Mhe. Spika,

Umuhimu wa wataalamu hawa, pathologists, hauwezi ukatiliwa mkazo zaidi ya maneno hayo yaliyosemwa na wataalamu hao na lililonivutia miye zaidi ni lile neno “earlier” yaani “mapema sana”, kwani hivi ndivyo daktari, mgonjwa na mwenye mgonjwa wanavyotaka. Maradhi yajulikane na mapema ili daktari aweze kuokoa afya na maisha ya mgonjwa yule na yule mgonjwa apate kupumzika na maumivu yatokayo na ugonjwa huo na jamaa wa mgonjwa aondokane na simanzi, aokoe fedha na muda ili apate kushughulikia mengine.

Mhe. Spika,

Kukosekana kwa wataalamu hao na vitengo hivyo kunawafanya wagonjwa wetu kila siku kiguu na njia na mara apande boti au ndege kufuatia kwengine. Mara hii nataka Mhe. Waziri aje na jibu la uhakika hasa nini mkakati wa Wizara juu ya uanzishwaji rasmi pathology laboratory yenye zana na siyo microscope tu.

Kwa mnasaba huo huo Wizara ina mkakati ngani wa kuzipatia hospitali zetu machine za CT Scan? Na kuingia kweli katika karne ya 21 ya hudma bora za AFYA.

Mhe. Spika,

Mimi binafsi nimeingia raghba kwani lile neno “earlier” yaani mapema sana limejitokeza tena katika kuelezwa uwezo wa mashine hii: “ACT Scan obtain images of parts of the body that cannot be seen on standard x – rays and has a diagnostic benefits which results in earlier diagnosis and more successful treatment of many diseases.”

Mhe. Spika,

Angalau Wizara ya Afya ingepiga hatua ikaanza na hii ijapokuwa iko kubwa zaidi na ghali inayoitwa MRI ambayo haitumii mionzi ya x-rays.,ingawa ingepatikana ni faida kubwa zaidi hasa kwa hospitali ya rufaa.

Mhe. Spika,

Ninalokusudia kulielezea hapa ni vipi TIBA yetu ilivyo nyuma na kutumia njia za kizamani (traditional) na kupoteza nafasi ya kutumia teknolojia ya kisasa katika kuwasaidia madaktari wetu kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi.

Mhe. Spika,

Madaktari karibu dunia nzima ni watu wenye huruma sana na hupenda sana kutumia muda wao mwingi kutoa hudma kwa wagonjwa. Hivyo kukosekana kwa zana hizi za uchunguzi siyo tu tunawanyima madaktari kutumia muda wao nzuri zaidi na kutoa matibabu sahihi, pia tunawanyima wananchi wengi kupatiwa matibabu hayo, ikiwa hiyo haitoshi hata ziara za madaktari mabingwa kutoka nchi nyingi za dunia huzuilikana kututembelea kutokana na vifaa hafifu au kukosekana kabisa.

Mhe. Spika,

Kwa kumalizia kuhusu zana nataka nitaje tena juu ya haja ya kupatikana kwa chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) katika hospitali za Pemba. Mimi sidhani kama suala hili limeshindikana kwa sababu ya matatizo ya kiuwezo bali naona na aina fulani ya dharau ipo. Ikiwa si hivyo Mhe. Waziri basi aje na mkakati wa wizara yake.

Mhe. Spika,

Utaratibu wa kumshughulikia mgonjwa mpaka akapata matibabu (patient care) pia nao umeingia kasoro kwa baadhi ya madaktari, manesi na wafanyakazi wengine, bado hairidhishi, naomba nitowe taarifa ya tokeo halisi.

Mnamo tarehe 26/06/2008 polisi walimpeleka hospitali kijana aliyejulikana kwa jina Sagafu Rajab Mdachi mkaazi wa Tomondo umri miaka 16 akiwa mahtuti baada ya kushambuliwa na majambazi mnamo saa 8.00 mchana. Alipelekwa hospitali akiwa na kauli yake.

Mhe. Spika,

Baada ya kufika jamaa zake walipewa taarifa kuwa ultra sound haifanyi kazi na hivyo wampeleke Al-Rahma.  Alirejeshwa kutoka Al Rahma. Baada ya kufanyiwa  ultra sound mnamo saa 12.00 JIONI na baada ya hapo alilazwa na kupatiwa drip tu na kuambiwa jamaa zake wakamnunulie vidonge.  Saa 8.00 ya usiku aliaga dunia. Kutokana na maelezo ya jamaa zake  huko Al Rahma waliambiwa wamrejeshe Mnazi Moja haraka kwani ametoka damu ndani ya tumbo. Haikueleweka ni kwa nini asipelekwe theatre kwa kushughulikiwa. Tunamuomba Mhe. Waziri afanye uchunguzi wa kina ili kesho akitoa majumuisho atueleze utandu na ukoko.

Mhe. Spika,

Ni kwanini Wizara na hospitali hazitoi tag za majina kwa staff wote wakalazimika kuzivaa wakati wote wakiwa kazini.  Kwanza itasaidia kuweka uwazi (transparency) juu ya nani anayetoa huduma lakini pia itapunguza kwa kiwango kikubwa shutma zinazotupiwa Wizara au hospitali za uzembe, lugha chafu au hata rushwa.  Naomba Mhe. Waziri aje na jibu la muafaka kuhusu suala hili.

Mhe. Spika,

Napenda nimkumbushe Mhe. Waziri kuwa naona utoaji huduma hizi za afya una taathira kubwa katika kupatikana au kutopatikana mafanikio, kama wataalamu wasemavyo: “Diseases and ailments prevalent in Africa can significantly be minimized or even eradicated by the establishment, excecution and delivery of a comprehensive health care reform emphasizing quality, equity and access.”

Hivyo lazima tubadilishe mfumo na tubadilike na Mhe. Waziri ana wajibu wa kusimamia haya.

Mhe. Spika,

Katika malengo ya milennia ni kupunguza vifo vya wajawazito na watoto wachanga.  Familia nyingi zinaishi katika hali ya umaskini Serikali ina wajibu wa kuongeza kipato cha Nchi na hivyo kuongeza kipato cha watu waweze kumudu lishe.

Kwa upande wa Wizara ya Afya bado wana wajibu wa kuandaa mipango mizuri kwa ajili ya hudma ya mama wajawazito.  Ni wakati wa kuamua kwa maslahi yao hawa, kizazi walichonacho na nchi kwa jumla kuwa yale malipo ya kufanyiwa uperesheni ya Mzazi yaondolewe kabisa.

Mhe. Spika,

Wizara haina budi irejeshe hudma za gari za wagonjwa (ambulance), hudma ambayo takriban inakaribia kusahaulika.  Mama wajawazito wanachukuliwa katika gari za aina zote, zikiwemo hata gari za ngombe na wengine juu ya mabega ya watu akiwa kwenye kitanda cha kamba kwa sababu huma hii haipo.

Mhe. Spika,

Umeshafika wakati ambulance zichukue wagonjwa kutoka vijijini na pia kuwapeleka katika hospitali nyingi. Tukianza tutafika.

Mhe. Spika,

Kuhusiana na madaktari na hospital za watoto, inalazimika kutiliwa mkazo zaidi ili kila hospitali iwe na Daktari wa watoto na pahala kama mnazi mmoja ni muhimu lijengwe jengo jengine kwani kila mtoto hufuatana na mlezi wake na msongamano unakuwa mkubwa.

Mhe. Spika,

Pia watoto wako katika hatari zaidi kuambukizwa maradhi hivyo ni muhimu kuwa siyo na daktari wao tu (padaetrcian) bali na jengo lao maalum.  Njia hii pia inatiliwa mkazo na fikra iliyoko ulimwenguni “Treating the whole child” yaani mtoto anapopelekwa hospitali asitibiwe lile alilopelekewa tu bali achunguzwe zaidi na mengineyo ili kuondoa uwezekano wa kupata athari nyengine ambazo zingeweza kugunduliwa mapema.

Mhe. Spika,

Wizara pia ingekuwa makini zaidi katika kuratibu madaktari walioko katika hospitali mbali mbali na mahitaji halisi.

Mhe. Spika,

Sisi ni nchi ndogo sana na hili lingefanyika kwa wepesi.  Inasikitisha sana kuona baadhi ya hospitali hasa za Pemba mara kwa mara huwa na upungufu wa madaktari bila ya hatua muafaka kuchukuliwa na Wizara.  Hospitali ya Mkoani mfano inapokea madaktari kutoka China lakini ni miaka mingi sasa hawaleti daktari wa watoto (paedatrician) bado Wizara haionekani kuchukua hatua ya kulisawazisha badili yake wapo wasaidizi tu kwa muda wote.

Mhe. Spika,

Bado, hakujakuwa na utaratibu wa kupeleka daktari pale ambapo madaktari wanakwenda likizo.  Hospitali hubaki haina daktari au madaktari mpaka warudi likizo.  Jee Wizara ina utaratibu gani wa kuondoa pengo hilo.

Mhe. Spika,

Ingefaa pia madaktari wadhamini wa hospitali ya Mnazi mmoja, Wete, Chake na Mkoani wakapewa uwezo wa kutawalia bajeti zao, inasikitisha kuwa wnaopewa dhamana hawapewi uwezo.  Wizara inachukua jukumu kwa hapa Unguja na Afisa Mdhamini kwa Pemba, jambo ambalo linapunguza ufanisi wa hudma za hospitali hiyo.

Katika makala yake Generation for change and Growth mtaalamu wa Kenya anaandika: “Unlocking possibilities in Africa’s health care sector begins with leadership that is commited and responsible. Talents are there but institutional framewok policies and standards of practice are needed to create the next generation of leaders in Health Care.”

Mhe. Spika,

Kwa ufupi wale wote wanaopewa dhamana katika nucleus ya Afya – Hospitali basi wapewe na uwezo wa kuamua na kutumia.  Ni lini mambo haya yatateremshwa kwa wanaohusika zaidi?

Mhe. Spika,

Hospital za Pemba zimekabiliwa na upungufu wa wafanyakazi katika sekta zote.  Manesi ambao wengi wao huwa hawarudi Pemba baada ya masomo wanapelekea hospitali za Pemba zikumbwe na uhaba mkubwa.

Mhe. Spika,

Ingefaa Wizara ikabadilisha mfumo wa kusomesha kama vile kuwapa mafunzo “Ward attendant” orderlies ya mwaka 1 na baadae wawe kama manesi wasaidizi na ili kukabiliana na tatizo hili

Mhe. Spika,

Ingefaa Wizara ikalitizama upya lile suala la Rotary doctors kutoka Sweden na wale wa UNDP kwani mbali ya kuziba mapengo bali pia husaidia baadhi ya vifaa ambavyo tayari vina upungufu au havipo kabisa katika vipindi tofauti.

Mhe. Spika,

Marekebisho ya mishahara yaliathiri kwa kiwango kikubwa wafanyakazi wengi ambao wako katika viwango vya Diploma na Certificate katika sekta hii ya Afya.  Ingefaa Wizara ikalitazama upya pamoja na kutoa kwa ukamilifu hudma za likizo, overtime na on call allowance.

Mhe. Spika,

Kwa kuwa kuna baadhi ya vitengo kama vile vya X – rays vinatumia mfumo wa – “cost – sharing” yaani wagonjwa wanachangia ingefaa vitengo hivi vikaachiwa fedha hizo ili kuvifanya vifanye kazi na uhakika.

CHUO CHA AFYA MBWENI

Mhe. Spika

Katika kitabu cha bajeti 2008/2009, Kiambatisho Na. 4, takwim ya chuo inatia moyo juu ya ongezeko la wanafunzi na mimi napenda niipongeze wizara. Pamoja na hayo kuna matatizo kadhaa ingefaa wizara ikayashughulikia yakiwemo:

  • Hali ngumu ya maisha na kujikimu kwa vijana wanaokaa hapo
  • Pamoja na wanafunzi kulipia usafiri bado hawapati hudma hiyo kikawaida
  • Malipo yaliyo wazidi vimo wakati wa kenda kenye practicals mwisho wa muhula
  • Kuna baadhi ya kada huna kufika hata miaka kosa msimamo wa muda wa masomo kwani huanzia mafunzo ya miaka mitatu na kumalizia mitano

Maslahi ya Walimu

Mbali na hayo inatia moyo kuwa ujenzi unaendelea lakini katika kitabu ni kimya, tungeelezwa nani mkandarasi muda na gharama.

Mhe. Spika,

Hospitali, Zahanati, Kliniki na famasia za binafsi ni sehemu muhimu sana katika kutoa hudma ikisaidiana na taasisi kama hizo za Serikali.

Serikali na Wizara ikitumia ule ule msimamo mpya katika utawala bora wa PPP- Pablic Private Partreship haina budi kaziunga mkono juhudi za wazalendo hao na kuwapa kila msaada badala ya kuwakamua tu katika kodi, na malipo ya leseni nyingi ambapo mzigo unawaelemea wananchi wanyonge.

KINGA NA ELIMU YA FYA

Mhe. Spika,

Idara hii inaonekana kufanya vizuri tu kwa yale maradhi yaliyopata ufadhili wa nje, hata hivyo kuna dalili ndogo ya uendelevu wa miradi (sustainability) wafadhili wanapoachia mkono. Hii si njia sahihi kwa kupambana na maradhi na tufuate msemo wa Kiswahili usemao “mjima hamalizi shamba.”

Mhe. Spika,

Tunawajibika kuendeleza kwa nguvu zetu zote mapambano dhidi ya malaria pale walipotuachia wafadhili wetu. Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kukipunguzia kwa kiwango kikubwa maradhi haya ya malaria chini ya usaidizi wa USAID na usimamizi mzuri wa Wizara ya Afya na Ustawi wa jamii, lakini bado napenda kudhihirisha hisia zangu (my concern) kwa Wizara namna wanavyochukulia kupungua huku kwa malaria.

Mhe. Spika,

Kutokana na hali halisi ya jamii yetu, sasa hivi harakati baina ya Unguja na Tanzania Bara na Tanzania Bara, Unguja na Pemba, naomba Mhe. Waziri  kuendeleza mapambano dhidi ya malaria kuirudisha hadi 0% na kuibakisha hapo, kwani Tanzania Bara bado malaria iko juu.

Mhe. Spika.

Maradhi ya kichocho yanahitaji kazi kubwa mbali na kutoa “drugs” kwa ajili ya matibabu lakini kunaonekana kuna kujirudia kwa wale wale waliotibiwa. Hii inaonesha bado jamii zetu hazijakubali kufuata utaratibu wa kujikinga na zaidi inaonekana kuwa haijapatiwa elimu ya Afya au waliopewa haitoshelezi. Ule utaratibu wa mabwana Afya kupita katika jamii, maskulini, kwenye madrasa umekosekana na ni vyema Mhe.Waziri akaja akatueleza mikakati ya Wizara katika elimu ya Afya.

Mhe. Spika,

Ushirikishwaji wa jamii katika program za kinga na chanjo ni muhimu kungefanyika kwa uangalifu sana. Kutokana na hali ya kutokuaminiana kisiasa ni vyema viongozi mbali mbali wakiwemo, madiwani, masheha, viongozi wa vyama vya kisiasa wakashirikishwa ili kuondoa utata unaoweza kujitokeza. Mara nyingi Wizara inaburuzwa upande mmoja na kuwaachia masheha wakafanya maamuzi peke yao ambayo huleta migogoro ndani ya jamii jambo ambalo huzorotesha utekelezaji wa miradi.

Mhe. Spika,

Naomba kuwasilisha.

Advertisements

2 thoughts on “Mbona SMZ inawaangalia hadi wagonjwa kwa jicho la U-unguja na Upemba?

  1. tunashukuru sana ndugu mtangazaji kwa kutufumbua macho hiyo shukrani.na hapo na wazo langu ndugu mtangazaji ya kwamba ungetoa majarida au vitabu hata copypapers ili ndugu na jamaa zipate kuwafikia vema.tuzidi jamani kufikiria maisha yetu na hata watoto wetu badae

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s