CUF yainyooshea kidole SMZ kutumia vikosi vyake kisiasa

…..Naomba niitumie fursa hii kuihadharisha SMZ kwa mara nyengine tena IACHE MARA MOJA mpango wake huo kwani sio tu unaidhalilisha DEMOKRASIA, lakini pia ni hatari, sio tu kwa wananchi wa jimbo la Chonga pekee lakini ni kwa Zanzibar nzima. Mimi, na kwa niaba ya Kambi ya Upinzanii, siko tayari hata siku moja kuona pesa za walipa kodi wa nchi hii zinateketezwa kwa kurundika vijana wa maskani katika makambi haya kwa ajili ya kuipigia kura CCM na kwa mantiki hiyo ni vyema tukaziba ufa kabla hatujalazimika kujenga ukuta.

Mhe Abdalla Juma Abdalla - Mwakilishi wa CUF Jimbo la Chonga

Mhe Abdalla Juma Abdalla – Mwakilishi wa CUF Jimbo la Chonga

Hotuba ya Waziri Kivuli Wizara ya Nchi Afisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Vikosi vya SMZ. Mhe. Abdalla   Juma Abdalla kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka 2008/2009: aliyotoa kwa Niaba ya Kambi ya Upinzani katika Baraza la Wawakilishi

Mhe. Spika,

Kwanza kabisa hatuna budi kumshukuru Mwenyezi Mungu, aliyeumba mbingu na ardhi pamoja na vyote vilivyomo ndani yake kwa kutujaalia hazina hii ya uzima na hatimae kutupa uwezo wa kuondoka MAJIMBONI mwetu bila ya kukamatwa mikono, kwa hali hiyo sote kwa  jumla hatuna  budi kumashukuru Allah.

Pia naomba niutumie fursa hii kukushukuru wewe binafsi Mhe. Spika, kwa kunipatia fursa hii muhimu sana  kutoa mawazo ya Kambi ya Upinzani kuhusiana na hoja hii iliyopo mbele yetu.

Mhe. Spika,

Ki msingi Wizara hii ina taasisi nane pamoja na mikoa mitano kama ifuatavyo:-

 • Idara ya Mipango na Sera
 • Idara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
 • Idara ya Usajili na Utoaji Vitambulisho vya Mzanzibari
 • Kikosi maalumu cha kuzuia magendo (KMKM)
 • Kikosi cha Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU)
 • Kikosi cha Vyuo vya Mafunzo (MF)
 • Kikosi cha Zimamoto na Uokozi (KUZ)
 • Na kikosi cha Valantia.

Pamoja na Mikoa ya :-

 • Mjini Magharibi
 • Kaskazini Unguja
 • Kusini Unguja
 • Kusini Pemba
 • Kaskazini Pemba

Mhe. Spika,

Utekelezaji wa UFANISI wa majukumu ya Wizara hii hutegemea zaidi, UMAHIRI, NYENZO ZA KUFANYIA KAZI (FEDHA NA VIFAA), pamoja na NIA SAFI na DHAMIRA NJEMA iliyokuwepo  ya kuanzisha  Taasisi hizo, wala sio kufanya kazi kwa kupitia misingi ya UBINAFSI, UBAGUZI au kwa misingi ya kisiasa au uzawa.

Aidha pale palipo na nia njema na bidii ya kazi huwezi kuona mipango dhaifu wala ukiritimba uliobobea unaoongozwa na dhamira za kisiasa kujitokeza ambao huweza hatimae kuchafua jina la taasisi hiyo na kuwaondolea wananchi imani na matumnaini.

Mhe. Spika,

Mara baada ya utangulizi huo mfupi, sasa naomba Baraza lako tukufu lipokee mawazo ya Kambi tukufu ya Upinzani kuhusu Taarifa ya utekelezaji, pamoja na kasoro zilizojitokeza katika baadhi ya Taasisi za Wizara hii, kwa kipindi cha mwaka 2007/2008.

UTEKEZAJI WA SHUGHULI ZA KAZI NA UENDESHAJI KATIKA IDARA MBALI MBALI ZA WIZARA HII.

Mhe. Spika,

Kwa mujibu wa hotuba yake Mhe. Waziri amekiri kuwa shughuli za utendaji wa kazi na uendeshaji katika Taasisi zake zote zilikwenda vizuri kwani upatikanaji wa fedha na vitendea kazi ulikua mzuri sambamba na kuwaendeleza watendaji wake kielimu. Aidha ameendelea kuzishukuru Kamati za Baraza la Wawakilishi pamoja na Wizara ya Fedha na Uchumi kwa juhudi zao zilizopelekea ufanisi wa Wizara yake.

Mhe. Spika,

Mhe. Waziri pia amekiri kuwa katika kipindi cha 2007/2008 Wizara yake iliidhinishiwa matumizi ya Tshs 21,692,760,000/- kwa ajili ya kazi za kawaida za Taasisi zake zote, na hadi kufikia mwezi wa April 2008 tayari walishapokea na kutumia jumla ya Tshs. 16,986,0055,734/- kwa mantiki hiyo upatikanaji wa fedha haukua na tatizo katika uendeshaji wa shughuli za Wizara.

Mhe. Spika,

Kwa mnasaba huu tulitarajia kwamba shughuli za uendeshaji katika taasisi za Wizara hii kwa kipindi hicho zingekwenda vizuri, bila ya ubaguzi baina ya Taasisi za Wizara na bila ya kujali jografia au Taasisi hiyo ilipo.

Mhe. Spika,

Jambo la kushangaza na la kusikitisha ni kuwa Wizara hii imekua ikifanya kazi katika misingi ifuatavyo:-

UBAGUZI, KUTAMBURIKIWA (KUKURUPUKA)

Suala la ubaguzi katika Wizara hii pamoja na Taasisi zake limekuwa likijitokeza mara kwa mara wakati wa kutoa ajira, ambapo ajira huwa haipatikani mpaka pale aidha uwe mwananchama wa  CCM, au mzaliwa wa kisiwa cha Unguja, inasikitisha kuwa, na haifurahishi hata kidogo kuona kuwa nafasi za wapiganaji wa Vikosi vya SMZ kwa upande wa Pemba zaidi hujazwa na watu wa Unguja badala ya Wapemba wenyewe au wapemba ndio hawana haki katika ajira hizi za Vikosi? Na pale ambapo hapana budi aajiriwe Mpemba basi lazima angaliwe itikadi yake ya kisiasa yaani awe mwanachama wa CCM aliebobea  Je mwana CUF yeye hana haki ya kuajiriwa katika Vikosi hivi, hivyo ni sheria gani katika nchi hii inayomzuia mwana CUF kuajiriwa katika Vikosi hivi? Au  Vikosi hivi ni vya CCM.

Mhe. Spika,

Katika kuendelea na ubaguzi wake dhidi ya Wapemba, SMZ imethubutu bila ya kuona  haya kuwataza Makamanda wote wa tano wa Vikosi vya SMZ kutoka kisiwa cha Unguja. Jee, ndio hakuna Mpemba yeyote mwenye uwezo wa kuwa Kamanda katika Vikosi hivi?.

Mhe. Spika,

Wakati Wizara ikiimarisha uwezo wa wafanyakazi wake pamoja na kuinua hadhi ya Taasisi zake zote inasikitisha kuona kuwa jengo la Afisi Kuu – Pemba bado halina hadhi ya kuchukua Afisi kubwa na ya Wizara muhimu kama hii- wakati Taasisi nyengine zikipewa uwezo wa kujenga uzio, MABWENI, nyumba za kisasa pamoja na  mambo mengine ya kifahari ambayo hugharibu fedha nyingi kama alivyotueleza  Waziri katika  hotuba yake ya mwaka jana uk. 119 katika Jedweli linalofafanua utekelezaji wa JKU ambapo kwa ujenzi tu walitumia Tshs.49,600,000/- ambapo kati ya hizo ni Tshs.5,700,000/- tu zilizotumika kwa upande wa Pemba na zilizobaki zote ziliteketea kwa upande  wa Unguja: sasa iweje jengo la Afisi Kuu – Pemba ambapo ndio uso wa Wizara mzima iwe bado ni la kurithi, na lililokosa hadhi sio tu ya Afisi, lakini hata kuwa bweni la wanafunzi, au hii imefanywa maksudi kwa ajili ya kuendelea kuwabagua wapemba?.

Mhe Spika,

Ukiachilia mbali suala la UBAGUZI kama ambavyo nimelieleza kwa ufupi, lakini baya zaidi ni pale SMZ kupitia Wizara hii inapofanya shughuli zake katika misingi ya kisiasa na kukurupuka kwa mfano tumeshuhudia mara kadhaa uanzishwaji holela wa makambi ya vikosi pamoja na kutoa uhamisho wa wapiganaji  holela wenye malengo ya kisiasa zaidi kuliko utendaji ambapo fedha nyingi za walipa kodi wa nchi hii huteketea kwa maslahi ya Chama kimoja tu cha CCM, kama ambavyo hotuba zangu za miaka ya nyuma zilivyotoa ufafanuzi wa kina katika hili.

Mhe. Spika,

Suala la SMZ kuitumia Wizara hii kuimarisha makambi ya vikosi hivi kwa malengo ya kisiasa sio tu limeathiri UCHUMI wa Nchi hii lakini hapo mbele linaweza kuhatarisha hata amani na usalama wa  wananchi – hivi tunavyozungumza hapa: pamoja na kwamba Waziri wa Wizara hii bado hajaleta hoja ya kuomba aidhinishiwe fedha za kujenga Kambi nyengine ya Valantia kule Pujini, tayari kazi hiyo imeanza na inatakiwa mpaka ifikapo 2009 iwe imekamilika na inasemekana ni kwa ajili ya kupeleka vijana wa maskani, ili waje waisaidie CCM katika uchaguzi wa mwaka 2010, kama ambavyo wamefanya katika uchaguzi uliopita.

Kwa niaba ya Kambi ya Upinzani na wananchi kwa ujumla, naomba niitumie fursa hii kuihadharisha SMZ kwa mara nyengine tena IACHE MARA MOJA mpango wake huo  kwani sio tu unaidhalilisha DEMOKRASIA, lakini pia ni hatari, sio tu kwa wananchi wa jimbo la Chonga pekee lakini ni kwa Zanzibar nzima, mimi, na kwa niaba ya Kambi ya Upinzani siko tayari hata siku moja kuona pesa za walipa kodi wa nchi hii zinateketezwa kwa kurundika vijana wa maskani katika makambi haya  kwa ajili ya kuipigia kura CCM na kwa mantiki hiyo ni vyema tukaziba ufa kabla hatujalazimika kujenga ukuta.

IDARA YA USAJILI NA KADI ZA UTAMBULISHO WA ZANZIBAR

Mhe, Spika,

Kwa mujibu wa ufafanuzi na taarifa kutoka Serikali pamoja na hotuba mbali mbali za Waziri ni kwamba,wajibu mkubwa  wa Afisi hii ni kuwasajili Wakaazi wenye umri wa miaka 18 na kuendelea. Aidha Afisi hii inao wajibu wa kutunza taarifa zote za wananchi zilizokusanywa kwa ajili hiyo: Mhe. Spika, kwa mujibu wa Hotuba ya Bajeti ya Mhe. Waziri ya mwaka 2007/2008 alilieleza Baraza lako tukufu kuwa hadi kufikia mwezi Mei, 2007, jumla ya  wazanzibari wakaazi laki nne tisini na sita elfu mia moja na kumi na nane (496,118) tayari wamesha sajiliwa ambapo ni sawa na asilimia tisiini na saba nukta tano(97.5)ya watu wanaotarajiwa kusajiliwa.

Mhe.Spika,

Kimsingi kwa hapa Zanzibar,kitambulisho cha Mzanzibar mkaazi sasa ndio ufunguo kila kitu-yaani bila ya hicho huwezi kupata leseni,wala ajira wala huwezi kuwa mpiga kura n.k. Kwa mantiki hiyo IDARA hii kwa kiasi kikubwa ndio inayosimamia vielelezo vya Wazanzibar kupata haki zao za msingi,jambo la kusikitisha na la aibu ni kwamba hivi tunavyozungumza katika kikao hichi zoezi hili linaendelea katika ofisi za wilaya katika mazingira yaliyojaa matatizo;kwa mfano kuna wazanzibar halisi wanaonyimwa vitambulisho hivyo kwa kukoseshwa  barua za masheha au  hutakiwa wainunue haki yao kwa pesa, jambo ambalo ni dhulma na ni ukiukwaji mkubwa wa haki.

Mhe. Spika,

Nnayo mifano kadhaa kuhusu hili, sambamba  na hilo inasadikiwa Afisi hii inaendelea kutoa haki hii ya Wazanzibari kwa makundi ya watu wasiohusika ili kuweza kukidhi malengo yao ya kisiasa na kuwachukulia wazanzibari haki zao za msingi kwa mfano Vijana wengi kutoka Tanzania Bara tayari wameshapewa haki hii ili waweze kuajiriwa  hususan katika vyombo vya ulinzi, la kusikitisha zaidi ni kuwa nafasi hizo huwa tayari zimeshatengwa kwa ajili ya wazanzibari, Mhe. Spika, mambo kama haya yasipochukuliwa hatua za dharura za kuyarekebisha  zikiwemo zile  za kulifanyia uhakiki daftari la vitambulisho hivyo, basi yatapelekea wazanzibri kukosa imani na Idara hi ya usajili.

Na kwa msingi huo kwa kuwa moja kati ya sifa za kuwa mpiga kura wa Zanzibar ni kuwa na kitambulisho hichi basi ni dhahiri sasa kwamba Wazanzibar watakua wakichaguliwa Rais wao na watu wasiokua wazanzibari jambo ambalo ni kusaliti Demokrasia katika kiwango cha kutisha.

Mhe. Spika,

Naomba kwa niaba ya kambi ya upinzani niitanabahishe SMZ kuwa uchaguzi wa Rais wa Zanzibar na Wawakilishi ni haki ya wazanzibar wenyewe na sio haki ya watu wengine, na sasa  wazanzibari wamesahachoka kusaidiwa maamuzi, ni vyema ikaacha mara moja kutoa uzanzibari kwa watu wasiohusika.

Mhe. Spika,

Kitendo cha Taasisi ya Vitambulisho cha kupora haki ya Wazanzibari na kuwapa watu wengine ni sawa na kupandikiza wageni ndani ya visiwa hivi, kitendo ambacho baadae  kinaweza kuleta TAATHIRA kubwa kwa Taifa letu  kwa mfano vurugu lililotokea hivi karibuni Afrika ya Kusini chanzo chake  ni Raia wa Afrika ya Kusini: kudai  haki zao wanazoendelea kuporwa na  wageni. Mhe. Spika, inafaa tuchukue kila tahadhari ili yaliyotokea Afrika ya Kusini na hapa kwetu yasijetokea.

VIKOSI VYA SERIKALI YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR

Mhe. Spika,

Vikosi vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar  inajumuisha Vikosi vifuatavyo:-

 • Kikosi cha Vyuo vya Mafunzo (MF)
 • Kikosi cha  Zimamoto  na Uokozi (KZU)
 • Kikosi maalum cha Kuzuia Magendo (KMKM)
 • Kikosi cha Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU)
 • Kikosi cha Valantia (KVZ)

Mhe. Spika,

Kwa mujibu wa SMZ, DHAMIRA kuu ya Vikozi hivi ni kuimarisha Ulinzi na USALAMA wa raia pamoja na mali zao kimsingi nia hiyo ilikua nzuri, lakini la kusikitisha  ni kwamba Vikosi hivi vimekua vikipoteza mwelekeo siku hadi siku, na kiujumla kutokana na mapungufu kadhaa yaliyojitokeza kutokana na kuwepo Vikosi hivi kwa niaba ya Kambi ya Upinzani na kwa niaba yangu binafsi naomba kusema yafuatayo:-

Nakiri kwamba Vikosi ni eneo moja linalotoa ajira nyingi kwa vijana, lakini ajira hizo hazionekani kuleta tija kwa jamii- yaani ni ajira isiyozalisha. Na kama ni kwa madhumuni ya ulinzi, basi Zanzibar ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano na dhima ya  ulinzi bado ni jukumu la Jamhuri ya Muungano, kupitia TPDF, POLISI NA IDARA YA USALAMA WA TAIFA. Na mimi binafsi sioni juhudi kubwa zinazochukuliwa na Vikosi hivi katika kulinda usalama wa raia na mali zao, na hivi juzi tu majambazi yalimpora mtoto wa miaka 16 pale Kinazini na kumpiga mpaka akafa. Je vikosi vilikua wapi? Kwa msingi huo mimi sioni sababu ya kurundika maelfu ya vijana katika kiwango hichi na kuteketeza mabilioni ya pesa za walipa kodi wetu pasipo na ulazima wowote wa kufanya hivyo.

Na kwa kuwa kwa sasa yaonekana kuwa vikosi hivi vipo kisiasa zaidi kuliko dhamira yake halisi, na mara nyingi mbali na kushiriki katika kuharibu uchaguzi pia hushiriki katika kuhatarisha maisha ya wananchi, hususan wapinzani, na  kwa kuwa silaha wanazozitumia kupiga na kuuwa wananchi (K.m. 2001) zilinunuliwa kwa fedha za walipa kodi wote wa nchi hii ni vyema silaha hizo zikagaiwa kwa vyama vyote vya siasa vilivyo na Wawakilishi Barazani na sio kuwaachia vikosi hivi pekee ambavyo kazi yao kubwa ni kuitetea CCM.

Kwa kuwa ajira katika vikosi hivi haipatikani mpaka pale aidha uwe mwana CCM au mzaliwa wa kisiwa cha Unguja jambo ambalo linaendeleza MPASUKO MKUBWA uliopo  baina ya watu wa visiwa hivi na baina ya vyama vya siasa, nashauri kuwa vikosi hivi vivunjwe kwani TPDF, POLISI na USALAMA WA TAIFA wanatosha kulinda nchi hii na raia wake na badala yake hao vijana waachiwe waendelee kupigia debe CCM na hilo fungu la fedha la zaidi ya Tshs. 16 bilioni ambazo zinatumika kugharimia mishahara ya Vikozi hivi likabidhiwe kwa  Wizara ya Kilimo ili yanunuliwe matrekta ya kusaidia kukuza sekta ya kilimo nchini.

Mhe. Spika, kwa mara nyengine tena narudia kutoa ushauri kwamba: kama nia ya Serikali ya SMZ ni kukusanya vijana hawa kwa ajili ya kuja kuisaidia CCM katika uchaguzi basi ni vyema tukabadilisha sheria za vikosi hivi na kutunga sheria nyengine itakayoviweka vikosi hivi kuwa ni vikosi vya CCM na wakapata mafao na mishahara yao kutoka Afisi ya CCM pale Kisiwandui.

IDARA YA TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA.

Mhe. Spika, kiutawala, Idara hii imegawika sehemu mbili kubwa:-

Tawala za Mikoa, ambayo inajumuisha Mikoa mitano ya Zanzibar, wilaya 10  pamoja na shehia 299.

Serikali za mitaa ambayo inajumuisha manispaa ya Mji wa Zanzibar, Mabaraza ya miji 3 ya Pemba pamoja na Halmashauri  9 za  Wilaya.

Mhe. Spika,

Kazi za Tawala za Mikoa zimebainishwa wazi katika sheria No.1 ya 1998 ambazo ni pamoja na utekelezaji na usimamizi wa sheria,  maagizo pamoja na sera za nchi, na kushughulikia matatizo yanayoibuka katika jamii n.k. Kazi za ukusanyaji wa mapato pamoja na utoaji wa huduma ni jukumu la Manispaa, Halmashauri za Wilaya pamoja na Mabaraza ya Miji.

Mhe. Spika,

Serikali yoyote iliyomakini hujikita katika kuiboresha sekta hii, serikali za Mitaa zinazowajibika ipasavyo huweza kukusanya kwa ufanisi kodi za wananchi wake na  kuzisukuma katika kuwaletea wananchi hao maendeleo. Kipimo cha ufanisi wa Serikali kuu hutokana na taswira ya utendaji mzuri wa serikali za Mitaa.

Mhe. Spika,

Jambo la kusikitisha na kutia uchungu ni kwamba SMZ mpaka leo bado haijaona umuhimu wa  sekta hii, jambo ambalo linapelekea kukosekana kwa ufanisi katika Taasisi hii nyeti. Inasikitisha  sana kuona mpaka leo, masheha wanajishughulisha na kupora mapato yatokanayo na mauzo ya mashamba, mifugo au viwanja kazi ambayo haiwahusu na ni jukumu la Madiwani.

Mhe. Spika,

Ukitembelea Halmashauri nyingi za Wilaya utakuta manung’uniko makubwa yanatokana na kunyimwa mapato yatokanayo na mauzo ya viwanja vya mahoteli na mashamba jambo ambalo linadhalilisha Halmashauri hizo na kuwafanya washindwe kutekeleza miradi kadhaa ya maendeleo waliojipangia.

Mhe. Spika,

Utashangaa kuona kua Taasisi muhimu kama hii ambayo fedha za walala hoi zinakusanywa lakini SMZ imeshindwa kuwapeleka wahasibu wenye uwezo wa kutunza fedha na matokeo yake fedha za walipa kodi zinatumika kiholelea. Kwa nini basi Serikali inashindwa hata kuwapatia taaluma wale watunza fedha wa Halmashauri ambazo ujuzi wao ni mdogo.

Mhe. Spika,

Jambo jengine baya zaidi ambalo nalo ni kikwazo kikubwa cha ufanisi katika Mabaraza ya Miji na Halmashauri za Wilaya ni ukosefu wa uongozi bora. Kimsingi Waziri amepewa uwezo wa kuteua Makatibu wa Halmashauri wenye Elimu ya kutosha na uwezo wa kisheria na uendeshaji ili waweze kusimamia vyema shughuli za ukusanyaji wa mapato, lakini ni bahati  mbaya sana nakuta katika baadhi ya Halmashauri  watendaji hawana sifa zilizotakiwa na badala yake wamechaguliwa wakereketwa wa CCM ili waweze kutimiza matakwa yao ya kisiasa.

Matokeo yake sasa imekua ni vurugu tupu, hakuna ushirikiano wa kutosha kati ya watendaji hawa na wastahiki madiwani kwa mujibu wa sheria za Halmashauri  na Mabaraza ya Miji maamuzi yote muhimu hufanywa na vikao ambavyo madiwani  ndio waamuzi wakubwa wa mambo yote muhimu katika vikao hivyo, lakini inasikitisha kuona kwamba maamuzi mengi yanayoamuliwa na madiwani watendaji hawa huyapuuza kabisa na huwa hawayafanyii kazi na badala yake hufanya maamuzi yao wenyewe kinyume na utaratibu: Utashangaa kuona kuwa hata bajeti inayopitishwa na madiwani: watendaji hawa hukaa pembeni wakafanya yao au mara nyengine unaweza kuona matumizi yanafanywa na Katibu wa Halmashauri pasi na idhini ya kikao halali na hii ni dalili kubwa ya ufisadi unaofanywa na watendaji hawa.

Na haya yanajitokeza zaidi katika baadhi ya Halmashauri za Pemba ambako waheshimiwa madiwani wote wanatoka katika chama cha Upinzani labda hilo ni agizo maalum la serikali kwa watendaji hawa, jee katika hali ya utengano kama hiyo jamii itarajie matokeo gani. Ni dhahiri kwamba pahali pasipo kuwa na ushirikiano na kuthaminiana hapawezi kuwa na ufanisi wowote.

Mhe. Spika,

Nachukua fursa hii kumshauri waziri kwamba kwa manufaa ya jami yetu ambayo ndio inayochangia serikali kupitia kodi zao, afanye ziara ya makusudi ya kutembelea Mabaraza ya Miji na Halmashauri za Wilaya zote za Zanzibar na kuonana na  waheshimiwa madiwani ili apate kujionea mwenyewe matatizo  yaliyomo katika   Serikali za Mitaa na hatimae achukue hatua za kurekebisha.

Mhe.Spika,

Jambo jengine ambalo limekua na kasoro kubwa katika serikali za mitaa na ambalo mimi kama Waziri Kivuli wa Wizara hii pamoja na Waheshimiwa Wawakilishi wa pande zote mbili tumekuwa tukiliona kuwa ni kero na kulipigia makelele sana ni jambo zima la maslahi ya Waheshimiwa  Madiwani wetu.

Kimsingi madiwani ndio wachanjagizi wakubwa wa kukusanya kodi katika Halmashauri za Wilaya na Mabaraza ya miji katika kutekeleza wajibu wao huo wastahiki madiwani hulazimika kutoka maofisini mwao na kutembelea maeneo mbali mbali katika Halmashauri zao na mabaraza yao a miji ili kufuatilia mapato katika vianzio tafauti. Wastahiki madiwani hulazimika pia kuwatembelea wananchi na kuona kero zao na kujaribu kuziandalia utaratibu wa kuzishughulikia.

Mhe. Spika,

Jambo la kusikitisha na kutia huruma ni kwamba wastahiki Madiwani wanazifanya kazi zao hizo katika mazingira magumu sana, bila ya hata baskeli wala usafiri wowote, na bila ya posho  lolote. Baya zaidi ni kwamba pamoja  na juhudi za Waheshimiwa  Wawakilishi  kuishauri  Serikali mara kwa mara, lakini mpaka leo serikali bado haijalipa umuhimu suala la kuwalipa Waheshimiwa Madiwani mishahara ; jambo ambalo linazidi kuwadhalilisha na kuwafanya washindwe kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Mhe. Spika,

Inasikitisha kuona kwamba Madiwani ambao wanafanyakazi kwa kuuma meno katika kuikusanyia jamii mapato, na ambao wamechaguliwa na wananchi kama ambavyo wamechaguliwa Waheshimiwa Wawakilishi lakini wao hawalipwi mishahara, lakini masheha ambao hawana ‘mandate’  ya wananchi lakini wao wanalipwa mishahara.

HITIMISHO

Mhe. Spika,

Mwisho napenda kuchukua fursa hii, kuwashukuru Waheshimiwa Wajumbe wako wote kwa kunisikiliza. Na mwisho kabisa nikushukuru tena wewe binafsi kwa kunivumilia hadi nikamaliza kutoa maoni haya ya Kambi ya Upinzani mbele ya Baraza lako.

Mhe. Spika

Naomba kuwasilisha.

Advertisements

One thought on “CUF yainyooshea kidole SMZ kutumia vikosi vyake kisiasa

 1. nakuunga mkono katika jitihada zako za kuwakosowa hawa wana ccm ili waweze kuona jinsi wanavyo kosea, badae tutalia sote sio wapemba pekeao watakao lia bali ni sote tu

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s