CCM imechoka, imechoka, imechoka

Prof. Ibrahim Lipumba akizungumza katika Kongamano la Diamond Jubilee, Agosti 28, 2008

Prof. Ibrahim Lipumba akizungumza katika Kongamano la Diamond Jubilee, Agosti 28, 2008

Wakati nchi ikitumbukia katika majanga makubwa ya kitaifa kama vile migomo ya wafanyakazi, migogoro ya wanafunzi, mfumko wa bei, nyufa katika Muungano, uchumi dhaifu, ufisadi mkubwa, mgawanyiko mkubwa na kushindwa kwa Rais Jakaya Kikwete kuutatua mpasuko wa Zanzibar, Chama cha Wananchi (CUF) kinaona kwamba kuna haja ya lazima sasa kuliziba ombwe hili la kiuongozi. Hii hapa ni hotuba ya Mwenyekiti wa Taifa wa CUF, Mhe. Prof. Ibrahim Lipumba, katika Kongamano Maalum la Kujadili Ukosefu wa Uongozi na Hatima ya Tanzania, Ukumbi Wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam, tarehe 28 Agosti, 2008

UTANGULIZI

Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia kuwa wazima na kuweza kukutana leo hii. Naamini ataendelea kutupa baraka na mwongozo wake ili tuweze kuutekeleza wajibu wetu kama viongozi, ambao ni watumishi wa Watanzania, kuweza kuwapa uongozi thabiti wenye hekima na busara na utakaoiepusha nchi yetu na shari ambayo watawala waliopo madarakani hivi sasa wanaonekana kuiandaa. Nawashukuru nyinyi kwa kukubali mwaliko wetu kuja kunisikiliza. Najua mmeacha shughuli zenu muhimu kuja kunisikiliza, na kwa hilo nasema Ahsanteni sana.

Madhumuni ya mkutano huu ni kuanzisha mchakato wa kubadilishana mawazo kuhusu hatima ya nchi yetu na umuhimu wa kuwa na uadilifu katika uongozi utakaoonyesha dira itakayoiwezesha nchi yetu kustawi kwa kujenga misingi imara ya demokrasia itakayohakikisha kuna haki kwa wananchi wote na kujenga uchumi endelevu unaokua na kuwaletea neema Watanzania wote. Hivi sasa nchi yetu ina ukosefu wa uadilifu katika uongozi na badala yake tunaongozwa na usanii wa kisiasa uliokithiri unaohalalisha ufisadi mkubwa na kuwakatisha tamaa wananchi wa kawaida.

UKOSEFU WA UONGOZI

Wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa 2005, Chama Cha Mapinduzi (CCM) na mgombea wake wa Urais waliahidi kuwa ikiwa watachaguliwa na kuunda Serikali ya Awamu ya Nne watahakikisha kutakuwa na Maisha bora kwa kila Mtanzania. Mimi niliwatahadharisha Watanzania kuwa mgombea wa CCM hana uwezo wa uongozi na dira ya maendeleo itakayowahamasisha na kuwawezesha Watanzania wawe wabunifu na kujenga uchumi wenye manufaa kwa wananchi wote. Nilimueleza mgombea wa CCM kuwa mtu wa mzaha mzaha na ikiwa nitachaguliwa kuwa Rais basi naweza kumteua aongoze Wizara ya Utamaduni na Michezo. Wengi walidhani kuwa haya ni maneno ya utani ya Mnyamwezi dhidi ya Mzaramo. Sikuwa natania. Nilieleza kuwa taifa letu linakabiliwa na ongezeko la rushwa na ufisadi kwa ari mpya, nguvu mpya na kasi mpya. Sikuwa natania. Hali halisi ya mwananchi wa kawaida inaonyesha wazi kuwa badala ya maisha bora kwa kila Mtanzania kuna maisha magumu kwa kila Mtanzania wa kawaida.

Katika hotuba aliyoitoa Bungeni wiki iliopita, tarehe 21 Agosti 2008, Rais Jakaya Kikwete ameeleza kuwa mambo ni mazuri, uchumi unakua, ajira zinaongezeka na ahadi alizozitoa kwa Watanzania amezitekeleza na anaendelea kuzitekekeza. Suala la kujiuliza mwaka huu wa tatu tangu Rais Kikwete kuingia madarakani ni kama kweli kuna maisha bora kwa kila Mtanzania au hata matumaini ya kuelekea huko?

Wananchi mnaelewa fika hali ngumu ya maisha na kutopatikana kwa ajira. Desemba 2005, wakati Rais Kikwete anaingia madarakani, kwa wakazi wa Dar es Salaam, bei ya kilo ya unga wa sembe ilikuwa shilingi 250/- hivi sasa ni shilingi 750/-; bei ya kilo ya mchele ilikuwa shilingi 500/- hivi sasa ni shilingi 1300/-; bei ya kilo ya maharage ilikuwa shilingi 400/- hivi sasa ni shilingi 1200/-; bei ya kilo ya sukari ilikuwa shilingi 600/- hivi sasa ni shilingi 1200/. Mafuta ya kula, ndoo ya lita 20 ilikuwa shilingi 10,500/- hivi sasa ni shilingi 43,000/-. Nazi moja ilikuwa shilingi 100/- hivi sasa ni shilingi 350/-. Gunia moja la mkaa lilikuwa shilingi 3,500/- hivi sasa ni shilingi 22,000/-. Nyama, kuku na samaki havishikiki. Hata dagaa wamekuwa kitoweo cha anasa ambapo kilo moja sasa inauzwa shilingi 8,000/- ukilinganisha na shilingi 3,000/- wakati Rais Kikwete anaingia madarakani mwezi Desemba, 2005. Wananchi wa Kanda ya Ziwa wanaambulia kula mapanki – mifupa ya samaki iliyobakia baada ya minofu ya samaki kukatwa na kusafirishwa Ulaya. Hata mapanki yamepanda bei! Haya ndiyo matokeo ya uongozi wa Rais Kikwete wa kuleta Maisha bora kwa kila Mtanzania. Alau angetupa pole Watanzania kwa maisha magumu; badala yake anatukejeli na kutueleza mambo ni mazuri, uchumi unakua, na ajira zinaongezeka.

Athari ya kupanda sana bei ya vyakula ni mbaya zaidi kwa kina mama wajawazito na watoto wachanga. Mama mjamzito akikosa lishe bora atajifungua mtoto mwenye utapiamlo na asiye na afya njema. Watoto wachanga wasipokuwa na lishe bora wanaathirika sana katika maisha yao yote ya baadaye kwa sababu hawajengi vizuri miili yao, kinga ya mwili na ubongo. Mtoto mchanga asiyepata lishe bora na virutubisho vya mwili hukua akiwa na uwezo mdogo wa kujifunza na kufundishika. Ni ukatili mkubwa kwa watoto kwa jamii kushindwa kuweka utaratibu wa kuhakikisha kuwa kina mama wajawazito na watoto wachanga wanapata lishe bora. Kwa kuzingatia umuhimu wa lishe bora kwa watoto, kwa maendeleo yao ya baadaye, niliwaahidi Watanzania nikipewa uongozi wa nchi nitahakikisha kwa kushirikiana na wazazi, mashirika ya dini, taasisi zisizokuwa za kiserikali na taasisi za kimataifa tunaweka utaratibu wa kutoa lishe bora kwa kina mama wajawazito wasiokuwa na uwezo na watoto wao wachanga katika vituo vya afya na vituo vya kulelea watoto. Vile vile tulieleza kuwa serikali inayoongozwa na CUF itahakikisha kuwa kila mtoto wa shule anapata alau mlo mmoja akiwa shuleni. Rais Kikwete ana uwezo wa kuyatekeleza haya. Ukosefu wa Uongozi unawanyima watoto wa maskini msingi muhimu wa kijinasua toka dimbwi la umaskini.

Upatikanaji wa huduma za afya unaendelea kuwa kitendawili kwa Watanzania wengi. Wananchi walihuzunishwa sana na kifo cha mama mjamzito aliyenyimwa huduma za kujifungua katika hospitali ya Mwananyamala kwa kutokuwa na vifaa vya kujifungulia wala fedha za kuvinunulia. Kina mama wajawazito wanaojifungua katika hali ngumu na bila msaada wa mkunga aliyehitimu ni wengi mno. Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa vifo vya kina mama wajawazito. Ukosefu wa uongozi umesababisha kushindwa kutumia elimu na utaalamu unaoeleweka kuhakisha kina mama wa Tanzania wanapata huduma bora za kujifungua. Kina mama wengi wanaojifungua katika hospitali na zahanati za serikali, huduma ni mbovu, kejeli na matusi ni mengi. Watanzania wenzangu, serikali isiyomjali na kumheshimu mama mjamzito, haiwezi kumheshimu na kumjali raia wa kawaida kwani sisi sote tumezaliwa na kina mama.

Maradhi kama vile malaria, safura na maradhi mengine ya minyoo, kipindupindu na kichocho yanaweza kuzuwiwa na wanaougua kutibiwa. Tunahitaji kuwa na mtandao mzuri wa zahanati na vituo vya afya na upatikanaji wa madawa ya uhakika ya kutibu maradhi haya.

UADILIFU KATIKA UONGOZI

Kuzungumzia uongozi na uadilifu katika siasa si jambo jepesi. Hisia na mitazamo ya watu wa kawaida kuhusiana na ‘siasa’ imekuwa ya kuihusisha fani hiyo na tamaa, ubinafsi, uroho, unafiki, ulaghai, upotovu, uovu, fitina, hiyana, na hata hujuma. Tena si watu wa kawaida tu bali hata baadhi ya wasomi wetu wanaonekana kuiona hivyo. Kwa wananchi wetu wa kawaida mtu akisifiwa kuwa huyo kwa siasa humuwezi, maana yake ni gwiji wa uongo na laghai. Hali hiyo kwa kiasi kikubwa imesababishwa na ubabaishaji wa uongozi wa kisiasa tuliokuwa nao na tunaoendelea kuwa nao.

Katika nchi masikini kama Tanzania, uongozi wa kisiasa ni muhimu katika kujenga na kuimarisha umoja wa kitaifa, kukuza na kupanua demokrasia na kuhakikisha kuwa nchi inaendeshwa kwa misingi ya utawala wa sheria, ambapo haki inatendeka na inaonekana inatendeka. Utawala wa sheria na haki sawa kwa wananchi wote ndio msingi imara wa amani na utulivu. Changamoto kubwa ya nchi yetu ni kujenga uchumi unaokua na kuneemesha wananchi wote.

Tanzania inakabiliwa na changamoto mbili kubwa kujenga uchumi wenye manufaa kwa wananchi wote na kujenga demokrasia ya kweli itakayohakikisha nchi inaendeshwa kwa kufuata sheria zinazotoa haki sawa kwa wananchi wote. Nchi yetu inahitaji uongozi ambao unaona siasa ni utumishi wa dhati na uliotukuka kwa umma uliozindukana na siyo nyenzo ya kukimbilia na kupigania vyeo, fursa na nguvu ya ushawishi kwa malengo ya kujilimbikizia uwezo wa maamuzi na wa utajiri binafsi usiohojiwa. Ndiyo maana ni muhimu kwa kiongozi yeyote makini kuzingatia misingi ifuatayo:

Kiongozi anaongoza, haongozwi

Kwa kuzingatia matatizo ya nchi yetu na changamoto zinazotukabili, nchi inahitaji kiongozi muadilifu. Kiongozi anapaswa kuonyesha njia baada ya kusikiliza ushauri wa wataalamu na wananchi wa kawaida na kutafakari. Ni muhimu kuzingatia kuwa kiongozi muadilifu hakubali kufuata upepo wa maoni ya jamii tu ambayo huyumba kulingana na wakati na mara nyingi hayazingatii maslahi ya muda mrefu. Kiongozi anayesikiliza mdundo na kisha kufanya maamuzi yake kulingana na ‘mdundo’ unavyokwenda huwa amekimbia dhamana kuu ya uongozi na huishia kuyumba na kuiyumbisha jamii anayoiongoza. Kusema hivi hakuna maana ya kiongozi kuwa dikteta na kutosikiliza maoni ya anaowaongoza. Hapana! Maoni na ushauri ni muhimu, lakini hayo hayaondoshi dhamana ya kiongozi kutumia kipaji, kipawa, taarifa na busara za uongozi kufanya maamuzi na kuyasimamia.

Uwezo na madaraka huambatana na dhamana. Hivyo, dhana ya kiongozi kuongoza badala ya kuongozwa inaambatana pia na dhamana ya kuhakikisha na kujiridhisha kuwa mara zote maamuzi anayoyatoa na kuyasimamia yamefanywa kwa maslahi ya nchi na watu wake. Kiongozi makini huepuka kufanya maamuzi kwa kukurupuka.

Ni wajibu muhimu wa uadilifu wa uongozi katika siasa kuwa kila maamuzi yanayofanywa yawe yametokana na kujiridhisha kwa kiongozi huyo kuwa yanawakilisha maslahi bora zaidi kwa anaowaongoza. Yanaweza kuwa na athari za muda mfupi na mara nyingine kuwa na machungu lakini alimradi tu machungu hayo ni ya muda mfupi, uadilifu wa uongozi unadai kiongozi kutoyumba wala kutetereka katika kuyatetea.

Kiongozi anatakiwa awe mfano kwa anaowaongoza

Kiongozi anapaswa kuwa mfano bora kwa anaowaongoza kwa kuwa na uhalali wa mamlaka, ‘moral authority’, ambayo huja kwa yeye mwenyewe kuyafuata na kuonekana anayafuata yale anayoyadai kutoka kwa anaowaongoza. Kwa maneno mengine, kiongozi anatakiwa atembee juu ya maneno yake. Kwa mfano, huwezi ukawataka raia wafuate sheria wakati wewe mwenyewe unaongoza kwa kuvunja sheria, huwezi kuwataka raia wasijiingizie katika rushwa wakati wewe unakula na kunywa, unalala na kuamka na rushwa. Huwezi kuwaambia raia wapambane wakati wewe unakimbia vita. Kiongozi muadilifu na mtu muungwana anapaswa kuona aibu iwapo vitendo vyake havilingani na kauli zake.

Kiongozi anapaswa azingatie haki na uadilifu kwa anaowaongoza

Msingi wa uongozi ni uadilifu. Kiongozi anapaswa kusimamia haki na uadilifu kwa wote anaowaongoza bila ya upendeleo wala chuki. Haki na uadilifu huu uonekane katika usawa mbele ya sheria, kufaidi fursa za nchi kwa usawa, na kuwepo kwa urari wa maendeleo kati ya sehemu zote za nchi. Isitokee sehemu ya jamii au nchi ikahisi inatengwa, kudharauliwa, kubaguliwa, kunyanyaswa au kukandamizwa. Watu wote wajione wana haki na fursa sawa. Waongozwa wakiona hayo na kuridhika, utiifu wao kwa viongozi huwa hauna shaka, na hutokana na hiyari ya kweli. Na kama wasemavyo wahenga, hiyari yashinda utumwa.

Kiongozi azingatie umoja wa anaowaongoza

Kiongozi muadilifu mara zote atahakikisha kunakuwepo umoja miongoni mwa anaowaongoza kwani huwa anauhitaji umoja huo katika kuhamasisha maendeleo ya nchi na watu wake. Kiongozi muadilifu hawagawi anaowaongoza kwa kuunda makundi na kisha kupendelea waliomo katika mtandao wake na kuwabagua wengine. Kwa hakika umoja wa Taifa analoliongoza ni fahari ya kiongozi muadilifu. Kiongozi anayewagawa watu ni muovu, huwa hawaamini anaowaongoza na huwaogopa. Ili kujihami yeye na madaraka aliyo nayo, kiongozi muovu huishia kuwagawa watu wake kwa kupandikiza chuki na fitina. Isitoshe, mara nyingi misingi ya umoja katika nchi humong’onyoka ikiwa ni matokeo ya kiongozi kushindwa kusimamia haki na uadilifu.

Kiongozi azingatie amani na utulivu katika nchi

Kama ilivyo kwa umoja wa kitaifa, kiongozi muadilifu pia hufanya kila bidii kuhakikisha amani na utulivu wa kweli katika nchi vinapatikana. Amani na utulivu ni chachu ya wananchi kwa kushirikiana na Serikali yao kujiletea maendeleo. Maendeleo hayaji mahala penye ugomvi na uhasama. Lakini na amani na utulivu pia haviji mahala pasipo na haki na uadilifu. Uvunjifu wa amani na utulivu wa nchi hupelekea hasara ya maisha na mali ya watu na hayo hayawi malengo ya uongozi muadilifu katika nchi

Kiongozi asikubali kuona ukandamizaji wa aina yoyote

Haki, uadilifu, umoja, amani na utulivu – yanapatikana pale ambapo hakuna ukandamizaji wa aina yoyote dhidi ya raia. Uadilifu wa uongozi katika siasa unadai kiongozi kuchukua hatua za makusudi, za dharura na za haraka kuondosha ukandamizaji wa aina yoyote ile iwapo utathibitika au hata kudhaniwa tu. Siasa ni mchezo wa dhana au hisia, kwa hivyo haki inapaswa sio tu itendeke bali ionekane kuwa inatendeka ili kuodosha uwezekano, hata kama ni mdogo kiasi gani, wa kuhisiwa kuwepo na ukandamizaji dhidi ya wengine.

Kiongozi awe muumini wa kweli wa demokrasia

Jamii siku zote haiachi kuwa na mgongano wa fikra, na mgongano huu ni muhimu na unahitajika katika kuipeleka jamii hiyo mbele. Fikra zinapogongana na kushindanishwa hupelekea hoja madhubuti kuibuka na hivyo maamuzi kufikiwa kwa kuzingatia nguvu ya hoja na fikra bora. Uadilifu wa uongozi unadai kuheshimu nguvu ya hoja na fikra bora na hayo yanaweza kupatikana tu iwapo nchi inaongozwa kwa misingi ya kidemokrasia. Hivyo, katika kutoa uongozi sahihi, kwa kuzingatia maslahi bora ya nchi na watu wake, haki, uadilifu, umoja, amani na utulivu, hapana budi kwa kiongozi kuiamini, kuiheshimu na kuifuata barabara misingi ya kidemokrasia.

Kiongozi anapaswa kuwajibika kwa yanayotendwa kwa jina lake

Binadamu si mkamilifu na kwa vyovyote vile hufikia pahala akafanya maamuzi ambayo si sahihi hata kama yalifanywa kwa nia njema na kwa kuzingatia taarifa zilizopatikana wakati maamuzi hayo yanafanywa. Hayo yanaeleweka na kiongozi muadilifu anapaswa kuyakubali. Hata hivyo, inapotokezea maamuzi yanayofanywa na dola au taasisi yoyote yakaleta madhara au yakasababisha kuchafua jina jema la wadhifa ambao kiongozi wa kisiasa anaushikilia, basi uadilifu wa uongozi unamtaka yule aliyesababisha hayo au ambaye maamuzi yanayohusika yalifanywa kwa jina lake awajibike. Hiki ndiyo kilele na kigezo kikuu cha uadilifu wa uongozi katika siasa – kukubali kubeba dhamana kwa madhara yaliyotokana na maamuzi yako au yaliyofanywa kwa jina lako.

Kiongozi awapende anaowaongoza

Ni wazi kwamba dhima anazotwishwa nazo kiongozi wa siasa ni kubwa na zinahitaji uimara wa nafsi katika kuzisimamia. Yote yanayofanywa hufanywa kwa jina la watu. Mara nyingine kiongozi hulazimika kufanya maamuzi yasiyopendeza kwa watu wake kwa wakati fulani lakini akayashikilia kwa kujiridhisha kuwa yana maslahi na anaowaongoza. Uamuzi kama huo huwa si mwepesi. Hapo basi, kipimo kikubwa ni mapenzi ya kiongozi kwa anaowaongoza. Uadilifu unataka kiongozi awe na mapenzi, imani na huruma kwa anaowaongoza. Uadilifu pia unamtaka kiongozi awape nafasi wananchi wake wafanye yale wanayoyapenda alimradi yana maslahi nao na hayaathiri maslahi ya jamii.

Kiongozi aheshimu misingi ya uongozi wa pamoja

Uongozi ni dhamana. Maamuzi makubwa yanapofanywa kwa jina la watu yanatakiwa yazingatie maslahi yao. Serikali au chama cha siasa huchangiwa nguvu zake kwa ridhaa inayotolewa na raia au wanachama. Wao huchagua viongozi wakuu na pia huchagua wawakilishi wao katika vyombo vinavyofanya maamuzi yanayowahusu. Baadhi ya wawakilishi hao hupewa dhamana ya kusaidiana na kiongozi mkuu katika uongozi na uendeshaji wa Serikali au chama cha siasa. Katika utaratibu huo, maamuzi hufanywa kwa pamoja. Kiongozi muadilifu siyo tu anapaswa kulifahamu hilo bali pia anatakiwa aheshimu misingi ya uongozi wa pamoja. Anaweza kutofautiana na wenzake katika kufikia maamuzi, lakini alimradi mwisho wa hoja zote maamuzi yamefanywa kwa taratibu za kidemokrasia, anapaswa aheshimu maamuzi hayo na akubali misingi ya uongozi na uwajibikaji wa pamoja.

Kiongozi awe na busara na hekima

Maamuzi ya mtu binafsi mara nyingi humuathiri yeye binafsi au labda na watu wachache waliomzunguka. Maamuzi ya kiongozi wa kisiasa huathiri taifa zima. Changamoto za uongozi hapa zinahitaji utulivu katika kufikia maamuzi na kuyasimamia. Jazba na hamasa mara nyingi hupelekea maamuzi ya pupa, yasiyozingatia hali halisi ya mambo na mara nyingi yenye manufaa (kama yatapatikana) ya muda mfupi tu. Kinyume chake, busara na hekima huzaa maamuzi yanayotokana na tafakuri ya kina, yanayozingatia hali halisi ya mambo na maslahi na manufaa ya muda mrefu. Kiongozi muadilifu anatakiwa ayaone haya na ayazigatie kwa kila hatua anayochukua.

Kiongozi awe anaijua jamii yake vilivyo

Kiongozi mzuri ni yule anayeielewa vyema jamii yake na ambaye ameisoma na kuijua vilivyo nguvu halisi ya jamii hiyo. Kiongozi kama huyo hachukuliwi na jazba za wananchi kiasi cha kutoona udhaifu wao lakini pia hapuuzi dhamira zao kiasi cha kutoona nguvu waliyo nayo. Akifika hapo, hatokwenda mbele wakati wananchi hawako naye wala hatobaki nyuma wakati wananchi wameshatangulia mbele. Kiongozi anapaswa kuwa kiongozi anayekwenda sambamba na wananchi wake kwa kujua nguvu na udhaifu wao. Uadilifu wa uongozi hauwezi kufikiwa bila ya kulitambua hilo. Kiongozi anaonyesha njia. Uwezo wa jamii au nchi unaweza kuwa mkubwa lakini hauonekana kwa sababu ya uongozi dhaifu. Kuielewa jamii ni pamoja na kuelewa “uwezo uliojificha” (potential) wa jamii yako.

Katika nchi inayokabiliwa na dimbwi la umaskini na inataka kujenga demokrasia ya kweli, uadilifu ndiyo unapaswa kuwa msingi wa siasa, msingi wa maongozi ya kisiasa. Ikiwa siasa haiwezi kuwa na uadilifu basi itakuwa imepoteza uhalali wake wa kuwa ni njia ya kuwatumikia watu. Nchi itabakia katika dimbwi la umaskini. Dhulma, rushwa na ufisadi vitatawala. Utumishi wa umma ni utumishi uliotukuka na unapaswa ubakie hivyo. Na msingi wake ni uadilifu.

Iko mifano mingi duniani ya nchi ambazo zilikuwa maskini lakini sasa zimepiga hatua kubwa za maendeleo kutokana na kuwa na uongozi muadilifu unaozingatia pamoja na mambo mengine, vigezo nilivyojaribu kuviorodhesha hapo juu. Mifano ya karibuni katika historia ni nchi za Mashariki ya Mbali kama vile Malaysia, Singapore na Thailand na pia nchi za Botswana na Mauritius katika bara hili la Afrika. Sisemi kwamba nchi hizo zina uongozi muadilifu uliotimia lakini kule kuzingatia kwao baadhi tu ya misingi muhimu niliyoitaja kumezifanya kupiga hatua kubwa za maendeleo kwa watu wake.

UKOSEFU WA UADILIFU WA UONGOZI KATIKA AWAMU YA NNE

Ukosefu wa dira na uongozi makini wa Rais Kikwete ulidhihirika katika hatua yake ya mwanzo ya kuunda Serikali. Lengo la kuitafuna nchi lilidhihirika wakati Rais alipoteua Baraza la Mawaziri kubwa kuliko yote yaliyopata kutokea katika nchi yetu. Rais aliteua Mawaziri 30 na Manaibu Waziri 31, utadhani nchi imetoka kwenye vita vya ndani na kwa hiyo inalazimika kuwapa nafasi ya uongozi kila kikundi chenye silaha ili vita vya ndani vimalizike.

Muundo wa Wizara ulionyesha wazi hakukuwa na uchambuzi wa malengo ya serikali na kuzingatia umuhimu wa kutumia fedha za umma katika maeneo yatakayotuletea tija na kuwaneemesha wananchi wa kawaida. Malengo ya Rais ilikuwa kuhakikisha kuwa wanamtandao wengi inavyowezekana wanapewa nafasi katika Baraza. Wanamtandao wengine ambao ni wabunge wameteuliwa kuwa Wakuu wa Mikoa mbali na majimbo wanayowakilisha Bungeni. Mkuu wa Mkoa ndiyo muwakilishi wa Rais na msimamizi wa utekelezaji wa shughuli za kiserikali katika mkoa anauongoza. Mkuu wa Mkoa ambaye ni Mbunge anawajibika kuhudhuria vikao vyote vya Bunge na kukutana na wananchi katika jimbo lake la uchaguzi. Kiutendaji mbunge wa kuchaguliwa hana muda wa kutosha wa kuwa mbunge madhubuti na Mkuu wa Mkoa. Katika kipindi cha miaka miwili na nusu cha uongozi wa Rais Kikwete, Baraza la Mawaziri limebadilishwa mara nne.

Kuna Mawaziri ambao katika kipindi hiki kifupi hivi sasa wanaongoza Wizara yao ya tatu au ya nne. Mathalan Dk. Shukuru Kawambwa, ambaye kitaalauma ni Injinia, alianza na Wizara ya Maendeleo ya Mifugo Januari 2006, akahamishiwa Wizara ya Maji, Oktoba 2006. Februari 2008 alihamishiwa Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia. Mwezi wa Mei 2008 akahamishiwa Wizara ya Miundombinu. Hiyo ilikuwa ni Wizara yake ya nne katika kipindi cha miaka miwili na nusu. Profesa Jumanne Maghembe ambaye ni mtaalamu wa mambo ya misitu alianza na Wizara ya Kazi na Vijana, akahamishiwa Wizara ya Maliasili na Utalii na sasa yuko Wizara ya Elimu na Mafunzo.

Waziri ndiye kiongozi wa kisiasa na msimaizi wa utekelezaji wa sera za serikali katika Wizara. Sheria zetu nyingi zinampa Waziri madaraka makubwa ya maamuzi. Waziri anapoteuliwa anachukua muda kujifunza majukumu yake katika Wizara anayoiongoza. Kubadilisha badilisha Mawaziri kila wakati kunaathiri utendaji wa Serikali. Mtazamo wa Rais Kikwete ni kuwa hakuna mtu anayesomea Uwaziri na kwa hiyo mtu yeyote anaweza kuwa Waziri Wizara yoyote.

Mama Sophia Simba aliteuliwa kuwa Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Watoto. Baada ya kusumbuliwa na maradhi, Rais Kikwete ameona kuwa sasa yuko imara kuongoza mapambano dhidi ya rushwa na ameteuliwa kuwa Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais anayeshughulilki Utawala Bora.

Udhaifu wa Uongozi na Kusimamia Utekelezaji

Katika uongozi wake Rais Kikwete anaonyesha umahiri wa kuzungumza na kueleza matatizo. Lakini hafuatilii utekelezaji wa ahadi anazotoa kwa wananchi. Udhaifu huu umejitokeza wazi katika maamuzi ya serikali kuhusu tatizo la upungufu wa umeme.

Mwezi Februari 2006 Rais alieleza kwa kina tatizo la ukame uliosababisha uzalishaji wa umeme kwa nguvu za maji kupungua sana. Alieleza hatua za dharura zinazochukuliwa kukodisha mitambo ya kuzalisha umeme. Pia alieleza hatua za muda wa Kati. Tuliomsikiliza Rais Februari 2006 alitupa matumaini kuwa Rais analifuatilia kwa karibu tatizo la umeme nchini. Kamati Teule ya Bunge ya kuchunguza kampuni ya Richmond imeeleza kwamba mnamo Desemba 2005, Shirika la Ugavi wa Umeme la Tanzania, TANESCO, liliiomba serikali iliruhusu kukodi kwa dharura, kwa miezi 12, mitambo ya kufua umeme kwa kutumia gesi. Serikali iliridhia maombi hayo na TANESCO wakaanza mazungumzo na kampuni inayochimba na kufua umeme wa gesi – SONGAS. Mwanzoni mwa mwaka 2006, CDC Globeleq, ambayo ni kampuni mama ya SONGAS ilitoa makadirio ya kufua MW 76 za umeme ambao ungeingizwa katika gridi ya taifa kuanzia Aprili 2006.

Bodi ya Wakurungezi ya TANESCO iliyakubali mapendekezo ya Globeleq ya ama kuwa na mkataba wa miaka mitano wa kufua umeme ambapo kila KWh moja itauzwa kwa senti za kimarekani 3.2 au mkataba wa miaka 3 na kila KWh moja itauzwa kwa senti za kimarekani 5.3. Baada ya kipindi cha mkataba mitambo ya kufua umeme wa gesi itakuwa mali ya TANESCO. Baada ya kuelezwa mapendekezo ya Globeleq, Baraza la Mawaziri chini ya uenyekiti wa Rais Kikwete liliamua kuwa Globeleq waelezwe kuwa ama waiuzie serikali majenereta ya kufua umeme au wayakodishe majenereta hayo kwa kipindi cha upungufu wa umeme. Pia majadiliano zaidi yafanyike kwa lengo la kupunguza bei ya umeme ya Globeleq.

Kinyume na maamuzi ya Baraza la Mawaziri, Siku hiyo hiyo ya kikao cha Baraza la Mawaziri, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini aliwaandikia CDC Globeleq. Badala ya kuwatumia ujumbe sahihi CDC Globeleq kuwa Serikali inataka wapunguze kipindi cha ukodishaji mitambo, washushe zaidi bei yao ya umeme na wawe tayari kuzalisha umeme ifikapo Mei 2006, ilipeleka ujumbe tofauti kabisa kuwa Serikali inafuta mpango wa kukodisha mitambo kutoka kwao na badala yake serikali imeamua kutoa fedha kwa TANESCO waweze kununua mitambo ya kufua umeme. Maamuzi ya Wizara ya Nishati na Madini yanastajabisha hasa ukizingatia kuwa tayari nchi ilikuwa ina matatizo makubwa ya umeme, mgao ulishaanza na wateja wengi wa TAESCO walikosa umeme kwa muda mrefu. Mradi wa shirika maarufu, ambao maandalizi yake yalikuwa yamekamilika na ungeweza kuzalisha umeme wa MW 76 katika kipindi cha miezi mitatu, uliachwa kwa kukiuka maagizo ya Baraza la Mawaziri. Wakati huo, Rais Kikwete alikuwa tayari ameshatueleza kuwa Urais wake hauna ubia.

Ilikuwaje maamuzi ya pamoja ya Baraza la Mawaziri chini ya Uenyekiti wa Rais kukiukwa na bila Rais kuchukua hatua dhidi ya wale waliokiuka maamuzi yake. Tatizo la Richmond kushindwa kuleta mitambo ya kuzalisha umeme wakati tuna tatizo la umeme lilijulikana mapema. Rais hakuingilia kati kuuliza kulikoni? Serikali ilikuwa na fursa ya kuvunja mkataba wa Richmond hasa ukizingatia kuwa mabwawa ya kuzalizisha umeme yalikuwa yamejaa maji kabla Richmond hawajafunga mitambo yao ya kuzalisha umeme, wakati huo tayari wakiwa wameshakiuka masharti ya mkataba.

Taarifa kuwa mkataba wa Richmond ulikuwa na matatizo zilikuwa bayana hata kwa wananchi ambao hawamo serikalini na hawana vyombo vya uchunguzi vya kukusanya taarifa. Ilikuwaje Rais ambaye katika mazungumzo yake na wananchi alionyesha kuwa anafuatilia hata kina cha maji katika mabwawa yanayozalisha umeme, ashindwe kufuatilia utendaji wa Richmond na kuzuia mkataba huo kuhamishiwa Dowans wakati nchi haina mahitaji ya umeme wa dharura? Je, tatizo la Rais ni udhaifu wa ufuatiliaji tu au kuna kitu zaidi kinafichwa katika sakata hili? Dowans ilikuwa inalipwa dola za kimarekani 121,811 (Tsh 152.264 milioni) kila siku kama gharama za kudumu za uwezo wa mitambo yao (capacity charge) bila umeme wowote kuzalishwa.

Mapambano Dhidi ya Rushwa

Ukosefu wa Uongozi unadhihirika katika mapambano dhidi ya ufisadi. Ufisadi ni matumizi ya dhamana na wadhifa uliopewa na umma kwa manufaa yako binafsi. Inajumuisha kudai na kupokea rushwa, matumizi mabaya ya fedha na rasilimali za umma na kuiba fedha za umma. Rushwa ni adui wa haki, na pia ni adui mkubwa wa maendeleo. Rushwa ni saratani (cancer) inayoua uchumi na kuwanyima wananchi haki ya maisha mazuri na maendeleo. Chanzo kikubwa cha rushwa ni ukiritimba wa madaraka, mishahara midogo ya watendaji serikalini, maamuzi yasiyofuata taratibu zinazoeleweka na kutowajibishwa kwa wanaoshiriki katika vitendo vya rushwa. Vita dhidi ya rushwa itafanikiwa ikiwa ukiritimba wa madaraka utaondolewa, maamuzi ya kiserikali yatafuata taratibu zilizo wazi na zinazoeleweka na kuwaadabisha wanaoshiriki katika rushwa.

Mfumo wa rushwa unapunguza uwekezaji wa vitega uchumi ulio makini na kwa hiyo kupunguza ongezeko la ajira na ukuaji wa uchumi. Kwa wawekezaji makini rushwa ni mbaya kuliko kodi kubwa kwa sababu haitabiriki na mtoaji hana uhakika kuwa aliyepokea atatimiza ahadi ya kutoa huduma iliyolipiwa rushwa.

Kukithiri kwa rushwa kunaathiri utumiaji mzuri wa vipaji vya ujasiriamali. Wafanya biashara wenye vipaji vizuri wanatumia uwezo wao kupata utajiri kwa njia rahisi za rushwa badala ya kuwa wavumbuzi wa njia bora za kuongeza uzalishaji, tija na faida katika shughuli halali za kiuchumi. Wafanya biashara wengi wameingia katika siasa kupitia CCM ili kujihami na kutumia vizuri fursa za rushwa kuendelea kujitajirisha.

Rushwa inapunguza uwezo wa misaada kutoka nje kusaidia kukuza uchumi na kupunguza umaskini badala yake inachochea nchi na serikali kuwa tegemezi milele. Kwa sababu ya rushwa mikopo na misaada ya nje haijengi miundombinu imara kama vile barabara, ufuaji na ugavi wa umeme, huduma za maji, afya na elimu. Rushwa inafanya gharama za miradi kuwa kubwa mno.

Rushwa inasababisha nchi iwe na miundombinu na huduma hafifu. Rushwa inahatarisha afya na maisha ya wananchi. Madawa hafifu au yaliyopitwa na wakati yanaingia nchini na kutumiwa na raia. Vifaa vibovu kama vile nyaya za umeme zinaingizwa nchini na kusababisha ajali zinazoweza kuunguza nyumba na kupoteza maisha ya watu. Maghorofa na madaraja yanajengwa bila kuzingatia viwango.

Rushwa inapunguza mapato ya serikali. Wafanya biashara na makampuni yanatumia rushwa kukwepa kodi na kuipunguzia uwezo serikali kutoa huduma muhimu kwa wananchi kama vile elimu na afya.

Rushwa ndani ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa serikali inachangia kuwepo kwa mikataba mibovu katika sekta mbali mbali ikiwemo madini inayoihujumu serikali. Mikataba inaandaliwa kwa makusudi iwe na gharama kubwa kwa serikali kama itaitekeleza na gharama kubwa zaidi ikiwa itaivunja. Upande wa pili ukivunja mkataba haupati gharama kubwa.

Rushwa inaendeleza matumizi mabaya ya fedha za umma. Miradi mikubwa yenye mianya ya rushwa inapendelewa zaidi kuliko matumizi yatakayochochea maendeleo ya watu. Uongozi wa Benki Kuu ulichangamkia sana ujenzi wa minara pacha (twin towers) kwa gharama kubwa bila shaka kwa sababu ya rushwa. Inawezekana kuwa robo ya gharama ya majengo hayo ingeweza kukidhi makao makuu yenye taratibu zote za kiulinzi wa Benki Kuu. Serikali ingeweza kutumia robo tatu iliyobaki kuanzisha kama mtaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo na Benki ya Maendeleo ya Viwanda.

Athari mbaya zaidi ya rushwa ni mmomonyoko wa maadili ndani ya serikali na katika jamii. Kuwepo kwa rushwa miongoni mwa viongozi waandamizi wa serikali kunaathiri uadilifu kwa watendaji wote wa serikali. Kama Mwanasheria Mkuu wa Serikali amejitajirisha kwa rushwa, kwa nini Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya naye asitafute mbinu za kujitajirisha hata kama rushwa hiyo itaongeza gharama za kupambana na Ukimwi. Kama wakubwa wanakula basi wadogo watataka alau walambe. Mwanasheria Mkuu mmoja wa Serikali inasemekana alitoa agizo lisilo rasmi kwa maafisa wake kuwa kila mtu ale kwenye meza yake mwenyewe. Saratani ya rushwa inaathiri mfumo mzima wa serikali.

Serikali ya Rais Kikwete haina nia ya dhati ya kupambana na rushwa kama inavyodhihirishwa na kutoshughulikia mafisadi wakubwa.

Kashfa ya Rada ya BAE

Ofisi ya kuchunguza rushwa kubwa ya Uingereza, Serious Fraud Office (SFO), iligundua kuwa kampuni ya BAE ililipa dola milioni 12 katika akaunti za Uswisi za Bwana Sailesh Vithlani, mfanya biashara, mzaliwa wa Mwanza ambaye hivi sasa ni raia wa Uingereza ambaye alikuwa wakala wa serikali katika ununuzi wa rada hii. Makachero wa SFO waliifahamisha serikali ya Tanzania kuhusu akaunti za Sailesh Vithlani na uhusiano wake na BAE. Makachero hao walimhoji Bwana Vithlani hapa hapa Tanzania mbele ya maafisa wa TAKURU. Hata hivyo, Sailesh Vithlani aliruhusiwa kuondoka nchini bila ya kubughudhiwa, na baada ya kuwa ameondoka ndipo TAKUKURU ikajikakamua kupeleka kesi mahakamani Novemba 2007 na kutoa wito kuwa Sailesh Vithlani anatafutwa. Hakuna afisa yeyote wa serikali aliyeshitakiwa pamoja na Vithlani. Suala la kujiuliza ni kwa nini Vithlani hakukamatwa na kuwekwa ndani kuisaidia TAKUKURU kuwanasa walioshirikiana naye baada ya serikali kupata taarifa ya akaunti zake toka SFO.

Kashfa ya Mhe. Andrew Chenge

Makachero wa taasisi inayoshughulikia ufisadi mkubwa ya Uingereza (SFO) wamegundua kuwa Mhe. Andrew Chenge ana akaunti yenye zaidi ya dola milioni moja katika kisiwa cha Jersey Uingereza. Taarifa hii ambayo ilitolewa kwanza na gazeti la kila siku la ‘The Guardian’ la Uingereza ilithibitisha wazi kuwa kuna mtandao wa wala rushwa katika maafisa wa juu wa serikali. Mhe. Chenge kabla ya kujiuzulu alikuwa Waziri wa Miundombinu, wizara ambayo inahusika na mikataba mikubwa yenye mianya ya rushwa. Kuteuliwa kwa Mhe. Chenge kuwa Waziri wa Miundombinu kulichukuliwa na Watanzania wengi wanaofuatilia kwa karibu mapambano dhidi ya rushwa kuwa Rais Kikwete hana nia thabiti ya kupambana na rushwa kwani Chenge amekuwa anashukiwa kuwa na matumizi yasiyolingana na kipato cha mtumishi wa serikali. Isitoshe akiwa kama Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa muda wa miaka kumi, hakuonyesha kuwa makini katika mapambano dhidi ya rushwa.

Mhe. Chenge hakukanusha kuwa ana akaunti Jersey ya zaidi ya dola milioni moja, bali alieleza kuwa akaunti hiyo ina vijisenti tu. Kauli hii inaweza kutafsirika kwamba ama yeye mwenyewe ana akaunti nyingine zenye “mapesa” ya sawa sawa au anawajua vigogo wengine wenye fedha nyingi zaidi ya hizo katika akaunti za nje. Ni wazi Mhe. Chenge hakuitolea taarifa akaunti hii ya Jersey katika fomu maalum ya kueleza mali alizo nazo ambayo kila Mbunge na viongozi wa juu wa serikali wanatakiwa kuijaza kila mwaka. Mhe. Sophia Simba, Waziri anayeshughulikia masuala ya Utawala bora katika Ofisi ya Rais na ambaye anaweza kuona fomu za mali walizo nazo viongozi, alishtushwa na taarifa katika vyombo vya habari kuwa Mhe. Chenge ana akaunti ya zaidi ya dola milioni moja. Mhe. Simba alinukuliwa akisema kuwa hata kama Chenge angeuza ng’ombe wake wote wa Bariadi hawezi kuwa na fedha nyingi kama hizo. Na kama Rais Kikwete alikuwa na taarifa rasmi kuwa Mhe. Chenge ana fedha hizo na bado akamteua kuwa Waziri, basi asingekuwa na sababu ya kukubali ajiuzulu kwa jambo ambalo analifahamu vizuri.

Ni kosa la jinai kwa mtu kutoeleza ukweli wa mali alizo nazo. Kama serikali ni makini katika kupambana na rushwa, Andrew Chenge hivi sasa alistahili kukabiliwa na mashtaka mazito ya kujipatia utajiri usioelezeka kwa kipato chake halali na kutoeleza ukweli wa mali alizo nazo. Pia kwa kufuatilia malipo yanayoingia na kutoka katika akaunti hii, mafisadi wengine wangeweza kukamatwa. Badala ya kuhojiwa na kufikishwa mahakamani, Mhe. Chenge amepokelewa na viongozi wa CCM wa mikoa ya Mwanza na Shinyanga kama shujaa.

Ufisadi wa Benki Kuu kutumia akaunti ya EPA

Ufisadi wa kutisha na usiokuwa na aibu ni wa Benki Kuu kutumia akaunti ya EPA kulipa makampuni 22 shilingi bilioni 133 kwa kutumia nyaraka za kughushi. Wizi huu wa kusikitisha ambao umeidhalilisha Benki Kuu na kuiondolea uhalali wa kuwa msimamizi wa sekta ya fedha nchini ulifanyika chini ya uongozi na bila shaka ushiriki, wa marehemu Gavana Balali.

Malimbikizo ya malipo ya nje yalianza mwaka 1979 na kuendelea miaka ya themanini kwa sababu ya upungufu mkubwa wa fedha za kigeni. Waagizaji wa bidhaa na huduma za nje walitakiwa, baada ya kupata kibali cha Benki Kuu, kulipa NBC shilingi za Tanzania sawa na thamani ya bidhaa wanazoagiza. NBC walitoa hati ya karadha (Letter of Credit) ambayo ni ahadi kuwa benki hiyo italipa fedha za kigeni pindi bidhaa zilizoagizwa zitapomfikia mteja wake. Kadiri ukosefu wa fedha za kigeni ulivyozidi kuongezeka ndivyo NBC ilivyoshindwa kulipa makampuni yaliyotuletea bidhaa zao kwa kuamini ahadi za hati za karadha za NBC. Waagizaji wa bidhaa walikuwa wamelipa shilingi za Tanzania lakini wauzaji wa bidhaa hizo hawakulipwa fedha za kigeni. Malimbikizo ya malipo ya fedha za kigeni yalizidi kuongezeka.

Izingatiwe kwamba katika kipindi cha miaka 1980, Serikali ilikuwa inapanga thamani ya shilingi ukilinganisha na fedha za kigeni. Bei ya dola ilikuwa ndogo. Kwa mfano mwishoni mwa mwaka 1980, thamani ya dola 1/- ilikuwa shilingi 8.18. Aliyeagiza bidhaa za dola milioni 1/- alilipa NBC shiling milioni 8,180,000/-. Ikiwa NBC hawakumlipa muuza bidhaa za nje dola milioni 1/-, deni hilo lilimbikizwa. Serikali ilipoamua kuwa thamani ya shilingi ipangwe na soko huria la fedha za kigeni, shilingi imeporomoka. Robo ya tatu ya mwaka 2005, dola 1/- ilikuwa sawa na shilingi 1165/- mara 142 ya thamani yake mwaka 1980. Limbikizo la deni la dola milioni 1 lililolipiwa na muagizaji wa bidha za nje shilingi milioni 8.18 sasa deni hilo ni shilingi bilioni 1 na milioni 165.

Mwaka 1985 serikali iliamua kuchukua rasmi jukumu la kulipa malimbikizo ya madeni ya nje na iliagiza madeni yote ambayo yalikuwa katika matawi ya NBC nchi nzima yahamishiwe Benki Kuu ambayo itakuwa wakala wa serikali wa kusimamia madeni haya. Malimbikizo ya madeni ya EPA yakawa madeni ya serikali na siyo ya NBC iliyotoa hati ya karadha kuahidi kuwa italipa fedha za kigeni. Kitengo cha kusimamia madeni ya nje kilianzishwa Benki Kuu. Hata hivyo kwa sababu ya utawala na usimamizi mbovu wa akaunti za NBC ambayo ilikuwa haitumii pragramu za kompyuta katika menejimenti ya akaunti zake, agizo la serikali halikutekelezwa kikamilifu.

Kimsingi akaunti ya EPA ni akaunti yenye madeni ya serikali. Kwa sababu ya kuporomoka kwa shilingi, fedha zilizolipwa na walioagiza bidhaa ni kiasi kidogo sana cha fedha zinazohitajika kununulia fedha za kigeni kuwalipa waliotuuzia bidhaa miaka ya 1980.

Serikali ilijaribu kupunguza madeni ya nje kupitia mchakato wa Klabu ya Paris wa kubadili muda wa kulipa madeni. Kati ya mwaka 1986 na 1994, ilibadilisha muda wa kulipa madeni yake mara nne. Hata hivyo kila ilipobadilisha muda wa kulipa madeni, malimbikizo ya madeni ambayo hayajalipwa yaliongezeka. Mwaka 1994, Benki ya Dunia ilitoa msaada wa programu ya kununua malimbikizo ya madeni ya kibiashara (Debt Buy Back programme). Mpango huu ulikuwa wa kununua deni la nje la dola 1 kwa senti 10 za kimarekani. Mpango huu ulikamilika mwaka 2004. Mshauri mkuu wa mpango huu ilikuwa kampuni ya Lazard Freres ambayo ilitoa taarifa ya kazi yake 2004.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa malimbikizo ya madeni ya nje yaliyobaki ya dola za kimarekani milioni 233 yalikuwa yamepitwa na wakati na kwamba Benki Kuu na Wizara ya Fedha wayafute katika vitabu vyao. Ni muhimu kuzingatia kuwa katika kukamilisha kazi ya kununua malimbikizo ya madeni, Benki Kuu ilitangaza katika vyombo vya habari vya kimataifa kuwa makampuni yanayoidai Tanzania kwa kuiuzia bidhaa yajitokeze na kuwasilisha nyaraka za madai yao. Sehemu kubwa ya malimbikizo ya madeni ya nje yaliyobakia yalikuwa hayana mtu aliyejitokeza na ndio maana Lazard Freres wakashauri yafutwe kwa kuwa yamepitwa na wakati. Benki Kuu iliajiri kampuni ya ukaguzi ya PriceWaterhouseCoopers kukagua taarifa na kazi ya Lazard Freres. PriceWaterhouseCoopers walieleza kuwa wameridhika na kazi iliyofanywa na Lazard Freres ya kulipa malimbikizo ya madeni ya nje na kwa hiyo jukumu hilo limekamilika

Inasikitisha sana, kwamba baada ya kazi ya Lazard Freres na ukaguzi wa PriceWaterhouseCoopers, mwaka 2005 serikali iliibuka na kutoa hati fungati za kununulia malimbikizo ya madeni ya nje. Ni wazi maafisa waandamizi wa Hazina akiwemo Katibu Mkuu na Waziri wa Fedha walijua kinaga ubaga kwamba hakuna sababu ya kulipa malimbikizo ya madeni ya nje. Gavana wa Benki Kuu na maafisa wake waandamizi pia walijua hilo. Ikiwa Wakurugenzi wa Benki walikuwa makini wa kazi yao na siyo wapokeaji wa posho tu, waliwajibika kuelewa kuwa baada ya kazi ya Lazard Freres hakuna sababu ya kulipa malimbikizo ya madeni. Yeyote anayedai alipaswa aende mahakamani.

Ni vigumu kuamini wizi huu ulifanywa bila idhini ya Ikulu.

Uporaji wa fedha za umma bila aibu kwa kutumia akaunti za EPA ulifanywa kwa ushiriki wa Katibu Mkuu Hazina na Gavana wa Benki Kuu. Bila shaka watumishi waandamizi hawa wa umma walipewa maagizo ya mdomo au vijikaratasi visivyo rasmi toka kwa viongozi wao wa kisiasa, Waziri wa Fedha na Rais. Kama Katibu Mkuu Hazina na Gavana wa Benki Kuu wangekuwa watumishi waadilifu wangekataa kutekeleza maagizo haya kwa sababu yanavunja sheria. Lakini kwa kuwa nao walikuwa ndani ya mtandao wa mafisadi na wakiwa na nia ya kulinda nafasi zao Rais wa Awamu ya Nne atakaposhika madaraka, hawakusita kushiriki katika uporaji huu ambao umeivunjia hadhi Benki Kuu ndani na nje ya nchi kwa kuifanya ionekane kuwa ni kichaka cha mafisadi.

Wizi wa fedha za EPA uligunduliwa na Deloitte & Touche, Mkaguzi wa Mahesabu ya Benki Kuu ya mwaka 2005/06. Walipokagua faili la Kagoda Agriculture Limited katika akaunti ya EPA walishtushwa na malipo ya dola 30,732,658.82 walizolipwa. Kati ya tarehe 10 Septemba 2005 na 3 Novemba 2005, Kampuni ya Kagoda ilikuwa imepata mikataba 12 ya makampuni ya nje kuwa wao ndio wamepewa dhamana ya kulipwa madeni ya makampuni hayo. Kipindi cha siku 55 ni kifupi kwa kampuni yoyote ile kuweza kujadili na kufanikisha mikataba 12 ya wadai wa nje walioko nchi mbali mbali za dunia.

Utafiti wa Mkaguzi wa Mahesabu ulionyesha kuwa kampuni ya Kagoda Agriculture Limited ilisajiliwa tarehe 29 Septemba 2005. Hata hivyo ilikuwa na mkataba wa tarehe 10 Septemba wa kulipwa madeni ya nje kabla hata haijasajiliwa rasmi. Wakaguzi wa Deloitte and Touche walistaajabu kuwa Kampuni iliyosajiliwa tarehe 29 Septemba 2005 ililipwa dola millioni 30.8 katika kipindi cha wiki 5 – 6 toka ilipoanzishwa. Hakuna utafiti wowote uliofanywa na Benki Kuu kuichunguza kampuni hii na uhalali wake. Ni vigumu kuamini kampuni changa inaweza kujadili na kufikia makubaliano mpaka kuweka sahihi mikataba 12 na makampuni yanayodai Tanzania toka Ujerumani, Italia, Yugoslavia (ambayo ilisambaratika miaka ya tisini) Uingereza, Ufaransa, Marekani na Japan katika kipindi cha muda mfupi.

Wakaguzi walikuwa na wasiwasi kuwa mikataba hii ni ya kughushi na inawahusisha maofisa wa juu wa Benki Kuu.

Walishauri Gavana kuwa uchunguzi wa kina ufanyike na wafanyakazi wa Benki Kuu waliyohusika na mikataba hii wasimamishwe kazi ili ushahidi wa wizi huu usiharibiwe. Benki ilishauriwa kupata wataalamu wa kuchunguza nyaraka na alama za vidole (Forensic experts) kusaidia katika uchunguzi wa kina.

Baada ya kuandika barua kwa Gavana kumjulisha kuwa ushahidi alionao unaonyesha kuwa yawezekana Benki imelipa dola 30,732,658.32 kwa kupewa nyaraka za mikataba ya madeni iliyoghushiwa, Mkaguzi wa Mahesabu wa Deloitte & Touche alikuja Dar es Salaam na kukutana na Gavana Balali. Gavana aliwaeleza wakaguzi wa mahesabu kwamba Waziri wa Fedha ana taarifa ya malipo haya na yeye ndiye atakayetoa nyaraka za kuthibitisha malipo kwa kampuni ya Kagoda Agriculture Limited.

Wakaguzi walikutana na Waziri katika wiki ya kuanzia tarehe 11 Septemba, 2006 na akawaeleza kuwa malipo haya ya Kagoda Agriculture Limited yalikuwa siri nzito ya kitaifa, kwa hiyo hawataweza kupewa vielelezo vya malipo hayo. Tarehe 14 Septemba Waziri wa Fedha aliwapa Delloite and Touche barua ya kuthibitisha kufahamu kwa malipo hayo kuwa ni ya halali lakini hakutoa vielelezo vyovyote. Bila shaka Waziri wa Fedha wa wakati huo, Mhe. Zakhia Meghji alimueleza Rais utata wa ukaguzi wa fedha.

Wakaguzi walieleza kuwa ni lazima waeleze udhaifu huu katika ripoti yao ya ukaguzi kwani kuna dalili za wazi kuwa wizi wa mamilioni ya dola umefanyika kwa kutumia nyaraka za kughushi. Wakaguzi hawa waligundua malipo hewa kwa kuchambua sehemu kidogo ya akaunti za EPA. Walitaka kufanya ukaguzi zaidi ili kubaini kama kuna malipo mengine ya kughushi katika akaunti za EPA.

Baada ya kutoa taarifa hizi kwa Gavana, mawasiliano yaliyofuata toka kwa Gavana kwenda kwa wakaguzi wa mahesabu yalikuwa ya tarehe 21 Septemba, 2006 alipowajulisha kuwa mkataba wao wa kukagua mahesabu ya Benki Kuu umesitishwa mara moja. Maadili ya kitaalamu na taaluma ya Ukaguzi ni kwamba mkaguzi hapaswi kusimamishwa baada ya kukamilisha ukaguzi na hasa ikiwa amegundua mambo ambayo yamemfanya atoe hitimisho kuwa mahesabu ya taasisi yana walakini. Wakaguzi walieleza kuwa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) wanataka kujua taarifa ya Ukaguzi wao. Wanaamini kuwa kuvunjwa kwa mkataba wao ni kwa sababu ya kugundua wizi kwa kutumia nyaraka za kughushi. Walieleza wazi kuwa watawasiliana na IMF kuwajulisha kusitishwa kwa mkataba wao wa kukagua mahesabu ya Benki Kuu.

Baada ya Mkataba wao kusitishwa wakaguzi waliwaandikia Wakurugenzi wote wa Benki Kuu, kueleza kuwa sababu ya kusitishwa mkataba wao wa kukagua Benki Kuu ni kugundua wizi wa zaidi ya dola milioni 30. Miongoni mwa Wakurugenzi hao ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha ambaye ni Mkurugenzi wa Bodi kwa wadhifa wake. Kwa jambo zito kama hili na kwa utaratibu wa utendaji, bila shaka Katibu Mkuu wa Hazina alimjulisha Katibu Mkuu Kiongozi ambaye alimtaarifu Rais. Kama Rais Kikwete angekuwa na usongo dhidi ya rushwa, angechukua hatua za alau kumsimamisha kazi Gavana wa Benki Kuu ili uchunguzi wa kina ufanyike na angesisitiza Deloitte and Touche wakamilishe ukaguzi wao hata kama ukaguzi huu ungeathiri hali yake ya kisiasa. Hakufanya hivyo, ama kwa udhaifu wake wa kutotaka kuudhi na kuwawajibisha watu anaowafahamu vizuri au kwa sababu ya kujua kuwa fedha zilizoibiwa katika akaunti za EPA zilimnufaisha kisiasa wakati wa uchaguzi mkuu mwaka 2005.

Serikali ilikubali Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu ateue kampuni ya nje ya Ernst & Young kuwa mkaguzi wa akaunti ya EPA baada ya shinikizo za IMF na wahisani wengine. Inasikitisha na kuaibisha kuwa kama serikali isingekuwa tegemezi wa misaada ya nje, ukaguzi maalum wa akaunti ya EPA usingefanyika na ukweli wa wizi huu ungefichwa fichwa tu.

Ukaguzi wa Ernst & Young ulionesha bayana kuwa makampuni 13 yalitumia kumbukumbu, nyaraka na hati zilizo batili na za kughushi na yakalipwa jumla ya shilingi bilioni 90.3. Makampuni mengine 9 yalilipwa jumla ya Sh 42.6 bilioni pasipo kuonyesha nyaraka stahili ya malipo na hivyo kuwafanya wakaguzi washindwe kuhakiki uhalali wa malipo hayo. Hii haina maana kuwa makampuni haya 9 huenda yana haki ya kulipwa. Kama Benki Kuu wangekuwa waadilifu wasingekubali kuyalipa makampuni haya kwa nyaraka zilizowasilishwa Benki Kuu. Kwa hiyo sh 42.6 bilioni zimeibiwa pia kwani makampuni haya hayakuwa na nyaraka stahili za kuifanya Benki Kuu iwalipe fedha hizo.

Baada ya kupokea ripoti ya Mkaguzi wa Mahesabu ya EPA iliyotayarishwa na Ernst & Young, Katibu Mkuu Kiongozi alitoa tamko la serikali lililoeleza kuwa “Mhe. Rais amesikitishwa na kukasirishwa na taarifa ya kuwepo vitendo vya ukiukwaji wa makusudi wa sheria, kanuni na taratibu za uuzaji wa madeni ya nje vilivyofanywa katika taasisi muhimu na nyeti kama vile Benki Kuu. Kwa hiyo, ameamua kuwa hatua za kisheria na kiutawala zichukuliwe dhidi ya makampuni na watu waliohusika na vitendo hivyo viovu.”

Rais alitengua uteuzi wa Dkt. Daudi A. Balali kuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania na akawaagiza; “Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Inspekta Jenerali wa Polisi na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, kuchunguza na kuchukua hatua zipasazo za kisheria kwa makampuni na watu waliohusika na uhalifu huu. Rais amewataka watumie ipasavyo mamlaka na madaraka waliyo nayo kwa mujibu wa sheria. Aidha, amewataka wakamilishe kazi hiyo katika kipindi cha miezi sita. Amemuagiza Mwanasheria Mkuu wa Serikali awe kiongozi wa kazi hii. Amewataka wahakikishe kuwa fedha zilizolipwa isivyo halali zinarudishwa.”

Wakati uteuzi wake unatenguliwa na Rais, Gavana Balali alikuwa yuko Marekani kwa matibabu. Hakuna hatua zozote zinazoeleweka zilizochukuliwa na serikali kumhoji na kupata maelezo yake kuhusu kashfa ya wizi wa mabilioni ya fedha za EPA. Msemaji wa Ikulu alikaririwa na vyombo vya habari akieleza kuwa serikali haimtafuti Dkt. Daudi A. Balali, na ikimtaka itampata kwani serikali ina mkono mrefu. Baada ya kauli hii haikuchukua muda mrefu Watanzania wakaelezwa, kwanza kupitia vyombo vya habari vya makampuni binafsi kuwa Dkt. Balali amefariki dunia. Ni ukosefu wa uadilifu wa uongozi kuwa Dkt. Balali hakuhojiwa kipindi chote hicho wakati wizi uliofanywa na Kagoda Agriculture Limited kupitia akaunti ya EPA ulifichuliwa na Delloitte and Touche tokea Septemba 2006 na Gavana Balali alisitisha ukaguzi wao kinyume cha utaratibu.

Ushahidi wa wizi wa kughushi wa makampuni 13 tayari ulikuwa umekusanywa na Ernst & Young. Ushahidi wa kutosha wa kughushi wa Kagoda Agriculture Ltd. uliokusanywa na Delloitte and Touche ulikuwa tayari mwanzoni mwa Septemba 2006. Hata hivyo mpaka hivi sasa hakuna wenye makampuni au maafisa wa Benki Kuu waliofikishwa mahakamani.

Katika hotuba yake Bungeni, Agosti 22 2008, Rais alieleza kuwa ameyapa makampuni 13 yaliyojipatia fedha isivyo halali kwa njia ya kughushi hadi mwisho wa Oktoba yawe yamerejesha fedha walizochota, la sivyo yatafikishwa mahakamani. Wezi wa mabilioni ya shilingi watakaporudisha hawatashitakiwa. Ni wazi Rais Kikwete hana nia thabiti ya kupambana na rushwa. Dagaa wa rushwa kama vile “Mhasibu wa Shule ya Sekondari ya Mbinga, mkoani Ruvuma, Omari Millanzi (56), aliyehukumiwa kifungo cha miaka 240 jela, baada ya kupatikana na hatia ya makosa 60 ya kughushi nyaraka za serikali na kuiba sh milioni 24.1” (Tanzania Daima, Agosti 9, 2008) wanaweza kushughulikiwa ipasavyo, lakini masangara na mapapa ya rushwa wanaoghushi nyaraka na kuiba mabilioni hayaguswi na badala yake wanapewa muda wa kurejesha fedha hizo kana kwamba walizikopa.

Rais Kikwete alieleza kuwa hadi kufikia Agosti 18, mwaka huu, kiasi cha sh bilioni 53.338 zilikuwa zimerejeshwa na kuhifadhiwa katika akaunti na ifikapo Oktoba 31, mwaka huu, wezi hao wanapaswa wawe wamerejesha sh bilioni 64.844. Katika hatua ambayo naamini lengo lake ni kuficha wizi wa akaunti ya EPA usikaguliwe na Mkaguzi wa Mahesabu ya Benki Kuu, akaunti ya EPA imehamishwa toka Benki Kuu na sasa itasimamiwa na Wizara ya Fedha na Uchumi. Kwa kufanya hivyo hapatakuwa ukaguzi wa Mkaguzi makini kuhakikisha kama kweli fedha hizo zimerudishwa na utaratibu wa kuendelea kuiba kupitia akaunti ya EPA utasitishwa. Utaalamu na kumbukumbu za madeni ya nje uliimarishwa Benki Kuu. Hazina haina utaalamu huo. Wizi wa fedha za akaunti ya EPA haukuwa wa makosa ya kiufundi bali maandalizi ambayo yalisimamiwa na wakubwa na ndio maana Waziri wa Fedha aliwaeleza wakaguzi wa Delloitte and Touche kuwa malipo hayo yalikuwa nyeti na yanahusiana na usalama wa taifa baada ya kushauriwa afanye hivyo na marehemu Gavana Balali.

Rais amejenga mazingira ya kuendeleza kuchota fedha kupitia mfuko wa EPA kwa kueleza kwamba Hazina sasa itasimamia kulipa madeni ya EPA yaliyobaki ya dola za kimarekani milioni 233. Hakugusa kabisa ushauri uliotolewa na Lazard Freres mwaka 2004 kuwa madeni haya yamepitwa na wakati na serikali haiwajibiki kuyalipa. Ni wazi amewaachia mlango mafisadi waweze kutumia akaunti ya EPA itakayosimamiwa na Hazina kuendelea kuiba.

Rais Kikwete alieleza kuwa fedha za akaunti ya EPA siyo za serikali bali za wafanya biashara wa nje. Akaunti ni akaunti ya madeni ambayo yamechukuliwa na serikali. Shilingi zilizolipwa na waagiza bidhaa haziwezi kulipa hata asilimia 1 ya madeni ya EPA. Fedha zinazolipa madeni haya ni za serikali zilizokopwa Benki Kuu. Rais mwenyewe amethibitisha kuwa hizo ni fedha za serikali kwa kuagiza kwa nia ya kuwahadaa Watanzania kuwa fedha hizo zitatumika katika kuongeza ruzuku ya mbolea na dawa za mifugo na nyingine zitapelekwa Benki ya Rasilimali (TIB) ili wakulima wakopeshwe mikopo yenye masharti nafuu na ya muda mrefu, lengo likiwa kutaka kuanzisha mchakato wa Benki ya Wakulima. Kwa kuzipangia matumizi fedha zinazoingia katika mfuko wa serikali bila idhini ya Bunge, Rais amevunja utaratibu uliowekwa na katiba.

Umoja wa Kitaifa

Kuwepo na kuonekana kuwa kuna utawala wa sheria unaotoa haki kwa wananchi wote ndio msingi imara wa kujenga na kuendeleza umoja wa kitaifa. Wimbi la demokrasia duniani kote na maendeleo ya teknolojia na utandawazi yameongeza changamoto za umuhimu wa uadilifu katika uongozi. Katika miaka ya nyuma dola ilikuwa na uwezo wa kuchuja na kuzuia habari zinazowafikia wananchi. Kwa kutumia propaganda ilikuwa rahisi alau kwa muda, kujenga hisia za kuwepo umoja wa kitaifa hata kama ulikuwa ni wa bandia na haukusimama juu ya msingi wa haki. Muongo wa mwisho wa karne ya 20 na hasa karne ya 21 umeshuhudia kuwepo kwa mapinduzi makubwa ya kupeana habari hata katika nchi maskini kama Tanzania. Umuhimu wa kuwepo na kuonekana kuwa upo utawala wa sheria unaotoa haki umeongezeka na ndio msingi pekee na uhakika unaoweza kujenga na kuendeleza umoja wa kitaifa.

Hivi sasa katika nchi yetu kuna mmomonyoko wa umoja wa kitaifa. Ndani ya Chama tawala na hata baadhi ya vyama vya upinzani siasa za vikundi na za kikanda zimejikita. Mpasuko wa kidini unainyemelea Tanzania. Ilani ya Uchaguzi ya CCM iliwaahidi Waislamu kuwa CCM ikichaguliwa itaanzisha Mahakama ya Kadhi. Na kwa kuwa kampeni za CCM zilifanikiwa sana kiasi cha baadhi ya viongozi wa madhehebu ya Kikristo kunukuliwa wakisema kwamba Jakaya Kikwete, mgombea wa CCM ni chaguo la Mungu, iliaminiwa na Watanzania wengi kuwa Ilani ya CCM imepewa baraka ya Kanisa. Hata hivyo mjadala ndani ya Bunge wa kuanzisha Mahakama ya Kadhi umejikita katika misingi ya dini. Wabunge walio Waislamu wanaunga mkono na wabunge walio Wakristo wanapinga. Kumbe hoja ya kuanzisha Mahakama ya Kadhi iliwekwa ili kugusa na kuwavutia Waislamu wakati wa kupiga kura bila kuwa na nia thabiti ya kuitekeleza. Matokeo yake Ilani ya CCM inachochea mpasuko wa kidini ndani ya jamii. Uadilifu katika uongozi unahitaji kuwa makini katika kutoa ahadi na kutekeleza ahadi unazotoa.

Watanzania wengi tulipewa matumaini na hotuba ya Rais Kikwete ya tarehe 30 Desemba 2005 kuwa ana nia ya kuutafutia ufumbuzi wa kudumu mpasuko wa kisiasa wa Zanzibar. Mazungumzo kati ya CCM na CUF yaliyochukua miezi 14 yalikamilika mpaka kufikia hatua ya kuandikwa rasimu ya makubaliano. Kumbe wakati wote wa mazungumzo na ahadi zake kwa Watanzania na viongozi wa kimataifa Rais Kikwete alikuwa hana nia thabiti ya kuupatia ufumbuzi wa kudumu mpasuko wa kisiasa Zanzibar. Alikuwa anapoteza muda kwa kuwapa matumaini feki Wazanzibari na Watanzania. Rais Kikwete alipata nafasi adimu ya kuwaunganisha Wazanzibari wayaone matunda ya kisiasa ya kuwa na Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, matunda ambayo yangewawezesha Wazanzibari kujenga misingi imara ya demokrasia na kujipatia maendeleo ya kiuchumi na kijamii kama nchi ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Badala ya kujenga Zanzibar yenye maelewano na inayoelekea kwenye demokrasia ya kweli, udhaifu wa uongozi wake umeibua mjadala usiokuwa na tija wa Zanzibar ni nchi au siyo nchi wakati inafahamika kwamba Tanzania ni muungano wa nchi mbili, Tanganyika na Zanzibar, zilizounda mamlaka ya pamoja inayotambuliwa kimataifa (sovereignty).

UADILIFU KATIKA UONGOZI NA DIRA YA MAENDELEO

Watanzania tunastahiki kuwa na dira ya taifa ya kujenga nchi inayoheshimu haki za binadamu, yenye misingi mizuri ya demokrasia ambapo raia wote watu wazima na wenye akili timamu wana haki ya kushiriki kikamilifu katika uamuzi wa masuala yanayohusu maisha yao na hatima ya nchi yao. Kila raia popote alipo awe na haki ya kuchagua na kuchaguliwa kuwa kiongozi toka ngazi ya kitongoji, kijiji, mtaa mpaka uongozi wa taifa.

Tujenge umoja wa kitaifa wa kweli ambako hakuna ubaguzi wa aina yoyote wa jinsia, kabila, rangi, dini au ulemavu. Tuhakikishe kuwa serikali inaheshimu dini zote na inajenga mazingira ya waumini wa dini mbali mbali kuheshimiana na kuvumiliana.

Tuhakikishe kuwa kila mwananchi ana uwezo au anawezeshwa kupata milo mitatu kwa siku. Hatua za makusudi zichukuliwe kuhakikisha kuwa kina mama wajawazito na watoto wachanga wanapata lishe bora kwani mtoto mchanga asiye na lishe bora ananyimwa haki ya kujenga mwili, kinga ya mwili na ubongo wake ili aweze kushiriki kikamilifu katika kujielimisha na kujiendeleza na kufikia uwezo wake aliojaaliwa na Mwenyezi Mungu.

Tuhakikishe kuwa kila raia ana haki na anapata huduma za msingi za afya. Hatua maalum zichukuliwe kuhakikisha kuwa kila mama mja mzito anapatiwa huduma za uzazi ili kupunguza vifo vingi vya kusikitisha vya kina mama wajawazito ambavyo vinaweza kuepukwa.

Wazee wengi baada ya kulitumikia taifa kwa muda mrefu wanaishi katika umaskini wa kutisha. Watoto wao hawana kipato cha kutosha na maadili ya kuwalea wazee yameporomoka. Kama taifa ni muhimu turejeshe na kujenga maadili ya kuwaheshimu na kuwaenzi wazee. Tuweke utaratibu wa kitaifa wa hifadhi ya wazee itakayohusisha jamii kuwalea wazee wetu.

Elimu

Elimu ndiyo ufunguo wa maisha. Ili kujenga taifa linalojiamini, watoto wote wa Tanzania wawe na haki ya kupata elimu bora ya msingi na ya sekondari. Taifa lijenge utamaduni wa kuamini kuwa elimu haina mwisho na kila raia ajiendeleze kielimu hasa kwa kutumia vizuri teknolojia ya habari na mawasiliano.

Elimu ya wasichama ni nyenzo muhimu ya kuleta haki sawa kwa wananchi wote na kuhakikisha kizazi kijacho kinakuwa na fursa sawa katika kuleta na kuneemeka na maendeleo. Wasichama wengi hawamalizi masomo yao kwa sababu ya uwezo wa fedha wa wazazi, mila zilizopitwa na wakati zinazowabagua wasichama na wanawake, mazingira mabovu ya shule kama vile kutokuwa na vyoo vya wanawake mashuleni.

Kuwaelimisha wasichana na wanawake kushiriki katika soko la ajira ni nyenzo muhimu ya kuvunja mduara wa umasikini unaorithisha umaskini toka kizazi kilichopo na kinachofuata.

Ili kufanikisha mabadiliko ya kiuchumi, kuongeza tija na ajira, Taifa litoe kipaumbele maalum katika kuendekeza elimu ya sayansi na teknolojia.

Tujenge uchumi wa kisasa wenye ushindani kimataifa na utakaohimili misukosuko ya utandawazi, unaokua kwa kasi bila kuharibu mazingira na wenye manufaa kwa wananchi wote. Wananchi wahisi na waone kuwa uchumi wa taifa unatoa fursa sawa kwa wananchi wote. Tofauti za vipato vya wananchi visiwe vikubwa mno huku tukizingatia kutoa motisha kwa raia kuwa wabunifu na wajasiramali hodari. Mikakati ya kukuza uchumi itafanikiwa iwapo itatoa fursa kwa wananchi wote kufaidi matunda ya kukua kwa uchumi.

Haiwezekani Watanzania kuondokana na umaskini bila kukuza uchumi unaoongeza ajira. Katika suala la kukuza uchumi hakuna miujiza. Uchumi unakua kwa kuongeza elimu, ujuzi na utaalamu wa wafanyakazi, ongezeko la rasilimali na vitendea kazi, na kuongezeka kwa ufanisi na tija katika uzalishaji na utoaji huduma. Dira ya maendeleo na sera za kutekeleza dira hiyo ni jambo la msingi katika kuleta maendeleo ya muda mrefu. Sera za ukiritimba wa dola katika mambo ya uchumi na kuwabana wananchi, kuwanyang’anya motisha wa kujiendeleza, na kufumbia macho rushwa ya hali ya juu inayoendelea nchini zitaporomosha uchumi wetu.

Dira yetu ya maendeleo iwe ni kujenga uchumi wa soko wenye ushindani halali na unaowashirikisha na kuleta maendeleo kwa wananchi wote.

Kilimo

Njaa na ukosefu wa lishe bora ni matokeo ya umaskini lakini pia ni kichocheo kinachokuza na kudumisha umaskini. Watu wenye njaa hawawezi kuwa wazalishaji wazuri na wenye tija ya juu. Watoto wenye njaa hawafundishiki na kwa hiyo hawanufaiki kikamilifu wakiwa shuleni. Watu na hasa watoto wanaokosa chakula bora na cha kutosha wanapoteza kinga ya mwili na kwa hiyo huugua mara kwa mara. Malaria huua kwa haraka watoto wasiokuwa na lishe bora

Nusu ya Watanzania hawana usalama wa chakula. Usalama wa chakula unakuwepo ikiwa watu wote, wakati wote, wana uwezo wa kupata chakula na lishe ya kutosha na salama kwa mahitaji yao kuwawezesha kuishi maisha yenye afya na tija. Serikali inapaswa ihakikishe Watanzania wote wana usalama wa chakula. Ili Tanzania ijinasue katika dimbwi la umaskini ni lazima pawepo na mapinduzi ya Kilimo. Kuendeleza kilimo tunahitaji:-

Kuongeza motisha kwa wakulima wapate bei nzuri ya mazao yao. Hatua za makusudi zinahitajika kuboresha huduma za kilimo na kuweka usimamizi wa kuwalinda wakulima wasinyonywe na wafanyabiashara wanaoshirikiana kupunguza ushindani katika soko huria na kwa lengo la kuangusha bei za mazao.

Kuendeleza kilimo kwa kuwawezesha wakulima ikiwa ni pamoja na wakulima wadogo wadogo kuongeza tija na uzalishaji kwa kuwapatia zana na pembejeo bora, masoko ya mazao na kurahisisha usafirishaji kwa kutengeneza barabara ziendazo vijijini.

Kuanzisha mapinduzi ya kilimo kwa kupenyeza sayansi na teknolojia katika kilimo. Kuongeza utumiaji wa mbolea ya samadi na kemikali, mimea na miti inayorudisha rutuba katika ardhi, mbegu bora na mifugo bora; miradi midogo midogo ya umwagiliaji maji, mafunzo kwa wakulima na jitihada za maksudi kuwafikia na kuwawezesha wakulima wanawake.

Upatikanaji wa umeme vijijini ni muhimu katika utoaji wa huduma za afya, kuendeleza viwanda vidogo vidogo vya kusindika vyakula, karakana za zana za kilimo, mawasiliano na matumizi ya kompyuta na mtandao. Serikali makini inapaswa itekeleze mpango kabambe wa usambazaji wa umeme vijijini na kuhamasisha matumizi ya vianzio endelevu vya nguvu za umeme kama vile mionzi ya jua, gesi ya samadi na mimea na upepo.

Watanzania wengi wanaishi vijijini na kutegemea kilimo katika maisha yao. Hata hivyo tija katika kilimo chetu ni ya chini sana na Watanzania wengi walioko vijijini ni masikini wa kutupwa. Ili kujinasua kutoka katika dimbwi la umaskini tunahitaji mapinduzi ya kilimo yatakayomuwezesha mkulima mdogo kuongeza uzalishaji wa chakula kwa kumuwezesha kupata na kutumia mbolea, mbegu bora, teknolojia rahisi ya kuhifadhi maji na kumwagilia mashamba madogo, na ufugaji wa kisasa wa mifugo bora na unaozingatia ulinzi wa mazingira.

Ongezeko la bei za vyakula ni changamoto na pia ni fursa inayowezwa kutumiwa kuasisi mapinduzi ya kilimo. Ni makosa makubwa kuamini kuwa mapinduzi yataletwa na uwekezaji katika mashamba makubwa yatakayopora ardhi ya wakulima wadogo. Mapinduzi ya kilimo katika nchi za Asia ikiwemo Taiwan, China na Vietnam yalijikita katika kuongeza uzalishaji wa wakulima wadogo. Kwa kuwa Tanzania inayo ardhi kubwa inayofaa kwa kilimo, uwekezaji katika mashamba makubwa uruhusiwe alimradi haupokonyi ardhi ya wakulima wadogo na unaratibiwa na mipango ya kuongeza uzalishaji na tija ya wakulima wadogo.

Viwanda

Hakuna nchi iliyoendelea na kupunguza umaskini bila kuongeza uzalishaji na ajira viwandani. Ukuaji wa uchumi na maendeleo yanaambatana na mabadiliko ya mfumo wa uchumi kutoka kutegemea zaidi kilimo na kuongeza ajira katika viwanda na huduma. Tanzania iko nyuma sana katika maendeleo ya viwanda. Katika mwaka 2007 inakadiriwa kuwa watu walioajiriwa katika sekta rasmi ya viwanda walikuwa 91,112 kati ya nguvu kazi ya watu milioni 20. Ongezeko la uzalishaji wa mazao ya kilimo na mifugo utachochoa ukuaji wa viwanda vya kusindika vyakula. Kunatakiwa kuwepo mkakati wa kukuza viwanda vidogo na vya kati kwani ndivyo vinavyotoa ajira kwa wingi.

Madini na Maliasili nyingine

Nchi yetu imejaaliwa na Mwenyezi Mungu maliasili nyingi yakiwemo madini ya aina mbali mbali. Lakini mpaka hivi sasa wananchi hawajafaidika na maliasili hii. Rushwa na mikataba mibovu inachangia katika kulinyima taifa mapato yanayotokana na maliasili na hasa madini, misitu na samaki. Tukiondoa rushwa na kuwa makini katika mikataba na kuwapa fursa Watanzania kumiliki maliasili tutaweza kuongeza mapato ya serikali na kuchochea ukuaji wa uchumi.

Tanzania inaweza kuendelea kiuchumi, kisayansi, kiteknolojia, kiutamaduni, kijamii na kimaadili ikiwa itakuwa na uongozi adilifu utakaotumia vizuri fursa zilizoletwa na maendeleo ya teknolojia duniani na kuwekeza katika elimu na afya za wananchi, kuimarisha miundombinu na hasa umeme, maji, barabara na njia nyingine za usafiri na mawasiliano.

Ili kufanikiwa kujenga uchumi wenye manufaa kwa wananchi wote ni muhimu kwa Serikali kuwa makini kuelewa malengo yake na kusimamia utekelezaji ipasavyo. Serikali itathmini utekelezaji na iwe tayari kujifunza haraka na kurekebisha makosa ikiwa malengo ya sera hayakufikiwa. Uongozi wa nchi uwe na uwezo wa kueleza sera zake na kuwahamasisha wananchi kuzielewa, kuzikubali na kuzitekeleza.

Hivi sasa Serikali inapaswa kuwa inatekeleza Mpango wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini Tanzania – MKUKUTA. Madhumuni makubwa ya MKUKUTA yamejikita katika kufanikisha malengo makuu matatu:-

  • Kukuza uchumi na kupunguza umaskini wa kipato
  • Kuimarisha ubora wa maisha na ustawi wa jamii
  • Kuimarisha Utawala bora na uwajibikaji

Katika hotuba yake Bungeni, Rais Kikwete hakutaja kabisa MKUKUTA kama vile hana taarifa kuwa huu ndio mpango unaopaswa kuiongoza serikali katika utekelezaji wa sera zake za uchumi.

Rais alieleza juhudi zake za kutafuta misaada na akasisitiza mbinu anazotumia za kuwasifu wenye fedha ili watoe ahadi za misaada kwa maeneo wanayotaka kusaidia. Maelezo yake yalikuwa kinyume na Mkakati wa Pamoja wa Misaada Tanzania (MPAMITA) ambao unastahiki kuwa mkakati wa serikali wa muda wa kati wa kusimamia misaada ya maendeleo ya wahisani isaidie utekelezaji wa sera na mipango ya serikali ili malengo ya taifa ya kukuza uchumi na kupunguza umaskini yafanikiwe.

Rais Kikwete anaonyesha haielewi mipango rasmi ya serikali yake ikiwa ni pamoja na MKUKUTA, MPAMITA na MKURABITA. Rais hatulii ofisini akasoma na kutafakari. Kila wakati yuko safarini. Wakati mwingine wananchi wanapata hisia kuwa anasafiri kukwepa majukumu.

Katika kipindi cha nusu ya kwanza cha Urais wake, Mheshimiwa Kikwete ameshindwa kuonyesha dira. Amehalalisha wizi mkubwa wa mali ya umma kuwa siyo kosa la jinai. Rushwa kubwa inashamiri nchini. Ni rahisi mtu kuweza kufikiria athari za kuendelea na uongozi kama huu unaoyumba baada ya kupoteza dira na mwelekeo. Ni muhimu Watanzania tukaelewa vizuri ukosefu wa uadilifu katika uongozi unavyotupeleka pabaya.

Baada ya miaka 47 ya utawala wa CCM na watangulizi wake, ni wazi kuwa CCM imechoka na haina tena mawazo mapya ya kukabiliana na changamoto mpya zinazohitajika kututoa katika umaskini huu wa kutupwa na kutupeleka katika maendeleo na ustawi.

CCM imechoka, ndiyo maana imeshindwa kuwaongoza Watanzania kutumia neema ya utajiri wa rasilimali tulizo nazo na kuwatoa katika dimbwi la umaskini linalowazonga.

CCM imechoka, ndiyo maana inaendelea kuwalisha Watanzania takwimu za kukua kwa uchumi huku wananchi walio wengi wakiendelea kuishi bila hata ya kumiliki mlo mmoja ulotimia kwa siku.

CCM imechoka, ndiyo maana imekuja na sera zinazopalilia tofauti kubwa ya kipato kati ya tabaka la matajiri wachache na tabaka la walalahoi wengi.

CCM imechoka, ndiyo maana inaimba wimbo wa kupambana na ufisadi huku ikiendelea kuwakumbatia mafisadi.

CCM imechoka, ndiyo maana imefikia mahala imesababisha kugawanyika kwa Taifa katika misingi ya kidini.

CCM imechoka, ndiyo maana imeshindwa hata kukabiliana na changamoto za kuuimarisha Muungano wetu kwa misingi ya haki na usawa kati ya Tanganyika na Zanzibar.

CCM imechoka, ndiyo maana imepoteza dira na mwelekeo ikilipeleka Taifa kusikojulikana.

CCM imechoka, ndiyo maana hata yenyewe imegawanyika.

CCM imechoka, hadi sasa imewachosha Watanzania na Watanzania wameichoka CCM.

CCM imechoka, ndiyo maana sasa Watanzania tunapaswa kuipumzisha.

Watanzania tunawajibika kujipanga kuleta mabadiliko. Tusipojipanga vizuri na kuwang’oa mafisadi wa CCM, umaskini utaongezeka na nchi inaweza kusambaratika. Lakini agenda ya mabadiliko katika nchi kama Tanzania ambayo watawala wake wamejipenyeza katika kila sekta ya maisha ya wananchi haiwezi kuwa ni jukumu la wanasiasa pekee. Viongozi wa kisiasa wa vyama vinavyoamini katika mageuzi ya kweli tumejitolea kuongoza harakati za kuleta mabadiliko haya. Wengine harakati hizi zimetugharimu sana lakini hatulijutii hilo. Tunaona fahari kwamba tumeweza kujitolea kwa ajili ya kuwaletea mabadiliko Watanzania. Imetuchukua muda mrefu kwa wananchi kuweza kuamini mabadiliko yanawezekana hapa nchini. Lakini sasa Watanzania wameanza kuamka na kuunga mkono kwa nguvu haja ya kuleta mabadiliko.

Watanzania wanataka mabadiliko yatakayowapa uongozi wa namna bora ya kutumia neema ya utajiri wa rasilimali tulizo nazo ili kuwatoa katika dimbwi la umaskini linalowazonga na kuwalekeza katika maendeleo na ustawi kwa wote.

Watanzania wanataka mabadiliko yatakayomhakikishia kila Mtanzania anamiliki alau milo mitatu ilotimia kwa siku.

Watanzania wanataka mabadiliko yatakayomhakikishia kila Mtanzania anaongeza kipato chake kupitia kazi halali na jasho lake na kumhakikishia kwamba gharama za maisha hazipandi kiholela.

Watanzania wanataka mabadiliko yatakayowapa huduma za msingi za afya zilizo bora, na kuwahakikishia watoto wao wanapata elimu bora ya msingi na sekondari.

Watanzania wanataka mabadiliko yatakayowapa maji safi na salama, na miundombinu ya umeme na barabara iliyo imara itakayowezesha sekta binafsi kuongeza ajira kwa vijana wetu.

Watanzania wanataka mabadiliko yatakayosafisha uoza wa ufisadi na rushwa na yatakayoleta uwajibikaji na utawala wa sheria.

Watanzania wanataka mabadiliko yatakayojenga misingi imara ya umoja, udugu na mapenzi kati ya wananchi wenye imani tofauti za kidini, wa makabila, rangi, na jinsia tofauti.

Watanzania wanataka mabadiliko ambayo yataupa uhai mpya Muungano wetu na kuuimarisha uweze kukabiliana na changamoto mpya kwa kuhakikisha haki na usawa kati ya Tanganyika na Zanzibar, na hivyo kuvutia nchi nyengine kujiunga nasi.

Watanzania wanataka mabadiliko yatakayowapa dira na mwelekeo mpya utakaolipeleka Taifa katika jamii inayozingatia haki sawa kwa wote na yenye uchumi imara unaotoa ajira na tija kwa wananchi wote.

Watanzania wanataka mabadiliko yatakayowapa uongozi makini, thabiti na wenye uzalendo wa kweli kwa Taifa letu.

Watanzania wanataka mabadiliko kwa sababu sasa wako tayari kwa mabadiliko.

Chama cha CUF kiko tayari kuwaongoza Watanzania kuleta mabadiliko hayo. Kimejiandaa vyema kuongoza jukumu hilo la kihistoria. Leo hii tumeona tutekeleze sehemu ya wajibu wetu wa kihistoria kwa kuwakaribisha Watanzania wote kuungana pamoja kutafakari ni namna gani tutaiondolea Tanzania aibu ya ukosefu wa uongozi na kuirejeshea heshima iliyokuwa nayo mbele ya macho ya wananchi wake na jumuiya ya kimataifa.

Inawezekana, tutimize wajibu wetu.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s