CCM haina uhalali wa kuiamulia Zanzibar

Makamo Mwenyekiti wa CUF, Mhe. Machano Khamis Ali

Makamo Mwenyekiti wa CUF, Mhe. Machano Khamis Ali

“Lakini mimi bado naelekea kwa watu wa CCM. Kuna mtego uliowekwa ndani ya viongozi wa CCM. Pinda si mwenda wazimu. Anasema suala hili lizungumzwe na chama cha CCM, maana ndio chama tawala. Waheshimiwa, mimi nataka nikuulizeni nyiye Wazanzibari, hivyo Wazanzibari sasa hatupunguwi milioni moja, CCM wanafika laki nne? Kwa hivyo, ukichanganya wanachama wa CUF na CCM hatuwezi kuwasemea Wazanzibari wote? Bado kuna Wazanzibari hawana uanachama wa CUF wala CCM, lakini bado wana haki na Zanzibar hii. Kama hao wana haki na Zanzibar hii, basi CCM hawana haki ya kuamua hili. Hili haliwezi kuamuliwa na Chama cha Mapinduzi. Hili ni la Wazanzibari wote. Lazima Wazanzibari wote washirikishwe. Matatizo haya haya ya kuyaachia mambo na CCM, ndio CCM wakenda kuamua kwamba Rais wa Zanzibar asiwe Makamo wa Rais.”

Kauli ya CUF kuhusu agizo la Waziri Mkuu Mizengo Pinda kwamba suala la hadhi ya Zanzibar litamalizwa na CCM…

Mimi niliwaambia Wakurugenzi watowe elimu na sikuwa na wasi wasi, kwani wananchi wanalijua hilo. Lakini nilikuwa nataka na CCM wayasikiye haya. Kwa hivyo, nafikiri Mheshimiwa Ismail Jussa ameshawasaidia sana leo.

Kubwa kuliko yote, kwanza, mimi nasema nyote kila mwanachama wa CUF – mkubwa, mdogo, mzee, kijana, mwendawazimu, vyovyote alivyo, mwana chama yeyote wa CUF – ampongeze Pinda.  Pinda sio mtu wa kumlaani. Pinda ni mtu wa kumpongeza. Nasema hivyo, kwa sababu sisi tumeanzisha chama cha CUF miaka 15 iliyopita na tulipokianzisha tu, Katiba yetu inasema tutakuwa na serikali tatu: Serikali ya Tanganyika Serikali ya Zanzibar na Serikali ya Muungano.

CCM wa Zanzibar hawakutufahamu. Kwa sababu wangetufahamu, kungekuwa na serikali tatu, maana yake Zanzibari ipo. Kwa sababu ingelikuwa inatamkwa: Serikali ya Zanzibar, Serikali ya Tanganyika na Serikali ya Muungano. Tungemuondoa Nyerere katika dhamiri yake yake ya kuimeza Zanznbar.

Wenzetu wakashindwa kutuelewa, (lakini sasa) wenzetu hawa wamepata nafasi ya kuelewa baada ya Pinda kumtaka kwamba Zanzibar si nchi. Kwa hiyo, mimi nampongeza. Nnachotaka kusema tu, bado hawajachelewa.  Wametuchelewesha sisi CUF, lakini wao hawajachelewa.

Na ndio maana Mheshimiwa Jussa na Mheshimiwa Bimani wakasema, sisi tutaungana na watu wa CCM kwa hili, kwa sababu sisi uchungu wa Zanzibar ushatupata tayari. Sasa CCM wanaposema hawakubali na wanaungana na CUF kusema hawakubali, sasa Zanzibar itarudi mikononi mwa Wanzanzibari. Baraza la Wawakilishi ni baraza la muda, wameshatumwa kwa muda wamemaliza.

Lakini mimi bado naelekea kwa watu wa CCM. Kuna mtego uliowekwa ndani ya viongozi wa CCM. Pinda si mwenda wazimu. Anasema suala hili lizungumzwe na chama cha CCM, maana ndio chama tawala. Waheshimiwa, mimi nataka nikuulizeni nyiye Wazanzibari, hivyo Wazanzibari sasa hatupunguwi milioni moja, CCM wanafika laki nne? Kwa hivyo, ukichanganya wanachama wa CUF na CCM hatuwezi kuwasemea Wazanzibari wote? Bado kuna Wazanzibari hawana uanachama wa CUF wala CCM, lakini bado wana haki na Zanzibar hii. Kama hao wana haki na Zanzibar hii, basi CCM hawana haki ya kuamua hili. Hili haliwezi kuamliwa na Chama cha Mapinduzi. Hili ni la Wazanzibari wote. Lazima Wazanzibari wote washirikishwe. Matatizo haya haya ya kuyaachia mambo na CCM, ndio CCM wakenda kuamua kwamba Rais wa Zanzibar asiwe Makamo wa Rais.

Juzi wanakaa wanasema turejeshewe makamo wa rais, kwamba ni Rais wa Zanzibar. Akurejeshee nani, na wewe ndiye uliyefuta? Kwani aliyefuta nani? Unataka akurejeshee nini? Wewe mwenyewe ujirejeshee. Kama sasa wameona na wanajuta, basi wakubali kujuta kwao. Kilichotokea waheshimiwa, baada ya mfumo wa vyama vingi, Nyerere akawaita kwenye chama cha CCM, akawambia kwamba yeye anakusudia kumuondoa Rais wa Zanzibar kwenye umakamo wa rais kwa sababu inawezekana chama chengine kikashinda hasa Zanzibar. Kwa hivyo haiwezekani makamo atoke chama chengine na rais chama chengine, Rais kama akiondoka, chama chengine kitashika nafasi ya nchi.

Baada ya kuelezwa hayo, wakasema sawa Rais wa Zanzibar asiwe Makamo wa Rais.  Wanazidiwa akili na mtu ambaye hana akili. Wakakubali.

Halafu ondoka hapo, mimi nasema tizameni tunaambiwa kuna Tume ya Kuondoa Kero za Muungano, mwakilishi wa Zanzibar ni Shamsi Vuai Nahodha, Waziri Kiongozi, ndio kiongozi wa kule kwa upande wa Zanzibar. Na kule (Bara) kuna Pinda. Miaka yote hii Waziri Kiongozi wanakwenda kuzungumza kugawana mafuta ya Zanzibar. Waziri Kiongozi kero aliyoiona yeye ni kugawana mafuta tena, mafuta ya Zanzibar, wanatafuta mpatanishi. Kero hii ya kuwa Zanzibar si nchi yeye haiyoni, na ndio maana mpaka leo hatoi kauli yoyote. Hasaini kitu, anaogopa mabwana zake.

Lakini sisi tuliokuwa hatuna mabwana, tutakusemea wewe kaa kimya! Sisi hatuna rafiki kwa nchi. Nchi hii ni yetu, itabakia kuwa yetu na sisi tutasema, tutashirikiana, tutahakikisha inabakia kuwa yetu. Kwa hivyo, ninaikubali kauli ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi ambayo imetolewa miongoni mwa wao, wawakilishi wa CCM, imetolewa na wawakilishi wa CUF.

Juzi tu Mwakilishi wa CCM kapeleka hoja binafsi juu ya suala la Zanzibar lizungumzwe katika Baraza la Wawakilishi na Mwakilishi wa CUF naye kapeleka hoja binafsi. Spika kakataa. Hao ndio CCM, hao ndio CCM. Anataka hata akifa, ile shuka yake iwe rangi ya kijani. Hawa wanapeleka hoja binafsi kwa ajili ya Uzanzibari, yeye anapinga. Hii ni ishara ya kuwa kama mwakilishi wa CCM naye kapeleka hoja binafsi, wameelewa. Kama wameelewa ni lazima tukubaliane nao. Kwa hivyo, hakuna CCM mbaya leo. Kuanzia leo, nakwambieni kama Makamo Mwenyekiti, kuanzia leo hawa ni wananchi wa Zanzibar. Tushirikiane nao kudai haki ya Zanzibar.

Hao ni wenzetu tutakuwa nao bega kwa bega mpaka tuhakikishe nchi hii tumeigomboa.  Hatugomboa kwa maana ya kujiondoa kwenye muungano, tunagomboa katika yale Mhe. Jussa ameshakusomesheni.  Kuna mambo yameongezwa wa maksudi kutaka kuimaliza Zanzibar.

Tume zote zilizoundwa na bara kina Shekilango, kuna nani lakini Tume moja tu ya Nyalali, Nyalali kasema kuondoa migogoro manung’uniko na kuna na ridhaa kwa Watanzania ni kuwa na serikali tatu, inakubaliana na Katiba ya CUF, wakamwambia silo tulilokuwa hilo.

Mtu mzima kama Jaji Francis Nyalali anayeheshimiwa na watu wote na dunia inamheshimu walimbambikizia: “Silo tulilokutuma!” Wanafahamu kwamba tukiingia kwenye serikali tatu, haki za Zanzibar zitarudi mikononi mwa Wazanzibari. Mheshimiwa Jussa kakwambieni njaa hii ni ya kutengeneza, ni ya kutengeneza kweli. Lakini kubwa, mimi nashangaa kwa nini CCM wasitanabahi mapema? Ali Hassan Mwinyi, wakati akiwa Rais, alisema madhumuni ya CCM ni serikali mbili kuelekea serikali moja. Hawakumsikia au hawakumfahamu? Hawa viziwi…. au?

Zanzibar ni nchi, imeteremshwa na baraka zake. Pinda kawaambia, ule muda wa kuwa Zanzibar haipo ushafika. Kumbe haujafika, alikuwa abaki kimya mpaka wamalize.

Mkutano wa leo ni mkutano wa kuelimishana na mikutano kama hii tutaifanya mingi sana. Mingi imeshafanyika. Tafadhalini nyote, nyinyi wanachama wa CUF mnaokaa mitaa mbalimbali, mnakaa na watu wa CCM. Msomeshe mtu wa CCM katika kuungana na Wazanzibari wenzake kudai nchi. La kwanza, ikiwa wewe hakufahamu, mshawishi aje mikutano ya CUF ili hii elimu aipate hapa.

Tunashangaa leo mtu anazuia kiwanja katika kutoa elimu kama hii ya faida yake mwenyewe. Hawa ndio wale….. Maana yake, wakati ule uislamu unateremshwa kwa Nabii Muhammad, Makureshi wa Makka waliwaambia watu wa Makka: “Msende nyinyi pale Muhammad anapotoa maelezo yake!” Ilikuwa wanawakataza. Sasa na hawa kama wanakatazwa hata kwa nchi yao. Lakini kama hawakulazwa, wasiwe  wavivu. Waje wajisomee ili tuzidi kushikamana tuokowe nchi yetu.

Hatuna nchi, Pinda hajasema uongozi, lakini kwa hatima ya nchi ni sisi wenyewe wa kulaumiwa, ni CCM Zanzibar. Nasema CCM Zanzibar kwa sababu wakati wa ASP haya hayakufanyika na kama Karume mwenyewe aliyeunganisha nchi hii angefufuka akakuta hali hii, mbona ingekuwa balaa. Kwa sababu Karume, (katika) suala la Azimio la Arusha tu kitu kidogo sana, anamjibu Nyerere: “Azimio mwisho Chumbe, Zanzibar haliwezi kuingia!” Karume katika uhai wake walikuja kuchukuliwa askari wa Jeshi la Ulinzi kwenda kupigana vita. Kawafuata bandarini, akasema: “Nani katowa amri askari wa Kizanzibari wapelekwe vitani? Mimi mbona sijuwi?” Akajibiwa: “Hii ni amri ya Rais wa Jamhuri ya Muungano!” Akasema: “Hana mamlaka kutoa askari Zanzibar bila ya mimi.  Hawa wamerithi wapi hawa!”

Karume anasema. Huyo ndio baba yake. Yeye (Amani Karume) hajazuia wala hajatoa kauli yoyote. Na anapoambiwa waunganishe Wazanzibari analia, ati: “Oo, namkumbuka baba yangu.” Baba yako hayo ndiyo aliyosema.  Baba yako alikuwa mtu anayejua anachokifanya kuhusu Zanzibar hii.

Waheshimiwa, sisi tulipoka kupigania nchi hii, CCM wa Zanzibar walisema: “Hawa ni waroho wa madaraka tu, hawa tumewafukuza, hawa wanataka kuleta Waarabu.” Sisi tunataka kuleta Waarabu, nyinyi mmemleta nani? Nyiye mmemleta Pinda kutoka kwao Mpanda, leo ndiye bwana, anasema Zanzibar si nchi na mnaridhika. Lakini mara hii naona hamkuridhika mmechukia kidogo.

Sasa tumeanza kufika baharini. Waheshimiwa naomba niseme: Msiondoke na niliyoyasema miye, ondokeni na aliyoyasema Jussa ili mkawafundishe wengine huko mitaani. Mimi nakwambieni kuweni nao CCM. Shikamaneni, msifanye chuki nao, maana viongozi wao washakubali. Hawa wadogo wadogo watabaki wachache, wengi tutaungana. Nchi itarudi mikononi.

Ahsante sana

Hakiii….

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s