Muungano uishie kwenye mambo 11 tu ya asili

Ismail Jussa akihutubia mkutano wa hadhara
Ismail Jussa akihutubia mkutano wa hadhara

“…Kifungu cha Nne katika Makubaliano ya Muungano kinataja mambo 11 tu ya Muungano. Leo ukiisoma Katiba hii ya Muungano, yameongezeka yamekuwa 22  – mara mbili zaidi. Lakini ni 22 ukisoma nambari, ukiyachambua moja moja, yanakaribia 35; pengine mpaka 40…mambo yote, ukiacha 11 ya asili, yaliyomo katika Katiba ya Muungano ni batili na Zanzibar ina haki ya kuyarejesha katika mamlaka yake mara moja…”

Msimamo wa CUF kuhusu hali halisi ya Muungano kwa sasa na hadhi ya Zanzibar ndani ya Muungano huu kama ulivyotolewa na Msaidizi Maalum wa Katibu Mkuu wa CUF kuhusu Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa, Ismail Jussa, katika viwanja vya Magomeni, Mjini Unguja, tarehe 16 Julai, 2008, katika muendelezo wa mikutano ya CUF kuwaelimisha watu kuhusu hadhi na nafasi ya Zanzibar ndani ya Muungano

Waheshimiwa, mkutano huu ni muendelezo wa mikutano yetu ya kawaida. Kama alivyosema Philip Habib (Salim Bimani, Naibu Mkurugenzi wa Haki za Binaadamu na Mahusiano ya Umma) kwa sasa tutakuwa na suala moja tu la kuwaelimisha wenzetu wa upande wa pili (Tanganyika) na hata na wa Zanzibar, kuhusu hadhi ya nchi yetu, Zanzibar. Tumekusudia tuelezane, tufahamishane ili tuweze kusimama kidete kuilinda, kuitetea na kuihami Zanzibar yetu.

Waheshimiwa, kwa waliokuwa wakifuatilia tangu Waziri Mkuu Peter Kayanza Pinda alipotamka Bungeni kuwa Zanzibar si nchi, yameelezwa mambo mengi na kwa urefu. Katika mkutano wetu wa Mtoni tulitoa msimamo wa CUF na wa Wazanzibari. Na Maalim Seif naye kaeleza kwa urefu historia ya Zanzibar na misingi ya Zanzibar ili tujijuwe na akaomba tutangaze Mgogoro wa Katiba ili suala hili lisije tena na tuheshimiane kama tunataka. Na kama hatutaki, basi tugawane mbao. Na katika hili hatutanii hata kidogo, baada kuelezwa haya kila mtu aweke akili yake sawa sawa.  Mzanzibari hatakuwa tayari kuona nchi yake inatawaliwa na mtu asiyekuwa Mzanzibari.

Kwa hivyo tunasema, historia imeshaelezwa, sasa twende mbele zaidi.

Juzi, Alkhamis, katika kile kipindi (cha maswali ya papo kwa papo Bungeni), Waziri Mkuu Mizengo Kayanza Peter Pinda, akaulizwa na wabunge wenye msimamo – wabunge wa CUF. Mbunge, Mheshimiwa Mohammed Habib Mnyaa, aliuliza suala dogo tu lakini la msingi. Alimuuliza: “Wewe, Mhe. Waziri Mkuu, kwa uzoefu wako umekaa Ikulu kwa muda mrefu, unaweza kuniambia, Katiba na Mkataba wa Muungano kipi kina nguvu zaidi na kilicho juu zaidi?” Jibu lake (Waziri Mkuu Pinda): “Mhe. Mnyaa hunitakii mema, nikijibu!” Mhe. Dkt. Ali Taarab (mbunge wa Konde) akauliza: “Muungano ni wa Tanganyika na Zanzibar, kwani unaachia chama kutatua jambo la wananchi?” Mhe. Salum Hemed (Mbunge wa Mtambile) akauliza ikiwa tafsiri juu ya kupiga kura hii haiyonyeshi Zanzibar ni nchi!

Spika Samuel Sitta akaingilia kati kuzuia maswali ya wabunge wetu. Alipojibu suala Pinda siku ya mwanzo, wakapiga makofi wabunge ndio imepita.  Hapa hakufanya kwa ujinga. Hizo ni njama za kututisha na kutunyamazisha, lakini hatunyamazi. Zama za kutishana zimekwisha. Suala lile kalikwepa kwa sababu Watanganyika wanajuwa vyema kwamba wakirudi kwenye Mkataba wa Muungano, watakuwa na hali ya kuumbuka na uchafu wao wote walioifanyia Zanzibar kwa miaka 45 utajitokeza.

Sasa kama wao wanataka kuzuia mijadala katika Bunge kuwa ndio mwisho, (wajuwe kuwa) tupo midomo ya Wazanzibari, Chama cha CUF. Tumeshikana pamoja kuona kwamba Zanzibar sio tu kama ni nchi lakini itaweza kurejesha mamlaka yake.

Suala tulilouliza lilikuwa la msingi kwa mujibu wa sheria. Mkataba wa Muungano unaitwa ni International Treaty yaani Mkataba wa Kimataifa; na unaposema Mkataba wa Kimataifa maana yake ni mkataba uliotiwa saini na zaidi ya taifa moja. Kwa hiyo wale wanaohoji hadhi ya Zanzibar, waelewe hivyo.

Lakini, pili, Mkataba wa Kimataifa hauwezi kurekebishwa tena, isipokuwa wale wale waliosaini mwanzo wakirudi na kuurekebisha kwa kupitia utaratibu ule ule walioanzisha pale mwanzoni. Sasa hawa wenzetu tunaowaita ndugu zetu wa damu – mimi siamini kama ni ndugu wa damu, kwani huwezi kuwa na ndugu wa damu ambao kila siku wanafuta njia ya kukumaliza – sasa hawa, wakiongozwa na hasidi mkubwa wa Zanzibar, Julius Nyerere, walianza kuuvuruga Mkataba wa Muungano (zamani sana). Waliurekebisha, wakaunyofoa, wakaupondaponda na sasa leo suala hili wanaliona chungu kwao, kwani wanajua likibainika utaonekana uchafu wao walioifanyia Zanzibar.

Mkataba wa Muungano ndio misingi hiyo maana yake nini? Kwenye sheria, kuna kitu kinaitwa grand norm, yaani sheria kuu. Pinda alipoulizwa, suala la kwanza alisema ati Katiba ya Muungano ndio sheria mama! Kamwambia nani? Labda Katiba mjukuu! Kwa sababu Msingi wa Muungano ni yale mapatano ya Muungano. Ile ndiyo grand norm. Maana yake, sheria nyingine yoyote itakayotungwa: ikiwa Katiba za nchi hizi, lazima ziheshimu Makubaliano yaliyokuwamo, lazima ziheshimu Makubaliano ya mataifa mawili – taifa la Zanzibar na Tanganyika. Taifa la Zanzibar ambalo lilitambuliwa miaka 1,000 kabla ya Yesu Kristo, na taifa la Tanganyika lililotambuliwa 1921, miaka 80 iliyopita.

Kwa hivyo makubaliano ndio msingi. Katika mikutano iliyopita hatukumjibu kisheria; tulikuwa tukimjibu kisiasa.  Leo tukiingia masuala ya kisheria, ati watutafutie pahala petu ati watuambie maamuzi yetu kwa kutumia Katiba wanayoiita ya Jamhuri ya Muungano. Hatutakubali. Na huu si mtazamo wa Pinda peke yake. Utawakuta watu – hata ukiwaona wamesoma namna gani, wana digrii ngapi, utawakuta wanashikilia: “kwanza Katiba, Katiba imesema, Katiba imesema.”

Katiba imeitwa tu katiba, lakini Katiba Mama ni Makubaliano ya Muungano na ndio maana Pinda suala hilo akalikwepa. Na si Pinda tu, hata baba yake Pinda, Julius Nyerere, alianza kuyakwepa kwa kwa alijua akiyaheshimu Makubaliano ya Muungano, utakuwa ni Muungano wenye haki sawa. Haidhuru na huo Mkataba una kasoro zake, lakini kwa msingi wa sheria yangepaswa kuwa ndio Makubaliano yetu.

Nasema, tuwaelimishe hawa kwamba hapana mahala popote Mkataba wa Muungano ulipozifuta Zanzibar na Tanganyika. Wala Mkataba wenyewe si mkubwa, ni kurasa tatu tu; ni rahisi kuusoma. Kwa hivyo, kifungu cha kwanza cha eti Katiba ya Muungano “Tanzania ni nchi moja, Jamhuri ya Muungano” ni kifungu ambacho ukikipeleka kwa wanaoheshimu sheria, watasema kifungu hicho ni batili, kiondoke katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano. Kwa sababu gani? Kifungu cha Makubaliano ya Muungano, Kifungu cha Kwanza: “Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar zitaungana na kufanya Jamhuri moja.” Jamhuri moja haina maana ya nchi moja. Jamhuri ina maana ya utawala, basi.

Si hilo tu, Kifungu cha Pili kinasema: “Kuanzia tarehe ya kusainiwa kwa Makubaliano haya, kabla ya kutungwa kwa Katiba ya Muungano, kwa kipindi cha mpito itaongozwa kwa Katiba ya Tanganyika lakini itaongeza mambo yafuatayo: kwanza kuwepo kwa Serikali ya Zanzibar na Baraza la Kutunga sheria la Zanzibar na litakuwa na Mamlaka kamili kwa mambo yote yasiyokuwa ya Muungano ndani ya Zanzibar.”  Kwa hiyo Zanzibar haikufutwa!

Sitaki kusoma (vifungu) vyote (vya Mkataba wa Muungano) kwa sasa, lakini Kifungu cha Tano kinasema: “Sheria zilizopo zitaendelea kutumika za Zanzibar na Tanganyika katika maeneo yake yaliyohusika.” Sheria ni pamoja na Katiba, ingawa Zanzibar ilifanya Mapinduzi haikuwa na Katiba, lakini ilikuwa na serikali iliyokuwa ikiitwa ni serikali ya kikatiba na utawala wa sheria. Maana yake hii sheria nyingine zote zitaendelea kutumika Zanzibar na zitaendelea kutumika Tanganyika.

Kifungu cha kwanza cha Katiba kimewekwa kinyumenyume. Nani kaifuta Tanganyika? Ni muhimu hili nalo kulijuwa, maana kule (Tanganyika) wanasema katika maelezo yao, kwamba: “Kwa nini Wazanzibari wanalalamika wakati na sisi Tanganyika imefutwa?”  Je, kwani tumeifuta sisi hiyo Tanganyika? Ni Julius Nyerere, tena bila ya kuzingatia sheria wala Makubaliano ya Muungano. Wamepeleka sheria katika Bunge tarehe 25 Aprili, 1964, kapeleka sheria kuifuta Tanganyika.

Lakini mnajua kilichojitokeza?  Hawakuifuta. Maalim Seif aliposema kwamba Nyerere ni sungura ni sungura kweli. Alitumia jina kwamba kaifuta Tanganyika lakini ukifuatilia utaona katika hili alifanya makusudi. Alitumia orodha ya sheria chungu nzima, akabadilisha Tanganyika akaifanya Tanzania. Na ndio maana ukipeleleza, kutokea siku ya Muungano, aliyekuwa Rais wa Tanganyika, JK akawa ndiye Rais wa Tanzania; iliyokuwa bendera ya Tanganyika, ikawa ndio bendera ya Tanzania.  Nembo ya Tanganyika ikawa ya Tanzania. Tangayika ikabakisha kiti chake Umoja wa Mataifa Tanganyika ikabakisha na jumuiya nyengine.

Inasemekana hata ile barua iliyopelekwa Umoja wa Mataifa haikusema futa kiti cha Zanzibar, na Tanganyika uweke kiti cha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, maana jinsi jina hasa la Muungano huu ni Jamhuri ya Tanganyika na Zanzibar. Jina hili la Jamhuri ya Muungano halijakuwepo. Lakini hayo ni katika zile zile njama za kuifuta Zanzibar, maana ukiita Jamhuri ya Tangayika na Zanzibar watu watajuwa huu ni Muungano wa nchi mbili. Ili kutufunika – na sana vijana muwe na tahadhari, mnaposoma magazeti kwa wanaandika kwamba TAN ni Tangayika na ZAN ni Zanzibar kisha mmeongezwa A isomeke vizuri. Si kweli. Oscar Kambona, mmoja wapo wa wapishi wakubwa wa Mapinduzi ya Zanzibar na Muungano, mwenyewe kabla ya kufa alisema Nyerere alibuni jina la Tanzania kwa kuunganisha Tanganyika na Azania, kwa sababu huko zamani, kiasi miaka 1,000, eneo lote hili la Afrika ya Mashariki na mwambao wake ukiitwa Azania.  Lengo sio Tanganyika na Zanzibar, ila ni kuifuta Zanzibar. Azania kwa Nyerere ni utawala wa eneo lote hilo. Kwa hiyo na yeye alikuwa na lengo, ndio maana akaingia katika migogoro ya eneo lote hili – Seychelles, Comoro, Msumbiji, yote haya, kenda yeye ili lengo la utawala wa Azania upate kutimia.

Ile barua haikusema futa kiti cha Zanzibar na futa cha Tanganyika, bali Katibu Mkuu wa UN (Umoja wa Mataifa) kapelekewa barua “futa kiti cha Zanzibar.”  Kile cha Tanganyika kikabadilika kikawa ni Tanzania. Lengo ni kuifuta Zanzibar. Na haya hasemi Jussa tu, lakini mtu anayeheshimika sana ulimwenguni, Profesa Ali Mazrui, (ambaye anasema) Muungano huu haukuwa kwa malengo ya Umoja wa Afrika. Makala tunayo, wakitaka siku moja tutayatoa.  Muungano huu ni ukoloni mdogo wa Tanganyika dhidi ya Zanzibar, ndio maana Zanzibar Rais wake akaondoka, ikawa haina madaraka, Zanzibar nembo yake ikaondoka, kiti chake Umoja wa Mataifa kikaondoshwa. Leo hata Mizengo Peter Pinda anathubutu kutwambia Wazanzibari kuwa Zanzibar si nchi.

Kwa hivyo, ndugu zangu na Wazanzibari wenzangu, tunataka tuelewe kuwa Mkataba wa Muungano haukufuta Tanganyika na Zanzibar na ndio maana Katiba ya Muungano imevunjwa, imevurugwa, haina maana. Lakini Katiba ya Zanzibar, Kifungu cha Pili kiko safi kabisa.

Kifungu cha Pili kinafafanua eneo la Zanzibar ni eneo lote lililozunguka na visiwa vidogo vidogo na bahari yake ambayo kabla ya Muungano ikiitwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar. Hivyo ndivyo Katiba ya Zanzibar inavyosema.

Hili la kwamba Zanzibar haikufutwa na Makubaliano ya Muungano kama ambavyo Tanganyika haikufutwa nataka niliwachie hapa kwa muda. Wameibadilisha wao tu ili wapate kututawala sisi.

La pili ninalotaka kulizungumza, ni haya maneno ambayo Zanzibar imeambiwa si nchi. Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Iddi Pandu, alisema Zanzibar ni nchi lakini si taifa. Wengine wanasema Zanzibar ni nchi, lakini si dola.  Mimi, kwa niaba ya Chama cha Wananchi, CUF, nasema Zanzibar ni nchi, ni taifa na ni dola katika mambo yake yote.  Na msingi wangu huu hapa: ni ule ule Mkataba wa Muungano.

Kwa sababu nchi maana yake nini? Nchi manaa yake ni eneo linalofahamika, lenye mipaka inayokubalika, watu wake wanafahamika na lina serikali inayofanya kazi.  Zanzibar yote matatu yapo. Lakini taifa linafahamika mipaka yake na lenye watu wanaofahamika, watu wake wana utamaduni na historia moja. Wazanzibari wanayo hayo. Dola ni uwezo wa kuingiliana na mataifa ya kigeni. Sasa mtu anaweza kusema Zanzibar wizara ya mambo ya nje haina, kwa hiyo Zanzibar si dola. Hapana. Kama nilivyosema, ukisoma Mkataba huu wa Muungano, unasema wazi kwamba kwa mambo yasiyokuwa ya Muungano, Zanzibar ina mamlaka yake kamili. Unapozungumzia mamlaka kamili, unazungumzia sifa ya udola. Lakini si hayo tu, ukenda katika Mambo ya Muungano, katika makubaliano ya asili ni Mambo ya Nje tu, Mahusiano ya Kimataifa halijapata kuwemo katika Mambo ya Muungano.

Unasema kuna Foreign Affairs (Mambo ya Nje) na International Cooperation (Uhusiano wa Kimataifa). Uhusiano wa kimataifa halijawahi kuwa suala la Muungano. Zanzibar ni Taifa, Zanzibar pia ni dola kwa mambo yake ambayo si ya Muungano.

Na Zanzibar ina sifa zote za kuwa dola kamili. Kesho tukiamka, tukiamua sisi Wazanzibari: kama hatuheshimiani, kama hatuna Muungano wa kuheshimiana, naiwe basi. Wakae kwao, tukae kwetu, tukae kwa ujirani mwema.  Narejea tena, hatuzungumzi kuvunja Muungano kama au ikiwa Muungano huu hatutakuwa na kuheshimiana. Kama kutakuwa na kuheshimiana, tutasikilizana.  Lazima tuheshimiane na Muungano huu uweke heshima ya Zanzibar kama mshiriki kamilifu katika Muungano kama ilivyokuwa Tanganyika.

La tatu ninalotaka kulizungumzia, na pengine kwa sababu ya muda litakuwa ndio la mwisho kwa leo, (ni kwamba) Mkataba huu wa Muungano umeweka makubaliano ambayo yataongoza Muungano wetu.  Huwezi kuongeza, nimesema mwanzo pale, huwezi kuongeza huwezi kubadilisha. Katiba ya Muungano (kwa hivyo) ni batili kwa sababu vifungu vyake vingi vimebadilisha Makubaliano ya Muungano.

Yaliyobadilishwa yako mengi – tutayaona tunakokwenda, lakini kwa leo nikamate hili la mwisho, Kifungu cha Nne (4). Katika Makubaliano ya Muungano kinataja mambo 11 tu ya Muungano, leo ukiisoma Katiba hii ya Muungano, yameongezeka yamekuwa 22 mara mbili zaidi. Lakini ni 22 ukisoma nambari, ukiyachambua moja moja, yanakaribia 35; pengine mpaka 40. Kwa sababu, unakuta nambari zilizoorodheshwa – nambari 12, kwa mfano, mambo yote yanayohusika na sarafu, mabenki na ubadilishanaji wa fedha za kigeni; kifungu cha 11 unaambiwa Bandari: mambo yanayohusika na usafiri wa anga posta na simui. (Kwa hivyo), mambo yote, ukiacha 11 ya asili yaliyomo katika Katiba ya Muungano, ni batili na Zanzibar ina haki ya kuyarejesha katika mamlaka yake mara moja.

Juzi katika Baraza la Wawakilishi kimetokea kitendo cha kihistoria kabisa. Wawakilishi wetu wa CUF na CCM wameungana wakapitisha kwa pamoja bajeti ya Wizara ya Maji, Ujenzi, Nishati na Ardhi.  Katika kufunga mjadala wa Wizara ile, Waziri Mheshimiwa Mansour Yussuf Himidi alichukua kwa moyo safi mapendekezo yaliyotolewa na Waziri kivuli Mheshimiwa Hamad Masoud Hamad.

Mheshimiwa Hamad Masoud alisema, sio tu kuanzia sasa analiomba Baraza kusiruhusiwe kuongeza jambo lolote la Muungano bila ya Baraza la Wawakilishi kutoa idhini yake, lakini hata yale yaliyoingizwa kinyume na utaratibu kama suala la mafuta na gesi asilia, hatujachelewa, yarejeshwe katika Mamlaka ya Zanzibar. Na akasema kwamba tufanye hivyo kwa Azimio la Baraza, kwa kupitisha hoja. Ile inaifunga Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na serikali yoyote itakayokuja kwamba suala la mafuta haliwezi tena kuwa la Muungano. Tunawahadharisha ndugu zetu, sisi katika suala la kutetea nchi tuko nao. Wakigeuka wao, umma wa Zanzibar mutawahukumu na mimi naamini mnao uwezo huo.

Kwa hivyo, nawaambia waheshimiwa Maamuzi ya Baraza la Wawakilishi, lakini nasema isiishie kwa mafuta tu, mambo yote 11 yaliyoongezwa zaidi ya yale mambo 11, Baraza la Wawakilishi lipitishe azimio yarejeshwe katika mamlaka ya Zanzibar.

Hawa watu wanatufanya sisis wapumbavu sana.  Juzi nilikuwa na mahojiano na Idhaa ya Kanda ya Ziwa. Wanasema: “Wewe unasema Zanzibar ni nchi, unatumia Katiba ya Zanzibar. Katiba hiyo hiyo inasema Zanzibar ina mamlaka zote tatu: mamlaka ya utawala ambayo ni Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, mamlaka ya kutunga sheria ambayo ni Baraza la Waakilishi na mamlaka ya utoaji haki ambayo ni Mahkama. Sasa mnavyosema Muungano unawabanabana, mnabanwa nini na mna uhuru wote huo?”

Nikamwambia, kama ungelikuwa katika darsa, ningekwambia sadakta. Kweli Katiba ya Zanzibar imesema tuna mamlaka ya utendaji ambayo ni serikali ya SMZ, kweli Katiba ya Zanzibar inasema tuna baraza la kutunga sheria ambalo ni BLW na kweli Katiba ya Zanzibar imesema tuna chombo cha utoaji wa haki ambayo ni Mahkama. Lakini mamlaka ya utendaji imeachiwa kipi? Ndio nikasema hawa wanatufanya sisi wajinga, lakini “jinga likierevuka, mwerevu yuko matatani!”

Mmetuachia wajibu wa mambo maisha ya kiuchumi ya kukuendeleza wewe Mzanzibari, huo ni wajibu wa serikali ya SMZ. Ndio maana katika SMZ, tukichambua, kuna wizara kama Elimu, Afya, Maji na Ujenzi, Nishati, Ardhi, Mawasiliano na Uchukuzi, Habari, Utamaduni, Biashara, Viwanda, Utalii na Tawala za Mikoa, Ajira, Wanawake na Watoto na Vijana. Haya wao (Serikali ya Muungano) wamejivua; na ukiuliza Bungeni, kule unaambiwa ukaulize Baraza la Wawakilishi.

Hayo ni wajibu wa SMZ, sisemi serikali ya CCM, lakini zile nyenzo za kuendelezea mambo haya, zote wamedhibiti mabwana wakubwa kutoka Tanganyika. Sasa Zanzibar itajiendeleza vipi? Akaniuliza: “Kama yepi yale?” Niliyomjibu, naomba niwasomee na nyiye.

Utaendelezaje uchumi, wakati mambo ya nchi za nje wanayo wao, mikopo na biashara ya nje wanayo wao, kodi ya mapato wanayolipa watu binafsi ushuru wa forodha ushuru wa bidhaa zinazotengeneza hapa nchini zinazosimamia na forodha wanayo wao.

Bandari mambo ya anga Posta na simu wanayo wao.

Mambo yote yanayohusika na fedha kwa ajili ya malipo halali wanayo wao.

Noti, mabenki, shughuli zote za mabenki, pesa za kigeni na usimamizi unaohusika na pesa za kigeni wanao wao.

Leseni za viwanda na takwimu, elimu ya juu wanayo wao.

Maliasili ya mafuta pamoja na mafuta yasiyochujwa na magari na mafuta ya petroli na bidhaa nyengine zitokanazo na mafuta na gesi asilia, hadhira juzi tumeyarejesha wenyewe.

Baraza la mitihani la taifa na mambo yote yanayohusika na baraza hilo wanayo wao.

Usafiri na usafirishaji wa anga wanayo wao. Utabiri wa hali ya hewa wanayo wao, takwim yao.

Hivyo, ukishanyang’anywa mambo yote haya, hivi utaweza kuendeleza elimu hapa, utaweza kuendeleza mawasiliano na barabara?

Wametumaliza, halafu wanatwambia mnalalamika nini! Tunalalamika nini? Tunataka mamlaka yetu mliyoyapora kinyume na sheria na Katiba.

Je, haya wewe mwananchi yanakugusa vipi?  Maendeleo yako, ustawi wako, ukuwaji wa uchumi unategemea nyenzo kuu za uchumi na nyenzo kuu za kuendeshea uchumi ndio hizi nilizozitaja. Kuchambua moja moja tutafika kesho asubuhi. Kwa sasa hivi naomba nichukuwe mifano miwili mitatu tu.

La kwanza, hizi ni nchi mbili; ni kama nilivyosema: suala la uchumi si la Muungano.  Wakati uchumi si suala la Muungano, lakini nyenzo zote kuu za uchumi wanazo wao. Maana yake nini? Chombo kinachoratibu ni Benki Kuu ya Tanzania, hii ambayo wamediriki kutwambia sisi hatuna hisa, lakini Mbunge wetu, Hamad Rashid, alisema kisawa sawa kwamba tunayo hisa na tunashukuru SMZ kwa kutia nguvu maneno ya Hamad Rashid kwa kusema kwamba tunayo hisa.

Lakini tunalosema ni uchumi sio suala la Muungano. Dunia nzima inaeleweka kwamba uchumi wa kisiwa kama Zanzibar na uchumi wa nchi kama Tanganyika ni chumi mbili tafauti. Hata namna ya uendeshaji wake ni tafauti, kwa sababu hata mambo tunayoyategemea kuendesha uchumi wetu ni tofauti. Uchumi wa kisiwa hutegemea bandari, biashara na mambo kama hayo. Uchumi wa nchi kubwa unaweza kutegemea kilimo. Sisi Zanzibar hatuwezi kutegemea kilimo kwa uchumi wetu. Hutokezea sadfa tu zilipokuwepo karafuu. Lakini uchumi wa visiwa hutegemea bandari na biashara.

Lakini leo Benki Kuu ya kutunga na kusimamia fedha na sarafu hawazingatii chumi zote mbili kwa sababu wao weshaweka hili la kiufuta Zanzibar na kuwa na serikali moja. Kwa hiyo, wao wanahudumia uchumi mmoja tu, nayo ni Tanznaia ambayo ni Tanganyika iliyojibadilisha jina.

Matokeo yake wameuuwa uchumi wa Zanzibar. Sera za sarafu na fedha hazizingatii uchumi wa Zanzibar. Matokeo yake wewe mwananchi unakamuliwa kwa mizigo ya kodi. Hapa ulikuwa uwe na viwango nafuu vya kodi ili uweze kuvutia wawekezaji ili serikali iweze kuwa na uwezo wa kukufanya wewe uweze kuwa na maisha mazuri.

Chombo cha pili ni TRA, Mamlaka ya Mapato Tanzania. Mamlaka ya mapato ndio inayokadiria kodi na mapato. Tulikuwa na viwango tafauti vya kodi. Tulikuwa na ushuru nafuu hapa, lakini walihakikisha wanaweka viwango sawasawa. Bandari wameikausha, wameyaua maisha ya wananchi wa Zanzibar.

Hata katika elimu ya juu, uchumi wa Zanzibar hauna namna ya kusomesha wataalamu wake. Wataalamu wake ilikuwa wazingatie mahitaji ya Zanzibar. Mahitaji ya uchumi wa Zanzibar – uchumi wa bandari, uchumi wa biashara, uchumi wa huduma. Vitu vyote vinapangwa wapi? Bara. Baraza la Mitihani liko Bara.

Hiii ni mifano michache. Tutaendelea siku nyengine, lakini ukiona bandari uchumi imekufa imedorora.  Hakuna mzunguko wa fedha, hakuna ajira kwa sababu kila kitu kinachoineemesha Zanzibar kinaamuliwa kule upande wa pili wa bahari. Inaamuliwa kwa lengo la kuikaba koo na kuimaliza Zanzibar na kukumaliza wewe Mzanzibari.

Nataka niwaulize ndugu zangu, mumesikia kisiwa gani duniani maskini zaidi ya Zanzibar na Comoro? Comoro kwa sababu wana mapinduzi kila siku yasiyokwisha, lakini hesabu angalieni Seychelles, angalieni Mauritius, angalieni Hong Kong ambayo imekuwa chini ya ukoloni wa Kiingereza na sasa chini ya China. Angalieni Singapore na nyingi nyingine.

Sisi tunafukarishwa kwa sababu ya kutimizwa njama za Nyerere. Ameziacha hakuzikamilisha na hatazikamilishwa huko tunakokwenda, hasa Wazanzibari tulivyoamka kutetea haki zetu.

Kwa hivyo, waheshimiwa, niteremke kwa kusema kitu kimoja: wanatwambia kwamba katika umoja ukubali kupoteza, sasa Wazanzibari mnapodai haya hamtaki Umoja wa Afrika. Hivyo Uafrika huu na umoja huu ni kwa Zanzibar tu?  Bara la Afrika lina nchi 52. Kwa nini hawajajiunga na Muungano huu mpaka leo? Wamejifunza baada ya Zanzibar kuchukuliwa na Tanganyika, kwamba hakuna nia njema katika Muungano huu, lengo ni kukandamizana.

Na mimi niliwauliza, na leo nawauliza tena, kama umoja wa Afrika tukubali kupoteza tu?  Kwa heshima ya Umoja wa Afrika, Iddi Amini alipoivamia Kagera, kwa nini wakatupiganisha vita wasimuachilie muafrika akaichukuwa Kagera? Walitupiganisha vita nchi nzima, na wajibu wetu kulinda mipaka yetu, wakachukuwa mpaka Zanzibar kwenda kulinda mipaka ya Tanzania. Kwa nini iwe ni kosa kwa Mzanzibari kudai haki ya nchi yake?

Tutatetea mpaka Kiama, na hatutakubali kuona Zanzibar ikichukuliwa.  Mwaka 1968 Nyerere alisema, ikiwa Wazanzibari kwa hiyari yao wenyewe wakiona Muungano huu hauna maslahi kwao na wakaamuwa kujitoa, hatutawapiga mabomu, kama walikuwa na uhuru wa kujiunga wana uhuru wa kujitoa.  Sisi hatusemi tunataka kujitoa katika Muungano. Tunasema tunataka Muungano wa kuheshimiana, utakaoheshimu Tanganyika na Zanzibar sawasawa. Utakaosimamia maslahi ya Zanzibar na Tanganyika sawasawa. Kinyume na hayo watakapoamua Wazanzibari….

 

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s