Aibu Tanzania kutatua migogoro ya wengine, ikashindwa na wa Zanzibar

Kilichotokea nchini Kenya na kupelekea ghasia na mauaji ya zaidi ya watu alfu moja na wengine wengi kukosa makazi, kinashabihiana kabisa na yaliyotokea katika chaguzi mbalimbali zilizowahi kutokea hapa nchini mwetu hasa katika chaguzi za Zanzibar za mwaka 2000 na mwaka 2005. Ni vyema kutambua kuwa, kuendelea kuchezea juhudi za kusuluhisha mgogoro wa Zanzibar kwa kisingizio chochote; na kushindwa kuanzisha mchakato wa katiba mpya utakaoshirikisha Watanzania wote kutengeneza mfumo halali wa kisasa na kiuchumi utakaotoa nafasi sawa kwa makundi yote kisiasa, kijamii na kiuchumi ni sawa na kuchochea mazingira ya machafuko makubwa zaidi hapa nchini mwetu. Hivi hatuoni haya manung’uniko mbalimbali yaliopo?

Mhe. Khalifa Suleiman

Mhe. Khalifa Suleiman

Hotuba ya Khalifa Suleiman Khalifa (Mb), Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani kwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, iliyosomwa tarehe 21 Agosti, 2008, kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hii kwa mwaka wa fedha 2008/2009

Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda kukushukuru kwa kunipa fursa hii ili kutoa maoni ya kambi ya Upinzani kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya wizara ya mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa kwa mwaka wa fedha 2008/2009 kwa mujibu wa kanuni za Bunge kifungu cha 99(7) toleo la mwaka 2007.

Mheshimiwa Spika, Napenda kumshukuru mwenyezi Mungu kwa kutujaalia Afya njema na uzima. Aidha, nachukua fursa hii kuwashukuru wananchi wa jimbo la Gando kwa kuendelea kuniamini na kunipa dhamana hii nzito ya kuwawakilisha katika Bunge hili tukufu.

Mheshimiwa Spika, sina budi kumshukuru kiongozi wa upinzani bungeni Mhe. Hamad Rashid Mohamed na naibu wake Mhe. Dr. Wilbord Slaa pamoja na wabunge wenzangu wote katika kambi ya upinzani, wataalamu wa sera wa vyama vyetu na vijana wasaidizi wetu katika ofisi ya kambi kwa msaada na maelekezo mazuri waliyonipa wakati wa kuandaa hotuba hii.

Mheshimiwa Spika, Kwa niaba ya Kambi ya napenda kukupongeza sana Spika kwa nafasi uliyoipata ya kuwa Rais wa C.P.A. Heshima hii ni yako wewe binafsi, ya Bunge hili na Taifa letu kwa ujumla. Aidha nimpongeze sana Kaimu Katibu wa Bunge na watendaji wake wote kwa kufanikisha ushiriki wetu katika mkutano wa C.P.A Kuala Lumpur, Malaysia. Pia namshukuru sana Balozi Sisko na wasaidizi wake kwa kuwa karibu sana na ujumbe wa nchi yetu ulioshiriki mkutano ule.

USULI

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Mambo ya Nje ni wizara nyeti yenye jukumu kuu la kujenga, kutetea na kulinda taswira ya nchi yetu katika nyanja za kimataifa. Utendaji bora na uliotukuka kinidhamu katika wizara hii ni muhimu sana katika kutekeleza jukumu lake la kuwezesha Taifa letu kuwa na sifa bora katika medani ya diplomasia ulimwenguni na kuweza kutetea maslahi yetu ya kiuchumi na kiusalama.

Hivyo basi tunapenda kulihakikishia bunge hili kuwa daima tupo tayari kusaidia kwa hali na mali mipango yote ya kiutendaji na kimaendeleo ya Wizara hii. Mipango ambayo inalenga kuboresha uwezo watendaji wetu katika kufanikisha majukumu yao.

SERA YA MAMBO YA NJE

Mheshimiwa Spika, wakati tunatambua mabadiliko ya hali ya kisiasa duniani na umuhimu wa sisi kubadilika kiutendaji, vilevile tunaamini kuwa kuna umuhimu mkubwa wa kuendelea kuenzi sifa nzuri tulizojijengea katika nyanja ya diplomasia duniani. Hata hivyo, wakati tunahakikisha kuwa sera ya mambo ya nje ya nchi yetu inaendana na hali na mahitaji ya sasa kisiasa duniani, vilevile tunapaswa kuhakikisha kuwa kamwe hatufanyi kosa la kukiuka ama kudharau misingi tuliyojiwekea kihistoria.

Mheshimiwa Spika, Moja ya misingi hiyo ni kuwasaidia wanyonge wa dunia hii, ama kivitendo pale tunapoweza au kuwaongelea pale tuliposhindwa kutenda. Uthabiti wetu katika kusimamia kidete na kupigania haki za wanyonge duniani umekuwa mfano wa kuigwa na kuweza kutupa nguvu za kimaadili zilizowezesha sauti ya nchi yetu kutambulika na kuheshimika duniani. Kamwe tusiache vishawishi vya maslahi harakaharaka na yenye tija ya muda mfupi kutufanya tufanye makosa ya kuacha misingi mikuu ya Taifa letu kwani hilo litakuwa kosa kubwa la kujutia hapo baadae.

MASUALA YA KIMATAIFA

Uhuru wa Wapalestina

Mheshimiwa Spika, ingawa sera ya nchi ya Mambo ya Nje ya mwaka 2001 inatilia mkazo suala la mafanikio kiuchumi, lakini bado misingi mikuu ya nchi yetu kama vile imani ya kuwa Watanzania ni marafiki wa wanyonge wote duniani bado inabaki pale pale. Kamwe sera hii haikusema kuwa tunapaswa kuwa marafiki wa kila nchi hata kama nchi hiyo inakandamiza uhuru na haki za marafiki zetu kama lifanyavyo taifa la Israel katika ardhi za Wapalestina.

Mheshimiwa Spika, Miaka yote Tanzania imekuwa ndugu wa karibu kwa watu wa Palestina ambao kwa miaka zaidi ya sitini sasa wamekuwa katika wakati mgumu kwenye ardhi yao. Nasikitika kusema kuwa wakati ambapo madhila yanayowapata ndugu zetu wa Palestina bado yanaendelea, tena kwa kasi kubwa kabisa, inaelekea Tanzania imeanza kupoteza dira na mwelekeo katika suala hili. Ukaribu wa kiuchumi, kisiasa na kiusalama unaoendeshwa na baadhi ya viongozi wa serikali yetu na serikali ya Israel, unajenga picha mbaya kwa ndugu zetu wa Palestina na wapinga ukandamizaji wengine duniani. Hali hii inatoa taswira mbaya ya kuhalalisha madhila yanayoendelea kuwapata ndugu zetu wa Palestina.

Mheshimiwa Spika, ni muhimu Waziri wa Mambo ya Nje akatutamkia wazi kama dira ya nchi yetu kuhusu ukombozi wa watu wa Palestina imebadilika, kwa nini na ni kwa kiasi gani.

Hali Mpya ya Ushindani Kiuchumi na Kijeshi kati ya Mataifa Makubwa

Mheshimiwa Spika, Baada ya miaka kadhaa ya kile kilichodhaniwa kuwa mwisho wa siasa za vita baridi, hivi karibuni tumeanza kushuhudia kuibuka upya kwa siasa za aina hiyo kati ya mataifa makubwa yale ya zamani na mengine mapya kama Uchina. Kuibuka kwa taifa la Uchina na kurudi upya kwa taifa la Urusi katika ulimwengu siasa za ubabe wa kiuchumi na kijeshi, kumeifanya dunia itumbukie katika mtihani mpya unaofanana na ule wa enzi za Vita Baridi.

Mheshimiwa Spika, hali hii inatulazimu kuwa makini sana na mahusiano yetu na mataifa haya haswa pale baadhi yao yanapoonyesha dalili za kutaka kutuchagulia marafiki na kutuamulia maadui. Ni wajibu wetu wote kuchukua hatua madhubuti ya kuoanisha wazi misingi ya mahusiano na mataifa haya makubwa kabla ya kujikuta tunaingia katika vita matatizo yasiyo na tija kwetu.

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Mambo ya Nje inapaswa kuanzisha mjadala maalumu kuhusu mahusiano yetu na mataifa makubwa katika mazingira ya sasa. Hili litatuwezesha kupata mawazo na mbinu elekezi kutoka kwa wadau mbalimbali wa masuala ya kimataifa wakiwemo wasomi na watafiti wetu, kuhakikisha nchi yetu inakuwa na dira madhubuti itakayotuwezesha kufanikisha maslahi yetu bila ya kukubali kutumika katika siasa hizi mpya za ushindani haribifu.

Mheshimiwa Spika, Suala la Umoja wa Nchi Zisizofungamana na Upande Wowote (NAM) bado lina umuhimu mkubwa sana kwa sasa. Kwa kushirikiana na wenzetu katika umoja huu tunapaswa kuchukua hatua madhubuti za kupitia upya shughuli na mikakati yake ili kuweza kujipanga upya kuendana na hali ya sasa kimataifa. Wote tunatambua ni jinsi gani umoja huu ulivyoweza kutusaidia katika kulinda na kutetea maslahi yetu duniani wakati wa enzi za vita baridi. Tunamtaka Waziri wa Mambo ya Nje kulieleza bunge lako, kwa undani, ushiriki wa Tanzania katika Umoja huo tangia mwaka 2006 na ni mikakati gani wameiweka kuhakikisha kuwa Tanzania inatumia ipasavyo umoja huu kujijenga, kujilinda na kujitetea katika dunia hii ya ushindani na ubabe mpya wa mataifa makubwa.

Ubabe wa Kivita wa Mataifa Makubwa

Mheshimiwa Spika, tofauti na matumaini ya wengi kuwa kumalizika kwa vita baridi kungeweza kupunguza madhila ya vita duniani, dunia imekuwa ikiendelea kukabiliwa na majanga ya vita mbalimbali. Vita iliyosababishwa na uvamizi wa taifa la Marekani na washirika wake huko Afghanistan na Irak vimeendelea kugharimu maisha ya watu wa nchi hizo na vilevile kuendelea kuathiri hali ya kiusalama duniani. Vita hivi vimepelekea kuathiri mfumo wa biashara na uchumi duniani na kuibua ongezeko kubwa la bei ya mafuta, ongezeko ambalo limeendelea kuathiri hali ya uchumi wa dunia ikiwemo hali za mataifa madogo kiuchumi kama jinsi ilivyo hapa Tanzania.

Tishio la Vita Vingine katika Ghuba ya Uajemi

Mheshimiwa Spika, inasikitisha kuwa wakati hali bado mbaya katika nchi za Irak na Afghanistan, kuna kila dalili kuwa kuna mataifa mawili yanajiandaa kuanzisha vita vingine huko Iran. Taarifa zilizopo ni kuwa tayari makubaliano yamefikiwa kati ya mataifa hayo kufanya uvamizi katika taifa la Iran kabla ya uchaguzi mkuu wa Marekani mnamo mwezi Novemba mwaka huu 2008. Tayari mataifa kadhaa ya Ulaya yameshatoka wazi kupinga hilo na sisi tunaamini kuwa nchi yetu inapaswa kutoa msimamo wake kuhusu hilo kwa uwazi bila ya kutetereka.

Masuala ya Bara la Afrika

Mheshimiwa Spika, hali ya mambo katika bara letu la Afrika bado inaendelea kuzorota. Katika mwaka wa fedha wa 2007/2008 tumeendelea kushuhudia matukio kadhaa ambayo yanaonyesha kukua kwa matendo yanayogandamiza maendeleo ya kidemokrasia na kiuchumi miongoni mwa nchi za kiafrika. Vita na migogoro ya kisiasa inayosababishwa na watawala wasioheshimu misingi ya kidemokrasia na haki za watu wao inaendelea kutaabisha wana wa Afrika na kurudusha nyuma juhudi zao katika kujiletea maendeleo.

Wakati hali ya Somalia inaendelea kuwa mbaya, kumetokea matukio kadha yanayoashiria kuharibika kwa maendeleo ya kupatikana kwa amani katika nchi ya Sudan. Vita bado imekuwa ikiendelea katika maeneo kadhaa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo huku maelfu ya watu wanaendelea kupoteza maisha yao. Burundi ambako tunaambiwa kuwa juhudi zetu zimeweza kurekebisha mambo, bado hali ni tete.

Mheshimiwa Spika, Machafuko na mauaji yaliyotokea nchini Kenya mara baada ya udanganyifu wa matokeo ya uchaguzi wa mwezi Disemba mwaka 2007, ni matukio ya kuvunja moyo wapenda amani na demokrasia duniani kote. Kitendo cha kuingilia utendaji wa tume ya uchaguzi kilichofanywa na viongozi wa chama tawala wakati huo na kupelekea matatizo makubwa kwa ndugu zetu wa Kenya ni kitendo cha aibu na cha kulaaniwa na wapenda amani, maendeleo na demokrasia nchini kwetu na duniani kwa ujumla.

Wakati tunapongeza juhudi za serikali yetu katika kusaidia kuwapatanisha ndugu zetu hao, vile vile tunawatanabaisha wanasiasa wa hapa nchini kusoma makosa ya wenzetu na kuepuka utamaduni wa kukandamiza nguvu za demokrasia. Itakuwa ni fedheha kubwa kama tutaendelea kuwa vinara kusaidia kupatikana kwa amani kwenye nchi za wenzetu, wakati hapa kwetu tunakosa nia thabiti ya kiuongozi kushughulikia viashiria vya kuvunjika kwa amani kama vile ukandamizaji wa demokrasia na ufisadi mkubwa unaojijenga hapa nchini mwetu.

Mheshimiwa Spika, kilichotokea nchini Kenya na kupelekea ghasia na mauaji ya zaidi ya watu alfu moja na wengine wengi kukosa makazi, kinashabihiana kabisa na yaliyotokea katika chaguzi mbalimbali zilizowahi kutokea hapa nchini mwetu hasa katika chaguzi za Zanzibar za mwaka 2000 na mwaka 2005.

Ni vyema kutambua kuwa, kuendelea kuchezea juhudi za kusuluhisha mgogoro wa Zanzibar kwa kisingizio chochote; na kushindwa kuanzisha mchakato wa katiba mpya utakaoshirikisha Watanzania wote kutengeneza mfumo halali wa kisasa na kiuchumi utakaotoa nafasi sawa kwa makundi yote kisiasa, kijamii na kiuchumi ni sawa na kuchochea mazingira ya machafuko makubwa zaidi hapa nchini mwetu. Hivi hatuoni haya manung’uniko mbalimbali yaliopo?

Ukandamizaji wa misingi ya demokrasia na maafa ya kisiasa Zimbabwe

Mheshimiwa Spika, Tunapenda kutambua mabadiliko makubwa ya kimtazamo ya serikali yetu kuhusiana na hali inavyoendelea nchini Zimbabwe kama ambavyo imeelezwa katika taarifa ya hivi karibuni ya Waziri wa Mambo ya Nje. Hata hivyo tunaamini kuwa tumechelewa mno kutoa msimamo huo na sasa hautaweza kubadili hali mbaya na ya hatari wanayokumbana nayo wananchi wa Zimbabwe. Kwa miaka kadhaa sasa Tanzania imekuwa ikionyesha kumlinda Robert Mugabe wakati akiendesha kampeni kubwa ya kukandamiza demokrasia na haki za wananchi wa Zimbabwe.

Mheshimiwa Spika, kuna sababu nyingi za kwa nini kuna umuhimu kwa mataifa ya Afrika kupitia jumuiya zake kama SADC na Umoja wa Afrika kuhakikisha kuwa wanachukua uongozi wa jukumu la kushurutisha utawala wa Zimbabwe kujisahihisha sasa. Miongoni mwa sababu hizo ni:

  • Kuepusha uwezekano wa kuongezeka kwa vitendo vya mauaji ya kimbari ambavyo vikiachiwa kuendelea kuna uwezekano mkubwa wa kufikia ama kuzidi yale yaliyotokea nchini Rwanda mwaka 1994.
  • Machafuko yaliyotokea nchi Afrika Kusini hivi karibuni ni kithibitisho tosha cha athari za hali mbaya ya kisiasa nchini Zimbabwe kwa usalama wa dunia na zaidi usalama wa nchi jirani.

Ni jukumu letu kama viongozi wa Kiafrika kuhakikisha tunachukua hatua muafaka na katika muda muafaka kusahihishana wenyewe, bila ya kutoa mianya kwa mataifa mengine ya nje kutumia kukosekana kwa uthabiti huo wa kiuongozi, kujenga ajenda zao ambazo kwa wakati mwengine huwa hazina manufaa kwetu.

Mheshimiwa Spika, tunapaswa kuwa makini na wakweli katika kusaidia juhudi hizo. Ni muhimu kuhakikisha kuwa demokrasia ya kweli inayotoa haki sawa kwa wote na yenye kuwezesha maendeleo kwa wote ndiyo inakuwa msingi wa dira yetu ya kusaidia kuepusha, kuzuia na kutatua migogoro katika bara letu la Afrika. Hili litafanikiwa zaidi kama tutaonekana wazi tukitekeleza dira hiyo hapa kwetu bila ya kujenga taswira ya uoga na unafiki.

Mheshimiwa Spika, Bara letu limekumbwa na dhuluma mpya ya ukandamizaji wa demokrasia. Viongozi walio madarakani, ama wao binafsi au vyama vyao, hulazimisha kushinda chaguzi na baadaye kusingizia mazungumzo ya kuunda Serikali za mseto. Hii ni hatari sana inayolikabili Bara letu. Tunapaswa kulaani sana mtindo huu, umma unaohitaji mabadiliko si vyema kuulazimisha kuutawala.

USHIRIKIANO/JUMUIYA ZA KIMATAIFA NA KIKANDA

Umoja wa Mataifa (UN)

Mheshimiwa Spika, suala la Mageuzi katika Umoja wa Mataifa linaendelea kuwa moja ya masuala muhimu kwa bara letu la Afrika na nchi yetu kwa ujumla. Taarifa ya kuwa tunaendelea kudai mageuzi katika Umoja wa Mataifa haitoshi. Watanzania wana haki ya kupata taarifa kamili ya hali ya harakati za kudai mageuzi zinavyondelea, ni nini kati malengo ya mageuzi kimefanikiwa, nini ambacho hakijafanikiwa, sababu ni zipi, nini msimamo wa nchi yetu katika hayo na nini ambacho Wizara ya Mambo ya Nje inafanya ili kuhakikisha kuwa mageuzi hayo yanafanikiwa kwa kadiri ya malengo ya nchi zinazoendelea, Afrika na nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, moja ya masuala nyeti ambayo yanaathari kubwa kwa nchi yetu kiusalama ni suala la Mkataba wa Kimataifa wa kukomesha biashara haramu ya silaha ndogondogo na nyepesi. Hili ni suala nyeti sana kwa Taifa ikitiliwa maanani hali ya hatari inayoendelea kujengeka katika maeneo ya mpakani mwa nchi yetu na jukumu zito la kusaidia wakimbizi kutoka nchi jirani zilizoathirika na vita. Ni muhimu kwa Waziri wa Mambo ya nje kulitaarifu bunge lako kuhusu hali ya mchakato suala hili na jinsi gani serikali yetu imeweza kulishughilikia.

Umoja wa Afrika (AU)

Mheshimiwa Spika, ni miaka arobaini na tano sasa tangia Umoja wa Afrika uanzishwe kama COMPROMISE ya ndoto ya kuwa na serikali moja ya bara la Afrika. Historia inaonyesha kuwa baada ya majadiliano marefu kuhusiana na jinsi gani ya kujenga serikali moja ya Afrika, wale waliopigia debe njia ya hatua kwa hatua walishinda wale waliona kuungana moja kwa moja ndio njia muafaka zaidi.

Mheshimiwa Spika, tunaitaka Serikali itoe maelezo yafuatayo:

  • Ni jinsi gani watawashirikisha watanzania katika mchakato huu ikiwa pamoja na kuwaelimisha watanzania kuhusu umuhimu wa kuunda serikali ya Afrika na jinsi gani tunaweza kushughulikia zile zionekanazo kama athari zinazoweza kutokea endapo tutakuwa na serikali hiyo.
  • Nini jinsi gani na kwa gharama gani uanachama wa jumuiya tofauti za kikanda miongoni mwa nchi za kiafrika unaathiri mipango ya kuunda serikali ya pamoja ya Afrika.

Ushirika Wa Kiuchumi na kibiashara kati ya Jumuiya ya Ulaya na Nchi za Afrika, Karibiani Na Pasifiki (EU-ACP)

Mheshimiwa Spika, moja ya nguzo kuu za misaada ya kiuchumi na soko la kibiashara la nchi yetu ni nchi za Jumuiya ya Ulaya. Kwa miaka kadhaa Tanzania tumekuwa tukishirikiana na Jumuiya ya Ulaya katika masuala ya maendeleo ya Uchumi, Biashara na Siasa. Tanzania inafaidika na uhusiano na Jumuiya ya Ulaya kupitia uhusiano wa Kiuchumi kati ya Nchi za Jumuiya ya Ulaya (EU) na Kundi la Nchi za Afrika, Karibeani na Pasifiki (ACP) kupitia Makubaliano ya Cotonou ya mwaka 2000. Moja ya sehemu ya makubaliano hayo yaliyoanza kutekelezwa mwaka 2003 ni mchakato wa majadiliano yanayolenga kubadili mfumo wa mahusiano ya kibiashara kati ya nchi za makundi haya mawili na hatimaye kukubaliana kuhusu Ushirika wa Usawa wa Kibiashara yaani Equal Partnership Agreement (EPA).

Mheshimiwa Spika, katika nchi yetu mchakato wa kupata maoni ya watanzania kuhusu Ushirika wa Kibiashara na Nchi za Umoja wa Ulaya (EPA) ulichelewa kuanza rasmi na pia hata ulipoanza kulikua na kusuasua katika utekelezaji wake. Watendaji wa serikali wamekuwa wakikwepa kusikiliza na kuheshimu maoni ya watanzania kupitia kwa wawakilishi wao bungeni ama kupitia asasi zao za kijamii kama ambavyo Makubaliano ya Cotonou ya 2000 yanavyoshurutisha.

Mheshimiwa Spika, Makubaliano ya Ushirika Sawa wa Kibiashara (EPA) yanahusisha kufungua mipaka yetu na kushindanisha kibiashara sekta zetu za viwanda, kilimo, uvuvi na utoaji huduma kwa usawa na nchi zilizoendelea kiteknolojia na kiviwanda za Ulaya ambazo ni wazi zitadumaza na hata kusambaratisha kabisa ukuaji wa sekta hizo hapa nchini.

Mchakato wa kujitathmini kiutawala, kijamii na kiuchumi-APRM

Mheshimiwa Spika, Kuanzishwa kwa mchakato wa Kujitathmini kiutawala, kijamii na kiuchumi (APRM) hapa nchini ni moja ya hatua muhimu katika kusaidia maendeleo ya kidemokrasia, kijamii na kiuchumi nchini. Chimbuko la mfumo huu wa kujithamini limetokana na mkakati wa NEPAD ambao umelenga kuhakikisha maendeleo ya kidemokrasia kama njia bora ya kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Moja ya njia muhimu ya kufanikisha zoezi hili kwa manufaa ya Watanzania ni kuhakikisha kuwa wale tunaowakabidhi jukumu la usimamizi na utekelezaji wa zoezi hili ni watu makini, waaminifu kwa watanzania na zaidi wenye ujasiri wa kusema yote bila ya woga wala upendeleo. Ni muhimu kuhakikisha kuwa wanaopewa nafasi za kuongoza na kuendesha sekretariati ya APRM ni watu watakaokuwa tayari kusema yote na siyo yale tu wadhaniayo kuwa viongozi wetu ndio wanayopenda wayaseme.

Diplomasia ya mikutano

Mheshimiwa Spika, diplomasia ya mikutano ni moja ya hatua muhimu kwa nchi changa kama zetu kuweza kujijengea mazingira mazuri ya ushawishi katika ajenda za dunia. Taarifa za kitafiti zinaonyesha kuwa nchi zinazokosa nguvu kubwa za kiuchumi na kijeshi kama Tanzania zina nafasi kubwa ya kutumia diplomasia ya mikutano kufanikisha maslahi yake kiuchumi kama vile uwekezaji na utalii. Hata hivyo ili kuweza kufanikisha hayo, nchi hizi zinapaswa kuwa na mikakati mizuri na makini katika utekelezaji wake ama sivyo kuna hatari ya kuishia kuzipa nchi hizo hasara kubwa bila ya faida yoyote.

Moja ya mikutano mikubwa iliyofanyika hapa nchini ni ule wa Kilele cha Leon Sullivan uliofanyika jijini Arusha na Zanzibar kuanzia tarehe 2 hadi 6 Juni 2008. Ni wazi mkutano huu ulifanikiwa sana kwa upande wa ushiriki wa jumla ingawa kukosekana kwa viongozi wakuu wa mataifa mengi ya kiafrika kulileta doa kwa kiasi fulani.

Kwa haraka tumegundua mapungufu yafuatayo ambayo Watanzania wanapaswa kupewa maelezo ya kina na kwa ufasaha ukitilia maanani kuwa kiasi cha shilingi bilioni tano za kodi zao ziliidhinishwa ili kufanikisha malengo ya mkutano huo:

  • Kuhudhuria kwa marais wa nchi sita tu badala ya kumi na moja kama tulivyotaarifiwa na kushindwa kuitika mwaliko kwa viongozi wa nchi zingine zaidi ya thelathini walioalikwa.
  • Mkanganyiko wa mipaka ya kiusimamizi na utekelezaji kati ya watendaji wa serikali ya Tanzania kwa upande mmoja na Leon Sullivan Foundation na Goodworks International Company kwa upande mwingine. Mkanganyiko ambao ulipelekea adha na usumbufu mkubwa miongoni mwa washiriki wa mkutano huo.
  • Kukosekana kwa mazingira mazuri na programu makini iliyohitajika kuwepo ili kuwezesha mijadala ya papo kwa papo kati ya wajasiriamali wa kitanzania na wenzao waliotoka nchi za nje, hali iliyopelekea hasara kubwa miongoni mwa wajasiriamali wetu waliojitokeza kwa ari na nguvu kubwa kushiriki.

CHUO CHA DIPLOMASIA

Mheshimiwa Spika, Chuo cha Diplomasia kilichopo Kurasini jijini Dar es Salaam, ni moja ya taasisi zinazofanya kazi chini ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa. Ni wazi kuwa kutokana na mabadiliko makubwa yanayohusu nyanja za siasa za kimataifa, chuo hiki kinapaswa kuwa chuo kikuu kinachotoa shahada za juu kuhusiana na masuala ya kimataifa na diplomasia. Katika miaka ya karibuni kulikuwa na juhudi za kugeuza chuo hiki kuwa sehemu ya Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam. Tunaamini kuwa juhudi hizo ama zimeshindwa ama zimesahaulika kama ilivyo katika mipango mingine ya serikali yetu. Serikali inapaswa kutoa ufafanuzi kuhusu uwepo wa mpango huo na nini kimefanyika hadi sasa na kama umeshindikana ni nini kilichokwamisha mpango huo?.

Mheshimiwa Spika, ili kusaidia Watanzania kujua maendeleo ya chuo hiki, tunahoji yafuatayo:

  • Ni jinsi gani chuo hicho kinasaidia katika kufanya tafiti mbali mbali na jinsi ambavyo zinasaidia katika kutekeleza mikakati sera yetu ya mambo ya nje.
  • Ni vipi watalamu wa chuo hiki na wale wa chuo kikuu cha Dar es Salaam na vinginevyo wanatumika kushauri maamuzi mbalimbali ya nchi yetu kuhusu siasa na mahusiano ya kimataifa.
  • Ni hatua gani imefikiwa hadi hivi sasa kutatua mkanganyo wa umiliki wa chuo hiki kati ya serikali yetu na ile ya Nchi ya Msumbiji.

Mheshimiwa Spika, kuna umuhimu mkubwa wa kuimarisha vitengo vya upashaji habari katika balozi zetu ili kuweza kuwatambua na kushirikiana na watanzania walioko nje katika juhudi za kujenga, kuendeleza taifa letu. Tunapendekeza Wizara ichukue hatua za mara moja za kubadili utamaduni wa kukwepa kuwa karibu na watanzania walioko nje uliojikita katika balozi zetu nyingi. Hili sio tu ni kukiuka maadili na wajibu wao lakini pia ni sababu kubwa inayofanya watanzania walio wengi kukosa utashi wa kusaidia nchi yao kwa moyo mmoja.

Mheshimiwa Spika, Vile vile tunapendekeza wizara ya Mambo ya Nje kuunga mkono na kuwezesha jitihada za watanzania mbalimbali za kuanzisha asasi za kitaaluma ambazo zitawaunganisha watanzania wenye utaalamu mbalimbali waishio nchi za ughaibuni. Uwepo wa asasi hizi utawezesha wataalamu wetu wanaoishi ughaibuni kukaa pamoja kuandaa mikakati ya kusaidia nchi yao kutoa huduma mbalimbali za kitaalamu nchini. Tukifanya hivi tutaweza kuligeuza tatizo la BRAIN DRAIN na kuwa BRAIN GAIN kama ambavyo wenzetu wa mataifa ya Uchina na India ama hata majirani zetu Rwanda wanavyothibitisha kuwa inawezekana.

UPASHAJI WA HABARI

Mheshimiwa Spika, katika hotuba ya bajeti ya mwaka jana (2007/08) Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Nje alilitaarifu Bunge lako kuwa wizara yake imefungua tovuti yake tangu mwezi mei, 2007. Tovuti inayopatikana kwa anwani  www.mfaic.go.tz.

Mheshimiwa Spika, kama ilivyo katika tovuti nyingi za asasi za umma, tovuti hii ambayo imetumia mamilioni ya fedha za walipa kodi wa Tanzania imekuwa inakosa uangalizi. Tovuti hii ambayo ni muhimu kwa Watanzania walio ndani na nje ya nchi kujua kinachoendelea nchini mwao na miono ama misimamo ya serikali yao kuhusu masuala mbalimbali yanayoendelea ulimwenguni, imebaki na habari za tokea mwaka jana bila ya kuboreshwa kwa muda mrefu.

Mapitio ya Bajeti zilizopita

Mheshimiwa Spika, katika mkutano wa bajeti ya mwaka 2007/08 tulihoji masuala kadhaa yahusianayo na mapato na matumizi ya fedha za bajeti ya wizara hii. Miongoni mwa mambo ambayo wabunge wengi walihoji ni kuhusiana na hati zenye shaka na zisizoridhisha ambazo balozi zetu kadhaa zilipewa katika ripoti ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali.

Mheshimiwa Spika, katika ripoti ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali inayoonyesha hali ilivyo hadi mwezi june 2007, inaonyesha masuala kadhaa ambayo wizara imeshindwa kuyashughulikia. Masuala hayo ni kama yafuatayo:

a) Matumizi ya kiasi cha shilingi 1,531,278,729 za ruzuku ambazo hazijatolewa maelezo.

b) Masurufu yasiyorejeshwa kabisa na yasiyorejeshwa kikamilifu ya jumla ya shilingi 13,819,000/-,

c) Karadha za samani kwa maafisa wa balozi zisizorejeshwa za shilingi 71,832,169/-

d) Kutokubaliana na makusanyo ya maduhuli katika balozi ambazo kiukaguzi yanaonekana kuwa pungufu kwa shilingi 689,084,355/-

e) Tofauti za matumizi zisizosuluhishwa kiasi cha shilingi 169,309,325/-

Mheshimiwa Spika, jumla ya fedha za walipa kodi ambazo matumizi yake yanahojiwa ni shilingi 2,475,323,578. Hiki ni kiasi kikubwa sana cha fedha na ni wajibu wa mheshimiwa waziri kuwaeleza wawakilishi wa wananchi hapa bungeni ni kwa nini masuala hayo hayakushughulikiwa na hadi sasa wamechukua hatua gani kutimiza wajibu wao.

Mheshimiwa Spika, katika ripoti hiyo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya mwezi june, 2007 inaonyesha kuwa balozi nane zimepata hati yenye kutia mashaka na balozi moja ya Cairo, Misri ambayo imepata hati isiyoridhisha. Balozi zilizopata hati yenye mashaka ni Bujumbura-Burundi, Kampala-Uganda, New York-Umoja wa Mataifa, Washington-Marekani, Abuja-Nigeria, Kinshasa-Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo, Lilongwe-Malawi na Roma-Italia.

Mheshimiwa Spika, ukiangalia ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya mwezi june, 2007 inaonyesha kuwa kuna jumla ya shilingi 1,432,752,626/- ambazo zimetumika katika masuala mbalimbali katika balozi nane, ambayo yanatia shaka na bila ya kufuata kanuni za fedha za serikali. Kwa kifupi matumizi ya zaidi ya shilingi 1,432,752,626/- yanaonyesha dalili za ufisadi kwa balozi hizo chache. Kati ya hizo jumla ya shilingi 249,362,148/- za walipa kodi wa Tanzania zimetumika katika balozi za Bujumbura, New York, Kinshasa na Lilongwe bila idhini ya bunge hili. Na jumla ya shilingi 192,051,370/- zimetumika katika ubalozi wa Cairo-Misri katika hali isiyoridhisha.

Mheshimiwa Spika, wakati tunasubiri ripoti ya mwaka 2008. Kambi ya upinzani inamtaka waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kutoa maelezo kamili ya hatua zilizochukuliwa na wizara yake kushughulikia matumizi haya ya jumla ya shilingi 4,100,127,574/- zilizotumika katika bajeti za mwaka 2005/06 na 2006/07 ambayo yana dalili za kifisadi. Haya ni yale yahusianayo na balozi zetu tu.

Mheshimiwa Spika, tunasikitika kusema  wakati watu wengine wanaharibu fedha nyingi namna hii, zipo balozi zenye shida kubwa sana hasa ikitiliwa maanani kuwa ndiyo kwanza zimeanzishwa.

PASPOTI KATIKA AFISI ZETU ZA KIBALOZI

Mheshimiwa Spika, lipo tatizo katika baadhi ya Afisi zetu za ubadilishaji wa Passport kwa raia wetu wanaoishi nchi za nje . Kimsingi suala  hili ni la Mambo ya Ndani lakini linatekelezwa na Afisi zetu za kibalozi. Watu wanasumbuliwa  pasipo sababu. Hivi Waziri anasemaje juu ya hali hii?

Mheshimiwa Spika, katika miaka ya karibuni serikali ilitoa fedha kwa ajili ya ununuzi wa mitambo ya kisasa ya kutengenezea visa ambayo ilipaswa kupelekwa katika balozi zetu mbalimbali. Tunamtaka waziri atutaarifu kuhusu masuala kadhaa katika hili;

a) Ni balozi ngapi na zipi ambazo zimepokea fedha za kununulia mitambo hiyo na jumla ya shilingi ngapi zilitengwa kwa zoezi hilo na ngapi zilikabidhiwa katika balozi hizo.

b) Ni balozi ngapi ambazo zimeanza kutumia mitambo hiyo mipya na kati ya hizo ni ngapi ambazo bado hazijatumika kikamilifu.

c) Jinsi gani matumizi ya mitambo hiyo mipya ya gharama kubwa imeweza kuboresha makusanyo ya fedha za visa.

Mheshimiwa Spika, kabla ya kuruhusu matumizi ya mabilioni mengine ya walipa kodi wa Tanzania, tunamtaka mheshimiwa waziri atekeleze wajibu wake kwa kuwapasha watanzania kuhusu matumizi yanayotia shaka na yasiyoridhisha. Matumizi ambayo ama hayajafuata viwango visivyo kamilifu vya uhasibu ama vina dalili za ufisadi.

Mheshimiwa Spika, Kabla ya kuhitimisha hotuba hii tunaomba Mhe. Waziri alieleze Bunge hili juu ya yaliyompata Diwani Mhe. Amina Mahmood Waziri diwani wa Kinondoni anayetuhumiwa kughushi umri na kunyimwa VISA na Ubalozi wa Marekani. Tunapenda kuelewa zaidi ni kashfa ya fedha Dola za Marekani elfu sita (6000) ambapo inasemekana alizipata isivyo halali. Nini hasa kilitokea, Jee alichukua kweli? Jee baadae alizirejesha au vipi?  Na yule aliyemsaidia Diwani huyo katika kughushi umri ni hatua gani za kisheria na kinidhamu dhidi yake zimetumika?

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha

…………………………………………………

KHALIFA SULEIMAN KHALIFA (MB)

Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.

21.08.2008

Tafadhali tutumie maoni yako kuhusu hotuba hii

Advertisements