Wazanzibari wana shaka za mkubwa kummeza mdogo

Wakili Ussi Khamis Haji

Wakili Ussi Khamis Haji

“Ninaeleza haya kwa sababu ya hila inayofanywa kwa makusudi kudhoofisha uhuru na madaraka ya Zanzibar hata katika yake mambo yasiyokuwa ya Muungano. Katika makubaliano ya Muungano ya 1964 kuna mambo 11 yaliyoorodheshwa kuwa ni ya Muungano.  Hayo tunaweza kusema ndiyo waliyokubaliana Rais Nyerere na Marehemu Mzee Karume.  Katiba ya muda ya mwaka 1965 yaliongezeka na kuwa 12 na Katiba ya 1977 yalizidi na kufikia 17. Mambo mengi hufanywa ya Muungano na Sheria nyingi hutungwa na Bunge na kufanya zitumike na Zanzibar bila ya mashauriano na Zanzibar.  Mpaka hapo Zanzibar inapopinga kufanywa mambo bila ya kushauriwa ndipo utaona Mawaziri kutoka Dar es Salaam wanakutana na wenzao wa Zanzibar kufanya “sulhu.”

Maoni ya binafsi ya Wakili Ussi Khamis Haji tarehe 30 Agosti, 1983, kwa Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi kuhusu Mapendekezo ya Marekebisho ya Katiba

MAONI KUHUSU MAPENDEKEZO YA MAREKEBISHO YA KATIBA

Nina heshima kuwasilisha pamoja barua hii maoni yangu binafsi kuhusu Mapendekezo ya Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi kuhusu Marekebisho ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano na Katiba ya Zanzibar.

(Ussi Khamis Haji)

Nakala:

Afisi Kuu ya CCM

Zanzibar.

KUIMARISHA MUUNGANO

Katika Utangulizi (Preamble) wa Makubaliano ya Muungano baina ya Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya watu wa Zanzibar ya 1964, imeelezwa:

“KWA VILE Serikali ya Jamhuri ya Tanganyika na Serikali ya Watu wa Zanzibari kwa kuzingatia mashirikiano ya muda mrefu ya watu wa nchi hizi na kushikamana kwao kidugu na urafiki, na kwa sababu ya uchu wa kuendeleza na kuimarisha mashirikiano hayo na kuendeleza umoja wa watu wa Afrika wamekutana na kuzingatia kuunganisha Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya watu wa Zanzibar.”

Maelezo haya yanatosha kutufahamisha kuwa Marais wetu waliamua kuunda Muungano baina ya Tanganyika na Zanzibar kwa shabaha kubwa, ya kuendeleza mashirikiano ya muda mrefu na udugu baina ya watu wa Tananyika na watu wa Zanzibar na kuimarisha umoja wa watu wa Afrika.  Na bila ya shaka Marais hao walikubaliana kuunda Muungano huu kwa faida ya wananchi wa kila upande, Tanganyika na Zanzibar, sasa ni kiasi cha muda wa miaka 20 ya Muungano na Muungano huo. Ili wananchi, hasa wananchi wa Zanzibar waweze kutoa maoni yao kuhusu mapendekezo ya kuimarisha na kuona kama ile dhamira na shabaha iliyokusudiwa imepatikana na ikiwa makubaliano ya muungano ya 1964 yalitekelezwa kama ilivyokusudiwa.

Tunaweza tukafahamu kwa nini mara baada ya Rais Karume kutia sahihi Makubaliano ya Muungano ya 1964, kulikuwa na haja ya kuweka utaratibu wa muda kuendesha shughuli za chombo kipya cha muungano na serikali ya Zanzibar na Serikali ya Tanganyika mpaka hapo utaratibu wa kudumu utakapowekwa.

Na moja ya utaratibu huo wa muda uliowekwa ni (1) kuifanya Katiba ya Tanganyika iwe Katiba ya Jamhuri ya Muungano na huku ikifanyiwa mabadiliko yanayofaa ili kutimiza yale yaliyotakiwa na (2) kuyakabidhi madaraka ya kuendesha mambo ya Tanganyika yasiyokuwa ya Muungano katika Bunge na Serikali ya Jamhuri ya Muungano.  Mambo hayo au utaratibu huo ulikusudiwa kuwa ni wa muda mpaka hapo Katiba ya Jamhuri ya Muungano itakapopitishwa.  Kifungu cha (ii) cha Makubaliano ya Muungano ya 1964 kinaposema:-

“Katika kipindi tokea kuanza Muungano mpaka hapo Baraza la kupitisha Katiba lililotakiwa liundwe katika kifungu cha (viii) litakapokutana na kupitisha Katiba ya Jamhuri ……….”

Kilitarajia Katiba hiyo ya Jamhuri ya Muungano ingekuwa na vifungu vinavyoelezea wazi wazi utaratibu wa kudumu wa kuendesha shughuli za Serikali ya Jamhuri ya Muungano, Serikali ya Tanganyika na Serikali ya Zanzibar, kila moja kwa upande wake.

Kifundu cha (vii) cha Makubaliano ya Muungano ya 1964 kimeelekeza kuundwa kwa Tume ya Katiba ili kutoa mapendekezo ya Katiba kwa ajili ya kujadili mapendekezo ya Tume hiyo na kupitisha Katiba ya Jamhuri ya Muungano.  Hili ni sharti la msingi sana ili kuweza kuipata hiyo Katiba ya Jamhuri ya Muungano.

Ni jambo la kusikitisha kuona sharti hili muhimu halikutekelezwa.  Kwa sababu hiyo njia nyengine yoyote iliyofuatwa au itakayofuatwa na Katiba yoyote itakayopitishwa nje ya Tume ya Katiba iliyotakiwa iundwe chini ya mkataba wa Muungano inakuwa ni kinyume na utaratibu na hiyo Katiba yenyewe inakuwa ni batili na haiwezi kusimama kisheria.  Hili ni kosa kubwa sana lililotendeka na lazima tukubali kuwa kosa hilo limetendeka.  Njia pekee iliyobaki kwa sasa ni kujisahihisha na kurejea kuyatekeleza Makubaliano ya Muungano ya 1964 kwa kuunda Tume ya Katiba itakayotoa mapendekezo ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano kama ilivyokusudiwa.

Hatutakuwa wa kweli kama tutazungumzia kuimarisha Muungano ikiwa sisi wenyewe tunakwenda kinyume na Makubaliano ya Muungano ambao sasa tunasema tuuimarishe.

Kuhusu kuendeleza mashirikiano na kuimarisha mshikamano wa kidugu wa wananchi wa Tanganyika na wananchi wa Zanzibar na kuendeleza Umoja wa Watu wa Afrika, ingefaa Halmashauri Kuu ya Taifa kupima na kuzingatia kwa makini kuona kiasi gani katika mas – ala haya tumefanikiwa.  Muungano wa aina yoyote lazima awali ya yote ulete faida kwa kila nchi iliyomo katika Muungano huo.  Lakini uchunguzi wa makini ukifanywa juu ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar utaonesha kuwa sio tu haukufanikisha shabaha na malengo yaliyokusudiwa bali umetoa manufaa na faida kwa upande mmoja tu, Tanganyika.

Makubaliano ya Muungano ya 1964 yaliunda Jamhuri ya Muungano na Serikali yake kwa kushughulikia mambo ya Muungano ambayo yaliorodheshwa.  Wakati huo huo shughuli zisizokuwa za Muungano ambazo zinahusu Tanganyika tu, pia zilikabidhiwa Serikali na Bunge la Jamhuri ya Muungano.  Katiba ya 1977 imetamka kwamba Tanzania ni Jamhuri ya Muungano (hili nalo ni kosa kubwa kwa mujibu wa Makubaliano ya 1964).  Hali ilivyo hivi sasa ya kuifanya serikali ya Jamhuri ya Muungano pia iendeshe zile kazi zisizokuwa za Muungano zinazohusu Tanganyika tu, imesababisha  upande mmoja wa Muungano, Tanganyika kupata manufaa makubwa ya Muungano kwa hasara ya Zanzibar. Na kila tunavyoendelea katika hali hiyo ndiyo Tanganyika inavyofaidika na Zanzibar inavyopata hasara na kudhoofika kisiasa, kiuchumi, kimila na hata kiutamaduni.

Ingawa ziko shughuli za Muungano zilizoorodheshwa mbali, lakini shughuli za madaraka mbili, yaani zile za Muungano na zile za Tanganyika huchanganywa na kuendeshwa kwa pamoja na chombo kimoja kwa jina la Tanzania, kunaleta hali ya kutatanisha. Halikadhalika kuna mtindo wa kuwafanya Mawaziri wa Tanganyika wanaoshughulikia mambo yasiyokuwa ya Muungano kuwa ni Mawaziri wa Muungano na hata Mawaziri hao kufika kuzungumzia mas-ala ya kazi zao kwa niaba ya Tanzania nzima ndani au wanapotoka nje ya Tanzania Kwa kutumia jina la Tanzania, misaada, mikopo, ruzuku n.k. hutolewa na hupokelewa kwa ajili ya Jamhuri ya Muungano, lakini mambo hayo inaishia Tanganyika, Zanzibar haifiki.  Zanzibar inapojaribu kutafuta njia ya kupata mikopo au misaada kutoka nje, huwa haipati chochote kwa sababu ama huambiwa kuwa Tanzania imekwishapata au kutokana na vikwazo vinavyowekwa na Wizara ya Fedha Dar es Salaam.

Kikwazo kimoja wapo kikubwa ni kuwa mkopo wowote unaotolewa na nchi ya nje kwa chombo chochote Tanzania ikiwemo Zanzibar, lazima ukubaliwe na Hazina, Dar es Salaam.  Mara nyingi kibali hicho huwa hakitolewi.  Iko mifano mingi  kuhusu suala hili.  Lakini inatosha kusema kuwa wakati mmoja aliyekuwa Waziri wa fedha, Ndugu Amir Jamal katika mkutano huko Ikulu Dar es Salaam 1981 ambao uliitishwa na Makamo wa Rais na kuhudhuriwa na Mawaziri wa Fedha na Mipango wa Bara na Zanzibar kwa wkati huo na Mkuu wa benki kuu ya Tanzania alikubali kuwa Zanzibar inapata taabu sana kupata mikopo kutoka nchi za nje kwa sababu ya vizuizi vinavyowekwa na Wizara ya Fedha, Dar es salaam.  Ingawa Ndugu Jamal aliahidi kuchukua hatua ya kuviondosha lakini mpaka sasa halikufanyika lolote na hali iko vile vile.

Zanzibar halikadhalika haishirikishwi katika jambo lolote litolewalo kwa jina la Tanzania, si ruzuku, si mikopo, si misaada.  Jambo dogo ni vifaa vya michezo vinavyotolewa na nchi na mashirika mbali mbali ya nje kwa ajili ya kukuza michezo Tanzania.  Misaada hiyo huishia Dar es Salaam na wanaohusika hata habari hawana kama Zanzibar nayo ni sehemu ya Tanzania na ina haki sawasawa kama Tanganyika.  Ikitokea Zanzibar kushirikishwa, basi ni kupokea Wageni ambao huwa wamekwishafanya mazungumzo na kutoa ahadi ya misaada huko Dar es Salaam.  Na wageni wengi huwa wa vyama vya kijamii kutoka nchi za mashariki.

Hali hii imetoa sura mbaya sana na kuwafanya Wazanzibari kuona kuwa Muungano huu ni kwa faida ya Tanganyika tu, na Zanzibar imewekwa kama ngazi ya kuiwezesha Tanganyika kuvuna matunda ya Muungano.  Wazanzibari wanahisi kuwa wenzetu Watanganyika hawaoneshi hata kidogo kuwa wanayo hisia na dhamiri ya kufikia shabaha na malengo ya kuendeleza mashirikiano na kuimarisha mshikamano wa kidugu kama ilivyoelezwa katika dibaji ya Makubaliano ya Muungano.

Ikiwa msimamo wa Tanganyika kwa Zanzibar ambayo ni mshiriki wenzake katika Muungano ni kama huo ulioelezwa, ni wazi kabisa kuwa Wazanzibari wanawaangalia jamaa wa Tanzania Bara (kama inavyojiita hivi sasa) kwa wasiwasi mkubwa na daima mawazo ya mkubwa kummeza mdogo hayatawaondokea.  Kutokana na maelezo hayo itaonekana kuwa ile dhamira na shabaha ilivyoelezwa huko nyuma haikufikiwa hata kidogo.

Wananchi wa Zanzibar wanataka sana Muungano uendelee kwa faida ya watu wa nchi mbili na kwa ajili ya kuendeleza Umoja wa Afrika.  Lakini lazima ifahamike kuwa Muungano huo ni wan chi mbili huru zenye haki sawa na zenye madaraka kamili ya kujiamulia mambo yake wenyewe.  Kwa hivyo njia pekee ya kuimarisha Muungano ni :-

(a) Kutekeleza vilivyo na kuheshimu Makubaliano ya Muungano ya 1964.  hii ni pamoja na kuunda ile Tume ya Katiba iliyotakiwa iundwe na kuitisha Baraza la Katiba ya Jamhuri ya Muungano kama ilivyoelekezwa katika mkataba wa Muungano.

(b) Katiba hiyo iweke mfumo wa Shirikisho kamili ndani yake mkiwa na Serikali ya Shirikisho, Serikali ya Tanganyika na Serikali ya Zanzibar.

(c) Katiba iainishe kinaganaga shughuli za Serikali  ya Shirikisho, shughuli za Serikali ya Tanganyika na shughuli za Serikali ya Zanzibar, kila moja upande wake.

(d) Kila upande wa Muungano huo wa Shirikisho uwe na madaraka na mamlaka kamili ya kuendesha shughuli zake zote zilizomo chini ya mamlaka yake bila ya kuingiliwa na chombo chochote kutoka sehemu yoyote. Kwa ajili hii suala la Chama kuwa na Madaraka ya mwisho haliwezi kuwa na nafasi katika mfumo wa Muungano wa Shirikisho.

Kwa sababu uwezo wa Chama siku zote utaingilia uhuru na madaraka ya kuendesha shughuli za Serikali iliyomo katika Shirikisho na hivyo kudhoofisha na hatimae kuondosha kabisa uwezo wa Serikali ya nchi hiyo wa kuendesha mambo yake yasiyokuwa ya Serikali ya Shirikisho.

(e) Katiba hiyo ya Shirikisho itoe madaraka kamili kwa kila upande kushirikiana na kutiliana sahihi na nchi yoyote kwa jambo lolote linalohusu shughuli zake zisizohusu Shirikisho bila ya kuekewa kikwazo au kizuizi chochote.

(f) Kuwe na utaratibu mzuri unaoeleweka wa kugawana mikopo, ruzuku na misaada inayotolewa kwa ajili ya Jamhuri ya Tanzania.  Sio ile itolewayo kwa ajili ya Serikali ya Tanganyika au Zanzibar.

(g) Shughuli za Shirikisho zitekelezwe na wananchi wa kila upande wa Shirikisho.  Kuwe na usawa wa kugawana madaraka na kuteua watumishi katika kazi za Shirikisho kwa nchi zote mbili.  Mpango wa haraka utengenezwe ili kuwatayarisha Wazanzibari kushika madaraka katika utumishi wa Muungano.

(h) Shughuli za Shirikisho zitekelezwe na Serikali ya Shirikisho ambayo itakuwa na Baraza la Kutunga Sheria la Shirikisho ambalo litakuwa na Wajumbe idadi sawa kutoka kila upande watakaochaguliwa na Bunge la Tanganyika kwa upande wa Tanganyika na Baraza la Wawakilishi kwa upande wa Zanzibar.

Pamoja na mashauri hayo yaliyoelezwa hapo juu, kuna mambo mengi muhimu sana ambayo Tume ya Katiba italazimika kuyaangalia na kuyaingiza katika mapendekezo ya Katiba.

Sikubaliani na pendekezo la Halmashauri Kuu ya Taifa ya kuunda Tume ambayo pamoja na mambo mengine itakuwa na kazi ya kupendekeza miongoni mwa mambo yale yasiyokuwa bado ya Muungano, ni yapi, kama yakiwekwa chini ya Muungano yataweza kuimarisha zaidi umoja wetu.

Muungano huo wa Shirikisho ambao utarejesha mashirikiano, umoja na kidugu na kuaminiana baina ya watu wa Tanganyoka na watu wa Zanzibar, ni muungano wa nchi mbili huru kila moja yenye madaraka kamili ya kujiamulia mambo yake wenyewe.  Nchi hizo ndizo pekee zenye haki ya kuamua ni mambo gani yawekwe chini ya Serikali ya shirikisho na yapi yatatekelezwa na kila Serikali kwa upande wake.  Madaraka ya kutekeleza shughuli za Zanzibar na kwa ajili ya Zanzibar yako chini ya Serikali ya Zanzibar na Baraza la Wawakilishi ambalo ni mwakilishi wa wananchi wa Zanzibar.  Kwa hivyo kauli ya mwisho ya kuamua shughuli gani iingie katika Muungano itolewe na Baraza la Wawakilishi.

Ninaeleza haya kwa sababu ya hila inayofanywa kwa makusudi kudhoofisha uhuru na madaraka ya Zanzibar hata katika yake mambo yasiyokuwa ya Muungano. Katika makubaliano ya Muungano ya 1964 kuna mambo 11 yaliyoorodheshwa kuwa ni ya Muungano.  Hayo tunaweza kusema ndiyo waliyokubaliana Rais Nyerere na Marehemu Mzee Karume.  Katiba ya muda ya mwaka 1965 yaliongezeka na kuwa 12 na Katiba ya 1977 yalizidi na kufikia 17. Mambo mengi hufanywa ya Muungano na Sheria nyingi hutungwa na Bunge na kufanya zitumike na Zanzibar bila ya mashauriano na Zanzibar.  Mpaka hapo Zanzibar inapopinga kufanywa mambo bila ya kushauriwa ndipo utaona Mawaziri kutoka Dar es Salaam wanakutana na wenzao wa Zanzibar kufanya “sulhu.”  Miongoni mwa mifano mizuri ni sheria za Leseni za viwanda, sheria ya Juwata, na sheria ya kuunda Bodi ya Biashara za nje.

Ni jambo la kujiuliza vipi jina la Jamhuri ya Tanzania hutumiwa kwa kufungiana mikataba na nchi za nje bila ya Zanzibar kushauriwa na wakati mikataba hiyo kwa mujibu wa mfumo ulivyo inaifunga na Zanzibar.  Haya yote bila ya shaka yanafanywa ili kupunguza uwezo wa Serikali ya Zanzibar katika kuendesha mambo yake au kwa kuichukulia kuwa Zanzibar katika kuendesha mambo yake au kwa kuichukulia kuwa Zanzibar ni Mkoa au Wilaya ya Tanganyika.  Njia pekee ya kurebisha makosa yaliyotokea ambayo yamewafanya watu wa Zanzibar kuifikiria Bara inawameza ni kwa kila nchi, Tanganyika na Zanzibar kuwa na Serikali yake itakayoendesha mambo yake yote ambayo hayamo katika Muungano huo wa Shirikisho bila ya kuingiliwa. Hiyo  ndiyo njia pekee inayoweza kuimarisha Muungano ikawa kweli tunayo nia ya kuimarisha Muungano.

KUIMARISHA UWAKILISHI WA WAKULIMA NA WAFANYAKAZI

Suala hili ni la msingi sana hasa tukitambua kuwa demokrasi ya kweli ni ile siyo tu inayotambua bali inayotimiza kwa vitendo itikadi kuwa wananchi ndio wenye kauli ya mwisho katika Serikali na Taifa lao.  Kwa hivyo Baraza la Wawakilishi la Zanzibar likiwa ndio chombo pekee kinachowakilisha wananchi liwe na idadi kubwa zaidi ya Wajumbe waliochaguliwa na wananchi wenyewe moja kwa moja katika uchaguzi.

Hapa vile vile ningeongeza kuwa kila mwananchi anayo haki kamili ya kushiriki kikamilifu katika kujadili na kufikia uamuzi katika mambo ya kitaifa.  Katika dibaji za Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya 1977 na Katiba ya Zanzibar, 1979 imeelezwa:-

“Kwa kutumia vikao vilivyowekwa, kila raia anayo haki ya kushiriki kwa ukamilifu katika kufikia uamuzi wa mambo ya Taifa na yanayomhusu”.

“Kuheshimu na kuthamini utu wa kila binaadamu pamoja na haki zake nyengine.”

“Kuhakikisha kwamba katika nchi hakuna namna yoyote ya dhulma, vitisho, ubaguzi, rushwa, uonevu au upendeleo”.

Ikiwa mwananchi hatapewa nafasi ya kugombea uchaguzi wa Baraza la Wawakilishi na hata ule wa Rais kwa sababu yeye si mwanachama wa CCM au si mwmachama hai wa CCM, atakuwa ananyimwa haki yake ya kushiriki katika kufikia uamuzi wa mambo ya taifa katika Baraza la Wawakilishi ambalo ni moja ya vikao vilivyowekwa kutumwa na wananchi.  Halikadhalika mwananchi huyo atakuwa hakuheshimiwa na kuthaminiwa kwa utu wake pamoja na haki zake na pia atakuwa amedhulimiwa, amebaguliwa na ameonewa kwa sababu ya kuwa si mwanachama wa CCM.

KUIMARISHA MADARAKA YA BUNGE

Ninakubaliana na mapendekezo ya Halmashauri Kuu ya Taifa kuhusu kuimarisha madaraka ya Bunge. Mapendekezo hayo hayo yawe kwa kuimarisha madaraka ya Baraza la Wawakilishi. Lakini mara nyingi inatokea kuwa katika kuiuliza Serikali maswali mbalimbali, na hasa katika kujadili utekelezaji wa kila Wizara wakari wa kikao cha Bajeti, Mawaziri hutoa ahadi nyingi kwa lugha fasaha na tamu sana.  Kwa mfano, Waziri husikika akisema Wizara yangu itachunguza suala hilo na kutoa taarifa, au Wizara yangu itachukua hatua ifaayo au Wizara yangu itaangalia na kuona jambo hilo halitokei tena au Wizara yangu itasimamia n.k. lakini mara baada ya Kikao cha Baraza la Wawakilishi halikubali kama ilivyokuwa na ahadi za Mawaziri zinabakia katika Hansard tu.

Hakuna mtu au chombo kinachofuatilia na kuona kuwa ahadi zilizotolewa na Mawaziri zimetekelezwa na kama zimetekelezwa, kwa kiasi gani.  Kwa hivyo ninapendekeza kuundwe Kamati ya Baraza la Wawakilishi ya Ahadi za Serikali ambayo itafanya kazi ya kufuatilia ahadi zote za Serikali zilizotolewa katika Baraza la Wawakilishi na kuona kuwa ahadi hizo zinatekelezwa kama zilivyotolewa.

Njia nyengine ambayo ni nzuri sana ya kuimarisha madaraka ya Baraza la Wawakilishi ni kulipa uwezo Baraza la Wawakilishi kumhoji Waziri yeyote ndani ya ukumbi juu ya vitendo vyake pamoja na kupiga kura ya kutokuwa na imani kwa Waziri huyo au kwa Baraza la Mawaziri ikiwa litahisi kuwa Waziri au Baraza la Mawaziri limeshindwa kutekeleza majukumu yake au vitendo vyake havilingani na madaraka yake.  Uwezo kama huo utolewe kwa Bunge la Shirikisho kuhusu Mawaziri wa Serikali ya Shirikisho na Rais wa Muungano wa Shirikisho na Makamo wake.  Ninapendekeza vile vile kuwe na utaratibu unaowapa uwezo wananchi na kumwondosha Mwakilishi wao katika Baraza la Wawakilishi ikiwa vitendo au uwakilishi wake unakwenda kinyume na maslahi na matakw yao.

MGAWANYO WA MADARAKA YA RAIS

Kwa kuwa zitakuweko Serikali tatu katika jamhuri ya Shirikisho, Serikali ya Shirikisho, Serikali ya Tanganyika na Serikali ya Zanzibar ninapendekeza kama ifuatavyo:-

1. Serikali ya Shirikisho iongozwe na Rais wa Shirikisho akisaidiwa na Makamo wa Rais wa Shirikisho.  Rais wa Shirikisho achaguliwe na wananchi, katika uchaguzi huo itizamwe asilimia ya wapiga kura waliopiga kura Tanganyika na waliopiga kura Zanzibar mbalimbali.  Ikiwa mgombea amepta zaidi ya nusu ya kura za watu waliopiga kura katika uchaguzi huo wa Rais kutoka kila upande wa Shirikisho, mtu huyo ahesabiwe kuwa amechaguliwa.  Lakini ikiwa ameshindwa kupata zaid ya kura katika sehemu moja wapo, basi ahesabiwe hakuchaguliwa.

2. Rais huyo wa Shirikisho aunde Serikali ya Shirikisho na kuteua Mawaziri wa Shirikisho pamoja na Makamo wa Rais wa Shirikisho.  Maofisa Wakuu, kwa mfano Makatibu Wakuu, Wakurugenzi, Mameneja Wakuu, Wakuu wa Wizara, Idara katika utumishi wa Shirikisho wateuliwe na Rais wa Shirikisho.

3. Uchaguzi na uteuzi wa Rais wa Shirikisho na Makamo wake ufanywe kwa kupokezana kama kinavyoeleza kifungu cha 12(1) na (2) cha Katiba ya Muungano ya 1977.

4. Serikal za Tanganyika na Zanzibar kila moja iongozwe na Rais wake ambae kila mmoja ataunda Baraza lake la Mawaziri katika nchi yake.  Marais hao pia waingie katika Baraza la Mawaziri katika nchi yake.  Marais hao pia waingie katika Baraza la Mawaziri la Serikali ya Shirikisho kutokana na dhamana zao.

5. Serikali ya Shirikisho itawajibika kujibu hoja mbele ya Bunge la Shirikisho na Serikali za Tanganyika na Zanzibar zitawajibika kujibu hoja mbele ya Baraza  la Kutunga Sheria la nchi inayohusika.

Ninasisitiza kuwa Tume ya Katiba  iliyotajwa  katika Makubaliano ya Muungano itafanya kazi nzuri ya kutoa mapendekezo mazuri ya Katiba itakayoendekeza na kuimarisha mashirikiano, umoja wa kidugu wa watu wa Tanganyika na Zanzibar na Umoja wa Afrika mbali na haya niliyopendekeza.

Ussi Khamis Haji

CURRICULUM VITAE (C.V)

Name: Ussi Khamis Haji

Date and place of Birth: 1940 – Mbuguani, Mkoani – Pemba

Parents’ Occupation: Father – fisherman; and mother – house wife

Employment Professional and Working Experience (Civil Service)

  • 1965: State Attorney – Attorney General’s Chamber
  • 1069 – 1970: Assistant Principal Secretary, Ministry of Works, Communications and Power (KNU)
  • 1977 – 1978: Principal Secretary to the Revolutionary Council and President’s Office
  • 1978 – 1979: Deputy Attorney – General, High Court Judge and Deputy Chief Justice respectively
  • 1981: Member of the House of Representatives (Presidential Appointment) and Ministry of State, President’s Office (Planning)
  • April 1981 – 1984: Secretary to the House of Representatives and Director of Elections.
  • May, 1984 – 1985: Registrar General

Other Functions and Posts Held (Public Institutions)

  • 1970 – 1977: Member of East African Legislative Assembly (EALA)
      • Board Member of Zanzibar Insurance Corporation
  • 1985 – 1995: Board Member and Vice Chairman of Zanzibar State Trading Corporation Board of Directors
  • 1988 – 1995: Chairman of the Rent Restriction Board (Rent Tribunal)
  • 1991: Member of Presidential Commission on Multiparty/Single Party Democracy in Tanzania (Nyalali Commission)
  • 1992 – 1995: Member and Vice Chairman of Zanzibar Electoral Commission Member of the Committee on Matters Affecting the Union (Shelukindo Committee)
  • October, 2002: Commissioner Zanzibar Electoral Commission

Leave a comment