Inakuwaje zitumike milioni 551 kununua picha za Ballali tu?

“Taarifa ya ukaguzi wa hesabu za Benki Kuu uliofanywa mwaka 2006/07 umebainisha matumizi ya shilingi milioni 551 kwa ajili ya kununua picha zenye sura ya marehemu Daudi Ballali kwa ajili ya kutundikwa katika jengo jipya la ghorofa pacha (BoT twin tower) na majengo mengine yenye ofisi za Benki Kuu. Uchunguzi unaonesha kwamba picha hizi zote zilikuwa na ukubwa sawa na hazikuwa na tofauti yoyote na zile picha zilizonunuliwa kwa kiasi cha shilingi milioni 4.76 kwa kila moja na vile vile ripoti inaeleza kwamba ni picha 43 tu zilizo katika hifadhi ya Benki Kuu ndizo zilizolipiwa na Benki Kuu kwa kampuni iliotengeneza picha hizo ambayo ni Zahr Ramj of Mediapix International.”

picha ferejiHotuba ya Mhe. Hamad Rashid Mohammed (Mb) Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani, Wizara ya Fedha na Uchumi, kuhusu makadiriio ya mapato na matumizi ya wizara kwa mwaka wa fedha 2008/2009

Mheshimiwa Spika, Awali ya yote napenda kumshukuru M/Mungu kwa kunijaalia uzima na uwezo wa kusimama mbele ya Bunge hili tukufu na pia kwa uwezo wake na si mwengine tunamshukuru kwa kutujaalia kukaribia kumaliza shughuli zetu za Bunge hili kwa amani na utulivu.

Mheshimiwa Spika,

Pili napenda kuchukua fursa hii kutoa shukurani zangu za dhati msaidizi wangu Dr. W. Slaa, Naibu Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni na   Wabunge  wa Kambi ya Upinzani pamoja na wale wote kwa njia moja au nyengine walinipa ushirikiano wa karibu katika maandalizi ya hotuba yangu hii.

Mheshimiwa Spika,

Na mwisho kabisa lakini kwa umuhimu mkubwa napenda kutoa shukurani zangu za pekee kwako wewe binafsi Mhe. Spika pamoja na naibu wako kwa kunipa fursa hii ya kutoa maoni ya Kambi ya Upinzani juu ya Wizara ya Fedha na Uchumi.

Mheshimiwa Spika,

Wizara ya Fedha imepanuliwa na kuwa Wizara ya Fedha na Uchumi. Tume ya Mipango bado haijaundwa kwa hiyo kwa sasa Wizara ya Fedha inasimamia sera za fedha na sera ya mipango ya uchumi. Hivi sasa ni mwaka wa tatu wa kutekeleza MKUKUTA. Hata hivyo kwa sababu ya kutokuwa na fedha za kutosha na gharama kubwa ya utekelezaji wa MKUKUTA kwa kweli mpango huu haujatekelezwa ipasavyo.

Mheshimiwa Spika,

Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kushirikiana na vyama vya upinzani, taasisi zisizokuwa za kiserikali na wananchi kwa ujumla kupitia Dira ya Taifa ya Maendeleo na MKUKUTA ili kuibua dira mpya ya maendeleo na mpango wa muda mrefu unaotekelezeka utakaoongoza mipango na bajeti ya serikali.

Mheshimiwa Spika,

Ni vizuri kazi hii ikaanza mara moja. Aidha tunatoa wito maalum kwa Rais kuunda Tume ya Mipango isiyojikita katika hisia za kuunga mkono chama tawala, ikabidhiwe kazi hii ili nchi iwe na dira inayotokana na mjadala wa kitaifa wa maendeleo ya nchi yetu. Hatari iliyopo hivi sasa ni kwamba Wizara ya Fedha na Uchumi itashughulikia matatizo ya kila siku ya bajeti bila kuwa makini katika maandalizi ya mipango mizuri ya muda wa kati na muda mrefu. Kama tulivyoona katika mjadala wa bajeti, kwa muda mrefu utekelezaji wa bajeti ya maendeleo umekuwa chini ya viwango vya bajeti.

OFISI YA MDHIBITI NA MKAGUZI MKUU WA HESABU ZA SERIKALI

Mheshimiwa Spika, kwanza kabla ya yote naomba nitoe pongezi kwa kazi nzuri inayofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali pamoja na watumishi wake wote.

Mheshimiwa Spika,

Pamoja na kazi nzuri inayofanywa na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, lakini bado kuna mapungufu ambayo tulijaribu kuyabainisha wakati Bunge lako lilipopitisha sheria ya Ukaguzi wa Hesabu za Umma ya mwaka 2008, na baadhi ya kasoro zinazosababisha Ofisi hiyo kukosa kile kinachotarajiwa toka kwa wananchi ni pamoja na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali kuwajibika kwa Bunge badala ya Rais, kama ilivyo sasa. Pia Ofisi ya CAG kuwa na bajeti inayojitegemea pamoja na kuwa na uwezo wa kuajiri na kufukuza, ili kuwa inajitegemea kiutendaji badala ya kuwa chini ya Wizara ya fedha.

Mheshimiwa Spika,

Katika hotuba ya Waziri wa Fedha ya mwaka 2007/08 katika ukurasa wa 40 kifungu cha 57 kinaeleza kuwa “malengo ya ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa hesabu za serikali kwa mwaka huo ni kuimarisha shughuli za ukaguzi, ofisi inatarajia kufanya Surprise cash Audit angalau mara nne kwa kila mwaka katika ofisi zote inazozikagua”. Kambi ya Upinzani, inapongeza juhudi za Serikali katika kuanzisha utaratibu huu kwa ngazi za halmashauri, sasa tunaitaka kazi hiyo ifanywe kwenye ngazi ya Wizara na taasisi za umma.

Mheshimiwa Spika,

Kambi ya Upinzani inakubaliana na wazo hili kwani ni njia moja wapo ya kuweza kudhibiti wizi na matumizi mabaya ya fedha za umma katika ofisi za Serikali. Lakini kwa kuiunga mkono hoja hii tunaitaka Serikali itupe ufafanuzi wa kina juu ya utekelezwaji wa ukaguzi huu, ni ofisi ngapi husika mpaka sasa zimekaguliwa na ni maendeleo gani yamepatikana kutokana na mpango huu.

Mheshimiwa Spika

Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali imejaribu kuweka wazi ni wapi Serikali inapoteza fedha nyingi kutokana na mapungufu ambayo kwa njia moja ama nyingine imewaagiza wahusika wayatolee ufafanuzi wa kina. Kwa maono ya Mdhibiti, upotevu mkubwa unasababishwa na mambo makuu matatu ambayo ni:

  • Kutokufuata sheria za manunuzi
  • Usimamizi dhaifu wa fedha na mali
  • Kutotekeleza mapendekezo ya ukaguzi

Mheshimiwa Spika,

Mapungufu hayo yaliyotajwa hapo juu yamelisababishia Taifa hasara ya kiasi cha Tshs.billion 25/- Hizi ni fedha nyingi sana kwa kuangalia hali halisi ya uchumi wetu. Lakini asilimia kubwa kati ya hiyo yanatokana na kutokuzingatia kanuni na sheria ya manunuzi.

Mheshimiwa Spika,

Sambamba na hilo Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kubadilisha vifungu vya sheria vinavyomzuia CAG kufanya ukaguzi kwa makampuni ambayo Serikali inamiliki hisa chini ya asilimia 50. Kambi ya Upinzani inauliza pale ambapo Serikali inamiliki hisa kidogo, ni nani anaangalia kama kweli gawio linalotokana na hisa hizo ni sahihi na stahiki? Hii inatokana na ukweli kwamba makampuni mengi yamekuwa yakidai kupata hasara wakati zinaendelea kuwekeza, jambo ambalo kwa hali ya kawaida haliwezekani.

Mheshimiwa Spika,

Kambi ya Upinzani inasisitiza tena kuwa mapungufu haya ambayo moja kwa moja yanawahusu watendaji/wahasibu na kama sheria ya CAG ya mwaka 2008 ingelikuwa imempa uwezo CAG ya kutoa adhabu kwa watendaji ni dhahiri mapungufu anayobainisha angeweza kuyarekebisha tofauti na sasa. Hivyo basi, Kambi ya Upinzani bado inasisitiza Ofisi hii ya CAG kupewa meno ili kupambana na masuala kama haya yanayofanywa na watendaji Serikalini.

Mheshimiwa Spika,

Kambi ya Upinzani inasisitiza tena  kuwa Serikali  inatakiwa kuifanya Ofisi hii ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali kuwa taasisi huru na hivyo kuifanya kutimiza majukumu yake kwa ufanisi, basi ni lazima kufanya mabadiliko ya vifungu vilivyotakiwa  ndani ya katiba ili kuruhusu uhuru huo wa Ofisi kama ilivyo kwa nchi wanachama wa INTOSAI na AFROSAI-E.

BENKI KUU YA TANZANIA

Mheshimiwa Spika,

Benki kuu ni chombo kinachomilikiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania kwa maana ya Tanganyika na Zanzibar   kwa asilimia 100 chini ya Wizara ya Fedha. Benki hii ni chombo muhimu sana na ndio nguzo mama wa uchumi wetu kwa sababu ndio kitengo pekee chenye mamlaka ya kuangalia, kudhibiti na kuratibu uchumi wa  nchi kwa kuratibu na kudhibiti mfumuko wa bei na kulinda thamani ya fedha yetu.

Mheshimiwa Spika,

Benki kuu ndio yenye jukumu la kusimamia uchumi na uimara wa shilingi yetu. Thamani ya shilingi ya Tanzania inawekwa kwa nguvu ya soko, kwa hio ni vyema Benki kuu ielekeze zaidi nguvu zake katika kujenga soko imara lenye uwezo wa kuweka thamani ya shilingi inayoendana na hali halisi ya uchumi wa nchi yetu.

Mheshimiwa Spika,

Kwa uchumi wa nchi umekuwa ni mbaya kwa kulinganisha na kipindi chochote ambacho nchi yetu imekipitia. Na hii ni dhahiri kwa kuangalia hali halisi ya maisha ya watanzania ambapo hadi sasa mfumuko wa bei umefikia asilimia 9.7 kwa kulinganisha na asilimia 6.1 mwezi April.2007.

Mheshimiwa Spika,

Kambi ya Upinzani ilitoa angalizo hili pale Serikali ilipopandisha bei ya bidhaa za mafuta jambo lililosababisha upandaji wa bidhaa zote muhimu kwa matumizi ya kila siku ya mtanzania. Bei za vyakula hasa unga kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania kilo moja ya unga imefikia Tsh. 1000/= kwa mkoa wa Dar es Salaam. Pamoja na angalizo hilo Serikali iliishia kutubeza, hatimae kutumia zaidi ya milioni 172 sawa na kilo 172,000 za unga wa mahindi kwenda nchi nzima kuelezea bajeti ya Serikali kana kwamba wananchi hawakuisikia na kuielewa. Kila siku ukweli haukubali  kukaa chini, nivyema tujifunze.

Mheshimiwa Spika,

Kambi ya Upinzani ina uhakika kabisa mbali na kupandisha bei ya bidhaa za mafuta lakini bado Serikali haina uwiano katika matumizi na mapato ya fedha zake kama ambavyo tunapitisha bajeti yake. Hii imewekwa wazi zaidi pale ambapo Mawaziri na Manaibu wao walizunguka nchi nzima kuitangaza bajeti.

Swali la kuuuliza ni je bajeti yao ya kufanya ziara hizo ilitengwa kwenye bajeti gani? jambo hili lilisababisha nakisi katika matumizi ya Serikali na kupelekea kukopa pesa kutoka nje (foreign sources) kiasi cha 100.4 billion na kupunguza akiba yake katika mabenki kwa 37.3 billion (BoT Monthly Report March 2008). Hiki ni kichocheo kikubwa cha kuongezeka kwa mfumuko wa bei. Ushahidi mweingine ni pale Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi ilipotumia jumla ya shilingi 4,100,127,574/- zilizotumika ambazo hazikupitishwa na Bunge hili.

Mheshimiwa Spika,

Vile vile katika kitabu hicho hicho cha mwaka 2005/06 ripoti inaonesha kwamba benki ilipata faida ya kiasi cha Sh. Bilioni 210.076 lakini gawio kwa Serikali lilikuwa ni kiasi cha Sh. Bilioni 37.110.

Mheshimiwa Spika,

BoT ni chombo muhimu sana kwa Taifa hili maskini ambapo mapato ya Benki hii kwa kiasi kikubwa yanatokana na biashara inayofanywa baina ya chombo hichi na Serikali yenyewe. Katika hotuba yangu ya mwaka jana niliulizia juu ya vigezo vinavyotumika katika gawio la faida (net profit) inayopatikana kutokana na biashara hiyo kwani katika ripoti ya BoT ya mwaka 2004/05 inaonesha kwamba benki hii ilipata faida kiasi cha Sh. Bilioni 127.5, lakini cha kushangaza zaidi ni kwamba Serikali ilipata kiasi cha Sh. Bilioni 5.0 ambacho ni sawa na asilimia 3.9.

Mheshimiwa Spika,

Matumizi haya mabovu ya Serikali ambayo kwa kila siku tumekuwa tukiyapigia  kelele yamethibitishwa pia na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali  kuwa yameongezeka kutoka Tshs. 844billion ambayo ni sawa na  21%  mwaka 2005/06 hadi Tshs. 1.098trillion ambayo ni sawa na 30% mwaka 2006/07. Hali halisi ni kuwa kada ambayo inanufaika na matumizi hayo ni kada ya viongozi walio Serikalini. Ushahidi wa hayo ni kuendelea kukopwa kwa waalimu na kutokulipwa wafanyakazi viwango vipya vya mishahara kwa wakati na wazabuni mbali mbali kutokulipwa pamoja na kwamba Serikali bado inatumia Cash Budget.

Mheshimiwa Spika,

Katika hali ya kusikitisha na ya kutia huzuni zaidi, katika hesabu za BOT mwaka 2006/07 kunaonekana kwamba kuna ufisadi mwengine wa fedha kiasi cha shilingi bilioni 4.7 ulibainika. Hii inaonesha dhahiri kwamba bado mizizi ya ufisadi haijakatwa na kuna haja ya kuchukua hatua madhubuti zaidi kwa kukabiliana na tatizo hili.

Mheshimiwa Spika,

Katika kikao cha Bunge kilichofanyika mwaka jana, Kambi ya Upinzani iliishauri Serikali kupitia Wizara ya Fedha juu ya kuundwa kwa Tume itakayochunguza ujenzi wa majengo ya BoT (twin tower). Lakini jambo la kusikitisha ushauri huu ulikataliwa bila ya sababu zisizojulikana.

Mheshimiwa Spika,

Taarifa ya ukaguzi wa hesabu za Benki Kuu uliofanywa mwaka 2006/07 umebainisha matumizi ya shilingi milioni 551 kwa ajili ya kununua picha zenye sura ya marehemu Daudi Ballali kwa ajili ya kutundikwa katika jengo jipya la ghorofa pacha (BoT twin tower) na majengo mengine yenye ofisi za Benki Kuu. Uchunguzi unaonesha kwamba picha hizi zote zilikuwa na ukubwa sawa na hazikuwa na tofauti yoyote na zile picha zilizonunuliwa kwa kiasi cha shilingi milioni 4.76 kwa kila moja na vile vile ripoti inaeleza kwamba ni picha 43 tu zilizo katika hifadhi ya Benki Kuu ndizo zilizolipiwa na Benki Kuu kwa kampuni iliotengeneza picha hizo ambayo ni Zahr Ramj of Mediapix International.

Mheshimiwa Spika,

Kwa hakika huu ndio uharibifu na ufisadi wa fedha za walipa kodi zinazotumika bila ya kuzingatia mambo ya msingi yenye kuleta faida katika kunyanyua na kukuza uchumi wa taifa hili. Kwani fedha iliotumika katika kutengeneza picha hizi zingelitosha kabisa kama zingelitumika katika ujenzi wavituo vya afya vya kisasa vipatavyo 7, kwa kila kituo kimoja kinagharimu kiasi cha Tshs.80million. Kutokana na ubadhirifu huu wa fedha na ufisadi uliokithiri ndani ya taasisi hii, kambi ya upinzani inapata wasiwasi kama kweli malengo ya benk kuu ya kuondoa umaskini yatafikiwa ifikapo mwaka 2010.

Mheshimiwa Spika,

Kambi ya Upinzani inajiuliza kama picha za kuweka BOT zimetumia fedha hizo, Je picha za Mhe. Rais ambazo ziko ofisi zote za Serikali Tanzania nzima zimetumia kiasi gani? Tunamtaka Mheshimiwa Waziri atupe sababu za msingi za Bodi ya BOT kuidhinisha matumizi mabaya kama haya.

Mheshimiwa Spika,

Hivi vyote mbali na kwamba kuna ufisadi ndani yake bali ni viashiria  vya kuzidisha mfumuko wa bei na sio mafuta tu.

DENI LA TAIFA

Mheshimiwa Spika,

Kutokona na takwimu zilizomo ndani ya taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali, ni kwamba hadi  sasa Tanzania  Inadaiwa Tsh. 1,832,420,666,865/=  kama deni la ndani na Tshs. 3,642,581,417,898/= kama deni la nje. Kati ya deni hilo likigawanywa kwa idadi ya watanzania milioni 40 kila mmoja atakuwa anadaiwa Tshs.45,810.51/= katika deni la ndani na Tshs. 91064.54/= katika deni la nje. Hivyo basi hadi sasa kila mtanzania anadaiwa jumla ya Tshs. 136,875.05/=

Mheshimiwa Spika,

Swali ni kwa kuwa tunatumia cash budget ni kwanini tunadaiwa madeni ya ndani? ukweli ni kuwa kila huduma ya ndani tayari inatakiwa fedha zake ziwepo tayari kwenye budget. Tukitumia maana yake fedha zipo, deni linatoka wapi? Swali hili linahitaji majibu ya kina, vinginevyo Bunge hili lielezwe faida hasa ya Cash Bajeti!

UBADHIRIFU KAMA ALIVYOBAINI MKAGUZI WA HESABU ZA SERIKALI

Mheshimiwa spika,

Hakika ubadhirifu wa fedha katika mashirika na taasisi mbali mbali za Serikali zimekithiri nchini na tatizo hili kwa kiasi kikubwa linaongeza mzigo kwa Serikali na kudumanza maendeleo ya nchi.

Mheshimiwa spika,

Mfano nzuri ni Mkataba wa ajira wa Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Mamlaka ya Tumbaku TTB ulisainiwa tarehe 28/Julai 2005 lakini ulirejeshwa nyuma na kusomeka tarehe 29/April/2005 kwa mshahara wa sh. 2,700,000 kwa mwezi ambao ni sawa na ubadhirifu wa sh. 8,100,000. kwa muda wa miezi mitatu na huu ni mfano wa taasisi moja tu lakini kuna nyingi zaidi ya hii, na hali hii inaonesha jinsi gani taasisi zinavyoendeshwa nchini kwa ubabaishaji na ubadhirifu mkubwa ambao ndio wanaochangia kuporomoa uchumi wetu.

Mheshimiwa spika,

Pia katika taarifa hiyo ya Mkaguzi wa fedha ilionyesha katika makubaliano ya malipo ya kodi ya kuendesha mradi wa songosongo kulikuwa na makubaliano ya kupunguzwa kodi kulingana na mauzo lakini jambo la kushangaza na kusikitisha ni ukaguzi wa taarifa za Hesabu unaonesha kiasi cha sh. 1,887,186,871 yalipunguzwa kutoka katika mapato hayo ambayo yalitakiwa kuwasilishwa serikalini, mkataba huu haunufaishi serikali wala wananchi zaidi ya yote unaongezea serikali mzigo.

Mheshimiwa spika,

Pia kutokana na taarifa ya mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa Hesabu za serikali katika kipengele cha ubinafsishwaji wa mashirika ya umma maduhuli ambayo yalikuwa  hayajakusanywa hadi tarehe 30/06/07 ni malipo ya Tsh. 7,942,247,030 toka kwa wawekezaji kwa ajili ya ununuzi wa mashirika yalikuwa bado hayajapokelewa ingawa hatua za uuzaji zilikuwa zimeshakamilika. Kambi ya upinzani inamtaka Mheshimiwa waziri atuelezee je! Fedha hizi zimeshalipwa na kulikuwa na jambo gani lililosababisha hata kutolipwa malipo hayo kwa muda wa makubaliano? Je ni hatua gani zilizochukuliwa kwa mujibu wa mkataba wa mauziano?

UDHAMINI WA SERIKALI KWA MAKAMPUNI BINAFSI

Mheshimiwa Spika, kwa kipindi kilichopita Serikali kupitia Hazina imetoa udhamini wa asilimia 100 kwa makampuni binafsi. Hili linafanyika kwa Serikali kuziagiza asasi za fedha kutoa mikopo hiyo. Na mbaya zaidi baadhi ya makampuni hayo yanaonekana kushindwa kulipa na riba imezidi kuwa kubwa mno, mfano NSSF wanadai Tshs. 100billion kiwanda cha Kagera Sugar kutokana na dhamana ya Serikali. Baadhi ya Makampuni binafsi ambayo yamepata udhamini wa asilimia 100 toka Serikalini mbali na Kagera Sugar na Mwananchi Gold Co. n.k

Mheshimiwa Spika, Katika hali ya kawaida pale ambapo Benki inatoa mkopo mkubwa kwa kampuni kuna taratibu za makubaliano ambazo zinafanywa kuhusiana na uendeshaji wa kampuni ili benki iweze kurejesha fedha zake.

Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kulieleza Bunge hili Serikali imeweka mkakati gani wa makusudi kuhakikisha viwanda hivyo vinarejesha fedha hizo? Tukumbuke hizi ni fedha za watanzania walipa kodi na dhamana ni kwa viwanda binafsi, je hii ni haki kwa walipa kodi wa nchi hii kulipa madeni ya makampuni binafsi kwa kodi ya wananchi pale ambapo makampuni hayo yanaposhindwa kulipa madeni hayo?

MAMLAKA YA MAPATO

Mheshimiwa Spika,

Mamlaka ya Mapato ya Tanzania (TRA), hiki ndicho chombo husika cha kukusanya mapato ambacho kipo chini ya Wizara ya Fedha kilichoanzishwa mwaka 1996. ingawa kimuono wa juu juu idara hii inaonekana kama kwamba imefanikiwa kwa hali ya juu lakini kwa undani kitengo hiki bado kabisa hakijafanya kazi hasa inayotakiwa na kama ingelifanya hivyo basi leo hii tungejitosheleza kwa bajeti yetu na wala tusengelihangaika na kuwategemea Wahisani.

Mheshimiwa Spika,

Katika mkutano uliopita wa Bajeti tulisema sana juu ya jambo hili la kutegemea wafadhili katika maendeleo yetu. Kambi ya Upinzani inaipongeza TRA kwa kukusanya mapato kwa kiwango marudufu kulingana na miaka iliyopita. Lakini pia tulisema kuwa uwezo wa Serikali kukusanya mapato ni mkubwa zaidi, ila kuna uzembe mkubwa na kutojali (laxity), ubadhirifu, na ufisadi kama inavyodhihirishwa na Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali mwaka hadi mwaka.

Mheshimiwa Spika,

Leo hii kuna makampuni mengi ambayo yapo na yanaendesha shughuli zake nchini na hata bila ya kulipa kodi au kulipa kwa kiwango kidogo sana kisichoendana kabisa na mapato yao, mfano nzuri ni kampuni zinazofanya biashara ya chai na katani wilayani korongwe vijijini kampuni hizi hazilipi ushuru wa asilimia 5 kiasi cha kuchangia kipato kidogo cha hamashauri na hivyo kushindwa kabisa kwa halmashauri kuendeleza shughuli zake za kiuchumi.

Mheshimiwa spika,

Hakika inaumiza na tena Inasikitisha sana leo hii sheria za fedha za serikali za mitaa ya mwaka 1982 ilikuwa inaruhusu ukusanyaji wa kodi kwa serikali za mitaa kwa makampuni ya machimbo kiasi cha asilimia 0.3 lakini lakushangaza ni kuwepo kwa makubaliano ya kukusanya si zaidi ya US dola 200,000 kwa mwaka na makubaliano hayo yanakataza kutoangalia mapato, faida, kiwango kinachopatikana cha fedha nakadhalika, hapa panauwezekano mkubwa wakupotea mapato kwa kiasi kikubwa kwani thamani ya sarafu inabadilika siku hadi siku huwezi kuweka kiwango maalum cha fedha badala ya asilimia hii ni kuikosesha serikali mapato. Ni vyema kuweka asilimia kuliko kuweka kiwango maalum.

Mheshimiwa spika,

Kana kwamba haitoshi kwa mujibu wa sheria ya kodi ya mapato ya 2004 inaitaka kampuni inayoendesha shughuli zote za machimbo kulipa kodi ya asilimia 30 kulingana na pato lake, jambo lakusikitisha ni kuwa zaidi ya miaka 5 sasa hakuna kampuni yeyote ya dhahabu iliyotangaza pato lake nchini nakufanya taasisi husika kushindwa kukusanya kodi hiyo kulingana na pato husika.

Mheshimiwa Spika,

Taarifa ya Alex Stewart (Assayers) ASA inaonesha kuwa kitengo cha ukusanyaji mapato nchini kinapoteza fedha nyingi sana na hasa katika kampuni za madini na hii inatokana na kitengo hiki kutokuwa na wafanyakazi wenye uwezo, taaluma, uzoefu na ujuzi wa kuchambua financial statement za kampuni za madini. Pia imechunguzwa na kuthibitika kuwa kitengo hiki kinauwezo mdogo mno wa kugundua na kuona kwa macho ya kitaalamu jinsi gani kampuni za madini zinavyoendeshwa nchini. Mfano mzuri ni kuwa imegundulika kuwa kampuni nyingi za madini nchini hazitoi taarifa sahihi za rekodi ya fedha ambayo ni kinyume kabisa na kifungu cha 99(3) na paragrafu 2(iii) mining Act ya 1998 ambayo inailazimisha kampuni hizi kurikodi na kutunza mahesabu kwa mpangilio uliowa wazi na unaoeleweka. Je ni kwanini Serikali inashindwa kufuatilia matakwa ya sheria hii?

KODI ISIYO KUSANYWA

Mheshimiwa Spika,

Kutokana na taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali (CAG) katika Wizara na Idara za Serikali tulizochambua mathalani tumebaini kuna upungufu wa makusanyo ya mapato, mrahaba usiokusanywsa kutoka kampuni ya almasi ya Williamson diamond Ltd ni shilingi 841,137,251. , Tansort, Tsh.206,662,556. Aidha, misamaha ya Kodi nayo imekuwa ya kutisha, kwani hadi kufikia mwezi huu wa Juni2008, kiasi cha Tshs.819.9 billion zilikuwa zimesamehewa kama kodi huku misamaha hii mingi ukiondoa ya mashirika ya dini ikiwa haijamnufaisha mwananchi masikini. Hiki ni kiasi kikubwa kwa nchi inayoomba misaada kila kukicha.

Mheshimiwa Spika,

Makampuni ya madini yamesamehewa kodi kwa asilimia 100 katika uingizwaji wa mafuta kutoka nje kwa ajili ya kuendeleza shughuli zao. Kwa mfano katika mwezi April 2007 ilielezwa kwamba kuanzia mwaka 2004 mpaka 2006 makampuni sita ya migodi ya dhahabu wameingiza zaidi ya lita milioni 178 ya mafuta ghafi ambapo kiasi cha shilingi bilioni 62.8 kilikosekana kutokana na kuondoa kodi hii.

Mheshimiwa Spika,

Vile vile makampuni haya yamepata punguzo la asilimia 100 kwenye ushuru wa bandari (custom duty). Mwanzoni makampuni haya yalikuwa yanalipa kiasi cha asilimia 5 lakini kwa sasa hakuna ushuru wowote unaotozwa kwa makampuni haya.

Kambi ya Upinzani inaona huu ni upungufu mkubwa wa mapato ya wanyonge wa Watanzania kwa kuyatupa bila utaratibu wa wazi na unaoeleweka, hivyo inaitaka Serikali mara moja kutekeleza mapendekezo ya Ripoti ya Bomani kufuta misamaha hiyo.

Mheshimiwa Spika,

Vile vile sheria hizi zimewapa madaraka makubwa makampuni haya kwa kumiliki haki za madini kiasi ambacho wana nguvu kamili ya kufanya wanavyotaka, kwa mfano wamepewa uwezo wa kununua na kuuza makampuni haya kwa makampuni mengine ambapo shughuli hizi zinayapatia makampuni faida kubwa sana.

Mheshimiwa Spika,

Katika mwaka 2003 kampuni kutoka Australia inayojulikana kwa jina la East Afrika Gold Mines ilipata kiasi cha US$ milioni 252 kwa kuuza mgodi mmoja wa dhahabu ndani ya Tanzania kwa kampuni ya Kanada Placer Dome ambayo baadae iliuzwa kwa Barrick. Vile vile katika mwaka 1999 Barrick ilinunua mgodi wa dhahabu wa Bulyanhulu kutoka kampuni ya Kanada Sutton Resources kwa kiasi cha dola za kimarekani milioni 280.

Mheshimiwa Spika,

Cha kustaajabisha ni kwamba katika mauzo yote yanayofanyika na makampuni haya si Serikali ya Tanzania wala raia wa kawaida wa nchi hii ambae ananufaika na mabilioni ya fedha hizi. Hii ni dhahiri kuwa Serikali yetu haina uchungu na mali zetu kwani tunaamini yanayotokea wanaya tambua lakini tu kwa sababu ya kuzingatia maslahi ya wachache ndio maana leo hii wanatufikisha hapa. Jee huku ni kuwavutia au kuwahonga mali zetu wawekezaji hawa?  Kambi ya Upinzani inamtaka Waziri kufanyia marekebisho sheria ya kodi ushuru wa stempu sura 189 na kodi ya mapato sura 332 ili mauzo ya hisa ambayo yanabadilisha umiliki pamoja ba controlling interest ya kampuni za nje ambayo kwa namna moja yanategemea raslimali iliyopo Tanzania yatozwe kodi Tanzania.

Mheshimiwa Spika,

Kutokana na ukusanyaji huu mbovu wa mapato, makisio yaliofanywa juu ya upotevu wa mapato yanayotokana na Royalty rate (kiwango cha mrahaba), corporation tax (kodi ya makampuni) isiolipwa na ukwepaji wa ulipaji kodi kwa muda wa miaka saba sasa ni zaidi ya shilingi bilioni 480. Kiasi hiki cha fedha hakijajumuisha makampuni yote ya madini wala punguzo la kodi nyinginezo ambapo ni vigumu kuweza kukisia.

Mheshimiwa Spika

Mbali na ukwepaji huo kuna aina nyingine ya ukwepaji inayofanywa na wafanyakazi wa kigeni walioajiriwa katika makampuni mbalimbali. Ukwepaji huu wa kodi ni ule wa kutokulipa kodi ya PAYE. Kwa sasa tunakadiria kuna wafanyakazi hao karibu 500 nchi nzima, na wengi wao wanapokea kati ya Tshs. 5milioni na Tshs 20milioni tuchukulie wastani wa Tshs.10milioni. Hivyo basi PAYE kwa mwezi mmoja Tshs 1.5bilioni, ambazo kwa mwaka mmoja ni Tshs.18bilioni.

Mheshimiwa Spika,

Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kulieleza Bunge hili sheria za kodi zinasemaje kuhusiana na wafanyakazi hao wageni kulipwa mishahara yao moja kwa moja kwenye nchi wanazotoka na kulifanya Taifa kukosa takribani kiasi tajwa hapo juu?

MSAMAHA WA VAT KWA WAFANYABIASHARA WAKUBWA CHINI YA SHERIA YA HOTELS ACT, CAP 105, RE 2002.

Mheshimiwa Spika

Kifungu cha 73A cha Marekebisho ya Sheria ya Ushuru wa Hoteli kinatoa msamaha kwa wafanyabiashara wakubwa kwa kusema kuwa sheria hiyo inatoa msamaha wa kutolipa kodi ya ushuru wa Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa mtu yeyote au Jumuia yeyote ya watu ambao wamesajiliwa chini ya sehemu ya (iv) ya Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani kuanzia siku ya kuanza kutumika kwa Sheria hii.

Mheshimiwa Spika, msamaha huu ni sawa na kuwapa nafasi wafanyabiashara hawa kutolipa kodi ambayo kimsingi kila mtu anayeuza bidhaa na kutoa huduma zinazopaswa kulipwa kodi hii analazimika kuilipa kwa mujibu wa kifungu cha 3(1) na 4(1) cha Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani ya mwaka 1998.

Jee kwa kuwa wamesajiliwa, hiyo inahakikishaje kwamba wafanyabiashara hawa watalipa kodi ya ongezeko la thamani inayohusu huduma za hoteli wanazozitoa au wafanyabiashara hawa hawapaswi kulipa kodi hiyo?

Mheshimiwa Spika, kodi ya ushuru wa hoteli ya asilimia 20% inayotakiwa kulipwa chini ya kifungu cha 26(1) imekuwa kero kubwa hasa kwa wafanyabiashara wadogo wadogo katika sehemu tofauti za miji, majiji manispaa na nyenginezo. Hii ni kwasababu kiwango cha asilimia 20% ni kikubwa na hakizingatii gharama za uendeshaji kwa biashara hiyo. Mfano tarehe 10/01/2008 Umoja wa Wafanyabiashara wa Nyumba za Kulala Wageni Mwanza (UWANZA) ulimuandikia barua yenye kumbukumbu namba UW/MZ/06, Waziri wa Fedha wakilalamikia kodi hii na manyanyaso wanayoyapata kwa sababu ya kodi hii. Malalamiko haya yalijibiwa kwa barua yenye kumbukumbu namba TYC/R/160/32. ya Waziri wa Fedha kwamba atalishuhulikia jambo hili lakini hadi leo hii halijashughulilikiwa ipasavyo.

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kuliangalia jambo hili kwa makini na kuchukua hatua zinazofaa ili kupunguza usumbufu kwa wafanyabiashara hawa.  Aidha kifungu hiki cha sheria kinawaondoka watanzania wenye mitaji midogo katika biashara na kuwapa fursa wafanyabiashara wakubwa kuendelea kwenye biashara hii (dhana ya ushindani iko wapi?).

SEKTA YA FEDHA

Mheshimiwa Spika,

Hii ndio sekta muhimu sana kwa maendeleo ya uchumi kwa ujumla wake, kwani ndio sekta inayotakiwa kuwa chachu ya sekta nyingine za uchumi kwa kuziwezesha ki-mtaji. Kwa hali ya kawaida mabenki ndio yanayotakiwa pamoja na kutoa mikopo pia yatoe ushauri na kusimamia mkopaji hadi aweze kusimama na kuwa mshindani katika biashara. Katika mchakato huo wote benki itapata riba yake na mkopaji atapata kile alichokusudia kukifanya.

Mheshimiwa Spika,

Mwishoni Desemba 2007 wastani wa riba za amana za akiba ilikuwa asilimia 2.75 wakati mfumko wa bei ni asilimia 9.7. Mtanzania mlala hoi aliyejikusuru na kuweka akiba ya shilingi 10000/- tarehe 31 Desemba 2007, thamani halisi ya akiba yake itapungua kwa asiliamia 7 sawa na shilingi 700/- ifikapo tarehe 31 Desemba 2008.  Mfumo mzima wa mabenki na taasisi zetu za fedha hazitoi motisha na msukumo katika kukusanya akiba ya Watanzania wa kawaida.

Mheshimiwa Spika,

Wastani wa riba ya mikopo ni asilimaia 15.25.  Tofauti kati ya riba ya mikopo na riba ya amana za akiba ni asilimia 12.5.  Ni wazi mfumo wetu wa fedha ni dhaifu katika kukusanya amana za akiba na unatoza riba kubwa kwa wanaokopa.  Makampuni madogo na ya kati hayapati mikopo.  Makampuni na wafanyabiashara 200-250 ndio wanaochukua zaidi ya asilimia 80 ya mikopo yote inayotolewa na mabenki ya Tanzania.  Sekta ya Kilimo ndiyo inayonyimwa mikopo kabisa. Hatuwezi kujenga uchumi wa kisasa ikiwa wajasiriamali wadogo na wakati hawana vianzio vya mitaji na mikopo.

Mheshimiwa Spika,

Utafiti umeonyesha kuwa upatikanaji wa huduma za  benki na fedha (financial services) kama vile kuweka akiba, kukopa, kununua bima na kulipia bidhaa na huduma bila kutumia fedha taslimu ni muhimu katika kukuza uchumi na kupunguza umaskini. Maendeleo ya teknolojia ya habari na mawasiliano imeongeza fursa za kusambaza huduma za fedha kwa mfano kwa kutumia simu za mkononi. Wizara ya Fedha na Uchumi kwa kushirikiana na Benki Kuu iandae mkakati wa kuwapatia wananchi wote huduma za fedha (financial services for all).

Mheshimiwa Spika,

Aidha pamoja na hilo taratibu za mikopo na zenyewe zina katisha tamaa sana, pale mkopaji anapotakiwa kuweka dhamana ya mkopo yenye thamani ya 125% ya mkopo anaotaka kukopa.

Ili sekta ya fedha iweze kuchangia katika uchumi wetu ni lazima masuala yafuatayo yaamuliwe:-

Suala la riba liamuliwe kama lilivyoamuliwa Kenya “Central Bank Intervention”.

a. Benki kuu ipunguze kiwango cha Riba kwa mikopo yake inayoitoa kwa mabenki ili mabenki nayo yapunguze Riba kwa wateja.

b. Serikali ilete sheria mahasusi ya utumiaji wa mtandao katika malipo na manunuzi  ya Benki,ili kurahisisha na kuharakisha ulipanaji wa fedha ikiwa ni pamoja na mishahara ya wafanya kazi.

c. Pamoja na maelezo yanayotolewa na Serikali juu ya “Dollarisation” Serikali ifutatilie taasisi ambazo bado hazijatekelza kwamba ni makosa kutumia Dollar katika biashara anbayo haikuidhinishwa na BOT kutumia fedha za kigeni.

d. Benki Kuu ifuatilie kwa makini fedha zinazotoka nje kwa matumizi ya Serikali ,na ziwekwe Benki Kuu na Benki za Biashara za Serikali. Serikali ilieleze Bunge ni kiasi gani cha riba kimelipwa kwa mabenki hayo katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.

Mheshimiwa Spika,

Wawekezaji walazimishwe kukopa katika mabenki yetu, na kama mabenki yetu hayana fedha za kutosha Benki Kuu iingilie kati kusaidia kupatikana kwa mikopo hiyo, ili tuepukane na kuwa na mzunguko mdogo wa fedha na akiba yetu kuwa ndogo, aidha tutaweza kudhibiti mserereko wa fedha yetu. Kwa njia hii Taifa litaweza pia kusimamia mwenendo mzima wa uwekezaji katika nchi yetu, ukiwa ni pamoja na uwezo wa kusimamia viwango vya uwekezaji yaani “plough back effects”

Benki ya Rasilimali (TIB)

Mheshimiwa Spika, Serikali imeiongezea mtaji Benki ya Rasilimali (TIB) na kufikia shilingi bilioni 50 ili kupunguza ukosefu wa mikopo katika viwanda na kilimo. Ukizingatia yaliyotokea katika akauti ya EPA ya Benki Kuu, taasisi ambayo ndiyo inayosimamia mabenki, serikali inaweka mfumo gani wa kiutawala kuhakikisha kuwa Benki ya Rasilimali haitoi mikopo kisiasa na fedha za walipa kodi zilizowekwa kama mtaji katika benki hiyo hazipotei. Utawala (Gorvernance) ya Benki ya raslimali unahitaji kuimarishwa ikiwa ni pamoja na kuteua watendaji makini wenye utaalam wa hali ya juu. Benki ifungue matawi katika kanda haraka ili kuweza kuwahudumia wawekezaji wazalendo.

TAKWIMU

Mheshimiwa Spika,

Ili kuwa na bajeti nzuri na inatakayoweza kuondoa kero na matatizo kwa wananchi, takwimu sahihi ni muhimu sana. Serikali imeshindwa kuwa na takwimu muhimu na sahihi katika upangaji wa vipaumbele vyake, na vipaumbele vinapangwa kwa kuelewa ni watu wangapi wanatarajiwa kutumia huduma husika.

Mheshimiwa Spika,

Wakala wa usajili ufilisi na udhamini-RITA ni taasisi pekee na ya uhakika ambayo inauwezo wa kutoa takwimu sahihi ambazo zinaweza kutumiwa katika shughuli za mipango ya maendeleo. Iwe ni kwa Nchi, Mikoa, Wilaya hadi Kata. Aidha Wakala huyu anaweza kwa kiasi kikubwa kupunguza mwingiliano wa shughuli zinazofanana kama zinavyofanywa na taasisi mbali mbali katika Wizara mbali mbali, mfano, Daftari la kudumu la wapiga kura, Usajili wa Makampuni, Bodi ya Mikopo, Vitambulisho vya Taifa vya Uraia, Namba ya Utambulisho ya mlipa kodi (TIN number), liseni za udereva, Pay roll za watumishi wa Serikali, Msajili wa hati. Sehemu hizo zote takwimu sahihi  zinaweza patikana kutoka katika wakala huyu.

Mheshimiwa Spika,

Aidha, mlolongo wa asasi za Serikali zinazofanya kazi zinazofanana ni kuiongezea Serikali matumizi yasiyokuwa ya lazima. Wakala wa vitambulisho vya Uraia (NIDA), ili kufanya kazi zake ni lazima apate takwimu toka RITA.

Kambi ya Upinzani inauliza ni kwanini kuunda wakala mwingine wakati kuna wakala anayefanya kazi hizo.

MFUKO WA HAZINA WA SERIKALI

Mheshimiwa Spika,

Mfuko wa hazina wa Serikali ambao upo chini ya Wizara ya Fedha ndio wenye jukumu la kutoa fedha kwa wizara zote baada ya Bunge kupitisha matumizi ya fedha kwa wizara husika. Kwa hivyo kama Wizara imepanga kuendeleza na kutekeleza miradi yake ya maendeleo kama vile ujenzi wa shule, barabara, zahanati na kadhalika hawawezi kuifanikisha miradi hiyo kama mfuko wa hazina haujatoa fedha hizo, hii inaonesha ni jinsi gani mfuko huu ulivyo muhimu kwa maendeleo ya huduma za jamii.

Mheshimiwa Spika,

Katika hali ya kushangaza tunaona kwamba karibu wizara zote wanapoulizwa ni kwanini Wizara imeshindwa kukamilisha miradi iliopanga kutekeleza  kwa muda ulioainisha lakini cha kusikitisha majibu yanayotoka ni kwamba ni kutokana na kucheleweshwa au kupewa nusu nusu  kwa fedha kutoka mfuko wa hazina wa Serikali.

Maelezo kuwa Fedha zilichelewa kutoka kwa wahisani na ishara tu ya kutokuwa na mipango makini na hivyo siyo sababu inayokubalika.

Mheshimiwa Spika,

Kambi ya Upinzani inaamini kuwa huu ni uzembe wa makusudi unaofanywa na wahusika wa kitengo hiki, hivyo ni lazima Waziri atupe maelezo ya kina na yenye kuridhisha ni kwa sababu gani imekuwa ni kawaida kwa ofisi hii kuchelewesha fedha hizi na hivyo hawaoni kuwa Serikali ndio wanakwamisha shughuli za maendeleo na hivyo kushindwa kufikia malengo waliyopanga wa kuondosha umaskini na kukuza uchumi?

Mheshimiwa Spika,

Baada ya kuyasema hayo kwa niaba ya Kambi ya Upinzani, naomba kuwasilisha.

……………………………………..

Hamad Rashid Mohammed (Mb)

Kiongozi wa Upinzani na Msemaji Mkuu Wizara ya Fedha na Uchumi.

22.08.2008

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s