Tanzania imekosa uongozi ulio makini

Hamad Rashid Mohammed, Mbunge wa CUF na Kiongozi wa Upinzani Bungeni

Hamad Rashid Mohammed, Mbunge wa CUF na Kiongozi wa Upinzani Bungeni

“….baada ya utafiti huu, sasa tunaweza kusema ni katika mwenendo upi taifa letu linakwenda? Kama tunapoelekea ni pazuri au la? Ikichangiwa na kukosekana kwa Uongozi Ulio Makini, viashiria vya siasa huria ya nchi yetu inajikita katika mambo mengine makubwa, ambayo ni mapungufu ya Katiba, chaguzi mbovu pamoja na ufisadi na umasikini, ambavyo vimewanyima Watanzania ajira na ukuwaji wa uchumi unaofikia angalau asilimia 8%. Mustakabali wa taifa haujengwi kwa maneno mazuri, na tabasamu linalovutia bali ni kwa utendaji ulio makini na unaozingatia matatizo ya Mtanzania.”

Kutoka mada “Changamoto za siasa huria na mustakabali wa taifa-Tanzania: Maoni ya Kambi ya Upinzani Bungeni” iliyotolewa na Mhe. Hamad Rashid Mohammed (Mb), Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, kwa Mpango wa Utafiti na Elimu ya Demokrasia Tanzania (Redet) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, tarehe 20 Agosti, 2008

Utangulizi

Mheshimiwa Mgeni Rasmi, kwa heshima na taadhima kwanza napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa kunipatia fursa hii ili niweze kutoa maoni ya Kambi ya Upinzani Bungeni juu ya mada iliyo mbele yetu. Mada hii si tu muhimu bali ni moja ya vitu ambavyo tunaweza kutumia kujipima na kujua nafasi yetu katika maendeleo ya siasa. Hii inaweza kututanabahisha kama tunasonga mbele au tunarudi nyuma au mwendo niwakutia matumaini au laa. Kambi ya Upinzani Bungeni imefurahishwa sana kupata nafasi hii ili nasi tuweze kuweka bayana mambo ambayo tunayaona kama changamoto za hali ya juu katika siasa ya nchi yetu.

Mheshimiwa Mgeni Rasmi, Kambi ya Upinzani imeona ni vyema kabla ya kutoa maoni juu ya changamoto za siasa huria na mustakabali wa Tanzania, ni vyema kwanza nikaweka bayana nini maana ya siasa huria kwa mtazamo wetu.

Dhana ya Siasa Huria

Kinadharia siasa huria ni siasa inayoongozwa kwa misingi ya kidemokrasia, utawala wa watu, ambao unawapa watu uhuru kushiriki katika shughuli zote za siasa, kufanya maamuzi sahihi na yenye maslahi kwa watu wote na kuchagua utawala wao, kwa ajili yao. Mihimili mikubwa ya siasa huria inajumuisha mambo yafuatayo:

  • Utawala wa Nchi kwa msingi wa Katiba na Sheria. (ambayo imeundwa kutokana na maoni ya wananchi)
  • Utawala wa Sheria (unaoheshimu Mipaka na Uhuru wa Mahakama, Bunge na Serikali yenyewe)
  • Uchaguzi Huru, Haki na wa -Wazi, utakao heshimu ridhaa ya watu.
  • Utawala unaoheshimu haki za binadamu na haki nyingine za msingi za raia.
  • Usawa katika huduma za jamii (unaoheshimu na kushirikisha makundi mbali mbali ndani ya jamii)
  • Ukweli na Uwazi wa Serikali katika Utendaji wake
  • Uwajibikaji bora wa Serikali kwa Wananchi
  • Uhuru wa-kiutendaji wa Vyombo vya Habari, Ulinzi na Usalama pamoja na Asasi za Kiraia

Mihimili niliyoitaja ndio hasa inayojenga dhana nzima ya siasa huria na nchi yoyote ambayo inazingatia na kufuata kwa makini, ni wazi itakuwa inajiendesha katika misingi ya kidemokrasia ya kweli na bila shaka itakuwa na utawala bora. Pamoja na kuwa hiyo ndio mihimili mikuu ya nchi inayoongozwa kwa misingi ya kidemokrasia, nitagusia machache tu, ambayo hasa ndio yanaleta changamoto kwenye siasa yetu.

Changamoto za Siasa Huria Tanzania

Ni ukweli usiopingika kuwa mfumo wa siasa huria hapa nchini kwetu unakumbana na changamoto nyingi sana ambazo kwa hakika unaweza kuona kwamba katika jukwaa la kisiasa ni tatizo kwa mtu mmoja mmoja na jamii kwa ujumla.  Lakini nitajaribu kuzifafanua changamoto chache ambazo zinalandana na jinsi nilivyo tafsiri maana ya siasa huria.

Uchaguzi Huru, haki na wa Wazi (Unaoheshimu Ridhaa ya Watu)

Sote tunafahamu kuwa nchi yoyote inayojengwa katika misingi ya kidemokrasia ni lazima iongozwe na sera safi ya kuendesha na kusimamia uchaguzi ili wananchi wake wapate uhuru wa kutumia vyema na kwa ufanisi  haki  yao ya kikatiba ya kuchagua na kupata kiongozi wanaemtaka. Uchaguzi huru, haki na wa-wazi wenye matokeo yanayo heshimika ndio kipimo mahsusi cha nchi kuwa ni ya kidemokrasia au kidikteta. Nchi nyingi duniani zenye kufuata mfumo wa vyama vingi hasa nchi za kiafrika Tanzania ikiwemo, zimekuwa zikishindwa kulitambua hili.

Kwa mfano hapa kwetu Tanzania, Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977, ibara ya 3(1) inasema wazi kuwa nchi yetu ni ya kidemokrasia na inaendeshwa kwa misingi ya kidemokrasia. Lakini pamoja na Katiba yetu kutamka hivyo, viashiria vingi sana ambavyo vinaonesha kuwa bado demokrasia ya kweli haijapatikana hasa katika suala hili la uendeshaji na usimamiaji wa uchaguzi katika ngazi zote. Masuala yanayohusu upatikanaji wa haki ya kupiga na kupigiwa kura, uwazi katika uendeshaji na usimamizi wa uchaguzi ni tatizo la muda mrefu.

Kwa mfano, chaguzi za Serikali za mitaa  katika kipindi hiki cha mfumo wa vyama vingi vya siasa, bado sheria zetu za uchaguzi zinaruhusu chaguzi hizi kuendeshwa na kusimamiwa na TAMISEMI, hili haliashirii uwezekano wa kuwa na chaguzu huru na za haki. Vile vile ukiangalia sura nzima ya uchaguzi mkuu uliowahi kufanywa takriban vipindi vitatu tokea tuanzishe mfumo wa vyama vingi unatoa picha halisi kwamba, uvumilivu wa kisiasa, kuaminiana na wanachi kuelewa haki zao ambazo ni vigezo muhimu vya demokrasia ya kweli Tanzania haijafikiwa. (Chaguzi za Zanzibar na kubatilishwa bila kufuata shera kwa matokeo katika maeneo mengi ambapo vyama vya upinzani vimeshinda katika chaguzi za vijiji na  vitongoji ni ushahidi tosha.)

Naomba ieleweke kuwa katika suala hili sina nia ya kurudia au kukumbushia mambo yaliyotokea mwaka 1995, 2000 na 2005(ambapo kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania ilizalisha wakimbizi (2000) na kuua raia wake wasiopungua (30) lakini ni kuonyesha kwa kiasi gani kuna changamoto ambazo Kambi ya Upinzani tunaziona bado zipo, na tunadhani zitaendelea kuwepo kwenye uchaguzi ujao-2009 na 2010 kama hazitachukuliwa hatua za haraka hasa katika maeneo yafuatayo:

Daftari la Kudumu la Wapiga Kura

Hili ni daftari muhimu sana kwani linasaidia kutambua idadi halisi na kamili ya watu waliojiandikisha kupiga kura na kupata idadi ya kura halali zinazostahili kupigwa. Hivyo inapotokea kura zimezidi idadi ya watu waliojiandikisha ni wazi kuwa uchaguzi huo utakuwa batili, lakini hata kama tunalo daftari hilo na tunaendelea kuliboresha, kama wananchi hawana elimu ya uraia daftari hilo halitatusaidia hata kidogo litasaidia zaidi Chama tawala ambacho kimejijengea uwezo mkubwa kutokana na raslimali za Taifa,ikiwemo raslimali watu. Cha kusikitisha ni kuwa katika maeneo mengine imetokea mara nyingi kwamba mtu amejisajili katika daftari la wapiga kura na kitambulisho anacho lakini anambiwa jina lake halionekani katika daftari hilo na kwa sababu hiyo anakosa haki yake ya kupiga kura. Jambo hili limetokea mara nyingi Zanzibar na wanatumia njia hiyo kama njia yakupunguza wapiga kura.

Kambi ya Upinzani tunatambua kazi inayofanywa na Tume ya Uchaguzi ya kuboresha daftari la wapiga kura, pamoja na upungufu mkubwa wa elimu ya uraia. Sanjari na hilo, ili kuweka mustakabali mzuri unaongozwa na uhuru na uwazi, basi wakati daftari hilo linaendelea  kuboreshwa ni vyema vyama vya siasa, wananchi pamoja na  wadau wote wa siasa wapatiwe nakala, ili nyakati za uchaguzi zikifika waweze kuchambua  na kama kuna mamluki basi waweze kutambuliwa. Na hii iwe katika ngazi zote za uchaguzi (kuanzia kata, jimbo na wilaya).

Mambo mengine ya kuzingatiwa ili kuhakikisha mpiga kura anapata haki yake, ni kwa daftari kuwa huru kwa wananchi (public document), yaoneshwe yatawekwa wapi na utaratibu gani utatumika ili watu waweze kukagua. Na katika elimu ya uraia, wananchi waelimishwe namna watakavyoweza kuweka pingamizi baada ya kukagua daftari hilo.

Ili kufanikisha mfumo mzima wa uboreshaji wa daftari la wapiga kura, ni vyema vyama vya upinzani kuwezeshwa na Serikali ili kuwawezesha mawakala wao kushuhudia uboreshaji wa daftari hilo.

Sharti la ukaazi, ambalo limekuwa kikwazo kwa raia kupata haki ya kuchagua na kuchaguliwa kutokana na kutokupewa haki ya kujiandikisha kwa sababu ya kutotimiza sharti la ukaazi (sheria kifungu cha 7 (2) na (3) katiba ya Zanzibar, na kifungu 12(1) na (3) cha sheria ya uchaguzi namba 1ya mwaka 1985 na marekebisho yake ya mwaka 1992.

Rushwa wakati wa Uchaguzi

Sote tunatambua kuwa rushwa ni adui wa haki, na kwa hakika hakuna mtu anayeipenda rushwa. Lakini rushwa katika nyakati za chaguzi zetu imekuwa ni kama jambo la kawaida. Napenda kuipongeza mahakama kwa kupinga matumizi na uhalali wa sheria iliyokuwa inaruhusu TAKRIMA. Lakini changamoto bado ipo kutokana na ukweli kuwa mpaka leo Muswaada wa kufuta sehemu hiyo ya sheria bado haujaletwa Bungeni.Aidha ule utaratibu aliusema Rais,wakati akihutubia Bunge tarehe 30.12.2005 kwamba atahakikisha kuwa utaratibu unawekwa ili kila mgombea na chama chake mapato yao yanawekwa wazi na kiwango cha matumizi kwa uchaguzi husika kinajuilikana. Hadi leo hakuna utekelezaji wake wakati ni mwaka mmoja tu kwa uchaguzi wa Serikali za mitaa na miaka miwili tuu imebaki tuingie kwenye mchakato mwingine wa uchaguzi mkuu.

Tume ya Uchaguzi

Tume ya uchaguzi ni chombo muhimu chenye mamlaka ya kusimamia na kuratibu mchakato mzima wa chaguzi zetu hapa nchini. Ikumbukwe kuwa Tume ya Uchaguzi ni chombo pekee chenye jukumu la kusimamia uchaguzi kuanzia katika hatua ya uandikishaji, upigaji,  kuhesabu kura na kutangaza mshindi. Katika nchi  inayoongozwa na siasa huria, Tume ya uchaguzi inastahiki kuwa huru ili iweze kufanya kazi zake kwa uwazi na isiwe na uhusiano wowote na Serikali inayotambulika wakati huo, kwani chama na  Serikali iliyo madarakani ni moja katika vyama vinavyopigana kushinda uchaguzi pia.

Hali halisi hapa nchini kwetu ni tofauti sana inaonesha kuwa Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi anateuliwa na Rais, na ana jukumu la kuripoti katika Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Bara na Ofisi ya Waziri Kiongozi kwa Zanzibar. Ieleweke kuwa sisemi kuwa Tume ya Uchaguzi ya Tanzania haifanyi kazi yake, bali suala la “loyality” ndio linalotutisha sisi vyama vya upinzani. Hivi kweli unaweza kufanya kazi ya kihalali ambayo inaweza kumtoa mwajiri wako madarakani? Hali hii si nzuri na inasababisha vyama vingine kutokuwa na imani na uchaguzi, na hata wale wenye dola wanaweza kutumia nafasi yao vibaya kwa kuwatumia wakurugenzi na watendaji wengine kwa kuwatishia nafasi zao kazini.

Hii ni changamoto kubwa, Kambi ya Upinzani inashauri kuwa Serikali iweke bayana kuwa Tume ya Uchaguzi ya Taifa ni lazima ijitegemee na isiingiliwe na mtu, taasisi, Chama au Serikali yoyote. Na uteuzi wa wajumbe wake uwe ni wa kuomba na unaozingatia viegezo katika ngazi zote.

Utawala kwa Misingi ya Katiba

Katika taifa lolote linalohitaji kuwa na demokrasia ya kweli katiba ya nchi huundwa kwa kuzingatia matakwa na mahitaji ya msingi ya wananchi wake hasa kwa vile wananchi ndio msingi wa mamlaka yoyote ile. Hii ni kwasababu katiba ndio yenye kuweka mipaka ya kila moja ya asasi katika jamii. Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imebainisha wazi katika ibara ya 3 (1) kuwa “Jamhuri ya Muungano ni nchi ya kidemokrasia na ya kijamaa, isiyokuwa na dini, yenye kufuata mfumo wa vyama vingi vya siasa.”  Kiujumla Katiba, ni sheria mama ya sheria zote nchini inayogusa nyanja na mifumo yote ya Utawala wa nchi kisiasa, kiuchumi na kijamii, na ndio  inayotoa mwelekeo wadea nyanja hizo ikiwemo mfumo wa siasa huria hapa nchini mwetu.

Katiba yetu katika ibara ya 20 (4) inapiga marufuku mtu kulazimishwa kujiunga na chama chochote cha siasa. Kama ni haki ya kila mwananchi kushiriki katika shughuli za Serikali yake; na kwa kuwa ni marufuku kulazimishwa kujiunga na  chama cha siasa ambacho katika sheria ya uchaguzi imefanywa kuwa ni kigezo pekee cha kupata haki ya kuchaguliwa, na wakati huo huo, kwa mujibu wa ibara ya 13 (2) ya Katiba, ni marufuku kwa Sheria yoyote kuweka sharti lolote ambalo ni la kibaguzi , ama wa dhahiri au kwa taathira yake, jee, kuendelea kupinga wagombea binafsi katika chaguzi zetu si ubaguzi wa aina hiyo  unaokataliwa na Katiba?

Kambi ya Upinzani inatambua kuwa matatizo haya yanayojitokeza ndani ya Katiba yanapaswa kurekebishwa kulingana na muda. Utamaduni usidumaze mabadiliko ya msingi yanayohitajika. Katika hali ilivyo sasa, tatizo hili ni changamoto ya hali ya juu kwa nchi yetu na siasa huria. Nadharia ya siasa huria inaweka wazi kuwa lazima watu wote wawe na haki sawa ya kushiriki katika siasa bila  kuwekewa vipingamizi visivyo na msingi, kama hiki cha mgombea binafsi.

Utawala wa Sheria

Utawala wa sheria ni moja ya nyenzo muhimu ya kuwezesha siasa huria na demokrasia makini katika taifa lolote lile. Kinyume chake ni vurugu. Hii ni kwa sababu uwepo wa sheria bora na taasisi zinazofuata sheria zinahakisha mwenendo sawia wa haki ya kila mmoja kushiriki katika siasa ikijumuisha kupewa haki yake ya kuchagua na kuchaguliwa.

Kwa Tanzania tuna changamoto kubwa katika kulifika hili kwasababu mara nyingi kumekuwa na matumizi ya nguvu za dola dhidi ya wananchi hasa katika kipindi cha harakati za uchaguzi na kampeni za uchaguzi. Vile vile changamoto nyingine katika hoja hii ni kuwa uhuru wa ushiriki wa wanachi katika siasa huria unabanwa sana na sheria za nchi ikiwemo katiba na sheria zingine kama vile za vyama vya siasa na nyinginezo. Inashangaza kwamba pamoja na kusema kuwa tuna demkrasia huria lakini hadi leo sheria zetu hazijahakisha uhuru wa kila mtu kushiriki katika siasa kwa kule kulazimisha ushiriki huo utokane na vyama vya siasa. Kwa upande mwingine siasa huria bado zinakabiliwa na changamoto ya kuweko na nguvu kubwa za kisheria zilizowekwa kwa watu au vyombo fulani ambavyo vina taathira kubwa katika upatikanaji wa matakwa halisi ya washiriki wa siasa hizo nchini.

Mfano, Katiba ya Jamhuri ya Muungano nchini inampa rais madaraka makubwa ya kuteua tume ya uchaguzi na watendaji wakuu wake wote. Ibara ya 74(1) na (2) inasema kuwa kutakuwa na Tume ya Taifa ya uchaguzi itakayoteuliwa na rais. Hii ni wazi kuwa tume hii itawajibika kwa rais na haiwezi kwenda kinyume na matakwa yake. Kwa msingi huu siasa huria za uwakilishi hapa hakuna. Katika nchi zinazofuata siasa huria, tume hiyo hata kama itateuliwa na Rais, huthibitishwa na Bunge, na  hutoa taarifa zake Bungeni.

Kana kwamba haitoshi, ibara ya 74(12) inaipa tume ya uchaguzi madaraka makubwa mno kwa kuipa uwezo kwamba uamuzi wake hauwezi kuulizwa katika mahakama yoyote ile ya Tanzania juu ya uchaguzi wa Rais. Swali jee ikitokea Tume imesimamia shughuli za uchaguzi na kutoa matokeo kinyume na uhalisia ni nani na kwa kipengele kipi tume hii itakosolewa kama katiba imeinyima uwezo wa kutekeleza hilo mahakamani. Kipengele hiki ni dhahiri kinyume na dhana nzima ya demokrasia. Tume ndiyo inayoanzisha mchakato wa uchaguzi, uaisimamia, unatangaza matokeo na kwa hatua yeyote, hata ikivuruga uamuzi wake eti ni wa mwisho!

Usawa katika Huduma za Jamii

Siasa huria kwa Tanzania bado hazijaendeshwa kwa mtazamo unaokubalika. Ni ukweli wa wazi kuwa katika baadhi ya maeneo hata usawa katika kutoa huduma za jamii unanyimwa kwasababu tu wananchi hao wanaonekana na itikadi tofauti ya chama. Mfano zipo sekta za umma mtu anaweza kukosa ajira au kuachishwa kazi kwasababu tu ya kuamini na kuwa mwanachama wa chama fulani.  Hakika hii ni changamoto kubwa sana kwani kwa kufanya hivi ni wazi kuwa jamii hailewi au inapuuza dhana mzima ya siasa huria.

Uhuru wa Kiutendaji wa Vyombo vya Habari na Ulinzi

Ni ukweli ulio wazi kuwa vyombo vya habari vina mchango mkubwa katika kufanikisha demokrasia na siasa huria. Changamoto inayoikabili sekta hii muhimu ni kule  kuandamwa, kutishiwa na kuingiliwa na mamlaka za kiserikali na hata viongozi wa ngazi za juu pale inapojaribu kufanya kazi zake hasa kwa kufichua maovu ambayo yanafanywa na viongozi wakubwa wa kiserikali. Hali hii haisharii kuwepo uhuru kamili wa vyombo vya habari.

Pia tatizo jingine ni rushwa katika vyombo vya habari.  Baadhi ya vyombo hivi vina kawaida ya kutumiwa na vyama tawala na serikali katika kutangaza sera zake na mambo yake na hutoa nafasi finyu kwa vyama vya upinzani au baadhi ya wakati vinaweza kupotosha ukweli wa jambo kwa sababu ya kulinda maslahi fulani na sio ya taifa kwa ujumla.

Aidha, vyombo vya ulinzi na usalama navyo vinatakiwa kutambua nafasi yao katika serikali ya vyama vingi na hivyo kujiepusha kushabikia chama chochote kwa minajili ya itikadi. Kwani vyombo hivi ni vyetu sote na vinaendesha kwa kodi zetu sote.Hapa pana changamoto kubwa kuvitoa vyombo vya ulinzi katika mazoea ya mfumo wa chama kimoja na kuviamini vyama vipya vilivyoanzishiwa na viongozi waliokuwa hawakuwazoe.

Ukweli na Uwazi wa Serikali Kiutendaji

Mheshimiwa mgeni rasmi, kwa nafasi ya kipekee napenda kuwapongeza wabunge wote wa Upinzani kwa kuweza kufanya kazi yao ya uwakilishi wa wananchi bila woga wowote. Nalitanguliza hili kwasababu, ndani ya miaka miwili wabunge wa Kambi ya Upinzani wamefanya kazi kubwa, wameweka historia, wameweza kuleta mageuzi makubwa bungeni hali iliyopelekea takriban wabunge wote kuweka UTAIFA MBELE NA ITIKADI NYUMA.

Lakini pia nitakuwa mwizi wa fadhila kama sitamsifia Spika wa Bunge letu Mhe. Samuel Sitta kwa kuridhia marekebisho makubwa ya kanuni za kudumu za Bunge ambazo sasa zinatupa uwanja mpana wa kufanya kazi zetu wakati wote, tukilindwa na kanuni za bunge. Pamoja na hayo, waswahili wanasema katika kila lenye kheri na shari ndani yake ipo. Nalibainisha hili kwasababu bado matatizo makubwa yapo ndani ya bunge letu na hasa kwenye nafasi ya Spika na namna ya upatikanaji wake. Katika sheria na kanuni zetu za bunge imewekwa wazi kuwa Spika atateuliwa miongoni mwa wabunge au nje ya Bunge ilimradi anatoka katika chama cha siasa kilichokuwa na usajili wa kudumu. Lakini kwasababu hatuna nafasi ya mgombea binafsi, basi katika bunge letu Spika ni lazima atoke katika moja ya vyama vya siasa. Na hivyo anashiriki katika vikao vyote vya chama chake na bado ataendelea kuheshimu maamuzi ya “party cocus.”

Katika hoja yangu hii sikusudii kusema kwamba Spika wetu anapendelea upande wowote, bali nataka niweke wazi kuwa laiti kama Spika angekuwa huru asiyefungamana na itikadi za chama chochote. Jee hatuoni kuwa demokrasia ingezidi kuwa nzuri zaidi?

Mfano: muhimili wa pili wa dola, yaani Mahakama, ili kutoa haki ipasavyo majaji hawaruhusiwi kikatiba kuwa wanachama wa chama chochote cha siasa. Je, kwa nini hili lisifanyike kwa Spika wa Bunge kutotoka chama chochote cha siasa kwa vile bunge ndio muhimili wa kwanza wa dola? Ni wasiwasi wetu kuwa baadhi ya wakati ‘party loyality’ ya Spika yaweza kuathiri maamuzi ya msingi ya bunge kutofikiwa.

Kambi ya upinzani inaona changamoto iliombele yetu nikuwa na mfumo kama wa Kenya, Mbunge akichaguliwa kuwa Spika alazimike kujiuzulu nafasi yake ya Ubunge ili aweze kuwa huru katika kuendesha shughuli za Bunge.

Uwajibikaji wa Serikali

Msingi mkuu wa uongozi wa nchi ni Katiba. Lazima kiongozi yoyote atii na aheshimu Katiba ya nchi na misingi yake. Na raia wote wanapaswa kutii Katiba ya nchi. Huo ndio unapaswa kuwa msingi mkuu wa utawala bora, kwa serikali na Watanzania wote (hata kama katiba hiyo ina mapungufu). Kuwa na nafasi ya uongozi katika serikali na taasisi yake isiyotoa taaswira ya utaifa ni moja katika misingi inayojenga hatma mbaya ya taifa letu. Mfano ulio hai ni muundo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ambapo imeitenga jamii ya kisiwa kimoja. Aidha watendaji wa taasisi na vyombo vya ulinzi havina taswira ya Utaifa. Kambi ya Upinzani inaona hii ni changamoto kubwa kwa ustawi wa Taifa letu hivyo ni lazima irekebishwe haraka.

Katika historia ya Tanzania na hasa katika kipindi hiki cha Serikali ya awamu ya nne mabadiliko makubwa yametokea. Nafurahi kutamka wazi kuwa Kambi ya Upinzani pamoja na uchache wetu na matatizo mengi tunayokumbana nayo lakini tumeweza na tutaendelea kufanya kazi zetu kwa msingi wa kulinda kiapo chetu cha kuwatumikia Watanzania bila ya woga. Hoja zinazoibuliwa na upinzani ni hoja nzito, zenye kujali maendeleo na ustawi wa kila mtanzania ambae anaishi katika mazingira ya umasikini uliokithiri.Utaifa, uzalendo na ushirikiano wa hali ya juu tunaoupata kutoka kwa wananchi, vyombo vya habari na asasi za kijamii unatupa sisi uwezo wa kuibua mijadala mizito ambayo pengine inaihusu Serikali, taasisi hata watu binafsi ambao hawana mapenzi na nia njema na nchi yetu.

Katika kipindi hichi mmeshuhudia udhaifu wa Serikali katika kusimamia na kutekeleza ahadi na Sera ambazo zinatokana na Ilani ya uchaguzi ya CCM hadi kufikia kiwango cha wabunge wa CCM kutafautiana katika kutekeleza baadhi ya yaliomo ndani ya ilani yao. Mfano ulio hai ni kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi, kuwachukulia hatua waliotuhumiwa kwa ufisadi, na hata matamko ya kukurupuka ya viongozi wetu wa ngazi za juu. Aidha kushindwa kwa CCM kukamilisha mazungumzo ya kutafuta ufumbuzi wa kudumu kwa Mpasuko wa Kisiasa Zanzibar, ucheleweshaji wa kupata maamuzi Serikalini  kinyume na ile sera ya ari mpya kasi mpya, ni changa moto kubwa kwa hatma ya Taifa letu kwani inazorotesha mageuzi ya kidemokrasia na utawala bora na Uwajibikaji.

.

Kambi ya Upinzani inaona kuwa hii ni changamoto kubwa na jambo hili likifanyiwa kazi haraka kutokana na ukubwa wake watanzania watarudisha imani kwa uongozi wao ambao sasa unaonekana kama umekosa DIRA.

Mustakabali wa Taifa

Mheshimiwa Mgeni Rasmi, tokea Nchi yetu ipate Uhuru (Tanganyika) 1961  kukawa na “Republic of Tanganyika”  na baada ya  Mapinduzi (Zanzibar) 1964, kukawa na “People’s Republic of Zanzibar” na hatimaye Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja Seriakali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Nchi yetu imeongozwa na TANU na ASP na Hatimaye CCM. Hivyo ni dhahiri kuwa mafanikio na mapungufu yote ya maendeleo ya Nchi yetu yametokana na Uongozi na Sera za CCM, ambayo ni mrithi wa TANU Na ASP.

Ni wajibu wetu sote kujiuliza, katika kipindi hichi chote cha uongozi wa aina moja. Je kwa sera zilizokuwepo na zilizopo Mtanzania wa kawaida maisha yake yameboreka? Kwamba sasa anaweza akapata angalau milo miwili bila ya wasi wasi? Mwananchi wa kawaida anaweza akasomesha watoto wake na watoto hao wakasoma vizuri na hatimaye wakapata ajira? Au anaweza kujiajiri kwa kupata mikopo kwa urahisi yenye riba nafuu? Au Anaweza kupata huduma ya kijamii bila ya kulipia kwa gharama kubwa na kama anaweza kupata bei muafaka ya mazao yake kwa kuuza anakotaka kama ilivyokuwa kabla ya Uhuru na Mapinduzi? Je hata anayefanya kazi amepata mshahara unaokidhi muda wake wa kazi na mahitaji yake? Je anaweza vile vile kuchangua na kuchaguliwa bila ya pinganizi lolote, au bila kutumia fedha (Rushwa), na kwamba anayechagua anaridhika na matokeo (KURA YAKE INAHESHIMIWA)? Je rasilimali za nchi zinatumika kwa maslahi ya wananchi au ni wageni na watanzania wachache tuu ndio wanaofaidika?

Tunapo kumbushana haya hatusemi kwamba Tanzania hakuna maendeleo au mabadiliko, lakini je maendeleo hayo ni endelevu kiasi cha kumhakikishia Mtanzania kwamba baada ya “Sera ya Kilimo ni Uhai” ya Mwaka 1976, je tunajitosheleza kwa chakula cha kutosha na hata ukame ukitokea tuna chakula cha akiba? Au bado tunaendelea kuhemea chakula? Kwamba hadi leo tunaagiza mbegu kwa kiwango kisichopungua asilimia sitini (60%),  Kwamba tuliwahi kuwa na hekta 450,000 za umwagiliaji sasa zipo 278,888 tu, hayo ni maendeleo endelevu? Kwamba Mwalimu alituambia “kupanga ni kuchagua.” Je, kununua ndege kwapesa taslim Tsh 42 billion, inayoweza kutua katika viwanja visivyozidi vitano katika nchi nzima na hata kushindwa kutua Dodoma ambayo ni Makao Makuu ya nchi na ya Bunge; ndege inayotumia wastani wa Tsh.6 million kwa saa ya kuruka na kuacha kuwatengenezea mazingira mazuri ya kujisomea wanfunzi wetu wa vyuo vikuu pamoja na kuwapatia fedha za kukidhi mahitaji yao ili kupata taifa lililo elimika?

Au ndio ule msemo wa Kiswahili kwamba “Punda afe lakini mzigo wa bwana ufike”. Kwamba huku unataka kumuondolea umasikini, upande wa pili unamuongezea kodi kwa mlango wa nyuma na kutumia rasilimali zake vibaya. Je kwa sera hizi zisizomjali mwananchi, uchumi utakua na umasikini kupungua kwa vigezo vya mellenium?

Mheshimiwa mgeni Rasmi, baada ya utafiti huu, sasa tunaweza kusema ni katika mwenendo upi taifa letu linakwenda? Kama tunapoelekea ni pazuri au la? Ikichangiwa na kukosekana kwa Uongozi Ulio Makini, viashiria vya siasa huria ya nchi yetu inajikita katika  mambo mengine makubwa, ambayo ni mapungufu ya Katiba, chaguzi mbovu pamoja na ufisadi na umasikini, ambavyo vimewanyima Watanzania ajira na ukuwaji wa uchumi unaofikia angalau asilimia 8%. Mustakabali wa taifa haujengwi kwa maneno mazuri, na tabasamu linalovutia bali ni kwa utendaji ulio makini na unaozingatia matatizo ya Mtanzania.

Laiti kama haya masuala yangefanyiwa kazi kwa wakati basi suala la ubaguzi kwa kigezo cha itikadi, mapungufu katika huduma za jamii, heshima katika haki za binadamu, ukuwaji wa uchumi unaotupunguzia utegemezi pamoja na matatizo mengine ya kijamii yangekuwa historia. Maendeleo hayapatikani kwa kuvumulia shida bali ni kwa kutafutia ufumbuzi matatizo yaliyopo mbele yetu. Shida haizoeleki.

Hitimisho

Hivyo basi mustakabali wa taifa letu hauna taswira nzuri, hasa pale tuliposhidwa kuwashirikisha wananchi kuwa na Katiba iliyo na ridhaa yao, kushidwa kupata ufumbuzi wa kudumu wa mpasuko wa kisiasa Zanzibar, kushidwa kumaliza kero za muungano na kuendelea kushindwa kutumia rasilimali za nchi kwa madhumuni ya kufikia lengo la kujitegemea. Hizi zote ni Changamoto za Siasa Huria na Mustakabali wa Taifa letu.

Ahsenti sana kwa kunisikiliza

……………………………………

Hamad Rashid Mohamed(MB)

Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s