Kukosa nia njema kwa viongozi ndicho kiini cha mgogoro wa Muungano

Na Juma Duni Haji

Juma Duni Haji, Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Zanzibar

Juma Duni Haji, Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Zanzibar

“Na hata kama hoja yetu (ya kutetea maslahi ya Zanzibar ndani ya Muungano) inaendelea kukataliwa, bado sisi hatuna sababu ya kuiacha eti tu kwa kuhofia kwamba tutatafsiriwa ni vibaraka wa walio nje ya Zanzibar. Watanganyika walikataa kutawaliwa na wakoloni wa Kiingereza wakapigania kujikomboa na mwaka 1961 wakawa huru. Na hata baada ya uhuru huo, wakakataa tena kunyanyaswa na Wakenya ndani ya EAC na mwaka 1967 wakauvunja umoja huo. Wazanzibari nao, kwa upande mwengine, walikataa kutawaliwa na Waingereza na Waarabu na wakadai na kupata uhuru wao takribani katika muda sawa na Watanganyika. Basi ni vyema ikaeleweka kwamba hawatakubali tena kutawaliwa na watu wengine, ukijumuisha hata hao wanaojiita waume zao. Kwamba haki ya kuwa huru ni haki ya kila jamii ya watu!”

Utangulizi

Ni ukweli usio shaka kwamba hoja na matatizo ya Muungano imekua ikizungumzwa sana kila mwaka unapofika mwezi wa Aprili na kwa bahati mbaya hakuna hatua ya vitendo iliyofanyika kuona kwamba matatizo hayo yanamalizika au angalau yanapungua. Kila mara tumebaki kuitisha makongamano ambayo wataalam huja kuonyesha umahiri wao au wanasiasa kueleza yale yanayowakera na kisha kila mmoja huondoka na kungojea kongamano lingine. Wataalam wa sheria na wanasayansi wa siasa hujifanyia utafiti na kujipatia digrii za kwanza, za pili na hata PhD kwa eti kufanya uchambuzi  wa matatizo ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Matatizo gani hayo yasiyokwisha maisha?

Tangu ilipotokea kuchafuka hali ya hewa hapo 1984 na kuishia kufukuzwa madarakani Mzee Aboud Jumbe na hapo 1988 wakafukuzwa akina Maalim Seif Sharif na wenzake 7, nimeacha kushiriki katika mjadala wa siasa za Muungano kwa sababu hakuonekani dhamiri njema  ya dhati kutoka katika viongozi wakuu wa nchi hii, iliyobatizwa jina la Tanzania, kumaliza lile tunaloliita tatizo sugu la Muungano.

Sishiriki kwa kuwa imekuwa ni utamaduni wa siasa za Tanzania kwamba asemapo Mzanzibari yeyote yule kuhusu hisia zake kwa Muungano huu, basi tafsiri yake ni kuchafua hali ya hewa hata kama anayoyasema yana ushahidi wa wazi na hoja yake ni madhubuti. Maisha wenzetu kutoka Tanganyika hawana kosa katika Muungano. Hata kama wanawatukana Wazanzibari matusi ya nguoni, bado huonekana wana haki hiyo maana wao ndio wenye kumiliki Muungano. Wazanzibari ni wabembezi tu. Hivyo ndivyo anavyoamini, kwa mfano, Mzee Pius Msekwa, Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, kwamba Wazanzibari hawana chao na wala hawana sababu ya kulalamika au kunung’unika.

Lakini, baada ya kuona na kusoma dharau isiyo mipaka ya baadhi – na si ajabu ya wote wanaoandika kuhusu Muungano kutoka Tanganyika, nimeona nami nieleze yale ninayoyaelewa. Kunyamaza kimya na kujitenga na mijadala hii, nimegunduwa hakutusaidii chochote kama watu wa taifa hili.

Tafsiri ya Muungano sasa inafanywa ikubalike kwamba ni ndoa ya Kikristo isiyo na talaka na kwamba Zanzibar imeolewa na Tanganyika. Katika jambo ambalo tumelielewa sana Waafrika ni uchungu wa kusikia au kuona Mzungu akimnyanyasa na kumnyima haki Mwafrika katika nchi yake na jina sahihi tunalompa Mzungu huyo ni mkoloni. Lakini bado manyanyaso, mateso au nchi moja ya Kiafrika kuitawala nyingine ya Kiafrika haikupata jina sahihi kisiasa.

Prof. Ali Mazrui aliuita Muungano wa Zanzibar na Tanganyika ni African-self-colonisation. Marehemu Mwalimu Julius Nyerere akipenda sana kutuambia kwamba ubepari hauna rangi. Ni sahihi pia kusema kwamba na ukoloni vile vile hauna rangi. Waindonesia waliitawala East Timor na hawakuiachia mpaka kwa kulazimishwa na Umoja wa Mataifa tena baada ya maisha ya watu wengi kupotea. Nchi za aina hiyo zinazopenda kuwatawala wengine katika Bara la Afrika zimeanza kuchipuka kwa kasi sana. Mfano wa wazi ni ule wa Ethiopia na Eritrea.

Tunajua kuwa mwaka 1964 Rais wa Zanzibar alikubaliana na Rais wa Tanganyika kuanzisha Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, ambao baadaye ulikuja kuitwa Muungano wa Tanzania, lakini leo mwaka 2006 Wazanzibari wamekua wakiitwa wanandoa wanaotafuta kuachwa: eti tumeolewa, ndivyo anavyoamini Hussein Siyovelwa (soma gazeti la Rai Toleo Na.667 (ISSN 0856-4973) la 11 Mei, 2006, makala ‘Muungano wetu hauna mwisho mwema ya Hussein Siyovelwa). Ati Hussein anatukumbusha kwamba sisi ni wake wa Tanganyika tu, na au kama hivyo sivyo basi ni vibaraka wa  mabwana zetu kutoka nje. Yaani hatuna uwezo wala hatustahiki kuwa na uwezo wa kudai haki zetu dhidi ya yule anayesema ni ndugu yetu wa damu.

Makala hiyo imefanya uchambuzi wa kina wa sifa na tabia ya ndoa inayolazimishwa kuvunjika na mwanamke asiyemtaka mumewe. Mwandishi amehakikisha kwamba ametoa kila sifa na ila za mwanamke wa aina hiyo na mwishowe bila kificho akaeleza kwamba hiyo ndiyo tabia ya Wazanzibari katika kulalamika kwao Muungano uliopo.

Mimi, kama Mzanzibari, lazima niseme kwamba nimesikitishwa sana na tashbiha ya Siyovelwa katika waraka ule na naona kwamba hayasaidii hata kidogo kuondoa udhaifu wa Muungano ambao umeendelea kuwepo kwa miaka 43 sasa.

Labda ni rahisi kwa watu kama Siyovelwa kuwadharau Wazanzibari katika kiwango hicho, lakini vipi kuhusu wale wataalamu wa Kitanzania wanaoheshimika kimataifa katika taaluma zao, kama Prof. Issa Shivji, Jaji Francis Nyalali na Jaji Robert Kisanga walioeleza udhaifu wa Muungano na kushauri marekebisho?

Huu ni upofu wa akili iliyokomazwa kwa itikadi ya chama kimoja na propaganda za vyuo vya ki-itikadi ambavyo, badala ya kutoa nafasi kwa vijana wa kizazi kipya kuuona ukweli, vimejenga umbumbu wa kiburi hata sasa wao wanawashinda wageni waliowatawala babu zao hapo zama za ukoloni!

Lakini Siyovelwa hayuko peke yake kutoka Tanganyika. Mwandishi mwengine maarufu, Makwaiya wa Kuhenga katika kipindi chake kinachorushwa na kituo cha televisheni ya Channel 10, Je Tutafika?, aliwahi kumuuliza Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad: “Vipi Maalim Seif, baada ya miaka 40 ya ndoa, leo bado munauliza kwamba baba yenu ni wa halali au si halali?” Maneno kama hayo yamekuwa yakisemwa ndani ya Bunge na hata katika mikutano ya kisiasa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) bila kificho.

Huku ni kukosa nadhari na kucheza na hisia za watu kiholelaholela. Nakumbuka, mwaka mmoja mara tu baada ya kuachiwa kutoka jela kwa ile kesi iliyoitwa eti ‘ya uhaini’, tulikutana na Jaji Sinde Warioba, aliyewahi kuwa waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano, pale Hoteli ya Mazsons Unguja. Tulimueleza kwamba hawana budi, kama watawala wakuu wa nchi hii, kumaliza matatizo wanayoyaita ya Muungano, kwani kama wanatuona sisi akina Duni ni wakorofi kizazi kinachokuja baada yetu kinaweza kuwa kikorofi zaidi maana hakuna anayekubali kufanywa koloni katika karne hii ya 21. Jaji Warioba alicheka na kutukejeli kwamba hayo ni mawazo ya uchungu wa kutoka jela, lakini leo kesi dhidi ya Muungano ipo mahakamani, tena imepelekwa na vijana wadogo sana na ambao hata si wanasiasa maarufu.

Tume ya Jaji Nyalali ilipita nchi nzima kukusanya maoni ya aidha tuwe na serikali mbili au tatu. Jaji Kisanga alitumwa kufanya hivyo na Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa. Kuna Kamati za Serikali aina kwa aina ikiwemo ile ya Shellukindo na ya Amina Salim Ali zikijaribu kutafuta ufumbuzi wa masuala haya ya Muungano. Makala nyingi zimekua zikiandikwa katika magazeti na kuzungumzwa kwenye vipindi vya redio na kuoneshwa kwenye vituo vya televisheni. Kwa jumla kila Rais mpya anapoingia, huja na kasi mpya ya ahadi nyingi kwamba suala la Muungano atalishughulikia.

Nakumbuka vyema wakati Rais Mkapa alipoingia madarakani, aliahidi mbele ya Bunge kwamba matatizo ya Muungano angeyamaliza kwa kipindi cha miezi sita tu. Leo ni miaka 10, naye ameingia Muungano ukiwa pabaya na ameuacha ukiwa pabaya zaidi. Kwa hakika, kama uovu alioufanya Mkapa, kwa kutumia kisingizio cha kulinda Muungano, kama wangefanyiwa ndugu za akina Siyovelwa, bila ya shaka Siyovelwa angekua wa kwanza kutaka Rais huyo mstaafu ashitakiwe.

Na hakika Siyovelwa anaonekana kupenda uhuru wa Waafrika na hasa Waafrika wa Tanganyika, na hivyo sijui angeonaje kama mtoto wake angebakwa na askari mbele ya macho yake na kulazimishwa atizame hilo likifanyika. Hayo yamefanyika Pemba na Unguja na Tume ya Hashim Mbita iliyathibitisha hayo, lakini mapendekezo ya ripoti hii hayajatekelezwa. Je, huo ndio uhuru tulioutafuta kutoka kwa Waingereza na Waarabu ulikusudia ni kuwoandoa watawala wa kigeni ili ipatikane nafasi na sababu nzuri ya kuwaua Wazanzibari?

Jichoni pa watawala wa Tanganyika na mawakala wao, maisha ya Mzanzibari hayana thamani ukiyalinganisha na ya Watanania wengine. Ushahidi umeonekana juzi tu ambapo mauaji ya Polisi dhidi ya wafanyabiashara kwa kisingizio cha ujambazi yalimlazimisha Rais Jakaya Kikwete kuunda tume kuchunguza vifo hivyo, na sasa wahusika wamefikishwa mahakamani kujibu mashitaka ya mauaji. Sijui ikiwa akina Siyovelwa wanajuwa – au angalau kama wanathamini – kwamba kwamba wale waliowauwa Wazanzibari, Unguja na Pemba, tarehe 26 na 27 Januari 2001 ni maafisa wa jeshi hilo hilo la Polisi na ambao wanajulikana, lakini hadi leo hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa na viongozi wa kitaifa au wa Polisi dhidi yao?

Lakini, yumkini akina Siyovelwa wanajuwa hayo, isipokuwa sababu za kutojali wala kutoshughulika nalo ni hili alilolisema kwenye makala yake, kwamba Wazanzibari ni wanawake tu walioolewa: hawana haki ya kuhoji kuuliwa kwao na waume au watoto wa waume zao.

Sisi Wazanzibari tunaumizwa na ukweli huu tunaoishi nao: wa kutothaminiwa maisha na hatima yetu ndani ya Jamhuri ya Muungano, ambao sisi ni washiriki muhimu. Hivi karibuni imetangazwa kwamba aliyemtesa mbwa wa mzungu kule Mererani, amefungwa muda usiopungua mwaka mmoja, lakini wakati huo huo Wazanzibari wamekuwa wakiuliwa kwa makusudi tena bila kosa na mwisho wauaji hupewa vyeo, tena si mara moja wala mbili. Ni bahati mbaya sana kwamba tunapolalamikia mambo kama hayo, akina Hussein huibuka wakasema kwamba kulalamika huko ni tabia ya mwanamke anapotaka kuachwa.

Vijineno hivi vya maudhi vinaweza kuwa na athari mbaya sana kwa Muungano huu. Inakumbukwa kwamba baina ya mwaka 1967 na 1977 kulikua na umoja unaoitwa Umoja wa Afrika Mashariki (EAC) na kwa taarifa yake ni kwamba Mwalimu Nyerere kwa kiburi cha kutompenda Charles Njonjo, Mwanasheria Mkuu wa Kenya, aliufunga mpaka kati ya Tanzania na Kenya na hatimaye akauvunja umoja huo. Na kisa ni hivyo hivyo vijineno vidogo vidogo vya dharau na kebehi kutoka kwa baadhi ya washirika wa Muungano, Tanzania ikiwemo.

Sina hakika kwamba na Mwalimu Nyerere alipokuwa akilalamika ilikuwa ni kwa sababu ya kukataa mume Mkenya au kwa sababu ya kuona kwamba EAC haikuwa na maslahi naye na kwa nchi pia. Si hilo tu, ila pia Tanzania ilijitoa katika Umoja wa Biashara ya Nchi za Mashariki na Kati (COMESA) kwa maelezo kwamba umoja huo ulikua hauna faida kwake. Pamoja na kubembelezwa na nchi nyenzake, bado Tanzania imetoka katika umoja huo.

Nimeamua kueleza upande mwengine wa hoja ya Siyovelwa ili kumuonesha udhaifu alionao yeye na wengi wale wasiopenda haki na maelewano ya Watanzania kwa maslahi yao au kwa sababu wao ndio wenye kunufaika. Sisi wenzenu tumeamua kueleza uovu wa Muungano kwa nia ya kujenga na wala si kwa nia ya kutaka talaka. Na ieleweke vyema kwamba hakuna asiyejua kwamba matatizo yapo na kama tutajidai kutafuta udhaifu wa maneno kuwakandamiza Wazanzibari, ni wazi historia itatuhukumu.

Na hata kama hoja yetu inaendelea kukataliwa, bado sisi hatuna sababu ya kuiacha eti tu kwa kuhofia kwamba tutatafsiriwa ni vibaraka wa walio nje ya Zanzibar. Watanganyika walikataa kutawaliwa na wakoloni wa Kiingereza wakapigania kujikomboa na mwaka 1961 wakawa huru. Na hata baada ya uhuru huo, wakakataa tena kunyanyaswa na Wakenya ndani ya EAC na mwaka 1967 wakauvunja umoja huo. Wazanzibari nao, kwa upande mwengine, walikataa kutawaliwa na Waingereza na Waarabu na wakadai na kupata uhuru wao takribani katika kuda sawa na Watanganyika. Basi ni vyema ikaeleweka kwamba hawatakubali tena kutawaliwa na watu wengine, ukijumuisha hata hao wanaojiita waume zao. Kwamba haki ya kuwa huru ni haki ya kila jamii ya watu!

Tunachoelewa ni kuwa mahusiano kati ya Tanganyika na Zanzibar katu hayakuwa ya mkubwa kumtawala mdogo, bali kujenga umoja wenye nguvu ili wengine waone na kutuunga mkono. Miaka 43 sasa hakuna hata nchi moja jirani yetu iliyopendekeza kujiunga nasi. Juzi wakati, akiwa safarini Marekani, Rais Kikwete alitamka bayana kwamba Shirikisho la Afrika Mashariki litakua na faida tu kama wananchi watalikubali, siyo viongozi watatu pekee. Hivyo pia ndivyo inavyopaswa kusemwa kwa uhusiano wa Zanzibar na Tanganyika.

Na hapa ni bora tukawakumbusha akina Siyovelwa ukweli mmoja: kwamba wakati wa kupigania ukombozi wa Zimbabwe, Wazanzibari walishiriki kwenye mapambano kama Watanzania. Wakati wa kumuondoa nduli Idi Amin wa Uganda alipochukua sehemu ya Tanganyika kule Bukoba, Wazanzibari walishiriki kama Watanzania. Na, kwa hakika, vita vyote vya ukombozi wa Kusini mwa Afrika ambavyo Tanzania ilipeleka askari wake, walikuwemo Wazanzibari wengi na wamepoteza maisha kwa niaba ya Tanzania. Wala haikusemwa hawa ni wanawake. Sasa kwa nini pale panapoonekana maslahi ya fedha au rasilimali asilia tu, ndipo Wazanzibari wahisabiwe kama wanawake? Kama hoja ya kuonekana mafuta huko Pemba ni kuwakera wakubwa pale Wazanzibari wanapotetea, mbona hivi sasa gesi ya Songosongo haizungumzwi kama ni yetu pamoja na akina Siyovelwa wamenyamaza kimya juu yahilo?

Basi ni kutokana na hali kama hii, ndio maana jina la waraka huu ni “Ukosefu wa nia njema kwa viongozi wa Muungano na wa CCM ndio kiini cha matatizo ya Muungano.” Ukweli ni huo: viongozi hawa ndio sababu ya kushindwa kupatikana ufumbuzi wa matatizo ya Muungano. Sasa Rais Kikwete amesema yuko tayari kutatua matatizo ya Muungano na kwa sababu hiyo amesema tuseme ukweli ulivyo. Naomba kueleza ukweli huo kwa kuchukua baadhi tu ya masuala ya msingi yaliyovurugwa na Mwalimu Nyerere ambaye wengi wetu tunashindwa kumsema eti kwa kuonekana ni nabii wa siasa.

Miongoni mwa makosa makubwa sana ya Mwalimu Nyerere ni kwamba, kila lilipotokea tatizo katika Muungano huu, hakuwa akilitatua bali akiliakhirisha, tena kwa kuwatisha wanaoyatoa ama kwa kuwafukuza katika uongozi wa Chama na Serikali au kwa kuwafungulia kesi za kubuni za uhaini na uchochezi. Mwalimu Nyerere alikuwa mgumu wa kujifunza kwamba njia hizo hazikuwa zikisaidia chochote na badala yake zilizidi kuyalimbikiza matatizo ya Muungano hadi leo tumeamua kuyabambikiza jina la kero, yaani mambo yanayoudhi. Kama kuna mtu yeyote, basi ni Mwalimu Nyerere ndiye aliyekuwa kiini cha matatizo ya Muungano huu na aliona aibu kujulikana kwamba udhaifu huo ameufanya yeye, ndiyo maana akawa anatafuta visingizio hivi na vile.

Mimi naomba nieleze kadhia ya Muungano chini ya vifungu vifuatavyo:

 • Kuwepo au Kutokuwepo kwa Serikali ya Tanganyika
 • Tume ya Fedha ya Muungano na Mahakama ya Katiba
 • Kuchezewa kwa Mkataba wa Muungano
 • Mchango wa Zanzibar katika Matumizi na Mapato ya Muungano
 • Kuanzishwa kwa Benki Kuu na Haki za Zanzibar katika Benki hiyo

Kuwepo au kutokuwepo kwa Serikali ya Tanganyika

Imekua ni mtindo wa viongozi wa siasa wa Tanganyika kutetea kwa kusema kwamba eti hakuna Serikali ya Tanganyika na hivyo haingewezekana kufanya mazungumzo juu ya mgogoro huu kati ya Serikali hiyo na ile ya Zanzibar. Mimi naamini kwamba hoja hii ni dhaifu. Kila mtu anafahamu kwamba Muungano huu ni kati ya nchi mbili, Tanganyika na Zanzibar. Popote penye Muungano, lazima kutakua na washiriki zaidi ya mmoja. Mwalimu Nyerere alisema hayo alipohojiwa na gazeti la Observer la Uingereza tarehe 20 Aprili, 1968:

“If the mass of the people of Zanzibar should, without external manipulation, and for some reason of their own, decide that the union was prejudicial to their existence, I could not bomb them into submission…The Union would have ceased to exist when the consent of its constituent members was withdrawn.” (Nyerere: London Observer: 1968)

Kwa ufupi, Mwalimu Nyerere alisema kwamba Muungano wa Tanganyika na Zanzibar hautokuwepo kama wale walioungana watatoweka au watakuwa hawapo.

Kama Mwalimu ni mtu wa hekima, basi ni vyema kukumbuka yale aliyokuwa akisema na kuandika, kwa hivyo kama hivi sasa hakungekuwa na Serikali ya Tanganyika – na kwa maana ya Mwalimu Nyerere – kungekuwa hakuna Muungano tena tangu hapo aliposema.

Lakini la kujiuliza ni ikiwa kweli Serikali ya Tanganyika haipo na, kama haipo, kaifuta nani na kwa nini. Ukitaka kuelewa hoja hii, ni vyema msomaji akarudia kwenye sheria zilizoamrisha kufutwa kwa serikali hiyo. Makubaliano ya Muungano ya 1964 kifungu Na.(iv) kinasomeka hivi:

“…and in addition (the Union Parliament) shall have exclusive authority in respect of all other matters in and for Tanganyika.”

Hiki ndicho kifungu cha Makubaliano kilichotumika kuanzisha mgongano wa Muungano. Maneno “and in addition” maana yake kwamba Bunge linatekeleza shughuli za mamlaka mbili. Lakini Mwalimu Nyerere akaifanya kuwa mamlaka moja ili ionekane kwamba Bunge la Tanganyika halipo na Rais wa Tanganyika hayupo.

Mara zote tunapotaja Tanganyika, wengi ya wale walio Tanganyika hasa viongozi wa dola na wale wa CCM huwa hawapendi na hutuona sisi kama tunawarejesha nyuma katika ‘kuimarisha’ Muungano. Ukweli ni kwamba jina hilo halipendwi kwa sababu kunafichwa aibu fulani iliyofanyika hapo 1964 ambayo ndiyo kiini cha mgogoro wa Muungano. Katika Makubaliano ya Muungano hakuna kifungu kinachotoa ruhusa   kufutwa kwa Serikali ya Tanganyika. Serikali ya Tanganyika imelindwa na kifungu Na.(v) cha Makubaliano hayo kinachosomeka kwamba:

“The existing laws of Tanganyika and Zanzibar remain in force in their respective territories.”

Yaani sheria zilizopo za Tanganyika na Zanzibar zitaendelea kutumika katika maeneo yake (za Zanzibar kwa Zanzibar na za Tanganyika kwa Tanganyika)

Mkataba wa Muungano ndio sheria kuu (grand norm) ya Muungano, kwa upande mmoja, na Katiba ya Tanganyika ya wakati huo ilikuwa ndiyo sheria mama ya Tanganyika. Vyote viwili, Mkataba wa Muungano na Katiba ya Tanganyika havijaagiza kufutwa kwa serikali ya Tanganyika. Kwa hivyo, Katiba hiyo ya Tanganyika inapaswa iwepo na viongozi wa Tanganyika wawepo ili kusimamia mambo ya Tanganyika ambayo si ya Muungano. Na la kujiuliza hapa ili kujiridhisha kwamba kumbe Tanganyika hasa ilikuwepo na imekuwepo ni kwamba kama hakuna Katiba, sheria hizo zingetumikaje katika Tanganyika isiyo Katiba?

Lakini inasikitisha sana kuona baada ya makubaliano hayo Bunge la Tanganyika lililokaa kupitisha sheria ya kukubali Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, kwa makusudi, lilikubali kuifuta katiba ya Tanganyika na hivyo kuifuta Serikali yenyewe. Maana ukishafuta katiba hizo sheria nyingine za Tanganyika zitasimama kwa katiba ipi? Katika sheria hiyo kifungu chake cha 7 kinasomeka hivi:

“On the commencement of the Interim constitution of the United Republic, the Constitution of Tanganyika shall cease to have effect for the Government of Tanganyika as a separate part of the United Republic.”

Yaani “Mara tu itapoanza kutumika katiba ya muda ya Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, katiba ya Tanganyika itasita kutumika kwa ajili ya Serikali ya Tanganyika kama ni sehemu mbali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.”

Hili lilifanyika kwa maksudi ili viongozi wa Tanganyika kujipa nafasi ya kujikweza na kuikweza serikali yao iliyojibadili na kuwa ndiyo Serikali ya Muungano. Kwa Kiingereza ni kwamba: The government of Tanganyika underwent metamorphosis to become a Union Government.

Huu ndiyo udanganyifu kwa kutumia kalamu ulivyofanyika hapo 1964. Sheria Na. 22 ya 1964 inayoitwa Union of Tanganyika and Zanzibar Act 1964 ilipitishwa na Bunge la Tanganyika 25/4/64 kabla Muungano kuanza. Wakati huo na siku ile kulikua hakuna Bunge la Muungano maana lililazimika liundwe baada ya sheria hii kupitishwa na wawemo wabunge wasiopunga 32 kutoka Zanzibar (wajumbe wa Baraza la Mapinduzi).

Makubaliano ya Muungano kisheria hayawezi kubadilika au kubadilisha katiba ya Tanganyika. Kufuta katiba ya Tanganyika hakuna uhusiano wowote na Makubaliano yale. Na hata kama katiba hiyo ndiyo iliyotumiwa kuweka Katiba ya Muda ya Muungano, lakini baada ya kufanyiwa mabadiliko ilipatikana katiba ya muda ya Muungano na kuiacha ile ya Tanganyika pekee.

Hakuna mahali katika Makubaliano palipoagiza kufutwa katiba hiyo wala kumuondoa Rais wake wa Tanganyika. Muda wote wa utawala wake, Mwalimu Nyerere alistahiki kuwa Rais wa Tanganyika na Rais wa Jamhuri ya Muungano kama ambavyo Mzee Abeid Karume alivyobaki kuwa Makamo wa Rais  wa Jamhuri ya Muungano na Rais wa Zanzibar. Maelezo haya yanaweza kufananishwa na hali ya Rais Kikwete hivi sasa, ambaye kuchaguliwa kuwa mwenyekiti wa chama chake cha CCM hakumfanyi asiwe rais wa Jamhuri, maana hizi ni dhamana mbili tafauti.

Kitendo hiki ndicho kilichotumika kuharibu utaratibu na mfumo mzima wa mwenendo wa uatawala katika shughuli za Muungano kwa miaka 42 sasa. Siku ile ile wafanyakazi wote wa Serikali ya Tanganyika wakawa wafanyakazi wa Muungano, Mahakama ya Tanganyika ikawa ndiyo ya Muungano, na Majaji wake wakawa ndio majaji wa Muungano, muhuri wa Tanganyika nao ukawa ndio Muhuri wa Muungano (Public Seal). Kwa nini udanganyifu huu? Ni kwa sababu ya ukosefu wa nia njema.

Katika sheria ile Na. 22 ya 1964, Rais wa Tanganyika amejipa madaraka ya kutunga kanuni zilizompa uwezo wa kutoa maagizo yanayohusu mambo ya Muungano kwa kutumia decrees za sheria ya Tanganyika. Pamoja na kupewa madaraka hayo na Makubaliano ya Muungano, lakini kanuni hizo zilikuwa zitungwe na Bunge la Muungano siyo Bunge la Tanganyika.

Siku ilipopitishwa sheria hii Na 22 pia zilipitishwa decrees mbili zilizotokana na kifungu Na. 5, 6 (3), na kifungu cha 8 cha sheria hii. Decrees hizo “The Provisional Transitional Decree 1964 na ile ya The Interim Constitutional Decrees 1964, zote, hazikua halali maana ni decrees zilizopitishwa na Bunge la Tanganyika zilizotokana na sheria ya Tanganyika.

Kifungu Na 3 (i) cha Provisional Transitional Deccree kinasomeka hivi:

“Every person who holds office in the service of Republic of Tanganyika immediately before the Union Day, on union day be deemed to have been elected, appointed or otherwise selected to the corresponding office in the service of the United Republic.”

Yaani “wafanyakazi wote wale waliokua wanafanya kazi katika Serikali ya Tanganyika kabla Muungano watakua wamechaguliwa au kuteuliwa moja kwa moja na kuwa watumishi wa Serikali ya Muungano.”

Mwaka 1993, wabunge wa Tanganyika waliojiita G55 walijaribu kurejesha Serikali ya Tanganyika kwa Azimio la Bunge. Mhe. Njelu  Kasaka, mmoja wa viongozi wa kundi hilo, alieleza kwa ufasaha kabisa hoja hii. Amri ya Mwalimu Nyerere, ambaye wakati ule hakuwa mbunge, spika wala rais, ikazuia Azimio la Bunge kutekelezwa. Kama hili ni Bunge la wananchi, kwa nini maamuzi yake yanafutwa na mtu ambaye hana nafasi hiyo kisheria.

Eti sababu ikatolewa kwamba kurejesha Serikali ya Tanganyika ni kinyume na Sera ya Chama cha CCM. Lakini katika Makubaliano ya Muungano, hapana mahala ambapo chama cha ASP au TANU vilishiriki ingawa vilikuwepo wakati Muungano ukiwekwa sahihi. Makubaliano yalikuwa kati ya Rais wa Tanganyika kwa niaba ya Watanganyika na Rais wa Zanzibar kwa niaba ya Wazanzibari.

Kwa hivyo tangu 1964 mara tu baada ya kuwekwa saini makubaliano ya Muungano yamekuwa yakichafuliwa kwa makusudi na kutoa nafasi kwa upande mmoja wa Muungano kujinufaisha chini ya kivuli cha kuimarisha Muungano, huku upande wa pili ukididimia. Prof. Shivji, katika moja ya mihadhara yake juu ya Muungano, anasema hivi:

“One of the essential features of that scheme was and is the distribution of Power between the Union Parliament and the Zanzibar Legislature. That scheme was implicitly made immutable and a fundamental condition of the association of the two states. To tamper with those provisions is the surest way to destroy the legal foundations of the Union. Addition to and subtle alterations of the reserved list on union matters is like hammer-blows delivered to the core of those foundations. The moral and political responsibility of those of us who simply watch the blows is probably greater than those who deliver them.” (Prof. Shivji: 1994: University of Dar es Salaam)

Hapa Prof. Shivji anasema kwamba kuivuruga misingi ya makubaliano bila kuitetea ni sawa na kutizama mtu akipigwa ngumi na wewe unachekelea. Wajibu wa wale wanaoyaona hayo na kunyamaza kimya ni sawa sawa na wa yule anayeyavuruga makubaliano hayo.

Kwa hivyo matatizo ya sasa ya Muungano ni matatizo ya kujitakia yaliyotokana na vitendo vya makusudi vya kijanja dhidi ya Makubaliano ya Muungano ya mwaka 1964. Serikali ya Tanganyika ilipandishwa daraja na kujifanya ndiyo bwana wa Zanzibar chini ya mtazamo wa Big Brother’s Attitude.

Tabia hii imejenga jeuri kwa wale wasioelewa mwanzo wake na hufika kuthubutu kulinganisha makubaliano haya kama kwamba ni ndoa. Ndio maana wanauliza kwa dharau: “Vipi nyinyi Wazanzibari munauliza uhalali wa baba yenu baada ya miaka 43 ya ndoa?”

Tabia ya ukubwa imejenga himaya na kufika hadi kusahau kwamba zilizoungana ni nchi mbili. Wengi utawasikia wakihoji: “Huwaje watu 1,000,000 wawe na wabunge 50 katika Bunge la Muungano!” Au: “Eti wabunge wanaotoka katika Vitongoji  kule Pemba wanataka wawe ndiyo wakuu wa Upinzani Bungeni!” Anasema Mbunge wa Tanganyika tena wa chama cha upinzani. Leo udogo na uchache wa Wazanzibari unaaza kuhojiwa kwamba hauna haki ya kupata kikubwa. Huko si kusahau na kukejeli maamuzi ya Mwalimu Nyerere na Mzee Karume ya kukubali ukweli kwamba wameungana wakijua kabisa kwamba mmoja ni mdogo na mmoja ni mkubwa lakini yote ni mataifa yaliyokua huru?

Hawa wanaosema haya, bado wanakubali kwamba China ina watu milioni 1,500 lakini ina kiti kimoja tu katika Umoja wa mataifa (UN) sawa na Solomon Islands yenye watu laki moja (100,000) tu. Kwamba Ushelisheli na Sudan, ambapo ya kwanza ni ndogo sana na nyengine ni kubwa sana, zote zina kiti kimoja kimoja tu katika Bunge la Afrika. Kwao wao hilo ni sawa, lakini si sawa kwa Zanzibar kuwa na haki sawa na Tanganyika katika Muungano ambao umeunganisha mamlaka mbili huru na kamili na sio ukubwa wa eneo wala wingi wa watu!

Lakini kote huko ni kukosekana kwa nia njema. Ndiko huko huko kulikosababisha kufutwa kwa nafasi ya Rais wa Zanzibar kuwa  Makamo wa Rais wa Jamhuri ya  Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, ambako nako kumetokana na kiburi hiki cha kujiona Tanganyika ndiyo Tanzania na kwamba kuletwa kwa Mgombea  Mwenza katika uchaguzi ni kwa dhamiri ya kuuwa nafasi hiyo ya Rais wa Zanzibar.

Juzi Mhe. Amani Karume ameapishwa kuwa waziri asiye wizara maalum katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano. Huwaje Rais awe waziri wa Serikali nyingine? Huaje waziri wa Muungano awe waziri bila kuwa mbunge kama alivyo Mhe. Karume? Kwa kupenda madaraka, masikini, naye amekubali hilo.

Kukamilisha nukta hii ya kuwepo au kutokuwepo kwa Tanganyika, ambapo kwa msimamo wetu ni kwamba ipo, nataka nikumbushe jambo moja la muhimu kthibitisha hoja yetu. Hapo mwaka 1964, neno “Jamhuri“ lilitafsiriwa kisheria kwa maana kwamba kila lilipo katika katiba ya Tanganyika lisomeke kwa maana ya “Jamhuri ya Muungano.” Lakini neno hili hili lilibadilishwa maana na kutakiwa litafsirike kila penye neno Jamhuri katika katiba na sheria zote zilizopitishwa baada ya Novemba 1972 lijulikane kwa maana  yake mpya ambayo ni Jamhuri ya Tanganyika  maana hiyo inajumlisha popote pale palipoandikwa Jamhuri ya Muungano. Katika sheria hiyo Na. 30 ya 1972 inasomeka hivi:

“All acts and all Public documents made or issued before or after November 1972 „ The Republic means the Republic of  Tanganyika and including “United Republic “ (Section 3 of the Interpretation of Laws and General clauses Act 1972 (No. 30 1972)

Hii maana yake ni nini, kisheria? Ni kwamba, hii tuliyonayo si Jamhuri ya Muungano wa Tanzania bali ni Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika. Sasa, je, tunakosa gani tukisema kwamba dhamiri halisi ilikua ni kuunda Tanganyika mpya yenye jina jipya na mipaka mipya – The United Republic of Tanganyika?

Kuchezewa kwa Mkataba wa Muungano

Utamaduni huu wa kukosa nia njema umezaa upotofu wa kila hali ikiwemo maandiko ya katiba na sheria mbali mbali. Kwa mfano, ukiangalia vifungu vya Katiba vifuatavyo vimeandikwa kwa jeuri kabisa huku waandishi wa Katiba hii wakijua, na Bunge la Jamhuri likijua, kwamba ni makosa:

Kifungu Na. 133 cha Katiba kinachozungumza Tume ya Pamoja ya Fedha (Joint Financial Commission) kinasomeka hivi:

“The government of United Republic shall maintain a special account to be known as the Joint Finance account and which shall be part of the consolidated Fund of the United Republic into which shall be paid all the moneys contributed by two Governments in such proportion as shall be determined by the Joint Finance Commission  in accordance with a law enacted by Parliament for the purposes of the business of the United Republic in relation to the union matters.”

Yaani, kwa ujumla, Serikali ya Muungano itafungua Akaunti ya Akiba Benki itakayoingizwa mapato yatakayochangwa na serikali mbili, ya Muungano ya Tanzania na ya Zanzibar.

Maandiko ya kifungu hiki inathibitisha kwamba hata katika kuchangia mambo ya Muungano upande wa Serikali ya Muungano wao wanajitambulisha kwamba ndiyo Tanganyika huku ikieleweka vyema kwamba hapa wanaostahiki kuchangia kwa ajili ya mambo ya Muungano ni Serikali ya Tanganyika na Serikali ya Zanzibar na siyo Serikali ya Muungano na ya Zanzibar.

Ndiyo maana, wengi wetu tunaamini kwamba kuuliwa kwa Serikali ya  Tanganyika hakukuwa na nia njema ya ushirikiano wa nchi mbili na hakukufanywa kwa bahati mbya.

Sura ya kujiona katika umbo hilo kumejitokeza pia katika Kifungu cha Mahakama ya Kikatiba ambacho kinasomeka hivi:

“The special constitutional court shall consist of members of whom one half shall be appointed by the Government of United Republic and the other half shall be appointed by the Revolutionary government of Zanzibar.”

Yaani “Kamati maalum ya Katiba itakua na wajumbe ambao nusu yake watatoka kutoka Serikali ya Muungano na nusu watatoka Serikali ya Zanzibar.”

Huwaje wajumbe wa mahakama nusu wawe wanatoka katika Serikali ambayo ndiyo inayoshtakiwa? Waliostahiki kuwemo katika kamati hii na wajumbe wa Tanganyika na wajumbe wa Zanzibar.

Maelezo ya vifungu vyote hivi viwili yanathibitisha kwamba Serikali ya Muungano ndiyo inayowakilisha matakwa na haki za Tanganyika, jambo ambalo linaonesha jeuri ya kutojali makubaliano mpaka kwenye Katiba yenyewe inayoitwa ya kudumu ya Muungano.

Kati ya tarehe 10 hadi 14 Disemba, 2002 nilihudhuria kongamano kwenye hoteli ya Golden Tulip lililojadili masuala ya kikatiba ambapo waraka uliotolewa na Mzee George Liundi, aliyekuwa Mwansheria wa Serikali wakati wa Mwalimu Nyerere, ulieleza masikitiko yake jinsi Sheria za Muungano na Katiba ya Muungano zilivyokuwa zikivurugwa na watawala bila kujali Makubaliano ya Muungano. Mzee Liundi anasema hivi kuhusu jina la Tanzania:

“Prior to the enactment of the Interim Constitution of 1965, another constitutional problem appears to have been created by the change of name of the United Republic from the United Republic of Tanganyika and Zanzibar to the United Republic of Tanzania, with effect from 11th December 1964 (declaration of Name Act 1964 (section 3). This change of name calls for scrutiny, because on the face of it the measure appears to have put into question the constitutional status (in terms of national sovereignty) of both the territories formerly constituting the Republic of Tanganyika and Zanzibar respectively.”

Anachosema Mzee Liundi ni kwamba majina ya Tanganyika na Zanzibar yalipaswa kubaki ili kulinda uhalisia wa nchi zilizoungana. Kubadilisha jina la nchi hii ni makosa na wala hakuna maagizo hayo kutika Makubaliano ya Muungano yaliyotoa ruhusa kubadili jina la asili la nchi hizi.

Lakini haya hayakufanywa kwa kubahatishwa, bali kwa nia ile ile ya Big Brother’s Attitude kuidhoofisha kwa makusudi Zanzibar na leo kubatizwa jina la ndoa ambayo Wazanzibari wameolewa na hivyo kujitetea kwao kunaonekana ni  maudhi kwa waume zao, Watanganyika!

Profesa Shivji kila mara huwa anatoa mfano wa mahusiano kati ya Tanganyika na Zanzibar kwenye Muungano huu kwa kutumia maneno mawili ya Kiingereza: Creator and Creature, yaani Muumba na Kiumbe. The creator of the Union is the Peoples’ Republic of Zanzibar and the Republic of Tanganyika. Union is a creature and, therefore, it is the one that is to be discussed. In the present circumstances, the creature has decided to sit with one of the creators and discusses the problems of the creature. This is an abnormality.

Yaani Waumbaji wa Muungano ni Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Jamhuri ya Tanganyika. Muungano ni kiumbe na, hivyo, ndicho kinachostahiki kujadiliwa. Katika mazingira ya sasa, hata hivyo, kiumbe kimeamua kukaa kitako na mmoja wa Waumbaji wake na kujadili matatizo ya kiumbe. Hili si jambo la kawaida.

Katika kuendeleza tabia za kuonesha jeuri ya ukubwa wa Tanganyika dhidi ya udogo wa Zanzibar ni kitendo cha kuvunja utamaduni uliwowekwa na Mwalimu Nyerere mwenyewe. Tangu Mwalimu Nyerere alipoacha madaraka, aliweka utamaduni kwamba katika uongozi wa Tanzania, na katika haja ya kulinda msingi wa Muungano, katika kipindi kimoja kiongozi wa kitaifa (Rais) atoke upande mmoja na kipindi kingine atoke upande wa pili wa Muungano.

Pamoja na makosa yake mengi, Mwalimu Nyerere alilidumisha hili. Hata kama lilikua na ubabaifu ndani yake, lakini alipomaliza alimpisha Mzee Ali Hassan Mwinyi kutoka Zanzibar, ambaye naye alipomaliza, akachukua madaraka Rais Mstaafu Mkapa kutoka Tanganyika.

Lakini kwa kiburi kile kile cha kukosa nia njema, Rais Mkapa akaamua bila kukubaliana na Zanzibar kwamba eti hakuna maandiko ya kikatiba au ya kisheria yanayosema hivyo. Ni ajabu kubwa kwamba yale yaliyomo kwenye katiba na maandiko ya Muungano, wakubwa hawayafuati na yale yaliyowekewa utaratibu wa kudumu yanajengewa hoja kwamba hayamo kwenye Katiba! Na wakati Wazanzibari wanapolalamikia vitendo kama hivi, huitwa wake walalamishi wanaonataka kuachwa. Huu ndiyo ukosefu wa nia njema ninaoueleza.

Matokeo yake ni kwamba, kuanzia sasa hakuna Mzanzibari ambaye ataweza kuchukua madaraka ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania maana hakuna tafsiri sahihi wa nani Mtanzania na nani Mzanzibari katika utaratibu wa madaraka ya urais ulivyo hivi sasa.

Mwananchi ajifunze matokeo ya kesi ya Mama Kome na aliyekuwa Mgombea Mwenza wa CHADEMA, Marehemu Jumbe, Uzanzibari wao ulivyotafsiriwa na Tume ya Uchaguzi ya Muungano.  Kwa tafsiri ya Tume, mgombea anaweza akatoka Bara na akawa mgombea mwenza hata kama haishi wala hakuzaliwa Zanzibar maana wanasema Sheria ya Uchagzi juu ya Mzanzibari iko kimya.

Je ni kweli iko kimya au tangu ilipoandikwa iliandikwa kwa nia hiyo ya kubaki kimya ili baadae itumike kama ilivyotumika? Baada ya miaka kumi suala hili litakua ni chanzo cha mgogoro maana kutakua hakuna Muungano wenye pande mbili. Kiungo kikubwa kilikua nafasi ya Makamo wa Rais ambayo imeuliwa kwa ujanja kidogodogo.

Mchango wa Zanzibar katika shughuli za Muungano

Hoja hii nayo imeleta jeuri na kiburi kikubwa sana kwa upande wa Tanzania Bara. Kama vile linavyoelezwa tatizo la uhaba wa Wazanzibari, kutokuchangia katika mfuko wa Muungano kunaonekana kuleta bughudha kubwa kwa Wazanzibari. Kama tulivyoonesha hapo juu kwamba wanaostahiki kulipia mchango huo ni Serikali ya Zanzibar na Serikali ya Tanganyika ambayo imefanywa iwe haipo. Kwa bahati nzuri tena, baada ya muda mrefu kupita, mwaka 2004 Tume ya Pamoja ya Fedha iliundwa na kuanza kazi zake. Hivi sasa inaendelea kutayarisha ripoti zake za awali ili kutoa picha halisi ya jinsi mchango wa Muungano uwe. Hata hivyo, mawazo kwamba ni upande wa Bara tu ndio unaotoa fedha nyingi yameendelea kujenga uhasama usiokuwepo kwa upande wa Zanzibar.

Kwa bahati nzuri mara baada ya kufukuzwa kwa Rais wa pili wa Zanzibar, Mzee Aboud Jumbe, Mwalimu Nyerere aliamua kuteua Tume Maalum Kuchambua Matatizo ya Muungano. Kwa upande wa Zanzibar, waajumbe wa Tume hiyo walikuwa ni Marehemu Said Mugheiry, Marehemu Abdulla Juma Khatib, Muhamed Seif Khatib na mimi, Juma Duni Haji. Kwa upande wa Bara, nakumbuka alikuwemo Mzee Kazaura, wakati huo akiwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha ya Serikali ya Muungano, Dk. Mujuni aliyekua Katibu Mkuu Mipango na Marehemu Prof. Kigoma Malima.

Tulifanya kazi kubwa kuchambua masuala haya na kuwasilisha ripoti yetu Kamati Kuu ya CCM, lakini ikapigwa pute kwa sababu waume hawakupenda yaliyopendekezwa maana ilifichua kwa uwazi kabisa nini hasa mambo ya Muungano na nini ni mambo ya Tanganyika. Badala ya kutatua matatizo yale wakati ule wakafukuzwa akina Maalim Seif Sharif na kundi lake kwa kutolewa nje ya Serikali na nje ya CCM. Na hivi ndivyo namna ambavyo Mwalimu Nyerere alivyokuwa ‘akiulinda’ Muungano wake na hivi ndivyo wafuatizi wake wanavyotaka iwe kwa wengine. Hii haiwezi kuitwa, hata kidogo, kuwa ni dhamira njema.

Tume ya Fedha ya Muungano

Hivi karibuni baada ya kuundwa Tume ya Fedha ya Muungano, kuna kampuni fulani ilipewa kazi kama ile tuliyoifanya mwaka 1984 na kufanya uchambuzi halisi wa mambo gani ya Muungano halisi na yepi ya Tanganyika na yepi ya Zanzibar. Baada ya orodha hiyo kupatikana, watafiti wakatafuta matumizi halisi ya bajeti ya vifungu hivyo kwa muda wa kiasi ya miaka 10 iliyopita. Watafiti hao walikwenda mbali zaidi ya hapo na kukusanya mapato yote kwa kila kifungu cha mambo ya Muungano halisi. Mwishowe wakalinganisha ikiwa mapato hayo yanakidhi matumizi au yana upungufu.

Kwa mwaka wa fedha wa 2003/2004, kwa mfano, watafiti waligundua kuwa matumizi halisi kwa vifungu vya Muungano ilikua shilingi milioni 537, 258.4 ilhali mapato halisi kwa mwaka huo ilikuwa ni shilingi milioni 1,030,826.1. Tafauti ya vifungu hivyo imetoa ziada ya shilingi milioni 593, 569.5 kwa mwaka huo. Ziada hii haingizi mapato yanayotokana na misaada kutoka nje au mikopo, ambayo hutumika kwa shughuli za Tanganyika au Tanzania Bara na wala siyo Zanzibar. Wazanzibari tunapolalamika tuna sababu za msingi kama vile Mwalimu Nyerere alipovunja EAC baada ya kuona haina faida na Tanganyika.

Ukweli umeonesha kwamba, kumbe hakungekua haja yoyote ya SMZ au Serikali ya Tanganyika kulipia fedha za ziada kama wahusika watatunza na kuweka kumbukumbu sahihi za mapato na matumizi ya mambo ya Muungano hasa na siyo yale ya Tanganyika kuchanganywa na ya Muungano na kutumika kwa maslahi ya Tanganyika. Mambo yasiyokuwa ya Muungano ya Tanzania Bara yalipotengwa nje ya yale ya Muungano halisi, gharama za mambo ya Muungano zimejidhihirisha wazi bila kujificha na kuonesha kwamba zinaweza kufidiwa na mapato ya mambo ya Muungano kama kuna nia njema.

Lakini hili limekua rahisi kwa kukubali ukweli kwamba, kuna mafungu matatu ya matumizi katika Serikali zetu mbili. Mafungu hayo ni ya SMZ, ya Mambo ya Muungano na ya mambo yasiyokuwa ya Muungano ya Tanzania Bara (ya Tanganyika).

Ndiyo maana, kwa miaka 15 sasa chama cha CUF kinaamini na kitaendelea kuamini kwamba ufumbuzi wa masuala ya Muungano ni rahisi kama kutakuwa na serikali tatu. Kwa nini CCM wanajificha chini ya serikali mbili, ni kwa sababu ya Big Brother Attitude na kukosa nia njema ya kuweka mbele maslahi ya kitaifa badala ya kibinafsi au ya Tanganyika.

Kuna viongozi wa CCM ambao wamekuwa wakiitumia hasara kubwa ya kuendesha serikali tatu kama ni moja ya hoja ya kuepuka kuzikubali. Wanasahau kwamba wakati wa siasa za Chama kimoja kushika khatamu, tulikuwa na mamlaka tatu zilizokua zikitumia fedha kwa ubadhirifu bila kuhojiwa. Kulikua na chama cha CCM kilichokuwa na Halmashauri Kuu ya Taifa na vikao vyake vya mara kwa mara (sawa na Bunge). Chama hiki kilikuwa na Kamati Kuu (sawa na Baraza la Mawaziri) na kilikua na Sekreterieti iliyokuwa na mawaziri wake ambao huitwa wakuu wa Idara za Chama.

Wakati ule chama kikitumia mfuko wa Serikali na wala hakuna mamlaka iliyokua na uwezo wa kukizuia. Mapesa mengi yaliyopotea kwa kupewa vyama vya ushirika na shirika la chama la SUKITA ilikua ni wakati huu. Sikuwahi kusikia Mchunguzi Mkuu wa Fedha za Serikali akisema wahusika wapelekwe Mahakamani kwa ubadhirifu. Badala yake waliokula na kuharibu fedha zile wakiitwa Dodoma na mambo yakaishia huko huko.

Kuanzishwa kwa Benki Kuu na Haki za Zanzibar katika Benki hiyo

Benki Kuu ya Tanzania (BoT) iliundwa kwa sheria ya Benki Kuu ya Tanzania ya 1965. Kabla ya hapo, nchi zote za Afrika Mashariki zilikuwa zikipata huduma za kibenki kutoka Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki (East African Currency Board) ambayo ilikuwa na makao yake makuu mjini Nairobi, Kenya. Sarafu ya Afrika Mashariki ndiyo iliyokuwa ikitumika kwenye nchi zote zilizokuwemo kwenye Bodi hiyo. Mbali ya Kenya, Tanganyika, Uganda na Zanzibar, Somalia na Aden (Yemen ya Kusini) nazo zilikuwa wanachama. Lakini kabla ya uhuru wa Tanganyika, nchi hizo zilijitoa, zikasalia nchi nne nilizotangulia kuzitaja. Kila nchi ilikuwa na mwakilishi wake kwenye Bodi hiyo kuangalia maslahi yake.

Baada ya uhuru wa Tanganyika, katika mwaka 1961, ambao uliutangulia ule wa Uganda (1962), Kenya (1963) na Zanzibar (1963) kukawa na haja ya kufikiria muundo mpya wa Bodi, kwani kabla ya hapo mtawala wa nchi hizo, Muingereza, ndiye aliyekuwa akiendesha na kusimamia Bodi hiyo. Sera za mambo ya fedha na uchumi za nchi hizo zililingana kwa kuwa mtawala alikuwa ni mmoja. Ndiyo maana kukawa na haja baada ya uhuru kufikiria vipi Bodi hiyo itaendeshwa, kwani sera za nchi hizo changa zinaweza kutafautiana sana na hivyo kufanya mifumo ya kiuchumi nayo kutafautiana.

Tanganyika wao wakamuajiri Dk. Erwin Blumenthal wa Bundesbank ya Ujerumani kuwa mshauri wake juu ya mfuko mpya wa Bodi hiyo, Waganda wakamuajiri bwana mmoja aliyeitwa Newton kufanya kazi hiyo na Kenya na Zanzibar hawakuwahi kuajiri washauri wao. Dk. Bluementhal alipendekeza kuwepo kwa East African Central Bank ambayo iwe na State Banks kwenye miji mikuu yote ya nchi wanachama. Hivyo basi kungekuwa na State Bank ya Tanganyika, Kenya na Uganda na ya Zanzibar mbali na hiyo Central Bank ya Afrika Mashariki. Newton yeye alipendekeza kuwepo na Benki Kuu ya kila nchi. Wakati Watanganyika wanatafakari mapendekezo ya Blumenthal, Uganda ikakubaliana na mapendekezo ya Newton, hivyo wakaanza utaratibu wao kuanzisha Benki Kuu yao. Kenya pia walifanya hivyo na Tanganyika nao wakaamua kuanzisha Benki Kuu ya Tanzania, BoT.

Kwa upande wake, EACB iliendela kutoa huduma huku wakisaidia uanzishwaji wa Benki Kuu ya kila nchi ya Afrika Mashariki na upande wa pili ikaanzisha utaratibu wa kujifunga yenyewe. Mambo yalichanganyika. Uhuru wa Zanzibar wa tarehe 10 Disemba, 1963 ulifuatiwa na Mapinduzi ya Januari 12, 1964 na baadaye Muungano wa Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar wa Aprili 26, 1964. Hata hivyo, Zanzibar iliendelea kuwa na mjumbe wake kwenye Bodi hii na Serikali ya Muungano wa Tanzania (kwa kuwa hapakuwepo na serikali ya Tanganyika) ndiyo ikiiwakilisha Tanganyika.

Wakoloni waliokuwa wanaendesha Bodi hiyo pamoja na Watanganyika waliokuwemo kwenye Bodi hiyo, akiwemo Mwenyekiti wa wakati huo wa Bodi hiyo ambaye naye alikuwa Mtanganyika, hawakufurahi na kuendelea kuwepo kwa mjumbe wa Zanzibar. Mipango ikasukwa baina ya Waingereza na Tanganyika kuhakikisha kuwa Zanzibar inatemwa kutoka Bodi hiyo na hilo halikuwa tabu kufanyika, kwani hata Idara ya Sheria ya EACB ilipania kusaidia mbinu hizo. Kwa mfano, maelezo yafuatayo ni ya Katibu wa Bodi hiyo, J. B. Loynes, kama yalivyo kwenye kumbukumbu za tarehe 1 Juni, 1964 akimuandikia mwakilishi wa Tanganyika kwenye Bodi:

“Indeed it could be highly embarrassing as a measure likely to give further encouragement to the separatist elements on the island.”

Lakini, kwa sababu masuala ya sarafu, mambo ya fedha na mabenki hayakuwa mambo ya Muungano, Waziri wa Fedha wa Tanganyika, J. D. Namfua, alijibu kwa EACB kwamba lazima muwakilishi wa Zanzibar aendelee kuwemo kwenye Bodi hiyo katika barua yake ya tarehe 9 Juni, 1964 kwa Loynes aliyetaka kujua nafasi ya Zanzibar baada ya Muungano.

“As you will appreciate the Act of Union between Tanganyika and Zanzibar does not specifically transfer matters relating to currency to the Union Government, and pending any relevant modifications as may be agreed, the membership of Zanzibar in the Currency Board remains unaffected.”

Baada ya barua hii, Mwingereza Loynes aliyejitokeza wazi wazi kutopenda kwake kuiona Zanzibar ikiendelea kubaki kuwa mjumbe wa Bodi hiyo, aliandika barua fupi tarehe 8 Septemba, 1964:

“We clearly do not want Zanzibar at our next meeting and I should hope that ways should be finding ways of keeping them out. All I should like to do now is to remind you on this point so that no papers are sent across the water until we are clear where we stand.”

Katibu wa EACB, Bwana Hirst, baada ya kuagizwa na Mwenyekiti wa Bodi, Bwana D.A. Omar (Mtanganyika), alimuarifu Edwin Mtei (wakati huo akiwa ndie Katibu Mkuu wa Hazina Dar es Salaam na baadaye gavana wa kwanza ilipoanzishwa BoT) juu ya maagizo ya Loynes.

Kwa hivyo baada ya hapo kilichobaki ilikua ni kubadilisha katiba ya muda ya Jamhuri ya Muungano ili iingize masuala ya fedha na mabenki kuwemo katika orodha ya mambo ya Muungano wakati uamuzi wa kutengwa Zanzibar kutoka EACB ulishachukuliwa zamani tangu 1964 hata Benki kuu yenyewe haijaanzishwa.

Kazi ya kwanza ikawa kuingiza sarafu na mabenki kwenye shughuli za Muungano. Kwa kutumia Interim Constitution of Tanzania, (1965 Act. No. 43 of 1965), Mwalimu Nyerere alipeleka Bungeni marekebisho ya kifungu Na. 85 cha Katiba hiyo na kuongeza kifungu kidogo Na. XII cha orodha wa Makubaliano ya Muungano kinachohusu masuala ya fedha, mabenki, sarafu, fedha za kigeni na udhibiti wa fedha za kigeni kuwa katika Orodha ya Mambo ya Muungano kama inavyosemeka.

“The following matters are hereby reserved to the Parliament and Executive of the United Republic and declared Union matters: currency, coinage and legal tender (including paper money; banks (including saving banks) and banking; foreign exchange and exchange control; and subsection (1) of the section 68 of the Interim constitution is hereby amended by adding the said matters as a new item (xii) to the definition “Union matters” therein.” (Interim Constitution 1965)

Gazeti la Serikali ya Muungano la tarehe 18 Juni 1965 ndilo lililotangaza kufanyika marekebisho hayo ambayo ni kinyume kabisa na Makubaliano ya Muungano. Baada ya kufanyika marekebisho hayo, Mtei aliandika barua rasmi kwa katibu wa EACB na kumueleza kwamba kuanzia tarehe 29 Disemba 1965, yeye ndiye atawakilisha Tanzania katika Bodi hiyo, jambo ambalo lilikuwa likisubiriwa sana na Bodi hiyo na kujadiliwa katika vikao jinsi ya kuitoa Zanzibar.

Lakini hata baada ya maelezo hayo, bado Mtei alikubali kwamba haki na mgawanyo wa faida za Bodi hiyo ubaki kama ulivyokua na kwamba Zanzibar iendelee kupewa haki zake na faida yake kutoka Bodi kama zamani. Baadhi ya maneno ya barua hiyo inasomeka hivi:

“One of the effects of this Act is that I will represent the whole United Republic on the Board, but as it was recognised at the meeting, this will not effect the reckoning of the distribution of profit or the purchase of treasury bills or other securities in respect of Zanzibar.”

Kumbukumbu tulizokusanya zinaonesha mawasiliano marefu kati ya Dar es Salaam na Nairobi kujadili njia sahihi kisheria itakayoweza kuzichukua fedha za Zanzibar na kuziingiza katika akaunti za Tanganyika, maana Katibu na Mwenyekiti wa Bodi EACB hawakutosheka na barua ya Mtei kama inaweza kuwalinda Bodi wasidaiwe baadaye. Bodi ililazimika, kwa hivyo, kuwapelekea Dar es Salaam rasimu ya barua ambayo ikipelekwa kwenye Bodi itawalinda Bodi baadaye wasije kudaiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar baada ya kuungana au Serikali ya Mapinduzi iliyokuwepo Zanzibar kabla kuungana na Tanganyika.

Baada ya kukamilika kufanyika marekebisho haya ya Katiba ya Muda ya Jamhuri ya Muungano, Waziri wa Fedha wa wakati ule, Amir H. Jamal alimuandikia barua (Kumb. Na. TYC.46/01 ya tarehe 22 Machi, 1966) Mwenyekiti wa Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki na kumuagiza rasmi kwamba haki zote na amana zote za Zanzibar zilizokuwemo katika Bodi hiyo zipelekwe katika Benki Kuu chini ya Serikali ya Muungano na kwamba kuanzia pale ni Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania pekee ndiye tu atakayeiwakilisha Tanzania katika Bodi hiyo. Haya yalifanyika baada ya kulazimisha kuingizwa kifungu Na. (xii) katika Orodha ya Mambo ya Muungano ambacho ni makosa kabisa ya makuabaliano. Baadhi ya maelezo ya barua hiyo ya Jamal yansomeka hivi:

“On behalf of  the Government of  United Republic of Tanzania (hereinafter referred to as “the Government”) I have to say that in view of sub-clause xi and sub-clause xii of the definition of  “Union matters” in section 85 of the Interim Constitution of Tanzania 1965 (No. 43 of  1965)….barua inaendelea  —— (a) —-,(b) all distributions of capital or profits made by the Board in respect of Tanzania including any share which but for the provisions of  the Interim Constitution, referred to above, would be payable direct to the  Executive for Zanzibar, are due and payable only to the Government.”

Huku ndiko huko tunakokuita Wazanzibari kwamba ni ukosefu wa dhamira njema tangu mwanzoni kabisa mwa Muungano huu. Kwamba, kwanza, kuongezwa masuala ya fedha kuwa ya Muungano ni kosa la kisheria na kikatiba maana halingeweza kufanyika  kwa idhini ya upande mmoja pekee. Lakini sababu, pili, Waziri wa Fedha wa Serikali ya Muungano hakuwa na  wala hajawa “Waziri wa  Fedha wa Muungano” na ndiyo maana hadi leo kuna wizara za fedha mbili. Wizara ya Ulinzi, Mambo ya Nje au ya Mambo ya Ndani, kwa mfano, ni za Muungano hasa, maana hatuna mawaziri wa wizara hizo kwa Zanzibar, lakini siyo ya Fedha. Kwa hivyo si Waziri wa Fedha wa Tanganyika wala Gavana wa Benki Kuu ambaye kisheria angeliweza kuamrisha chombo kinacho mahusiano ya kifedha na Serikali ya Zanzibar kitoe amana za Zanzibar na kuzipeleka katika hazina ya Benki Kuu au Hazina ya Muungano. Huu ulikuwa na umeendelea kuwa utovu mkubwa wa nidhamu na wizi wa wazi wazi kwa kutumia jina la sheria.

Kama kuna kitu chochote kilichofanywa kuwa cha Muungano baada ya Marekebisho ya Katiba ya Muda ni usimamizi wa taratibu na utoaji wa sarafu, na pili udhibiti wa mwenendo wa kubadilisha thamani ya shillingi ya Tanzania (currency and exchange rate control). Tafsiri ya hili sio kuchukua amana za Zanzibar. Maana huko EACB kulikua na amana za nchi nne, lakini Waingereza walijua hazikuwa zao, zilikua za makoloni yake na ndiyo maana kila moja ya nchi hizo alipewa fedha (amana zake), aidha baada ya kuvunjwa Bodi au baada ya kupata uhuru.

Kama kazi ya EACB ilikuwa ni kumiliki amana hizo, basi Waingereza wasingekuwa na sababu ya kuzigawa kwa makoloni husika baada ya kupata uhuru wao. Barua ya Serikali ya Uingereza, wakati ikijitoa kwenye shughuli za kuisimamia EACB, ilieleza wazi kwamba inakabidhi dhamana za uwakilishi wa Bodi  kwa makatibu wakuu wa wizara za fedha za nchi husika na siyo kwa Gavana wa Benki na barua hiyo ilitumwa na ikaagizwa kutangazwa rasmi katika magazeti ya serikali. Barua hiyo Ref. LEG/199 ya tarehe 13 Septemba 1963 ilipelekwa kwa makatibu wakuu fedha wa nchi zote tano: Kenya, Uganda, Tanganyika, Aden na Zanzibar baada ya mwenyekiti wa Bodi hiyo kutoa notisi yake juu ya uamuzi wa waziri wa makoloni wa Uingereza.

Kwa nini Serikali ya Muungano wakazichukua amana za Zanzibar na pia kuingiza kifungu katika sheria ya Benki Kuu kwamba haki na amana hizo zote ziwe za Benki Kuu? Kama kulikuwa na nia nzuri, si ingekuwa vyema kwa Tanzania kuwa na wawakilishi wawili kwenye Bodi moja? Kwa nini iwe sisi wenyewe kwa wenyewe, tunaojiita ndugu wa damu, ndio tulofanya jitihada ya kuitoa Zanzibar na kuitaka Tanganyika ibaki peke yake kuiwakilisha Zanzibar wakati rasilimali fedha si sehemu ya Mambo ya Muungano? Tunahitajika zaidi ya hapa kuthibitisha kwamba viongozi wa serikali ya Muungano hawakuwa na hawana nia njema kwa Zanzibar?

Bila kujua nini kikifanyika nyuma ya mgongo wake, Waziri wa Fedha wa Zanzibar wa wakati huo, Abdulaziz Twala, aliandika barua nyingi kupinga hatua za Waziri Jamal za kuanzisha Benki Kuu bila kwanza kukubaliana juu ya mahusiano ya benki hiyo yatakavyokua na Serikali ya Zanzibar, hasa juu ya haki na amana za Zanzibar zilizokuwa katika EACB. Vikao mbali mbali vilifanyika kati ya Zanzibar na Dar es Salaam kujadili masuali hayo bila mafanikio.

Kwa sababu tayari uamuzi wa kuzichukua haki za Zanzibar ulishafanyika tangu 1964, kwa makusudi kabisa Waziri Jamal na Balozi Nsekela pamoja na Mark Bomani wakatayarisha sheria ya Benki Kuu iliyoacha, kwa makusudi, kuyalinda maslahi ya Zanzibar. Sheria hiyo iliingiza kifungu kilichoshusha hadhi ya Serikali ya Zanzibar kuwa sawa na Baraza la Manispaa na pia kuingiza kifungu kwamba haki zote za Zanzibar zilizokuwa katika EACB zihamishiwe katika BoT bila Zanzibar kulipwa chochote.

Kwa nini tunasema kwamba Serikali ya Zanzibar ilishushwa hadhi hadi kuwa sawa nay a Baraza la Manispaa, ni kwa kuwa neno ‘Public Authority’ ya sheria hiyo ya mwaka 1966, limepewa maana kwamba ni: “any political subdivision of the United Republic including the Executive for Zanzibar.” Kwamba Serikali ya Zanzibar mbele ya BoT haina tena fursa kama vile serikali yenye mamlaka ya kidola kama ilivyokua chini ya EACB.

Hakuna mahala popote katika Makubaliano ya Muungano panapotoa amri kwamba fedha za kigeni za nchi hizi mbili zichanganywe au kwamba zitakuwa za shirika. Hata baada ya kuandikwa Katiba ya Muungano ya Kudumu, bado fedha za kigeni ziliendelea kuwa ni za nchi mbili mbali mbali. Wapi walipata madaraka ya kuzichukua haki na amana ya fedha ziliomo EACB? Maana kubadili katiba hakukutoa madaraka ya kumiliki mali za Zanzibar. Kilichofanyika ni kwamba kuanzia pale fedha za kigeni ni suala la pamoja na kwamba Zanzibar hawatakua na sarafu yake ya kigeni kama vile ilivyo Marekani au Uingereza. Haikua na maana kwamba fedha za kigeni ni zetu shirika au zichanganywe. Fedha za Zanzibar zikaibiwa kimachomacho na baada ya hapo wizi huo ukahalalishwa kwa kuingiza kifungu katika sheria ya BoT kwamba mali zote za Zanzibar ziingie huko.

Baada ya kukamilisha wizi wa kalamu, Waziri Jamal alimuandikia Waziri Twala juu ya maamuzi yake hayo siku moja tu baada ya kwisha kuiagiza EACB kuhamisha haki za Zanzibar kwenda BoT, huku sasa akidhania kwamba ana nguvu za kusema suala hilo ni la Muungano.

Lakini wakati akioandaa rasimu ya kuongeza kifungu Na (xii) kupeleka Bungeni apate Mabadiliko ya Katiba, Waziri Jamal aliacha kuwasiliana na Waziri Twala kwa sababu alikuwa hawezi kuchukua fedha za Zanzibar wakati hana kinga. Ndiyo maana barua ya kuhamisha fedha za Zanzibar kuingiza BoT iliyopelekwa EACB iliandikwa tarehe 22 Machi, 1966 (Ref Na. TYC.46/01) na ile ya kujibiwa Waziri Twala ikaandikwa tarehe 23 Machi 1966 (Ref Na. TYC.46/08/01). Hii haiwezi kabisa kuitwa kuwa ni dhamira njema ya viongozi wa Muungano kwa Zanzibar.

Tanganyika yameza donge nono la Zanzibar

Kulikuwa na mawasiliano makubwa kati ya Serikali ya Muungano na Bodi hii hata kufikia kufanikisha nia yao ya kuing’oa Zanzibar kwenye Bodi. Kuna wakati gavana mtarajiwa aliwasiliana na uongozi wa Bodi akiwashauri kikao kilichopangwa kufanyika Dar es Salaam kihamishiwe mji mwengine kwa hofu kuwa Wazanzibari huenda wakapata taarifa kwa urahisi juu ya kikao chao hicho cha siri.

Mwisho walifanikiwa kutekeleza azma yao hiyo na Zanzibar ikawa haina mwakilishi kwenye Bodi ya Sarafu. Bahati njema, hesabu na mgao wa faida (dividends) ulibaki kwa jina la Zanzibar na Tanganyika na ingawa mapato hayo yakilipwa Serikali ya Muungano. Haki hiyo ya Zanzibar ambayo ilikuwa ikilipwa kwa Serikali ya Muungano na kutolipwa Zanzibar ilifikia zaidi ya paundi za Kingereza 950,000. Wenzetu walimeza donge hilo nono na kunyamaza kimya huku wakiendelea kudai mchango wa Zanzibar kwenye shughuli za Muungano na kujisifu kwenye majukwaa kwamba wanatetea Muungano dhidi ya maadui kutoka nje. Hapa ni nani adui?

Kwa hivyo, katika BoT kuna mchango wa Serikali ya Zanzibar ambao kwa muda mrefu Serikali ya Zanzibar ilipokuwa ikidai ikipata hujuma eti inahatarisha Muungano. Si hivyo tu, ila pia kumbukumbu zinaonesha kwamba wakati wa kuanzisha benki kuu za kila nchi ulipofika, Bodi hii iliamua kutoa fungu kuzisaidia nchi hizo kuanzisha benki kuu zao. Tanganyika ilipewa paundi 668,884 sawa na Kenya. Uganda pia walipewa fungu lao kama hilo. Zanzibar kwa vile ilikua imeungana na Tanganyika haikupewa chochote wakati ule, kwani uongozi wa Bodi ya Sarafu uliona kuwa kutaanzishwa Benki Kuu moja, hivyo watoe mchango kwa Benki kuu moja ya Tanzania kwa kuwa ni washiriki katika Muungano na ikapeleka paundi 82, 810 kama mchango wa Zanzibar katika uanzishwaji wa Benki Kuu ya Tanzania.

Fedha hizo zilimezwa na Tanganyika na kuundwa benki kuu moja, BoT, kwa mtaji wa paundi milioni moja wakati huo ikiwa ni sawa na shilingi milioni ishirini (20,000,000) za Afrika Mashariki. Kasoro ya kufikia pauni 1,000,000 ilijazwa na Serikali ya Muungano. Kwa urahisi zaidi tazama hesabu hizi chini:

Mchango wa Serikali ya Tanganyika = Paundi 668,884

Mchango wa Serikali ya Zanzibar = Paundi 82,840

Jumla ndogo (ST + SZ) = 751.724

82, 840: 668, 884 = (11.02:88.08)

Muda wote ule wa uhai wa EACB, Zanzibar ilikuwa ikipata 11.02% ya mgao wowote ule unaotolewa na Bodi kwa Tanganyika. Na ndio maana utaona kuwa hata kwenye mchango wa uanzishaji wa BoT, Zanzibar ilipewa asilimia hiyo hiyo. Hii ni kusema kuwa pauni 668,884 za Tanganyika ukijumlisha na pauni 82,840 za Zanzibar ni sawa na pauni 751,724, na, kwa hivyo hisa ya Zanzibar katika BoT kwa asilimia ni sawa na asilimia 11.2 (82,840 x 100 ya 751,724 = 11.02%)

Juu ya kuwepo kwa haki hiyo kwa Zanzibar – kama Zanzibar na siyo kama mshirika wa Tanganyika kwenye Muungano – Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania haikutaja kabisa kama Zanzibar ni mmoja ya wenye hisa wala haikutaja kwamba Tanganyika nayo ina hisa. Kinyume chake, mwenye hisa 100%, kwa mujibu wa sheria hiyo, ni Serikali ya Muungano peke yake: si Serikali ya Tanganyika wala Serikali ya Zanzibar.

Lakini kwa mujibu wa hesabu hizo hapo juu wenye hisa katika BoT ni watatu: Serikali ya Tanganyika, Serikali ya Zanzibar na Serikali ya Muungano. Kila moja ikiwa na hisa zifuatazo: Tanganyika iliyochangia paundi 668,884 katika mtaji wa paundi 1,000,000 ina hisa 66.9, Zanzibar iliyochangia paundi 82,840 katika mtaji huo wa paundi 1,000,000 ina hisa 8.3 na Serikali ya Muungano iliyochangia paundi 248,246 katika mtaji huo ina hisa 24.8. Na kwa sababu katika hizi pauni 248,246 za Muungano, asilimia 11.02 ni za Zanzibar basi 27,356.71 (11,02% x 248,246 = 27,356.71) ni za Zanzibar. Jumla ya fedha za Zanzibar, kwa hivyo, katika uanzishwaji wa BoT ni paundi 110,196.7, ambazo ni sawa na asilimia 11.2 (110,196.7 x 100 / 1,000,000 = 11.02%) kama ilivyochambuliwa hapo juu.

Lakini, kama tulivyosema, pamoja na ukweli huo, bado Serikali ya Zanzibar haikutajwa kabisa kwenye sheria ya kuanzishwa kwa BoT, na badala sheria hiyo iliingiza kifungu kilichoiteremsha hadhi Serikali ya Zanzibar kwa kuilinganisha kuwa sawa na Serikali ya Baraza la Manispaa. Matokeo yake ni kama Serikali za mitaa zisivyoweza kukopeshwa na Benki Kuu, vivyo hivyo na Zanzibar nayo haikuweza kukopeshwa. Kama Serikali ya Zanzibar inahitaji kukopa, basi inabidi ifanye hivyo kupitia Serikali ya Muungano. Mtiririko wa mawasiliano na mijadala mikubwa kati ya Waziri Twala na Waziri Jamal inathibitisha wazi kwamba kulifanyika njama za makusudi kuuwa uchumi wa Zanzibar ili usiweze kujitegemea wenyewe.

Hali hiyo ndiyo inayojitokeza hivi sasa. Pamoja na madai mengi ya SMZ kutaka kufanyike mabadiliko ya sheria hiyo ya Benki Kuu, lakini hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa. Katika haja ya kuzibwa macho SMZ, viongozi wa Serikali ya Muungano wamefanya ujanja wa kuiingiza kifungu ndani ya Katiba kinachosema kuwe na Tume Maalum ya Fedha kushughulikia masuala ya Muungano. Hali imeachwa hivyo kwa makusudi kwa sababu wenzetu hawakuwa na nia njema tangu awali.

Na hoja hii inakwenda ya ukosefu wa nia njema inaweza kuchambuliwa zaidi na zaidi. Kwa mfano, hata kama Sheria ya Benki Kuu iliitambua Serikali ya Muungano pekee kama mwenye hisa, kwa nini Serikali ya Muungano, baada ya kupokea mgawo wa faida za benki hiyo, inaweka katika mfuko wake tu bila ya kugawana na Zanzibar, wakati yenyewe (Serikali ya Muungano) ndiyo iliyopokea fedha kutoka EACB, fungu la Tanganyika na la Zanzibar kuanzisha benki hiyo?

Kwa miaka 31, Benki Kuu ya Tanzania ilikuwa ikitoa mgawo wa faida kwa Serikali ya Muungano bila ya Serikali ya Zanzibar kupewa chochote. Baada ya vita, mabishano na mara nyingine Wazanzibari kuonekana wasaliti wasiokwisha kunung’nika, kwenye mwaka 1996, ndiyo IMF ikapendekeza eti SMZ ilipwe na Serikali ya Muungano 5% tu ya mgawo huo kuanzia mwaka huo. Hili limekuwa likijenga taswira kwamba benki hiyo wenyewe ni Watanganyika na kwamba Wazanzibari wanajipachika tu. Hali hii iko kwa kila taasisi ya Muungano. Na ndiyo maana tukasema kwamba hakuna nia njema. Sheria zote za Muungano zinatungwa kama kwamba ni za Tanganyika siyo za shirika na Zanzibar. Huu ndiyo udhaifu wa Muungano unaofichwa usisemwe; na hii ndiyo dhamira mbaya ambayo sisi hatutaacha kamwe kuisema.

Siasa za Mkoloni Kuelekea Zanzibar

Mashaka ya sasa ya Zanzibar kufanywa himaya ya Tanganyika, yamenipelekea nitafute kwani hapo Zanzibar ilipokua chini ya himaya ya dola la Uingereza huku Waarabu wakionekana ndio wanaotawala, mambo yalikuwaje? Ndipo nilipogundua kwamba hakuna tafauti yoyote kati ya mbinu za Muingereza za kuitawala Zanzibar na zile za Mwalimu Nyerere na warithi wake.

Historia inaeleza kwamba wakati wa miaka 1850 hadi 1897, madola makubwa ya Ulaya yalikuwa katika harakati za kugawana Bara la Afrika na kuweka makoloni yao. Madola ya Kiingereza na Kijerumani yaligawana eneo la Afrika Mashariki ambalo lilikuwa Dola la Zanzibar (Zenj Empire). Ugawaji huo wa eneo hili ulimpunguzia sana nguvu na uwezo Sultani wa Zanzibar katika mwambao wa pwani ya Afrika Mashariki na hasa ya Tanganyika, ambapo ukanda ya pwani ya Tanganyika ulichukuliwa na Dola la Ujerumani na Zanzibar kulipwa akali ya fedha.

Nguvu za Ujerumani zilimpa shida sana Sultani wa Zanzibar na nguvu hizo zilitikisa hata kuwepo kwa ufalme wake. Kwa kutafuta apendwe, Muingereza alimtisha sana Sultani na kumtahadharisha hatua ambazo Mjerumani angeweza kuchukua dhidi ya ufalme wake. Ndipo Sultani Barghash, wakati huo akiwa ndiye mtawala, akaona kheri ya Muingereza kuliko Mjerumani na hivyo akakubali Muingereza awe mshauri wake katika mambo ya kisiasa na kiuchumi kama anavyoeleza Norman R. Bennet (1978).

Miaka miwili tu baada ya Sultan Barghash kufariki hapo 1888 na kutawala Sultani Ali bin Said, visiwa vya Zanzibar viliwekwa chini ya Himaya ya Uingereza hapo 1890. Kutoka mwaka huo, Sultani wa Zanzibar alikuwa kama mamluki kwani chini ya makubaliano hayo alitakiwa afuate masharti yafauatayo:

 • Mahusiano yake na nchi za nje lazima yafanywe kwa kibali cha Dola la Kiingereza. (Linganisha na hali ya mahusiano ya Zanzibar na nchi za nje tangu 1964 hadi sasa ambayo lazima yapate kibali cha Tanganyika)
 • Dola la Kiingereza ndilo lilikuwa na madaraka ya kuteuwa nani atawale pindi Sultani aliyepo madarakani akifariki. (Linganisha na hali ya sasa ya Zanzibar katika kubadilisha watawala wake, ambapo uamuzi lazima utoke Tanganyika, na hata kama Wazanzibari wanamkataaa huyo aliyeletwa kwa nguvu, majeshi na mauaji hutumika kulazimisha wanayemtaka watawala wetu wa Tanganyika)
 • Sultani alitakiwa asiingilie shughuli zozote za utendaji ambazo zikifanywa na Waingereza. (Linganisha na hali ya sasa ya utendaji na uwezo wa Serikali ya Zanzibar isiyoweza hata kukusanya mapato kwa ajili ya kuendeleza shughuli zake. Rais wa Zanzibar anateuliwa kuwa waziri asiye na wizara maalum huku akiwa si mbunge wa Jamhuri ya Muungano).

Hivyo kuanzia terehe 4 Julai, 1890, utawala wa kifalme Zanzibar ulimalizika ingawa visiwa hivi bado viliitwa vya kifalme. Maana hata mshahara wa Sultani uliamuliwa na Waingereza. Ushahidi wa jinsi Waingereza walivyomaliza nguvu za kifalme Zanzibar kwa ujanja na maguvu ni pale alipokufa Sultani Ali bin Said bin Sultan mwaka 1893. Waingereza walikataa kumuweka mtoto wa Seyyid Barghash ambae katika mfumo wa kifalme ndiye aliyekuwa anastahiki kuchukua nafasi ya ufalme huo. Hakupewa kutawala kwa sababu alionekana sugu na hakuwa akikubaliana na Waingereza walivyokuwa wakitaka wafanye Zanzibar.

Pamoja na kutumia nguvu kuingia katika jumba la kifalme, mtoto huyo wa Barghash, Khalid bin Barghash, aliondolewa kwa nguvu katika jumba hilo na kuwekwa Hemed bin Thuweyn mtoto wa mfalme aliyekuwa akitawala Oman siyo Zanzibar. Kwa sababu alitunukiwa ufalme alilazimika kukubali kula kiapo kwamba:

 • Malkia wa Uingereza ndiye Mkuu wa Himaya ya Zanzibar. (Linganisha na kuapa kwa Rais wa Zanzibar kuwa ni mjumbe wa Baraza la Mawaziri la Serikali ya Muungano)
 • Atakubali amri na maelekezo ya muwakilishi wa Dola la Kiingereza aliyekuwepo Zanzibar. (Linganisha na amri za kukusanya mapato ya Zanzibar zinavyofanywa na wawakilishi wa Tanganyika)
 • Atakubali mshahara aliopangiwa na Waingereza ambao uliku ni rupia 12,000 tu kwa mwezi. (Linganisha namna SMZ ilivyoamuliwa kugaiwa asilimia 4.5% tu ya misaada kutoka nje).

Sultan Hemed bin Thuweyn alikubali yote haya ilimradi tu atambuliwe na Waingereza kwamba yeye ni mfalme wa Zanzibar. Je, hivi sivyo alivyo Amani Karume hivi sasa?

Hali ya kukomaa kwa nguvu za Dola la Uingereza dhidi ya ufalme wa Zanzibar ilitokea pale alipokufa Sultan Hemed bin Thuwein mwaka 1896. Ingetegemewa kwamba wakati huu ufalme wa Zanzibar apewe Khalid bin Barghash, lakini badala yake akapewa Sultan Seyyid Hamoud ambae hakuwemo katika mkondo wa utawala wa ufalme wa Zanzibar na baba yake hakuwahi kutawala si Oman wala Zanzibar. Khalid bin Barghash alipoingia tena kwa nguvu katika jumba la kifalme, alitolewa kwa mizinga na Waingereza. Hivi ndivyo vita vinavyoitwa vya Alkhamisi. Angalia hali halisi ya uchaguzi wa  2000 na 2005, Wazanzibari walivyopigwa kwa mabomu na kuletewa askari wasiopungua 30,000 wakati wa uchaguzi, kuhakikisha kwamba mtawala hasa ni Tanganyika na  anayetakiwa na Tanganyika ndiye atakayetawala hata kama matokeo ya uchaguzi hayako hivyo.

Hivyo katika miaka yote 50 kati ya 1850 na 1890, Waingereza walikuwa wakimtumia Sultan wa Zanzibar kama kivuli kutekeleza lengo lake la kuitawala Zanzibar vile wanavyotaka wao. Kuwekewa watawala wanaotakiwa na Tanganyika katika kipindi cha miaka 45 chini ya kile kinachoitwa Muungano, ilikuwa ni kivuli tu cha kuhakikisha wanaitawala Zanzibar watakavyo Watanganyika. Kupigwa mabomu Zanzibar katika vita vya Alkhamisi kulidhihirisha nguvu ya Kiingereza na kuwathibitishia wafalme wa Zanzibar kwamba Waingereza ndio hasa watawala.

Basi kuna tafauti gani kati ya mwenendo wa viongozi wa Tanganyika wa sasa na Waingereza wa miaka ya kifalme hapa Zanzibar?

Hali halisi ya Zanzibar

Hebu sasa tuzingatie masuala yafuatayo na halafu tuone daraja ya Zanzibar kama Serikali ikoje:

 • Serikali huwa na jeshi la ulinzi na usalama. Je, Zanzibar inalo jeshi, ukiacha Janjaweed ambao wanatumiwa chini ya maagizo ya watawala wetu?
 • Serikali hua na bendera yake. Tumepewa bendera yenye kuonesha kwamba sisi ni himaya ya Tanganyika maana katika bendera yetu kuna bendera ya watawala. Angalia bendera kadhaa za nchi ambazo huumba mashirikisho ya kweli. Mfano Ujerumani ina mataifa 16. Kila moja kati ya hizo, zina bendera yake tafauti na nyingine na tafauti na ile ya Shirikisho. Bendera ya SMZ ina tafauti gani na bendera ya jeshi la Polisi, ambalo ni kikosi kimoja tu kati ya vikosi vingi vya Wizara ya Mambo ya Ndani?
 • Serikali huwa na sarafu yake. Tumenyang’anywa uwezo huo tangu 1965 na rasilmali fedha zetu kuchukuliwa
 • Serikali huwa taifa pale wananchi wake wanapokuwa na uraia. Imedhihiri mwaka huu kwamba kumbe sisi ni wakaazi tu siyo raia tena wa Zanzibar.
 • Serikali huwa na Polisi na masuala ya uahamiaji. Zanzibar hatuna vyote.
 • Serikali huwa na uhusiano na nchi za nje. Zanzibar hatuna na wala hatuthubutu kuwa nao. Kumbuka suala la OIC lilivyopingwa pamoja na kwamba lilikuwa halali.
 • Serikali humiliki Benki Kuu.  Zanzibar hatuna.
 • Serikali huwa na madaraka ya kupitisha sheria za ushuru na kodi kwa faida ya maendeleo ya nchi yake. Zanzibar hata kodi inakusanywa na watawala na sisi kugemewa tu watakacho watawala hao.
 • Serikali humiliki eneo lake la anga na eneo lake la bahari. Yote hivyo havipo kwa Zanzibar maana hata leseni za kutumia bahari ya Zanzibar sasa lazima zikatwe Dar es Salaam.

Kwa hivyo, ni wazi kwamba Zanzibar imepoteza kila sifa ya nguvu ya Serikali na kubaki bamba tupu kama anavyosema Prof. Shivji katika maandiko yake:

“The addition and amendments to the reserved list discussed herein are repugnant to section (5) of the Act and articles of the Union. In a serious and fundamental way, they undermine the basic scheme of the Union provided in the original agreement. If such additions and amendments of the Union matters were held to be lawful, Zanzibar’s autonmy and the federal principle in which the association is rooted would be an empty shell.” (Shivji: Legal Foundation of the Union: 1990)

Hitimisho

Dhamira ya waraka huu ni kuwaeleza wataalamu wa Chuo Kikuu na Watanzania watakaosoma makala hii kwamba kama kuna nia njema ya kisiasa mgogoro wa Muungano ni mwepesi mno na wala hautaki miujiza kutoka mbinguni au kwa Wazungu. Zaidi nilikusudia kueleza kwamba sisi, Wazanzibari, hatuko kwenye ndoa na Watanganyika na wala hatudai talaka. Isipokuwa, kama walivyodai haki Watanganyika kutoka kwa Waingereza, sasa na sisi tunadai haki zetu kutoka kwa wale wanaojigamba kwamba ni ndugu zetu wa damu! Na hilo la kudai haki si jambo geni wala la kutoa haki si jambo la ajabu. Yote ni ya kawaida.

Kila mara ninapopata nafasi  huwa natoa mfano hai wa Afrika ya Kusini, kwamba kilichofanya nchi hiyo itoke katika mapambano ya wenyewe kwa wenyewe ni viongozi waliokuwa na khatamu za Dola (yaani Fredrick De’Clerk na wenzake) kuheshimu na kutekeleza makubaliano yao na African National Congress (ANC).

De’Clerk angeweza kabisa kudharau makubaliano hayo, kama alivyofanya Mwalimu Nyerere dhidi ya Makubaliano ya Muungano au Mkapa dhidi ya Makubaliano ya Muafaka II, kwa sababu naye alikuwa na kila uwezo wa kudharau. Nani haelewi kwamba Afrika ya Kusini ina uwezo mkubwa sana kijeshi mara kumi zaidi ya Tanzania, lakini mbona De’Clerk hakuzitumia nguvu hizo? Hakufanya hivyo kwa sababu alikuwa ana nia njema. Ni suto na kijembe kilioje kwa akina Nyerere na Mkapa, kwamba kaburu De’Clerk alikuwa na dhamira njema kwa nchi yake lakini wao hawakuwa nayo kwa nchi yao!

Wa Afrika Kusini ni mfano mmoja tu, lakini si pekee. Kuna pia ule wa nchi ya Burkinafaso, ambayo mara tu baada ya uhuru ilikumbwa na mapinduzi ya kijeshi mara tano. Baada ya miaka 10 ya mfumo wa vyama vingi, kiongozi wa nchi hiyo aligundua kwamba chama chake kilikuwa kina wabunge wengi mno kuliko vyama vya upinzani na hivyo kuwanyima wananchi wake nafasi ya kutetea maslahi yao katika chombo chao. Kati ya viti 111 vya Bunge, chama tawala kilikuwa na wabunge 104 na kuacha viti 7 tu vya wapinzani. Katika kumchagua, Rais chama hicho kikipata si chini ya 76% ya kura zote za urais. Rais Blaisse Kampaore hakujisifu kushinda kwa kishindo cha Tsunami, badala yake aliruhusu mjadala wa kitaifa juu ya udhaifu huu na akafanya mabadiliko makubwa ya mfumo wa Tume ya Uchaguzi kwa kuwashirikisha wadau wote, na kubadilisha utaratibu mzima wa kupiga kura. Kuanzia uchaguzi wa 1998, chama tawala kilibaki na 51% ya kura za Rais na viti 57 vya Bunge na kuwaachia kura asilimia  49 za kura na viti 54 katika Bunge  wapinzani. Haya yaliwezekana kwa sababu Rais Kampaore alikua na nia njema.

Kilichokosekana hapa Tanzania ni nia njema ya viongozi. Katika Muafaka II wa Zanzibar, Rais Mkapa alikuja mbele ya jumuia ya kimataifa na kuweka ahadi ya kuutekeleza ili kuepuka maafa katika uchaguzi wa 2005. Tukategemea Rais angejifunza na kujutia yale yaliyotokea 2001 wakati wa maandamano. Badala yake Rais huyo mstaaafu akatayarisha majeshi na vikosi vya maharamia kuvuruga uchaguzi mzima na kusababisha maafa na uhasama zaidi, bila kuona aibu. Sasa ameondoka na kuiacha Zanzibar katika mgogoro mkubwa zaidi kuliko hapo mwanzo. Yote ni kwa kuwa Mkapa hakuwa na dhamira njema na Wazanzibari.

Mfano mwengine wa viongozi wa Tanzania kukosa dhamira njema ni kushindwa kutekeleza sheria wanazozitunga wenyewe. Sheria ya  Ruzuku Na. 6 ya 1997 ya vyama Vingi ya Zanzibar, ambayo ni sheria ndugu ya ile ya Muungano, inatoa nafasi kwa vyama vya upinzani kulipwa ruzuku kwa mujibu wa wingi wa viti na wingi wa kura zilizopatikana katika uchaguzi. Sheria ambayo imetoa utaratibu wa jinsi ya kugawa ruzuku ya vyama haijatekelezwa na SMZ za awamu zote zilizotawala Zanzibar tangu kuja kwa vyama vingi vya siasa.  Matokeo yake chama cha CUF kinaidai SMZ mabilioni ya fedha za ruzuku katika kipindi cha miaka 15 iliyopita bila kulipwa. Pamoja na kulalamika kwa msajili wa vyama vya siasa, hadi niandikavyo waraka huu CUF haijalipwa fedha ya ruzuku kwa upande wa Zanzibar. Yote ni kwa sababu ya ukosefu wa nia njema.

Hii ni mifano michache tu, lakini ndio picha halisi ya watawala wetu. Kutokuheshimu sheria na kauli zao wenyewe; nayo ni aibu kubwa. Kila siku nimekuwa nikisema kwamba sheria si maandishi yaliyo vitabuni tu, bali sheria ni uamuzi wa makusudi wa muhusika kuheshimu maandiko hayo kwa vitendo. Kwamba hebu tuulizane: nani aliyewapangia viongozi wa nchi tatu za Afrika Mashariki kuanzisha Bunge lenye wabunge 27, kila nchi ikitoa wabunge 9? Kwa nini wabunge 9 tu, wasiwe 40 au 50? Bila ya shaka, hayo ni maamuzi ya makusudi ambayo yameheshimiwa na wahusika. Lakini nchi tatu hizi bado zina mabunge yao nje ye Bunge hili. Si hivyo tu bali pia nchi hizi udugu walionao hauwezi kulinganishwa na udugu tunaoutetea na kuupigia kelele kati ya watu wa Zanzibar na wa Tanganyika. Nakusudia kusema kuwa Watanganyika na Wazanzibari ni ndugu zaidi kuliko walivyo Watanzania na Wakenya na Waganda.

Sasa kwa nini sisi tulio ndugu zaidi, bado tumeshindwa kwa kipindi cha miaka 43 sasa kuweka mfumo wa hiari na maridhawa wa kuendesha Muungano wetu? Waafrika weupe na weusi wa Afrika ya Kusini waliouwana na kujenga uhasama wa muda mrefu, waliposema yaishe yakaisha, kwa kuwa waling’amua kwamba lazima nia njema iwepo kumaliza matatizo yao. Kinachokosekana hapa Tanzania ni nia njema tu.

Nani atatuzuia kama tutasema: “Watanganyika chagueni Bunge lenu, Wazanzibari chagueni Bunge lenu, na baada hapo tafuteni wabunge 10 wa Tanganyika na 10 wa Zanzibar wawe wabunge wa Muungano?” Hilo linawezekana na wala mbingu hazitaanguka wala ardhi kupasuka.

Zaidi ya kuwa na nia njema uongozi wa Tanzania vile vile unakosa mfumo wenye daraja za kihekima kusimamia na kutatua matatizo ya kitaifa. Wenzetu wa Afrika ya Kusini, baada ya uhasama wa muda mrefu, wamejiwekea daraja ya mwisho ya kutatua matatizo ya kitaifa, ambayo ni Supreme Constitutional Court, chombo ambacho hakiingiliwi na wanasiasa na maamuzi yake hayana siasa. Huko hata Rais atahojiwa au kuulizwa kulikoni!

Inasikitisha sana kwamba petu Tanzania, Rais ndiye chanzo cha mateso na fujo na hakuna wa kumwambia hivyo sivyo wala huwezi kumzuia kisheria. Tunamngojea mpaka anaacha madaraka, ndipo tunaaza kumuandama wakati ameshatumaliza. Kazi yetu Watanzania ni kuwasifu maraisi na kuwatukuza huku tukilalamikia chini ya miti.

Ushauri wangu ni kwamba, kama tunataka kumaliza mgogoro wa Muungano na hata ule wa Zanzibar, lazima Rais Kikwete na wenzake wa CCM wabadilike na wabadilishe mtazamo wao kwa Zanzibar, ambao kama nilivyokwishaonesha unatawaliwa na Big Brother Attitude. Wakati akihutubia Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM mwaka 1988, mkutano ambao ndio uliowafukuza akina Maalim Seif na wenzake, Mwalimu Nyerere alisema hivi: “Mtwara na Mwanza zilikua nchi mbili; aliziunganisha Mjerumani kwa bunduki. Tanganyika na Zanzibar zilikua nchi mbili mbali mbali. Sisi tumeziunganisha kwa kalamu.”

Hili la ‘sisi’ hapa ndio mtazamo ulio ndani ya vichwa vya watawala wa Tanganyika unaotakiwa kubadilishwa. Kwa Mwalimu Nyerere na wenzake, wao ni Watanganyika wanaotetea visiwa vyao ambavyo wanaamini kwamba kama si kosa la Mjerumani kuvikabidhi visiwa hivyo kwa Muingereza hapo tarehe 1 Julai, 1890, basi vingeliweza kuwa ni sehemu ya Tanganyika.

Hicho ndicho, kwa hakika, alichokuwa akikipigania Mwalimu Nyerere katika uhai wake wote na sasa ndicho kinachoendelezwa na warithi wake. Na ndiyo maana Mwalimu Nyerere anasema hivi katika kitabu chake cha Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania:

“Pwani ya Tanganyika na Zanzibar ya sasa zilikua pamoja kwa muda mrefu sana kabla ya kutengwa na Wakoloni Waingereza na Wajerumani. Kama zingebaki zimetengana kwa “Wazalendo” hao hiyo ingekuwa ni halali maana zilitengwa kwa hila na mitutu ya bunduki za mabwana.” Lakinj uamuzi wa Tanganyika huru na Zaznibar huru kuungana na hivyo kuwaunganisha tena ndugu waliokuwa wametengwa na Mabeberu, tendo hilo kuna viongozi wetu wanaosema kuwa halikua halali.” (Mwalimu Nyerere: 1994:58)

Mwalimu Nyerere akiamini hivyo kwamba ni makosa kwa Zanzibar kubaki kama nchi, lakini anakubali mipaka ya nchi nyingine ibaki kama ilivyoachwa na wakoloni kama alivyoshauri katika kikao kimojawapo cha OAU huko Addis Ababa, mwaka 1963. Hivyo kosa ni Zanzibar tu? Tatizo ni dhamira mbaya.

Uingereza ni taifa kubwa lakini ni visiwa vilivyo karibu na fukwe za Magharibi ya Bara la Ulaya, lakini si Wajarumani wala Wafaransa waliowahi kusema kwamba kwa sababu visiwa hivyo vipo karibu na fukwe za nchi zao, basi ni vyao. Ujapan ini taifa kubwa sana, na ni visiwa vilivyopo karibu na pwani au fukwe za Korea, lakini Wakorea hawadai kwamba ni visiwa vyao. Singapore ni karibu sana na fukwe za Malaysia, na kwa hakika nchi hizo mbili ziliwahi kuwa na muungano kama huu wetu, lakini Malaysia haijawahi kudai kuwa Singapore ni kisiwa chake. Kwa hapa Afrika, Mauritius ni kiswa kidogo kuliko hata Unguja pekee, lakini ni nchi kamili; na licha ya kuwa kwake karibu na Madagascar, bado Madagascar hawajakinyakua.

Kosa la Zanzibar ni kuwa karibu sana na fukwe za Tanganyika na, kwa tafsiri ya Mwalimu Nyerere, ni lazima visiwa hivyo viwe vya Tanganyika! Huu ndiyo udhaifu wa mgogoro wa Muungano, tangu awali malengo ya Muungano siyo yale yaliyomo kwenye maandishi ya makubaliano. Maandishi ni babaisha toto tu. Na ndiyo maana, Mzee Aboud Jumbe anasema ni mara moja tu wakati wa kupitisha Makubaliano hayo hapo Dar es Salaam kwenye bunge la Tanganyika ndipo  Mwalimu Nyerere aliwahi kumwita Mzee Karume kama Rais wa Zanzibar:

“This is one of the rare occasions when Nyerere spoke to Karume as an equal partner. President of Tanganyika speaking of or speaking to the President of Zanzibar, both of them enjoying the same status (as Presidnets). From then on, except in the incident quoted above it was the Union President meeting or talking to his Vice president be it on Union matters or non- Union matters. The President of Zanzibar never again met his counterpart to discuss non- Union matters which were finally absorbed unconstitutionaly by Union Government into Union matters. Surely Nyerere must have known what he wanted all the time in the light of what followed afterwards.” (Jumbe: The Partnership: 1994: 14)

Sasa Tufanyeje?

La msingi kuliko yote ni kukubali kwanza kwamba sisi vizazi vya Zanzibar vilivyopo leo haviwezi kuhukumiwa kwa makosa yaliyofanywa na watawala wa Zanzibar wa miaka 1850 mpaka 1963. Kututia adabu Wazanzibari wa leo ni kufanya makosa yale yale yaliyofanywa na Waarabu waliotawala wakati huo. Na kama babu zetu hayo waliyaona ni mateso na wakapambana nayo, walifanya hivyo ili sisi kizazi cha leo tuishi maisha ya uhuru ya heshima na ya umoja.  Hilo limekosekana Zanzibar kwa miaka 43 sasa baada ya kuingia kidudumtu mwenye dhamiri potofu ya Waafrika kuwatesa Waafrika.

Kwa hivyo kilicho muhimu ni nia njema na hivyo yafuatayo yafanyike:

 • Lazima viongozi tubadili utamaduni na kuona kwamba Muungano huu ni baina ya big brother na small brother. Sisi ni nchi mbili huru zilizokubali kupunguza baadhi ya madaraka yake kwa faida ya umoja huo.
 • Kuzingatia kwa moyo safi malalamiko ya muda mrefu ya pande zote mbili na kuyatafutia ufumbuzi
 • Kuupitia tena Mkataba wa Muungano kwa nia ya kuuimarisha na siyo kuudhofisha upande mmoja dhidi ya mshiriki mwengine
 • Ijulikane wazi kwamba mjadala wa matatizo ya Muungano si wa wengi dhidi ya wachache. Ni mjadala wa wawakilishi wa Zanzibar na wa Tanganyika. Muungano ndiyo unaojadiliwa na hivyo viongozi wa Tanganyika ambao kwa sasa ndio wanatawala Serikali ya Muungano wasijikweze na kuona wao wapo juu ya wahusika, yaani Tanganyika na Zanzibar.

Mwisho, tuchukuwe indhari ya McGarry na O’Leary, wataalamu wa masula ya migogoro inayotokana na Serikali za Shirikisho, ambao wameeleza kwamba: shirikisho lolote lile la nchi mbili zilizotokana na siasa za chama kimoja huishia kuvunjika kutokana na tabia zake za aina tano: coercision to come together (matumizi ya nguvu kulazimisha muungano), authoritarianism to stay together (matumizi ya udikteta kulazimisha kuendelea kuwepo kwa muungano), maltreatment of the smaller partner (kumtendea vibaya mshirika mdogo), distribution conflicts in economic policies (taifa dogo kunyimwa nguvu za kiuchumi) na centralising processes (mbinu za kupunguza nguvu za taifa dogo kwa kulazimisha).

Huu ni utabiri wa wataalamu ambao unaweza ukatokea kwa Tanzania kama vile ulivyoweza kutokea kwa Muungano wa Urusi, Yugoslavia na kwengineko duniani. Ni nia njema tu ndiyo inayoweza kunusuru hilo!

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s